Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, August 3, 2017

DUWA LA KUKU....28


Nilipofika kituoni, nikaanza kuhojiwa tena kwa vitisho, na kuambiwa nitatapelekwa jela, nisipotaja wapi alipo huyo mdada, wakazidi kusema kuwa nisiposma ukweli,  watanifunga, au hata kunitesa, mimi nikaendelea kusema huo ukweli ninaoujua mimi;

‘Mimi sijui wapi alipo na hakuwahi kuniambia anakwenda wapi, ni jambo la kushangaza kwangu kusikia kuwa kaondoka,…?’ nikasema

‘Je kwa mara ya mwisho mlikutana lini na wapi..?’ nikaulizwa.

‘Tulikutana sokoni, tukaongea, lakini hakuwahi kuniambia ana mpango wa kutoroka…’nikasema
‘Alikuwambia ana mpango gani…?’ akaniuliza

‘Aliniambia ana mpango lakini hawezi kuniambia mimi kwasababu sitauweza….’nikasema

‘Kwahiyo kumbe alikuambia ana mpango, si ndio hivyo…?’ akaniuliza

‘Ndio….’nikasema

‘Mpango gani…?’ akaniuliza kwa hasira

‘Hakuwahi kuniambia…’nikasema

 ‘Wewe unasema uwongo, na nimesikia ni tabia yako ya kuficha ukweli, hata kama unaujua huo ukweli, sasa hapa ujue ni wewe mwenyewe kuamua, kusema ukweli, au ukalale jela, unakufahamu jela kulivyo, huko utapambana na watu watukutu, watakufunza adabu, na ukitoka huko hata ukiusema huo ukweli tena hautakusaidia kitu, bora uuseme sasa uwe huru, unajua msema kweli ni mpenzi wa mungu…’nikaambiwa.

‘Lakini mimi nimeshawaambia ukweli, mnataka ukweli gani zaidi, niambieni huo ukweli mnaoutaka nyie ni upi, na mkiniweka jela  na hali kama hii, mtakuwa mnanionea bure…’nikasema.

‘Utajua wewe mwenyewe huko jela, watu wanajifungulia huko, sembuse, wewe, nakuambia usiposema ukweli, utakuja kujuta,…’akazidi kusema kwa ukali, na mara akaingia jamaa mmoja, usoni, kakunjamana kwa hasira, kifua ni cha wale wainua vyuma, akaniangalia, mpaka nikahisi mwili ukinisisimuka kwa uwoga.

‘Unamuona huyu, huyu ndiye atakuuliza maswali, na ukijibu uwongo, atajua jinsi gani ya kukufanya, kama hutatoka hapa huwezi kutembea tena, shauri lako, ulishawahi kuwekewa nyoka mdomoni, um-meze, huyo anayo huyo nyoka, hebu muonyeshe…’akasema na kunizidishia uwoga, na hapo hapo nikahisi kutapika, kichwa kinaniuma , moyo unakwenda mbio.

Yule jamaa akamtoa nyoka kwenye mfuko wake, na kunielekezea mimi, unajua kuogopa, nilitoa jicho, nikahisi mwili umekufa ganzi,…nilipanua mdomo kupiga yowe, na jamaa akataka kuingiza yule nyoka mdomoni kwangu…halafu akamrudisha huku kanikazia macho.

‘Haya upo tayari kusema ukweli…?’ akaniuliza nikawa kimia, maana siwezi hata kuongea, na aliponiona nipo kimia, akasema;

‘Haya inuke unakwenda huko ulipokutaka wewe..atakuuliza maswali, na mtamalizana huko,..hutanilaumu kwa chaguo lako…’akasema na mimi nikaganda, siwezi kuongea, siwezi kuinuka.

‘Nimekuambia simama….’akasema kwa sauti iliyonifanya nishtuke na kwa haraka nikasimama…hapo nikasema.

‘Lakini mimi nimesema ukweli wote.., mama yangu alinifundisha nisiseme uwongo, nyie mnataka niseme kitu gani mnachokitaka..?’ nikauliza.

‘Utuambie wapi huyo rafiki yako alipokwenda, au huo mpango aliotaka kukuambia, ni mpango gani…?’ akauliza sasa akiwa kasimama, na mimi nikajibu maneno yale yale kuwa mimi sijui alipokwenda na wala hajawahi kuniambia huo mpango wake.

Ghafla nilistukia nimeinuliwa juu juu kama katoto na huyo jamaa akiwa kanishikilia shingoni, na sikweza hata kuhema, alivyonishikilia shingoni, na kuniinu juu kwa mkono mmoja tu,..ikawa kama ile ndoto ya majinamisi, nikahisi kichwa kikijaa…masikio yanataka kupasuka…siwezi kuhema…macho yakanitoka..nikajua sasa nakufa.

Akaniachia na mimi nikaporomoka chini, na kudondokea sakafuni, nikajaribu sasa kuitafuta pumzi, na hata nilipoipata, nikaishia kukohoa, na kuanza kutapika.. nahisi hata mkojo ulipitiliza, na haikupita muda, giza likatanda usoni, na sikuelewa kingine kilichotokea, kwani nilipoteza fahamu, nilipozindukana nikajikuta nipo hospitalini.

***************

Nilipozindukana, sura ya kwanza kuonana nayo, ilikuwa ya yule kijana wa mfadhili wangu wa kwanza, alikuwa kasimama mbele ya kitanda, huku akiniangalia kwa mashaka, kama ana wasiwasi, ni kama kajiiba kuja kuniona, akainama kuniangalia, na akukutana ma macho yangu.

‘Oh, umeamuka,..vipi, unajisikiaje…?’ akaniuliza

‘Sijambo…’nikasema nikishangaa kumuona huyo kijana hapo.

‘Pole, nimesikia yaliyotokea, hivi kweli, hujui wapi huyo mtu alipokwenda, na niambie walikuuliza nini, na wanataka kujua nini…?’ akaniuliza

‘Mimi sijui wanasema yule mdada, aliyekuwa akifanyia kazi kwenye katoroka, ..na pesa na vito vya thamani, sasa mimi sijui kaenda wapi, na sikujua kuwa atakuja kufanya hivyo…’nikasema

‘Shilingi ngpi..na vito gani hivyo..?’ akaniuliza.

‘Mimi sijui shilingi ngapi, na hata hivyo vito sijui ni kitu gani…’nikasema

‘Ssshit…’akasema hivyo na kugeuka kutaka kuondoka.

‘Mwambie mama yako aje kunisaidia, maana mimi sitaki kwenda jela wataniua…’nikasema

‘Mama…unasema nini, mama, aje kukusaidia wewe, hahaha, labda useme aje kukugandamiza, watu hao hawataki hata kukuona, wewe umekuwa ni chanzo, cha matatizo, wewe na mwenzako, …hata mimi kuja hapa nimekuja tu, niliposikia umeletwa hapa, nikawa napita hapo nje, nikaona kwanini nisije kukuona, lakini,….’akasema na kuanza kuondoka.

‘Sawa, lakini haya yote sijayataka mimi, na matatizo haya kama ni chanzo, labda ni huyo mdada, na nyie mkachangia kuniingiza kwenye mambo nisiyoyajua, …’nikasema hapo akatulia baadae akageuka na kusema;

‘Sikiliza, jaribu sana kujipigania wewe mwenyewe usiwategemee sana hao akina mama, usiwaamini sana ukawaambia kila kitu chako..na…, na usikimbilie kumlaumu mtu, maana kama ni matatizo, unayo, sasa hata ukilalamika, yataondoka hivi hivi kwa kulalamika,.., na hata ukimtupia mtu lawama, kuwa ndio yeye sababu je huyo mtu atakusaidia, jiulize sana hayo. Kwasasahivi dunia ilivyo kila mtu anajali tumbo lake…’akasema

‘Lakini hata wakijali matumbo yako , kuma mambo mengine mtu akiwa na na uwezo wa kusaodia, wengine anatakiwa afanye hivyo,..wewe mwambie mama yako, namfahamu yeye ni mtu mnzuri, ..’nikasema

‘Ni kweli yeye ni mtu mnzuri, lakini kwa wazuri kwake, wewe hukutaka kuwa mnzuri kwake, ..na…wote hata hao marafiki zake, sasa hivi wanakunyosheeni vidole kuwa nyie ndio sababu ya hayo matatizo…’akasema.

‘Lakini sio kweli, mungu anajua mimi sijahusika kwa yote hayo wanayoyasema, wananisingizia tu..’nikasema.

‘Mungu anajua sawa,… sasa…hebu niambie, mungu atakusaidia hivi hivi tu…nimeshakushauri tu..mimi naondoka, lakini kumbuka , pambana na matatizi yako usitarajia msaada wa kutoka kwa wengine , hasa hao akina mama, na ukilemaa kwa jinsi nilivyosikia wewe utaenda kufia jela,…’akasema.

‘Ni bora nife tu, mama yangu si alishakufa, kwani mimi nina tahamani gani tena…’nikasema.

‘Sawa kama ndilo unalolitaka, lisubirie tu linakuja hilo, muda si mrefu.., nina imani wakikupeleka huko jela hutatoka mzima,..na wenzako wataendelea kula nchi, unakumbuka kuna kipindi nilikubembeleza sana uwe mpenzi wangu uliniambia nini,…sasa utanikumbuka kwaheri…’akasema .

‘Samahani kabla hujaondoka, nimesikia na wewe una matatizo, unaumwa, unasumbuliwa na nini…?’ nikamuuliza na akasimama kwa muda bila kunijibu halafu akasema.

‘Matatizo yangu nayajua mimi mwenyewe, na kama ni mama, kawaambia hilo, …sawa, waache wasema wanayosema, ila kiukweli matatizo yangu chanzo chake ni wao, wazazi wangu…’akasema.

‘Kwa vipi, wazazi wako wamekufanya nini..?’ nikamuuliza.

‘Wao wakigombana, wakiishi bila kupendana, mimi naumia sana, mimi nawapenda sana wazazi wangu nataka waishi kwa raha, wapendane kama zamani…’akasema.

‘Kwani hawapendani, kwanini hawapendani, kama zamani…?’ nikamuuliza.

‘Mimi sijui, ningelijua ningafanya kila niwezalo warudie hali yao ya zamani, lakini sijui, na mlipofika nyie mkazidisha matatizo, iliniuma sana, na zaidi nasikia wamegundua kuwa nyie mumesababisha mataizo haya yanayotokea sasa,..niliapa nitafanya nifanyalo mpotee kabisa, lakini nawaonea huruma….’akasema.

‘Unaamini hayo kuwa sisi ndio sababu..?’ nikamuuliza.

‘Niamini nisiamini, lakini ushahidi upo, niliwahi kumuona yule mdada akifanya mambo ya kishirikiana uchi, niliwaambia siku ile ya kikao..na nilipomgundua ndio akawa ananisema umbea kwa wazazi wangu, wakati nilikuwa najitolea kumsaidia, hata pesa za kujikimu, hana shukurani…’akasema.

‘Lakini yaonekana wewe na mdada mlikuwa na jambo lenu wawili…?’ nikasema.

‘Kiukweli ilikuwa hivyo,…kama nilivyotaka iwe kwako, unajua ujana tena..lakini yeye, alikuwa mjanja sio kama wewe, nampenda sana kwa hilo, ana kichwa cha kutafuta, kuona mbali sio kama wewe…wewe ni mtu wa mungu mungu tu,…’akasema.

‘Kwahiyo hicho alichofanya unaona ndio ujanja..?’ nikamuuliza.

‘Hapana mimi siongelei hayo, wizi …hapana, kama kafanya kafanya yeye, sijamsifia kwa hilo, na najua akishikwa ataishia kubaya , lakini hakuwa na tabia hiyo ya wizi, sijui kwanini alifanya hivyo…’akasema.

‘Yeye aligundua kitu gani akakusema kwa wazazi wako..?’ nikamuuliza na hapo, ikawa kama nimemfukuza, akasema;

‘Kwaheri, fikiria yako, usiwazie ya kwangu maana ya kwangu hayakuhusu na hakuna anayeweza kuyatatua..zaidi yangu na wazazi wangu…’akasema na kutembea kwa haraka kuelekea mlangoni, lakini kabla hajafika mlangoni, mara akaingia mama yake. Akashtuka na kushikwa na butwaa…

‘Wewe umefuata nini huku..?’ mama yake akamuuliza.

‘Nilikuja hospitalini, kufuatilia kiliniki yangu…’akasema.

‘Kliniki yako uko huku …?’ akaulizwa.

‘Nilisikia huyu mdada kalazwa hapa, kwa vile namfahamu ndio nikaona nije kumjulia hali..’akasema na hapo mama yake akageuka kuniangalia uso ulikuwa umejaa hasira.

‘Achana na hawa watu mwanangu, unajua ni nini walichotufanyia, ..sasa hamueleweki wewe na baba yako, unajua chanzo ni nani, ni hawa watu, ..ni watu wabaya sana, sitaki hata kuwaona, lakini kwa vile nina maswali ya kumuuliza nimeona nije tu, ubinadamu unaniponza,..haya ondoka hapa …’akasema na huyo kijana wake akatoka mbio mbio.

***************

‘Haya mdada, niliwahi kukuambia kuwa kuna siku utanihitajia, nikakuomba uniambie ukweli ili uwe pamoja na mimi, lakini ukaniona mimi sina maana, unaona dunia inavyokufunza…’akasema.

Sikusema kitu, nilikaa kimia tu, nikiwazia ni kitu huyu mama alitaka nimuambie nikashindwa kumuambia, ni kuhus mume wake, sasa ningesema nini, kuwa alitaka kunibaka, je ni kweli alitaka kufanya hivyo, mimi sikuwa na uhakika na hilo, na kama ningelimuambia huenda ingelikuwa mwisho wa ndoa, yao, …hapana nilichosema ni sahihi kabisa.

‘Sasa niambie huyo rafiki yako kaenda wapi, unaona mlivyo, mnaaminiwa mnakabidhiwa dhamana za watu, maana mtu akiondoka kwenda kazini, na wewe ukabakia na nyumba unakuwa umekabidhiwa dhamana ya kila kitu kilichopo ndani, sasa nyie mnaingiwa na tamaa mnaiba, …niambie ukweli huyo rafiki yako kakimbilia wapi..?’ akaniuliza.

‘Mama kiukweli mimi sijui, wewe unanifahamu nilivyo, siwezi kusema uwongo…’nikasema

‘Mimi ninavyokufahamu ni kuwa unaweza kuficha ukweli kwa kumuonea mtu mwingine huruma kwa ujinga wako ulio nao, na huyo mtu hawezi hata kukuonea huruma,..ukiogopa kuusema ukweli, sasa huku ni kwingine, huko kuna mateso, hapatakuwepo wa kukuonea huruma, nimekuja hapa kukusikiliza kama unahitajia msaada wangu…’akasema.

‘Ndio mama mimi nakutegemea wewe, nimegundua kuwa wewe ni mama mwema unaweza ukanitetea kwa hili, maana ukweli mimi sijui, alipokwenda huyo mtu…’nikasema.

‘Lakini mlionana naye huko sokoni, au sio..?’ akauliza.

‘Ndio…’nikasema

‘Ni mara ya ngapi kuonana naye, kabla ya hiyo siku..?’ akaniuliza.

‘Mara nyingi tukija sokoni namuona kwa mbali tu, na hatukuwahi kuongea naye kama siku hiyo…’nikasema

‘Kwanini siku hiyo mliongea,..?’ akaniuliza.

‘Yeye aliponiona aliniita kuwa anataka tuongee…’nikasema.

‘Kwahiyo yeye ndio alikuita..sio wewe ulimfuata..?’ akaniuliza.

‘Yeye aliponiona alinionyeshea ishara ya mkono, kuwa nimfuate…’nikasema.

‘Uliwaambia jamaa zako mliokuwa nao, kuwa umeitwa na mtu ..?’ akaniuliza.

‘Ndio, nilimuambia mama, akasema nisichelewe…’nikasema.

‘Lakini hakukuuliza ni nani unataka kuongea naye..?’ akaniuliza.

‘Hakuniuliza, ila niliporudi baada ya kuongea naye, ndio akaniuliza ni nani niliyekuwa nikiongea naye…’nikasema.

‘Mlipokuwa mnaongea naye, mliongea nini na nini..?’ akaniuliza.

‘Tuliongea mambo mengi, kuhusu maisha yetu yatakuwaje, tutafanya kazi gani ambayo inaweza kutuingizia, kipato, na baadae ndio akaniambia ana mpango wake, lakini anaogopa kuniambia mimi …’nikasema.

‘Kwanini anaogopa kukuambia wewe..?’ akaniuliza.

‘Ananiona mimi sio mjanja,…akasema mimi  kauli yangu ni mungu anajua, mungu anajua, nikae na kauli yangu hiyo kama itanisaidia…lakini hakuwahi kuniambia huo mpango wake, akisema haniamini, na kitu kama hicho..’nikasema

‘Mimi pamoja na mengine nakuamini, lakini hao walioibiwa hawawezi kukuamini, nimejaribu kuongea nao, wakaona kama na kutetea, mpaka tumeishia kugombana, hata urafiki umemeguka, kisa ni wewe..sisi kabla yenu tulikuwa marafiki wakubwa tunasaidiana, sasa mumekuja nyie, mumeharibu urafiki wetu…’akatulia akiangalia simu yake.

‘Sasa utanisaidiaje…maana sina mtu wa kunisaidia zaidi yako wewe…?’ nikamuuliza

‘Unajua nikuambie kitu, unachoniuliza kinaniweka njia panda, nikikusaidia wewe, ina maana navunja mahusiano yangu na rafiki yangu, huyo mama aliyeibiwa, na ndivyo alivyoniambia tulipokutana, amesema mtu anayemjali awe upande wake kuhakikisha kwanza anampata huyo mdada, na pili nyie mnaishia jela, …sasa hebu niambie hapo mimi nifanye nini, nikusaidie nivunje urafiki wangu, au nibakie kwa rafiki yangu wewe uende jela…?’ akaniuliza

‘Nitaendaje jela wakati mimi sikuiba, na wala sijui huyo rafiki yangu kakimbilia wapi na wala sijui huo mpango wake ulikuwa nini, na kama ningelijua mpango wake ndio huo, ningemkanya, na kumuambia akiiba nitamuambia madamu wake

‘Je angelikuambia huo mpango ungalifanya hivyo…?’ akaniuliza

‘Kufanyaje…?’ nikauliza.

‘Ungelimuambia madamu wake kuwa mwenzako ana mpango wa kuiba..?’ akaniuliza

‘Nikuulize wewe mama, mtu kaja kukuambia kuwa ana mpango wa kuiba mahali, je unaweza kwenda kwa hao watu ukawaambia kuwa kuna mtu anataka kuwaibia, je asipoiba, …mimi ningelijitahidi tu kumkanya kuwa asifanye hivyo, na ningelimtisha kuwa nitamuambia madamu wake, najua angeliogopa kufanya hivyo,ila mungu alizuia hilo akijua ungelikuwa ni mtihani kwangu…’nikasema

Mara simu yake ikalia…akaiangalia, na kusema.

‘Haya tunakutana mimi na wenzangu, moja ya ajenda ni hiyo, jinsi gani ya kufanya, na shauri la awali ni kuwa nyie mrejeshwe kijijini, mimi nilijaribu sana kulizuia, na kulichelewesha nia, tupata sehemu ya kukuweka wewe, lakini imeshindikana kutokana na matatizo ya mume wangu, sasa hili limetokea, ajenda sasa sio wewe kupelekwa kijijini tena, bali ni kuhakikisha unapelekwa jela, kama usiposema wapi huyo rafiki yako amekwenda..’akasema

‘Lakini mama, ujue mimi nitakwenda jela bila kosa lolote , na hali hii je itakuwaje, na hali hii imetokea nikiwa kwenu, je kama unawahusu watu wa nyumbani kwako,....?’ nikauliza

‘Hapo mimi siwezi kusema kitu, na ukizidi kusema kuwa hali hiyo uliyo nayo imetokea kwangu ndio unazidi kuniti hasira,..lakini nikuambie kitu, hiyo hali umejitakia wewe mwenyewe, kama ungenishirikisha, ukaniambi aukweli mapema, nikajua ni kitu gani kinachoendelea isingelifikia hapo…’akasema

‘Kwani mimi nilikuwa najua…’nikajitetea

‘Ulipojua, ulipohisi kuna hali kama hiyo, unaota sijui, na hata kama kuna tabia ambayo ulihisi sio ya kawaida kwa mume wangu ungeliniambia, mimi ningelijua jinsi gani ya kufanya, na huenda sasa hivi ungelikuwa labda unaishi na huyo bwana, au kungelikuwa na mpango madhubuti wa kuhakikisha kuwa haki yako inapatikana, sasa wewe hukutaka kujisaidia, mimi ningeliwezaje kukusaidia..?’ akaniuliza

‘Sawa mungu mwenyewe atajua ,kwa vile mimi nazungumza ukweli, na hayo niliyosema kwa polisi ni  kwako ndio ukweli ulivyo, kama nitapelekwa jela na kufungwa, najua ni mipango ya mungu, yeye anajua zaidi, na kwanini itokee hivyo,  lakini sitachoka kuongea ukweli, na huo niliokuambia ndio ukweli,…kama utanisaidia mungu atakusaidia na wewe…’nikasema na huyo mama akanigeukia na kuniangalia machoni, niliona namna ya huzuni usoni mwake.

‘Mhh….huu sasa ni mtihani…’akasema hivyo tu na kuondoka.


WAZO LA LEO: Ukweli ni silaha kubwa katika maisha yetu, watu wanafikia kusema uwongo ili wafanikiwe mambo yao, wengine wanafikia kusingizia wengine uwongo, kujenga fitina, kisa wao waonekane ni wazuri na wengine ni wabaya, kisa wanataka wafanikiwe kwenye mikakati yao ya maisha, iwe ya ajira, au uongozi, lakini tunasahau kuwa yupo ambaye anatujua sisi zaidi ya tunavyojijua.., je ukisema huo uwongo,labda…ndio ukafanikiwa unaijua kesho yako itakuwaje,..wangapi walipata, lakini hawakuweza kutumia, na wangapi walianza kutumia lakini hawakuweza kufaidi matunda yake…..Tufanyeni mambo tukijua kuna leo na kesho.

Ni mimi: emu-three

No comments :