Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, March 16, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-96



Binadamu tulivyo, hata ujitahidi vipi, hata uwe mjanja wa kuvumilia usingizi, kuna muda utafika, hasa usiku, ni lazima usingizi utakutinga,..inafika sehemu unashindwa kabisa kuvumilia na ndivyo ilivyotokea kwangu, lakini ni zaidi ya hapo, hadi leo sijaweza kutambua ni kwanini nilishikwa na usingizi mnzito kiasi kile...’ Shahidi akaendelea kuongea.

‘Japokuwa nilitaka usiku huo nikeshe, ili kuhakikisha mambo yangu yote yamekamilika,  kama nilivyopanga...si nimeshazima mitambi ya kuonyesha matukio,..sasa kwanini nishindwe,...kikwazo ilikuwa ufunguo wa chumba cha Makabrasha...

Sasa cha ajabu,...usingizi mnzito ukanipitia,

Unajua ilikuwaje, inabidi niwaambia kila kitu kwenye sehemu , maana ni muhimu sana..

Baada ya kumaliza shughuli za usafi, kupanga mambo kama alivyonielekeza Makabrasha,..na kuweka vitu vyote kama alivyotaka yeye, maana alitakiwa kukutana na wageni wengi, na miongoni mwao ni mume wa familia, na kila mtu alikuwa na muda wake maalumu...kiukweli nilifanya kazi nyingi usiku huo, bila kupumzika, na sikuwa na msaidizi, hakutaka msaidizi...nikajikuta nimechoka sana.

Niliongea kidogo na Makabrasha kuhakikisha kuwa kila kitu chake kipo sawa, na akaniambia hatanihitajia tena kwa usiku huo, na  yeye akatoka kwenda chini kwenye sehemu ya hoteli kujiburudisha na watu wake.

Mimi sio mtu wa kujiruisha , kunywa kunywa, hapana, mimi naijali kazi yangu, na hata hivyo, siku hiyo kwangu ilikuwa muhimu sana, nilikuwa na mpango kabambe, lazima ukamilike.

 Baada ya hapo ndio nikaingia chumbani kwangu kubadili nguo...sasa kabla ya kufanya hivyo, nikaamua nijilaze kidogo kitandani kupumzisha mwili...na hapo akili yangu inawaza mpango huo wa usiku..., nikiwa kwenye hayo hayo mawazo, nikiwa nimejiegemeza tu,... kidogo kwenye mto, nikiwa nimeweka mikono yangu nyumba na kichwa changu kulalia viganja vya mikono, hapo hapo usingizi ukanipitia.


 Kiukweli, sio kawaida yangu kulala hivyo nikiwa vitani..maana kutokana na mpango wangu huo, hiyo ilikuwa ni vita kufa kupona...…hata sielewi ilikuwaje, ila ninachoweza kusema ni kuwa nilishikwa na usingizi mnzito, ulionifanya nisifanye kazi yangu….

Nilishituka ni asubuhi, na kilichoniamusha ni simu yangu , iliyokuwa ikilia, nilikuwa nimeweka mlio wa kutikisika tu, ...bila kuangalia mpigaji , nikaipokea hiyo simu kwa haraka, 

Nikasikia sauti ya mdogo wa mume wa familia..hapo hapo nikakurupuka na kukaa vyema kitandani...kwa haraka nikamuuliza kuna nini, na hapo nikasikia mlilio ya ndege nje, purukushani za nje, kelele za magari, kuna nini tena hapo, ni  asubuhi 

'Mbona asubuhi hivi kuna nini...?' nikajikuta nime muuliza hivyo,

Ndio akaniambia yupo karibu na eneo la hilo jengo alimleta kaka yake.

‘Oh, kumbe kumekucha...kwahiyo, mpo na kaka yako? ’nikamuuliza huku nikipiga miayo.

‘Hapana, yeye keshaingia huko, mimi nipo mbali kidogo na hapo, ina maana wewe bado umelala…?’ akauliza kwa mshangao, sasa kwa haraka, na aibu ndio nikasimama,kiukweli huu ni uzembe kama ningekuwa vitani, sijui ingekuwaje.

'Hapana mbona nipo macho,...nimechoka tu...'nikamwambia hivyo

‘Sawa mimi nimemlata mara moja na sitakiwi kuonekana eneo hili, vipi mambo yaliendaje..?’ akauliza

‘Mambo gani...eeh, sawa, hamna shida, yalikuwa safi, ngoja tuone itakuwaje…’nikasema

‘Kwahiyo nije kuichukua saa ngapi…?’ akauliza

‘Nitakuambia..usijali…’nikasema, sikuwa na mashaka hata angeliongea sana kwani kule kwenye mitambo nilikuwa nimeweka OFF, na kwa vile kumepambazuka natakiwa kwenda kuweka ON...

Kwa haraka nikainua godoro, pale nilipoficha silaha yangu, nikaiona ipo, nikarudishia godoro kwa haraka, kwani nilihisi kuna mtu anakuja kwa nje, nilisikia mlio wa nyayo za mtu, nikajiweka sawa, nilijua nitakuwa nahitajika kuweka mambo sawa, kwa ajili ya wageni, ...

Hata hivyo hakutokea mtu,  nikafungua mlango kuchungulia kwenye korido, sikumuona mtu, lakini nina uhakika kulikuwa na mtu anakuja muelekeo wa chumba changu. Ni nani huyo kaingia kwenye chumba gani cha karibu, …nikapotezea tu, ila moyo wangu ukawa na mashaka.

Nikarudishia mlango na kutulia kidogo, nikamigia mdogo wa wa mume wa familia, nikamuuliza kama kaka yake ameshaingia ndani, nikaona haina haja ya kukaa na hiyo silaha tena , maana kazi yake ilikuwa ni usiku, kwahiyo nikaona nimrejeshee, yeye  akasema;

‘Kwa hali ilivyo hapa nje, huwezi kunipa hiyo silaha, je usiku wa leo hutaihitajia…?’ akaniuliza?’ akaniuliza.

‘Kazi muhimu nimeshaimaliza, ila kuna kitu nataka kukufanya, kama itawezekana, lakini sio muhimu kwa sasa nilishaongea na kaka yako, kama akiwa mjinga na kusaini huo mkataba atakuwa kaharibu kila kitu, yote inategemea yeye, vinginevyo, kwa vile ni mchana siweze kufanya lolote na hiyo silaha, kwahiyo sio muhimu kwa mchana wa leo, lakini kama unaona hakuna usalama huko nje, basi ngoja ikae kae huku, huenda nikaihitajia...’nikamwambia.

‘Sawa hamna shida, kama alisema atafanya kama mlivyokubaliana, sijui mume kubaliana nini na kaka, ila yeye aliniambia kila asubuhi nije kuichukua, sasa ni bora muwasiliane naye,...’akasema na mimi nikamwambia.

‘Tutaongea baadaye, je unamuonaje kaka yako, yupo safi, anaweza kufanya niliyomuagiza afanye au bado kalewa na madawa ..mimi sijui hizo dawa kwanini wanampatia, anakuwa kama zezeta...?’ nikamuuliza, akasema;

‘Yupo safi, sikuona tatizo lolote kwake...nahisi hawakumpatia hizo dawa, kwasababu wanampa pale anapokuwa kachanganyikiwa, ili kumfanya alale, au sio, na sasa hivi huwezi kufahamu kuwa ndio yeye, nahis ni kutokana na mambo yenu, ..mimi sijui…’akasema na mimi nikakata simu…nikaenda zangu kuoga na kujiweka sawa, kiofisi zaidi, nilimpigia simu mume wangu, kumtakia hali…ili niwe nauhakika kama bado ana msiamo wake wa kuja huko kijijini;

‘Mume wangu haujambo, samahani sikuweza kukupigia simu usiku nilichoka sana, na simu inakuwa haina chaji, ila naendelea vyema, usiwe na wasiwasi..’nikasema kazi...’nikamwambia.

‘Una uhakika,…ina maana huwezi hata kuazima kwa mtu ukanitakia hali, mimi nataka kuja huko kukuchukua, ili ukakutane na docta mmoja mwenzangu....’akasema.

‘Kwanini, nilishakuambia sina tatizo la docta, ni matatizo yangu, ..na nina imani hivi sasa nitayamaliza, nitakwua, sawa..hata simu naona imeisha chaji  ...’nikamwambia.

