Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, March 17, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-27



‘Hii kesi imekaa vibaya kweli, kwani polisi wana ushahidi wa kutosha wa kuonyesha kuwa wewe na mdada mlishirikiana kumuua mtoza ushuru, ...’akasema wakili na kuniangalia kwa makini.

‘Lakini kama nilivyowaambia mimi sihusiki kabisa kwani nilitoka mle ndani, mtoza ushur akiwa hai, na kipindi hicho aliyekuwa kajeruhiwa ni mdada,..kwahiyo yaliyokuja kutokea baadaye mimi sikuwepo,....’nikasema

‘Kwa ushahidi gani, ..mlinzi kaulizwa, na kusema kuwa alisikia milio ya bastola kabla hujatoka ....kwahiyo inavyoonekana baada ya kutenda kosa hilo ndio ukaamua kukimbia,...’akasema wakili

‘Mimi?!, ..hapana, nikuambie ukweli, muheshimiwa wakili, mimi sijui kabisa hata kuitumia bastola, ..nitawezaje kumuua huyo mtu, na kwanini nimuue, hapaan hapo nitakuwa nasingiziwa kosa ambalo sio langu....’nikasema

‘Bastola unaweza ukaitumia hata kama hujawahi kuitumia kabla kwa kuona wanavyofanya watu, ...kwenye sinema nk, ...ni ujasiri mdogo tu, na inavyoonekana ulifanya hivyo,ndio maana ukaogopa na kuanza kukimbia....’akasema huyo wakili.

‘Muhehimiwa unavyoongea nakuona kama huniamini, sasa nikuulize wewe hapa unataka kunisaidia au nia yako ni kuzidi kuniweka matatani..?’ nikauliza nikionyesha mashaka ya wazi.

‘Kukusaidia kwangu kutakuwa rahisi nikiufahamu ukweli,..’akasema na kuangalia saa na kabla sijasema kitu akasema;

‘Ndio ni kweli, nataka kukusaidia kwani hiyo ni moja ya kazi yangu, lakini ni lazima nifahamu ukweli ulivyokuwa, na kukuhoji hivi ni moja ya njia ya kutafuta ukweli ili niweze kukusaidia, kazi yangu itakuwa rahisi kama utanipa maelezo yanayojitosheleza, nafikiri hadi hapo umenielewa,...’akasema na mimi nikatulia na yeye akaendelea kusema;

‘Ninachotaka kwanza kufahamu ni kiini cha tatizo lenyewe, je kuna jambo gani jingine linaweza kuwa chanzo cha haya yote, ...huenda kuna kitu kingine kilitokea, huenda kuna jambo lilikuwa linafanyika kukawa hakuna makubaliano, ....kuna sababu nyingi, mimi kama wakili siwezi kuota,....ndio maana nataka unifahamishe mahusiano yako wewe na mdada..’akatulia kidogo

‘Hakuna mahusiano mengine kati yangu mimi na mdada, zaidi ya hayo ya kikazi.....kama nilivyokuelezea awali ndio hivyo hivyo tu..’nikasema huku moyoni nikijisuta , sijui kwanini niliamua kusema hivyo. Wakili akachukua simu yake na kuandika kitu huenda alikuwa anatuma ujumbe halafu akasema;

‘Haya twende sehemu nyingine, kuhusu marehemu ,...’akatulia kidogo kuniangalia.

‘Kuhusu marehemu, ...kuhusu nini ?’ nikauliza

‘Je huyu mtu mlikuwa mnafahamiana naye kabla?’ akaniuliza

‘Kwakweli hapana, zaidi ya kukutana njiani, na watu wengi wanamfahamu siwezi kusema siwezi kabisa kumfahamu,...’nikasema

‘Hamajawahi kukutana naye uso kwa uso, mkaongea mkapanga, ...kwa namna moja au nyingine?’ akaniuliza

‘Kukutana naye uso kwa uso, ni kama mara mbili, ...na ilikuwa ni muda mchache tu, akiniuliza maswali, kama namfahamu mdada, nafanya kazi naye...lakini sikuwa na mazoea naye, kihivyo,.....’nikasema

‘Kwahiyo hamjawahi kuwa na mahusiano naye ya kikazi, au kwenda ofisini kwake, au kufanya kazi naye ya jambo lolote?’ akaniuliza

‘Hapana, sijawahi, maana kama ni kikazi, mimi sikuwahi kupata akzi ya kuonana naye uso kwa uso, na nje ya kikazi, sijawahi kukutana naye kwa hili wala lile...’nikasema

