Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, May 23, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-63

                   

Huyu mzee anataka nionane naye kwa haraka,mimi na yeye tulishamalizana, na sitaki tena kazi zake...akasema mdada na mpelelezi akamuangalia kwa mashaka na kumuuliza

Ina maana kumbe hayo unayoyafanya ni kwa ajili ya huyo mzee? akauliza mpelelezi akimkazia jicho mdada, na mdada akacheka kwa dharau na kusema;

Sikiliza wewe mtu,  tusifuatane fuatane, mimi siwezi kumfanyia kazi mtu kama yule, hivi unanionaje mimi, kuwa nina shida sana ya pesa au...atanipa nini yule mzee...nilikataa aliponipa kazi ndogo kwa ajili kumchunguza huyu mtu wako...akasema akinionyeshea mimi na mimi nikabakia kimya, akaendelea kuongea

Eti alitaka kuhakikisha kuwa kweli huyu mtu anaweza kumuoa binti yake, na kama kuna mambo mabaya anayoyafanya, nimuarifu kwani keshamharibu binti yake na wamewekeana mikataba kuwa atamuoa binti yake..ni hivyo...akasema mdada, na kabla mpelelezi hajasema neno akendelea kuongea;

Na, kwa vile ni nilishamuona mhasibu ni mtu asiye na msimamo, nikaona nimuweke sawa, ...unaona jambo moja likazaa jingine, nimegundua kuwa anaweza kuishi na mimi,..okey, hata kama kamzalisha huyo binti yake, lakini hiyo ilikuwa Ini bahati mbaya, muulize huyu mtu kama hajazimia kwangu, ananihitaji mimi kama ninavyomuhitaji yeye....akasema

Sasa huyo mzee, kaligundua hilo, akawaka, nimekutuma kazi, wewe unanigeuka, unamuibia binti yangu mchumba wake,..nikamuambia, katika makubaliano yetu, hatukuwahi kugusia hilo kuwa mimi na huyu mtu tusije kupendana, imetokea tumependana kiukweli, sasa tufanyeje...akaendelea kusema

Mdada...nikawa nataka kusema lakini akaniashiria ninyamaze, na mpelelezi akauliza

 Okey, sasa unataka kuonana na huyo mzee kwa ajili gani? akauliza mpelelezi

Binti yake alinitumia ujumbe wa vitisho, kuwa nisipoachana na mchumba wake, atanifanyia kitu mbaya, na waakti huo huo walishakaa kikao na kukatisha uchumba wake na mhasibu, kwahiyo uchumba wao haupo tena....akasema

Sasa tuwaelewe vipi,huo ujumbe wao una maana gani,unajuawanielewe sana, hata wewe unielewe hivyo,kuwa sipendi kutishwa, kwanza kuhusu hiyo familia, mimi...nataka hilo swala la uchumba wao na mhasibu waliweke wazi, kama bado upo tuelewe, na mhasibu atamke wazi ni mimi au ni huyo mshamba wao...akasema

Na pili waachane na vitisho vyao kwani mimi sio mtu wa kutishika,hata hivyo mzee huyo namuheshimu sana nisingelipenda aje kuniona mtu mbaya kuna lolote jingine aniambie, vinginevyo, watanijua..akasema mdada

Lakini na wewe mdada, huoni kama unaingilia uchumba wa watu, kwanini usitafute mchumba wao mwingine, kwani ni lazima huyu mhasibu, wanaume wapo wengi, au una ajenda gani ya siri na mhasibu? akauliza na mdada akageuka kumuangalia mhasibu, huku akitabasamu kwa dharau na akasema.