‘Sawa, uonavyo,..ila ni lazima nije huko...’akasema na tukamalizana hivyo

  Kiukweli mume wangu alinijali sana, alinionyesha mapenzi yote tena ya dhati lakini sijui niwaelezeje, akili na mwili wangu wote ulikuwa kwa…ndio hivyo, asiyekuthamini hawezi kukuelewa...’akasema na kumwangalia mume wa familia ambaye alikuwa kainamisha kichwa chini kwa hivi sasa, lakini kaka kwenye kiti upande akimgeukia muongeaji.

‘Hata hivyo, kama isingelikuwa Makabrasha, na huyo mpenzi wangu wa asili kuja kuniharibia mipango yangu, mimi ilishafikia hatua, nikaamua kuwa huyu ndiye mume wangu nitajitahidi kumpenda hadi siku ya mwisho, lakini ghafla ndio akaja mume wa familia na matatizo yake, ikabidi niwe mtu wa kumliwaza, kumuhangaikia, kuwahangaikia yeye na familia yake, hawajui tu….

Swali wengi watauliza iliwezekanaje mimi kuishi na mume na huku huyu mume wa familia anakuja kwangu…iliwezekana sana,…lakini sio kila siku,…na tulijitahid sana kuhakikisha hakuna anayelifahamu hilo, aliyeweza kulifahamu hilo ni huyu Makabrasha baada ya kuwekeza vitu vyake.

Kuna kipindi mume wangu alinishuku…unajua tena binadami…yeye aliona kuna mabadiliko niliyokuwa nayo, lakini kwa vile mimi naifahamu kazi yangu vyema niliweza kumficha kabisa kuweza kunifahamu undani wangu…, japokuwa moyoni nilikuwa naumia sana, na sikuweza kumwambia mume wa familia kuwa mimi naumia sana kuendelea kumdanganya mume wangu...

Wakati nawaza hayo, nikasikia tena mtu akitembea kwenye korido, na mimi nikafungua chumba haraka na kutizama nje, nikaona mtu akingia kwenye moja ya chumba kilichokuwepo mbele yetu, sikuweza kumuona vyema, alikuwa ni mwanaume,ilikuwa ni kitendo cha haraka,...

Yeye...aliingia kwenye chumba kilichokuwa bado kwenye matengenezo, kilikuwa hakijamalizwa, nikahisi huenda ni mmoja wa mafundi, kaamua kuwahi, lakini kwa uhakika, nikaona niende nihakikishe. Lakini sikuwa nimevaa vizuri kutoka nje, …

Nikarudi ndani kidogo na kuvaa nguo za kikazo, nilifanya haraka haraka, nikatoka na kwenda hadi kwenye kile chumba, sikuona mtu, nahisi huyo mtu alishatoka, lakini atakuwa kafanya haraka sana, na atakuwa ni mwepesi sana, ila kulikuwa na dalili zote kuwa huyo mtu aliingia hapo, na kutoka. Nikatoka kwenye kile chumba na kuangalia sehemu zote hakukuwa na mtu maeneo ya karibu, nikajaribu kuangalia kila pande, lakini sikumuona huyo mtu.

Ili kuwa na uhakika zaidi nikawapigia walinzi kuwauliza kama kuna wafanyakazi wa ujenzi wameshawahi asubuhi, wakasema hawajafika. Hapo nikaingiwa na wasiwasi, na afadhali kama mitambo ingelikuwa ON, ningeliweza kujua ni nani, kwa kwenda kuangalia huko.

Mimi nikaondoa wasiwasi, nikajiandaa na kuelekea ofisini kwangu. Kabla sijafika huko, nikapitia chumba cha mitambo ya usalama, nikaingia na kuweka ile mitambo ON, halafu kwa haraka nikarudi ofisini kwangu....

Nilikuwa na ofisi yangu na humo nilikuwa kama mhasibu, mtunza masijala, na pia ni katibu muhutasi wa Makabrasha, kwahiyo utaona jinsi nilivyokuwa na kazi nyingi. Na hapo ndipo mara nyingi nakaa kama hakuna kazi nyingine. ni ofisi iliyokamilika kila kitu, komputa simu, mafile..nk.

Ofisi yangu hiyo ipo mbali kidogo na ofisi ya Makabrasha, ile ni kwenye korido moja. hiyo ni ofisi wakati nafanya kazi za kuweka kumbukumbu, ila nikiwa nafanya kazi za ukatibu muhutasi, huwa ninakuwa kwenye ofisi kubwa karibu na Makabrasha. Katika maswala ya usafi yupo mtu anafika kufanya hiyo kazi lakini kipindi hicho alikuwa likizo, kwahiyo nilikuwa na kazi kubwa ya usafi,na kazi nyingine....

