Niliposikia bosi anataka kuongea na mimi nikaanza kuhisi
owoga fulani, na moyoni nikawa nikijilaumu, kwanini nakuwa mwepesi sana
kumkubalia mdada, hata kaam naona ni kujiweka kwenye matatizo.
Nilijua bosi anaweza akakata tamaa ya kunisaidia na huenda
asiniamini tena, na kwa mtaji huo, huenda hata kibarua hakipo tena, kwani bosi
kajitahidi kunitafutia wakili, lakini sikuweza kutoa ushirikiano,na kesi
yenyewe ni mauaji, huenda ikachukua muda
Kwa mkono wenye kusita,nikaipokea ile simu kutoka kwa wakili,
halafu nikaiweka hewani, nikaanza kwa kusema;
‘Habari za saizi bosi...’nikasalimia nikionyesha kuchoka na
kukata tamaa.
‘Habari nzuri kiasi, mtoto wangu anaumwa, imebidi nimuhangaike
kwenye hospitali kubwa, huko mjini, bado nipo huku mjini huenda nikarudi kesho au keshokutwa,
ndio maana ukaniona nipo kimiya....’akasema
‘Hkuna shida bosi...nakuamini sana huwezi kunitupa...’nikasema
‘Ndio maana sijaweza kuja kukuona, lakini hata hivyo,
niliacha maagizo yote kwa wakili wetu huyo, nikijua ataweza kukusaidia ili
kwanza upate dhamana, ambayo ni muhimu kwa afya yako, unafahamu huko gerezani
kulivyo, ...lakini pia ni kuangalia jinsi gani kesi ilivyo, kupata ukweli wote,
ili aweze kukutetea,...’akatulia kidogo
‘Lakini cha ajabu nashangaa kusikia wakili akisema hutaki
kutoa ushirikiano, akama anavyokuuliza, hebu niambie tatizo lipo wapi?’
akaniuliza
‘Bosi mimi nimejitahidi kumuelezea jinsi ilivyokuwa, lakini
naona kama haniamini, na mimi sijasema jambo la kuonyesha kuwa sitoi
ushirikiano, nikijua kuwa mimi ndiye nahitaji msaada...mimi sijui anataka
nimwambia nini zaidi....’nikasema
‘Yeye kama wakili anahitajia kufahamu kila kitu, ili aweze
kujua ni jinsi gani ya kuiingilia hiyo kesi,hasa chanzo cha hayo yote, anahisi
huenda unafahamu mengi, lakini unaogopa kusema,...kajaribu kukuuliza baadhi ya
maswali anayohisi huenda yana chachizo la hayo mauaji, lakini hutaki
kumuelezea, sasa atawezaje kukusaidia vipi kwa hali kama hiyo...?’ akauliza
‘Bosi mimi ndiye niliyekuwepo humo ndani,japokuwa sikuona
jinsi gani huyo muuaji alivyompiga risasi marehemu, na nimemuelezea yote hayo,
lakini yeye anang’ang’ania nimuelezea mahusiano yangu na mdada, kama nina kazi niliwahi
kufanya naye....yaani anayoniuliza ni mbali kabisa na tukio lenyewe, nahisi ana
ajenda ya siri na mdada....’nikasema
‘Unahisi ana ajenda gani ya siri na mdada!?’ akauliza
akionyesha mshangao
‘Nihisia tu, kwa jinsi anavyouliza maswali yake, nahisi, kuwa
pengine wanamsuguano yeye na mdada, na huenda wakili huyu anataka kunitumia
mimi kufahamu mengi kuhusu mdada, kitu ambacho mimi sijui, siwezi kujua kila
kitu kumhusu mdada, na kwanini aniulize maswali mengi kuhusu mdada, kwani yeye
ndiye muhusika mkuu...?’ nikauliza
‘Wewe na mdada ndio wahusika wakuu ndio, ndio maana polisi
wamewashika nyie, kwahiyo ni muhumu kuwafahamu, nyendo, na tabia zenu, huenda
katika mahusiani yenu kuna kitu mnakifahamu kinachoweza kuufichua
ukweli...kwanini uogope kusema kile anachokuuliza...’akasema
‘Sijaogopa, nisichopenda ni jinsi anavyonitaka niongee kila
kitu, ....mengine naona ni mambo binafsi...’nikasema
‘Kila wakili ana njia yake ya kuliingilia tatizo, huenda yeye
kaona njia iliyorahisi ni kupitia kwa mdada, kumfahamu , ili ajue ni kwanini
huyo marehemu alifika hapo, kwanini aje na bastola,...hata mimi hapo naona kuna
hoja...’akasema
‘Ndio maana nikamuuliza anijulishe ni kipi ni muhimu kwa
ajili hii kesi, kama ni hivyo, basi nitamuambia yale ninayoyafahamu kuhusu
mdada, na siwezi kumuambia yale nisiyoyafahamu, ....’nikasema
‘Nikuulize kwanini mdada anataka kukutafutia yeye wakili?’
