‘Mdada anataka kuongea na wewe kwa kupitia kwa wakili
wake,...na anataka muongee naye kwa siri, kama alivyoniambia wakili wake, mimi
namwamini sana wakili wake, kwani ni mwalimu wangu, ...sasa kazi ni
kwako,...’akasema na kunikabidhi simu yake, na yeye akatoka na kuniacha peke
yangu, nikaiweka ile simu hewani na kwanza nikasema
‘Mdada unaendeleaje?’ nikauliza huku nikiwa na hamasa ya
kusikia sauti yake, ilikuwa kama vile ni mtu mwenye kiu na maji yake ni sauti
ya huyo mdada.
‘Usiwe na shaka na mimi,...muhimu ni hili ninalotaka
kukuambia, unisikilize kwa makini...’akasema na mimi nikatulia
‘Kwanza hakikisha kuwa upo na mimi,...ninachoongea mimi kiwe
sawa sawa na unachoongea wewe,unanielewa hadi hapo?’ akauliza na mimi nikaguna
hata sikujua niseme nini.
‘Na ili iwe hivyo, uache kabisa kupanua domo lako kupita
kiasi, elewa lugha yangu hiyo, elewa kuwa ukiropoka ovyo, mimi sipo na wewe
tena..., kama ulivyosikia, mimi sina lolote kuhusu hayo mauaji,...sikujijua na
sijui kilitokea nini,...hilo linajulikana sio dhamira yangu, japokuwa sizani
kama mimi ndiye niliyefanya hayo mauaji,....’akasema
‘Nasema sizani, kwani,nisingeliweza kufanya hivyo, halafu
nijipige kitu kichwani kwa nyuma, na kupoteza fahamu,..., dakitari wangu
atathibitisha hilo,na muda wa kilichotokea ni muhimu sana, muda ndio ngao yetu...’akatulia.
‘Sasa wewe ukifungua domo lako na kusema mambo yasiyokuwepo, utajikuta
unaingia matatani, mimi nafikiria sana kuhusu wewe kuliko mimi, ....’akatulia
kidogo.
‘Kinachojulikana ni hivi, huyo mtu alikuja kwangu akitaka
nimlipe pesa zake za gari, wewe hulijui hilo, ....na nilishangaa alipoingia na
wewe akiwa kakuwekea bastola nyuma, sasa sijui kwanini alifanya hivyo, na sijui
kwanini alitaka nimlipie nyumbani na sio kazini kwake, hayo wewe huyajui, hujui
chochote,...unanielewa...?’akatulia
‘Nilikubali kufanya hivyo, kuwa akija nitamlipa pesa yake,
...kama watafutailia maongezi yangu kwenye simu watasikia hivyo, ....sasa kinyume
na nilivyotaajia, kuwa anakuja na mzigo wangu, ambao ni pesa, yeye akaja na
silaha, akiwa kakunyoshea wewe, mimi
nilipoona hivyo ndio hasira zikanishika, nikabadilika,
na kilichotokea baadaye mimi sijui...hapo unaachiwa wewe uwanja wa kuongea....uwe
makini sana hapo’akasema
‘Sasa mimi hapo nitaongea nini, maana ulipobadilika hukuwa na
urafiki na mtu hasa mwanaume, ukaanza kunivamia na mimi,
nikakimbia,...nilipopata fahamu, kwani kuna kitu kilinigonga na kupoteza fahamu
sijui ni nani ...ni wewe ulinigonga?’ nikauliza
‘Hicho kitu nilikipata wapi, unakumbuka nilikuwa na kitu
mkononi, kabla ya hapo...sijui, na sikumbuki kuwa na kitu, ambacho polisi
wanasema ni kitu kama nondo, je uliniona nikiwa na nondo humo ndani,...?’ akauliza
‘Hapana kwa kumbukumbu zangu sikukuona na kitu kama hicho, na
...’nikatulia nikijaribu kukumbuka
‘Ueleze kilichotokea, kwani hukumbuki kulitokea nini,wakati
huo..?’ akaniuliza
‘Ndio hivyo najaribu kukumbuka...’nikasema
‘Sasa sikiliza sema ulivyoona, sio ulivyosikia, au
wanavyotaka watu useme, usilishwe maneno, hapo kila mtu ana dhamira yake, na
huenda wengine wana lengo la kunimaliza,..’akasema
‘Kwanini...?’ nikauliza
