Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, June 2, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-68


‘Unasema humo kwenye huo mkoba kuna bastola, oh, hiyo bastola unahisi ni ya nani?’ nikauliza na yeye akaangalia ule mkoba pale chini, akausogelea ule mfuko na akiwa amevalia kinga mkononi mwake, akautoa ule mkoba, akaufungua, mimi nilitaka kumzuia lakini akawa ameshafungua ule mkoba.

Alipofungua ule mkoba,bastola ilionekana dhahiri ikiwa na makabrasha mengine, na moja ya jarida hilo kuna  maandishi makubwa yaliyoandikwa: `HATI ZA SIRI’ Na mimi nilipoona hayo makabrasha na ile bastola nikajikuta nikisema;
‘Kweli….’

Niliiangalia ile bastola, kwa wasiwasi, na nilimuona mdada akiitizama ile bastola bila kuigusa, akasema;

‘Hata hivyo, japokuwa sijaikagua vyema, ...ila inaonekana imetumika, ..’akasema

‘Umejuaje?’ nikamuuliza

‘Mhh, ....kuna risasi zimepungua...’akasema

Mimi nilipoitizama ile moyoni niliumia sana, nikikumbuka kuwa kitu kama hichi kimeshatoa uhai wa mtu, moyoni nikawa naogopa hata kuitizama zaidi, lakini nikajikuta nikisema;

‘Oh, Mungu wangu, ina maana hawa watu walitaka kunibambikia kesi ya mauaji, kwanini watake kuniwekea bastola, na hizo hati za vidhibiti vya polisi, kwanini wanataka kufanya hivyo, wakati wanajua fika kuwa mimi sikumuua mtoza Ushuru, wananitafuta nini hawa watu, ni kwasababu ya hicho cheo…?’ nikawa namuuliza mdada na mdada akatabasamu kidogo, na mimi nikaendelea kuongea.

‘Eti Mdada, hebu niambie, kwanini wafanye hivyo, kwanza mimi sijawahi kumilii bastola, na hata hiyo bastila sijui ni ya nani....’ nikasema, na mdada akawa anaufunga ule mkoba na kuurudisha kwenye ule mfuko wa nailoni akaubeba na kuuweka kabatini kwake na kulifunga lile kabati, akasema;

‘Hiyo bastola ni ya kwangu....’akasema aliporudi kutoka kuweka vile vitu kwenye kabati,na kuniangalia machoni, na mimi nikabakia mdomo wazi na nilisimama nikionyesha mshangao,nilikodoa macho kumuangalia mdada, kama vile nimeona kitu cha kutisha.

Mdada bila wasiwasi akakaa kwenye sofa dogo lililopo mbele yangu, na kujiegemeza, halafu akakunja nne, mguu mmoja akauweka juu ya mguu mwingine, na kwa kufanya hivyo sehemu kubwa ya mapaja ilikuwa wazi.

Mimi bado nikiwa na ile hali ya mshituo, lakini macho hayana pazia, kwa haraka ikaona ile hali, na macho hayakutosheka, yakataka kuhakikisha, kwahiyo yakahama kumtizama mdada usoni, yakawa yanaangalia yale mapaja ya mdada, ibilisi sio mchezo,….

Tuendelee na kisa chetu….

**********
Mdada akiwa hana wasiwasi akainua kichwa kuniangalia, hakuhangaikakujifunika vyema, akasema;

 ‘Hiyo bastola uliyoiona hapo ni yangu, sijawa na uhakika ni kwanini,imewekwa hapo,….’akasema

‘Waliichukua lini, ?’ nikauliza nikipumua kidogo, na yeye hakujibu swali langu mara moja akaendelea kuongea.

‘Ni lazima kuna sababu muhimu ya kuifanya hivyo ....’akasema

‘Sababu gani , mimi hata sielewi....’nikasema

‘Hivyo ni vidhibiti vya polisi, hayo makabrasha walikuwa wakiyatafuta polisi kipindi fulani mwanzoni na ikasadikiwa kuwa yamepotea, sasa kama ni hivyo, hata hiyo bastola itakuwa na jambo muhimu kwa polisi....’akasema.