akaniuliza
‘Mhh, yeye anasema kwa vile hilo tukio limetokea wakati tupo
tunamsaidia, na yeye anataka kulipa fadhila kuhakikisha haki inatendeka, ndio
akaona anitafutie wakili mzoefu wa mambo hayo,...nilishamkatalia,..lakini
akasisitiza kufanya kutaka kufanya hivyo...mimi ningefanyaje..’nikasema
‘Kwa hali hiyo, basi mimi itabidi nimtoe wakili wetu, ..sioni
haja ya kugonganisha watu, mimi namuamini sana huyo wakili wetu, kwa sababu
pamoja na mengine ni mtu anayejua kutunza siri, nimefanya kazi naye kwa muda
mrefu, na hutaamini, hajawahi kuniangusha...’akasema
‘Yeye ni wakili wa maswala ya kazi na sheria za kazi, au sio
..na...’akanikatiza
‘Na hapo ndio maana nakuambia huyu mtu ni msiri sana,
keshawahi kufanya kazi za kesi hizo za mauaji, na hakuna kesi aliyowahi
kushindwa, kwasababu msimamo wake, ni kujua ukweli wa tukio, na akishalijua
anakushauri kuwa kesi hii ipoje, na inawezekana kutetewa vipi....hachukui kesi
kwa kutafuta pesa tu, lakini pia analinda heshima ya kazi yake...’akasema
‘Ina maana pia ana utaalamu wa kesi za mauji?’ nikauliza
‘Ndio kitu alichosomea awali, lakini kwa vile alitaka
kumrizisha mzazi wake, akaacha hicho alichosomea na kujikita kwenye mambo ya
sheria za kazi...lakini kesi za mauaji ndiyo fani yake...’akasema
‘Oh, mimi nilikuwa sijui, hata mdada halijui hilo ndio maana
akataka kumtafuta mtu aliyebobea kwenye fani hiyo, ya kesi za mauaji..’nikasema
‘Mdada ana ajenda yake ya siri,...nimejaribu kumpigia simu, lakini
kazima simu yake, nahisi hataki kuongea na mtu,...sasa uamuzi ni wa kwako, je
unamataka wakili huyu, au unasubiria wakili wa mdada...nakuachia wewe hiyo kazi
hadi kesho, .....’akasema
‘Sasa bosi ukisema hivyo unaniacha kubaya kwani, mpaka sasa
wakili ninayemfahamu ni huyu uliyenisaidia, nijuavyo mimi, mdada alitoa hilo kama
ombi tu la kunisaidia akijua kuwa huenda wakili wetu huyu hana uzoefu wa kesi
kama hizi za mauaji. Mimi naona leo akinipigia simu nitamuhakikishia kuwa huyu
wakili wetu anaweza kunisimamia bila matatizo, nafikiri atatuelewa...’nikasema
‘Hilo nakuachia wewe....na sijui kama mdada anajua hayo zaidi
yangu, msijidanganye,...kumbuka hiyo ni kesi ya mauaji, sio mchezo wa kuigiza,
utakuja kujuta siku ukisikia unahukumiwa kifungo cha maisha kama sio
kunyongwa,....’akasema bosi na kunifanya moyo unilipuke
‘Bosi usiseme hivyo, kweli naogopa sana, nakutegemea sana
wewe bosi...’nikasema
‘Haya wewe nipo huyo wakili niongee naye.....’ akasema na
mimi nikagonga meza kumpa ishara wakili huko nje alipo kuwa aje, na haikuchukua
muda akaingia na kuuliza
‘Vipo umemaliza kuongea na bosi wako?’ akaniuliza
‘Bosi anataka kuongea na wewe...’nikasema na kumkabidhi simu,
akaishika na kuiweka sikioni, halafu akasema
‘Mbona hayupo hewani,...’akasema na kuanza kumpigia, lakini
ilionekana kama simu ya bosi haipatikani , akajaribu tena na tena, lakini
haikupatikana
‘Inaonekana simu yake imekwisha chaji, sasa, kwa hali ilivyo,
mimi nitaondoka, na kesho nitawasikiliza nyie, vinginevyo, nitajua kuwa
