Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, May 13, 2016

YOTE MAPENZI YA MUNGU-6
‘Lakini kabla ya kukuuliza hayo maswali,  nataka uhakika, nataka huyo mtoto awe salama…na wewe unipe uhakika huo…’nikasema na jamaa akataka kubisha sikumpa nafasi nikasema;

‘Mimi nafahamu kabisa kuwa wewe ni mtaalamu unaweza kufanya mambo yenu na hiyo mizimuikatulia…si ulipewa madawa na huyo mtaalamu, au sio, sasa nataka uhakika huo ili tuongee kwa amani, …’nikasema na yeye akatulia kidogo, na mara nikaona anacheza na simu, anaandika ujumbe, sijui alikuwa  kama anaandika kitu kwenye simuu yake, halafu akasema;

‘Mimii sio mtaalamu,…nilishakuambia, mimi natekeleza yale aliyoniagiza na huyo mtaalamu, wewe uliza hayo maswali yako….hayo ya mtoto niachie mimi, mimi ndiye baba yake nitajitahidi niwezavyo, maana  haya tumekuwa tukipambana nayo muda sasa, wewe hukuwepo….na hujui…lolote, tatizo huyu mtu,mtaalamu…’akatulia akiandika ujumbe kwenye simu.

‘Huyu mtu unayemtumia ujumbe kwanini usimpigie simu….’nikasema kwa lugha ya kumfanya aone na sisi tunakubaliana na yeye, na kweli kauli hiyo ilimfanya akunjue uso, na kwa haraka akasema;

‘Ngoja bwana, hayakuhusu haya, ….’akasema akizidi kucheza na simu yake, halafu akasonya na kusema

‘Kweli sasa yabidi nifanye hivyo,…unajua , tatizo ni kuwa nyie mlishaanza kuleta madharau yenu,…lakini ngoja niongee naye tu, sawa kabisa,  itakuwa ni vyema zaidi,….’akasema akinza kupiga simu. Alitulia kusikiliza , lakini ilionekana hakuna mawasiliano.

‘Haiwezekani,…imekuwaje tena….huyu jamaa kaenda wapi..unajua hii sio kawaida yake , simu yake muda wote ipo hewani…..sasa sijui leo kuna nini…’akasema akituangalia sisi kama anatuuliza na mpelelezi akauliza

‘Ni Jamaa gani huyu..?’ akauliza mpelelezi

‘Si huyo mtaalamu mwenyewe, kwani nilikuwa nampigia nani, mwenzako si  katoa wazo kuwa tumpigie huyo jamaa simu,…ili aweze kutusaidia, unajua , bila ya yeye mimi siwezi kuwahakikishia hilo,…nataka ajaribu awezavyo, ..afanye juhudu zake, ili hiyo hali isijirudie tena kwa mtoto, maana kwa jinsi alivyoniambia yeye, hiyo hali ikijirudia tena, hata nani, hata yeye mwenyewe hataweza kufanya lolote….’akasema.

‘Kwani mtoto alipopandisha homa muda mfupi uliopitia wewe ulifanyaje, maana hiyo ilikuwa zaidi ya mara ya nne, tuseme ukweli hapo..’nikasema na jamaa akatikisa kichwa kama kusikitika, na mimi sikumuachia nafasi nikaendelea kusema

‘Wewe mwenyewe  ulisema ikitokea safari nyingine huwezi kufanya lolote tena,…je mbona imewezekana,…na ilikuwa ni mara ya nne, au….sasa kumbe wewe  unaweza au ndio tuseme, umeshakuwa mtaalamu na wewe….’nikasema

‘Unajua wewe huelewi, tatizo sio kufanya dawa, tatizo ni miiko…kama miiko haitakiukwa, hilo haliwezi kutokea,…ndio  mimi nilifanya  hivyo nilivyoelekezwa japokuwa ilikuwa zaidi ya mara nne, kinyume cha alivyoniagiza mtaalamu, kwa kubahatisha tu, sasa mimi sijui madhara yake itakuwaje, mimi sijui, labda mimi mwenyewe naweza kudhurika, sijui….’akasema

