Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, May 21, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-62


 Mimi kwa muda ule nikageuka kuangalia pembeni, niliona watu wamesimama hatua chache kutoka pale nilipokuwa, hawa watu hawakuwepo kabla, na uvaaji wao ni kama alivyokuwa kavaa mpelelezi, suti nyeusi na mawani meusi, ...

Mdada aliponiona nimegauka kuangalia na usoni mwangu kuonyesha mshangao, naye akageuka kuangalia huko nilipokuwa nimeangalia, akageuak kushoto na kulia, ...na hapo hapo akauliza;

 ‘Mpelelezi hebu niambie hawa watu wamefuata nini hapa, kwanini umekuja na hao watu, ina maana mimi unanishuku kama mhalifu au...?’ akauliza mdada.

Sikiliza mdada, hao watu wanafanya majukumu yao, usiwe na wasiwasi nao, mimi siwezi kuwaingilia kwenye kazi zao,...’akasema mpelelezi

Kwa hilo mimi sikuelewi, ...akasema mdada akisimama kutaka kuondoka na wakati anataka kufanya hivyo , simu yake ikaingia ujumbe wa maneno, akaitizama na ilionekana alikuwa akisoma huo ujumbe...alipomaliza akageuza kichwa kuwaangalia tena wale watu...

Mdada akasogeza kiti nyuma na kuonyesha kuwa anaondoka, na mpelelezi alipoona hivyo, akawaangalia wale watu waliokuwa wamesimama tu, wakiwa hawaonyeshi dalili zozote za ubaya, ni kama vile wanamsubiri mtu, niliwahesabu, ni karibu watu watano upande wa kushoto, na watu sita upande wa kulia...

Mdada alikuwa keshaanza kutembea kutoka eneo hilo la meza, na mpelelezi akasimama kumkabili mdada, akawa yupe mbele ya mdada, na niliona kama anaonyesha ishara fulani kwa wale watu, nikawaona wakisogea  karibu, na mdada aliona ile hali, akasimama;

Mimi pale nilipokuwa nimekaa , nikawa nimeshika kichwa huku nimainama chini, nikiogopa kuangalia , nilijua sasa mambo yameharibika,.....

Tuendelee na kisa chetu......

Sasa mdada unataka kwenda wapi hatujamalizana...akasema mpelelezi akiwa kasimama sambamba na mdada, na mdada akamuangalia wa macho ya dharau, na kusema;

Kwahiyo unataka kunizuia nisiondoke, ....? akauliza mdada

Hapana sitaki kufanya hivyo, na hayo sio makubaliano yetu, ila nakuomba urudi mezani ili tuweze kuongea , ni vyema mdada, ukatulia ili watu wasijue ni kitu gani kinachoendelea, siunafahamu waandishi wa habari, ndio maana hawa watu wapo hapa kuhakikisha kuwa hakuna anayetusogelea...akasema mpelelezi.

Makubaliano yetu kwanza umeyavunja, tuliahidiana kuwa tuongee sisi wawili, hukufanya hivyo, pili hili la kuzungukwa na watu kama mhalifu mimi sikulipendelea...akasema mdada.

Mengine yamefanywa na wakubwa kwa mtizamo wao, na mimi sikupenda kuwaingilia,..sikiliza mdada, hebu rudi tuongee sitachukua muda wako mrefu, nakuahidi hilo...akasema mpelelezi, na mdada akamuangalia huyo mpelelezi kwa macho yaliyojaa chuki na kusema;

Mpelelezi, ukihitaji kuongea na mimi uwe na hekima, sio wote wanaopenda kuongea ongea ovyo hadharani, hii hali ya kuulizwa maswali huku watu wanakuangalia hainipendezi kabisa, na maswali ambayo unaiuliza yanagusa maisha yangu binafsi, hii sio haki, huu sio utaratibu, haya sio makubaliano yetu,...kwahiyo wewe umevunja mkataba, na kwa hayo tuliyoyaongea yanatosha...akasema mdada akianza kuondoka na mpelelezi akamzuia kwa mkono na kusema;

Mdada haya mazungumzo ni muhimu sana, na yana kibali, sio kwamba naongea na wewe kujifurahisha tu, kwahiyo nakuomba urudi kwenye kitu,utulie, tuongee...akasema mpelelezi kwa sauti nziti kidogo,na mdada akageuza kichwa kuwaangalia wale jamaa akatabasamu na kusema;

Hivi mpelelezi unafanya hivyo kwa kujiamini, kuwa hao jamaa zako wanaweza kunifanya nifanye mnavyotaka nyie, au kazi yao ni nini? akauliza mdada akigeuza mcho huku na kule, na mimi pale nilipokaa nikaanza kuingiwa na mashaka, nikawa najiuliza nifanye nini ili kuokoa ile hali.

