Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, February 17, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-13‘Natumai mumekuja na taarifa kamili, kama nilivyowaagiza,  kuhusiana na upotevu wa stakabadhi za malipo, na kwanini hundi za malipo ziliandikwa bila ukamlifu wake, hadi benki wakazikataa...’akaanza bosi, nikamwangalia mdada, ambaye alionekana hana wasiwasi kabisa.

‘Nataka niliweke hili wazi, kuwa baada ya makosa ya nyuma ambayo yalileta hasara kwenye kampuni na hata wateja kujenga picha mbaya dhidi ya kampuni, kwasababu ya udanganyifu wa baadhi ya wafanyakazi, waliokuwa sio waaminifu, nimeamua kuweka taratibu mpya za malipo, ambazo hazitaruhusu hundi kupita benki mpaka benki wawasiliane na mimi, na hni hiyo ni lazima iwe na viambatishi maalumu, mlipwaji anahitaji kuwa navyo..’akasema

‘Kwahiyo kama mlivyoona, hundi zingine zote zilipita, lakini hizo hundi mbili zikawa na walakini, mlipwaji hakupeleka hivyo viambatishi, pili hata nilipouliza habari zao hao wateja, walionekana ni kama kampuni hewa, na mimi kwa kumbukumbu zangu sina taarifa za mikataba yao, huenda ni hawa wa karibuni kutokana na huo mzigo mpya, ndio maana nataka maelezo kutokwa kwenu, kabla sijaruhusu hizo hundi zipite benki...’akasema.

Bosi akageuka kuniangalia mimi, halafu akamwangalia mdada, mdada, alikuwa kama hayupo, hakuwa anaangaliana na bosi, alikuwa kaangalia nje, kwa kutizama dirishani, naona bosi anamfahamu tabia yake, hakumsemesha akasema;

‘Niliwaambia toka awali kuwa tushirikiane kuhakikisha kuwa kampuni hii inaendeshwa kwa haki na ukweli, na taratibu zote za kikazi ziwe zinafuatwa...taratibu hizo sio kwa hapa tu, ukienda kwenye kampuni yoyote, hizo taratibu utazikuta...sasa nashangaa inakuwa kama vile hatujui ni nini tulichokisoma....’akageuka kumwangalia mdada.

‘Mdada, wewe ndiye umepewa jukumu la uofisa utawala, nilitarajia sana wewe uwe karibu sana na mimi katika maswala ya utendaji, na usimamizi wa mambo ya kampuni...haya matatizo tusingeyaongea hapa sasa kama wewe ungelifanya kazi yako vyema,....sawa labda kuna wateja wapya, waliofika kwako, ulitakiwa utoe taarifa hiyo idara ya masoko,nimewauliza idara ya masoko wanasema hawana taarifa ya wateja wapya...ni wateja gani hao, utuambie...’akasema bosi, na kunigeukia mimi.

‘Na wewe mhasibu, mimi nilikuwa nakutegemea sana, katika mambo ya malipo, wewe unafahamu ni nini kifanyike kabla hundi haijaandikwa, ...sio kwasababu tuna pesa bila kila anayedai analipwa, siku ile nilisema tuwalipe wanaotudai, ulielewa nina maana gani, ...wewe kama mhasibu ulitakiwa kusimamia hilo...haya niambie hao wateja ulikuwa na kumbukumbu zao, viambatishi vyao sijui utaniambia nini, ...’akasema na kuniangalia.

‘Sasa nataka mniambie ukweli kuhusu hao wateja, na kwanini stakabadhi zao, zikapotea, ni nani kazichukua...’akaniangalia na kumwangalia mdada.

‘Bosi mimi nina uhakika kuna mtu kazichukua, na kuhusu hao wateja ni nani, nafikiri mdada atanisaidia kwa hilo, ..nakiri nilifanya makosa ya kumwamini mdada moja kwa moja, nikijua kuwa kila kitu kipo sawasawa, nakiri hilo kosa, na nahitajika kuwa makini ...’nikasema na bosi akamwangalia mdada, ambaye alikuwa kama hayupo, hajali, hana wasiwasi, na alipotuona sote tunamwangalia akasema mdada akasema;.

‘Hao wateja ni kweli ni wateja wapya, na nilijua kuwa mhasibu anawafahamu, kwasababu kumbukumbu zake , viambatishi vyote vilikuwepo,...nawashangaa hao watu wa idara ya masoko,wanakataa bure, nilishawaambia kuwa kuna wateja wapya ambao watasaidia kuhakikisha hiyo mizigo mipya inafikishwa sehemu husika kwa wakati, nikaongea nao nikakubaliana nao....sasa naona kama wanakwepa majukumu, kwa vile tu, hili limetokea,...’akajitetea mdada.

‘Kwahiyo baada ya tukio hili, wewe ukaamua kuchukua kumbukumbu zao...?’ akauliza bosi.

‘Ndio ilibidi nizichukue nizirudishe kwa wenyewe, ili wazilete upya kwa jinsi unavyotaka wewe, kwani kama nilifanya vile inavyoonekana ni sahihi, na umeona sio sahihi, kwanini nyaraak za watu ziendelee kuwepo ofisini...’akasema mdada kwa nyodo kama anaongea na mwenzake tu.