sihusiku katika kuisimamia hii kesi, nijipange kwa ammbo mengine...’akasema
‘Tumeongea na bosi wewe ndiye utasimamia hii kesi yangu...’nikasema
‘Ni hapo utakapokubali kuniambia ukweli wote...’akasema
‘Nitakuambia, ukweli kuhusiana na tukio zima, na sijui kuna
kitu gani sijakuambia, labda tuende kwa mtindo wa maswali, ili niweze kukumbuka
zaidi...’nikasema
‘Vyote ni sawa, cha muhimu ni kuhakikisha unaongea ukweli
wote, na mimi nilitaka kuanzia kwenye mahusiano yako na mdada, kwani tukio
lilivyo, inaonekana marehemu alikuja kwa nia ya kukutana na mdada,
kwanin...kuna nini kilikuwa kinaendelea, je wewe unahusikana vipi na mdada, unafahamu lolote..ndio
lengo langu...’akasema.
‘Kama ni hivyo mbona nimeshakujibu, ....’nikasema
‘Hayo tutayaona kesho, sasa nakwenda kuonana na watu wangu,
najua wameshapata taarifa za kutosha kutoka huko polisi, na asubuhi nitadamkia
kukupigania, upate dhamana, hilo ni muhimu sana, vinginevyo watakupeleka
gerezani, na huko sio kuzuri sana...’akasema
‘Naomba tafadhali jitahidi kufanya hivyo,..’nikasema
‘Yote inategemea wewe, kuna jamaa yenu mmoja wa pale ofisini,
kulitokea wizi nilimwambia hivyo hivyo, aniambie ukweli, kuhusu anavyowafahamu
hao watu anaofanya kazi nao,...yeye kwa ujumla alikuwa hahusiki, lakini kwa
vile alikuwa kitengo hicho na siku hiyo alikuwa zamu, akajikuta anaunganishwa
kwenye hiyo kesi,...
‘Nilimshauri sana, kuwa ili niweze kuimaliza hiyo kesi ni
muhimu nifahamu nyendo na tabia za watu anaofanya kazi nao, maana wizi, mauaji,
hayaji kwa bahati mbaya, mara nyingi ni vitu vya kujipanga, ...labda iwe ni
ajali tu...akajifanya hafahamu, kumbe anafahamu
‘Hapa na hapa akajikuta yupo gerezani, alikaa wiki mbili,
alipotoka hutaamini, alikuwa kaisha, na wiki moja baadaye akaanza kukohoa,
kifua kikuu kikamuandama, ...huyo jamaa alikwenda kuponea kwao, ....ilikuwa
akribu tumzike...sasa nikuambie ukweli, gerezani sio kuzuri, ...’akasema
‘Tfadhali nakuomba sana, nisaidie, nisiende huko...’nikasema
huku nataka kupiga magoti
‘Yote inategemea wewe, ninachotaka kutoka kwako, ni kuniambia
ukweli kuhusu mdada, nyendo na tabia zake, pili kuhusu marehemu, na tatu, wewe
ulikuja vipi ukawa karibu na mdada....na tukio la siku hiyo itakuwa ni
kumalizia tu....ni kazi rahisi je upo tayari...?’ akaniuliza na kabla sijamjibu
simu yake ikaita, na kwa haraka akaipokea
‘Nani mwenzangu?’ akauliza
‘Mdada, unataka nini tena?’ akauliza na akawa anasikiliza kwa
muda, bila kusema neo na baadaye akageuka kuniangalia na kusema;
‘Mdada anasema keshampata wakili ambaye ataweza kusimamia
kesi yako, na anakuja kesho asubuhi kuonana na wewe.....’akaniambia
‘Lakini....’nikaanza kusema
‘Sikiliza nikushauri kitu, nafahamu hali uliyo nayo kwa sasa,
sasa nakushauri hivi,wewe usikatae moja kwa moja ....., kesho akija huyo wakili
aliyemtafuta mdada, kwanza jifanye kama unamkubali, uone anataka kukuhoji nini,
...uwe na akili ya haraka ya kutafakari...’akasema na kunifanya nimwangalia
moja wa moja usoni.