‘Itakuwa na jambo gani muhimu maana mimi nijuavyo, na hata mahakamani walipokuwa wakitoa ushahidi bastola iliyotumika kwa mauaji ni bastola ya mtoza ushuru mwenyewe...sasa hii bastola yako ina maana gani?’ nikauliza

Mdada akanitizama, na alitaka kusema kitu, lakini akaghairi, akawa kama anawaza jambo, na akautoa ule mguu juu ya mwingine, na nahisi aliona jinsi ninavyomtizama, akapandisha vyema nguo yake na kujifunika, halafu akaiweka miguu yote chini akasema;

‘Lolote lawezekana.....’akasema

‘Wewe unafikiriaje ni kwanini bastola yako iwepo hapo,na hata wewe mwenyewe usiwe na taarifa, kwani wewe ….’nikataka kuongea zaidi lakini nikasitai. Mdada akajiweka sawa na akawa kama anachezesha miguu yake, na kutoa mlio sakafuni, na mimi nikawa naangalia hicho kitendo, akashika kichwa kama anajikuna, akatabasamu na kusema;

‘Hebu tumia akili kidogo.....’akasema

‘ Kwa vipi mdada, hilo sio fungu langu....’nikasema na yeye akakunja uso kwa kutafakari, akasema;

‘ Kama unakumbuka vyema,siku ile wakati tunaongea na mpelelezi , unakumbuka alisema nini kuhusu bastola yangu....?’ akawa kama ananiuliza na mimi nilipotoka kusema kitu, akanikatiza na kusema;

‘Mpelelezi alitaka kujua kuhusu bastola yangui,mimi pale pale nilihisi kuna jambo....’akasema

‘Na hapo bado ulikuwa hujajua kuwa bastola yako haipo?’ nikauliza na hakujibu swali langu moja kwa moja, aliendelea kusema;

‘Mimi niliporudi nyumbani nilienda sehemu ninapohifadhi bastola yangu,nikiwa najiamini kabisa, mhhh, sikuiona…’akatulia kidogo

‘Mhh, ina maana ilichukuliwa siku nyingi au...?’ nikauliza

‘Hapana sio siku nyingi, maana siku kabla ya kifo cha mtoza ushuru niliiona, nilitaka kuwa nayo tayari, kama mtoza ushuru atakuja na shari....’akasema

‘Oh, ..sasa....’nikasema

‘Mpelelezi aliposema kuwa anataka kufahamu kuhusu bastola yangu akilini nilianza kuingiwa na wasiwasi, na kujiuliza kuna nini kuhusu silaha yangu, na nilitaka wakija hao vijana wake kama hawana kibali, nisiwape,...’akasema

‘Walipofika uliwaambia nini?’ nikauliza

‘Hawakufika ….’akasema akibenua mdomo kwa tabasamu lisilo la furaha.

‘Kwanini hawakufika….?’nikauliza kwa mshangao

‘Kwakeli siwezi kujua , lakini ukiangalia kwa makini,inaonyesha kuwa mpelelezi alikuwa anafahamu kuwa hiyo bastola haipo mikononi mwangu,na aliniuliza palekunitega,….’akasema

‘Aaah, hapana mpelelezi hawezikufanya hivyo, kwanini afanye hivyo…?’ nikauliza na mdada akanitizama kwa mashaka, akasema;

‘Acha ushamba wewe, naona mpelelezi keshakuweka sawa, unamuamini tu….huyu mpelelezi amekuwa akinitafuta sana, amekuwa akinishuku , kwanza alihisi mimi na mtoza ushuru tuna biashara ya pamoja, akakosa ushahidi,....na hata hivyo hakukoma, nahisi kuna jambo ananihisi vibaya, na nia yake ni kuona mimi naingia matatani, na kwahiyo amekuwa akiniwinda kwa muda mrefu…’akasema

‘Mhh, lakini  mpelelezi hana nia mbaya na wewe, nijuavyo mimi lengo lake ni kuhakikisha haki inatendeka, wewe humfahamu vyema huyo mtu, ni muadilifu na anatimiza wajibu wake tu….’nikasema

‘Wewe ndio humfahamu vyema huyo mtu,…’akasema mdada huku akiegemeza kichwa kwenye sofa akiangalia juu.