‘Kwanini, kwanini...haina haja kwa sasa, cha muhimu hadi
hapo, mimi na wewe hatufahamu kitu, usiongee sana, kuongea kwako sana, kunaweza
kukuponza. Unasikia wanaofahamu zaidi ni mimi na wewe kwasababu ndio
tuliokuwepo humo ndani, sasa wasikudanganye watu useme watakavyo
wao...unanielewa hapo?’ akawa kama anauliza
‘Ndio hivyo nataka niwaambie ukweli, ...’nikasema
‘Ukweli eeh, sema ukweli, usiohatarisha maisha yako ya
baadaye, ukijikanyaga, kitanzi kipo shingoni mwako, mengine ya nyuma, mimi
siyajui, na wewe huyajui, au kuna kitu unafahamu, ambacho mimi sikijua, kama
kipo niambie?’ akauliza na kabla sijajibu akasema
‘Jibu ni kuwa hufahamu chochote au lolote...sawa...sasa
ropoka ukaozee jela, mimi sipo, mimi nina kinga, je wewe unayo, jiulize mara
mbili kabla hujaropoka...’akasema
‘Pili, kama huna wakili mwaminifu useme,mimi naweza
kukutafutia wakili atakayeweza kukulinda, mimi nawafahamu wengi tu, hakikisha
wakili wako sio mbabaishaji wa kukulazimisha kuongea kila kitu hata kama
hakihusiki...umenielewa, usiogope kutishiwa jela, wewe ni mwanaume bwana...’akasema
‘Huyu niliye naye ni wakili anafahamu zaidi yangu ni wajibu
wake kuniambia kipi nimueleze na kipi nisimueleze, na hapa alipo hajui tukio
lilivyokuwa, natakiwa nimueleze ilivyokuwa, ...’nikasema
‘Inategemea....sikiliza usiongee kila kitu, mengine yanahusu
nini, nafahamu kabisa hao watu , wengine lengo lao ni kukuchimba kwanza ili
baadaye aje kukuweka mikononi mwake...mimi nawafahamu sana hao watu, sio kila
kitu unahitajika kuwaambia, utakuja kuumbuka baadaye, ....’akasema
‘Kwahiyo...unataka niseme nini..?’nikauliza na yeye akasema;
‘Una maana gani kuniuliza hilo swali, wewe mjinga kweli,
unataka nikufundishe cha kusema, ..nimeshakuambia uwe makini, usiropoke kila
kitu ambacho ni siri za maisha yako, ambayo usingelipenda kuyaongea, ongea yale
yanayohusiana na hiyo kesi, na kesi iliyopo mbele yetu ni ya mauaji, ni nani
kaua,ulionaje, alikuja kujaje ...mengine hayawahusu, unanielewa..?’ akasema
‘Mhhh...lakini...’nikataka kusema na yeye akasema;
‘Kazi ya muhimu ni kumtafuta huyo aliyemuua huyo jamaa,...kumpata
kabla hawa askari hawajakata tamaa, maana wakikata tamaa, wanaweza kukubambikia
kosa ambalo sio lako,...mimi nina uhakika, huyu mtu aliyefanya hivyo ni mmoja
wa watu wenye nia ya kunimaliza, na mimi natakiwa kumgundua ni nani mapema
iwezekaanvyo,...’akasema
‘Watu gani hao,ina maana kuna watu wanaotaka kukumaliza
kwanini na ni akina nani? Nikamuuliza
‘Hilo halikuhusu, mimi nina wapinzani wengi, wasiotaka
maendeleo yangu, natakiwa nipate muda wa kuwachuja, nitawapata tu,...’akasema
‘Ina maana wewe hukumuona huyo mtu aliyeingia na kufanya hivyo...?’
nikamuuliza
‘Ningemuonaje, siwezi kukumbuka kilichotokea baada ya mimi
kubadilika, I wish ingelikuwa
hivyo,....huyo mtu inawezekana alipoingia, alijua sehemu ya kunipata ni
kunigonga kichwani, akaniwahi, nahisi alinipiga na kitu kizito kisogoni, kama
walivyosema kuwa ni chuma kama nyundo nzito,...nikapoteza fahamu, ...ningemuona
asingeliniweza,...naapa nitampata tu, na nikimpata nitambeba juu kwa juu hadi
kwa hao polisi...’akasema akionyesha hasira, nikaogopa asije akabadilika,
japokuwa sikuwa karibu naye.