‘Uwe makini sana na maswali yake, na akimaliza mwambie
unahitajia muda wa kufikiria, nikija mimi utaniambia ni kitu gani kakuhoji,
nitajua lengo lao ni nini, sasa hapo na mimi nitakushauri je uendelee naye au
vipi,....’akasema
‘Lakini kwanza nataka kufahamu je wewe kweli upo tayari
kunisimamia kwenye hii kesi?’ nikamuuliza huku nikimwangalia kwa makini na yeye
akiwa haonyeshi dalili yoyote usoni, akasema;
‘Mpaka nisikie na kujua ukweli wote, kama nilivyokuambia,....
kwa hivi sasa siwezi kukupa jibu la moja kwa moja, kwani nimeshaanza kuingiwa
na wasiwasi na jinsi gani unavyonificha mambo muhimu...nahisi kuna kitu
unaficha, ambacho kinahusiana na hayo mauaji, na hiyo ni hatari sana kwako...’akasema
‘Sio kweli, ...sikufichi kitu muheshimiwa, ....mengine unayoniuliza
ni mambo yangu binafsi,ambayo sio lazima na nina uhakika hayahusiani na hii
kesi..’nikasema
‘Na kama ni mambo binafsi,na yana mahusiano na mdada, nahisi,
huenda ndio chanzo cha hayo mauaji, ...’akasema
‘Kwanini unasema hivyo...?’ nikauliza kwa mshangao.
‘Mdada ni mtata sana...nimeshakuambia mimi namfahamu sana, hata
hivyo ni binti mjanja sana, anafahamu kuuma na kupilizia...na huwa hafanyi
jambo bila malengo, na faida,...sijui kwa hili alikuwa na malengo gani....’akasema
‘Maisha ya mdada, au maisha yangu binafsi, yanaingilianaje na
hayo mauaji, mimi ina uhakika hayahusu kabisa hayo mauaji,...niamni hivyo....’nikasema
‘Wewe unasema kwa kukwepa jambo, lakini mimi nikifahamu hayo
ninayokuuliza,nitaweza kujua undani wa hili jambo,ninahisi kuna kitu
kilichosababisha hayo mauaji, na hayo mauaji hayakutokea kwa bahati mbaya, kuna
sababu kubwa iliyofikia hapo, ....nakuambia hili kwa manufaa yako, namfahamu
sana mdada, nahisi kuna kitu anataka kisijulikane, ....kwahiyo mimi naondoka,
nasubiri maamuzi yako , hiyo kesho...’akasema na kuanza kuondoka na baadaye
akakumbuka jambo na kusema;
‘Ukumbuke pia polisi wa upepelezi anataka kukuona hiyo
kesho....’akasema na kunifanya nizidi kuishiwa nguvu.
`Mhhhh...’ nilipumua kwa muda nikijinyosha, na hatimaye
nikaingia kwenye chumba cha mahabusu, na nilivyokuwa nimechoka, nikashikwa na
usingizi mzito,....na asubuhi iliingia kama mchezo, na askari akaja na kusema;
‘Kuna mgeni wako....’nikajua ni huyo wakili wa mdada
NB: Je wakili yupi ataweza kunitetea
WAZO
LA HEKIMA: Maamuzi ya hekima ni yale yanayolenga ukweli na haki, pia
busara na hekima ya kulitatua hilo jambo. Siku hizi, ushabiki, ubinafsi , na
masilahi ndio unaotawala maamuzi ya watu hata katika sehemu nyeti, ambazo
zinahitajia utaalamu wa hali ya juu. Tuwe makini na hili, kwani unachofanya
leo, ujue kinaweza kuathiri mustakabali wa kizazi hadi kizazi, na historia
itakuja kukuhukumu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment