Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, May 20, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA -61


‘Ni bora nimewakuta wote wawili, nitaongea na nyote wawili, kama hautajali mdada...

Hiyo likuwa sauti ya mpelelezi, sauti ambayo ilinifanya mwili wangu uanze kutetemeka ndani kwa ndani nikiogopa kutokea na vurumai, kwanza nilimuangalia mdada, kuona atakachofanya, mdada alikuwa kakaa vile vile akiwa anaangalia, au kumuangalia huyo mpelelezi.

Na mpelelezi akarudia kauli yake ile, kwa msisitizo, akasema;

Leo ni bahati kubwa sana, kuwakuta wote wawili, ni bora tuongee yote , mkiwa wote wawili, au unasemaje mdada...? akauliza na mimi hapo nikageuza kichwa kumuangalia mpelelezi,

Alikuwa kavaa mawani meusi, na kwa muda ule alikuwa kasimama karibu kabisa na kiti changu, huku akimuangalia mdada, na mdada alitulia kidogo , halafu akasema;

 ‘Unataka tuongelee hapa hapa, haiwezekani,.....akasema

Kwanini haiwezekani mdada,hakuna kitu cha siri, kati yenu wawili, nyote mnajuana, na hapa mezani hakuna atayetusikia, hii meza mliyochagua ipo sehemu nzuri, mnaonaje wapendwa? akauliza

Sawa uonavyo wewe, ila natoa tahadhari, maswali yako yawe ya moja kwa moja sio ya kuzungukazunguka, na uwe makini na kauli zako, tusije tukabadili hali ya hewa hapa...’akasema mdada

‘Usiwe na wasiwasi mdada, hiyo ndiyo kazi yangu, sizani kama tutafikia huko, na sijui kwanini unasema kuwa hali ya hewa itabadilika kwa vipi mpendwa...? akauliza

Unanielewa nina maana gani usitake kupoteza muda, kwanza niambie ni kwanini unanihoji mimi kwa kosa gani? akauliza mdada.

Mdada usiwe na wasiwasi kabisa, mimi kama kazi yangu ilivyo nina haki ya kumhoji mtu yoyote kwa nina njema tu, na sio kumshika mtu ubaya,... hata hivyo nikuambie ukweli mdada, nimekuwa nikijaribu kukutafuta ili tuongee, na kila mara nikikuarifu tufanye hivyo, unasema huna nafasi, inaonekana kama vile unanikwepa...akasema

Kwanini nikukwepe? akauliza mdada kwa mshangao.

Hata mimi sijui, ndivyo nionavyo mimi, lakini kama nimekosea haina shida, ilimradi leo ipo nafasi basi tuongee, na tuondoe hizo sintofahamu zinazojitokea, ili na mimi nitimize wajibu wangu, kama ilivyo nyie, au sio? akauliza mpelelezi.

Naona wewe unapoteza muda, kaa kwenye kiti uanze kuuliza hayo mswali yakounayotaka kuuliza, mimi siogopi chochote, maana nafahamu ni nini ninachokifanya...akasema mdada, na mimi nikainuka ni kukaa kiti kilichokuwa karibu na mdada, na mpelelezi akasogea kwenye kiti nilichokuwa nimekaa mimi mwanzoni, kwahiyo yeye akawa anatuangalia wawili moja kwa moja

Alipokaa vyema akayavua mawani yake na kukaa vyema kwenye kile kiti , halafu, akamuangalia mdada, na kusema;

Leo ni siku ya pekee sana, kukutana nawe hivi, na nahisi ni mwanzo mzuri, na sioni kwanini tuwe tunakwepana...akasema mpelelezi

‘Mimi siwezi kukuwepa wewe, hivi unanionaje mimi, na kwanini nikukwepe, labda wewe unajihami tu....ongea kilichokuleta hapa, maana muda unakwenda mbio, nina mambo mengi ya kufanya...’mdada akasema

‘Sawa tuanze na mimi nitafurahi sana, kama maongezi yetu yatakuwa ya kirafiki zaidi, kwani ninachokitafuta mimi , ni kwa ajili ya usalama wa jamii, jamii imetupa dhamana, ya kuona usalama wao upo,...na kila mmoja ni lazima afahamu kuwa hilo ni jukumu lake...akasema

Hilo lipo wazi...akasema mdada

Pale kunapotokea uvunjwaji wa sheria, watu wa usalama wanapewa jukumu hilo, kuangalia chanzo chake,na mimi ni mmojawapo,....akatulia na kuniangalia mimi kwanza, halafu akageuka kumuangalia mdada.

