Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, June 19, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-79


 Mpelelezi akawa ameshapita kwenye kizimba cha kusimama watu wanaotoa ushahidi, baada ya kukamilisha taratibu zote kwa mujibu wa sheria, baadaye akaanza kutoa maelezo yake akiongozwa na muendesha mashitaka.Mimi niliwatupia macho kundi la washitakiwa niliwaona wengine wakificha nyuso zao.

‘Hebu tuambie wewe ni nani.....?’ akaulizwa         

‘Mimi ni askari mpelelezi wa kesi mbali mbali kwa mujibu wa sheria....’akasema

‘Kwahiyo wewe ni askari kanzu kama wanavyoita watu....’akasema muendesha mashitaka

‘Ndio hivyo kama wanavyoita watu...’akasema

‘Hebu tuambie utaalamu wa kazi hii uliupatia wapi?’ akaulizwa

‘Mimi baada ya kujiunga na jeshi la polisi, nikitokea chuo kikuu, nilipelekwa nje kusoma, nikisomea mafunzo hayo hayo ya upelelezi, lakini katika kitengo cha maswala ya ujasusi, yaani makosa yanayotokana na makundi haramu, ambayo yanafanywa kitaalamu zaidi, na hasa katika uhalifu mkubwa wa kimataifa.

‘Lakini sisi tujuavyo askari kanzu wanajificha huwezi kuwatambua, mbona wewe hujifichi, na wakati mwingine unaonekana ukiwa rasmi na mavazi ya kipolisi..?’ akaulizwa

‘Ndio wapo askari wa namna hiyo lakini pia wapo askari wapelelezi wa namna yangu ambao hawajifichi, ambao tupo wazi kwa raia, na raia wenyewe wanafahamu kabisa kuwa huyu ni askari mpelelezi....ni mgawanyo wetu wa kazi....’akasema

‘Kwasababu wewe ni mtaalamu, hebu sasa tuelezee, elezea mahakama hii kwa makini jinsi ulivyoweza kuifanya hii kazi hadi kuligundua hili kundi haramu,hatua kwa hatua...’akasema muendesha mashitaka

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, baada ya kutokea wizi mkubwa na upotevu wa mara kwa mara wa nyaraka za serikali, serikali iliona kuwa kuna umuhimu wa kufanya uchunguzi wa kina, kwahiyo kwa vile walikuwa na watu tayari wameandaliwa kwa kazi hizo wakawatuma watu wao kufanya hiyo kazi...

‘Kiukweli mwanzoni, ilifanyika kazi nzuri, na kukabainika kuwa kuna kundi limejijenga kwa mbinu na linafanya kazi yake kimiya kimiya likiwa limejificha ....wao wakatoa taarifa yao, lakini utekelezaji wake, ukaishia kimiya kimiya. Na mwanzilishi wake hakubainika moja kwa moja...

Hali ikatulia kidogo, lakini kumbe watu hawa walikuwa wakijipanga upya, ilikuwa kama wamegundua kosa lao lipo wapi, serikali ikaliona hilo, na wao wakajipanga kinamna ambayo inaweza kulimaliza abisa hilo kundi, ndio wakanipa hiyo kazi maalumu ya kuchunguza hili kundi kiundani zaidi.

Kwa ujumla hili ni moja ya makundi haramu, ni kundi la kijasusi lenye mbinu za hali ya juu, kiasi kwamba huwezi kufahamu kuwa wanajishughulisha au wana nia mbaya katika jamii. Kwa nje wataonekana ni watu wema sana, wanatoa misaada , wanajenga mashule, na kila aina ya huduma wanakuwepo...

Muanzilishi wake, aligundua kuwa ili uweze kuwateka wanajamii kirahisi, ni vyema ukajikita kwenye shida zao, udhaifu wao,...hasa kwenye maadui wakubwa wa binadamu, ujinga , umasikini na maradhi,...huko ndipo walipowekeza, kitaalamu kabisa...

 Wakaanzisha mashule, mahospitali, majumba ya ibada, na hata mabenki, na vitega uchumi, na hivyo vyote vilitoka humo humo kwenye kodi ya wanajamiii, na misaada toka nje, kwa mbinu, na utaalamu wa hali ya juu...

‘Watu hawa ni wazawa, wamesomeshwa na kodi ya serikali, na sasa wanakuja kulipa hizo fadhila, na hizo ndizo fadhila zao,...wananchi hawajui, wanachojua ni kuwa hao watu wamekuja na elimu yao ya kuweza kuwasaidia , maana kweli wamejenga mashule, wamejenga, mahospitali,...yote hayo ni muhimu kwa jamii....’akatulia kidogo pale wakili alipoonyesha kumzuia asiendelee, na wakili akasema;

‘Hebu hapo tufafanulie, jinsi hawa watu walivyoweza kuwekeza, walipatia wapi hizo pesa, na jinsi gani walikubalika, elezea kwa undani, kuhusu kundi hilo , jinsi lilivyoanzishwa hadi kuanza kuleta matatizo katika jamiii....’akasema muendesha mashitaka.

‘Kundi hili lilianzishwa na jamaa moja aliyekuwa na ndoto ya kuja kuwa mtu mkubwa sana duniani, na ndoto yake hiyo ilianza wakati akiwa anasoma huko nchi za nje..na alijengwa na tamaa hiyo kwa vile alikuwa msomaji mnzuri wa vitabu vyenye maelezo ya kijasusi, akavutika, na watu kama akina Carlos, na wengineo.

Siku moja akakutana na marafiki zake ambao walipenda sana kusoma hivi vitabu vya hadithi, wakawa wanahadithiana, na mmoja wao akasema;

‘Hivi kweli hivi vitabu tunavyovisoma, ni kwa ajili tu ya kujifurahisha, hivi humu ndani hakuna cha kujifunza zaidi ya kujifurahisha, hamuoni kuwa kuna mambo tunaweza kuyafanya, tukawa kama wao, mimi nimekuwa nikivisoma katikakati ya mistari hamjaliona hilo hata nyie...?’ akawa anauliza

‘Mhh, ni hadithi, tu bwana, lakini kwa mwenye akili anaweza kujifunza jambo...ila mimi ninavyoona wengine wametunga kinjia ya propaganda, watunzi wengi wanatumia sana hii mbinu, kushawishi watu kwa ujanja, ili waamini kile wanachokitaka wao, au wanachokitaka watu fulani, au kundi fulani, hilo ndilo nililoliona mimi....’akasema mwenzao.

‘Mimi nina wazo, sisi sote ni wasomi, na akili zetu zinatambuliakana, sisi ni wale waliojaliwa akili za hali ya juu,...tulikuja huku kusomea mambo ya kisayansi, lakini kwa bahati mbaya, tukajikuta tunasomea mambo ya kijamii,...hebu tuiangalia hii jamii na haya tuliyoyasomea tuyaweke kisayansi zaidi, hapa hatuwezi kugundua jambo linaloweza kutusaidia baadaye....’akasema mmojawapo

‘Sasa unataka tufanye nini?’ akauliza mwingine ambaye aliingiwa na hamasa.

‘Tutengeneze tofauti, angalia watu walioweza kufanya maajabu, walikuwa ni watu kama sisi, wakabuni mambo, wakaweza kujenga jamii kwa namna moja na katika namna nyingine wakawa wanafaidika...hebu angalia watu kama eeeh...

‘Watu hawa waliibuka kutoka chini kwenye jamii, kwa ajili ya akili zao wakavumbua mambo, wakaweza kuunda jambo likakubalika katika jamii, lakini kisiri wana ajenda zao, wakatajirika, na kuanza kuogopwa.....’akasema

‘Nahisi wewe kuna kitu umekigundua huenda ndio hicho hicho nilichokuwa nikikiwaza mimi, hebu tuwekane sawa maana tunakaribia kurudi nyumbani...’akasema mwingine

‘Wewe kwanza umegundua kitu gani... tuambieni wewe kwanza...’akasema mwingine     

‘Nataka tuanzishe kitu ambacho tunaweza tukaitawala dunia....’akasema

‘Kuitawala dunia kwa vipi, unaota...’akasema mwingine kwa kumaka

‘Kuitawala dunia sio lazima uwe mfalme, sio lazima uwe kiongozi mkubwa wa kisiasa, unaweza kuitawala kiuchumi, na hilo ndilo la msingi, na kuitawala kiuchumi sio lazima uanza na miradi mikubwa mikubwa, hapana...’akasema

‘Sisi tukirudi nyumbani tutakwenda kuwa viongozi kwenye mashirika mbali mbali, cha muhimu kwanza tuhakikishe kitu ujamaa kinasahaulika, na yale makampuni yenye mlengo huo yanakuja kumilikiwa kibinafsi, na wamiliki wake wanakuja kuwa sisi au watu wetu...tutaanzia hapo...’akasema

‘Muhimu sana tuwe na akiba zetu nje...ili lolote likitokea, tunajua wapi pa kukimbilia...’akasema mwingine

‘Oh, hilo wazo jema, ...tupeani nafsi ya kulifanyia kazi, lakini ni lazima tuwe na kitu kama chama, au kundi, na tupate jina zuri tu...’akasema mwingine

‘Mimi napendekeza tuliite kundi letu....`dunia yangu...’

‘Mimi bado hapo sijawakubalia hiyo ni ndoto, hiyo dunia yenu mnayotaka kuianzisha labda mkaianzishe kwenye sayari nyingine...’mmojawapo akawa mpinzani mkubwa, lakini baadaye alikuja kukubali baada ya kuwa wanakutana mara kwa mara kulipangilia vyema, wakaja kukubaliana na hilo wazo, na wakaanza kulifanyia kazi

‘Ujue hawa watu wana akili sana, wao wangelipata nafasi ya kusomea masomo waliyoyaendea ya kisayansi huenda tungelikuwa na wataalamu, lakini walipofika huko kwasababu mbalimbali wakajikuta wanasomea masomo ya kijaamii, na hili ni tatizo sana....’akasema mpelelezi.

‘Wenzetu hawataki tuwe na watalaamu wa namna hiyo, au sisi wenyewe tunavutika na mambo mengine ya kupata utajiri...sasa hawa watu walikuwa na akili ambazo tungezitumia kwa masilahi ya nchi, lakini wao wakaja kuzitumia kibinafsi zaidi,...

‘Walichokuja kukubaliana ni kuwa wakirudi cha kwanza ni kuhakikisha kuwa katika kila taasisi kuna watu wao, katika kila idara wana watu wao, hata kwenye makampuni binafasi wanapandikiza watu wao, lakini je hilo lingefanikiwa vipi...

‘Wakajipanga kwanza kwa kupata wafuasi wakiwa huko huko....’akasema

‘Watu hawa waliendelea kusoma huko nje, huku wakilifanyia kazi hilo wazo walilolibuni, kwahiyo wenyewe wakagawana malengo, kila mmoja akasomea fani fulani kwa undani zaidi,...na somo la ziada ni la kiujasusi wa kimataifa, ili waweze kutamba kokote kule...

Huyu muanzili wa wazo hilo akamaliza masomo yake kwanza na kurudi hapa nchini, na wenzake wakabakia huko wakimalizia masomo yao,na wakawa wanarudi mmoja mmoja, lakini kila mmoja akiwa na lengo walilokubaliana na hata walipokamilika, wakaitana.

Kikao hicho kilifanyika kwa siri sana, kilianza kama sherehe ya kukutana kwa wale waliosomea nje, na baada ya shamra shamra jamaa wakaitana na kukumbushana malengo yao...

‘Waliwachukua watu , na kuanza kuwafundisha kinamna, wao kama wadhamni, wakawaambia watu hao waanzishe taasisi za kijamii, wao watawatafutia wadhamini, na misaada kutoka nje...

‘Taasisi zikaanzishwa nyingi tu...za wasio jiweza, mashule, nakadhalika, na kila taasisi jamaa hao wana mikono yao, walifanya hivyo kwani ili kujenga ukaribu wao na wananchi, wakawa wanapata misaada toka nje, walipojiona wamepata sana, wakaanzisha mashule yao, ambayo humo ndipo wapopata watu wao wanaowataka, na waliwalenga sana watoto wenye vipaji maalumu, nia na lengo ni kupata vichwa, au majembe...

Na hao vijana walioweza kusomeshwa na kuchaguliwa na wao wenyewe kwa uchunguzi maalumu, vijana hao kwa siri wakawa wakapata mafunzo maalumu, ambayo waliyalenga kwenye mikakati yao, na vijana hao walipomaliza hayo mafunzo wakasambazwa kwenye maidara, maofisi na kila sehemu kutegemeana na kile walichokisomea..

Kazi sasa ikaanza, kila mmoja alipewa majukumu, na majukumu hayo ni kuhakikisha, kila mmoja anaingiza kiasi fulani kwenye mfuko wa kundi,dunia ikaanza kujengwa, maana ili dunia iweze kuzunguka, ni lazima iwe na mali, na mali hiyo itapatikana wapi, ni kwenye shughuli zetu, kodi zetu,mali asili yetu....wakaanza kujijenga

Kila sehemu nyeti walihakikisha wana watu wao na kila sehemu zenye masilahi walihakikisha kuwa kuna mirija yao...wakahakikisha pia sehemu za kuingizia mizigo zinakuwa na watu wao, ili waweze kufanya biashara zao haramu bila kujulikana, ...kundi likazidi kukua, na uimara wa kipesa, utajiri, ukawajengea kiburi, utaenda wapi usiwakuta....

Katika hali halisi watu hawa walijulikana kama kundi la kusaidia jamii, na kila walipopata nafasi walifanya hivyo, ila walifanya pia kwa msilahi, ingiza rupia upate dola, nini kama dola bwana, watu wakawa wanajiunga bila hata wao kujijua, na wanajikuta wakikaribishwe kwenye shughuli za kupongezana, na humo wakifika wanaulizana, nani mwenzetu, wao wenyewe `uwenzetu...’ una maana yao.

Kwasababu ya pesa, kwasababu ya utajiri, kwasababu ya kuwa wao sasa wameshika kila eneo nyeti wakaanza kuonyesha kiburi,..ile hali ya kujificha sana ikawa inaanza kufutika, wakaanza kuonyesha makucha yao, kila aliyeingia akawa sasa anapewa amri kuwa ukiingia hutakiwi kutoka unatoka ukiwa maiti, na kama ni mwenzetu ukiwa kwenye sehemu nyeti ni lazima utii masharti ya kuwezesha wengine au kuwezesha kundi....

Kipindi cha nyuma kundi hili liliingia matatani, kuna watu wa usalama waliwashutukia, na upelelezi ukaenda hadi kugundua kuwa kuna kundi kama hilo, na kuonekana wanafanya mambo kinyume na sheria ya nchi, na viongozi wao waanzilishi wengi wakakimbilia nje....

Hata hivyo hakukuwa na haja ya kuwafuatilia kwani bado walikuwa hawajafanya jambo la kuwatia hatiani, na wenyewe walipofika huko wakiwa wawekezaji maana walishawekeza huko, na walishajipanga mapema kuwa kitu kama hicho kitatokea, na wafanye nini, na huko wakajifanya hawahusiki tena,...lakini baada ya uchunguzi wangu nimegundua kuwa bado wapo wanatoa amri, wanaelekeza, na wanafaidi matunda ya mambo yao..

Katika kila kitengo nyeti wana watu wao, na wanajuana na kusaidiana, ...huku wakijifanya wanazalisha, huku wakitoa misaada huku wakifanya mambo yao kinyume cha sheria, kama biashara haramu, kukwepa kodi, na kuingiza bidhaa kutoka nje bila kufuata taratibu,na zaidi wakawa wanafanya biashara ya madawa ya kulevya, ili kuzidi kuangamiza vijana wetu....’akasema

‘Kama nilivyotangulia kusema hawa jamaa walishaandaa watu wao, ambao wamesoma kwa taratibu zote, lakini wakiwa wanafadhiliwa na kundi, wakiwa wamepitia mafunzo maalumu, na wanajua ni ni wanachokifanya, na wakati mwingine wanapewa maelekezo kuwa wafanye jambo fulani, liwe la heri au baya,...

‘Kama nia yao ingekuwa nzuri, maana taasisi hizi za jamii zipo nyingi na zina malengo maalumu, ya kusaidia jamii, na zinakubalika, lakini hawa jamaa walianzisha taasisi zao ikiwa na malengo ya nje mazuri lakini ya ndani kuna mipango ya kuwanufaisha, kwa migongo ya wengine...’akaendelea kutoa maelezo na wakili muendesha mashitaka akamwambia.

‘Kuna silaha kubwa wanayoitumia wao, nayo ni propaganda potofu, kila wakitaka kugundulikana wanageuza maneno, wanageuza ajenda kinamna ambayo hali halisi inasahaulika, na ajenda zao zinapenyenzwa kinamna....kuna miradi kama mahoteli ya kitalii, humo kuna mambo yao, kuhakikisha jamii inazama kwenye anasa zaidi na kujisahau...

‘Watoto wetu wanajikuta wakizama kwenye starehe zaidi, elimu inakuwa ni lugha tu, lakini elimu yenye mlengo wa kisayansi, yenye kuelimisha kiuzalishaji zaidi wanakuwa nayo wao na watoto wao...kwahiyo wao wanakuwa wamiliki, viongozi na wazalishaji, wengine ni bendera fuata upepo...’alipofika hapo wakili muendesha mashitaka akasema;

‘Sasa hebu tuingie moja kwa moja kwenye kesi yetu, tumeona kuwa kundi hili lilianzishwa kama makundi mengine ya kijamii, likasajiliwa, na wanachama wake ni watu mashuhuri tu, wanajitolea kusaidia jamii, je imekuwaje liwe na mafungamao mabaya, ya hata kuua?’ akaulizwa na wakili

‘Nia ya kundi ni kuunda kitu kama dola, lakini sio dola ya utawala, kuwa washike nchi hapana, wao walilenga mbali zaidi, dola la kiuchumi... , ya kuwa hataka kama kutakuwepo mtawala, basi awe anafuata amri zao, kwasababu kila sehemu wameshikilia wao..na kama atatokea mtawala mtu wao basi itakuwa bora zaidi, lakini hawakutaka sana kuonekana kwenye majukwaa...’akasema

‘Haya tuje kwenye kesi yetu moja kwa moja, ni kwanini huyu mtoza ushuru aliuwawa...?’ akaulizwa

‘Kabla sijajibu swali lako, kwanza ni vyema tukamtambua huyu marehemu, alikuwa nani hadi kifo chake, ...’akasema na wakili mtetezi akaweka pingamizi kwa kusema hayo ni kumsema marehemu wakati hayupo, hakimu akapinga hilo pingamizi akasema shahidi aendelee.

‘Marehemu ni vijana wa mwanzo walioandaliwa na hilo kundi, na alipewa hiyo kazi mwanzoni kabisa, na hadi anafariki, alikuwa ameshafikia kiwango cha u-mwenzetu,...mwenzetu ni kiwango cha juu katika kundi, wana vyeo vyao wenyewe, na hadi anafariki, alikuwa katika maandalizi ya kupewa cheo kikubwa...’akatulia

‘Kwasababu ya kugombea vyeo kukatokea mgongani, wenyewe kwa wenyewe wakaanza kupigana vita, na marehemu akashutumiwa kwa kujijali mwenyewe, na baadaye wakamshuku kuwa anasaliti kundi..na hi ilitokea kipindi akiwa na mahusiano na mdada...’akasema.

‘Hebu sasa tuingia moja kwa moja kwenye hoja ya mauaji, najua sasa kundi au chanzo cha kundi kimeshajulikana, lakini nimeona kuwa wenzetu wana dukuduku, naona tuwape nafasi wamuulize mtaalamu, mpelelezi wetu...’akasema wakili muendesha mashitaka.

Wakili mtetezi mmojawapo akasimama na kumsogelea shahidi akitaka kuanza kuuliza maswali, yule wakili akasita kidogo pale alipoona mtu akiingia mlangoni, na mara watu wakasikika wakisemeshana na hata shingo zao kugeuka nyuma kuangalia ni nani aliyeingia...

NB: Haya mambo hayo....jana hatukuweza kuwakilisha sehemu hii maana ni sehemu nyeti kidogo, ilibidi ipitiwe kwa makini.

WAZO LA LEO: Utajiri ni mnzuri, na kila mtu anatamani kuwa hivyo, lakini utajiri huo usitokane na dhuluma, usitokane na jasho la wanyonge, ukafaidika wewe , huku watu wanakufa njaa, watoto wao wanakosa elimu, mayatima, wajane wanaongezeka kutokana na utajiri wako, huu ni unyama.


Na kwanini unafanya hivi, kuwa wewe utaishi milele, kuwa wewe jamii na familia yako itaendelea kuneemeka, tusijidanganye, dhuluma kamwe haidumu, na ikiendelea ujua amani haitakuwepo kamwe..
Ni mimi: emu-three

No comments :