Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, March 7, 2011

Mpende jirani yako-2


Sauti ya panga likigonga ukuta, lilinishitua, na upepo wake ulinifanya niiname nikidhania panga hilo lilikuwa limedhamiriwa kukikata kichwa changu. Niligeuka kwa hasira kutaka kuiandaa kwa mapambano kama ikibidi, lakini nikaona ni ujinga, kwani walishaingia ndani kwao huku wakisema;


`Unasikia, sina jirani na yoyote hapa, mimi na familia na nyumba yang utu, nyie kivyenuvyenu. Sitaki kabisa kusikia mambo ya ujirani, …eti, ujirani, uijirani…kaeni na familia zenu na mimi na familia yangu. Sitegemei kabisa kuja kuomba chochote kwa yoyote…na sitaki mtu yoyote atumie kisingizio cha ujirani kuja kwangu…sitaki kabisa, hata msikia kuna nini kimetokea hapa, simtaki mtu kuingia humu nyumbani mwangu…umesikia…sina ujirani na yoyote…kwaheri…’ akafunga geti lake kwa nguvu, utafikiri ndilo lenye makosa.

Nyumba ya mwenzetu huyu ni nzuri kwakeli, kubwa na imezungushwa ukuta mkubwa uliozungushiwa waya za umeme za usalama. Ukiingia ndani kuna ukuta mwingine unaounguka nyumba ambao una nyaya ndogo sio sawa na wa ndani , halafu kuna mbwa mkubwa aliyejengewa karibu na geti, hufunguliwa usiku, au hata mchana kama wao hawapo, na mlangoni kuna `onyo kali’ nyumba hii inalindwa na vyombo vya usalama, na pia kuna mbwa mkali, usiingie humu ndani…’

‘Jamani kama familia imo humo ndani, tuvunje hili geti tuiokoe, na kama atakuja kusema aseme tu, hawo malaika humo ndani hawana hatia yoyote, kama ni tabia yao mbovu ni wao wenyewe, sidhani watoto wadogo kama hawo inawahusu…’ nikasema na mjumbe akakubalia na wazo hilo, na kazi ya kuvunja lile geti ikafuatia, kwa kumtumia fundi maalumu anayejua kubandua viatasa bila kuliharibu geti, na akafanya kazi yake vyema kabisa.

`Nasikia mlinzi alishaacha kazi baada ya kuchoka manyanyaso. ..’ akasema mjumbe, lakini hakuna aliyemjibu kwani wote mawazo yote yalishakwenda mbali kuhusiana na hicho tutakachokutana nacho ndani. Kwani inatisha kumuona mwanadamu kateketea na moto, …ukizingatia ni watoto wadogo wasio na hatia..

‘Mungu awanusuru watoto hawo…’ nikajikuta nikisema kwa sauti.

‘Wewe moto kama huo unafikiri tutakuta usalama kweli…sijui yote ni majaliwa…’ akasema jamaa mmoja

Tuliingia ndani na kujikuta na tatizo la kufungua geti la pili ambalo hufunguliwa kwa mitambo ya ndani ya umeme. Na kwasababu ya huo moto, tunafiikiri mitambo imenasa, kwani tulijaribu kwa kila ujuzi tukashundwa kufungua, hata fundi wetu akachemsha.

‘Sasa tufanyeje mjumbe…? Akaluliza jamaa mmoja

‘Livunjwe kinguvu, kwani hata ukiacha litakuwa na faida gani, kwani moto utalivaa litharabika tu…’ akasema mjumbe.

Fundi wetu akatuonyesha njia ya kulivunja sehemu za pembani mpaka likakubali na tukatumia nguvu kidogo tukapata upenyo. Tukaingia eneo la nyumba, ambayo ilizunguka na bustani za kupendeza na kwa pembeni tukaona bwawa la kuogelea `swimming pool’ .Moto ulishaanza kupamba-moto, sehemu ya nyuma ilikuwa ni moto mtupu.

Nyumba yenyewe ilikuwa imezungushiwa `madril ya chuma’ na bahati nzuri yalikuwa hayajafungwa tukaingia kwa ndani na kukuta milango imefungwa…!

‘Bora tuvunje viyoo..’akatoa rai mjumbe, na tukafanya hivyo, dirisha moja likavunjwa viyoo na tukajipenyeza na kuingia ndani ya jumba la kifahari…wote walioingia humo ndani walishusha pumzi, kwani vyombo vilivyokuwemo humo ni vya kifahari…lakini hatukuwa na muda wa kuviangalia sana, tukawakimbilia watoto wawili waliokuwa wamlala chini kwenye busati la manyoya ya fisi…walikuwa wamezirai. Harakaharaka wakatolewa nje kupitia dirishani kwani mlango mkuu ulikuwa haufunguki.

‘Yupo wapi mfanyakazi wao…?’ akauliza jirani yake, lakini hata tulivyotafuta kwa muda hatukumuona, tukadhani labda alikuwa kaenda dukani. Wakati tunahangaika kuuzima ule moto kwa kuchota maji yaliyopo kwenye bwawa la kuogelea, tukagundua mwili umelala kando ya ukuta huo wa ndani, kumbe alikuwa yule mfanyakazi, inavyoonekana alijaribu kuruka ukuta ili akatoe taarifa au kujiokoa akasahau kuwa ukuta huo umezungushiwa umeme. Naye akachukuliwa haraka na kutolewa kabisa nje na eneo hilo.