‘Kwanini sasa hukusema awali, maana nimeuliza mara mbili hizo kumbukumbu zao zipo wapi, mpaka nikawapa muda wa kwenda kuzitafuta,sikuelewi mdada, ....?’ akauliza bosi kwa hasira.

‘Bosi wiki mbili hizi nimekuwa na mambo mengi yaliyonichanga kichwa, kuna kazi nyingi zipo mbele yangu, nina matatizo mengo ya kifamilia, kama nilivyokuelezea,...mimi nilipotimiza wajibu wangu, nilijua mhasibu naye atafanya kazi yake, ..kamaa kulikuwa na makosa angeniuliza, hakuniuliza akaandika hundi,....na ilipotokea hilo, kwa haraka ili nisiwakwaze hao wateja, nilichukua hizo kumbukumbu kwenda kuongea nao, ....’akasema

Bosi akataka kumuuliza swali jingine akasita, akaniangalia mimi, halafu akashusha ile hasira aliyokuwa nayo na kusema;

‘Kwahiyo hizo kumbukumbu unazo, ...baada ya kuwapelekea na kurekebisha walikupa kumbukumbu nyingine, au ni zile zile, nilitaka nizione...?’ akauliza bosi.

‘Nimesema nimeshawapelekea wahusika, na kuwaarifu kuwa wafuate utaratibu unaotambulikana na wewe, wao walikuwa hawaujui huo utaratibu wako, kwahiyo watazileta kwa jinsi nilivyowaelekeza...watakuja kwako moja kwa moja..’akasema mdada mdada kwa sauti kama ya kukasirika.

‘Mdada uwe makini na kazi zako, kwa jinsi unavyotenda, nakuona kama haupo na sisi, unaposema taratibu zangu, kama ninavyotaka mimi, ..huo usemi unaonyesha kama ahupo hapa, kwani nilishawaelezea, na tukaanza kufanya hivyo,...pili kwanini uwakubalia  kiasi hiho kikubwa cha pesa, wakati kazi hawajaimaliza,ilikuwa jukumu lako kuwaulizia, au hiyo kazi huiweze niwape watu wengine, kama umezidiwa na kazi useme ...’akasema bosi.

‘Sijasema siwezi kuzifanya hizp kazi...na maswala ya kawaida yaliyonikwanza, ...’akasema na kutulia.

‘Hebu nikuulize hao wateja walifanya kazi gani, na kwanini majina yao hayapo wazi,mikataba haipo, mikataba ni jukumu lako, ndio maana nasema hiyo kazi tuwape watu wa masoko, ulidai kwa vile uliisomea utaifanya, naona majukumu kwako yamekuwa mengi, utawala na kusaidia kazi za masoko hutaweza.....’akasema bosi.

‘Bosi mim naomba niwafuatilie hao watu, kila kitu kitajieleza pindi wakileta kumbukumbu zao, ni nini walichokifanya , na wamefikia wapi, hayo watajieleza wenyewe, mimi kazi haijanishinda, ni kazi ndogo sana hiyo, ni kwa vile sikupata msaada wa akribu kutoka kwa wenzangu, ndio maana lawama zote zinaangukia kwangu....’akasema mdada kwa sauti ya kukereka.

‘Lakini ni kweli kuwa ulikwenda kinyume na utaratibu wetu wa kiofisi, kwa vile wewe uliona ha wateja ni muhimu sana, ukakimbilia kuwalipa, sijui labda kwa vile mizigo hiyo ilitakiwa kufika mahali fulani kwa haraka, hata hivyo, bado, ulikuwa na nafasi ya kuongea na wenzako, au kuniambia mimi, hilo ni kosa na unahitajika kukiri, ni sawa si sawa...?’ akauliza bosi.

‘Mimi sioni kosa langu lipo wapi hapo, ilitakiwa mhasibu baada ya kuona kuwa kumbukumbu hizo hazipo sawa, anirejeshee, ili niweze kumpa maelezo, au nifuatilie, ....unakumbuka nilitakiwa kuzileta hizo kumbukumbu haraka kwa vile ulikuwa unataka kusafiri, na kama nilivyojieleza, nilikuwa nimetingwa na mambo binafsi, kwahiyo nilichofanya nikuchukua bahasha yenye kumbukumbu za maombi ya malipo, na kuzifikisha kwa mhasibu,...’akasema akiniangalia.

Bosi akatikisa kichwa kama kusikitika, halafu akanigeukia na kuniangalia, akasema;

‘Mhasibu nafahamu mwisho wa siku lawama zote zitaelekezwa kwako, ...ni kweli kwa swala la malipo wewe ulitakiwa uhakikishe kuwa vimbatishi vyote vipo, hakuna swala la kumuamini mtu hapo, ...ninaweza kukutetea, maana bado hujawa na uzoefu wa kutosha wa taratibu za hii kampuni,...lakini hizi ni za kawaida popote, na hata vyuoni vimefundishwa,..sasa lawama zinakuangukia wewe, kama alivyodai mdada,...’akaniambia lakini bado akamgeukia mdada.

‘Mdada, mimi badi nipo na wewe, je mikataba ya hao watu ipo, maana hiyo tunakuwa na nakala yake, unaweza kunipatia mikataba yao...au uliamua kuwalipa kwanza halafu ndio make, mjadili, sijui huo ni utaratibu wa wapi,...nikuambia ukweli, makosa yote yametokana na wewe, kwani kama wewe ungetimiza wajibu wako vyema haya yasingelitokea, ...’akasema bosi.

‘Mimi sioni kosa langu bosi,...na hata tukilaumiana kosa limeshatokea, cha muhimu, ni kurekebisha hayo makosa, sio kunilaumu, haya umenilaumu, nio kusema hilo kosa litajisahihisha, na isionekane kulikuwa na kosa, hilo limefanyika, kila mmoja keshajirudi,...’akasema mdada akionyesha kukereka zaidi, ni kama hakutaka kuulizwa.

‘Tuchukulie mfano kama hundi hizo zingepita, na hao walipwaji wakaja kugundulikana kuwa sio sahihi, tungelisema nini, hizo gharama ungezibeba wewe...ndio maana nataka kila mtu ajione, na aone uzembe wake, ili hili kosa lisirejewe tena, ....’akasema bosi na mimi nikaitikia kwa kichwa.

‘Mimi nilishahisi kuwa kuna malipo bandia yametengenezwa, ...na bado nafuatilia, kama nikigundua kuwa hilo lipo, sitasita kuwachukulia wote wanaohusika hatua za kisheria, wewe mdada, na mhasibu mtawajibika kwa hilo...’akasema bosi akimwangalia mdada, halafu akaniangalia mimi.

Mdada akageuka pembeni akiwa kakunja uso, hakusema neno, na bosi akasema;

‘Ok, hilo tumeelewana, lakini kuna hundi hii ya mwisho iliyolipwa bila hata nakala moja ya stakabadhi,..hebu niambieni, hilo nalo lilikuwaje...nimewaambia benki hiyo hundi wairejeshe kwetu, nataka kuiangalia mwenyewe, ilikuwaje, mhasibu...?’ akauliza bosi na mimi kabla sijafungua mdomo mdada akasema

‘Hao wateja wapya walitaka kianzio, na walisema hawataweza kuendelea na kazi bila kupata chochote, nikaona ni bora nichukue hizo pesa, nikawape,....walikuwa wakinikera sana kwenye simu, nikamwambia mhasibu, ...yeye alikuwa na kazi zake, hakulichukulia umuhimu, ...’akasema mdada.

‘Ninachojiuliza wewe uliipataje hiyo hundi, na kwanini ukaiandika wewe , na sio mhasibu, toka lini ukafanaya hiyo kazi, ndio kuna dharura, ninaweza kutoa kibali uandike, ...na hapo ni mpaka upate kibali kutoka kwangu, ...na hiyo ni dharura kama mhasibu hayupo...je mhasibu alikuwa kaenda wapi...?’ akauliza bosi.

‘Muulize mhasibu mwenyewe ,yeye alikataa, hilo lisifanyike, na akaniambia kama mimi ninaweza kulithibitisha hilo, niongee na wewe, hivi kulikuwa na haja gani ya kuwepo na hizo hundi, si kwamba kukitokea malipo ambayo ni muhimu, tuzitumie, ...ndivyo nilivyofanya,... mimi kwa vile nafahamu umhimu wa hao watu nikaamua nichukue hiyo stakabadhi niandike mwenyewe....’akasema mdada.

‘Hilo ni kosa jingine umefanya mdada, unachukua maamuzi, bika kibali cha mdhamana wa majukumu hayo, ...mimi mwenyewe,siwezi kuja kwa mhasibu na kuchukua kitabu cha hundi, na kujiandikia mwenyewe hata siku moja, hilo ni kosa kubwa sana la kiutendaji....’akasema bosi.

‘Kwanini ulimdharau mhasibu kwenye majukumu yake..., huyu ndiye tumempa majukumu hayo, na anawajibika kwa hilo,..hilo ni kosa kwa wote wawili...ninaliweka kwenye kumbukumbu zangu, na nitatoa onyo kali kwa maandidshi...’akasema akiniangalia.

‘Hiyo hundi kama imerejeshwa, mkabidhi mhasibu , haitalipwa tena,mpaka nione kumbukumbu za hao watu, na mikataba yao...’akasema bosi.

‘Sawa bosi, ...’nikasema

‘Na muelewe hilo nalifanyia kazi, maana sijapata taarifa iliykamilika, ...mnaweza kwenda,..’akasema na mdada alikuwa wa kwanza kuondoka akiwa kakasirika, na mimi nikamfuataia nyuma, bosi akasema;

‘Mhasibu baadaye nataka kukuona.....’akasema na sisi tukatoka chumba cha bosi, huku siamini kuwa hayo yamepita kwa amani, moyoni nikaapa kuwa sitafanya hayo makosa tena.

 Tulipofika ofisini kwangu, mdada akapiga ngumi ukutani na kusema;

‘Ssshit, sasa huu ni ujinga mtupu......haya yote umeharibu wewe...huyu bosi wako anajifanya hii kampuni ni yake peke yake, hajijui....’akageuka na kuniangalia.

‘Na wewe zumbuekuku, unaona ulivyoharibu, kama nisingeliingilia kati ungeropoka ovyo..huna maana kabisa...’akasema akiniangalia kwa hasira

‘Nimeharibu nini mimi, wakati yote umeyatunga wewe mwenyewe, unafanya mambo ya kitoto, huoni kuwa hayo hayapo na hukustahili kuyafanya, unaniharibia kazi yangu....’nikasema

‘Ni kuambia wewe mwanaume, utakufa masikini,...ukiendelee kufanya hivyo, utabakia kusindikiza wenzako, utaona wenzako wanajenga, wana magari, wana miradi wewe unakalia kuangalia makaratasi,...’akanisogelea kama vila hataki sauti ifike mbali.

‘Huyo bosi wako anasema hivyo kwa vile unamjengea maisha yake na miradi yake, wewe unapata nini hapo , ndio huo mshahara eeh?’ akawa kama aniuliza

‘Eti mshahara, ni mshahara  gani huo unaopata, mhasibu mzima, ...mshahara ambao huwezi hata kuweka akiba, amuka mwanaume, kama hawakulipi vizuri, tafuta njia ya kujilipa, mimi ndio nimeanza kukufundisha, lakini naona kama napigia gitaa mbuzi,.....’akasema.

‘Nikuambie ukweli usiponisikiliza mimi , ukajijenga, ukawa na wewe na kitu chako, utakuja kunikumbuka, na utanikumbuka kipindi ambacho umeshaharibikiwa na kukosa kila kitu, huku una mke, una watoto, na majukumu kibao, ndio hapo unashituka na kuanza kuhaha..’akasema huku akiniangalia moja kwa moja usoni.

‘Utaamuka wakati wenzako wanakimbia hujui uende wapi, kiwanja huna, sijui utajenga wapi na kwa vipi, amuka mwanaume, ni mwanaume gani wewe usiyebebeka, hivi uhasibu wako ndio huo wa kushika makaratasi, nikuambia ukweli, sio kila kitu ufundishwe, mengine unatakiwa utumie akili yako, hata bosi anafahamu hataki kukuambia tu, unafikiri yeye angelifika hapo alipo, kama hakuyafanya hayo,  ...’akasema huku akiniangalia kwa macho makali.

‘Kwa hili lililotokea mimi nimeamua moja, hiyo ndoa yako unayoisubiria haitakuwepo tena...labda nifanikiwe...sijajua kwa vipi, vinginevyo, ndoa itakuwa kati yangu mimi na wewe, na siku nitakapoamua mimi, naona kabisa wewe ni kichwa ngumu,...na unahitajia kuishi na mtu kama mimi,...tatizo lako wewe hujanielewa mimi ni nani,...umenikasirisha sana leo,...’akasema

‘Kwanini unasema hivyo , ndoa yangu inahusiana nini na hayo mambo yako...?’nikamuuliza

‘Huoni eeh, unataka nikuonyeshe,...hivi hujaona ulichokifanya, umenicheleweshea kufanikisha mipango yangu, hivi sasa naumiza kichwa nitapatia wapi hizo pesa, ...wewe bado unaona huna kosa, na hapo ulipo mchumba wako ni muhimu sana...sasa sikiliza kwa makini, kama nisipopata hizo pesa, ...nitahakikisha kuwa baba mkwe wako anafahamu kila kitu...’akasema akiniangalia kwa macho makali.

‘Mimi mbona sikuelewi, ninakuuliza, hili linahusiana vipi na ndoa yangu, ...na baba makwe hapa anakujakujaje, na ulitaka mimi nifanye nini....?’ nikamuuliza na yeye akabadili uso na kuongea ka tabasamu, na kama ananong’ona akasema;

‘Ngoja nikuambie kitu, kwa kujikosha, ..leo usiku kuna dili moja nataka kuicheza, na wewe ni lazima uhusike, .....nitakupigia simu nikiikamlisha, usipofika nitaituma ile barua,...yenye upuuzi wako kwa baba mkwe wako...tuharibikiwe sote.....unasikia tuharibikiwe wote...’akasema akiniangalia huku akitabasamu, utafikiri sio yeye anayeongea huku akinipitisha kidole tarataibu usoni.
‘Unafahamu mimi nakupenda sana, sijui kwanini vinginevyo nisingelipoteza muda wangu kwako, ni wangapi wananitaka mimi, lakini.....oh, kweli penye miti hakuna wajenzi,...’akasema huku akipitisha vidole vyake mdomoni kwangu, nilitamani niuondoe mkono wake, lakini yeye akauondoa haraka na kusema;

‘Hata hivyo, mimi sitaharibikiwa kwa maana nimeshajipanga vyema nafahamu ni nini ninachokifanya..., je wewe, ukikosa kazi  hapo kwa bosi wako utakwenda wapi, bado unatarajia kuishi kwenye nyumba ya kupanga hata kiwanja cha kudanganyia huna, na hapo ulipo maisha yako, yanategemea kubebwa na baba mkwe,....’akasema akiniangalia kwa dharau.

