Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, June 12, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-75


Baadaye ilibidi niondoke pale hospitalini na kumuacha mpelelezi akiendelea na uchunguzi wake,wakishirikiana na polisi, na msako wao ukamlenga kumtafuta yule nesi aliyekuwa akimuhudumia mzee, ambaye kwa muda huo hakuonekana tena maeneo ya hapo hospitalini, na hiyo ikazidi kutia shaka kuwa huenda anahusika na na hujuma hiyo.

‘Kinachonipa mashaka ni huku kutoweka kwake ghafla, japokuwa hatuna uhakika wa moja kwa moja kuwa sumu hiyo kaiweka yeye, au ndiye aliyempa mzee hiyo sumu, lakini yeye ndiye aliyempa maji mzee, na inavyoonekana sumu hiyo kainywa mzee kupitia kwenye maji,...na mtu ambaye alipewa kazi ya kuhakikisha usalama wa kitu anachokula mzee, ilikuwa mikononi mwa huyo nesi.

‘Hata hivyo ile gilasi alikunywia maji mzee haikuonekana....’akasema

‘Docta anasema sumu , japokuwa wamewahi kumpa mzee dawa ya kuituliza hiyo sumu, lakini ni vyema upasuaji wa haraka ukafanyika kwani sumu hiyo hula  mwili taratibu, ...’akasema

‘Baada ya mabadiliko ya hali ya mzee na kufikishwa kwenye vipimo, na kugundulikana hilo tatizo, watu wa usalama walimtafuta huyo nesi  lakini hakupatikana,...alishaondoka hata kabla ya muda wake wa kazi....unaona hapo...’akasema

‘Kwani huyo nesi ni wa siku nyingi hapa hospitalini?’ niauliza

‘Kwa maelezo yao, huyo nesi sio wa siku nyingi hapa hospitalini, yeye alifika hapo akitokea hospitali ya jirani akija kutoa msaada, na alikuwa na vyeti na barua rasmi za kumhamishia hapa kwa muda, kwa vile barua hizo ni halali, hakuna aliyekuwa na shaka naye na kwa vile kweli hospitali hiyo ilikuwa  na uhaba wa wafanyakazi, ilimpokea nesi huyo kwa mikono miwili.

‘Inaonekana ni jambo lililopangwa kwa umakini wa hali ya juu, na ni kama vile walijua mzee huyo atazidiwa na kuletwa hapo, ni jambo la aina yake kutabiri kuwa mtu ataumwa na hospitali yake ya matibabu ni hapo,na kama walivyokuwa wamejipanga huyo nesi akapangiwa kuwa mmoja wa watu waliokuwa wakimsaidia dakitari na moja ya kazi yake ni kuhakikisha usalama wa vyakula na vinywaji anavyotumia mzee, kwani watu walishashuku uwa hayo yanaweza kutokea.

Watu wa usalama walikwenda hadi huko alipotokea huyu nesi, na wengine wakaenda nyumbani kwake, kote hakuonekana, na walipojaribu kuchunguza habari zake huko alipokuwa kifanyia awali,ikibainika kuwa na hapo alihamishiwa kutoka hospitalini nyingine za mikoani,…na hauko alipotokea walikubali kuwa ni mmoja wa wafanyakazi wao aliyekuwa akitokea chuo cha wauguzi, na alikuwa mtendaji mzuri wa kazi,na akapata uhamisho

‘Ni nani alimpa huo uhamisho?’ akauliza

‘Ni mkurugenzi anayehusika na kazi ya uahamisho, na uhamisho huo hakufanyika kwake peke yake, ililkuwa ni kampeni rasimi ya kuwatawanya wafanyakazi kwenye hospitali mbali mbali ili kuweka uwiano ulio sawa, kwani baadhi ya hospitalini zilikuwa na mapungufu ya wafanyakazi ,

‘Mimi namshuku huyo mkurugenzi pia, kuwa anaweza kuhusika...’nikasema

‘Mkurugenzi ana ushahidi wa kuweza kumlinda hata kama unamshuku,...hili ni kundi lililojipanga vyema na kila mahali kuna watu wao, ...anaweza akahusika au kundi hilo lilitumia mwanya huo kupandikiza watu wao...’akasema

‘Kwahiyo sasa?’ nikauliza

‘Uchunguzi bado unafanyika na hiyo kazi ni ya polisi, ...mimi nitaingiza mguu wangu kwa mambo yangu, lakini sitalifuatilia sana hilo tukio, ..’akasema mpelelezi