‘Kwahiyo sasa mtoto yupoje…?’ akauliza mpelelezi akimuangalia mama yake na aliyejibu ni huyo huyo jamaa akasema;

‘Kwa hivi sasa mtoto hana tatizo si huyo hapio kambeba mama yake mkague kama ana homa yoyote, ndugu zanguni, mjue tatizo kubwa ni ukiukwaji wa miiko, munielewe hapo, najua nyie hamuamini hayo mambo, lakini yapo,…. ndio maana hiyo hali inatokea,, …’akasema na mimi nikatabasamu tu, na kitendo hicho kilimfanya awe kama hapendi akasemaa

‘Sijui nyie mnataka niwaelezeje ili mlielewe hili….labda niwaulize je hayo mnayofanya , au mnayotaka kuyafanya je hayaendi kinyume na hiyo miiko, kama nilivyokuelezea awali?’ akaniuliza akiniangalia mimi

‘Miiko gani….?’ Akauliza mpelelezi, na mimi nikadakia kwa kusema;

‘Hiyo miiko yenu haiwezi kuizua serikali kufanya kazi yake, hebu nikuulize, hiyo miiko yenu,….,haitaki haki itendeke…?’  kabla ajanijibu nikazidi kusema

‘Hiyo miiiko yenu inataka hii familia idhulumiwe haki yao,  hiyo miiko yenu, inataka tusijue ukweli kuhusu hilo deni,…wewe huoni kuwa hiyo mizimu imesetiwa tu, ili watu wasifuatilie kujua ukweli, sasa ni nani kafanya hivyo, kama sio hao….wanaotaka kumdhulumu mjane na watoto wake, sisi tunachohitajia hapa ni kutafuta  huo ukweli….je kufanya hivyo tumekiuka hiyo miiko, hebu tuambie…?’nikasema na mpelelezi akatikisa kichwa kukubaliana na mimi.

‘Unajua mimi …..nafuata nilivyoagizwa…’akasema

‘Na nani…?’ akauliza huyo mtaalamu

‘Na huyo mtaalamu…..ni kiukweli yeye ndiye  angeliweza kutupatia hilo jibu la hayo uliyosema,…na sio yeye, ni mzimu wa kaka…ndio unaongea,…yeye anafanya mambo yake tu, ili huo mzimu useme una tatizo gani,….sasa huo mzimu umekuja ukaingia kwa mtoto..ndio tatizo hapo…sasa huyu jamaa ndio hapatikani kwenye simu,….yeye ndiye angetusaidia kutupatia hilo jibu, ili tusije kuharibu tena…’akatulia akijaribu kupiga tena.

‘Mimi naona tuendelee tu…., sizani kama hilo litafanya mizimu ikasirike, tuomba tu isje kulete madhara mengine kwa mtoto ….na huyo ni baba yake, anataka deni kulipwa, na huwezi kusema kwanini unamtesa mtoto wako, kwake yeye huko alipo, haijalishi ni nani ataleta huo ujumbe, ili watu waelewe……’akasema akijaribu kutabasamu.

Nilimuangalia shemeji, bado alionekana kuwa na uso wa huzuni, mashaka..na alikuwa kwenye hali  ya kutaka kuondoka, nikasema;

‘Shemeji  wewe kaa, usiendelee kusimama, maana haya mazungumzo yanaweza kuchukua muda, na nia ni kuhakikisha ukweli wote leo unajulikana,…..na baada ya hili utakuwa huru kuamua mwenyewe  kuondoka au kuendelea kukaa kwenye nyumba yako, ukweli wote tutaubaini hapa hapa, …..’nikasema kwa kujiamini japokuwa moyoni sikuwa na uhakika huo.