 Hata hivyo kazi kubwa nilishaifaya usiku, nikapitia pitia sehemu muhimu na kuhakikisha kuwa zipo safi, baadaye nikataka kwenda  chumba cha Makabrasha, nilifahamu wakati kama huo yeye na rafiki yake yaani mume wa familia watakuwepo kwenye chumba cha maongezi, wakipata vinywaji, kabla hawajaingia ofisini .

Kumbuka mume wa familia anatambulikana kama ni mgonjwa, na jinsi gani aliingizwa humo bila watu kufahamu ni kitendawili, au sio..lakini kwa Makabrasha hiyo iliwezekana, maana hata mdogo wa familia alipomleta kaka yake hapo, anasema alimleta lakini akiwa kama sio yeye…

 Muda wangu muhim ni huo, wakati wanazungumza mambo yao ya mikataba, nawafahamu sana taratibu zao kila wanapokuja kuonana, na wakikutana hivyo ndipo nafasi ya mume wa familia ya kupata kinywaji, kwani akitoka hapo anatakiwa kuigiza kuumwa...na ukumbuke kufika hapo sio mara ya kwanza..kuna ..haina haja kuwaelezea hilo,…muhimu muelewe kuwa hiyo sio safari ya kwanza kwa mume wa familia kufika hapo, tena akiwa mgonjwa.

Nilifika ofisi ya Makabrasha nikaona kafunga na ufunguo, kama nilivyotarajia,...huwa hataki kufanya makosa, chumba chake kama hayupo huwa kimefungwa, na hakuna mtu anaruhisiwi kuingia kama mwenye hayupo, hamuamini mtu, hata mtoto wake mwenyewe haruhusiwi kuingia hapo kwenye ofisi yake kama hayupo.

Hata mimi sina ufunguo wa chumba hicho wa akiba. Sikuwa na kazi kubwa kwenye chumba hicho, kwani usiku nilishakifanyia usafi, haikuwa na haja ya mimi kufanya usafi mwingine. Na hata yeye alishaniambia hanihitajii ofisini kwake mpaka aniite,kwahiyo haikuwa na haja ya kuingia tena humo, nikarudi ofisini kwangu

Nikiwa pale, nikapigiwa simu, na mtu ambaye hakunitajia jina lake, akaniambia;

‘Acha hayo unayokusudia kuyafanya, kwani tumeshakujua njama zako, kama utaendelea na mambo yako hayo,utakuja kujuta..ondoka kwenye hilo jengo haraka, ...’halafu simu ikakatika.

Mhh..hapo sikuelewa kitu, kwanza huyo mtu ni nani, na namba aliyopigia ni ngeni kabisa hata nilipojaribu kuigundua kama imesajiliwa kwa jina gani, ilionekana haijasajiliwa, ni nani, ni sauti ngeni kabisa, na..hata sauti ilionekana kama ya kuigiza, maana ilikuwa ya kukwaruza kwaruza, nahisi kaweka kitu mdomoni kuzuia sauti halisi, ...sikusema neno.

Kiukweli kutokana na kazi zetu vitisho kama hivyo tumeshavipata sana, na mara nyingi nina hulka yangu kuwa mtu mwoga hutanguliza vitisho, na mtu kama huyo hana lolote, mtu jasiri ni yule, anayetanguliza vitendo.

Na wakati nimetulia nikiwaza cha kufanya, mara simu nyingine ikalia, hii ilikuwa ya aliyekuwa bosi wangu, akaniambia yeye anaondoka,..kurudi ulaya masomoni

‘Sawa. Samahani nimeshindwa kuonana na wewe, lakini natumai mambo yanakwenda vyema, na mtoto wako umeshampata...’nikamuuliza.

‘Mtoto sijampata, licha ya kuwa nimewatimizia mambo yao yote, wameniambia nitakutana naye huko uwanja wa ndege, kwahiyo hapa nilipo sina amani kabisa, ila hawanijui tu, huyu mtu Makabrsha, nitamfanyia kitu hataweza kunisahau, kabla sijaondoka...’akasema.

‘Mimi nina uhakika mtoto utampata na yupo salama, huyo anayekaa naye, ni dada mwema sana anafahamu jinsi ya kulea watoto, nilimtafuta mwenyewe, niliambiwa nimtafute, kwahiyo kwa usalama wa mtoto wako acha iwe hivyo, unasikia, watakueletea huko uwanja wa ndege, usiwe na shaka na hilo...’nikasema.

‘Kwahiyo wewe upo wapi?’ akaniuliza.

‘Usijali, nakutakia safari njema, ukirudi natumai mambo yatakuwa yamebadilika,...’nikasema na kukata simu.

Baadaye nili-itwa na Makabrasha, nikaenda ofisini kwake, alikuwa peke yake, sikumuona huyo mgeni mwingine, ...sikuuliza, kwa makusudi…, yeye akasema;

‘Jamaa yako ameshafika, yupo wash-room,…. nimekuita mara moja, kuna kumbukumbu zangu sizioni kwenye mtandao wetu, na kwenye laptop ambay ndiyo ina namna ya kunasa vitu na kumbukumbu muhimu…neno lake la siri limebadilishwa, hatuwezi kuingia kwenye laptop,…hujui kama umeharibi kila kitu, ..niambie sasa ni wewe, je umefanya nini huko, unajua ile ndio kila kitu, mtoto wangu anasema anakushuku ni wewe…’akasema

‘Nimefanya nini..mimi…hapana, …unasema ni mtoto wako kasema hivyo, kuwa ni mimi nimefanya hivyo, na wewe ukamuamini….oh…ina maana wewe unanishuku mimi, kwa vipi…nimekuwa na wewe hapa kwa muda gani, kwanini nifanye hivyo,…sikiliza kama wewe unamuamini sana mtoto wako, kuliko mimi, ni sawa, lakini je wamfahamu huyo mtoto wako alivyo, mangapi anayokufanyia nyuma ya mgongo wako mimi nayafahamu, lakini naamua kumtunzia siri zake ili…’nikasema

Hapo akanikatisha na kusema….

‘Sikiliza mimi nakuambia alichoniambia yeye, unasikia, ..yeye kasema huenda ni wewe umeweza kuingia kwenye komputa ya kuhifadhi kumbukumbu na kuziharibu, maana ni nani angeliweza kuingia huko,…..hebu niambie ukweli,mimi ninakuamini sana wewe na haya nayafanya pia kwa jili yenu, mbona hamnielewi…’akasema

‘Mimi nakuelewa sana, wewe na mtoto wako…zaidi ya unavyofikiria wewe…’nikasema

‘Unanielewa kivipi eeh!..sikiliza mimi, sitaki tuje kukosana, unanielewe, tumetoka mbali jamani..huu ni wakati muhimu sana wa kuwa kitu kimoja, kwanini mnataka kunivuriga eeh, mtoto…sasa wewe….sikiliza mimi sitaki nije kuwaumiza nyie watu, nyie ni watu  wangu muhimu sana katika kulikamilisha hili, hivi mnafahamu wenzetu wamejipangaje..hamjui ...’akasema na mara simu yake ikalia, akaniangalia na kusema;

‘Ondoka tutakuja kuongea badaye, na kama ni wewe unahusika na hayo, kama anavyodai mtoto wangu,…kasema ana ushaidi,…sasa kama akinileta huo ushahidi, mimisizani kama nitaweza kuvumilia, unanifahamu nilivyo…., hutaamini nitakachokufanyia, nitakufanyia jambo ambalo hutaweza kulisahau maishani mwako, na utajua, kuzaliwa…sitajali urafiki wetu..’akasema

‘Sawa, …ukweli upo wazi, muulize vyema huyo mtoto wako, huyo anataka kukuonyesha kuwa yeye ni nani, anataka kukurithi ukiwa hai, hata wanawake wako,  ..kwanini huelewi…nisingelipenda kuwagombanisha, unasikia….’nikasema, na niliposema hivi nikaona kama uso unakunjama kwa hasira, halafu akasema

‘Huyo nitashughulika naye, ..huyo niachie mimi…nimeshamuelewa …, ila nilitaka kujua ukweli kutoka kwako, haya ondoka….ila sikia, kama ni wewe kweli, maana nitajua tu, usije kunilaumu…’akasema.

‘Mimi sijui unachokiongea, nitawezaje kuingia kwenye komputa na kuharibu hizo kumbukumbu, mimi sina ujuzi huo, na hapo huoni ...anayeweza kufanya hivyo, ni mtoto wako, kwanini umuamini  mtoto wako, wakati kaonyesha dhahiri dalili za kukusaliti…hivi wataka nini tena kuligundua hilo,...’nikamweleza,

 Mara nikasikia kitu kama mtu anataka kuja kutokea kule chumba cha chooni, na Makabrasha hakutaka huyo mgeni wake anione hapo, akawa ananiashiria nitoke na mimi nikasema huku natembea kuelekea mlangoni;

‘Mimi nahisi aliyefanya hivyo ni mtoto wako huenda kazificha hizo kumbukumbu kukukomoa, kwa vile hutaki kukubaliana naye, sasa ananitupia lawama mimi, ili kutukosanisha..nia yake ni hiyo hiyo unaifahamu wewe., hebu fikiria hilo kwa makini...’nikasema na yeye akakunja uso kama anawaza, na kuniashiria nitoke humo ndani haraka, akiashiria kwa mkono

Mimi nikatoka, na wakati natoka, hadi sehemu ya mapokezi ya ofisi hiyo, huwa mimi nakaa hapo kama kuna wateja maalumu, ila kwa leo sikutakiwa kukaa hapo, na mara mlango wa chooni ukafunguliwa akatokea mtu, ..

‘Mbona sio mume wa familia huyu…ni nani huyu…’ nikajikuta nikijisema moyoni,

Kilichonifanya niwe na mashaka zaidi ni jinsi ya utembeaji wake, kwa jinsi nilivyomzoea mume wa familia ningelimgundua kwenye utembeaji, lakini haikuwa hivyo, ila…kutembea kama kuchechemea, kuonyesha ana tatizo mahali,..

Kama ni mume wa familia basi wamefanya utundu wa hali ya juu, mpaka mimi nimeshindwa kumgundua, huyo mtu hakuniona, kwani alitoka kwa haraka na kuelekea kwenye mlango wa ofisi ya Makabrasha na kuingia huko. 

Utembeaji wa kuchechemea, lakini mwendo ni wa kasi…huyu mtu keshapona hivyo…nikacheka kimoyo moyo..

Mimi nikatoka humo haraka, na kuelekea ofisini kwangu, ...sikuhitaji silaha kipindi kama hicho, ingenisaidia kama mume wa familia angesema hataweza kuifanya hiyo kazi niliyomuagiza, nilitaka akatae na kucheleweza kuweka saini kwenye hiyo mikataba, ili niweze kusafisha kila kitu kwenye kumbukumbu zao, nilijua humo ndani kwa Makabrasha huenda bado kuna kumbukumbu humo, nikawa nimepumzika nikifanya kazi zangu zingine.

Sikuonana na hawo watu, nikawa na kazi zangu zingine za kiofisi hadi mchana, na muda ukafika wa mimi kuondoka kurudi sehemu ninapolala, nikawasiliana na Makabrasha kwenye simu kuwa mimi natoka, na yeye akajibu kwa mkatao kwa kusema;

‘Sawa...’ na kabla hajakata simu akasema;

‘Natakuhitajia baadae...usije kuondoka…’akasema kwa sauti iliyonitia wasiwasi, nikafahamu labda, kama kweli mume wa familia kafanya hivyo, basi kuna kutokuelewana, nikahisi huenda zoezi limakamilika.

***********

Nikaelekea chumbani kwangu ninachojipumzisha, nilipumzika hapo nikiwa na mawazo ya kutaka kufahamu kilichoendelea huko, na baadaye nikarudi ofisini kwangu, baadaye nikampigia simu mume wa familia, simu ikawa haipatikani.

Kiukweli hapo nilikuwa na mashaka sana….baadae nikaona ni kwani ni nisiongee na Makabrasha mwenyewe,..

Nikafika ofisi kwake, …

‘Bosi vipi mambo yalikwendaje…?’ nikamuuliza

‘Bado….’akasema hivyo tu

‘Bado kwa vipi…?’ nikamuuliza akawa katulia tu,..baadae alipoona nasubiria jibu lake akasema

‘Kikao kimeahirishwa hadi baadae kidogo, tu wako alihitajika kurejeshwa hospitalini kwa haraka. …mambo yameharibika…’hapo akasema kwa hasira

‘Mhh..sasa?’ nikauliza

‘Bwanaeeh…hebu ondoka, …’akasema hivyo, hapo nikajua kumbe mambo hayakufanikiwa, na ndio nilikitaka, na wakati natoka, yeye akasema;

‘Ni lazima zoezi hili likamilike leo, kwa vyovyote iwavyo vile....sijui kwanini alichelewesha kuweka sahih hadi anaitwa huko hospitalini, mjinga sana huyo mtu wako..’akawa anaongea kwa ukali

‘Pole…labda haitawezekana kwa sasa…au..?’ nikasema.

‘Leo ndip mwisho,…hakuna baadae…na hili litafanyika, hanijui mimi, labda sio mimi..hawajui mimi nasubiriwa, hawajui, nilivyo kwenye wakati mgumu…zoezi hili ni muhimu sana hadi kwa wakubwa zangu…sitakubali lisifanikiwe, kabisa…jamaa yako ataniona mbaya, asipofanya hivyo, kwanini yeye..na hajui umuhimu wa hili…’akasema.

‘Haya utaniambia kinachoendelea mimi naondoka..’nikasema

‘Ondoka, msinichanganye, ila….bado sijamalizana na wewe, unasikia..ondoka, sitaki ni…basi ondoka…’akasema  hivyo, niliondoka.

*********

  Baadae nilitingwa na shughuli nyingine ikabidi nitoke kabisa kwenye hilo jengo, ..nikitoka humo nakuwa mtu mwingine kabisa,..nilitoka kwenda kununua vitu vya ofisi…, baadae nikarejea kwenye hilo jengo, nilihisi mwili ukinisisimuka, sikuelewa ni kwanini, nikawauliza walinzi kama mtoto wa Makabrasha alifika, wakasema hajafika siku nzima ya leo.

Kiukweli huyu mtu akiwepo, sina amani,… nikashukuru mungu, na nilipofika kwa Makabrasha akawa hayupo sawa vile vile…, nahisi ni kwa vile mume wa familia alimkatalia kusaini huo mkataba, na hakutaka kuongea na mimi kama alivyotaka asubuhi. Mimi sikujali, nikaingia kwenye chumba changu, nikahakikisha ile silaha bado ipo.

Silaha ilikuwepo pale pale, sikuigusa, maana nilikuwa mikono mitupu, nilikuwa mwangalifu sana kuigusa ile silaha, nilihakikisha kuwa siigusi mpaka niwe nimevaa kinga kwenye mikono yangu.

Nahisi hapo ndipo nilipofanya makosa..ya kiutendaji…, kwani ukumbuke, kuwa nilishaweka ile mitambo ya kuangalia matukio ya humo ndani, ON, kuruhusu kuonekana kwa matukio yote kwenye hilo jengo, na wakati naangalia hiyo silaha, sikukumbuka kuchukua tahadhari hiyo…, kwahiyo ni lazima itaonekana.

Ilipofika jioni mambo yakaanza, nikawa napilika pilika za hapa na pale, na nilitaka nihakikishe kuwa mkataba huo hausainiwi, hata kama mume wa familia atakuja tena ...ndilo lengo langu kubwa kwani yale yaliyokuwa yakitushinikiza kufanya hivyo, nilishayaharibu, atatushinikiza kwa jambo gani sasa.

Yawezekana huenda wana kumbukumbu hizo sehemu nyingine. Na ndio nilitaka nipate nafasi niweze kuingia chumba cha Makabrasha wakati hayupo...na ili hilo lifanyika ni vyema mtoto wa huyu mzee asiwepo.

Baadae…nikajaribu kumpigia mtoto wa Makabrasha ili kuhakikisha kama kweli hatakuja, na simu yake ikawa haipatikani,...nilijaribu simu yake nyingine ya siri, hata hiyo ikawa haipo hewani.

Baadae nilipata taarifa kuwa mume wa familia keshafika tena

Hapo mapigo ya moyo yakawa yanakwenda mbio, nifanye ili kulizuia hilo, nikafuatilia nikajua sasa wapo kwenye maongezi ya kushawishiana, ..hapo ilikuwa jioni ya kuingia usiku.

Siku waliongea muda mrefu..kubishana na ..nilijua itatokea hivyo, kwani nilishamshawishi mume wa familia asikubali,…na hapo ndio nikajiwa na maamuzi, maana hili jambo lisiposimamishwa, basi haitawezekana tena, ni lazima jambo lifanyike.

 Hatua ya kwanza niliyoifikiria ni mimi kwenda kuichukua silaha, sasa silaha nitaichukuaje wakati mitambo ya kuonyesha matukio ipo ON,

Kwahiyo hatua muhimu ni kwenda kuzima mitambo, na nikichelewa najua mume wa familia ataweka sahihi, hataweza kuhimili mikiki mikiki ya Makabrasha, haraka nikaelekea chumba hicho cha mitambo…. Ili nikazime..

 Bado nilikuwa na ufunguo wa kile chumba, nilikuwa bado sijaurudesha huo ufunguo kwa Makabrasha, huo ufungu huo ulikuwa nakala ya Makabrasha..japokuwa ana nyingine ya akiba, anaiweka anapojua yeye…ufunguo huo nilikuwa nimemuomba mapema sana, kuwa nataka kufanya usafi huko kwa kipindi kile hakuwa na wasiwasi na mimi, si anajua mimi sifahamu chochote kuhusu hiyo mitambo, au komputa.

Nilipofika kwenye hicho chumba, nikaingia na kuweka OFF kuzuia mitambo isione matukio, nikaingia kwenye komputa na kufuta matukio ya nyuma tangu pale nilipoweka ON, ,..ni lazima nifanye hivyo la sivyo mtu akija kutafiti, atagundua mtu aliyeingia mwishoni ni mimi…
Sikuwa na muda wa kuwachungulia maana ukiwemo humo unaweza kuona vyumba vyote, sikutaka kuingia huko kutokana na muda…

Haraka nikarudi ofisini kwangu ili niweke mambo yangu sawa kabla sijawaingilia Makabrasha na mume wa familia, nilitaka nikiwaingilia hapo nipo nimejiandaa silaha ipo mwilini,..kama ni kutumia nguvu basi itafanyika hivyo…lakini ni lazima hilo zoezi lizuilike leo, mikataba hiyo isisainiwe, na ikibidi niwapigie simu polisi aje, waone uozo wa huyu mtu.

Unajua..nayafanya haya nikijiamini kuwa zile kumbukumbu za picha zake za kashfa nimeshazifuta kwa watu wote…sikuwa na uhakika kama kuna nyingine lakini, vyovyote iwavyo, hilo zoezi liwe mwishi, kwani nilishakuwa na ushahidi wa kutosha wa kuonyesha uhalifu wa huyu mtu…

 Pia ukumbuke niliwahi kumuambia mume wa familia, akiwa anaongea na Makabrasha ahakikishe simu yake inachukua maelezo yote, na nilitaka wakati nawavamia niwahi kuchukua ile simu yake na ya Makabrasha anayohifadhi maongezi yake na watu, ili iwe ni ushahidi.

Yote hayo yataweza kufanyika kiurahisi kama mtoto wa Makabrasha hatakuja, lakini akifika, itakuwa kazi nzito kidogo, hata hivyo, nilishajipanga nipambane nao.

Sikujali tena kwa ni hadi hapo, nimeshafanya mengi ambayo yatanifanya mimi na Makabrasha tusielewane tena, hasa akija huyo mtoto wake, na kumuonyesha kuwa ni mimi ndiye niliyefuta mambo yake kwenye kumputa ya kuhifadhi uchafu wake, kama atakuwa na ushahidi wa kufanya hivyo, sikuwa najali tena....

Leo ni leo…

NB, …Ngoja nimalizie…

WAZO LA LEO: Kila jambo utakalolifanya au ukiwa na nia ya kufanya jambo, usisahau kuwa kuna mwenye mamlaka ya kukupa pumzi,nguvu, na uwezo na uhai wa kulifanya hilo jambo liwe la jema au la ubaya. Wengi twajiona tuna mamlaka hayo, hadi kufikia kusema ‘unajua mimi ni nani..’ au ni lazima nitafanya, au lazima itakuwa, jeo ni nani anayefahamu kesho ya mtu….


Kumbuka kusema nitafanya hiki au kile mola wangu akinijalia…
Ni mimi: emu-three

Ni mimi: emu-three

No comments :