Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, February 12, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-11


Siku mbili ambazo niliachiwa ofisi zilikuwa za mtihani mkubwa kwangu, kwani Mdada, alinikalia kooni, alitaka pesa nyingine zaidi, na hata kufikia kunitishia kuwa anaweza kuniharibia maisha yangu kama sitakubaliana na matakwa yake;

Baada ya kunioana nimekataa kata, kata, akaamua kuniingia kwa njia nyingine, na kuanza kuongea;

‘Sikiliza mpendwa, hii ndio nafasi yako pekee, ya kumaliza shida zangu na zako, na wenzako walikuwa wakifanya mambo yao wakati bosi hayupo, kama alivyoondoka hivi sasa, ...’akasema na mimi nikawa sitaki hata kumsikiliza kwani akilini mwangu nilikuwa nawaza jinsi gani bosi akigundua hayo malipo, atakavyokasirika na ndio mwanzo wa kutokuaniamni tena.

‘Mpenzi, unajua mimi kila ninachokifanya nakufikiria na wewe, usione kuwa nimefanya ile kwa dili kwa ajili yangu tu, nikuambie ukweli, hilo gari likitoka bandarini, litakusaidia na wewe hutatembelea tena ile pikipiki wewe ni mhasibu mwenye sifa zote za kuwa na gari,...usione kwa vile hilo gari litakuwa limeandikishwa kwa jina langu ndio uone kuwa ni langu,hapana, mimi ni mtu mwema sana, hili gari lina mkono wako, kwahiyo kiundani mimi  wewe ni mau muhimu, hilo gari ni letu, hasa kama mambo yatakwenda vyema, na ukaweza kuachana na huyo mshamba....’akaniambia.

‘Mdada, naomba hiyo kauli yako ya dharau, ya kumuita mchumba wangu mshamba uachane nayo, ..humfahamu vyema, na sivyo kabisa kama unavymfikiria wewe...mimi ndiye nilimuhadaa, tukashindwa kuvumilia, ikatokea hilo lililotokea, hata mimi ninajuta sana kwa tendo hilo...’nikasema

‘Hahaha...wanaume bwana, ...haina haja ya kuniambia hayo..nafahamu yote, ...na ukiwa sambamba na mimi, tutayamaliza,...nafahamu kabisa moyoni unanipenda sana mimi, kama ninavyokupenda wewe...cha muhimu, nisikilize, ....utaona matunda yake...kwanza unaona hii dili ilivyopita kilaini, ulikuwa unaogopa nini..hivyo ndivyo wanavyofanya wenzako....’akasema

‘Mdada, mimi sitaki kabisa unihusishwe na mambo yako, sijui cha gari lako wala pesa hizo ulizochukua, hayo mambo ni yako, kwangu mimi nafahamu kuwa pesa hizo zimetoka kwa bahati mbaya kwa wateja, sikuwa makini kuangalia nyaraka zao, nikalipa nikujua kuwa ni wateja wa kila siku, wa kusafirisha mizigo...kwahiyo hata bosi akiniuliza nitasema hivyo na hivi sasa natayarisha ripoti yangu...’mimi nikasema

‘Unasema nini, kama unataka kufukuzwa kazi na hata kufungwa wewe fanya hivyo,...andika huo ujinga wako kuwa ulikuwa hujui, ..eeh, umelipa kwa bahati mbaya, ...wewe kweli huna akili, kwa mtaji huo utakufa masikini, nikuambie ukweli, hilo halitajulikana kabisa na likijulikana wewe kama mhasibu utajua jinsi gani ya kulifunika, ..hivi wewe mbona upo hivyo..’akaniambia

‘Huwa hatuendi hivyo, sio kwa vile unaitwa mhasibu,ndio unafahamu jinsi gani ya kutafuta pesa kwa njia haramu, najuta kwanini niliziandikia zile hundi, sitafanya hayo makosa tena, ....maana najiingiza kwenye matatizo ambayo sina faida nayo...’nikasema

‘Nimeshakuambia gari hilo ni letu, na sasa nataka kumalizia nyumba yangu,...nataka iwe yetu , mimi na wewe...nimekuja na mpango mwingine, nikufundishe jinsi gani ya kutafuta maisha,....’akaniambia

‘Ina maana unajenga, na kujenga kwenyewe ni kwa pesa za wizi..?’ nikamuuliza

‘Nani kaiba wewe..huu sio wizi, ni ujanja kutumia elimu yako kwa faida, sio wizi, maana wenzetu wanatumia jasho letu, nguvu zetu, wanatulipa mshahara mdogo, wanajijenga, na sisi tukipata mwanya wa kuzirejesha nguvu zetu walizotunyonya inabidi tufaye hivyo, bila hivyo, hebu niambie utajenga lini...’akawa kama ananiuliza.