Nimekuambia hao wanakazi zao, usiwajali..na umbali huo waliposimama hawasiki kabisa tunachoongea, kama unavyoona sehemu hii mkiongea hakuna mtu anayesikia sauti zetu,....akasema mpelelezi

Kwa mfano nikiamua kuondoka, unafikiri hao watu wako watanifanya nini, au wewe utachukua hatua gani, au unajiamini kuwa utaweza kunizuia, au unataka tujaribu hilo...akasema mdada, na niliona kama mikono yake inaanza kucheza cheza

Sikiliza mdada, mimi sipo huko kwenye shari na vurumai, sipendelei kabisa hizo taratibu za ubabe,..mimi ninachokuomba, ni wewe na mimi tujaribu kusaidiana kwa hili, tufikie sehemu tuwe na maridhiano ya pamoja, nakuomba tafadhali, rudi kwenye kiti tuendelee na mazungumzo yetu, kwanini unafanya mambo yawe magumu? akauliza mpelelezi na mdada akaangalia saa yake, halafu akaniangalia na kusema

Mhasibu unasemaje, unaweza kuendelea na hawa watu, wewe ongea na huyu mtu wako, kwani yote yaliyotokea mle ndani unayafahamu zaidi yangu, muda wangu wa kuongea na huyu mtu umekwisha, sasa hivi nina miadi na watu wengine...akasema mdada, na mimi nikaona hapo hapo naweza kusaidia jambo, nikasema;

Mdada tafadhali, mimi naona tumalizane na huyu mtu,  ili tuondoe hiyo sintofahamu, unajua mdada, ukiondoka sasa hivi itaonekana kama unaogopa, na labda kuna ukweli unauficha kitu ambacho sio sahihi, tukabaliane na hili kihekima na kiujasiri...nikasema na mdada akageuka kumuangalia mpelelezi, halafu akageuka kuniangalia, kwa macho makali, halafu akarudi kinyume nyume hadi kwenye kiti chake akakaa na kusubiria.Na mpelelezi naye akarudi kwenye kiti chake, na hakupoteza muda akasema;

Hebu turejee siku ile ya tukio...akasema mpelelezi

Mhh, unataka kujua nini zaidi ya hapo, nimekuambia siku ile ya tukio, mimi nilikuwa nimepoteza fahamu nilikuwa mtu mwingine kabisa, inapotokea hiyo hali mara nyingi huwezi kujitambua,  sikujua kilichotokea, sasa unataka nikuambie nini tena hapo...?

Nataka kujua yale uliyoyaona kabla ya tukio na baada ya tukio,pale ulipozindukana na yaliyoendelea kutoka hapo...pili ili niweke mambo yangu sawa, nataka kujua mahusiano yako na marehemu ambayo yalimfanya afike hapo kwako, na tatu ni kwanini alifikia hatua ya kuchukua bastola, ...hapo kuna jambo hutaki kuliweka wazi, ...akasema

Kuna jambo gani unalihisi, hebu weka wazi wewe unahisi kuna jambo gani...okey, ili twende sambamba, hebu niulize maswali yako moja moja, nitakujibu kama utakavyo wewe....akasema mdada akitulia vyema kwenye kiti

Kwanza hebu turejee kabla ya tukio, kuna utata ambao hadi sasa haujafahamika..akasema

Utata gani? akauliza mdada.

Kumuhusu huyo mtu aliyekuwa na ndevu, ina maana alikuwa humo ndani kwako,je huyo mtu ni nani...? akauliza

Simjui...akasema mdada.

Kama humjui,...ina maana basi kuna kitu mlicheza nyie wawili na mimi nahisi ndivyo ilivyokuwa nyie wawili mlicheza mchezo fulani wa hadaa..? akauliza mpelelezi

Mchezo gani huo? akauliza mdada

Mliigiza sura bandia....mhasibu alivaa ndevu, tumefanya utafiti huo, tukagundua kuwa mhasibu wewe ulivaa ndevu za bandia ...akasema mpelelezi akiniangalia mimi na mimi nikabakia kimiya.

Mbona nimeshakujibu hilo swali,...mimi huyo mtu simfahamu, na ilivyo huyo mtu hayupo, huenda mlinzi kamzua huyo mtu kwa masilahi yake binafsi, na ama kama unavyodai kuwa tulicheza huo mchezo, nikuulize ili iweje, na kwanini tufanye hivyo,mbona haiingii akilini...akasema mdada

Mimi namfahamu sana huyo mlinzi, kuna mengine kadanganya,...na nilipombana kakiri hivyo, lakini hilo la kuonana na mtu wa namna asema ni kweli alionana na mtu aliyekuwa na ndevu,...na jinsi alivyoongea hilo ni kweli, ni kweli kuwa alionana na mtu wa namna hiyo, .....akasema akiniangalia mimi, halafu akamuangalia mdada.

Ndugu zanguni, hapo kuna kitu mnakificha, sijui kwanini mnafanya hivyo, hebu semeni ukweli tulimalize hili....akasema mpelelezi

Hiyo ni shauri yako, kama unataka kujiwekea hisia zisizokuwepo ili uweze kufikia lengo lako wewe endelea tu, ila kauli yangu mimi, huyo mtu hayupo, na kama unahisi ni mhasibu ndiye aliywkuwa kavaa ndevu, huyo hapo mbane aseme ukweli, mimi siiingilii....akasema mdada kwa kujiamini

Hebu tuangalia pale tukio limeshafanyika,..kwanza  hebu niambie kuhusu nyumba yako, huwa una tabia ya kukagua madirisha yako kabla hujalala....swali hili lilimfanya mdada ashituke kidogo halafu akasema;

Kwanini unaniuliza hivyo, ..ndio huwa nafanya hivyo ni muhimu sana....mara nyingi nafanya hivyo, kwani vipi?akasema na kuuliza

Je baada ya hilo tukio uliweza kukagua madirisha yako, ya chumbani, ukaona yapo sawa sawa, ndivyo yalivyokuwa ...? akauliza na mdada akatulia akimuangalia mpelelezi kwa muda, halafu akauliza;

Hebu niambie ukweli hayo uliyapatia wapi, uliongea na mlinzi akakusimulia au umejuaje kuhusu maswala ya madirisha ya nyumba yangu...? akauliza mdada

Kujua kuhusu nini, mimi nimekuuliza hayo maswali nikiwa na maana yangu, nataka unijibu tu? akasema mpelelezi na mdada kwanza akatulia, na bila kuniangalia mimi akasema;

Ni kweli kuna dirisha langu nilikuja kuligundua kuwa lina matatizo, siwezi kuwa na uhakika wa moja kwa moja kuwa lilivunjwa, hilo siwezi kudanganya, lakini tangia kabla dirisha hilo lilikuwa na matatizo ya kufungika vyema...akasema na mpelelezi akasema;

Unaona mlivyo, mnaficha ukweli muhimu sana, mpaka watu tuhangaike ndio mseme ukweli, mdada mimi ni mpelelezi, na nafahamu sana kazi yangu, haya ninayokuuliza mengi nameshayafanyia uchungzi wa kina, nafahamu majibu yake, lakini wakati mwingine nakuuliza ili kukupima ukweli wako...akasema

Kama unafanya hivyo kwangu unakosea sana...mimi sio kama hao watu wa kawaida, pale ninapokujibu ,nakujibu kwa maana fulani, najua ni kitu gani ninachokifanya, na ninaposita kukuambia ukweli fulani ujue nafanya hivyo kwa mainajili fulani...akasema

Kwahiyo...mpelelezi akataka kuongea na mdada akamkataiza na kusema;

Wakati mwingine siwezi kuusema ukweli ulivyo, huenda sijawa na uhakika na huo ukweli, bado naufanyia uchunguzi, nikiwa na uhakika  nao, siwezi kukuficha,...ndio tabia yangu na ndivyo nifanyavyo mambo yangu, huwezi kunilazimisha niseme kila kitu, wakati nafahamu binadamu tulivyo, tukisema jambo, litachukuliwa kama lilivyo, kumbe ulisema tu , ya kubali yaishe,...siwezi kufanya hivyo,...akasema na mpelelezi akamuangalia kwa makini, halafu akauliza swali

Kuna kitu chochote kiliharibiwa, au kupotea ndani ya chumba chako, baada ya hilo tukio? swali hilo likamfanya mdada ageuka kumuangalia mhasibu, nahisi moyoni mwake, alihisi huenda mhasibu kamsimulia huyo mtu hayo anayoyauliza, na baadaye akamuangalia mpelelezi na kusema.

