Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, May 7, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-52


Nikiwa nimejipumzisha kwenye hoteli baada ya shughuli nzito ya mahakamani, nilijilaza kitandani, na kiuweli akili yangu yote kwa muda huo ilikuwa ikimuwaza mdada, mdada ambaye alitaka tuongee naye kipindi kesi ikiendelea lakini ikashindikana kwani mpelelezi naye alikuwa na mazungumzo na mimi, ikabidi nimtumie mdada ujumbe wa maneno kuwa nipo na mpelelezi,ana maongezi na mimi na akajibu.

‘Fanya uonavyo, ila uwe makini...’basi hatukuweza kuongea naye tena kwa siku hiyo, kwani yeye aliondoka mapema, na sikujua anakwenda wapi, au litaka kunimbia nini, nikabakia kwenye mahakama nikifuatilia hiyo kesi kwani hata mpelelezi naye aliondoka kama alivyoniambia kuwa kaitwa na wakubwa zake, nikawa najaribu kukumbuka mazungumzo yangu na mpelelezi huyo;

‘Hawa watu siwaelewi, wanataka nini, ...ukweli umeshabainika, wao wanaufukia, hii kweli sio haki, mambo kama haya hayataki siasa....’akasema

‘Ukweli upi huo bosi unaotaka kufukiwa, wakati mahakama ipo kwa ajili ya hilo?’ nikamuuliza na hilo neno bosi likamfanya aniangalie machoni na kusema

‘Bosi wako sio mimi bwana,...’akasema huku akionyesha kwa mkono kuwa niache hilo neno.

‘Aaah,...kwa hivi sasa wewe ni bosi wangu, ila mimi nauliza kuhusu hiyo kauli yako, ulivyosema wanataka kuufukia ukweli, ni akina nani na ni ukweli gani huo?’ nikamuuliza

‘We acha tu,...lakini anyway, nitajua huko mbele kwa mbele, usijali, kazi zetu hizi zinakutana na mitihani mingi, unaweza kupoteza muda wangu mwingi, halafu watu wengine wanakuja kuingilia na kusema hayo mambo yamalizwe kienyeji..., ‘akasema

‘Watu kama akina nani...?’ nikauliza

‘Unajua kwa hali kama hii udhalimu hautaisha,...ni lazime tufike mahali tuseme sasa basi, wadhalimu washugulikiwe, bila kujali huyu ni nani,vinginevyo tukiendelea hivi, kupindisha-pindisha mambo tutaleta mtafaruku katika jamii, na wananchi hawatakuwa na imani na viongozi wao...’akasema

‘Kwanini unasema hivyo, kwani hao wakubwa wako ni akina nani, sio hao hao polisi?’ nikamuuliza

‘Mimi ni mpelelezi wa kazi maalumu, sio lazima nishirikiane na polisi...ngoja mimi niende, ila ule mpango wangu wa kuongea mimi na wewe, bado upo pale pale, ni vyema, tukawa kitu kimoja, ili kuukomesha huu udhalimu, nafahamu ni kazi nzito, hasa pale siasa zinapojichomeka, lakini, haki ni haki tu, kama sheria inasema hivi huwezi ukasema sio hivi kwa vile huyu ni mwenzetu, hilo halipo...’akasema

‘Oh, unajua nimekuwa na wakati mgumu sana mimi, maana watu ninaokuwa nao karibu, ambao nawaona ni marafiki zangu , wamekuwa kama wananitega, hakuna anayetaka kuniambia ukweli wa moja kwa moja...inafikia mahali hata sijui ninachokifanya, mwisho wa siku nashindwa hata kujua nimwambia nani nini...’nikasema

‘Tumia akili yako, ...na kagua nafsi yako kwanza, kwa kujiuliza je hilo ninaloambiwa ni sahihi,...kama sio sahihi nahitajika kufanya nini, pili, je hilo nitakalofanya mimi ni la haki, je ningelitendewa mimi ingekuwaje, je jamii itaneemeka nini na hilo...cha muhimu usiwe mbinafsi wa maamuzi ya kijamii...’akasema

‘Sijakuelewa mkuu...’nikasema

‘Utanielewa tu, cha muhimu, tuwe pamoja, kivitendo, tenda kwanza niliyokuambia, na majibu yake utayaona baadaye.....’akasema na kuangalia pale alipokuwa ameketi mdada, ambaye kwa muda huo alikuwa hayupo akasema;

‘Nilikuona kama mlikuwa mnawasiliana na mdada kwa macho, kuna miadi ya kukutana naye leo?’ akaniuliza

‘Hapana,...alinionyesha ishara kuwa anatoka, ...’nikasema

‘Hivyo tu basi...?’ akaniuliza

‘Ndio hivyo tu mkuu, kwani vipi, ...’nikasema

‘Sawa, kama unahitajia kuonana naye nenda mkaonane, lakini naona yeye  keshaondoka, mtakutana huko hotelini au....?’akasema kama anauliza

‘Hapana sina cha kuongea naye kwasasa,...na sijui kama atakuja hotelini, siku hizi ana mambo yake mengi, hatunani mara kwa mara, ...sasa ngoja mimi nikasikilize kinachoendelea kwenye hii kesi maana naona itachukua muda, tofauti na nilivyofikiria...’nikasema

‘Yah, ndio hivyo, tatizo ni kuwa hii kesi imeshaingiliwa, maana imegusa masilahi ya watu, na hapo hapo siasa imeingia na kuweka kambi,itikadi zimeshika hatamu, na hili litamfanya huyo mlinzi aozee jela, huenda bila hata hatia,...’akasema

‘Siasa za chama gani, maana hapo sioni mtizamo wowote wa kisiasa...’nikasema

‘Kwenye masilahi, kila mtu anatafuta kinga, na hao mafisadi, kinga yao kubwa ni kwenye siasa, sio lazima awe wa chama fulani, lakini porojo zikizidi, na sheria ikawekwa pembeni, hiyo ni siasa, ...’akasema

‘Kumbe ni hivyo...’nikasema

‘Hapo tatizo ni ubinafsi, kwa mtizamo wa hao watu kwa vile wapo majumbani kwao, wanapulizwa na viyoyozi,wanaona hayo wanayoyaamua ni rahisi tu,...huyo si atakaa jela tu, baadaye tutamtoa, lakini hawaoni athari za kibinadamu, huyu mtu ana familia yake inahangaika huku na kule...haya huyo mtu mwenyewe ana-athirika kisaikolojia, kiafya..hilo halionekani kwasasa maana mwenye  shibe katu hatamtambua mwenye njaa...’akasema

‘Je hakimu hana mamlaka ya kuingilia kati na kuona haki ikitendeka haraka iwezekanavyo?’ nikauliza

‘Hakimu anakwenda kutokana na muendesha mashitaka, kazi yake ni kuona haki inatendeka kwa ushahidi, vielelezo na mashahidi, ...kama muendesha mashitaka atakuwa ananunua muda, kutokana na shinikizo fulani, yeye anaweza asijue lolote, na hataweza kuhukumu tu...’akasema

‘Je wewe una mpango gani kwa hili, kama hao wakubwa zako wakiamua watakavyo, na sio kwa jinsi haki ilivyo, kutokana na uchunguzi wako wewe utafanya nini, kwanini usisimame mahakamani na kutoa huo ushahidi wako ili haki itendeke?’ nikamuuliza

‘Nitajua huko mbele...kwa hivi sasa ni lazima nikamlishe upelelezi wangu haraka iwezekanavyo, nikimaliza hiyo kazi, ninachohitajika ni kuwakilisha kazi hiyo kwa mkubwa wangu, kazi yangu imekwisha,...’akasema

‘Oh, kumbe huwezi kuuatilia tena kuwa hayo uliyogundua yamefanyiwa kazi..’nikasema

‘Majukumu yangu yana mipaka yake, mimi nimetimiza wajibu wangu, hata hivyo, nitauma sana, kama watafanya kinyume cha uchunguzi wangu, lakini siwezi kuingilia kati,..hata hivyo mimi nina imani kuwa haki na ukweli wakati wote una nguvu, zaidi ya dhuluma...’akasema

‘ Ni kweli lakini mimi nina mashaka na hilo....maana pesa na utajiri unaweza ukaitengeneza haki ikawa vingine, na ukweli ukawa tofauti....’nikasema