‘Tutajenga tu....kuna njia nyingi halali, ...’nikasema.

‘Kama zipi, hebu niambia kwa huo mshahara wako utajengaje,...sasa hivi ndio unatarajia kuitwa baba, ..ina maana majukumu yanaongezeka, kwa hiyo gharama za maisha zinaongezeka, kipato chako kinapungua, si ndio hivyo, mhasibu...’akawa kama ananiuliza

‘Kila kitu kina wakati wake, na mipangilio yake, ikifika muda huo, nikiwa na familia, nitajipanga upya, lakini sio kwa njia hiyo unayotaka wewe, hiyo sio haki,....’nikasema

‘Nisikilize kwa makini, mimi ninachotaka ni kukusaidia wewe kwa kukupanua akili yako na mawazo, mimi nafahamu jinsi gani wengi waliotajirika wanavyofanya, nimekaa nao nakuwauliza kwa undani, hasa nyie mnaojiita wahasibu, wengi waliojaliwa nimejaribu kuwadadisi na kuwachunguza...’akasema

‘Hakuna mtu anayeweza kufanya uchafu huo akakuambia, hilo nalipinga, hayo ni mawazo yako ...’nikamwambia.

‘Hahaha, uchafu huo....mimi ni mtoto wa mjini, nikitaka jambo ni lazima nilipate, hiyo ndio siri ya maisha yangu,...’akaniambia

‘Unataka kusema nini?’ nikamuuliza

‘Nimekuja na mkakatai wa kukusaidia wewe, na kukusaidia wewe ni pamoja na kujisaidia mwenyewe, hakuna kitu cha bure siku hizi, asikudanganye mtu, ukiona unafanyiwa fadhila ujue kuna gharama zake...unisikilize kwa makini....’akasema

‘Unataka nini tena, hebu subiri, tuangalia hili janga ulilolifanya litaishaje, na sijui utalimazliza vipi, maana kiukweli ni lazima bosi akiniuliza nimwambie ukweli...’nikasema

‘Utamwambia ukweli gani, hebu niambie, ..ukimwambia utaonekana mjinga, hujui kazi yako, na utaonekana unafahamu mpango wote, kwanini ulikimbilia kuzipitisha hizo nyaraka, kwanini uliandika hiyo hundi, kwanini hukumwambia bosi wako...tumia akili, hilo cha kufanya ni kulinyamizisha kiaina, lisahau, na katika mahesabu yako lifiche kinamna,...ukipiga gharama zake, unaziweka kwenye sehemu isyogundulikana, mimi nafahamu yote hayo....’akasema

‘Oh...kweli una ndoto za ajabu,siaminu, nilikuwa nakuona mtu mwema, na nilivutika sana kwako, nikijua una mapenzi ya dhati, ...lakini sasa naanza kukuogopa, ...’nikasema na yeye akanisogelea na kuanza kunipitisha mikono yake mgongoni, na kusema;

‘Sikiliza mpendwa, mimi nakupenda sana, ndio nafanya haya yote, ...ili na wewe uwe mtu miongoni mwa watu, nakutafutia maisha bora, usione wenzako wana maisha bora ukafikiri wamefanya kihalali, hakuna hiyo, asikudanganye mtu......sasa nataka mimi na wewe tuwe kitu kimoja, na ....’akachukua simu yake, iliyokuwa ikiita,;

‘Halloh mpenzi, niambie dear,.....umeshaupata huo mzigo, ....?’ akauliza

‘Unasema nini, haiwezekani, kwani uliambiwa nini ulipozipeleka benki?’ akauliza kwa mshangao, huku akiniangalia kwa macho yaliyojaa mshangao, akasikiliza kwa muda halafu akageuka kama anataka kutoka nje, halafu akasema;

‘Usijali, nitahakikisha nalifanyia kazi, ...naomba tafadhali, nisaidia, litoke hilo gari,....nipo chini ya miguu yako, unaona livyojitahidi, ...fanay unavyoweza, mimi nitahakikisha unazipta hizo pesa...ngoja nifanye uchunguzi, maana sijui kwanini wamezikataa....’akasema na baadaye akakata simu na kuniangalia.