Hebu kwanza mpelelezi,....kuna kitu sikielewi, hayo unayoyauliza umeyapatia wapi, ulishaongea na mhasibu akakusimulia au, ....? akauliza mdada

Haya ninayokuuliza mhasibu hayafahamu, sijaongea na mhasibu kuhusu hayo ...nisingelimuuliza yeye kuhusu maswala ya chumba chako,nakuuliza wewe uniambie huo ukweli,kwani hicho ni chumba chako na mhasibu hakifahamu, au ? ....ni muhimu sana mdada kunijibu hilo swali...akasema mpelelezi.

Kwahiyo wewe unataka kujua nini hapo? akauliza mdada bado akionyesha mshangao, nahisi alishanizania mimi vibaya kuwa huenda nimeongea hayo na huyo mpelelezi

Je baada ya hilo tukio wewe ulipochunguza chumba chako, uligundua mabadiliko yoyote, kuna kitu kilipotea, kuna kitu kilivunjwa, kuharibiwa na vitu kama hivyo,...? akaulizwa na mdada akatabasamu kama kebehi halafu akasema;

Ni kweli nilipotulia na kukagua vyema chumba changu niligundua kuwa moja ya kabati langu lilivunjwa,...lakini sikuona cha muhimu kilichopotea kwahiyo mimi sikufuatilia sana...akasema mdada akiwa kaangalia mbele hakuwa amemuangalia mpelelezi moja kwa moja usoni.

Kwa maelezo hayo, mimi ninafikia hitimisho kwa kukubali kuwa kuna mtu alivunja dirisha, akaingia kwa kupitisha dirishani, na huyo mtu ndiye aliyevunja kabati lako..nafikiri hapo unakubaliana na mimi...akasema

Inaweza ikawa hivyo,...akasema mdada.

Invyoonekana ndivyo hivyo kuwa huyo aliyeingia kwa kupitia dirishani ndiye huyo aliyefanya hivyo, ...ndiye aliyevunja kabati lako, na kama ulivyosema wewe ni mtu unayejijua, unafanya uchunguzi wa mambo yao, basi ni lazima kuwa ulifanya uchunguzi wa hilo, je wewe ulipofanya huo uchunguzi wako hukuligundua hilo, kwani ni muhimu sana, sijui kwanini hukuwaambia polisi? akauliza mpelelezi

Kama nilivyokuambia, hilo kwangu halikuwa na umuhimu sana, nahisi huyo kibaka alijua hapo naficha pesa, ...na alivunja akakuta hakuna kitu, hata hivyo mimi kama mimi sikuona umuhimu wa kuwahusisha polisi, kwani jambo ukilipeleka kwa hawa watu, sio jambo dogo tena,...akasema mdada

Huoni kuwa huyo mtu aliyeingia kwa kupitia dirishani anaweza kuwa ndiye aliyetoka na kuwagonga nyie kwa nyundo, mkapoteza fahamu, huoni kuwa huyo huyo anaweza kuhusika na mauaji ya mtoza ushuru...mdada hilo ni kosa kubwa sana ulilolifanya, hebu liangalie kwa makini kama wewe ni mpekezi yakinifu...akasema mpelelezi.

Mimi ninajua ni nini ninachokifanya, kama itabidi kulisema hilo kwa hao polis wako nitalisema wakati ukifika, kwa wakati huu naona halina maana kabisa kwangu, kama wewe unaona lina maana sana kwako basi, lifanyie kazi, sinimeshakuambia unaweza kuchukua hatua unazoona ni sahihi...akasema mdada

Mdada kwani wewe unamfanyia nani hiyo kazi? akauliza mpelelezi

Hahaha,mpelelezi, umeshamaliza maswali  yako, niondoke? akauliza mdada huku akitabasamu

Wewe unamiliki bastola? akaulizwa mdada na mdada akageuka kumuangalia mpelelezi kwa mashaka huu akitabasamu na kusema;

Ndio namiliki bastola, nina kibali nayo, unasemaje kuhusu hilo? akauliza mdada

Bastola yako siku ya tukio ilikuwa wapi? akaulizwa

Bastola naiweka sehemu nzuri tu, sipendi kukuambia hiyo ni siri yangu, ...akasema mdada

Ni muhimu kulijua hilo,kwani kama huyo mtu aliingia, akavunja akbati, pia anaweza kuichukua hiyo bastola na kufanya lolote, nipatie namba yake...na kuna watu watakuja kuikagua hiyo silaha yako ni muhimu sana ...akasema mpelelezi

Kwani hiyo silaha yangu inahusiana vipi na hili tukio,...marehemu kauwawa na bastola iliyokuja nayo yeye mwenyewe, kwa ushahidi wao wenyewe polisi...ina maana huwaamini hata watu wenu, au wewe unataka kusema nini?akauliza mdada akionyesha mashaka.

Ni muhimu kila kitu kiangaliwe kwa makini, kwani hata hao polisi ni binadamu, makosa ya hapa na pale yanaweza kutokea,ni kwa kumbukumbu tu, naomba ushirikiane na hao watu watakaokuja kwako....akasema huku akiangalia saa, halafu akauliza

Mlinzi wako umemchukua kwenye kampuni gani? akauliza mpelelezi, na mdada alionekana kuzidiwa, hakutarajia maswali kama hayo kutoka kwa huyo mtu, na akawa kama anawaza jambo, halafu akasema;

Sijamchukua kwenye kampuni zilizosajiliwa, nimemchukua kutoka kwa mdhamini anayemfahamu, huwa mara nyingi anajitegemea yeye mwenyewe, kama nijuavyo mimi...akasema

Mdhamini wake kwako ni nani? akauliza mpelelezi na mdada akabakia kimiya kwa muda bila kujibu hilo swali, na mpelelezi akarudia hilo swali

Umesema aliajiriwa kwako kwa mdhamana wa mtu anayemfahamu, ningelipenda kumfahamu huyo mtu, au hatakiwi kujulikana? akauliza mpelelezi, na mara simu yake ikaita kuashiria ujumbe wa maneno, akaangalia na kuusoma huo ujumbe, halafu akainua mkono juu, kama ishara fulani, na niliona wale jamaaa waliokuwepo pale wakaanza kuondoka.

Maana yake ni nini? akauliza mdada akiangalia ile hali

Ni majukumu tu ya kikazi,....akasema mpelelezi huku akisimama kama anataka kuondoka halafu akasema;

Kwa leo inatisha, lakini bado hatujamalizana, nahitajika makaoni, kuna dharura kidogo, ...mzee hali yake sio nzuri, na zaidi ya hayo ananihitaji nikaonane naye, ...akasema

Mzee yupi, baba yako, au? akauliza mdada akimuangalia mpelelezi kwa makini

Hapana sio baba yangu...akasema mpelelezi na kabla hajafafanua, mimi nikauliza

Ni baba mkwe wangu au? nikauliza

Ndio ni baba mkwe wako...hata wewe anakuhitajia pia...akasema

Oh, kwahiyo, ...itabidi niondoke nikamuona..nikasema

Kwa mujibu wa taarifa hiyo mzee anawahitaji watu watatu, mimi na wewe, na sijui huyo mtu wa watatu ni nani....akasema

Na mimi nikageuka kumuangalia mdada, na mdada alionekana kuzama kwenye mawazo, akainua uso kuniangalia, hakusema neno na mpelelezi akasema

Na mdada inavyoonekana ni lazima wewe usimamishwe kutoa ushahidi, dakitari wako kasema kwa hivi sasa huna tatizo unaweza kufanya hivyo,nafikiri upo tayari kwa hilo.. akasema kama anauliza na mdada akaangalia simu yake iliyoingia ujumbe wa maneno, ...akausoma huo ujumbe halafu akasema;

Huyu mzee anataka nionane naye kwa haraka, mmh, hata hivyo nilishapanga nionane naye, naona imejipa kuna zaidi wakubwa mimi naondoka, mhasibu, nitakuja hotelini kwako nina mazungumzo na wewe, uniambie ukweli......akasema huku akiwa ananiangalia kwa macho makali....

NB: Kuna jambo nzito anataka kulisema mzee, ni jambo gani hilo, na je mdada atasimamishwa kutoa ushahidi, ni nini kitatokea , tuwemo kwenye sehemu ijayo kwa majibu hayo na mengine mengi.

WAZO LA LEO: Maisha yalivyo ni kama safari ambayo unajua wapi ulipotoka, lakini huna uhakika na wapi unapokwenda,na lini utafika huko unapotakiwa kwenda. Cha muhimu ni kuwa na maandalizi mema ya safari yetu hiyo, kila tufanyapo kiwe na malengo mawili , kwa ajili ya maisha yetu ya hapa duniani na pia kwa akiba ya maisha ya huko tunapotarajia kufika, na muhimu ni matendo  mema, haki na ukweli.  

Ni mimi: emu-three

No comments :