Shemeji alisita kidogo, baadaye akasogea hadi kwenye sofa akakaa upande upande, ni kama kuturizisha tu, na mtoto wake Yule mkubwa akakaa vyema kwenye sofa na kujiliza, alionekana naye kachoka, na haukupita muda na yeye akalala.

‘Sasa tuendelee, ila ndugu,….hakikisha huyu mtoto haumwi…hali ya mtoto ikijirudia tena, sasa  itakuwa kazi yako mpelelezi, maana umeshaiona jinsi hali ilivyo,na ukweli kiasi, umeshaanza kuuona, hii ndio hali halisi ya dunia ilivyo…mimi nina imani baada ya haya maswali nitakayomuuliza, utaujua ukweli wote, na sizani kama tatizo hili litakuwa kubwa tena, zaidi ni nyie kuchukua hatua….’nikasema na jamaa aliposikia hivyo, akasema;

‘Lakini ….mbona siwaelezi, mimi kuhusu huyu mtoto nimejitahidi kwa hivi sasa hana tatizo…najua nyie hamna nia mbaya, su sio…ndio maana hata hiyo mizimu itakuwa imelewa, sioni kwamba kuna haja ya kuwa na mashaka….’akasema halafu kwa sauti ya huruma akasema

‘Eti shemeji, kuna kitu ulitaka kukifanya kinyume na  miiko,kwa  jinsi ulivyoagizwa, maana ulisikia mwenyewe, siku ile…. hawa watu hawawezi kuelewa, zaidi yetu,… sisi ndio tunafahamu maana tulikuwepo siku hiyo, sisi ndio tunafahamu jinsi gani mtoto anateseka, hawa hawajui…..sasa tusaidiane kwa hilo, je kuna jambo , …?’ akauliza na shemeji hakujibu hapo hapo, ila alipoona wote tunasubiria jibu lake akasema;

‘Mimi nimeshasema nataka kuondoka, nawasikiliza nyie tu, lakini leo hii silali kwenye hii nyumba, kama ni nyumba, ndio imefikia kutaka kuwaumiza watoto wangu, ….haya,  chukueni, …mimi nataka kuondoka…ninakwenda kwetu….’akasema.

‘Lakini shemeji hiyo kauli yako inautata, ni nani achukue nyumba, unavyosema ni kama vile na mimi nahusika na mambo hayo,…usiwasikilize hawa watu, wao wanashinikiza tu,ili mwisho wa mwezi wa kinge mshahara ,…na hata hivyo, sijamuamini …’akageuka kuniangalia

‘Shemu…hawa watu, hawajui ukweli,  ukweli halisi tunaufahamu sisi,… sisi ni kitu kimoja,….nia ni kuhakikisha roho ya kaka inatulia, nia ni kuhakikisha familia inaishi kwa amani, hebu fikiria kama  haya yangelitokea  tu, na tukawa hatujui sababu ni nini, unafikiri ingelikuwaje, mtoto angeendelea kuteseka tu….sasa shukuru tumejua sababu ni nini….’akasema, na mimi nikaingilia na kusema;

‘Dada wewe tulia,mambo sasa yanakwenda sawia, …..kuna mambo yanfanyika, ukweli utaajulikana, kama ni kweli au la…kama anavyodai shemeji yako , kama kweli kuna ukweli, kwanini litokee hili, mtoto kuumwa, huoni kuna utata…sasa subirini tuone, …’nikasema na jamaa aliposikia hivyo, nikamuona anaangalia simu yake,akainua na kuipiga tena, …naona namba ilikuwa haipatikani, akawa sasa uso unaonyesha hali ya mashaka, akasema;

‘Unajua tatizo ni kuwa nisipoweza kuwasiliana na huyu mtu, mambo yanaweza kuharibika ,, na mimi sitaweza kufanya kitu,…na huyu mtu sio kawaida yake, simu yake muda wote ipo hewani, ni lazima kuna tatizo..sio kawaida yake….’akasema

‘Naona sasa mumepatikana..’nikasema kwa sauti kama ya mzaha, na yeye akanitupia jicho la aina yake halafu akasema;

‘Tumepatikana, kwa vipi,i…..wewe maneno yako bwana mimi  siyapendi ,kwanini unasema hivyo, kwani wewe unanishuku nini mimi, mimi ninajaribu kufanya kile kiwezekanavyo ili kuisaidia familia yangu, sasa hapo nimefanya kosa gani…?’ akauliza

‘Mimi naona tuendelee….’akasema mpelelezi akiangalia saa yake.

‘Sawa tutaendelea ila nilitaka uhakika kuwa huyo mtoto hali hiyo haitajirudia tena, maana, ….sisi tunachotaka ni kujua ukweli wa hilo deni,  na tukiwa tunalifuatilia hilo, mama wa mtoto na familia yake wawe na amani…’nikasema

‘Lakini kama maswali yako yanalenga huko, kutafuta ukweli wa hilo deni, mimi sizani kama mimi…sijui lakini,….tuone utakavyoniuliza,….ila kama lengo lako ni kutaka kukwepesha deni lisilipwe, hilo ni moja ya tatizo, tukipekenyua undani wa hilo deni tunakuwa tumekiuka miiko, kwanini , kwanini, mimi naona haina maana tena ….kwasababu deni ni kweli ni la kaka….’akasema
‘Hebu nikuulize kitu, mbona wewe ulifanya hivyo..?’ nikauliza

‘Kufanya nini…?’ akauliza

‘Wewe uliposikia kuwa kuna deni,  kaka yako ana deni, ulifanya nini, si ulihakiki, sasa kwanini hutaki na sisi tufanye hivyo,….wewe ulipohakiki, hakuna mtu aliyeumwa, au kuna mtoto wako aliumwa,..hakuna….sasa, kwanini  alipoanza kufanya hivyo shemeji, si ndio  mtoto wake akaanza kuumwa,….au sio, mtoto hakuanza kuumwa ulipoanza wewe kutafuta ukweli, ni kweli si kweli, sasa ni  kwanini?’ nikamuuliza

‘Kwahiyo unataka kusema nini…?’ akauliza

‘Ndio nataka kukuhakikishia hilo,…na wewe ndiye unayeweza kutupatia jibu hilo, ni kwanini...na nataka kulithibitisha hilo deni je kweli ni la kaka yako au kuna ujanja ujanja hapo…na hili litapatikana kwa kupitia maswali nitakayokuuliza wewe…..umenielewe, je upo tayari…?’ nikamuuliza

‘Wewe uliza maswali yako , tatizo lako, unanishuku mimi, wakati mimi sijui lolote, haya uliza hayo maswali yakoo ….’akasema na mimi nikatulia, nilikuwa nasubiria taarifa fulani kutoka kwa vijana wangu, lakini niliona wanachelewa kunipigia,…, lakini moyoni nilijua watakuwa wamefanikiwa. Jamaa alipoona nachelewa kumuuliza maswali akasema akimuangalia mpelelezi

‘Unaona mwenzako alivyo, hivi hayo maswali yapoje, mbona hayaulizi,…yeye ni hivi hivi,….kwanini haulizi hayo maswali…?’ akasema akimuangalia huyo mpelelezi, na mara simu ya mpelelezi ikalia, na akawa anaangalia simu yake, na ndipo akasema;

‘Samahani kidogo, ….kuna simu ngoja nikaisikilize nje….’akasema na kutoka nje, na mimi nikabakia na jamaa, jamaa, akamwangalia shemeji yake, nilimuona jinsi gani alivyotahayari, hakusema neno, akawa anatikisa tikisa mguu, na mimi nikasema;

‘Tukimsubiria jamaa, ngoja na mimi niwasiliena na watu wangu kidogo…’nikasema na mimi nikatoka nje, ile simu yangu iliyopo mezani nikawa nimeiacha pale pale… nikawa natumia simu nyingine. Nilipoongea na watu wangu, maana pamoja na hayo kulihitajika kibali, kwani hayo sasa ni mambo ya kisheria, na wakili wa kujitolea ndiye alikuwa anakitafuta ili sisi tutambulikane kisheria, kwa ajili ya kazi tunayoifanya japo kwa huyo mama lakini ilionekana kuna utata.

Kwahiyo nikawa bado nipo  kwenye njia panda, hata nikiweza kuupata huo ukweli ni nani atanisaidia, ni huyo mpelelezi, …lakini tutakuwa tumeingilia kazi za watu, …kama tusipopata mwanasheria wakili wa kutusaidia hilo kazi itakuwa nzito sana, nilikuwa sijajua ni wapi mwanasheria huyo kakwama….wakati nasubiria nikaona nirejee ndani.

Wakati narejea ndani,  Jamaa alionekana akiongea na shemeji yake kwa ukali kidogo maana nilisikia sauti kama ya kukaripia, japokuwa sikuyasikia hayo maneno, na nilipoingia nikamkuta huyo mdada akionekana kulia, ilipoona hivyo nikasema;

‘Vipi tena, kuna nini zaidi….?’ Nikauliza

‘Wewe uliza maswali yako, haya ni maswala ya ndani mimi na shemeji yangu , hayakuhusu…wewe si uniamini bwana, mimi ni baba wa hii familia, muulize shemeji ni nini nilichowafanyia…..mimi nimekuwa naye bega kwa bega, niijali hii familia kama watoto wangu,lakini leo hii nafikiriwa vibaya,…sasa sijui, ndio tulikuwa tunaongea hayo,..haya  wewe uliza maswali yako hayo…..’akasema
                                                *********
Mara simu yangu ikalia, nikasimama na kusogea dirishani, nikawa naongea kwa sauti ya chini, ili jamaa asisikie,  nikasikiliza kwa makini, halafu nikauliza

‘Kapatwa na dharura gani….sasa mumempata mtu mwingine?unasema nini,…anahitajia malipo…oooh…mtihani….’nikasema na kusikiliza naona kuna mambo yanaibuka kwa sasa, kwenye mali kuna mitihani yake, nikawasikiliza maelezo yao halafu nikasema;

‘Una uhakika, ni nani, mtu wa usalama, ni nani huyo, sio huyu huku, ni mwingine yupi….kwahiyo …tuendelee, au …kukamatwa, kwa kosa gani…usijali,…’nikasikiliza halafu nikauliza

‘Kwani wao wanataka kibali gani….nani , polisi , kwanini..?’ Nikauliza na kusikiliza kwa muda,halafu nikageuka kumuangalia shemeji, nilitaka aniangalie kwani hadi hapo nilihitajia msaada wake, lakini nitaupataje wakati ndio yupo kwenye kifungo cha miiko…Jamaa alikuwa kasimama na kwenda dirishani akawa anatizama nje, alikuwa kanipa mgongo.

Nikaendelea kuongea na simu nikasema, …’Nyie fanyeni muwezavyo,…huku nitapambana tu,…Mungu yupo pamoja nasi…nina imani kesho itakuwa siku nyingine, lolote lawezekana…., hata nikitoka hapa usiku tutamwendea huyo hakimu….nina uhakika atatuelewa ongea  na huyo wakili, namfahamu sana, ni mnzuri lakini hafanyi bure….kama  anahitaji malipo yatapatikana tu….’nikasema nikiwa sina uhakika na hilo, yote hapo nacheza  bahati nasibu.

 Niliwasikiliza maelezo yao, mpaka nikahisi vibaya,….naona mambo yanaharibika, ….kuna vizingiti vingi, vimejitokeza, na ilionekana kama kuna watu wameshaweka masilahi mbele, na sijui ni nani yupi nyuma ya hilo, kwani huyu jamaa muda wote tunaye hapa…
‘Unasema wakili anataka kuongea na mjane,…lakini muda…’nikasema na kusikiliza…sikulipenda hilo wazo la huyo wakili la kutaka kuongea na mjane…kwani hakuna muda kabisa, na isingeliwezekana kwa hali ilivyo!

‘Hilo kwa hivi sasa ni gumu….mimi naliona gumu kwasababu nipo hapa na naiona hali ilivyo….’nikasema huku nikijaribu kumuangalia huyo mdada, kama naweza kumtoa pale nikaongee naye mahali kwingine , ili nimwambie kinachoendelea na ikibidi awe tayari kwenda kuonana na huyo wakili mpya, lakini niliona itakuwa ngumu sana.Nahisi jamaa ndio maana hataki kucheza mbali,….

‘Kwahiyo mnataka kusema nini….?’ Nikauliza na wakati huo shemeji aliinua uso wake, machoni kulikuwa kumejaa machozi bado alikuwa analia, sijui jamaa alimuambia kitu gani….nikageuka kumuangalia mpelelezi naona naye alikuwa kwenye harakati zake, alichelewa kurudi. Kazi inaanza kuwa ngumu!

Kulikuwa na sintofahamu nyingine….,benki walikuwa hawakubaliani na ombi letu kuwa mnada huo uahirishwe kwani wao walishafuata taratibu zote , na amri ilishatolewa, na imetolewa na mahakama,  na kama kuna watu wanazuia wanakwenda kinyume na mahakama, ni wakosaji…tunahitajika kushitakiwa kwa kukiuka amri halali ya mahakama, na hilo limeshafikishwa polisi ili sisi tuchukue hatua.

‘Je ni nani kawaambia hayo…?’ nikawauliza wakatoa maelezo yao, yaonyesha kuna mtu , huenda alikuwa akiwasiliana na huyu jamaa na kawaambia wajaribu kufuatilia uhalali wetu , sikuwa na uhakika nalo, lakini ni nani angenishuku uhalali wetu kama sio huyu jamaa!

Hata hivyo, watu wangu walikuwa kwenye harakati , wakihangaika huku na kule….kuhakikisha wanazuia huo mnada wa kesho, na pili kunapaitikana ushahidi ,lakini wakili mpya anadai mtu anayeweza kuleta huo uzito ni mjane, ….alimuhitaji akutane naye na ikibidi waongozane naye mguu kwa mguu hadi kwa hakimu…na pili anahitajia kuwe na ushahidi mnzito, utakaoweza kubadili mawazo ya hakimu na polisi waweze kuingilia kati! Mambo yameharibika mwishoni…

‘Na zaidi ya hayo kuna mtu wa usalama mkubwa kasema sisi yawezekana ni matapeli kwahiyo tukamatwe, …’akasema mtu wangu

‘Huyo mtu wa usalam mkubwa ni nani….?’ Nikauliza na kusikiliza!

Oh, hilo sasa ni balaa jingine, nikajua kumbe tatizo hilo sasa lina mikono mingi, yote kwasababu ya mali , na mali yenyewe ni mali ya mjane na yatima, watu wameshaanza kuimezea mate…. Ni kweli nyumba ikiuzwa kihalali kutapatika pesa nyingi sana, sasa ni kiasi gani watapewa hawa wahanga na kiasi gani kitakwenda kwa hao wapambe…dhulumati. Ni lazima kifanyike kitu, …hii si haki kabisa
’Mungu wangu toa msaada wako…’nikajikuta nikisema  huku bado nimeshikilia simu nikisikiliza maelezo ambayo kila hatua yalikuwa yakinikatisha tamaa…sikujua kuwa jambo hili lilikuwa limeshawahusisha watu wengi hivyo, lakini kama wakili Yule wa mwanzo angelikuwepo,….mambo yasingelikuwa magumu hivi,….kapatwa na nini ghafla hivyo….!

‘Sasa tufanyeje….?’ Nikauliza na kusikiliza maelezo ya watu wangu wakitoa mapendekezo yao, kwa ujumla wao walishafikia kuzuri…lakini ushahidi waliopata unahitajia muda kuuweka sawa. Na kesho ndio kesho…! Nikakata simu na kugeuka kumwangalia mjane na mwanae..huruma ikanitinga!

Kwa hali ilivyo hadi hapo mtu atakayeweza kunisaidia hadi hapo ni huyo mpelelezi,…kwanza  aniamini, ili tu asikilize huo ukweli, …..ukweli una nguvu, na yeye sizani kama ana uwezo wa kupingana na wakubwa zake, kwani huyu amayeleta vikwazo huko ni mkubwa wa huyu mpelelezi!

‘Sasa huu ni mtihani…..’nikajisema nikiinua hatua kurudi kwenye sofa…nilitingwa na mawazo mazito sasa,…hata hivyo, bado nilikuwa na matumaini,….nilikuwa na uhakika kama huyo mpelelezi atakubali kuusikiliza huo ukweli kwa kupitia kwenye maswali yangu ambayo nitambana huyo jamaa basi yeye atakuwa upande wetu na kesi hiyo itakuwa na mshiko. Lakini pili awe tayari kutoa ushirikiano, ili kuwashawishi wenzake na  hasa hakimu…na kwa muda huo muhimu ni hakimu ilii akubali ombi letu, ili huo mnada wa kesho usifanyike…miujuiza!

Sikuweza kukaa, nikawa natembea tembea nikiwaza, na mpelelezi hajarudi, bado anaongea na simu huko nje, nilijawa na wasi wasi, ….

Nikatembea hatua chache hadi kwenye dirisha la upande wa pili, nichungulia nje, …nilimuona mpelelezi akiongea na jamaa wawili, kumbe kuna wenzake walikuwa nje…nilimuona akiongea kwa vitendo, yaonekana kuna kitu kikubwa sana, kwani ishara ile ya mikono, ilikuwa kama kutokakukubaliana au kuna kitu kimekosewa…nikazidi kuingiwa na mashaka….kuna nini…nikageuza kichwa kumwangalia jamaa yangu, huku ndani…

Huyu jamaa alikuwa akijinyosha na nilimuona hana wasiwasi….anaonyesha kujiamini zaidi, tabasamu mdomoni….aliponiona namuangalia yeye akasema;

‘Nyie watu,… mimi siwezi kupoteza muda wangu siku nzima hapa, kama hamjawa tayari basi tupange siku nyingine, lakini kesho,….keshoo si ndio mnada au…..’ akawa kama anauliza halafu akamgeukia shemeji yake na kumuuliza.

‘Au sio shemeji……?’ akamwangalia shemeji yake aliyekuwa kajiinamia tu, na alipoona hajibiwi akaendelea kusema

‘Kesho walisema ndio siku ya mnada… na sisi hatuna jinsi, kama tulivyokubaliana,…..hawa jamaa hapa sizani kama wana msaada wowote, wanapoteza muda bure, mpaka nafikia hatua siwaamini, kama wana msaada wangelikuwa huko kwa hakimu…labda wafanye jambo, jambo lakuonyesha kuna namna ya kulipwa hizo pesa..maana muhimu hapa ni deni lilipwe, au sio shemeji, likilipwa hatuna maneno,…lakini hawa mmmh,nina mashaka nao …yawezekana ni matapeli tu…’akasema kama anamnongeneza shemeji wake! Shemeji yake aliposikia kauli hiyo akainua kichwa kidogo, akitaka kuniangalia lakini akasita,na jamaa akamsogelea shemeji yake ili awe naye karibu akawa anaongea kwa sauti ya chini chini…


‘Sisi kama tulivyokubaliana…huo mnada ufanyike tu…maana hakuna njia nyingine ya kuzipata hizo pesa…na pesa itakayopatikana, watachukua deni lao itakayobakia tutajenga nyumba nyingine, sio lazima iwe kama hii… ili roho ya kaka isiteseke au sio,….yule ni mume wako anahitajia msaada wako sana…na jingine ni hili la mtoto, je hali ikijirudia tutafanyaje….tuwahurumie hawa watoto….na hilo ni kwa kuondokana na hilo deni, au unasemaje shemeji,….’akasema  na shemeji yake alikuwa kimia tu

‘Na hiyo ya mnada sio amri yetu, hatuna la kufanya…maana kila kitu kipo wazi, stakabadhi zote zina sahihi ya kaka, …sasa hawa watu wanataka nini,…. ndio maana hawataki kwenda huko benki, na huko benki hawawezi kuvumilia tena walishaniambia iwe isiwe ni lazima wachukue chao…sasa,…. haya ngoja tuone, ….’akasema akimuangalia shemeji yake, na shemeji yake alikuwa  kimia tu.

‘Na kama wewe unataka kunaondoka wewe nenda tu…, mimi nitayasimamia mambo yote,usiwe na wasiwasi….hilo lisikutie shaka, na ikishapatikana hiyo pesa, eneo lipo..ujenzi utaanza mara moja…nitajitahidi hata kutia nguvu zangu, naweza hata kuuza sehemu ili mpate nyumba yenu nyingine….’akasema kwa sauti ndogo ili nisisikie…na shemeji yake hakumjibu kitu, alikuwa kainama tu.

‘Nikuambie ukweli, hawa ni matepeli,….mwenyewe utaona,…nimeshawajua,….wanacheza na mimi…shemeji mwenyewe utaona….ngoja usikie vumbi langu...’akasema na kugeuka kuniangalia, na mimi nilikuwa najidai naandika ujumbe kwenye simu, yeye alipoona hivyo akamgeukia shemeji yake akitaka kumwambia kitu, lakini akasita,…kuna ujumbe wa simu uliingia kwenye simu yake….akawa anausoma, na alipomaliza akasema

‘Nilijua tu…hawa ni matapeli, sasa ngoja waionje joto ya jiwe….shemu usiwe na wasiwasi, hawa sasa hivi wanakamatwa, wewe utaona tu…’akasema na shemu wake sasa akainua kichwa kwa wasi wasi akaniangalia , lakini hakusema kitu, na jamaa alipoona shemeji yake hamjibu akanigeukia mimi na kusema


‘Sasa sijui nyie mumefanya juhudi gani kwa hilo….’akasema

‘Juhudi ya nini….?’ Nikamuuliza kama simuelewi

‘Kuhusu huo mnada wa kesho….’akasema

‘Usiwe na shaka kwa hilo…wewe mwenyewe baada ya hapa utatusaidia kuhakikisha hilo halitendeki…’nikasema na yeye akaniangalia kwa macho ya kushangaa, akasema;

‘Mimi….kama nani, maana hiyo ni amri ya mahakama…’akasema.

Mara mpelelezi akaingia… cha ajabu sasa alipoingia alikuwa kashikilia pingu mkononi, ….akawa  anatembea mwendo wa hatua za kuhesabu, na anakuja muelekeo wangu, pale nilipokuwa nimekaa…akanifikia, na akawa ananiangalia kwa jicho la kujiuliza mpaka nikahisi kuna tatizo…

NB: Ehee…sasa ni nanii hii tena,….uone mtihani wa mali ulivyo…. tuwemo sehemu ijayo.


WAZO LA HEKIMA:  Mali na madaraka ni mtihani kwetu…wangapi wangapi wametumbukia kwenye mtihani wa mali, na madaraka, ..wakasahau kutenda yaliyo haki , wakaupindisha ukweli, wakadhuluma wenye haki zao,  kwa sababu tu ya kupata mali na madaraka…, kisa ni nini pesa. Wangapi wangapi wameshindwa kuutetea ukweli, kwasababu ya ubinafsi, wakataka kumfurahisha bosi wao, huku wakijua wanchofanya sio halali,… tukumbuke jamani, Haki na ukweli havipindishwi kwa kujua kuongea vizuri, ukaipindisha sheria….hiyo ni dhuluma,…ipo siku utaumbuka tu!
Ni mimi: emu-three

No comments :