Sasa ili tuweze kutimiza majukumu yetu, ni muhimu sana kukawa na mshirikiano, kati ya raia wema na watendaji waliokabidhiwa hiyo dhamana, inakuwa vigumu sana kutamba uweli wa tukio kama watu wa usalama hawatapata mashirikiani na raia wema, na ukweli ndio unaotafutwa, na katika mazungumzo yetu ninachoomba kwenu nikuniambia ukweli ulivyokuwa, ...akasema

Hakuna atakayesema uwongo hapa, wewe uliza maswali yako ujibiwe, usianze mambo ya kisiasa hapa hatupo jukwaani, kama unataka ubunge au uongozi na hapa unatafuta kura huu sio muda wake...akasema mdada na mpelelezi akatabasamu na kuuliza;

Mdada, ni kweli uliyoongea, na tusipoteze muda, mimi, nataka mniambie ukweli, wewe na mhasibu ,jinsi ilivyotokea siu ile mlipokuwa ndani pamoja, wakati alipokuja marehemu, hadi kifo chake kutokea, ...nitauliza maswali yangu yakienga hiyo hoja muhimu, ...’akasema mpelelezi

‘Lakini hayo yote umeshaambiwa na, na mhasibu kama sikosei,....eti mhasibu hayo ulishaulizwa natumai ulimuelezea ilivyokuwa, maana mimi siku ile, asilimia kubwa sijui kilichotokea...’akasema mdada akiniangalia mimi,na mimi nikawa kimiya, na mpelelezi akasema;

‘Nilimuuliza akiwa peke yake, lakini inaonekana kuna mambo alichelea kunielezea , nahisi ni kwasababu hana uhakika nayo au anachelea kuongea mambo wakai wewe hupo, ni kama ukulinda wewe, sasa ni heri tuliongelee hili tukiwa wawili ili kila mmoja awe amerizika na isonekane kama kuna kusalitiana...akasema

Hayo ni mawazo yako...akasema mdada akiniangalia mimi, na mimi nikaendelea kuwa kimiya.

Jamani hebu tulimalize hili, ili haki itendeke, yametokea mauji, na hadi sasa ukweli halisi haujabainika, japokuwa mlinzi ameshikwa kama mshukiwa, lakini undani wa hili jambo haujawekwa wazi, na ni vyema likabainika, ili kuondoa hii sitofahamu inayoendelea....’akasema mpelelezi.

‘Unapsema tulimalize hili, kwani mimi au mhasibu tunazuia nini, hebu kuwa muwazi wewe unakitaka nini kwangu, kama ni muuaji keshapatikana, kuna nini zaidi unakitafuta kwangu, au umenishuku nini, hasa mimi...?’ akauliza mdada.

‘Kazi yangu ni kutafuta tatizo lenye utata dhidi ya uvunjaji wa sheria...na nikiwa nafanya hilo,siangalii mtu, naangalia ukweli, natafuta ukweli, lakini kwa kupitia wa nani, ni lazima nipitia kwa watu ambao ndio watendaji...akasema

Kwa msemo huo inaonyesha kuwa nyie mnanishuku kuwa nimevunja sheria au? akauliza mdada, na mpelelezi hakujali hilo swali lake akaendelea kuongea.

Ni lazima nipitia kwa watu, kwani wao ndio wahusika, na wanajue mengi, nikishirikiana nao, tatizo linakuwa rahisi utatuliwa, kwahiyo sina jinsi ni lazima niwahoji watu, ni lazima niangalie nyendo za watu, na vitendea kazi vyao na mazingira ya tendo lenyewe,...'akasema

'Na unaposema watu ni yoyote yule, sio lazima awe ametenda hilo kosa, anaweza akaona, anaweza akatoa mawazo ya kusaidia, hivi hapo mimi nimefanya kosa kukuhoji mdada...’akauliza

‘Mhh, mpelelezi, usinifundishe kitu ninachokifahamu, mimi sio mgeni wa hilo, ila ninakuhakikishia kuwa kunihoji mimi, uaumiza ichwa chako, uapoteza muda wako hutafaidika na lolote lile, kama nina kitu muhimu ambacho kinaweza kukusaidia, nisingelisita kukuona...akasema mdada.

Nashukuru kusikia hivyo, basi ili kuokoa muda, labda niwaulize yale ninayohisi kuwa nyie wawili mnaweza kunisaidia, ...akasema.

Nimeshakupa nafasi hiyo tayari, wewe uliza, na sioni kwanini unapoteza muda, na nakuthibitishia kuwa kwangu huwezi kupata kitu kabisa,unapoteza muda wako bure, labda unataka nikusaidie kazi yako tu,..akasema.

Kwanini unasema hivyo mdada, ..? akauliza mpelelezi.

Nikuambie ukweli, jinsi ilivyo, kila mmoja anaangalia wajibu wake, siwezi kukuingilia kwa hilo maana hapo unatafuta unga wako na familia yako au sio..hata hivyo ni vyema nikuhakikishie kuwa mimi sivyo kama unavyonifikiria, ipo siku utalijua hilo, lakini anyway mimi nipo kwa ajili yako mkuu’ akasema na mpelelezi akatabasamu na kuniangalia mimi, halafu akageuka kumuangalia mdada.

‘Sio mbaya nikianzia mbali kidogo, nikiwahoji mambo yenu binafsi, kama mpo huru kujibu ,siwalazimishi kwa hilo, kama mtaona linaingilia mipaka yenu, munaweza kusema hilo hamuwezi kujibu kwasababu kadhaa, au sio, lakini mimi litanisaidia katika kuweka kumbukumbu zangu sawa...’akasema mpelelezi

‘Wewe uliza maswali yako huna haja ya kujihami, mimi nilishafahamu unachotafuta wewe,kupekenyua maisha ya watu,jamani hebu kuweni serious na kazi zenu, maisha ya watu binafasi yatawasaidia nini, haya uliza unalotaka kuuliza...’akasema mdada na mpelelezi akamwangalia kwa muda halafu akauliza

‘Mdada pamoja na kuwa mhasibu ni mfanyakazi mwenzako je mna mahusiano mengine zaidi,...?’ akauliza mpelelezi huku akitabasamu.

‘Mahusiano mengine kama yapi, hebu kuwa muwazi,,,maana ndio kazi yako hiyo, nilijua tu, kuchunguza maisha ya watu,  hebu fafanua hilo swali lako..’akasema mdada naye kitabasamu.

‘Je mna mahusiano ya kimapenzi?’ akauliza na mdada akasema

‘Tupo katika utaratibu huo, lakini hatujafikia hatua ya kujitambulisha kama wapenzi, hayo ni mambo binafsi na yanakwenda hatua kwa hatua, kama tutafiki hatua ya kujitambulisha kwanini tujifiche, hilo ni jambo la kawaida tu, nafikiri umepata jibu muafaka...’akasema mdada akimuangalia mpelelezi moja kwa moja usoni.

‘Nijuavyo mimi mhasibu ana mchumba wake tayari iweje wewe uwe tena mchumba wake, huoni kwamba unatafuta mtafaruku fulani katika hiyo familia husika?’ akauliza

‘Uchumba sio mkataba wa ndoa, huo ni utangulizi tu, ...mtu anaweza akawa na wachumba hata zaidi ya mmoja,lakini ikifikia maamuzi ya ndoa , ni swala jingine, hilo lipo wazi,...’akasema mdada

‘Kwahiyo kwa namna hiyo, kwa vile ni marafiki na mpo mbioni kujitambulisha kama wachumba ni halali kwa mhasibu kuja kulala kwako au wewe kwenda kulala kwake, mimi naona huo sio utaratibu wa kiafrika au nimekosea?’ akauliza

‘Inawezekana...lakini mimi ni mtu mzima kama alivyo mhasibu, naweza kujua baya na zuri, sioni tatizo hapo,..ila ni kweli kimaadili sio vyema, na kila mmoja anakiri hilo kuwa ni kosa, ama kwa vila unazungumzia hilo kwa vile mhasibu alikuwa kwangu kwa usiku mzima wa siku ile ya tukio ambalo lipo mahakamani,kwanini mhasibu usimueleze kwanini wewe ulikuja kwangu, au ....?’akageuka kuniangalia mimi na mimi nikawa kimiya.

Je mhasibu alishawahi kufika kwako kabla? akaniuliza

Mhh, sikumbuki, ...mara nyingi tunakutana hotelini? akasema

Lakini nyie ni marafiki wakubwa ambao mnatarajia kutambulishana kama wachumba kwahiyo nilitarajia kuwa yeye atakuwa ameweza kuja kwako mara nyingi tu ....au sio?

Mbona unajichanganya, kwanza ulisema kuwa sio vyema kwa taratibu za kiafrika, kwa vile hatujafunga ndoa, ....sisi tuliliona hilo, ndio maana tulikuwa tunajitahidi kutokufika majumbani mwetu...unaonaeeh...akasema mdada

Kwahiyo kufika kwake siku ile ilikuwa kwasababu maalumu, sio kwa mazoea fulani, sio kwasababu ya kuwa ni nyie wawili ni marafiki? akauliza

‘Yeye mwenyewe alishakuelezea ni kwanini alifika kwangu, au unataka mimi nirudia maelezo yake ?’ akauliza

‘Hebu twende moja kwa moja siku ile, pale mkiwa ndani, najua muda huo wewe ulikuwa bado unaumwa, umechanganyikiwa, au sio, je wewe hukuwahi kuamuka mkaongea lolote?’ akauliza

‘Sikumbuki, mwenyewe umeshasema nilikuwa nimechanganyikiwa na hilo umelipata kwa uthibitisho kutoka kwa dakitari, au sio...’akasema mdada kama anauliza

‘Nauliza hivi kwasababu, kama ulichanganyikiwa na ulikuwa unaumwa, ilikuwaje umuarifu mhasibu kuwa atakuja mgeni, na akija yeye achukue mzigo wake, kwahiyo ina maana kuna muda hali ilikuwa nzuri, mlikaa mkaongea su sio?’ akauliza

‘Nakumbuka kitu kama, yah,...hali ile ya kuchanganyikiwa iliondoka muda wa usiku, na karibu na asubuhi, ...sikumbuki saa ngapi, na kichwani nikakumbuka kuwa kuna mgeni anatarajia kuja,...nikamuita mhasibu, na kumuelekeza kuwa kuna mgeni wangu atafika, kwahiyo yeye aongee naye, na kama kaja na mzigo wangu anipokelee...’akasema

Kwahiyo huyo mtu ambaye alitarajiwa kuja na huo mzigo, mlishaongea naye kabla, siku moja kabla, au siku nyingi au mliongea naye muda gani, ...na mkaafikiana kuwa atakuja na huo mzigo? akauliza

Siku moja kabla, niliongea naye akasema atakuja siku hiyo...akasema mdada

‘Tunapozungumzia mtu huyo tuna maana mtoza ushuru, au marehemu au sio, wewe ulimuagiza mhasibu akachukulie mzigo kutoka kwa mtoza ushuru, mzigo huo ulikuwa wa kikazi au binafsi..? akauliza

‘Inajieleza yenyewe hapo, kama ingelikuwa ni wa kikazi tungefanya mambo hayo maofisini au sio, kifupi mzigo huo ulikuwa wa kibinafsi...’akasema

Kwahiyo wewe na mtoza ushuru mlikuwa na biashara au shughuli fulani ya kibinafsi, ambayo iliwafanya muwe pamoja, je mnafahamiana naye kivipi? akauliza

Nilimfahamu kama mtu wa mambo ya ushuru, na nikiwa na kazi muhimu za kiofisi nilikuwa nawasiliana naye..ni kihivyo tu...akasema

Kwahiyo kufahamiana kwenu sana sana ni kikazi zaidi au hata kiurafiki wa kimapenzi? akauliza

Ni kikazi zaidi, lakini kwa vile nimemfahamu kwasababu ya kikazi, hata mimi nikiwa na mambo binafsi, niliweza kutumia mwanya huo, na nikuambie ukweli, mimi siwapendi wanaume kabisa, kwahiyo hiyo hisia yako moyoni kuwa huenda nilikuwa na urafiki naye, ondoa...akasema.