Hayo hayakuhusuau na hiyo ni mojawapo ya kazi zako, tuambie tujue, kama upelelezi wako ni pamoja na maswala ya mahusiano na ndoa za watu....akasemana mpelelezi akatabasamu, na mdada akiwa kakunja uso akasema;

Hata hivyo, nina imani haya yatakwisha tu, ila ni lazima niionyeshe hiyo familia kuwa mimi sio mtu wa mchezo,mimi sitishiki na ndumba au kwa lolote lile,.., anyway, kwa vile nilishapanga nionane naye, haina shida, naona kila kitu kimejipa kama nitakavyo...akasema mdada, na kuangalia saa yake huku akiwa ameshaweka mkoba wake mkononi

Mpelelezi, naye akaangalia saa yake, na hakuonyesha dalili ya kutaka kuondoka, kwa muda huo alikuwa akimtizama mdada, na mdada alimpomtupia jicho mpelelezi na kumuona anamuangalia yeye, kwa haraka,akatikisha kichwa kama kusikitika akasema;

Natumai tumemalizana...sitaki tena kufuatana fuatana...akasema halafu akageuka kuniangalia mimi, na kusema;

Na wewe mtu wewe, nitakuja hotelini kwako nina mazungumzo na wewe, na wakati naongea na wewe sitaki usumbufu na huyu mtu wako, it will be strictly business, between me and you,....umenielewa wewe mtu....akasema akinisogelea na aliponikaribia akawa kama ananibusu shavuni huku akininongonezea akisema;

Ole wako urope ovyo, hakuna zaidi ya hayo niliyosema...akasema na akawa kama ananibusu shavuni

Mpelelezi akawa anatuangalia huku akitabasamu, nahisi alijua ni mambo ya wapendanao, halafu mdada akamgeukia mpelelezi na kusema;

Kama una maongezi na huyu mtu mumalizane kabisa, sitaki tena nikiongea na huyu mtu wangu wewe kuja kupiga chabo, unapenda sana kuniingilia mambo yangu...akasema huku akitabasamu kwa dharau na mpelelezi akawa anatabasamu tu

Usijali, nitajiathidi nifanye hivyo, ilimradi na wewe uwe mkweli...lakini huyo ni mtu wa watu, ukumbuke hiloakasema mpelelezi

Nani kasema ni mtu wa watu,  huyu mtu , ni mtu wangu kwa ndani na nje...sasa semeni mpendavyo,mmh, najua mtasema oooh, mdada kaiba mchumba wa mtu, hivi mapenzi yanalazimishwa jamani, kama hapendwi mtu hapendwi tu ....akasema mdada halafu akanigeukia na kuniminyia jicho moja, na kugeuka kuanza kuondoka, na mimi nikasema.

Mdada hivi unavyofanya sio sahihi... nikasema na yeye akaniashiria na mkono kuwa ninyamaze, halafu akabenua mdomo wa dharau na kusema;

You will see...akaanza kundoka bila kuangalia tena nyuma

Tuendee na kisa chetu...

Mdada alitangulia kuondoka, baada ya kunipa vipande vyangu kuwa atahitaji kuongea na mimi hotelini kwangu, na alipoondoka tukabakia mimi na mpelelezi, mpelelezi akaniuliza;

Wewe unahisi mdada anafanya hivyo kwa ajili ya nani, sidhani hayo anayoyafanya anayafanya kwa masilahi yake binafsi au kwa ajili ya huyo mzee, huyo mzee, hawezi kumpa kazi zake huyu binti, maana huyu binti anafahamika, haaminiki, unahisi anamfanyia nani hiyo kazi anayoifanya? akaniuliza

Kiukweli mimi simuelewi kabisa mdada, huwa hatabiriki, na mipango yake mingi ipo hivyo,sijui anachofanya ni nini, na kwa masilahi ya nani, nimuonavyo mimi ni mambo yake ya kufanikisha kazi zake, kama anataka biashara, au kutoa gari bandarini, anaweza kumvaa yoyote ili kuhakikisha anafanikiwa,lakini alivyo, hawezi kukuambia kitu, na ujue akikuambia hicho kitu atakuwa keshajipanga na huwezi kumpinga tena...nikasema

Mhasibu ni kwanini hamsemi ukweli kuhusu huyo mtu aliyekuwa na ndevu, mimi nimegundua kuwa huyo mtu ni wewe, ni wewe uliyejibandika hizo ndevu, lakini nashindwa kujua ni kwa madhumuni gani,....akasema

Kama alivyokuambia mdada, mtu kama huyu hayupo...nikasema

Kama mtu kama huyo hayupo basi ni wewe, haya niambie mlifanya hivyo kwa makusudioa gani? akaniuliza na mimi nikabakia kimiya nikijiuliza kichwani sijui nimuambie ukweli yaishe tu, lakini kwa hali nyingine nikakumbuka onyo la mdada akinikanya kuwa hilo jambo liwe kati yangu mimi nay eye tu, nikasema;

Mpelelezi, nikuambie kitu, mimi sioni kwanini upoteze nguvu zako nyingi kumtafuta mtu kama huyo, kiufupi huy mtu hayupo, kama alivyokuambia mdada, na hawezi kuhusika na hayo ,mauaji...nikasema

Kwa kauli yako hiyo mimi nahitimisha hapo kuwa huyo mtu alikuwa ni wewe, na mlifanya hivyo na mdada, ili wewe usijulikane na marehemu, labda kwa usalama wako, kwa vile wewe ulitumwa kuchukua huo mzigo...akasema mpelelezi na mimi nikakaa kimiya.

Kwa kukaa kwako kimiya natumai tumekubaliana na hilo, ila kwa tahadhari, polisi bado wanamtafuta huyo mtu, kwani kwa jinsi walimvyomuhoji huyo mlinzi, wanahisi kuna jambo jingine limejificha wenye hayo mauji...akasema mpelelezi

Jambo gani? nikauliza

Kwanini huyu mtu awepo na kutowekabila hata kuonekana, na wewe ulikuwa na nafasi zaidi ya kumuona, kama hakuna mlango mwingine wa nyuma, na kwanini kazi aliyofanya huyo mtu iwe sawasawa na kaziuliyofanya wewe...akasema mpelelezi

Una maana gani kusema kazi aliyofanya yeye, ni sawa na kazi niliyofanya mimi? nikamuuliza

Huyo mtu aliongea na mlinzi, na mlinzi akampa taarifa ya huyo mgeni, yaani marehemu na maelezo hayo hayo ndiyo uliyotupaambia sisi kuwa uliongea na mlinzi, hapo umejinasa na polisi wanawatizama nyie wawili, kama mna ajenda fulani inayohusiana na hayo mauaji...akasema

Polisi wanaweza kusema lolote, je wewe unahisi nini kuhusu hayo yote...? nikamuuliza

 Lolote linawezekana kwa sasa, hasa ukiwa na watu kama hao, na mtu kama mdada, mdada ni mjanja sana...lakini nitakuja kugundua mwenyewe ni kitu gani kipo nyuma ya haya yote, nilichotaka kukifahamu zaidi ni mazingira ya ndani ..ni nini kilitokea kabla na baada ya hayo mauji, kipindi hicho mpo humo ndani....akasema na kuangalia saa yake.

Natumai yote umeyasikia, sizani kama unahitaji maelezo zaidi...nikasema

Nikuulize kitu, wakati upo chini, ulisema mdada, alimtupa marehemu kama kagunia kutoka chumbani hadi bchumba cha maongezi, na halikadhalika wewe,  ukaangukia karibu na marehemu, marehemu kwa muda huo alikuwa akijaribu kujizoa zoa, kuifuatilia ile bastola, je kwa muda huo mdada alikuwa katika hali gani? akaniuliza na mimi nikatulia kama nawaza jinis ilivyokuwa

Nilimuona mdada kama anayumba yumba hivi....sio kama alivyokuwa ndani, na wakati huo, marehemu alikuwa karibu kuishika ile bastola.....na pale nikajiona  napambana na maadui wawili, lakini pia nikiwa na lengo la kumsaidia mdada, japokuwa kwa muda huo nilikuwa namuogopa, kwani marehemu alikuwa akiiendea ile bastola, na akiishika atamua mdada, na mimi pia...nikasema

Kwa maelezo ya dakitari, na hata wanandugu waliowahi kumshughulikia mdada, ni kuwa ile hali ya kubadilika kwa mdada, ikianza kuondoka, ili arejee katika hali yake ya kawaida, huwa anaishiwa nguvu, kama alikuwa amesimama ni lazima atadondoka....akasema mpelelezi na mimi nikawa nawazia siku ile ilivyokuwa, na kuanza kuhisi jambo ambalo sikuweza kuliweka vyema kichwani.

Kama ni hivyo basi,marehemu alikuwa na uwezo wa kuichukua ile bastola na kufanya lolote, kwanini ...hapo sielewi,..ina maana hapo mdada, alikuwa hana nguvu tena kama awali,kuyumba kwake kulionyesha kuwa ile hali ya ushetani ilishakwisha, au sio, ...nikawa naongea

Hivyo basi yeye asingeliweza kuichukua ile bastola na kumuua marehemu, atakuwa alidondoka chini, ina maana basi hapo ni lazima kulikuwa na mtu mwingine na huyi mtu ni lazima atakuwa ni huyo mlinzi ..huyo mtu mtu mwingine ndiye aliyemaliza kazi, ni nani huyo...nikasema.

Yawezekana pia asiwe mlinzi, ndio maana mpaka sasa polisi wanaendelea kumtafuta huyo mtu mwenye ndevu, ...kama mlinzi amekataa kata kata kuwa hakuwahi kuishika hiyo bastola, na anadai kuwa mlio wa bastola aliusikia akiwa ndani,..chumbani mwa mdada, akitafuta kitu alichotumwa na bosi wake....akasema

Mhh, hapo nashindwa kuelewa, kwanini polisi wasimlazimishe huyo mlinzi akamkataja huyo bosi wake,...huoni hapo kuna jambo,..., huyo bosi wake ni nani? nikauliza

Inavyoonekana huyo bosi wake ni mtu ambaye hatakiwi kujulikana, huenda ni  kiusalama, nahii inadhihirisha kuwa, kifo cha mtoza ushuru, kinaweza kuwa mchezo wa kuigiza, na haya yanayoendelea sasa ni kupoteza muda tu, kuna wakubwa wa ndani ya idara ya usalama wanaweza wakawa wanalifahamu hilo .....lakini hayo mimi nitayagundua tu...akasema mpelelezi

Lakini wewe ni mmojawapo, wewe ni mtu wa uslama au sio, kwanini usilijue hilo? nikamuuliza

Mambo mengine ni ya kiujasusi zaidi, yanaweza kufanyika kwa siri kubwa, na wanaoweza kufahamu wakawa watu wachache na wanaoaminika...hayo ni mambo ya 

kintelejensia...huwezi kuyafahamu...akasema

Sasa kwanini kupoteza muda, gharama, na hamuoni kuwa mnaua watu bila kuhukumiwa, na hiyo sio haki..nikasema

Hakuna aliyesema huyo mtu kauliwa na watu wa usalama,...na watu wa usalama hawawezi kulifanya jambo hilo kihivyo...wana namna zao nyingi za kummaliza mtu kama wanamuona ni tishia, kwa hilo, lilivyofanyika, sio sahihi, limefanyia kisivyo, nahisi sio kusudio la watu wa usalama kama ni wao, kuna watu wamelifanya ionekane hivyo,nahisi kuna jambo jingine nyuma ya pazia....akasema

Wewe unaweza kuhisi ni jambo gani hilo nyuma ya pazia...? nikamuuliza

Kuna vitu vichache navihitaji kuvifahamu, nikiongea na mlinzi nitavijua, na pili nyie wawili mkiniambia ukweli uliobakia, nitaweza kufikia tamati ya uchunguzi wangu, ila mpaka sasa nimegundua jambo, kuwa mauaji haya yamepangwa yatoee kwa mdada, kwa vile kulishaonekama kuwa kuna kutokuaminiana kati ya mdada na mtoza ushuru, na wewe wakakutumia kama chambo....akasema

Mimi hapo sielewi unajua mpaka sasa nawaza hilo ulilosema kuwa mdada,akianza kuondokewa na hiyo hali, anapoteza nguvu, na mimi nakumbuka kabisa alishaanza kuyumba yumba, kwahiyo hakuwa na uwezo wa kufanya lolote, unaona hapo sasa ni lazima awe ni huyo mlinzi aliyefanya hayo mauaji ni kweli kabisa hapo, ...nikasema na mpelelezi akasema;

Huyu mlinzi aliingia kwa kupitia dirishani, na ndiye aliyevunja kabati la mdada, akitafuta nyaraka muhimu, ni nyaraka gani hizi,....na kipindi hicho wewe na wenzako mpo katika harakati za mapambano,...huyu mlinzi aliwezaje, kufanya hiyo kazi ya kuvunja hilo kabati, na bado awe na muda wa kutoka na kuwagonga na nyundo, na hata kumua mtoza ushuru....ukipiga mahesabu ya muda hapo, hautoshi, naona kuna msaada wa mtu mwingine hapo...akasema

Mhh, atakuwa alipitia wapi, ukumbuke mimi nilikuwepo, na nikatoka nje, kukimbia, na wakati natoka huku nyuma ndio nikasikia mlio wa risasi, huyu mtu atakuwa kapitia wapi,...nikasema

Nilichunguza mlalo wa marehemu, kama hakuhangaika wakati anakata roho, basi, mpigaji wa hiyo bastola, atakuwa upande wa...mmmh, yes, sasa nimegundua jambo, ..akasema mpelelezi akiinua ngumi ya kuashiria ushindi

Umegundua nini mpelelezi...? nikamuuliza na mimi nikiwa na hamasa

Nitakuambia nilikithibitisha hilo, ...ngoja niwahi sehemu, wewe tangulia kwa mzee, nitawakuta huko, ni lazima kazi hii niifanye leo hii, hii maana kesho ndio mwisho wake, faili lake linafungwa,...akasema na mimi nikataka kumuuliza lakini yeye akaendelea kuongea

Lakini kuna kitu muhimu, nataka uniambie ukweli, maana nina mashaka nacho bado, kuhusu wewe kujivika ndevu, nina uhakika ni wewe ulifanya hivyo , ni kwanini mlifanya hivyo....akasema akitaka kuondoka,

Lakini mimi sijafanya hivyo, na ukisema una uhakika una maana gani? nikamuuliza, na mara akatoa mfuko wa plastiki na ndani mkoba wake na unionyesha ndani ya kile kifuko cha plastiki kulikuwa na ndevu za babdia...akanionyesha na kusema;

Ushahidi huu hapa....akasema na kabla sijasema kitu,akaondoka kwa haraka

NB: Mpelelezi kagundua nini, mzee anawahitaji hawa watu kwa jambo gani

WAZO LA LEO:Tunaposikia maneno, tetesi, uvumi, au kupewa taarifa kutoka kwa mtu mwingine, tusikimbilie kuziamini kwanza, ni vyema tukajenga tabia ya kuzihakiki hizo taarifa, au tetesi hizo,  kabla ya kuchukua maamuzi yoyote yale.


Dunia sasa hivi imegubikwa na propaganda, na propaganda nyingine zina malengo mabaya ya kuchonganisha na kuleta uhasama katika jamii kwa masilahi binafsi, watu hao wanaochchea hizo propaganda potofu,hawajali maisha ya watu, hawajli athari za hizo propaganda, ilimradi wao wananeemeka. Tuwe makini .

Ni mimi: emu-three

No comments :