‘Jamani mchango wa usafiri upitishwe haraka…’ akasema mjumbe , na kila mmoja alitoa alicho nacho, mpaka ikapatisha hela ya bajaji na wale watoto na mafanyakazi wao wa ndani wakakimbizwa hospitali. Ukumbuke jamaa hawa wana magari matatu, mke ana gari lake na mume anagari lake ma watoto wana gari lao lakuwapeleka na kuwarudisha shuleni, lakini mtihani ulivyotokea kwa muda huo hapakuwepo na gari la watoto, kwani dereva wa kuwapeleka shule alikuwa katumwa mjini kununua mahitaji ya dukani kama tulivyoambiwa baadaye na mfanyakazzi wa ndani.

Hutaamini watoto hawo wa matajiri kwa mara ya kwanza ndio wanapandishwa kwenye bajaji wakiwa hawajitambui…kwa michango ya walalahoi ambao hawatahaminiwi kabisa na familia hiyo!

‘ je sasa tutawafahamishaje wahusika?’ tukaulizana, na wakati huo polisi waishafika na zimamoto, lakini walikuta moto umeshazimika kwa juhudi za majirani. Polisi walihoji na kupewa taarifa yote inavyoonekana kwani ukweli halisi wa chanzo cha moto huo, unaweza ukajulikna kutoka kwa watoto hawo au mfanyakazi wao, na wao walishakimbizwa hospitalini wakiwa hawajitambui.

Majirani kwa wasiwasi ilibidi wawaambie polisi ukweli wa jirani huyo kuwa kuna wasiwasi wakija watazua zogo, kwani wanaweza wakija wakaleta matatizo na lawama na hata vurugu badala ya kutushukuru. Polisi walisema hilo tuwaachie wao, kama wataleta matatizo wao watajua jinsi gani ya kuwaweka sawa.

‘Kwanini hamuishi vyema na jirani yenu huyu, au mnamuonea wivu tu na jumba lake hili, na kuna mambo humo ndani yanatutia mashaka, lakini hayo tuyaache kwanza..?’ akauliza polisi na kuonyesha wasiwasi fulani ambao hakuna aliyejua wana maana gani.

‘Huyo ilivyo sio jirani yetu, amejenga hapa kimakosa, na kama ingekuwa uwezo wake angetufukuza hapa sote akaishi mwenyewe au angetuhamisha ili asipate usumbufu…’ akasema jirani yake.

Kila njia ya kuwasiliana na huyu mwenye nyumba ilishiundikana kabisa, na watoto wameshafikishwa hospitali na hali zao zilikuwa bado ni tete.

‘Yaani majirani wote hakuna anayejua wapi mwenzenu anapofanyia kazi na hakuna hata mmoja anayejua namba yake ya simu….ajabu kabisa’ akasema polisi huku akihangaika huku na kule kuwasilina na wenzake.

‘Afande sisi tunachoshukuru ni kuwa watoto wameokolewa, na wamo kwenye usalama , tunatumai huku watapata matibabu, mengine ni kazi yenu…’ akasema mjumbe

‘Kazi yetu haiwezi kukamilika bila msaada wenu, kama mngesubiri mkisema ni kazi yetuu hawo watoto wangeteketea kabisa, …hii ni kazi yetu sote…kama kuna mwenye kujua wapi tutwawailina na hawo jamaa tunaomba mtujulishe…’ akasema polisi akiwa katahayari.

‘Ni kweli afande , hayo tunajua saana, ila mwenzetu hayo hayajui kabisa, huwezi kuamini hata mimi mjumbe niliwahi kufukuzwa kwenye nyumba hii kama mwizi, wakati nilikuja kutimiza wajibu wangu kama mjumbe, waliniambia kama wana matatizo na mjumbe watakuja, …kuli nyingina sitaki hata kuzisema…lakini sio mbaya mimi kama mjumbe nameza yote, matamu na machungu…’ akasema mjumbe.

Wakati tunahangaika huku na kule kuulizia kama kuna yoyote anayejua yule mlinzi wake aliyeondoka anapatikana wapi kwani huenda akawa anajua wapi bosi wake anafanyia kazi, mara likaja gari na kusimama karibu na sisi, akatoka msichana mmoja alipoona ile hali akaingia ndani ya gari haraka na kuchukua simu yake, hata bila kutuulizia nini kimetokea, tukajua ni damu ile ile…..

Je na huyu ni nani na kuliendelea kitu gani. Samhanani kwa kukatisha, lakini imebidi kwani nahitajika kutoka kidogo , nimetumwa na `mabosi’ kuwajibika.

Ni mimi: emu-three

2 comments :

John Maembe said...

Daaah!!! Hapo patamu sana Emu-3. Huyo ambaye anaweza kuwa damu mmoja ataleta msaada. Lakini hao majirani watajirudi wenyewe na kuja kutoa shukrani, kwani mmewafanyia bonge la wema ambao ni shule tosha kwa wao na kujifunza nini maana ya ujirani.
Kisha kuwa na mali nyingi kama hizo sio kigezo cha kupelekea kumfukuza hadi Mjumbe ndio maana "NI JINSI GANI ILIVYO VIGUMU KWA TAJIRI KUUONA UFALME WA MBINGUNI KULIKO NGAMIA KUPENYA KWENYE TUNDU YA SINDANO"
Hayo ni mapenzi ya Allah mwenyewe kuwaonyesha kuwa Mali si kitu katika Maisha ya Binadamu anachokisisitiza ni Kumpenda Jirani kama unavyojipenda au kama nyinyi wasamaria mlivyofanya na Mwenyezi atawazidishia.
Naishia hapo kwa leo, ila kesho naomba utuandikie kwa kirefu Mkuu.

malkiory said...

Ubinafsi na utajiri wa humu duniani ni mambo ya mpito tu. Hata kama wangelikuwa wanamiliki mbingu nadhani bado wasingetosheka nayo. Hivyo bora ubinadamu kwanza mali na utajiri baadaye.