‘Mbona polisi wanasema bastola ina alama za vidole vyangu na
vya kwako, na mimi sikumbuki kabisa kuishika hiyo bastola,...?’nikamuuliza.
‘Hapo na mimi ndipo ninapojiuliza, ...huyo mtu alichofanya ni
kuhakikisha kuwa alama za vidole zangu na zako zinabakia kwenye hiyo
bastola,....ni ujanja wa kijinga, kwasababu hata polisi, hawawezi kukubali hilo
kirahisi,...kama kweli mtu alikuwa na nia ya kuua...’akasema
‘Kama ni hivyo kwanini wamenishikilia mimi..?’ nikauliza
‘Huenda ni kwa usalama wako...’akasema
‘Kwa usalama wangu, kwa vipi?’ nikauliza kwa mshangao
‘Huwajui hao watu,...hawafanyi kosa, hukutakiwa uwe hai,
....hata mimi siku zangu zinahesabiwa, kama wataona sina umuhimu nao
tena.....sema na mimi sio mchezo , kama wamenikosa hapo, hawanipati
tena.....’akasema
‘Inaonekana unawafahamu hao watu...?’ nikauliza
‘Ningeliwafahamu ningelishawamaliza....lakini dawa yao
inachemka, iogopi kufa, ila kabla sijafa, nitahakikisha na wao wameonja
kifo..’akasema
‘Mhh, kwahiyo ....wanakata mimi nisote jela, hata kufungwa
kwa kosa nisilolifanya kwanini?’ nikauliza
‘Ndio lengo lao hilo, ili uwe hatiani, ionekane mimi na wewe
ndio tuliofanya hivyo,...sasa ndio maana nakuambia uwe makini na maelezo yako,
mimi nitafanya uchungzi nitamgundua huyo mtu kabla kesi haijaanza, nakuhakikishia
hilo..’akasema
‘Una uhakika gani?’ nikamuuliza
‘Usijali, hiyo kazi kwangu ni ndogo sana, nasubiri kibali cha
hawa watu, maana wananilinda utafikiri mimi ni jambazi, wangelijua
wasingelifanya hivyo ....lakini usimwamushe alieyelala, maana akiamuka mtu kama
huyo, hujui itakuwaje...umenisikia, huyo wakili wako ni nani?’ akaniuliza
‘Yule wakili wetu wa kampuni...’nikamwambia
‘Ohooo, ...yule na kesi ya mauaji wapi na wapi, yeye ni
mtaalamu wa sheria za kazi, na utawala, lakini anyway, labda anataka kupanua wigo wake,....okey ngoja mimi ,nitaongea naye,kama ni huyo, nitajua jinsi gani ya
kumweka sawa ...’akatulia kidogo nahisi alikuwa akiongea na mtu halafu akasema;
‘Cha muhimu, uwe makini na huyo jamaa ni mjanja sana, kwa
watu kama nyie,....umenielewa eeh?’ akauliza na mimi nikaguna halafu yeye
akasema
‘Umenielewa, kama hujaelewa niambie...au una lolote la
kusema?’akasema na mimi nikamuuliza
‘Hii ni kesi ya mauaji, na kwa maelezo yako ni kama wewe
unataka kuvuta muda, bila kujua kuwa mimi nipo rumande na sasa nasubiria
kwenda, gerezani, na hapo ina maana mimi ndiye nitakayepata shida kwa vile wewe
unachukuliwa kuwa hukuwa unajua ni nini kilitokea kutokana na matatizo yako,...’nikasema
‘Kwahiyo wewe unaogopa kwenda jela huogopi kwenda kunyongwa
eeh, juhudi ninayofanya kwa sasa ni kukuokoa wewe na kitanzi, kunyongwa au
kufungwa maisha, hiyo ya kwenda gerezani kwa muda sio tatizo kwa sasa...wewe ni
mwanaume, ukomae, unafikiri maisha ni lele mama eeh, masikini mhasibu...’akasema
kwa sauti ya kunibeza.