‘Huoni kuwa tukio hili linaweza kukupeleka ahdi kwa hao watu?’ nikamuuliza

‘Hiyo sio muhimu sana kwa sasa, kiujumla watu hao wapo wengi, na mimi nilitaka nichimbe kundi hilo hadi mzizi mkuu, wapi tatizo hili lilianzia, na japokuwa mzee kanipa ushahidi mkubwa wa wapi kundi hili lilianzia, lakini mimi mwenyewe nilishajua mengi kabla, na kuwagundua baaadhi ya wahusika wakuu, iliyokuwa imebakia ni ushahidi wa kuwafikisha hao watu kwenye sheria...’akasema

‘Mzee yeye alikupa ushahidi wa maneno, je kuna ushahidi wowote unaoweza kuufikisha mahakamani ukasaidia kisheria...?’ nikauliza

‘Kwanza kuna kitu muhimu sana natakiwa nikipate, na hicho mzee alisisiiza sana kuwa nikipate kwani kina kila kitu, i...’akasema

‘Kitu gani hicho?’ nikauliza

‘Hizo nyaraka nyeti, zipo kumbukumbu na ushahidi mbali mbali ...’akasema

‘Sasa unazo wewe?’ nikamuuliza

‘Sijazipata zote, nilzopata ni kumbukumbu tu za kikasi, bado kuna nyaraka nyeti ambazo ndizo mzee alizifanyia kazi, na kuweka kila kitu wazi,....’akasema

‘Sasa utazipatia wapi hizo nyaraka nyeti...?’ nikauliza

‘Kwa mdada, nina uhakika nyaraka hizo anazo mdada....’akasema

*****

Nilipomaliza kuongea na mpelelezi, akili yangu haikuwa na utulivu niliona ni bora nikaonane na mdada mwenyewe, na sehemu ya kumpata kwa muda huo ilikuwa ni nyumbani kwake, sikupoteza muda nikaelekea nyumbani kwa mdada, nikiwa na uhakika nitaonana naye huko maana nilipopiga simu yake haikuwa hewani.

Nilipofika eneo la nyumba anapoishi mdada, nikakutana na mlinzi, alikuwa akisoma gazeti na aliponiona akaliweka chini na kuja pale getini, na aliponiona ni mimi akasema

‘Oh, bosi wangu, karibu sana....pole na majanga, maana nilisikia walikushikilai tena, kumbe wamekuachia...’akasema na mimi sikutaka kuongea naye sana nikamwambia;

‘Nataka kuonana na mdada...’nikasema

‘Mhh, huyo mtu kaondoka mapema kabisa alifika na hakukaa sana, akatoka akiwa na mizigo kuonyesha kuwa anasafiri, na sizani kama ni safari ya hapa karibuni...’akasema

‘Kwanini unasema hivyo?’ nikamuuliza

‘Kwasababu aliondoka na vitu vingi, ni kama vile mtu anahama, na haikuchukua muda akaja mpangaji mwingine kwenye hii nyumba...’akasema

‘Ina maana hii nyuma sio mali ya  mdada?’ nikauliza

‘Nijuavyo mimi ni nyumba ya familia yao...na aliyeingia kwasasa ni mmoja wa ndugu zake...mrembo kama yeye, kwahiyo usijali, unakata mti na kupanda mwingine, kazi kwako...’akasema huku akitabasamu, na mimi nikasema;

‘Oh, naweza kumuona huyo ndugu yake, huenda akanisaidia kujua wapi alipo mdada..’nikasema na huyo mlinzi akasema;

‘Wewe tena, ..usijali ngoja nikakuunganishie, najua ukifanikiwa hutanisahau....’akasema na kuelekea kwenye hiyo nyumba, baadaye akarudi.

Aliporudi aliniambia huyo mdada ananisubiria kwani na yeye alikuwa anataka kutoka kwenye shughuli zake, na mimi nikaingia ndani, nilikuwa nimeliacha gari langu sehemu niliyozoea kuliacha, kwahiyo niliingia hapo bila gari.

Niliingia ndani nakukutana na huyo binti, ni kweli ni ndugu yake hata ukiangalia sura yake wanafanana sana na kama alivyodai mlinzi kweli dada huyo alikuwa mrembo kama mdada mwenyewe, tukasalimiana na nikajitambulisha  na yeye akasema aliwahi kusikia mdada akinitaja mara kwa mara

‘Akinataja kwa mema au mbaya?’ nikamuuliza na yule binti akatabasamu , tabasamu lile lile la mdada linalonipoteza akili yangu aasema akionyesha aibu;

‘Mhh, kwa mema,...alisema wewe ndiye mtarajiwa wake...’akasema na safari hii akawa kaangalia chini

‘Ndio maana nataka kuongea naye , naweza kumpata wapi, maana simu zake zote hazipatikani...?’ nikamuuliza na huyo mdada akasema;

‘Mhh,sijui kwakweli, kwani alivyoondoka, kasema anakwenda kikazi, na huko anapokwenda hatarajii kurudi hivi karibuni, na hakutaka kutaja ni wapi, ....tumeshamzoea, akipata kazi zake huwa ndio hivyo, anaaga kuwa anaondoka na hasemi anakwenda wapi...’akasema

‘Kwani mdada ana kazi gani nyingine hasa?’ nikamuuliza na yeye atakaniangalia kwa haraka akionyesha kushangaa akasema;

‘Ina maana wewe hujui,...nilijua labda wewe unaweza kujua zaidi, maana Mdada mwenyewe hasemi ana kazi gani, na hakai sehemu moja, mara leo ana kazi hii , kesho anakuwa na kazi nyingine, ukimuuliza mara nyingi anasema yeye kasomea uwakala, mtu kati, kama una biashara , au kama una kazi yoyote ya kufuatilia, unampa yeye anajua jinsi gani ya kuonana na wahusika, hadi kazi yako inakamilika...ndivyo tunavyojua sisi, na ndivyo alivyotuambia , ....’akasema

‘Oh, kwahiyo nitampataje?’ nikauliza

‘Kwakweli hapo siwezi kukusaidia maana anapotuaga, hasemi anakwenda wapi, sana sana atakuambia anakwenda kikazi, wapi hakuambii, na mawasiliano yake yanasitishwa hadi hapo atakapokupigia  yeye mwenyewe,..siwezi kabisa kujua wapi pa kumpata, sisi mwanzoni tulikuwa tukiumiza kichwa sana kumfuatilia, lakini baadaye tukamzoea, ndivyo maisha yake yalivyo, na hakuna anayeweza kumuingilia...’akasema

‘Oh,na hii nyumba ni mali ya nani?’ nikamuuliza

‘Hii ni nyumba ya familia, na nilitakiwa mimi nije kuishi hapa mapema tu, lakini nilikuwa bado nasoma, na nilipomaliza shule, ikapangwa kuwa mimi nije kuanzia maisha yangu hapa na mdada ataenda kuishi kwenye nyumba zake...’akasema

‘Na nyumba zake zipo maeneo gani na wapi, maana huenda naweza kumpata huko..’nikamuuliza na yeye bila hiana akanipa ramani ya wapi nyumba zake zilipo, na kusema;

‘Sizani kama unaweza kumpata huko , nyumba zote zimepangishwa...’akasema lakini mimi nikaona nikajaribu tu

‘Sawa hamna shida, nitazidi kuja kuonana na wewe kama nikikwama, huenda akakupigia simu...’nikasema na yeye akasema;

‘Hamna shida, unakaribishwa wakati wowote...’akasema na mimi nikaondoka hapo

Nilikwenda hadi huko kwenye nyumba zake, lakini zote nilikuta zina wapangaji  kama alivyoniambia mdogo wake mdada, na wapangaji hao hawakujua wapi alipo mdada, walisema wao ikifikia muda wa malipo, wanawasaliana na mdada, na mara nyingi yeye ndiye anapiga simu na kuwaelekeza wapi pa kuzililipa hizo pesa, na hawana tabia ya kunana naye mara kwa mara...

Nilirudi hotelini kwangu nikiwa sijui la kufanya, nikampigia simu mpelelezi kumuelezea hayo yam dada na mpelelezi akasema, hata yeye hawezi kujua wapi alipo mdada, na mawasiliano yake yote hayafanyi  kazi, na kwa vile hana umhimu sana kwake, hajajiangaisha kumtafuta.

‘Simu zake zote hazipo hewani....’akamalizia kusema mpelelezi

‘Sasa nitampataje?’ nikauliza

‘Kwakweli mimi hapo sijui, na siwezi kuhangaika naye kwa sasa, najiandaa kutoa ushahidi wangu kesho ambao utahitimisha hili tatizo...’akasema

‘Kwani umeshazipata zile nyaraka nyeti?’ nikamuulza

‘Sijazipata, kama nilivyokuambia mdada ndiye inawezekana anazo,..lakini ndio haonekani, lakini hazitanifanya nishindwe kutoa maelezo yangu, ambayo yatathibitisha mambo mengi tu, na mlinzi atakuwa shahidi yangu mkuu, na kama atakubali kushirikiana nami, nitaweza kujua mengi ambayo yataweza kumaliza hoja muhimu ya kifo cha mtoza ushuru....’akasema

‘Na inavyoonekana mlinzi anaweza kukutwa na hatia ya kuua vinginevyo amtaje aliyemtuma, kwani inavyoonekana yeye alitumwa, na muhusika hajaweza kutambuliakana, je huyo aliyemtuma ni nani....?’ nikamuuliza

‘Mpaka nione naye, kabla sijaweza kulijibu hilo swali lako,  sasa hivi naelekea huko kuonana naye, sijafika bado ,nikiongea naye naweza kujibu hilo swali, na pia nitakuwa na uhakika wa mambo fulani fulani,..tatizo kubwa ni kuwa wakili wake hataki kumpa nafasi hiyo, lakini mwenyewe mlinzi kanipigia simu kuwa niende tuonane naye kwa haraka,  bila ya wakili wake kufahamu, alisema ana jambo muhimu sana la kuniambia;....’akasema na niliposikia hivyo nikavutika kujua kinachoendelea, nikasema;

‘Naweza kuja kuungana na wewe..’nikasema

‘Kwanini bwana, usijiingize kwenye haya matatizo...lakini kama upo tayari unaweza kuja, utanikuta nje ya gereza alipo huyo mlinzi, ila hutakuwepo wakati naongea naye, nikimaliza kuongea naye, utaweza kumsalimia, na nitakuambia kila kitu atakachoniambia...’akasema

‘Sawa nakuja mkuu...’nikasema nikiwa na shauku, hata kama sitakuwepo wakati wanaongea, lakini nitaweza kupata maelezo ya awali kutoka kwa mpelelezi akimaliza kuongea naye.

Niliondoka na gari hadi kwenye gereza hilo, na nilipofika nilimkuta mpelelezi akisubiri, na tulisalimiana kidogo, baadaye akaja mkuu wa gereza hilo, akasema;

‘Mpelelezi hebu tuongee kidogo,......’akasema na wakasogea pembeni na wakawa wanaongea kwa sauti ya chini, niliweza kusikia wanachokiongea kwa shida,

‘Kuna tatizo limetokea....’akasema huyo mkuu wa gereza

‘Tatizo gani...?’ akauliza mpelelezi

‘Mlinzi kakutwa kwenye chumba chake akiwa haijiwezi, na akakimbizwa hospitalini, lakini hakufika hospitalini, akafia njia, na docta alipomchunguza alisema huyo mlinzi kafa kwa sumu, alikuwa kanywa sumu....’akasema

‘Haiwezekani.....’akasema mpelelezi kwa hasira

‘Ndio hivyo mpelelezi, nimezipata hizi taarifa kwa machungu makubwa sana, na upelelezi wa haraka unafanyika, na inavyoonekana ni kama aliamua kujiua mwenyewe...’akasema

‘Sizani kama alifanya hivyo, hilo la kujiua halipo, atakuwa kauwawa...’akasema mpelelezi

‘Tutaliona hilo baada ya uchunguzi,....’akasema huyo mkuu, na mpelelezi akauliza

‘Na huyo wakili wake yupo wapi? Akauliza mpelelezi

‘Alikuwepo hapa, hajaondoka, nimetoka kuongea naye muda mfupi uliopita, yeye alifika mapema tu alipopewa hizo taarifa, alifika kujua ilivyotokea, na kama wakili wake,amesisitiza upelelezi wa hali ya juu ufanyike, ....’akasema mkuu huyo.

‘Nataka kuonana na huyo wakili ni muhimu sana nikutane naye aniambie ukweli, haiwezekani hili litokee, na kwanini mara nyingi alikuwa akinizuia nisiongee na huyo mtu, huyo wakili, yupo wapi, ana jambo analifahamu...?’ akauliza mpelelezi kwa sauti ya hasira.

‘Nipo hapa mkuu...’sauti nzito ikatoka nyuma yetu,

NB: Haya mzee, kapewa sumu, yupo chumba cha upasuaji, mlinzi mtuhumiwa mkuu keshamalizwa, ni nini kitatokea.


WAZO LA LEO: Ubinafsi ni hulka ya kibinadamu, kila mmoja anapenda apate yeye, na ikiwezekana apate yeye zaidi ya wengine. Upendo wa kweli , imani ya kweli ya kiroho, inatokana na jinsi gani mtu atakavyoweze kuishinda hiyo hali ya ubinafsi, ikakufanya ukapambana na tabia hiyo ya ubinasfi.

Ili ujione umeshinda, ni pale utapokeweza kumjali mwenzake kuliko wewe,...awe tayari kukosa kwa ajili ya mwenzake, uwe tayari kuona mwenzako anapata kabla yako...na ukifikia kwenye hilo daraja basi wewe ni muumini wa kweli, wewe una upendo wa kweli, wewe ni mcha mungu wa kweli.

Ni mimi: emu-three

No comments :