‘Ni swala la muda, ..sikukatalii kwa hilo...siku hizi propaganda potofu zinasikika sana kuliko ukweli..., ni kweli, na ndio maana hadi sasa dunia haina amani, watu wanauwana ovyo, na kila anayepata mwanya wa kujaribu kuelezea kilio chake, anajikuta kwenye wakati mgumu, ndio maana wengine wanaamua kutumia kinga za namna kwa namna wengine hufikia kutumia hata imani zao za dini kufikisha ujumbe wao...na ukiangalia ni mambo yao binafsi tu, sio dini, lakini wameona ndio sehemu sahihi ya kufikisha ujumbe wao, na wale wahusikaa kama sio sahihi...’akasema

‘Ndio wengine wanafikia kuua watu wasio na hatia....?’ nikamuuliza

‘Hilo ni kosa kubwa sana wanalolifanya,...dhuluma inamfanya mtu aingiwe na chuki,...keshakata tamaa, anachotaka yeye kwa muda huo ni kulipiza kisasi, na hali hiyo inamgeuza mtu kuwa mnyama na hata kufanya unyama zaidi ya yale aliyofanyiwa...’akasema

‘Haiwezekani, ...ili iweje sasa?’ nikauliza

‘Ndio hivyo, kwa muda huo akili imeshaganda,..hasira, chuki, ndivyo vimemtawala, hajali atakachokifanya, na hapo jamii haitaweza kumuelewa tena na hilo ndilo kosa kubwa, katika harakati zozote, unatakiwa uweke jamii yako mbele, ufanye jambo kwa masilahi yao,...baadaye watakuelewa tu, japokuwa jamii inaweza kupotoshwa na propaganda potofu, na hata kukuona wewe unayetetea masilahi yao ni mbaya....’akasema

‘Sawa bosi, naona wewe ni mwanaharakati sasa, ngoja mimi niende ndani kusikia ni nini kinachoendelea kwenye hii kesi...’nikasema

‘Sawa wewe sikiliza tutapashana habari, japokuwa mimi nafahamu ni kitu gani kitaongelewa hapo leo na mamuzi ya leo ni nini...’akasema huku akiondoka.

‘Nakusikiliza wewe...’nikasema

‘Sawa tupo pamoja...ila ukumbuke ahadi yetu...’akasema

‘Ahadi gani...?’ nikamuuliza

‘Ya kuniambia ukweli wote, tukikutana mimi na wewe ujiandae kwa hilo, kama utaongea na mdada kwanza, mimi sijui, cha muhimu ni kuniambia ukweli, sizani kama wewe utafurahi mtu ateseke au ahukumiwe kisivyo halali,..hata kama kuna shinikizo la namna gani, lakini sheria ni lazima ishike mkondo wake...’ akasema na kundoka.

************

Nikiwa bado kitandani nikiwaza , mara bosi akanipigia simu kuwa anataka tuonane naye ofisini kwake kesho yake...nilifurahi sana kusikia sauti yake, na hakuwa na muda mwingi wa kuongea naye kwenye simu, na mimi nikamkubalia kuwa nitafika ofisini kwake kesho yake asubuhi, ili baadaye nikitoka hapo nikutane na mpelelezi.

Kesho yake asubuhi nikajiandaa kama mtu anayekwenda kazini, na walinzi wakaniuliza na kwenda wapi, nikawaambia nimeitwa na bosi wangu, ikabidi wawasiliane na wahusika, na baadaye nikaruhusiwa nikisindikizwa na walinzi wawili, ili kuhakikisha kuwa kweli nakwenda huko kulikohitajika.

Nilipofika ofisini , wafanyakazi wengi waliniangalia kwa bashasha, na hata hivyo, sikuweza kuongea nao, kwani ratiba na muda haukuniruhusu, nikaingia moja kwa moja kwa bosi wangu, ..kabla ya hapo nilikutana na mhasibu aliyepewa kukaimu nafasi yangu, tukabadilishana maneno mawili , matatu , halafu nikaingia ofisini kwa bosi.