Kwanini uwachukie wanaume, ...! Na pia umesema wewe na mhasibu mna urafiki na mnarataji kwenda mbali zaidi, ...yeye ni mwanaume, au sio? akauliza mpelelezi kitabasamu huku akimuangalia mhasibu.

Mhasibu ni tofauti, na hao ninaowaita wanaume...mimi mwenyewe moyoni nimemuweka kwingine,...siwezi kukuelezea hilo, uliza swali jingine..akasema mdada.

Mdada wewe unamiliki gari, na hilo gari kwa kumbukumbu zetu, limetolewa bandarini kwa usimamizi wa marehemu, na malipo ya kulitoa gari hilo yalidhaminiwa na marehemu, ...akasema mpelelezi na mdada akatabasamu kidogo.

Kuna maandishi kuwa marehemu alichukua dhamana, akalipa kwa niaba, ili baadaye wewe uje kumlipa yeye, je huo mzigo  aliokuja nayo siku hiyo hauhusiani na hilo gari?’ akaulizwa

‘Kama ungelihusiana na hilo gari, mimi ndiye niliyetakiwa kumpelekea huo mzigo, nikiwa na maana pesa, unaona hapo, kwahiyo huo mzigo ni mambo mengine tofauti kabisa na gari, usichanganye hivyo vitu viwili...’akasema mdada kwa kujiamini.

Ina maana wewe ulishalipa deni la marehemu, ? akauliza

Deni gani?akauliza mdada

Deni la kulipa pesa alizolipa yeye binafsi katika kulitoa gari lako, yeye alilipa kwa kwa niaba yako? akauliza

Kama ningelikuwa sijalipa hilo deni, nina imani kuwa hilo lingelitambulikana mapema, hata kabla marehemu hajazikwa, kama sikosei kwenye mazishi yake tuliulizwa ni nani anamdai au kudaiwa na marehemu,...kwa kifupi mimi sidaiani na marehemu...akasema mdada

‘Ni kwanini sasa marehemu alipofika na kumkabidhi mhasibu huo mzigo wako, baadaye akamgeukia na kumtolea bastola mhasibu, ina maana kuna kutokuelewana kati yenu wawili, wewe na marehemu ?’ akauliza.

‘Mimi sikuwa na tatizo na yeye, na wala sijui kwanini alifanya hivyo, huenda alikuwa hamuamini mhasibu, akaona aje hadi ndani, kwa kweli hata mimi sijui ni kwanini alifanya hivyo....akasema.

Kwa maelezo ya mhasibu walipoingia ndani, wewe hukuwepo kitandani, ina maana ulishafahamu kuwa jambo kama hilo litatokea,ukaamua kujificha, ...ni kweli su si kweli? akauliza

Mimi nilitoka kwenda kujisaidia, na sikujua kabisa kwa hilo litafanyia, mimi kwa muda huo nilijua kuwa mzigo wangu utapokelewa na kuletwa kwangu, hilo la huyo marehemu kuja na bastola ilikuwa ni shitukizo kwangu, na nilipoona hivyo, nikaanza kuchanganyikiwa, na sijui kilichofuata baadaye...akasema

Mle ndani mlikuwa wangapi? akauliza

Kwanza walipofika mhasibu na bosi tulikuwa watatu, baadaye akaondoka bosi, kipindi hicho bdo sijawa makini zaidi, nilikuwa naona mambo kindoto ndoto, lakini nakumbuka aliondoka bosi nikabakiwa na mhasibu

Kila muda ulivyokwenda, hali yangu ikaanza kuwa njema, nikawa najielewa, na ikafikia muda nikawa nipo kama kawaida tu...akasema

Na muda huo wote mlikuwa pamoja na mhasibu? akaulizwa

Mhasibu hakuwa chumbani kwangu kwa muda wote huo, na sizani kama alifahamu kuwa mimi nimeshazindukana na hali yangu ilikuwa kama kawaida, alikuja kugundua baadaye pale nilipomuagiza kuwa alikifika huyo mgeni anichukulie mzigo wangu...akasema

Kwanini sasa hukutaka kuuchukua mwenyewe, mpaka ukamuagizia mhasibu? akaulizwa

Sikutaka kuongea na watu wengine nilitaka kupumzika, lakini kwa vile huo mzigo ulitakiwa kuletwa, sikuwa na jinsi, na kwa vile mhasibu yupo, nikaona ni bora nimpe hilo jukumu yeye...akasema

Kwahiyo uliyemuagiza kufanya hivyo ni mhasibu, hakukuwa na mtu mwingine zaidi yenu wawili? akaulizwa

Nijuavyo mimi ndivyo ilivyokuwa, sizani kama kulikuwa na mtu mwingine, na kama alikuwepo mimi sikuwahi kumuona...akasema

Lakini ulisema hali yako ilikuwa kawaida, na uliweza kutambua kila kitu kilichokuwa kikiendelea humo ndani, au sio? akaulizwa

Ndio , hata hivyo bado nilikuwa na uchomvu, na nilitaka kupumzika, na sikutaka kuhangaisha akili yangu sana...na nilijua yupo mhasibu, ...akasema

Huyu mtu aliyekuwa na ndevu ni nani? akaulizwa

Huyo mimi simgahamu, sikuwahi kumuona...akasema mdada

Mlinzi anasema huyo ndiye mtu aliyeongea naye, na sio mhasibu...akasema mpelelezi

Mimi hayo siyajui, kama alikuambia hivyo, huenda alikutana na mtu kama huyo, lakini mimi niliyemuagiza ni mhasibu,...akasema

Si kwamba ulimuagiza mhasibu avae ndevu za bandia ili huyo mgeni akija asimtambue, mdada hebu wekeni hilo wazi? akauliza mpelelezi

Ili iweje, kwanini tufanya hivyo? akauliza mdada

Ina maana mlinzi anadanganya, hakukuwa na mtu kama huyo,na  kwanini adanganye? akaulizwa

Kamuulizeni mwenyewe, atawaambia ni kwanini alifanya hivyo...akasema mdada na kunitupia jicho la haraka na mpelelezi akaandika kitu, na kuniangalia mimi, akasema;

Mhasibu , mlinzi alitaja sifa zinazoendana na wewe , kuwa ulikuwa na ndevu, na alifikia hata kuulizia mhasibu yupo wapi, akaambiwa yupo ndani na mdada, unauhakika sio wewe uliyevalia ndevu za bandia...? akauliza

Nilishakujibu na mdada kathibitisha hilo, sasa sisi wawili tumekupa hilo jibu, wewe bado unaamini maneno ya mlinzi...nikasema na mdada akatabasamu, na mpelelezi akamgeukia mdada na kusema;

 ‘Inavyoonekana nyie wawili yaani wewe na marehemu mtoza ushuru, mlikuwa na biashara, lakini biashara hiyo ikawa hakuna kuaminiana ndio maana marehemu akaja juu, na kutokana na uchunguzi wetu, ilionekana kuwa marehemu alishukiwa kuwa alikuwa akifanya biashara nyingine kinyume na taratibu za kazi yake, wasi wasi wetu ni kuwa huenda na wewe uliguswa na hiyo hali, ndio maana mkafikia kutokuelewana...’akasema

‘Wewe umenena hivyo, na ni dhana yako siwezi kukukatalia, na kama umeligundua hilo, nafahamu fika unafahamu wapi pa kulipeleka, au sio, kuwa marehemu alikuwa akifanya biashara zisizo halali, na kama unashuku kuwa na mimi nilikuwa mwenza wake, basi lifikishe mahali husika, au unataka mimi nikusaidie...?’ akauliza mdada

Je ni mara nyingi marehemu anafika kwako? akaulizwa

Yah, ni mara nyingi, ni mtu ambaye nilizoeana  naye kwa namna fulani, lakini sio kwa undani zaidi, ...na nikisema ni mara nyingi simaanishi kuwa alikuwa anakuja mara kwa mara, hapana, ni wakati nikiwa na shida na yeye, ...akasema

Kwa kauli yako hiyo inaonyesha wewe na yeye mlikuwa mkifanya biashara fulani zilizowaweka karibu karibu au sio? akauliza

Unaweza kusema hivyo, ni mambo ya kawaida, mtu umekwama utoa itu chako, unakwenda kuongea naye, anakusaidia, na hilo amefanya kwa watu wengi, sio siri,...akasema mdada.

Kuna siku wewe na yeye mlikutana hotelini, kukatokea mzozo, na watu walisema ni maswala ya kimapenzi zaidi, na inasemakana kuwa huyo marehemu alikasirika alipokuona na mhasibu je kuna ukweli wowote? akaulizwa

Watu wanasema wapendavyo, sio kweli....akasema mdada.

Kuna kumbukumbu zilipotea ofisini kwa mtoza ushuru, na mtoza ushuru akadai huenda wewe ndiye uliyezichukua, na baadaye iakgundulikana kuwa sio kweli, lakitika kufuatilia kwetu, inaonekana bado mtoza ushuru alikuwa akikushuku wewe, tunahisi kuwa kilichomfanya marehemu afike kwako na hata kutoa bastola ni katika kuzitafuta hizo kumbukumbu....akasema mpelelezi

Nipeni ushahidi wa kutosha, maana hizo ni shutuma nzito, unasikia mpelelezi, kama hilo lipo kimaandishi, mimi nitalifuatilia kisheria , maana hamuwezi unishuku kwa jambo ambalo sihusiki...akasema mdada kwa hasira.

Mdada, mimi nakuuliza kwa nia njema tu, ninachotaka kutoka kwako ni kauli yako ya ukweli, kama sio kweli, niambie sio kweli,..hatupo hapa kushitakiana, naomba unielewe hilo..akasema mpelelezi.

Umesema katika kumbukumbu zenu, ina maana hiyo shutuma ipo kimaandishi, na inasadikiwa hivyo, kwahiyo ili nijisafishe ni vyema nikafuatilia kisheria, ...akasema mdada.

Kila ninachokuhoji, nakiweka kama umbukumbu, sio maana kuwa kuandika hivi ndio kweli, hapana, ni katika kuweka kumbukumbu ili zije kusaidia baadaye,...habu twende siku ile ya tukio hadi marehemu anapigwa risasi,...akasema mpelelezi

Mimi kwa muda ule nikageuka kuangalia pembeni, niliona watu wamesimama hatua chache kutoka pale nilipokuwa na uvaaji wao ni kama alivyokuwa kavaa mpelelezi, suti nyeusi na mawani meusi, ...mdada akaniona jinsi nilivyogeuka kuangalia na yeye akaguka uangalia huku na kule, ...na hapo hapo akauliza;

 ‘Mpelelezi hebu niambie hawa watu wamefuata nini hapa, kwanini umekuja na hao watu, ina maana mimi unanishuku kama mhalifu au...?’ akauliza mdada.

Sikiliza mdada, hao watu wanafanya majukumu yao, usiwe na wasiwasi nao...’akasema mpelelezi

Kwa hilo mimi sikuelewi,naona hapa una ajenda ya siri, ...akasema mdada huku akisimama kutaka kuondoka, nilipogeuza kichwa niliwaona wale watu wakisogea kuja pale tulipokaa...

NB; Kwanini mdada kataharuki


WAZO LA LEO: Ukikosea ni vyema ukajirudi na ikibidi ni vyema ukakiri hilo kosa, huo ndio uungwana, lakini pale unapokoselewa kwa kosa ulilolifanya ukawa mkaidi na hata kuja juu, na kusema `kwanini,...Ujue wewe una walakini. Ni vyema tukajenga tabia ya kukubali makosa, japokuwa wanasema, mtu mzima hakanywi bali anashauriwa. 

Ni mimi: emu-three

No comments :