Kuna mambo ambayo mwanadamu hatuna maamuzi au uwezo nayo, na sidhani kama kuna wataalamu wapo kwenye maabara hivi sasa, wakitafuta dawa ya kupambana na matatizo kama haya ambayo yapo juu ya uwezo wetu...sina uhakika na hilo! Moja ya tatizo hili ni kifo. Hii ni kusema kuwa kila mtu atakufa, apende asipende, ni swala la muda. Hii wanakubaliana wote wawe wanasayansi au waumini wa dini mbali mbali.
Kiubinadamu ni vyema tukawa tunawakumbuka `marehemu’ waliotangulia mbele za haki, kwani wao wametangulia, sisi ni watarajiwa, hakuna anayejua lini na muda gani ataondoka, basi kwa waumini huwa tunafanya maombi au duwa kuwakumbuka au kuwarehemu waliotangulia mbele za haki.
Mwenzetu katutumia tangazo lake hili kama kumbukumbu ya mama yake mzazi, tangu atangulie mbele za haki sasa ni miaka miwili. Sisi kama wadau, ambao tumejaliwa kuwa na mitandao(blogs), tunaungana na familia ya mama huyu kwa `kumrehemu’ au kumombea dua kwa mwenyezi mungu amsamehe madhambi yake, kwani sote ni wanadamu na dhambi hazikwepeki, na kumuomba ni huyohuyo aliyetuumba.
Kwake tumetoka na kwake ndio marejeo (Inna lilah waina ilaih rajiuna)
OMBI:
Kuna mdau aliniomba nijaribu kuwauliza watu, kuwa watu wanafanya sherehe za kukumbuka zao siku maalumu katika hii dunia(birthday party), na imekuwa ni mazoea na sherehe kama hizi hugharimu hela nyingi tu! Sherehe kama hizo ambazo hupewa anuani ya `sherehe ya kuzaliwa’ ni muhimu sana si kwa watoto hata wakubwa.. Lakini binadamu tulivyo, au tulivyopangiwa na muumba ni kuwa utazaliwa, utakuwa mkubwa ukijaliwa na hatimaye utaondoka kwenye hii dunia. Kama tunaweza kufanya sherehe za kuzaliwa, mbona hatufanyi sherehe za kuondoka duniani(kufa)?
‘Utafanyaje sherehe wakati wewe umeshafariki dunia?’ akauliza mdau mmoja.
‘Inaa maana ukishakufa basi wewe umeshasahaulika?’ akauliza madau mwingine, kumuuliza mdau wa kwanza.
‘Hapana ukishafariki dunia,sio kuwa umesahaulika, ni kwamba tu umetangulia mbele ya haki, na kwa vile tupo sisi watarajiwa, ni jukumu latu sote kuikumbuka ile siku aliyoondoka mwenzetu , siku ambayo kwetu ilikuwa ni majonzi. Kama kweli tulimpenda huyu mtu, kama kweli tunahitaji kumkumbuka, kama ilivyokuwa akiikumbuka siku yake ya kuzaliwa, au tulivyokuwa tukiikumbuka siku yake ya kuzaliwa, basi tuikumbuke sikuyake ya kuondoka kwa ibada, na kumuombea maghafira, kuwa `mola msamehe mpenzi wetu huyu mdhambi yake na umlaze mahala pema peponi.
Ni ombi tu wapendwa, najua wengi wanafanya hivyo, lakini kuna wachache ambao hawafanyi hivyo, ni vyema tukakumbushana jukumu letu hili muhimu!
Ni mimi: emu-three
1 comment :
Ni wazo zuri, binafsi naliunga mkona kwa asilimia 100.
Post a Comment