‘Mhasibu pole sana na matatizo yaliyokukuta, kiukweli yamenikwaza sana hata mimi, kama ujuavyo mimi nilishakuandaa uwe mtu wangu, lakini ghafla, haya yanatokea,....siwezi kukulaumu sana,lakini kwa namna nyingine, wewe mwenyewe umechangia ...’akasema

‘Kwa vipi bosi?’ nikauliza

‘Hujiamini, na huna msimamo,...nikuambie ukweli, kwenye maisha ya kujitegemea, kujiamini na kuwa na msimamo ni kitu muhimu sana, maana wewe sasa hivi utakuwa na familia yako, sasa kama hujiamini, kama huna msimamo hutaweza kuiendesha fanilia yako,...na halikadhalika, katika kazi, utakuwa kiongozi wa kampuni au kundi fulani, kama hujiamini, na kama huna msimamo, utayumba, na kampuni au kundi hilo halitaweza kusimama kwenye lengo lenu...unanielewa hapo...’akasema

‘Kwahiyo mimi siwezi hayo, au?’ nikauliza

‘Kuweza unaweza, ila kuthubutu, inakuwa ngumu kwako...wengi wanapoteza muda wao, wanahindwa kuendelea kwasabbu ya kuogopa kuthubutu...naona hata wewe ni hivyo hivyo...amua,pale unapoona ni sahihi, na utajuaje kuwa ni sahihi, ni kutoana na taaluma yako...au sio, kama huna utaalamu na hicho kitu unauliza, utaelewa, na hapo utaweza kufanya jambo kwa kujiamini...matokeao yake utayaona au sio...’akasema

‘Sawa bosi, naona mimi nina bahati ya kukutana na walimu, kila hatua nakutana na wakufunzi wa namna moja au nyingine, nashukuru sana bosi....’nikasema

‘Nimekukosa sana, tena sana, wewe na mdada, hasa niliposikia mumepata akzi nzuri, japokuwa mdada alinificha kuwa na yeye atakuwa kwenye kazi kwenye vitengo hivyo hivyo, lakini nilikuja kuambiwa...’akasema

‘Mbona mimi hilo sijui...’nikasema

‘Kazi siku hizi ni kujuana,...kubebana,....’akasema huku akicheka, na akainua kichwa kuniangalia, huku akisema;

‘Niliposikia hivyo kuwa mumepata kazi sehemu nyeti kama hizo nilifurahi sana,  niliona kuwa huenda itakuwa ni neema kwenu,lakini kwa taarifa nilizozipata baadaye inaonekana  kama kuna mchezo mchafu unaotaka kuchezwa, kwa kukutumia wewe, ..hebu niambie vyema ni kitu gani kinachoendelea?’ akaniuliza bosi huku akiniangalia moja kwa moja usoni.

‘Bosi kiukweli hata mimi hadi sasa sijaelewa ni kitu gani hasa kinachoendelea na zaidi ya hayo, hadi sasa sijaelewa mustakabali wa maisha yangu, kwani hata hiyo ajira yenyewe niliyoahidiwa,bado sijakabidhiwa na nilichoambiwa hivi karibuni ni kuwa hilo litafanyika baada ya kesi inayotukabidli kuisha kwani kuna watu wameweka pingamizi….’nikasema

‘Mhasibu unakumbuka toka awali nilishakuambia uwe makini na mdada,....sio kwamba namuona mdada ni mtu mbaya, hapana, yeye ni mtu mzuri, licha ya mapungufu yake kibinadamu,....unajua nikuambie ukweli, hata mimi bado sijamuelewa sana mdada, japokuwa nimeishi naye, na ni mfanyakazi wangu, lakini ana mambo mengi ya chini kwa chini, mpaka unafikia mahali simuaminiamini  ni kweni ni mfanyakazi  wangu na baba yake ni mwenza wangu katika biashara…lakini kwa hali ilivyo sasa, naona ni heri aende huko anapokwenda, sitamuweza tena...’akasema

‘Kwahiyo hata mimi umefurahia kuondoka kwangu?’ nikamuuliza

‘Wewe hapana, ...nilishakufahamu na nilijua nikikaa na wewe hatua kwa hatua nitakujenga, uwe mtu wa kuweza kushika hatamu, lakini mdada akakuteka mawazo....nikajaribu kukushauri, lakini hukutaka kunisikia, ndio tatizo hapo...’akasema

‘Bosi mbona mimi nilijaribu sana kukusikia na nikajitahidi kufanya hivyo, lakini mengi yaliyotokea naweza kusema sio kusudio langu....yametokea tu ili iwe sababu..’nikasema na bosi akatikisa kichwa kama kukataa, na mimi nikaendelea kuongea,

‘Bosi kwa ushahidi wa kutetea hoja yangu, hebu angalia kifo cha mtoza ushuru kilivyotokea, je mimi nilijua hilo litatokea, mimi na wewe tulikwenda kumsaidia mdada,...,kama unakumbuka kwenda kwangu kwa mdada ni kutokana na makubaliano yangu mimi na wewe, kwa nia kumsaidia mdada, na tulikwenda wote, ulipoondoa tu ndio hayo yakatokea,…’nikasema.