‘Mhh,haya wewe niambie kwanini sasa yeye hashirikiani na polisi,akakufunga maana ushahidi mwingi anao wa kuonyesha kuwa wewe unahusika…’nikasema

‘Ushahidi upi unaonyesha hivyo, …?’ akauliza na mimi nikawa kimiya na yeye akainuka pale alipokuwa amekaa na kukaa vyema akainua mguu kutaa kuweka juu ya mwingine, lakini alipoona nguo yake unamuacha wazi mapajani, akasimama huku akisema;

‘Mpelelezi ni mjanja sana, ndio maana hataki kushirikiana na polisi wengine baada ya kubaini kuwa hawala lengo alilonalo yeye, .....yeye anatafuta sifa, anataka kuwa shujaa, kwa kufanya jambo ambalo wenzake wameshindwa kulifanya....’akasema

‘Mhh, .....’mimi nikaguna na  yeye akaendelea kusema;

‘Hata huu mtego utakuwa umepangwa na huyo mpelelezi, nia ni kutaka mimi na wewe tusimame kizimbani kwa kosa la kushiriki katika mauaji ya mtoza ushuru, baada ya kuona kuwa hatuhusiki moja kwa moja…’akasema mdada

‘Lakini sisi hatuhusiki na yeye anafahamu hivyo, ndio maana hajafikia hatua ya kutuweka ndani, mimi hayo unayoongea wewe, hata sikuelewi na nikuulize swali, wewe ulipoona kuwa bastola yako haipo ulichukua hatua gani? nikamuuliza.

‘Mhasibu, mimi najua nini ninachokifanya, sikusema lolote kwa yoyote, zaidi ya kufanya uchunguzi wangu binafsi…..’akasema

‘Oh,mdada, kwanini,  wewe unafahamu hatari iliyopo na vyombo vya hatari kama hivyo, watu watavitumia vibaya,mwisho wa siku utaonekana ni wewe uliyefanya hilo tukio…’nikasema

‘Lengo langu ilikuwa kwanza kupoteza muda ili nijue wapi bastola yangu ipo, sikuwa kimiya tu, nilijitahidi kufanya uchunguzi wangu binafsi, lakini hata watu wangu hawakuweza kupata lolote kuhusiana na bastola yangu ….’akasema

‘Watu wako, watu wako, ni akina nani hao watu wako?’ nikamuuliza na mdada hakutaka kusema lolote kuhusu hilo swali langu, akaendelea kusema;

‘Nilipoona hivyo, bastola yangu haipo, na hata huko polisi kwenyewe hakuna taarifa yoyote, nikajua watu waliofanay hivyo, ni kundi lisiloshirikiana moja kwa moja na polisi, na hapo nikajua ni undi la mpelelezi…’akasema

‘Uliwahi kumuuliza?’ nikasema

‘Lini...! wewe unaona mambo yalivyojitokeza kwa haraka, sijapata muda kabisa wa kuonana na huyu mtu, ....’akasema

‘Ungempigia hata simu, ili uweze kufahamu zaidi,...’nikasema

‘Mimi ni mtaalamu, najua nifanye nini kwa wakati gani, ningelionana na mpelelezi kwa muda huo nisingeliweza kupata chochote, nilitaka kuvuta subira, na subira yangu ndio hii, bastola nimeiona, lakini ndani ya vidhibiti vya polisi....’akasema

‘Sasa...?’ nikauliza

‘Kuna maswali nataka nipate majibu yake,  ni kwanini bastola yangu ichukuliwe, tena kwa siri,halafu imewekwa pamoja na vidhibiti vya polisi... .ndio maana nafanya uchunguzi wa haraka’akasema

‘Kwahiyo sasa umeshapata majibu ya uchunguzi wako?’ nikamuuliza

‘Kiujumla bado, nilimtegemea sana  mtu wangu anayenisaidia ndani ya polisi, lakini hata yeye kashindwa kulibaini hilo na sasa kahamishwa, japokuwa hakuwa peke yake kwenye kazi zangu lakini huyo alikuwa karibu sana na jikoni…..’akasema

‘Haiwezekani, sasa ni polisi wa namna gani, ....sisi tunajua polisi wote ni kundi moja...’nikasema

‘Polisi ni kundi moja lakini ndani yake kuna idara tofauti, na kila idara ina namna yake,...ila mwisho wa siku kama ni tukio kama hili la maujaji, watendaji hukaa pamoja na kujenga hoja ya pamoja, na baada ya uchunguzi kila mmoja analeta taarifa yake...’akasema

‘Kwahiyo waliofanya hivi ni kundi gani, ni idara gani?’ nikauliza na mdada hakujibu swali langu akaendelea kusema;

‘Sasa natafuta majibu ya maswali yangu, kwanza kwanini walichukua bastola yangu, pili kwanini watake kukuwekea wewe huo ushahidi, na kwanini iwekwe kwenye hivyo vidhibiti vya polisi….’akatulia

‘Sasa utayapata wapi majibu ya maswali yako?’nikamuuliza

‘Majibu  ya maswali yangu nitayapata kutoka kwa huyo mpelelezi,yeye anafahamu ukweli wa hayo yote…lakini kwa hivi sasa nashindwa jinsi gani ya kumuingia, huyu mtu sasa amekuwa ni adui yangu mkubwa,na sitakii kushirikiana naye kwa lolote lile, maana atanitumia kujijengea sifa anayoitaka….’akasema

‘Mhh mdada kwanza nikuulize hayo yote unayofanya wewe ni kwa masilahi ya nani, maana na wewe unajifanya polisi, kwanini unaingilia kazi za watu?’ nikamuuliza na yeye akaniangalia kwa makini,na badala ya kunijibu swali langu akasema;

‘Mimi nataka nikupe kazi,....’akasema na mimi nikashituka na kumuangalia, na bila kunipa nafsi ya kumuuliza swali akasema;

‘Nataka, ili kulikamilisha hilo zoezi, wewe  unisaidie kupata majibu ya hayo maswali yangu, na sio kunisaidia, ni kwa ajili ya kujisaidia wewe mwenyewe….’akasema na mimi nikamuangalia mdada kwa mashaka, na kichwani nikawa najiuliza huyu mtu kachanganyikiwa nini, mimi nitayapata wapi hayo majibu,sijui chochote kuhusu nyanja hizo, mwishowe nikamuuliza;

‘Mdada una uhakika na hicho unachokisema?’ nikamuuliza na yeye akatabasamu na kuniangalia moja kwa moja usoni, akasema;

‘Hiyo kazi ninakupa wewe, …utafute,ujue ni kwanini bastola yangu ilichukuliwa kwa siri, na kwanini imewekwa hapo kwenye vitu vinavyotafutwa na polisi kama ushahidi wa mauaji ya mtoza ushuru,…..’akasema

‘Kwa vipi,mimi nitajuaje hayo maana hiyo sio fani yangu kabisa, unafahamu fika  mimi sio mpelelezi na hebi niambie nitaanzia wapi kupata taarifa kama hizo, mdada nahisi umeshaanza kuchanganyikiwa…’nikasema;

‘Hahaha, mhasibu ninataka wewe uongee na mpelelezi, yeye ni rafiki yako, na anaweza kukuambia, cha muhimu ni kuwa na uhakika, ...tumia akili ya kuzaliwa sio lazima utumie utaalamu wa kipelelezi.….’akasema na mimi nikabakia kimiya, na yeye akaendelea kuongea;

‘Huyo rafiki yako, nimegundua kuwa anafahamu mambo mengi ambayo hata mimi siyafahamu, kama angejikita kwenye mambo yake, nisingelikuwa na matatizo na yeye, lakini sasa keshafikia hatua ya kunitishia mimi amani,nashindwa kukutana naye tena uso wa uso, nita….’akasema mdada na kukatisha akionyesha kukerwa, hadi nikaogopa asije akabadilika.

Ulipita muda kidogo, halafu mimi nikauliza;

‘Oh,mimi nitamuanza vipi huyu mtu…na hivi sasa keshakata mguu kwangu kasema haniamini tena,kwa vile nimemficha ukweli kuhusu maswala hayo ya ndevu…’nikasema na mdada akasema;

‘Sasa kamuambie ukweli ulivyokuwa kwanini ilitokea hadi ukaweka hizo ndevu, lakini kwa ajili ya kupata ukweli kuhusu huu mzigo hasa kuhusu hiyo bastola, na hili linatakiwa kujulikana haraka iwezekanavyo kabla sijasimama kesho kutoa ushahidi,…’akasema

‘Nitampataje maana kwa hivi sasa nikimpigia simu,hapokei…’nikasema

‘Ulimpigia lini simu kwa mara ya mwisho akaacha kupokea simu yako?’ akaniuliza

‘Wakati nipo hotelini, nilipowaona wale jamaa wawili...’nikasema

‘Sasa mpigia tena, na usitume ujumbe kuwa unao huo mzigo, mpigia tena na tena, mpaka atahisi upo kwente tatizo, akipokea usiongee naye sana, wewe mwambia kwa kifupi, ninao mzigo wanaoutafuta polisi, fika tuonane, kata simu, yeye mwenyewe atakupigia.’akasema

‘Mdada hapana,..hiyo kazi mimi siiwezi kwanini usiwape hao vijana wako, huoni kuwa hilo sasa ni bomu,…..’nikasema

‘Sikiliza mhasibu ina maana mimi niliyejitolea kuliondoa hilo bomu chumbani kwako kukuokoa wewe mimi ni mjinga,….okey, kama unanion mimi ni mjinga  mimi nitaurudisha huu mzigo huko kwako, wewe mwenyewe utajua jinsi gani ya kufanya,kazi kama hizi hazihtaji kubembelezana….’akasema mdada

‘Sikiliza mdada,wazo langu ni hili huo mzigo wanautafuta polisi njia nzuri na sahihi ni kuupeleka huu mzigo huko huko kwa hao polisi, natumai  wao watajua jinsi gani gani ya kufanya,…au tuuweke sehemu ambayo wenyewe watakuja kuuona’nikasema, na mdada akacheka na kusema;

‘Kama kuna watu kichwa maji,basi na wewe ni miongoni mwao, hebu jiulize kwa kutumia akili yako ndogo tu usiumie kichwa ni, kwanini polisi hao hao walitaka kuuweka huo mzigo hapo kwako….jiulize kwanza hilo swali, halafu wewe unauchukua na kuwarudishia wao……tumia akili kidogo kuliwazia hilo…’akasema

‘Kwani ni polisi waliouweka au ni wale jamaa wawili, kama hatuwaamini hao polisi wengine basi sisi tupeleke kwa mkuu wa polisi wa kituo, yeye atajua la kufanya….’nikasema

‘Sikiliza kazi kama hizi ukipewa jukumu hutakiwi kukaidi, ...sasa mimi nitaurudisha huo mzigo chumbani kwako, na nitawaambia polisi,waje huko kwako watakuja kuuchukua huko kwako,na wewe utajieleza mweneywe, sasa tuone ni nini kitafuta baadaye….’akasema na mdada kwa sauti ya hasira na hapo mimi nikaanza kuingiwa na wasiwasi,

‘Sasa unataka mimi nifanye nini?’ nikauliza

‘Nimekupa ushauri wa bure, wa wewe kuonana na mpelelezi, na nafahamu sasa hivi atakukwepa kuongea na wewe, sasa hivi anahisi mimi na wewe ni kitu kimoja, lakini tunaweza kumvuta kwa kutafuta jambo zito, na jambo zito kwa sasa ni huu mzigo,huu mzigo una uzito mkubwa kwa sasa na ni bomu ambalo hatujui litalipukaje…mtaalamu wa kulitegua hilo bomu  ni huyo mpelelezi, ….’akasema

‘Kwahiyo nimpigia simu huyo mpelelezi nimuambie kuwa huo mzigo ninao hapa kwako,au?’nikauliza

‘Huu mzigo hautakiwa kuwa hapa kwangu, nilichofanya mimi nikuuondoa pale kwako kwa muda ili polisi wasiuone, mimi nitaurudisha pale kwako,na wewe muite mpelelezi mkutane  hapo kwako yeye atajua jinsi gani ya kufanya,….unanisikia umenielewa,au sio, sasa wewe ondoka,huu mzigo utaukuta huko kwako..’akasema

‘Utafikaje huuko kwangu….?’nikauliza

‘Hiyo sio kazi yako,…’akasema na mara tukasikia mlango ukigongwa, na mdada akasimama na kuelekea pale mlangoni, akawa anaongea na mlinzi wake, na baadaye nikasikia akisema muite aje, kukawa kimiya kidogo, halafu nikasikia mdada akiongea na mtu mwingine, waliongea kwa dakika kadhaa, baadaye madada akatoka pale mlangoni na kuja kukaa name kwenye sofa akasema;

‘Hali sio shwari,...’akasema

‘Kwani vipi...?’ nikauliza nikiwa na wasiwasi

‘Polisi.....’akasema mdada akiangalia kule kwenye kabati lake.

NB: Polisi wamechachamaa, je bomu litalipukia wapi, tuwemo  kwenye sehemu ijayo.


WAZO LA LEO: Ucha mungu wa kweli wa mtu unaonekana katika matendo yake.  Siku hizi uchamungu unakuwa kama maigizo,watu wanakwenda kwenye nyumba za ibada, ili waonekane kuwa wao ni wacha mungu, hata kujinadi kwa watu, kuwa wao ni wacha mungu,  lakini ndani ya mioyo yao na katika matendo yao, ni afadhali ya shetani, mimi najiuliza tunamdanganya nani,  hivi kweli mwenyezimungu anadanganyika, kamwe mwenyezimungu hadanganyiki,  kwani yeye ni mjuzi wa siri na dhahiri. Tujirekebebishe ili tujenge jamii ya watu waadilifu.
Ni mimi: emu-three

No comments :