‘Sawa mimi nimekubali kashifa zako, na hayo ndio maisha yangu niliyokubaliana nayo, hayakuhusu, kwahiyo, ...’nikataka kusema na yeye akaniangalia huku akitabasamu na kusema;

‘Masikini mhasibu, unatia huruma...mmh,...akawa kama ananisogelea, na mimi nikarudi nyuma na kusema;

‘Mimi nimeshakuambia sitaki kujihusisha na mambo yako, na hilo la kumpelekea baba mkwe hayo mapicha, limetoka wapi...?’ nikamuuliza na yeye akatabsamu akataka kusema kitu, lakini mimi sikumpa nafasi nikamwabia

‘Hebu mdada achana na huo upuuzi wako, hivi kwanini unanitafuta ubaya, nini lengo lako, unataka nikuchukie,....nikuambie ukweli nikiamua kupambana na wewe, hutaamini....na nikikuchukia hutaamini kuwa ni mimi....’nikasema kwa kujipa moyo.

‘Nataka uamue hivyo,tupambane,...yaani ninavyoombea itokee hivyo,...lakini nafahamu kuwa huna ubavu huo,mtu mwenyewe umeshazimia kwangu, sema ukweli....pili nina siri zako nyingi, nikiziweka hadharani hata huyu bosi wako, hatatamani kukaa na wewe...unabisha ?’ akaseme an kuniuliza huku akijiangalia na kuniangalia usoni, mimi sikumjibu nikawa namwangalia tu, na alipoona namwangalia akasema;

‘Tutaonana usiku...’akasema huku akinikonyesheza na kuondoka, huku akitingisha maungo yake kimiondoko ya kinamna, akitikisha makalio yake,...nikabaki nimeduwaa, na kuhema muhemo wa mtu alitoka kupandisha mlima....


********

Baadaye nilikwenda kumuona bosi, na niliingia bila kugonga mlango, kumbe alikuwa akiongea na simu, ikabidi nitoke na wakati natoka nikasikia akisema;

‘Una uhakika hakuna kampuni kama hizo,  na je ulifuatilia account zao ukagundua ni watu gani....ni kweli beni jawawezi kuruhusu kuangalia accounti ya mtu , lakini nafahamu wewe unaweza kupata hizo taarifa, nakuomba unisaidie kwa hilo...’akasema na kukata simu.

‘Mhasibu unaweza kuingia...’akasema, na nilipoingia akawa kainama kama anasoma kitu kwenye komputa yake, alionekana kutokuwa na furaha kama siku nyingine, alionekana mwingi wa mawazo, sijui ni kutokana na hilo lililotokea au ana mambo yake mengine binafsi

‘Inabidi mambo mengine niyafuatilie mwenyewe, na hayakuwa na umuhimu wa mimi kuyafuatilia sio kazi yangu, lakini bila kufanya hivi, kampuni haitaenda, wakati mwingine natamani nitafute watu wengine, niondoe wafanyakazi wote wabovu, lakini, sio vizuri,...unapokuwa bosi unakuwa kama mzazi, ...huwezi kumfukuza mtoto wako kwa tabia mbaya, unatakiwa kumuadibu kwanza, ikishindikana ndio unasema, ngoja dunia imfunze......’akasema.

‘Bosi ina maana ndio unawaulizia hawo wateja, ambao nyaraka zako hazionekani....?’ nikamuuliza

‘Kuna mambo mengi nafuatilia, na hilo ni mojawapo, mimi nilitarajia wewe na mdada mtaweza kunisaidia kwa kiasi kikubwa, lakini kwa tukio hili lililotokea, naanza kuwa na mashakanyie, inaonekana wewe mwenyewe huna msimamo, kwanza wa maisha yako na pili wa kazi yako na usipoangalia kazi, itakushinda, na maisha yako yatakuwa ya kuyumba yumba....’akasema

‘Bosi, nakuhakikishia hilo halitarejea tena, wakati mwingine unapofika sehemu ngeni, inabidi kukutana na changamoto kama hizi, kwasababu bado sijawajau vyema, ni nani wakuaminika, na ni nani ana tabia gani, nimeshaanza kuwasoma wafanyakazi wa humu tabia na nyendo zao....’nikasema.

‘Sizani, ...kama huyu uliye naye karibu, ambaye muda wote mpo naye umeshindwa kumsoma, utawezeje kuwasoma hao wengine, ambao mnakutana mara moja moja...’akasema.

‘Kwanini bosi?’ nikauliza

‘Mfano mzuri ni huo, inawezekana vipi mtu aje kwako na kuchukua hundi ya benki, ambayo ipo kwenye himaya yako na kuandika mwenyewe, huoni kuwa ana mamlaka juu yako...kitu ambacho hata mimi mwenyewe siwezi kukifanya, siwezi nikaja nikachukua hundi na kujiandikia bila ya rizaa yako, lakini yeye anafanya hivyo, ...’akasema bosi.

‘Bosi huyo nimeshamsoma, sikuwa na uhakika kuwa alichukua hiyo muda gani, nilikuja kugundua baadaye..mwanzoni wakati tunaongea mimi nilijua ni utani tu, kumbe wakati nahangaika na mambo mengine, ndipo hapo aliweza kukichukua hicho kitabu cha hundi na kuchana hiyo nakala moja, ....’nikajaribu kusema uwongo.

‘Mhh, haiingii akilini, ...lakini ok nitahakikisha hilo linakoma, na wewe uwe makini, maana hili swala nitalifuatilia kwa karibu, nataka kuhakikisha hii kampuni hii inaendeshwa kisheria, na utaratibu uliokubalika, kama watu hawawezi kufanya hivyo, sitakuwa na namna nyingine, nitawaondoa, ili niajiri watu wenye kukubaliana na taratibu za kazi,...’akasema

‘Bosi usilichukulia hivyo, ni bahati mbaya, nita....’nikajitetea.

‘Hiyo sio bahati mbaya, jambo la bahato mbaya linajionyesha, hapo kuna dhamira ya kweli ya kulifanya hilo, lakini kwa bahati, limetokea wakati nimeshaweka huo mfumo mpya..vinginevyo, sasa hivi tungelikuwa tunahangaika na polisi...’akasema.

‘Oh....’nikasema hivyo.

‘Ndio hivyo ikitokea tena, sitasita kuwaita polisi,waje wawakamate hao wote wanaohusika,..wakaishi jela kidogo, na wakitoka ajira hakuna tena....’akasema.

‘Bosi nitahakikisha hilo halitendeki tena, naithamini sana ajira yangu, nimehangaika sana kuipata, na nihitajia sana kwa maisha yangu ya baadaye......’nikasema na yeye akasema;

‘Kusema ni rahisi, lakini vitendo ndivyo vinavyohakiki ukweli wa mtu,kila mtu anaweza kusema naweza, lakini je ni kweli anaweza,kama anaweza vitendo vyake vitamuhukumu...’akasema bosi, huku akiniangalia kwa makini.

‘Bosi mimi naweza....nakuhakikishia hilo....’nikasema huku kichwa kikianza kuniuma.

‘Kuna kitu nimejifunza kutoka kwa wafanyakazi wangu, japokuwa sasa kidogo wanaaza kubadilika, kuna tabia ya kufanya kazi kwa nia ya kumuonyesha bosi kuwa wanafanyakazi, sio kwa nia ya kutimiza wajibu wao..hili linanikera sana, ...maana bosi ukiondoka, ina maana kazi hazifanyiki  mpaka urudi, huo ni utumwa wa akili , ...na kwa hali kaam hiyo,hatutaweza kufikia malengo..’akasema.

‘Natumai watu watabadilika, mimi sina tabia hiyo...najituma wakati wote, tatizo ni changamoto za watu wengine,...’nikasema

‘Ni vyema ukajitambua, upo wapi unafanya nini, na kwanini, anyway,...nataka iwe hivyo, mimi nitajitahidi kadri ya uwezo wangu,  ili wafanyakazi wangu wabadilike, wajitambue,wajue wajibu wao ni nini, nahisi ni vyema, kila mmoja awe na utashi wa kujitambua, na kuwa tayari kujituma, na hili litawezekana kama kila mmoja ataweza kuweka mbali matamanio yake binafsi, na kujua kuwa hii ni kampuni, inayoendeshwa na watu, kwa manufaa ya wote, sio kwa manufaa ya mtu mmoja...’akasema

‘Matarajio yangu ni kuwawezesha kila mmoja aweza kupata mahitaji muhimu, kila mmoja kutokana na kipato chake aweza kupata mahitajio yanahitajika kwa mwanadamu, chakula malazi,na matibabu,...nafahamu kabisa, kama familia,  zikiwa hazina matatizo, mfanyakazi ataweza kujituma vyema, akili yake itatulia kazini, lakini kama kaacha matatizo huko nyuma, ni dhahiri, akili yake haitauwa kazini... tatizo ni kwa wale wenye tamaa kubwa, wanataka zaidi, ya uwezo wa kampuni....’akasema bosi.

‘Nashukuru kusikia hivyo bosi, inanipa moyo kuwa nimefika sehemu inayojali mfanyakazi...’nikasema

‘Tuyaache hayo kwa muda, nataka nikusimulie sehemu ndogo ya makaribisho yangu kwa mama mkwe...’akasema bosi,....

‘Unakumbuka tulipoishia kwenye kisa changu, baada ya kikao cha wanafamilia, wakakubaliana kuwa twende huko huko kwa mama mkwe, kutoka hapo tulipokuwa kwa shemeji, hadi huko kwa mama mkwe, ilikuwa ni safari ndefu, iliyotakiwa kuchuka meli, na safari hiyo ilikuwa ni ya usiku...., haya tuendelee......

****

Ilipofika usiku tuliondoka na meli, na pale nilipokuwa nimekaa,akili yangu haikuwa sawa, kwani nilikuwa nikiwaza mengi, nilikuwa nikiwazia yaliyotokea na yanayoendelea kutokea, na huko sijui nitakwenda kukutana na majanga gani, hasa hayo yaliyoanza kujitokeza ya mama mkwe.

Kwa ujumla nilikua sina raha, nilikuwa sina amani kabisa kwenye nafsi yangu, sikuelewa ni kwanini mimi nikutwe na mitihani yote hiyo,  je mimi nilikuwa na kosa gani, au kwa vile mimi ni mwanamke, lakini mbona wasichana wengine hawakukutwa na masahibu kama yaliyonikuta mimi, kama kweli hayo yanatokea kwa vile mimi ni mwanamke.

‘Mbona haupo sawa, ...unatakiwa ufurahi, unakwenda kuanza maisha mapya...’akaniambia mmoja wa jamaa wa mume wangu.

‘Ningeliomba iwe hivyo, na ndivyo matarajio yangu yalivyokuwa, lakini sijui kwanini mnasema mama mkwe hanitaki, hilo ndilo naliwazia...’nikasema.

‘Unafahamu tena akina mama, huenda yeye alikuwa na mipangilio yake, lakini wenzake hawakumsikiliza...’akasema

‘Kwanini wasiseme mapema...’nikauliza

‘Tulijua ni maswala ya muda tu, mama atakubaliana na hiyo hali, ...lakini usijali, hayo ukifika huko yataisha tu, ni hasira za muda...’akaniambia.

 Niligeuka kumwangalia mume wangu aliyekuwa kasimama akiangalia dirishani, alionekana na yeye katingwa na mawazo. Kwa namna fulani nilimuonea huruma, maana mama ni mama, kama hamkubaliani na mama ni lazima utakuwa na wakati mgumu sana, sikujua ni kwanini hawakuwa kitu kimoja, je ni kuhusu mimi, kuwa hanitaki, kuna mtu mwingine alimtaka yeye, au kuna mengine ...  ..

Basi nikajitahisi kujizuia, maana kila nilivyozidi kuwaza, niliona machozi yakikaribia kunitoka, na sikutaka watu wanione ninalia, nikajipotezea, na huku safari ikiendelea.

Tulifika huko tunapokwenda asubuhi,na hapo nilipo moyo ulikuwa ukinienda mbio, jinsi gani nitaweza kukabiliana na huyo mama mkwe asiyenitambua, asiyenitaka...

Tulipofika nyumbani, tulipokelewa na baadhi ya wanafamilia , ilionekana nyumba haina raha, tofauti na ilivyotakiwa kuwa, kwani nilitarajia kuwa kutakuwepo na shamra shamra za kumpokea bibi na bwana harusi, lakini hilo halikuwepo,na hata dalili ya kuwa kunakuja mgeni, ilikuwa kama watu wa kawaida tu wamefika.

‘Huyu ni wifi yako mkubwa na yule anayefuatia, ni wifi yako pia....’wakaanza kunitambulisha juu kwa juu,

‘Hilo litafanyika baadaye...wageni wafike watulie, familia ikutane, ndio utambulisho uanze, mnafanya kama anaondoka leo...’akasema mke wa shemeji.

‘Hicho kikao cha familia kitakalika kweli, mama atakubali...’akasema wifi na kukatishwa na mwenzake, kama kumkanya asiongee.

Alyekuwa karibu nami zaidi alikuwa shemeji wa mume wangu, nahisi ni kwa vile na yeye ni mtu wa kuja kama mimi...., na kama alivyosema wifi, hakukuwa na kikao cha wanafamilia, au hata ile shamra shamra, na kwa vile nilijichokea, nikaona bora iwe hivyo tu

Tukakaribishwa ndani, kwenye varanda kuu, hakukuwa na mpangilio kama kuna wageni muhimu wanakuja, kila kitu kilikuwa kama kawaida tu,....mimi kwasababu ya kuchoka, nikajipweteka kwenye kiti hata bila kuambiwa karibu ukae, nilikuwa nimechoka, kiakili na kimwili.

Nilitizama huku na kule kama nitamuona mama mkwe, lakini hakuwepo karibu, nikawa nimetulia kusubiria nini kitakachoendelea, baada ya kutulia kidogo, mume wangu akaniambia twende ndani chumba kingine, ili tukamsalimia mama yake. Hapo moyo ukaanza kunienda mbio, nakwenda kumuona mama mkwe.

Kwasababu ya kuogopa, kukutana na huyo mtu, nikawa kama nasita, na mume wangu akatangulia, kuelekea kwenye hicho chumba, na mimi nikamfuatia kwa nyumba na mume wangu akagonga mlango, karibu mara tatu, hakuna mtu aliyeitikia, mwishowe akaamua kufungua mlango.

Tukaingia kwenye hicho chumba, nikamuona mama kakaa pembeni ya kitanda, kashika shavu hakutuangalia, alikuwa kainama chini, na mtoto wake alipomsalimia, akainua kichwa na kumwangalia kwa uso uliojaa hasira, kanuna kabisa hakuitikia hata salamu ya mtoto wake, sembuse ya kwangu. Baadaye tukatoka bila hata ya kusikia neno moja kutoka kwa mama mkwe, nikaona sasa hapo ipo kazi.

‘Sasa tufanye nini, kwani kwanini mama hanitaki mimi?’ nikamuuliza tena mume wangu.
‘Usijali yatakwisha hoyo...’akasema inaonyesha hakutaka kuniambia ni kwasababu gani mama hanitaki.

Tukarudi varandani, na kukaa kidogo, kwani kuna watu walifika, ni wanandugu wengine kwa baba mdogo au mkubwa, wakawa wanatusalimu na kutambulishwa; Wengine walionyesha furaha zao, lakini wengine niliwaona wakiniangalia kwa jicho baya, nikawa najiuliza kuna nini kuhusu mimi kwa hawa watu,...,

Tulipomaliza kusalimia na watu mbalimbali, nilionyeshwa chumba changu, na kwa jinsi nilivyokuwa nimechoka nikaenda moja kwa moja chumbani kupumzika, nikiwa na dukuduku moyoni la kujua kulikoni, hakuna aliyeweza kunieleza, nikasikia nikiitwa kuwa chai ipo tayari.

Nilitoka chumbani, na hapo kidogo niliona maandalizi ya kifamilia, tulikaa pamoja, akiwemo mama mkwe, na kwa mara ya kwanza nilisikia sauti yake, lakini alikuwa akiongea na watoto wake wa kike, na hao mawafi zangu niliwaona wakiniangalia kwa macho ya husuda, na ilionekana wapo upande wa mama yao.

Muda wote wa kunywa chai hakuna aliyeniongelesha, walikuwa wakiongea na mama yao, na kunifanya mimi kama sipo kabisa hapo, nilikuwa na wakati mgumu hata hiyo chai ilikuwa hainyweki vyema, nikajitahidi hivyo hivyo hadi nikamaliza kunywa hicho kidogo nilichoweza.

Mume wangu alikuwa akinywa chao na wanaume upande wao mwingine, kwahiyo sikuwa na mtu aliyeweza kabisa hata kuniuliza chai vipi, nikajitahidi hivyo hivyo tu.

Tuliendelea kunywa chai hivyo hivyo, huku mama mkwe hataki hata kuniangali, na ikitokea bahati kageuka upande wangu, uso niliouona ulikuwa wa chuki, na hali ilivyoendelea hata mawifi nao wakawa hawaniangalii kwa tabasamu, walianza kufanya kama anavyonifanyia mama yao, kuniangalia kwa chuki,..., kiadabu, nilisubiria hadi wote walipomaliza kunywa chai, na nilipotaka kuondoa vyombo, mmoja wa amwifi akasema;

‘Wifi wewe nenda kapumzike, ...’akasema mmoja wa mawifi, na ndipo nikaondoka na huku nyuma nikasikia wifi mwingine akisema

‘Kwanini unajipendekeza kwake, muache aondoe vyombo, kwani kaolewa hapa kuja kufanya nini, ukianza kumvimbisha kichwa atajiona kafika...’akasema huyo wifi

‘Sio vizuri,tusimfanyie ubaya mapema mapema hivyo,...ngoja akusanye nguvu, sijui kaka kampendea nini, kati ya wanawake wote , anakuja kumuoa huyu, kweli kaka hana maana...., ‘ akasema huyo wifi mwingine

‘Tutaona ...’ilikuwa sauti ya mama, .....lakini alikuwa akiongea kwa sauti ya chini sana kama ananong’ona, sikuweza kumsikia vyema.

 ‘Dada,  huyu tusimpe muda, ikiwezekana akimbie mapema, eti mama eeh, .....?’ nikasikia akimuuliza mama yake,

Mama yake aliongea jambo lakini sikusikia alichoongea ni nini, mimi kwa muda huo nilikuwa bado nimesimama mlangoni sijaingia chumbani kwangu,...’nikageuka kuwangalia nilipogeuka uso wetu ukakutana na huyu wifi aliyeonekana kunichukia sana, na niliona akiniangalia kwa dharau na mama mkwe kwa muda huo nay eye alikuwa akinitizama, uso wake ulionyesha chuki kabisa...

.
Moyoni nikasema kama maisha yenyewe ndio hivi, basi ni heri niachike, nirudi kwetu, na hata kama wazazi wangu hawanitaki, nitakimbilio kokote nikaishi, lakini sitakubali kunyanyaswa tena, nitamshauri mume wangu kama kweli ananipenda tutafute sehemu nyingine ya kuishi, na hapo nikasikia sauti ikisema;

‘Kwa vile tutakuwa naye humu ndani, ...hawana sehemu nyingine, tutahakikisha, anakimbia mwenyewe,amuache kaka yetu , .....

NB: Ni hayo kidogo kwa leo


WAZO LA LEO: Kwanini tuchukiane, kwanini mioyo yetu, haitaki kujenga urafiki wa kweli, na kuondoa mafundo yaliyojikita nafsini kwetu. Urafiki, raha, tabasamu na kupendana, huleta murua mwema usoni, na matokeo yake ni upendo na amani, lakini chuki, fitina, hasira visasi, dharau, ...hujenga sura mbaya usoni, na matokeo yake ni vita, uhasama na baraka katika ardhi huondoka. Tupendane kiukweli siku zote,bila unafiki na ajenda za siri, ili dunia iwe kisiwa cha amani chenya baraka na upendo.
Ni mimi: emu-three

No comments :