‘Hayo ni matokea ya matendo yenu ya nyuma...na kama hayo mauaji yansingelitokea nahisi kuwa ungebadilika kabisa, ukawa kama atakavyo mdada....lakini mauaji hayo, yamezuia kila kitu...’akasema

‘Bosi mbona uanaongea kama unafahamu mambo mengi kumhusu mdada...’nikasema

‘Mhasibu hebu niambie kuna kitu gani alichokufanyia mdada hadi ukawa mtumwa wake,sizani kama unafanya yote hayo anayoyataka yeye uyafanye kwa utashi wako,nahisi kuna shinikizo jingine, hebu niambie ili tuweze kwenda sawa kama bado unaniamini kama mshauri wako?’ akaniuliza

‘Bosi hakuna kitu, mimi na mdada tumezoeana kikawaida tu,na mengi aliyonifanyia baadaye nilikuja kugundua kuwa ulikuwa ni mzaha tu,ili niwe karibu na yeye, nahisi alinihitaji mimi niwe mwenza wake, ndivyo mtizamo wangu ulivyo, hata hivyo, bado sijakubaliana na yeye….’nikasema na bosi akawa ananiangalia tu hasemi neno, nikaendelea kuonga

‘Bosi nikuambie ukweli, ukiwa na mdada kama humjulii vyema , unaweza kuhisi vinginevyo, kuwa huyu binti ni muhuni, ana tabia mbaya, anaringa,...lakini sivyo hivyo, nimekuja kugundua kuwa mdada ni binti mnzuri tu,...ana utani mwingi, na ni mtu wa kuona mbali kimaendeleo...bosi kiukweli mdada hajanifanyia kitu kibaya, cha kunifanya hivyo, kuwa niwe mtumwa wake, hapana, mengi ninayofanya, nayafanya kwa hiari yangu tu …’nikasema

‘Siamini...hayo ninayoyasikia, kweli kupenda ni kubaya,...unajua mhasibu, nakuuliza haya kwasababu nimeongea na baba mkwe wako, na kanilalamikia sana, kuwa wewe umebadilika kabisa tofauti na jinsi alivyokuwa akikuamini, na hata hicho cheo yeye ndiye aliyekuhangaikia,...unalielewa hilo..’ akawa kama ananiuliza

‘Baba mkwe wako alitegemea kuwa utakuwa upande wake, ndio maana akakupigia debe ili ukipate, lakini umemgeuka na kumsaliti…umekuwa upande wa mdada, ...mdada ambaye kutokana na kauli ya baba mkwe wako mdada kawa adui ayke mkubwa...sijui kwa vipi...’akasema

‘Bosi mimi sijafanya lolote baya, ninachoshangaa ni baba mkwe wangu kuyasema hayo kwa watu wengine  badala ya kuniita mimi mwenyewe tukayaongea,nikamueleza yangu kwa upande wangu….mimi bado namthamini kama baba mkwe wangu na ninajali juhudi zake,ndio maana nikakubali hicho cheo…’nikasema

‘Je ni kweli kuwa wewe na mtoto wake mumeshavunja uchumba wenu?’ akaniuliza

‘Nani kakuambia kuwa tumevunja uchumba wetu mimi na Binti….bado mimi nafahamu kuwa huyo binti ni mchumba wangu ikizingatiwa kuwa Binti ni mama wa mtoto wangu…’nikasema

‘Walioniambia ni baba mkwe wako,na pia nikiwa naongea na mdada alisema hivyo hivyo, niliongea nao kwa wakati tofauti,kwahiyo hata kama wewe hutaki kuniambia ukweli, lakini ukweli nimeshaufahamu…sijui ni kitu gani kinachoendelea kati yenu watatu, wewe mdada na huyo binti, lakini kwa hayo mnayoyafanya mjue mnamuumiza sana huyo mzee...’akasema

‘Lakini mimi siyafahamu lolote baya,….’nikasema kiunyonge

‘Sajajua zaidi, nilitaka kupata ukweli kutoka kwako, lakini naona hilo halitawezekana, hamna shida...’akasema

‘Bosi ukweli ndio huo, mimi sijavunja uchumba wangu na huyo binti, kama wamefanya wao, mimi sijui..’nikasema

‘Haya hamna shida ila ninachotaka kukuambia kwa sasa ni kuwa kutokana na hali inavyoendelea kwasasa, na sijui ni nini hatima ya kesi yetu, mimi nimeonelea tufikie hatua nikutambue kuwa wewe sio mfanyakazi wangu tena, japokuwa hilo tulishaliongelea kwa mdomo…lakini sasa nataak tulifanye kisheria, unafahamu tena taratibu za kikasi, ningelifurahi uwe nami, lakini hilo naona halitawezekana tena’akasema

‘Bosi mimi naona unipe muda...mimi bado nataka kufanya kazi hapa kwako, huko wanapotaka kunipeleka naona kama wanataka kunitega tu...’nikasema

‘Usijali, ....cha muhimu ni nini kesi yenu itasema...zaidi siwezi kukubeba, maana hata mzazi hubeba mtoto wake, mwisho wake, anashindwa kumbeba tena, anahitajia huyo mtoto atembee mwenyewe...sasa naona umekuwa, unaweza kutembea mwenyewe, au sio..’akasema

‘Bosi, sikatai, na nisamehe sana kwa kutokuwa mtiifu sana kwako, lakini kiukweli mimi nimejitahidi sana na nimekuwa nikifanya yote yale uliyonishauri, hata hivyo, nakiri kila binadamu ana mapungufu yake, huenda mimi kutokana na udhaifi wangu sikuweza kufikia lengo kama ulivyotaka, ...nahitajia muda, nilikuwa naomba usichukue hatua zaidi,hadi hii kesi iishe....maana hata hicho cheo cheneywe kina mizengwe....’nikasema

‘Mhasibu kama ingelikuwa ni mimi mwenyewe, nisingelichukua maamuzi haya, lakini ujue kampuni yangu, sipo mwenyewe, nina wenzangu, wawekezaji wenza, na wao wana kauli zao, na kwa pamoja kwa nia njema wameamua hivyo,...kwahiyo siwezi kwenda kinyume na wao...wewe kwasasa pigania haki yako, na kesi hiyo ipite, mengine yatafuata baadaye....’akasema

‘Oh, naona kama naanza kutupwa, maana kama baba mkwe keshaanza kunishutumu na kuniona sifai, na hata kuvunja uchumba wangu na binti yake, nahisi mabaya zaidi yataniandama....sasa na wewe tena ambaye nilishakuona kama mzazi wangu, umeamua kunitupa, sijui hatima ya haya yote itakuwaje...’nikasema

‘Cha muhimu ni kupambana, vumilia shida, vumilia matatizo, ukiwa katika msimamo thabiti wa haki na ukweli...jitahidi sana kusimamia hayo, ..nina uhakika, kama kweli upo kwenye kutenda haki, ukawa mkweli, utafanikiwa, kwani walisema wahenga, baaada ya dhiki mara nyingi huwa ni nini....?’ akauliza na mimi nikamwangalia huku nikitamani kulia, na mwishowe nikasema

‘Ni faraja....’na hapo simu yangu ikalia,...alikuwa mdada akinipigia.

NB: Tumalize tusimalize..


WAZO LA LEO: Mungu hana kasoro katika uumbaji wake, na kila jambo kalifanya kwa makadirio yake, inakuwa ni ajabu binadamu kuanza kukashifiana kutokana na maumbile ambayo mtu hakuyaomba, kazaliwa hivyo, kajikuta yupo hivyo, wewe unamcheka, wewe unamkashifu, ...ina maana gani hapo, ni kuwa wewe unampinga mwenyezimungu. Kumbuka aliyekupa wewe ndiye huyo huyo aliyemnyima huyo unayemcheka, na kumkashifu, utakuja kuulizwa mbele ya hukumu.

Ni mimi: emu-three

No comments :