`Wewe njoo kwangu Mabibo nitakupa mchongo wa maisha, usikose ni
muhimu sana. Sasa ufanye hivi, wewe, ukifika makutano, nyosha moja kwa moja
hadi kwenye transfoma, pinda kulia, hesabu nyumba tatu, mtaa unaofuta kuna
nyumba nyekundu, ulizia bob Dulla,…
Mimi hapo najulikana sana kama mpiga dili, au wakala,…wengine
wanaijua kama Ubwabwa...kwenye shughuli hapo' nilisikiliza maelekezo kwenye
simu kutoka kwa huyo jamaa, mchekeshaji wa kutupwa . Na kwa vile nimewahi
kuishi maeneo hayo ya Mabibo, nilishajua wapi anapaongelea, kwahiyo
nikamhakikishia kuwa nitafika tu bila matatizo.
Niliwahi
sana siku ya pili yake asubuhi, manake nilikuwa nahitaji sana kupata shughuli
za kuingiza kipato, na jamaa mwenyewe sio haba anajua sana kufuatilia mambo kama
hayo,…na hapo aliniambia kuwa kesho anakwenda safari, mikoani kidogo.
Nilipofika kituo cha Sokoni, kama kinavyoitwa nikashuka, nikaanza
kutenmbea shoto kulia na TZ 11 yangu, hadi eneo linaloitwa Makutano. Nilipofika
pale nikaona nichepuke kimtaa cha mkato, sinilishawahi kuishi maeneo hayo,
kwahiyo vimitaa vilikuwa bado kichwani.
Nilipofika mbele nikakuta kile kimtaa kimefungwa na ukuta umepita
kuizunguka nyumba. Ohoo, jiji hili kila siku mabadiliko. Ikanibidi niingie
mtaa mwingine, nikatembea wee, sifiki!.
Nilishangaa mbona sitokei barabarani, nikaona ngoja nirudi nyuma
nianze upya. Wee nilichoka, nilitembea nikajikuta natokea eneo tofauti kabisa,
nikasema ngoja nipinde kushoto niongoze ile barabara, labda nitatokea barabara
kuu, nilijikuta natokea eneo kama la Kigogo vile, basi nikasema ngoja nirudi
nyuma, kama ni Kigogo nitakuwa nimeenda mbali. Nilicheza kushoto kulia, nenda
rudi hadi masaa matatu yakanikatikia...
Kilichonisaidia
niliamua kuangalia simu kuwa ni saa ngapi. Niliogopa hata kumpigia mwenyeji
wangu simu kwani angenishangaa. Nitachekwa, nitaonekana wakuja, siunajua tena,
ukikutana na mtu kama Bob, Dulla, anaweza kukuanika juani, bila kujali umri
wako.Kuangalia kumbe simu nayo ilishazima, haina chaji. Nikaiwasha ili angalau
niangalie muda na mara simu ikaita.
'Wewe mtu, vipi
mbona huonekani..' jamaa akaniita
'Hutaamini,
naitafuta nyumba yako siioni, sijui nimepotea..' nikasema
'Wewe, umekanyaga
mdudu…’akasema kwa mzaha
‘Nimekanyaga mdugu..?’ nikamuuliza kwa mshangao.
‘Ndio…sikiliza wewe fanya hivi, geuza shati lako hilo, kwangu sio
mahala pa kupotea, na wewe siulishawahi kuishi maeneo ya huku bwana, acha
ushamba...’akasema
‘Sawa nitafika tu…’nikasema
‘Sikiliza, …wewe umekanyaga mdudu, geuza shati hilo,…unajua ni saa
ngapi saa hizi, kama uusipofanya hivyo utakesha ukiitafuta nyumba, shauri lako...'
akasema huku anacheka.
Nikafikiri
wee, nikaangalia kushoto, kulia, nikaona watu wanapita, nikachepuka kwenye
uchochoro, nikavua shati haraka nikageuza, kwasababu ilikuwa fulana, isingeweza
kugundulika. Nilipomaliza, nikatokeza barabarani...oooh, barabara ya kwenda
Ruhanga, kumbe nilipitiliza. Nikarudi nyuma kwa kuelekea Mabibo makutano, na mara
nyumba ile, inaonekana wazi kabisa.
Swali likanitinga
kichwani, je ni kweli nilikanyaga mdudu, au ni imani tu?
Na je nilifanikiwa kwasababu nimegeuza shati…huu sasa ushirikina, …!’
Unajua sikuamini hadi nilipofika kwa rafiki yangu na ikawa stori,
na kwasababu kulikwa na jamaa zake kila mmoja anasema ilishawahi kumtokea, na
dawa ikawa hiyo kugeuza shati, nikajipa imani kidogo ya kuamini, ili nisije
kuonekana mshamba wa mji...sijui labda wewe au yule ilishawahi kumkuta hiyo.
Jamani maisha sasa kila mmoja anasema ni magumu,..kila mtu
anaongea lake, wengine ni mageuzo, wengine ni siasa, wengine …ooh, kila mtu na
lake, na hakuna nayejaribu kukumbuka dhamira yetu ya awali,…kupambana na
mafisadi na wala rushwa
Na ni karibu
tu, uchaguzi utakuja, na ni vyema tukaangalia njia zetu, kwani nahisi
tumepotea. Tusipoangalia tutapuyanga wee, hadi miaka nenda, rudi, na mika
mingine mitano itapita, bila kujua wapi tunapokwenda. Ni heri yangu nilipigiwa
simu na mwenyeji wangu, lakini sie tutapigiwa simu na nani? Haya, labda kama tutapigiwa
simu, dawa yake ni kugeuza shati? mbona shati lenyewe halina ndani na nje,
limeshachujuka hiloo! Labda dawa ni kule kuligeuza kulikokuwa ndani kuwe nje,
kwasababu hivi sasa hali ilivyo haina cha ndani wala nje kote ni sawa. Wenye
macho watizame na wenye akili watafakari kwani nahisi tumekanyaga mdudu.
From miram3
1 comment :
Also visіt mу web-ѕite :: more info about tantric massage
Also visit my web-site :: erotic massage
Post a Comment