‘Hebu nielezee alipokuja huyo mtoza ushuru usiku wa tukio,ilikuwaje, ulikuwa unafahamu kuwa atakuja huyo mtu?’ akauliza

‘Hapana sikuwa nafahamu kabisa kuwa atakuja, maana huyo alikuwa ni mgeni wa mdada, na mimi nilifika hapo tu kusaidia,kama unavyofahamu kuwa mimi na bosi tuliamua kuja hapo kumsaidia mdada kama mfanyakazi mwenzetu, sasa ningeliwezaje kufahamu kuwa atakuja, wakati mdada alikuwa kalala, hajitambui kutokana na hizo dawa, ....kwakweli sikuwa nafahamu kuwa huyo mgeni wake atafika...’nikaelezea hivyo.

‘Maelezo yako na mlinzi ya mlinzu yanajikanganya, mlinzi alisema inaonyesha kuwa ulikuwa na unafahamu kuwa huyo mgeni atafika, na ulimwagiza akamuulize huyu mgeni wake kama ana mzigo, hebu niambie huo mzigo ni kitu gani hasa?’ akauliza

‘Mzigo!?’ nikauliza kwa mshangao

‘Ndio mzigo ina maana hufahamu hilo...?’ akaniuliza

‘Ndio....najaribu kukumbuka, ...ndio mdada aliniambia hivyo, kuwa kuna mzigo atakuja nao huyo mtu..’nikasema.

‘Hii inaonyesha kuwa wewe na mdada mlipata muda wa kuongea, kuhusu huo mzigo, ndio maana yeye akakuagiza, kuwa huyo mtu atakuja na mzigo, ...’akasema huyo wakili

‘Lakini wakili nia na lengo letu hapa ni wewe kunisaidia,....au sio,  na sio kunitia matatani, hayo maswali yako yanaonyesha unataka kunitia matatani, inakuwa kama wewe ni polisi, unatafuta kunihukumu...’nikasema

‘Kukuhukumu kwa vipi, ....?’ akaniuliza na mimi nikatulia na yeye akasema;

‘Usipoaniambia ukweli sizani kama nitakuwa na nafasi ya kukusaidia, kama nilivyokuambia, kama hakuna maelezo mengine, ni bora tutafute wakili mwingine, mimi kwa hali kama hii naona sitaweza kukusaidia, ninachotaka ni wewe kunijibu maswali yangu na kuelezea kila kitu ili niweze kuchanganua kipi na kipi  ...’akasema

‘Kwanini iwe hivyo, unaamini kuwa mimi nina hatia kuwa nilihusika kwa hayo yaliyotokea,.... kiukweli mimi nimeshakuambia kila kitu ninachohitajika kukuambia, mengine haya umuhimu hapa....’nikasema, na yeye bila kujali maelezo yangu hayo akauliza swali

‘Huo mzigo aliokuagiza mdada ni mzigo gani?’ akaniuliza

‘Siwezi kufahamu, maana aliposikia kuwa kuna mgeni wake amefika,.. mdada akaniuliza huyo mgeni ni nani, nikamwambia simfahamu, akasema nifuatilie nifahamu ni nani,...na akaniambia huenda ni mgeni wake aliyefika na mzigo wake, kama ni huyo basi aulizwe kama kaleta mzigo wake, ..’nikatulia kidogo nikitafuta maneno zaidi.

‘Ndio nikamtuma mlinzi akamuulize, ..’nikasema na kutulia na wakili akawa ananiangalia tu, na nilipoona bado katulia nikasema;

‘Nikapeleka taarifa kwa mdada, na mdada akasema kama ni yeye, basi mimi nikauchukue huo mzigo wake maana hakutaka kusumbuliwa, na mimi nikafanya hivyo,..nakumbuka kabisa alisema mimi nikamalizane na huyo mgeni....’nikasema

‘Mkamalizane na huyo mgeni, kuhusu nini...?’ akaniuliza

‘Kuhusu huo mzigo kuwa niuchukue mimi, nimpelekee..ndivyo nilivyoelewa mimi kwa kauli hiyo...’nikasema

‘Ok, kwahiyo wewe ndiye uliyeambiwa ukauchukue huo mzigo kwa huyo mgeni, baada ya mlinzi kuja kutoa taarifa kuwa kuna mgeni, ukamwambia mlinzi aende kumuuliza huyo mgeni kama ana huo mzigo, akaenda na aliporudi uliambiwa nini na huyo mlinzi?’ akauliza.