‘Mimi hapo sikuelewi, unasema nisiropoke kwa wakili wangu, na
kwa hali hiyo ina maana nitashindwa kumwambia yote ambayo huenda yakamsaidia
katika kazi ya kunitetea mimi,...hapo unaniweka pagumu nashindwa kuelewa ni
nini na kipi nisimwambie, na yeye kama wakili anahitajika kujua kila kitu, ili
ajue jinsi gani ya kunitetea,..au sio?’ nikamuuliza
‘Sikiliza wewe mtu, hakuna kitu kama hicho, kuwa umwambie
wakili wako kila kitu, kwanini umwambie kila kitu, wakati wewe mwenyewe kwa
akili zako unafahamu hiki kinahusiana na hiyo kesi na hiki hakihusiani, je
unamwamini vipi kuwa ataweza kulinda masilahi yako mpaka mwisho, huyo huyo
anaweza kukugeuka baadaye..je yeye na baba yako mkwe hawajuani,...uwe makini.’akasema.
‘Hapo unaniweka pabaya,...mpaka sasa sijajua msimamo wangu ni
upi, na wakili wangu ndiye anayeweza kunisaidia, ...’nikasema
‘Hivi wewe mtu hujanielewa,...cha muhimu ni kuwa makini ,
usiropke ovyo, sina la kukuambia zaidi, akili kichwani kwako, kama unataka
uozee jela, na huku mchumba wako akikusuta na kululaani kwa kumharibia maisha
yake, na hapo hapo baba mkwe wako akitamani asikuone tena katika maisha yake
wewe, ropoka ovyo, ....niamini mimi nitahakikisha upo salama....’akasema na kukata
simu.
Nilikaa kwa muda nikitafakari, huku nikimuwazia huyu mtu, je
ni huyo huyo mdada niliyesikia kuwa yupo mahututi, kwa jinsi alivyokuwa akiongea
hapo haonyeshi kabisa kama alikuwa na hali mbaya.
Baadaye wakili akaja, na kuniangalia kwa muda, halafu
akasema;
‘Nafikiri mdada keshakugeuza mawazo yako maana huyo mdada
namfahamu sana ni mjanja kupita kiasi, lakini hili tatizo lililopo mbele yako,sio
la ujanja-ujanja, ujue hii ni kesi ya mauaji, hauna ujanja wa kuongea
.....ujanja wake ni kuwa na ushahidi utakaokuweka mbali na tukio hilo,...sasa ni
wakati wa kulifikiria hili kwa makini, je utamsikiliza huyo mdada, ambaye kwa
jinsi ninavyomfahamu atakuwa na malengo yake, ujue na yeye ni mshukiwa kwahiyo
hapo alipo, anatafuta njia ya kuitetea nafsi yake...je una uhakika ana uwezi wa
kutetea na nafsi yako?’ akaniuliza.
‘Mimi sijui, na kiukweli mimi simuelewi kabisa
mdada...’nikajikuta nikisema
‘Ndio hivyo,..kwani kakuambia nini?’ akaniuliza na mimi kwa
haraka nikasema;
‘Alichoniambia yeye ....eeh, ni kujaribu kunikumbusha yale
yaliyotokea mle ndani,na yeye akataka kujua ni kitu gani kilitokea baadaye, baada
ya kuanza kuchanganyikiwa, kwani hapo hakumbuki kama unavyomfahamu akichanganyikiwa
anavyokuwa, huwa hawezi kukumbuka ni kitu gani kinatokea kwa muda huo
aliochanganyikiwa...’nikasema.
‘Mhasibu ujue hii ni kesi ya mauaji, sio rahisi kihivyo,
mdada hapo alipo anahangaika kujiokoa, na usizani ataweza kuangalia mstakabali
wake na wako kwa wakati mmojO.Nikuambie ukweli, yeye hapo alipo hajijui hatima
yake itakuwaje,kuwa hivyo kuwa ana matatizo ya akili sio tija, kunahitajika
ushahidi wa hali ya juu, ili aweze kujiokoa, na kukubalika kwa hakimu...sijui
kama unaliona hilo kwa mapana yake, au unafikiri hii ni kesi ndogo ndogo
tu,...’akasema
‘Naliona hivyo,...na ninaogopa kweli, lakini unataka mimi
niseme nini, nikiri kosa ambalo sijalifanya, au unataka niseme nini, hebu
niambie maana labda mimi nashindwa jinsi ya kujielezea...’nikasema huku moyoni
nikishauri nifanye nini, kwani kama alivyosema mdada, nikiropoka, huenda aibu
yangu yote itajulikana, na nikajikuta kwenye kesi nyingine ya mambo ya mdada...na
sijui ana mambo gani zaidi.
‘Sawa ngoja mimi niongee na bosi wako, maana alikuwa
anasubiria nitoe jibu langu kuwa nitakusimamia au la....’akasema na mara simu
yake ikaita na kuipokea hapo hapo
‘Ni nani mwenzangu?’ akauliza
‘Mdada...!?’ akauliza kwa mshangao halafu akasema
‘Mdada unataka nini kwangu...una wakili wako au sio?’
akauliza na kuanza kusikiliza alionyesha kutokufurahishwa na hicho anachoongea
mdada,lakini kila akitaka kuongea kitu mdada hakuwa akimpa nafasi, na mwisho
wake akauliza;
‘Kwahiyo unataka mimi nifanye nini?’ akauliza na kusikiliza kwa
muda na baadaye akageuka kuniangalia , halafu akasema;
‘Nitaongea na bosi wake, na yeye atajua la kufanya lakini
mimi siwezi kufanya hayo unayotaka wewe, mimi ni mwanasheria nafahamu kazi
yangu ni nini, huwezi kuniamurisha nifanye unavyotaka wewe...nisikilize mdada,
kuongea sana hakusaidii..eti nini,...nilishakukanya kuhusu hilo..kumbuka kesi
mlio nayo, sio ndogo, ni kesi ya mauaji,....sikuelewi...na huwezi kunitisha kwa
hilo....’akakata simu kwa hasira.
‘Huyu binti vipi,..mbona simuelewi...’akasema
‘Kwani vipi tena?’ nikauliza
‘Ukicheza na hii kesi wewe utaozea jela,...utafungwa, na
huenda kikawa kifungo cha maisha mwenzako sijui anataka nini...mimi sijamuelewa
hadi hapo, lengo lake hasa ni nini...’akasema huku akifunga funga vitu vyake
‘Sa-sa—sa, mbona unaondoka?’ nikauliza
‘Mdada kasema atakutafutia wakili mwingine...mimi naona bora
iwe hivyo, kwa hali kama hii, sitawaweza kukusaidia, maana wewe mwenyewe hutaki
kuniambia ukweli,....na sasa huyu mdada analeta mambo mengine, nyie watu,
siwaelewi, hamjuia kuwa kesi hiyo ni mbaya sana, ni kesi ya mauaji,...okey, mimi nitawasiliana na bosi wako,
nione tutafanya nini, ...’akasema na kuanza kuondoka.
‘Tafadhali, usimsikilize mdada, wewe ndiye tegemeo langu, ukiondoka
mimi nitafanya nini...’nikaanza kulalamika
‘Mtajua wenyewe....siwezi kuzalilika kwasababu ya watu
wasiojitambua, na huyo binti, anataka kunichezea, nilishamkanya kuhusu mambo
yake, anafikiri mimi siwezi kumfanya lolote eehe..huo mchezo wake utamtokea
puani, nahisi sasa huko anapokwenda ni kubaya...’akasema huku akiondoka,
akionekana kukereka sana.
Nilibakia pale nimetulia nikijiuliza ni nini hatima yangu,
maana sasa kesi yote imaniangukia mimi, na sijui kweli mdada anaweza
kunisaidia, na hata akimtafuta wakili ni nani atamlipa, ni mdada...kwanini
afanye hivyo...
Na wakati naendelea kuwaza mara yule wakili wa kampuni akarudi, na kuniangalia kwa muda kabla ya
kusema neno, baadae akasema
‘Ongea na bosi wako...’akasema akinikabidhi simu.
NB: Haya wapendwa kwa leo ndio hayooooh
WAZO
LA LEO: Matendo ni dhamira ya kweli, kuliko maneno ya kupendeza.
Wengi hujiona wanajua sana, kwa vile wanajua kuutumia mdomo wao, kwa kuongea
sana, lakini kwenye matendo yao inakuwa ni kinyume. Huku ni kudanganyana,
matendo yako mema ndio ushahidi wa kweli.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment