Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, March 21, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-98




Shahidi alipoona mwenyekiti kashikilia simu, akajua sasa kila kitu kimeharibika,

Akawa anamuangalia mwenyekiti kwa mashaka, akiangalia vidole vya mwenyekiti vikianza kugusa batan za simu, ili kuanza kupiga namba, kama vile anavyoangalia adui wakati anataka kufyatua risasi, mara nyingi unaangalia kidole kinachovuta kiwambo cha kuruhusu risasi itoke...hapo ndio unatakiwa uchukua maamuzi ya haraka.

Shahidi kwa haraka akasema;

‘Mwenyekiti hivi wewe huoni , kama usipoufahamu ukweli wote uliobakia inaweza ikaja kukuathiri wewe kisiasa maana ukweli umepotoshwa na nia ni kukuharibia wewe kisiasa na kiuchumi, hulioni hilo….’akasema shahidi na mwenyekiti akawa kama hajali

Vidole vya mwenyekiti vikabonyesha namba au sehemu tatu....huenda sasa ....

‘Najua mwenyekiti unatimiza wajibu wako kisiasa, lakini ninaomba unipe muda kidogo tu nimalizie kazi yangu, nina uhakika hata wewe mwenyewe utakuja kunishukuruu kwa hilo, …’akasema mzungumzaji na kunigeukia mimi, kama vile anaomba msaada kwangu. Mimi nilikuwa kimia tu…

 Shahidi sasa akakata tamaa …mimi nikaona na mimi nijaribu bahati yangu, hapo nikafunua mdomo na kusema;

‘Baba naomba tumpatie muda, huyu shahid ili aweze kutimiza kile alichokianza, hatujui ukweli wa haya yote, nimependezewa na kazi yake,…mimi naona labda akimalizia kazi yake aliyoianza, tunaweza kumuamini, naomba tafadhali baba usiwaite polisi kwanza, jitahidi waendelee kusubiria…’nikasema

Hapo baba akawa kama anaiweka simu pembeni…

Ndipo huyo mzungumzaji ambaye ni shahidi akasema;

‘Mwenyekiti nashukuru sana kama mtanikubalia ombo langu hilo.., hapa nilipo nipo kazini, nawasiliana na watu wangu wanaonisaidia kwa hili, najua nikitoka nje sasa hivi kwa hali ilivyo ninaweza kukamatwa, lakini muda mchache tu nitapata taarifa muhimu ninayoitegemea,…’akasema.

‘Kwahiyo ina maana huo muda unaoutaka kuikamilisha hiyo kazi, sio lazima utoke hapa, hata ukiwa hapa unaweza kuifanya hiyo kazi yako..?’ akauliza mwenyekiti

‘Ndio mwenyekiti…ikibidi nitatoka, lakini, kwa hivi sasa…’akasema mzungumzaji na kukatiza akiwa anaoma ujumbe pepe kwenye simu yake.

‘Sawa..mimi sijui wao wamesema tukimaliza hiki kikao, watafika, kuna watu wanawahitajia, sasa kwanini, watakuja kutuambia…’akasema mwenyekiti

‘Kwahiyo hawajasema kwanini wanawahitajia hao watu..?’ akauliza wakili wa mume.

‘Wamesema kuna watu wanahitajika kuisaidia polis wapo humu kwenye hiki kikao chetu, wanataka kuja kuwachukua, …mimi siwezi kuwazuia kwani aliyeniambia hivyo sio mtu mdogo…ila yeye kwa kuniamini wamesema tuendee na kikao chetu tu, hadi hapo tutakapomaliza…ila asitoke mtu, au sisi tusiongelee swala la marehemu maana hilo lipo polisi....’sasa akasema mwenyekiti.

Mdada shahid akasema;

‘Najua wao mpaka sasa wanahisi kuwa mimi na mume wa familia tumeshirikiana kulifanya hilo jambo, …muhimu nipate muda wa kutafuta ushahidi wa kuliwakilisha hili jambo kwao…’akasema shahidi  na kabla mwenyekiti hajaongea shahidi akaendelea kusema;

‘Mimi…ninajua baada ya kukamilisha hiyo kazi, haki itatendekea, sasa kama wao kweli wanaoushahidi kuwa sisi ndio tumehusika,..tutapambana kwenye mahakama…’akasema shahidi

Sasa mwenyekiti akawa anashughulika na simu, kuonyesha anawasilian na watu…baadae mwenyekiti akasema;.

‘Elewa nafasi yangu kwa sasa…, hayo uliyoyaelezea hapa yalitakiwa yawafikie wao, je ukisimamishwa kizambani ukasema uliwahi kunilezea haya mimi,  je kisheria mimi nitakuwa kwenye nafasi gani, ukumbuke nilishapewa amri kuwa swala linalohusiana na marehemu tusiliongelee hapa, sisi tumekiuka..’akasema mwenyekiti.

‘Na haya nimeyasikia uliyoyaongea , mimi nitaulizwa je nilipoyasiki hayo kama kiongozi wa siasa nilichukua hatua gani…unaona ilivyo, mimi nitasema nini, nikisema bado nilihitajia ushahidi zaidi , nitaambiwa je wewe ni polisi…’akasema

‘Ni kweli mwenyekiti, mimi naona…basi tuendelee na mambo mengine huku nikifanya kazi yangu, au na hilo siruhusiwi..’akasema shahidi.

‘Tutaendelea lakini ilitaka hili swala limalizike ili tuweze kuwa huru kuendelea na vipengele vingine….’akasema mwenyekiti.

‘Ndugu mwenyekiti mimi ninakuahidi nikishakamilisha hii kazi,mimi mwenyewe kwa wakati wangu nitakwenda kuonana nao, bado kuna mambo machache nahitajia ushahid wake, nipo hapa lakini nayafuatilia mambo fulani fulani…’akasema

‘Sawa hilo …unasikia baada ya kikao, wewe ndio utaongea nao, sisi baada ya kikao tutakuwa hatuna mamlaka ya kumzuia mtu yoyote asiwajibike kwenye vyombo vya usama…’akasema mwenyekiti.

‘Hamna shida ndugu mwenyekiti…’akasema shahidi kwa kujiamini.

‘Najua mwenyekiti unatimiza wajibu wako, lakini kwa jinsi ilivyo, ukitoa kauli yako waje kunikamata, ambacho ndicho hao watu wanakihitajia, itakuwa na nguvu sana kwao, na utaona magazeti yao yatakavyoandika..kisiasa…’akasema

‘Kwahiyo unavyosema hivyo, ina maana leo polisi hawatakukamata au, wakati wameshajiandaa kuifanya hiyo kazi?’ akauliza

‘Hapo mimi sijui, kama wamejiandaa kufanya hivyo, lakini wanatakiwa wawe na jambo la kunnikamatia nalo, hapo ndio wanasita kufanya hivyo hata wao bado hawajawa na uhakika na kazi waliyoifanya,haijakamilika ..na na..’akasema akasita baadae akasema

‘Mimi kama raia mwema nina haki zangu, sawa watasema wananikamata ili mimi nikaisaidie polisi, haya kwanini niisaidie polisi…na hili tukio limtokea lini, ndio wanahaki hiyo ya kuniitakisheria niende kituo cha polisi au wao waje hapa kunikamata, lakini hata mimi nina haki zangu za  kujitetea….’akasema

‘Nikuulize swali wewe unapofanya kazi zako , huwa wakati mwingine unashirikiana na polisi..?’ akauliza mwenyekiti

‘Ndugu mwenyekiti naomba mnielewe ..kazi zangu mimi sishirikiani na polisi ,kuna wakati inabid niombe kibali chao, ikibidi lakini ilivyo,  mimi sikutakiwa kufahamika na mtu kuwa naifanya hiyo kazi,…’akasema

‘Je una kibali cha polis cha kuifanya hiyo kazi..?’ akauliza mwenyekiti

‘Ndugu mwenyekiti inapofika polisi kunihoji lolote kuhusu kibali changu cha kazi, anayeweza kuyajibu hayo maswali ni bosi wangu, ndio maana sitaki polisi waje kunikamata kwa hivi sasa…na kwa hili kama nilivyoeleza tokea awali, sijapata kibali kwa bosi wangu, au sikutumwa na bosi wangu, hii ni kazi yangu binafsi, nimeifanya hili kazi kwa manufaa yangu...’akasema.

‘Sasa kumbe hata kibali cha kufanya kazi kama hiyo huna huoni bado unanitia mashaka..?’ akauliza mwenyekiti

‘Kwa kauli yako hiyo mwenyekiti hata mimi unanitia mashaka, kwanini unachelea kusubiria, wakati hayo ninayotaka kuyafanya pia ni kwa masilahi yako…ninahis ni kwanini, lakini hisia zangu nazo zinaanza kuingiwa na mashaka..’akasema

‘Mimi natimiza wajibu wangu kwa mujibu wa sheria,…’akasema mwenyekiti.

‘Ni sawa, je ni kweli kila kazi unayoifanya inafuata mtiririko huo, tuseme ukweli ndugu mwenyekiti,..angalia mwenzako aanavyocheza rafu, na bado haonekani kuvunja sheria ni kwanini, ni kwavile kwenye uwanja wenu huo, kuna mambo mengina yanakubidi tu ufanye hivyo, kwa masilahi ya uma...’akasema

‘Kwahiyo wewe unataka na mimi nifanye hivyo…?’ akauliza mwenyekiti

‘Mimi sina mamlaka ya kukushauri ufanye hivyo ndugu mwenyekiti, ila nakuelezea hali halisi…’akasema

‘Kwa mimi nilivyoona,  ninahisi umeifanya hiyo kazi hasa hasa kwa manufaa ya mpenzi wako wa zamani,..na hapo ndio inaigusa familia,..unielewe hapo,..vinginevyo ,eeh, hili jambo lisingelizungumziwa hapa,..kwahiyo hayo yakusema kuna mkono wa siasa, na unataka kulifanya hivyo ili hata mimi nifaidikie …hapana, siliungi mkono kinadharia,…’akasema

‘Lakini kivitendo, nafahamu sana hizo mbinu zipo, lakini sio kwangu,..sasa ngoja nione, kuna kitu kidogo nataka nikiweke sawa, ngoja niongee na wahusika, wanipe muda kidogo…’akasema na kuanza kupiga simu, aliongea kwa muda, kukawa kama vile hilo ombi linakataliwa, na baadae akamaliza na kusema;

‘Unajua nimegundua kitu..wewe kwa jinsi ulivyompenda mwenzako, ulikuwa tayari kufanya lolote kwa ajili yake, nimeyafuatilia maelezo yako yote, na hasa pale ulipofikia kuacha kazi kwa mtu wako wa kwanza kwa ajili ya kwenda kupambana na wale walioingilia maisha yenu na mipango yenu,na mpenzi wako au sio, wivu ukakutawala, ni kweli si kweli…?’ akauliza mwenyekiti

‘Mwenyekiti unaweza kuliweka hilo, kwa jinsi unavyoliona wewe, lakini kwanini hujiuliza kama nilifanya hivyo kwa ajili yake kwanini niseme kila kitu ambacho kinaweza kumuhatarisha yeye, au mimi ….kwanini sijaficha hu ukweli na nilikuwa na nafasi ya kufanya hivyo…, nimefanya hivyo kukwepesha athari zake ambazo zitakuja kutokea baadae…’akasema

‘Ni sawa nakuelewa sana, hapa nataka kufahamu jambo, kwanini ujitolee kufanya kazi hiyo ya hatari, wakati kisheria ina wenyewe,,…sawa labda ulijihimiza hivyo ili uweze kufuta kashfa alizokuwa nazo marehemu dhidi yako…, na ilionekana ulifanikiwa ..sasa kwanini bado ukaendelea kujiweka hatarini..na hapo ndipo inaonekana lengo lako sasa ilikuwa kumaliza hiyo kazi kabisa, na kuimaliza hiyo kazi ka-bi-sa, ni kuhakikisha huyo mtu hayupo au sio…?’ akaulizwa

‘Ndugu mwenyekiti..majibu ya swali lako, yangeliweza kujibiwa kwenye ukamilifu wa uchunguzi wangu, tafadhali nipeni muda, nina uhakika majibu hayo pia yatawasaidia hata hao polisi….’akasema

‘ Mimi nataka kusema hivi…unajua kila mtu ana ndoto zake, lakini tuwe makini katika kujitolea muhanga kwa nafsi nyingine..halafu unafanya hivyo hata bila kibali..unaona hatari ilivyo…’akasema

‘Ndugu mwenyekiti mengine siwezi kukuambia…kuwa nina kibali au sina…siwezi kuongea kila kitu hapa, kwa …anajua sana rafiki yangu hapa, kwanini sitaki kujielezea zaidi mimi kuhusu kazi yangu…’akasema na mwenyekiti akageuka kumuangalia rafiki wa mke wa familia, ambaye kwa muda huo alikuwa kama anawasiliana na watu wake kwa njia ya ujumbe wa maneno.

‘Sawa umenikatiza …nilitaka kusema hivi, ni sawa unawajibika, ..lakini kwanini usifanye hayo kisheria, na kama unawajibika kwa mtu, je kweli huyo unayewajibika kwake yupo na wewe….., huenda mwenzako anakutumia tu, kwa masilahi yake, hali kama hiyo ni hatari…umeona sasa kinachotokea…’akasema mwenyekiti na shahidi akatikisa kichwa kukubaliana na ushauri huo.

Mwenyekiti akaendelea kuongea….

‘Kwa uhakika zaidi, hebu mwangalie mwenzako, alivyokufanyia wewe naona humfahamu vyema huyo mpenzi wako, kama unavyodai unamfahamu kihivyo, yeye kwa tabia yake, imeonyesha dhahiri kuwa yeye ni mbinafsi, yupo tayari akutumie wewe kwa manufaa yake, na mwisho wa siku anaweza asiwe nawe tena....’akasema mwenyekiti.

‘Ni sawa…lakini…’akasema shahidi na kukatisha pale aliposikia mume wa familia akikohoa kama vile kusafisha koo. Akatulia akimuangalia, akitamani mtu huyo azungumze neno..

Mume wa familia, aliinua kichwa na kumwangalia mwenyekiti, akiwa kakunja uso,wa kutafakari, nahisi kuna kitu alitaka kukizungumza, lakini akawa anasita kukiongea, hakusema neno, alimwangalia mwenyekiti kwa muda, halafu akageuka kumwangalia huyo shahidi, .

Wawili hawa waliangaliana tu, na baadaye akatikisa kichwa kama kusikitika,  halafu akainamisha kichwa chini na kutulia, hakusema neno, na mwenyekiti ambaye alikuwa akiwaangalia wawili hao,…akitarajia kauli kutoka kwa mume wangu, lakini alipomuona huyo mtu katulia tu, akaendelea kusema kwa kumchokoza huyo mtu;

‘Kama ni uwongo kuwa huyu mtu unayemuhangaikia, hana huruma nawe, kama nimemzulia uwongo, huyo hapo muulize, ...kama kweli yupo na wewe mia kwa mia, kama kweli, yupo na wewe au kama kweli yupo na mke wake aliyemu-oa, ambaye kamuoa kwa ajili ya mali, ili tu kujinufaisha, aseme tusikie, uwanja ni wake, ...’akasema mwenyekiti.

Walipoona mume wa familia kakaa kimiya, shahidi aliyepita, akasema;

‘Ndugu mwenyekiti, mimi nafahamu ni kitu gani ninachokifanya, na sikufanya hayo kwa ajili yake tu, nilifanya hayo kwa vile nawajibika kufanya hivyo, kwa ajili ya watu wengi, hata akiwemo yeye, na mungu wa ni shahidi, nimeyafanya hayo , bila kutarajia kitu kwa mtu yoyote…’akatulia

‘Ni kweli…kama ni kweli nilitarajia msaada wa kauli njema kutoka kwake, …naona kama anakusanifu tu…’akasema mwenyekiti akimchokoza mume wa familia.

‘Sasa kama yeye ataona kuwa mimi ni mjinga, sikuwa na maana njema kwake, hilo ni yeye na kichwa chake, na haliniumizi sana kichwa changu,ingeniumiza sana, kama ningelikaa kimiya baada ya kuona hayo yalitokea…’akatulia kidogo halafu akaendelea

‘Nimeyaona yote…lakini sasa, kwa jinsi yanavyokwenda, badala ya kutafuta ufumbuzi, inakuwa kinyume chake, jambo hilo sasa linatumiwa kisiasa, na sio kwa nia njema, bali ni kwa masilahi ya mtu…aheri sasa yangelifanyiak hivyo ili na haki itendeke, lakini sivyo hivyo…, ndio maana nikaamua kuusema huo ukweli kwenu, kwani nafahamu nyie ndio waathirika wakubwa wa kadhia hii yote...kweli si kweli ndugu mwenyekiti’akasema huyo shahidi.

Mwenyekiti, akiwa bado kamuangalia mume wa familia akasema

‘Kweli si kweli mume wa familia mimi sasa hivi nahitajia kauli yako, awali ulijifanya mjanja unaongea sana,…, nataka  nikusikie sasa ukijitetea…’akasema mwenyekiti na mume wa familia alibakia kimia.

‘Ok, ndugu shahidi, ..sasa kama unakubali kusema ukweli na kufichua maovu kwanini usishirikiane na wale walipewa dhamana hiyo na serikali, ambao ni polisi, kwanini ufanye hayo kimiya kimiya, peke yako, huoni kuwa kwa kufanya hivyo ni makosa…au bado unahisi nyie wawili mna makosa?’ akauliza mwenyekiti alipoona mume wa familia kabakia kimia tu.

‘Muheshimiwa Mwenyekiti , nafahamu fika wewe unafahamu vyema hilo ninalolifanya, na sio geni kwako, kuwa kuna mambo mengine hutakiwi kukimbilia kuwaambia polisi kwanza…’akatulia

‘Wewe unasema…’akasema mwenyekiti na watu wakacheka kidogo

Aaah….naomba mwenyekiti nieleweke vyema, nafahamu kwanini huwezi kukubaliana na mimi, lakini kiuhalisia unalifahamu hilo..wakati mwingine, inabidi ujirizishe mwenyewe kwanza, kwani ukikimbilia huko, wao watakachokifanya ni kukushika, wakisema unakamatwa kwa ajili ya kuisaidia polisi, na hata kama hawatakukamata kwa bahati mbaya, wao watakuzuia usifanye uchunguzi wako, ili wao waufanye, kwani ndio kazi yao au sio...’akatulia kidogo, halafu akasema.

‘Ndio ni utaratibu wao, kwa nia njema lakini, wakakushika au kukuzuia, ila wao wafanye wajuavyo wao, kiutalaamu wao, huenda wakafanikiwa au wasifanikiwe kwa kile ulichokianza au kukigundua…’akatulia kama mwalimu anayetaka wanafunzi wake waelewe.

‘Lakini kwa vile wao wanaona ni kazi yao, hata kama itawashinda hawatatka kukubali,..lakini mimi kama raia mwema huenda ningelifanikisha hilo kwa njia zangu za usalama-raia, na kuwarahishia kazi, kwa vile mimi nina utaalamu huo kwa namna ya kijamii zaidi..’akasema

Mweyekiti akamkatiza kwa kusema;

‘Sasa kosa lipo wapi, wewe ukienda kushirikiana nao, ukawaonyesha kile ulichokigundua, kijamii-usalama …itawapa nafasi nzuri kukamlisha kazi yao..au sio…’akasema mwenyekiti.

‘Ni sawa usemavyo mwenyekiti, lakini ukumbuke ushahidi mkubwa walio nao umeshachakachuliwa, na wao, watakuwa wakiutumia ushahdi huo kuwakamata wasio husika na wakifanya hivyo, ndio itakuwa mwanya wa wahalifu kuzidi kujilinda, na ukweli unaweza kupotea kabisa…ni nani ataumia, kama sio upande wako mwenyekiti..’akasema.

‘Usipende kuyafanya hayo kama vile ni mimi nimekutuma, sijakutuma..unanielewa hapo..’akasema mwenyekiti

‘Unajua Ndugu mwenyekiti, nayafanya haya kwa vile nafahamu, sio mara yangu ya kwanza kukutana na vitu kama hivi, wao sasa hivi ukisema mtu wenu yupo hapa njooni mumukamate,..watanikamata, na nikiwaelezea haya, ooh, wewe ndiye tulikuwa tunakutafuta…naenda kusota jela…na hapo kila kitu kitaharibiwa, ukweli utageuzwa, maana bado sijafanikisha,…’akatulia.

‘Mimi kutokana na utendaji wangu wa hii kazi,nimejifunza mengi, kwahiyo sioni kama nafanya kosa, kutokuwaambia yale niliyoyaona, nafahamu wengi mtaona hivyo,...’akatulia

‘Ila mimi nafahamu nafasi yangu kama raia mwema, ni wakati gani niwakilishe hayo niliyoyaona kwao, na muda huo ukifika, utaona matunda yake, sio mara ya kwanza kuyafanya hayo..nakuhakikishia ndugu mwenyekiti, baada ya kukamlisha kazi yangu haki itatendeka, na mwenyewe utakuja kuja kunishukuru, labda hawo wahusika waniwahi na kuniua...’akasema.

‘Na wakiniua ni ajali kazini, ni kama askari kufa vitani, sioni ajabu...’akasema  hivyo baada ya kutulia kidogo, na mwenyekiti akatabsamu na kusema;

‘Ndio hapo unapokosea, labda hao wakikuwahi na kukuua, huoni kwa kusema hivyo unahitajia ulinzi wa polisi,..maana wao ni kazi yao kulinda raia, na kuhakikisha haki inatendeka, na kwa jinsi unavyoongea ni kuwa una wasiwasi kuwa hao jamaa wanaweza kukudhuru, au sio… ni vyema ukajisalimisha kwa usalama, na wao watawajibika kwa hilo, kwani wao wana mamlaka na uwezo wa kukulinda...’akasema mwenyekiti.

‘Una uhakika na hilo ndugu mwenyekiti, kuwa wanaweza kunilinda,  mbele ya hao upande wa pili,…hahaha...’akasema

‘Kwanini nisiwe na uhakika, hao watu hawapo juu ya sheria, au…ni nani hao,…hapana ni wakati raia mnatakiwa muwaamini watu wenu wa usalama, wao wamekula kiapo cha uaminifu au sio…’akasema mwenyekiti.

‘Mwenyekiti nazungumza haya maana mimi katika kazi hii nimekuwa nao japokuwa sipo kwa mujibu wa taratibu zao, nimekuwa nao kwa kupitia bosi wangu ambaye kasajiliwa kisheria, ni kweli wapo wengi watendaji wazuri lakini pia wapo wakosaji wachache wanaharibu kazi njema ya kazi zao,…’akasema

‘Una uhakika gani na hao wachache…’mwenyekiti akataka kuendelea, nahisi alikuwa akipoteza muda kwa makusudi maalumu, anayoyafahamu yeye mwenyewe

Hapo mzungumza akasema ..

‘Ni wangapi wangapi waliahidiwa hivyo kuwa tutakulinda, na sasa tumeshawasahau, kukulinda kwao ni kukuweka jela, wanasema kwa manufaa yako, au manufaa ya jamii, au sio..huko jela kweli ni sehemu nzuri ya kumlinda mtu, ndugu mwenyekiti, ulishawahi kukaa jela…?’ akauliza

‘Hebu muulize binti yako, akuambie ukweli,na ukumbuke yeye aliweka sehemu nzuri, je wote wanaweza kuwekwa sehemu hizo, na je hizo sehemu nzuri, ni nzuri kweli, muulize binti yako atakuambia,

‘Kwa kifupi,…, jela sio mahali pema pa kuishi, kuna hatari zake hasa za kiafya, achilia mbali kuathirika kisaikolojia, huko pia kuna watukutu wasiojali, wao huko wameona ndio miliki yao....sawa ikibidi nitaenda huko, lakini kuna jambo bado nalifuatilia, nisingelipenda kuliongelea hapa kwa hivi sasa na hasa kutokana na hali ninayoiona…, tafadhali mwenyekiti nakuomba unielewe hivyo...’akasema.

Mwenyekiti akamgeukia mume wa familia na kumwangalia, akageuka kuniangalia mimi, halafu akasema,;

‘Kama alivyosema shahidi, hayo ya nani muuaji wa Makabrasha ni mambo ya polisi, na hatutakiwi kimujibu wa sheria, kuyaongelea hapa, kilichotuweka hapa na mambo yetu ya kifamilia, tufanye yale yaliyopo kwenye mipaka yetu, tusipende kujifanya tunajua saana, na kuingilia kazi za watu wengine waliopewa dhamana hiyo na wanao-elewa,…

‘Aheri ya kwako wewe mwenzetu anajua jua mambo hayo, sasa sisi tukiulizwa kwanini, tutasema nini....hilo kwa hivi sasa tuliache…tuwaachie wanaohusika, sasa turejee kwenye msingi wa kikao chetu…au sio mawakili’akasema mwenyekiti na kuwaangalia mawakili.

Muda wote mawakili hao walikuwa kimia…, kuacha wakili wa mume wa familia

‘Ninashukuru tuna watu wetu wa sheria, na wameona juhudi zetu katika kuliweka hilo sawa, kama tunakosea wao watatusahihisha, ila cha muhimu ni kufuata ajenda zetu…

‘Sasa kabla hatujaingia kwenye kipengele kuhitimisha tatizo hili, ili baadae tuingie kwenye hukumu, au suluhu…’hapo akatulia kidogo

‘Unajua sisi kama wanafamilia, kwa kupitia vikao hivi, na sio mara ya kwanza hii, tuna jinsi yetu ya kuhukumu, au kusuluhisha migogoro ndani ta familia, na tumekuwa tukijitahidi tusiende kinyume na sheria za nchi, au sio…mnielewe hapo…’akatulia

‘Mfano mkosaji, kakosea, na hukumu yake ni kulipa alichoiba au kupoteza, tutamuhukumu hivyo, alipe…lakini kuna hukumu zitabakia kwenye mikono ya wanandoa, mfano kama hukumu ni talaka, je ni nani atamlazimisha mume kuacha mkewe wake…, hapo eeh,…sisi tutajaribu kushauri iwe hivyo kama ni lazima lakini mwishi wa siku kazi hiyo ni ya mume na mkewe, japokuwa kama kikao kitaona ni heri ya kutoa talaka au sio…na vitu kama hivyo, naomba mnielewe hapo.

‘Pia naongeza kidogo hapo samahani, kwa vile ukiangalia ilivyo, kinachotizamwa hapa ni mali, watu wamaingiwa na tamaa jinsi gani ya kumiliki mali, isivyo halali, kwahiyo tatizo hapa ni mali, sisi kama wanafamilia, tukiona kiongozi fulani hafai kwa ubinafsi wake, kama kikao kitasema mtu huyo hafai, tutampendekeza mtu mwingine au sio..ndio hukumu zetu zipo kwa mtindo huo.

‘Sasa kwa hili la familia wameturahishia, kumbe wao walikuwa na mkataba wao, ..mkataba ule halali eeh, sio huo wao wa kugushi,…’akasema akimuangalia wakili wa mume.

‘Sasa kama bado wahusika hawajaridhiana na hilo…ila sisi kama kikao tumerizika kuwa mkataba halali ni ule wa mwazo, huu wao wa kugishi hautambuliki, sasa kama wahusika wana pingamizi, sisi hatutakuwa na neno zaidi ya hapo, itabidi swala hilo lifikishwe mahakamani.

 ‘Sasa kama mkataba wa zamani umepitishwa…hapa hakuna hoja, sisi kama kikao, tutafuata mkataba wao, tutaona jinsi gani unavyosema mtu akikosea makosa kama hayo, ambayo yana ushahidi..au sio……’akatulia

‘Lakini kabla ya kufanya hivyo, kabla ya kufikia hapo, najua hadi hapo kuna tatizo..kuna mgogoro, kuna mtu anatakiwa kuwajibishwa kifamilia, au sio…’akatulia mwenyekiti alipoona wakili akiteta na mtu wake, wakawa kama hawaelewani, na mwenyekiti akaendelea kusema;

‘Hata hivyo kikao hiki ni cha familia, tupo wazee, wapo mawakili,..wapo watu walioenda shule…hakuna jambo litaharibika, tutahakikisha kila mtu kapata haki yake na hiyo familia itakuwa na amani, au sio, sisi wajibu wetu ni huo…’akatulia

‘Baada ya kuongea hayo, mimi kwa upendeleo kabisa, ningelipenda tumsimamishe mume wa familia aongee, ajitetee, kwa nafasi yake, na hili hatutaki wakili wake aliingilie kati, kwani kwa hivi sasa kila kitu kipo wazi, ...ukweli umedhihiri, na uwongo umejitenga...’akasema mwenyekiti, na kumwangalia mume wa familia.

‘Mume wa familia kwanza tnahitajia kauli yako je unakubali kuwa mkataba huo ndio halali mliotayarisha wewe na mke wako, kwa ajili ya masilahi yenu., pili je hayo aliyoyaongea mke wa docta ni kweli…?’

Mume wa familia kwanza alitulia kimia,…baadae akainua kichwa, akitaka kumuangalia mwenyekiti….akawa kama anawaza jambo, wakili wake alikuwa kainama tu akisoma kitu kwenye makabrasha yake..

Baadae sana mume wa familia…akainamisha kichwa, …halafu akainua tena..

NB: Naona niishie hapa


WAZO LA LEO: Ni kwanini watu hawataki kuubali ukweli hata kama wamekosea, watu huona ulimi, kuongea sana, kubishana,  kujitetea , au kutetea madhambi yao ndio njia pakee ya kujisafisha, hata kama nafsi inamsuta, je kwa kufanya hivyo tunamdanganya nani…huenda tukashinda au tukapata kwa njia hiyo, je hatuoni tunakula mali ya dhuluma, tunaishi maisha ya dhuluma, tunatawala tukiwa watawala wa dhuluma, …ina maana kila chumo hapo litakuwa la dhuluma! Kiukweli mwisho wa mtu kama huyo hautakuwa ni mwema…

Ni mimi: emu-three

No comments :