‘Mlinzi aliporudi alisema huyo mgeni anadai kuwa na yeye anahitajia mzigo wake kutoka kwa mdada, ilionyesha kuwa ni biashara ya kubadilishana mizigo, nipe ni kupe,...’nikamwambia

‘Ulijuaje kuwa ni biashara...na kuwa ni biashara ya nipe nikupe?’ akaniuliza

‘Nilipopeleka taarifa kwa mdada, mdada alinipa bahasha, na kuniambia kuwa nimpe hiyo bahasha, na mimi nitapewa huo mzigo...’nikasema.

‘Kwahiyo ilikuwa ni bahasha ya namna gani?’ akauliza

‘Bahasha kubwa hizi za kuweza kuweka kitu cha siri na maandishi ya CONFIDENCIAL,juu yake,..’nikasema

‘Umesema ilikuwa ni biashara ya nipe nikupe, ulikuwa na maana gani hapo?’ akaniuliza

‘Kwasababu nilipokwenda kumuona huyo mgeni nay eye alidai kwanza nimpe huo mzigo wake kutoka mdada, ndio atoe mzigo aliokuja nao...’nikasema

‘Kwahiyo wewe ulikuwa ni wakala wa mdada, au sio?’ akaniuliza

‘Kwa namna hiyo na kwa muda huo, unaweza kusema hivyo, kwani nilikuwa nimekubali kumsaidia mdada, kwa vile alikuwa mgonjwa, na yeye alishanipa huo mzigo wa kubadilishana na huo mzigo aliokuwa nao huyo mgeni..’nikasema

‘Hukuweza kugundua ni mzigo gani, au kukisia?’ akaniuliza

‘Zilikuwa ni bahasha kubwa kama nilivyosema awali,...unaweza ukahisi kuna kitu kigumu ndani kilichopo kwenye bahasha pia, lakini sio rahisi kugundua ni kitu gani, ....kwakweli hata mimi nilijiuliza sana ni kitu gani kipo kwenye hizo bahasha lakini sikuweza kugundua...’nikasema na mara simu ya huyo wakili ikalia.

‘Samahani ngoja niongee ni hii simu, akasema na akasogea pembeni, alikaa kwa muda akiongea na simu baadaye akarudi na kuniangali kwa makini, halafu akasema;

‘Una uhakika umeniambia ukweli...?’ akaniuliza alipomaliza kuongea na simu

‘Ndio hivyo sijui unataka nikuambie nini zaidi...’nikasema

‘Polisi walimuita tena yule mlinzi wa mdada, wakamuhoji kwa mara nyingine tena, na mlinzi anasema, marehemu alipofika siku hiyo, hakuonekana kama livyokuja awali, alionekana hana raha, na hayupo sawa kama alivyosema mlinzi, na alipolizwa kwa vipi, ndio akasema alipofika mara ya kwanza, mgeni huyo alikuwa mnyenyekevu, na hata alifikia kumpigia magoti mdada...lakini safari hii alifika akiwa na hasira, kitu ambacho kilimtia mashaka huyo mlinzi...’akasema wakili.

‘Na ili kuondoa mashaka, akampigia simu mdada, lakini mdada hakupokea, ndio maana akaamua kuja kuonana naye ana kwa ana....na hakufahamu kuwa mdada alikuwa katika hali mbaya kiasi hicho kwani hakuambiwa, alijua ni kawaida yake kuumwa na dakika chache anakuwa mzima....’akasema

‘Kitu cha ajabu kwake kuwa bosi wake anaumwa, wanakuja watu, lakini yeye haambiwi kuwa bosi wake ni mgonjwa kiasi gani, hilo lilimkera sana, lakini hakuweza kulisema kwa vile kazi yake ni kulinda usalama wan je...’akasema

‘Mimi hayo siyajui, ni maisha yake na bosi wake, au?’ nikamuuliza

‘Polisi wanasema huyo mlizi alisema kuwa huyo jamaa alipoingia hakutaka kuongea sana alionyesha kuwa na hasira na majibu yake yalikuwa ni ya mkato, sio kama alivyofika awali, na alipopiga simu kuongea na bosi wake hakujibiwa, kwahiyo hakuwa na la kufanya kwa vile huyo jamaa sio mara yake ya kwanza, akamuamini, na hakuwa na nafasi ya kumkagua kama ana silaha au hana silaha,...’akasema huyo wakili

‘Kwani huwa anakagua watu wakiingia?’ nikauliza

‘Anasema akiwa na mashaka na mtu, huwa anafanya hivyo....’akasema

‘Kwa maelezo ya polisi, huyo mlinzi alisema hata alipokuja kumuona mdada, ili kuhakiki kama kweli huyo mgeni, anatambulikana, hakupata ushirikiana wa kawaida kwani hakuonana na mdada, yeye aliambiwa kuwa mdada kapumzika, na hataki kuonana na mtu...’akasema

‘Ndio hivyo ilivyokuwa kama nilivyokuambia..unaonaeeeh.’nikasema kwa kujiaminisha

‘Mlinzi anasema alipofika kumuona mdada, alikutana na mtu asiyemfahamu...’akasema na mimi hapo nikashituka kidogo na kusema;

‘Lakini mimi namfahamu huyo mlinzi, tunafahamiana na tulionana na mimi, kwanini anasema hivyo?’ nikauliza

‘Una uhakika humo ndni hakukuwa na mtu mwingine? Akaniuliza na mimi nikashituka kidogo, na kutulia, nikasema

‘Nina uhakika, nilikuwa mimi na mdada...’nikasema na yeye akaniangalia kwa muda akasema

‘Polisi wanahisi kulikuwa na mtu mwingine humo ndani, zaidi yako wewe, na huyo ndiye wanamtafuta, ...’akasema

‘Mtu mwingine zaidi yangu mimi, mbo-mbona sielewi .....’hapo akili ikanikaa sawa nikajikuta nikitikisa kichwa na kujiona sina la kusema, nilishashahu kabisa nikajiuliza kwanini nifanye kosa hilo,...ooh, too late

‘Polisi wanasema kulikuwa na mtu mwingine aliyekuwa na ndevu, za kidevuni na puani, ndiye aliyeongea na mlinzi, ...na sio wewe, ..hebu niambie ni mtu gani mwingine mlikuwa naye humo ndani..?’ akaniuliza na mimi nikabakia kimiya

‘Polisi wanahisi huenda huyo mtu mwingine ndiye aliyefanya mauaji, baada ya kupokea huo mzigo toka kwa marehemu, ..na ulipotoka kuonana naye akakuona na kukugonga kichwani na kitu kizito ukapoteza fahamu na baadaye akafanya hivyo hivyo kwa mdada lakini wakawa wanashindwa kufahamu jinsi ilivyotokea kwa mdada kujeruhiwa na risasi, je alifanyiwa hivyo na marehemu au na huyo mtu, wakati wanapambana...hizo ni hisia za mwanzo za polisi..’akasema

‘Kuna hisia za pili?’ nikauliza

‘Hisia za pili ni kuwa huenda wewe na mdada mna jambo, mna biashara ya pamoja, na marehemu alikuja kwa ajili ya kulipana, na kukawa hakuna makubaliano, ndipo ugomvi ukatokea, wewe ukamzidi marehemu nguvu, ukachukua bastola, na ukampiga mtoza ushuru, na huyo mtu wa tatu, akaona atumie nafasi hiyo, alipoona mdada kazidiwa, akakupiga kitu kichwani ukapoteza fahamu, akatokomea na huo mzigo..na vitu vingine...’akasema

‘Zote hizo ni hisia hakuna ukweli...na vitu gani vingine havipo,?’nikasema nikikumbuka jinsi gani nilivyozibandua zile ndevu kwa haraka, nilipozindukana, na kuzitupa kwenye bustani wakati nalifuatilia lile pikipiki....

‘Haya niambia huyo mtu wa tatu aliyekuwa humo ndani ni nani, kwa melezo ya mlinzi kimaumbile mnafanana sana, umbile lake ni kama lako, lakini kinachomtofautisha yeye ni wewe ni ndevu, na nguo alizokuwa amezivaa, na alikuwa na viatu vya wazi....vilivyombana, kuonyesha sio size yake....’akasema bila kunijibu swali langu la hivyo vitu vingine vinavyosaidikiwa vimechukuliwa.

‘Huyu mtu gani mbona sikumbuki kumuona, huyo mlinzi anasema alimuona huyo mtu pamoja na mimi...?’ nikauliza na hapo nikaanza kukumbuka, nilishasahau kabisa, sijui ni kwasababu ya tukio zima, au ni kwasababu ya kugongwa kichwa, nikatulia na hapo kumbukumbu za tukio zima zikaanza kunijia kichwani, nikabakia nimeduwaa

‘Wewe ndiye uniambie ukweli, je huko ndani mlikuwa watu wangapi, maana bosi wako anasema alipoondoka ulibakia wewe na mdada, sasa huyo mtu mwingine alikuja saa ngapi, na huyo ndiye aliyeongea na mlinzi, lakini wewe unaniambia kuwa wewe ndiye uliyeongea na mlinzi, ...una uhakika umeniambia ukweli ulivyokuwa,...maana sasa nashindwa kuunganisha maelezo yako na mlinzi je ni nani anayesema ukweli ni mlinzi,au ni wewe...?’ akaniuliza

‘Mhh, naomba muda nifikiri kidogo...’nikasema

‘Kwa sasa huna muda wa kufikiri, polisi wanataka kuja kuonana na wewe....unaweza kuwakatalia kuwa huwezi kuongea nao, ...hiyo ni haki yako, na au ukaongea nao nikiwemo,nia na lengo lao ni kutaka kukuhoji tena...’akasema

‘Kinachonikwanza ni kuwa bado sijapata maelezo y akutosha,..kwa hivi sasa sina ujanja,itabidi niwakubalie wakuhoji, ili na mimi niweze kuona wapi kuna kitu kimejificha, bila hivyo siwezi kuishika hii kesi,...’akasema

‘Nikikataa kuongea nao, nikasema waongee na wakili wangu itakuwaje?’ nikauliza

‘Unaye wakili wako?’ akaniuliza

‘Si ndio wewe, bosi kasema wewe ndiye wakili wangu...’nikasema

‘Mhh, unafahamu, usifikiri mtu anaweza kukubali tu kuwa wakili wa mtu bila kujua chanzo cha tukio...hatufanyi kazi kwa pesa tu, ....tunaangalia na akzi yenyewe, kesi yako ni ya mauaji, na ni ngumu, ...’akasema

‘Kwahiyo hutaiweza?’ nikamuuliza

‘Kwanza ni wewe uniambie ukweli,...mimi kwasasa nionavyo, nitawakubalia polisi wakuhoji, mbele yangu,au niongee nao mwenyewe ukiwemo, lakini ili hilo likubalike ni mpaka mimi nikubali kuwa wakili wako, je nitakubalije kuwa wakili wako wakati hujaniambia ukweli,...unanielewa hapo, sasa unahitajika kuniambia ukweli wote ili niweze kujirizisha kama kweli naweza kuwa wakili wako...’akasema

Akilini nikawa sina la kufanya, nilijikuta katika wakati mgumu, nikisema ukweli nitajiweka kwenye wakati mgumu, kwa baba mkwe na huenda nikaharibu kila kitu, na mdada anaweza piaa kaniruka, ...nikiacha kusema ukweli, ninakabiliwa na kesi ya mauaji, na wakili keshaweka wazi, hataweza kunisaidia,..

‘Ni bora niseme ukweli....’nikajikuta nasema hivyo, na nilipofikia maamuzi hayo mara simu ya wakili ikaita, na wakili akaipokea na kuuliza

‘Wewe ni nani?’ akauliza na kutulia kusikiliza kwa muda bila kusema neno, halafu akasema kwa mshangao

‘Mdada, anataka kuongea na.....unafahamu hilo haruhusiwi muheshimiwa, ni kinyume na utaratibu, nimeaminiwa kwa hilo,siwezi muheshimiwa,...kuhusu nini, ni lazima nifahamu anataka kuongea nini,...mimi ni wakili wake,...’akasema wakili na kugeuka kuniangalia, halafu akasema tena;

‘Ninachotaka kufahamu ni kuwa anataka kuongea nini na mteja wangu...?’ akauliza na kugeuka kuangalia pembeni na baadaye akanisogelea na kusema

‘Hili haliruhusiwi, limefanyika kinyume na utaratibu, wakili wa mdada, anasema mdada anataka kuongea na wewe kwenye simu, lakini mimi nimemkatalia, na akawasiliana na bosi wenu, na bosi wenu kanisisitiza muongee naye tu, sasa ankuuliza...una uhakika unataka kuongea na huyu mdada?’ akaniuliza

Mimi nikabakia kimiya kwa muda halafu nikasema;...........

NB: Haya hiyo ndio sehemu nyingine ya kisa chetu, na naona tunakaribia kwenye hitimisho, je wewe wasemaje

WAZO LA LEO: Nafsi ya mwanadamu ni kichaka kinene chenye giza, ndani ya usiku mnene, huwezi kujua mwenzako ana dhamira gani.Inapifikia kipindi cha kukubali kubeba dhamana ya mwenzako unatakiwa uwe makini, kuna watu wamejikuta wakibeba kesi za waliowadhamini.Cha muhimu ni kufahamu historia ya unyemdhamini,kesi yenyewe, na je wewe una ufahamu wa sheria, kama huna ni bora kuwahusisha wataalamu wa hizo nyanja, kumbuka majuto ni mjukuu huja baada ya kitendo.

Ni mimi: emu-three

No comments :