‘Ujinga gani umefanya wewe mtu...’akasema kwa hasira huku kanitolea macho

‘Mimi sikuelewi, unaongea nini...’nikasema huku sijui kwanini ananiambia hivyo

‘Zile hundi mbili, za hao wafadhili, ....ambao ndio wananisaidia kutoa hilo gari zimekataliwa benki, zimezuiliwa....ni nani anaweza kufanay hivyo  kama sio wewe mhasibu maana bosi hayupo...niambie kwanini umefanya hivyo?’ akaniuliza huku akiwa kanitolea macho ya hasira.

‘Kama imekuwa hivyo, mbona nitashukuru sana, ..kweli wamezikataa,oh, ahsante mungu, ...’nikasema huku nikiangalia juu

‘Wewe mjinga, na utakufa kwa umasikini, na sikiliza sasa hivi nampigia baba mkwe wako na namtumia mapicha ya uchafu wako, si unajiona wewe ni mjanja, ngoja nikuonyeshe kuwa mimi ni nani...’akasema na kuchukua simu akapiga, mimi nilijua kuwa anatania, akasema;

‘Shikamoo, baba, ni mimi, nilikuwa nakujulia hali na kukupa taarifa ya kile ulichoniambia nikufanyie kazi...ndio baba, nitakutumia taarifa zote, ....mmh, yupo ofisini kwake, kama unataka kuongea naye....hebu subiri nimfuate....’akasema na kuiziba ile simu sehemu ya kusikilizia akasema;

‘Ili kukuhakishia kuwa mimi sitanii, ongea na baba mkwe wako...’akasema huku akinipa simu, na mimi nikiwa nimeduwaa, nikaipokea hiyo simu, na sikujua niongee nini, nikawa nimeduwaa, nikaiweka sikioni.

 Sauti ya baba mkwe wangu ikawa hewani, na mimi kwa heshima nikasema;

‘Shikamoo mzee, ...’nikasamilia

‘Nimesikia taarifa zako....’akaanza kuongea

‘Taarifa zangu,....hapo nikahisi mwili ukiniisha nguvu, nikamwangalia Mdada, ambaye alikuwa akitafuta kitu kwenye kabati langu, nilitaka kumzuia, lakini baba mkwe alikuwa hewani, na mara mdada akatoa kitabu cha hundi akakifungua na nilimuona akitoa nakala moja ya zile hundi alizosaini bosi, akaichana na kuanza kuondoka nayo...

‘Ndio taarifa zako...’akasema baba mkwe, na hapo nikawa nataka kumkimbilia mdada kumzuia, na huku nataka kumsikiliza baba mkwe anataka kuniambia nini kuhusu hizo taarifa zangu..

***********

Nikiwa nyumbani, bosi alinipigia simu, akaniambia benki walimpigia simu, na kumpa taaarifa za hundi mbili zisizo kamilika vigezo vya malipo, ..

‘Hundi gani hizo bosi....?’ nikamuuliza huku nikiwa na mawenge kichwani, kichwa kilikuwa kinaniuma sana, na nilitaka kukipooza kwa kinywaji.

‘Sijazijua vyema, na hata huyo mlipwaji simtambui vyema, nikaona jambo jema ni kuzizuia, hadi hapo nitakaporudi, jaribu kuzitafiti, umeshapitia nyaraka zote vyema?’ akaniuliza

‘Nilipitia wakati ule naandika, na kwa vile nilikuwa naandika kwa haraka, huenda niliandika bila kuangalia vyema, ngoja nipitie tena...’nikasema

‘Tafadhali fanya hivyo, na hakikisha kuwa hawo wateja, unaangalia mikataba yao, kama kweli wapo kwenye kumbu kumbu zetu au wametoka wapi, na ongea na mdada, yeye anawafahamu wateja wote, ni muhimu sana na wewe ukawafahamu ....’akasema
‘Sawa bosi nitafanya hivyo, samahani sana, maana imenijia kwa mshituko, sikuwa na wasiwasi, nilijua kuwa mdada, kaambatisha kila kitu...’nikasema.

‘Katika kazi hasa hiyo yako, usimwamini mtu yoyote, unachotakiwa kuamini ni nyaraka, ni kumbukumbu za malipo, sio mtu,...inaweza mtu mwingine akatumia mwanya wa uzaifu wako kujipatia malipo yasiyo sahihi....sitaki nikufundishe majukumu ya kazi zako, lakini ni muhimu sana uwe makini...’akaniambia

‘Sawa bosi nitahakikisha kuwa hilo halitarudiwa tena....’nikasema

‘Sijui, hilo ni jukumu lako, usije ukaghilibiwa na uzuri, tamaa, udugu na kujuana, katika kazi yako, ukiwa katika kazi yako, kumbuka, stakabadhi, kumbukumbu, mikataba, na nyaraka ndizo kigezo cha malipo ....hakuna jingine, ....na hakikisha umepata taarifa za hawo watu wawili, niliozuia hundi zao, nikirudi nipate maelezo....’akasema

‘Sawa bosi...nimekusikia, nitafanya hivyo ....’nikasema huku nikikumbuka hiyo hundi nyingine aliyoichukua mdada, sijui kaanzika kiasi gani, na kwa nani...

‘Je kuna malipo mengine umeyafanya kwa hivi sasa?’ akaniuliza na hapo nikashikwa na kigugumizi, na hakusibiri jibu langu akasema;

‘Nina salio kidogo hapa, ngoja nikusimulie sehemu ya kisa changu, halafu kama kuna lolote utaniambia....’akasema na kuanza kunisimulia sehemu hii ya kisa chake...

*********

Nikiwa nasubiri hiyo ndoa, akili yangu ilishajenga mipango mingine, kuwa nikatae kabisa kuwa mimi sipo tayari kuolewa na huyo mtu, kwani simpendi na ndoa hiyo ni kama ya kulazimishwa, na niliona ndio njia pekee ya kuwakomoa hawa watu, lakini kwa upande mwingine, nilimuonea huruma mama, ina maana lolote litakalolifanya hapo, madhara yake ni kwa mama

‘Hapana, siwezi kukubali, ni lazima niwaonyeshe baba kuwa na mimi naweza kujiamulia mambo yangu mwenyewe, ...lakini mama ataumia sana,..sasa nifanye nini...’nikasema kimoyo moyo.

‘Je umekubali kuolewa na ndugu fulani, kwa mahari yake....’nikasikia nikiulizwa, ilikuwa kama sipo, na hata yule muulizaji akashikwa na mshangao, kwani aliniona kabisa kama mimi sipo makini..yeye kabla hajauliza tena, akamnong’oneza msaidizi wangu, na msaidizi wangu, akanisogelea na kuniuliza

‘Vipi kuna tatizo mbona umekuwa hivyo, unaumwa, nikawa kama mtu aliyeshituka toka kwenye usingizi, nikasema;

‘Hamna tatizo...oh, samahani, siumwi, nipo tayari,....’nikasema na kukaa tayari, na huyo mtu wa kufungisha ndoa akaanza kuniuliza maswali tena, na wakati huo nilishaamua ni nini la kufanya, lakini mdomo haukufanya hivyo, nikajikuta nikikubali, sikuweza kupinga tena, nikakubali kuwa nimekubali kuolewa na huyo mume, ndoa ikafungwa.....sehemu hiyo ikapita, na kutangazwa kuwa mimi sasa ni mke halali wa mume wangu,....

Baada ya ndoa, kukawa na shamra shamra ndogo, kama ilivyoandaliwa, ilikuwa kama sherehe ya kifamilia tu, japokuwa kulikuwa na vigelegele vya hapa na pale, na washambenga wakibeza kwa kusema;

‘Hii ni harusi gani, ni harusi ya mkeka...’

Hata hivyo mimi nilishukuru, nikijua sasa mimi ni mke wa mtu , sina ujanja tena kwani lile jukumu muhimu la harusi ambalo ni kufunga ndoa limekamilika, mengine ni kushehesha tu, na hapo nikawasikia wengine wakiimba huku wakiruka ruka;

‘Mlisema hayawi sasa yamefika, mke kapata bwana, ....’kukawa na nyimbo za hapa na pale na nyingine za kupigana vijembe, hata hivyo ukweli ulibakia kuwa harusi hiyo haikuwa kama zilivyokuwa harusi za wengine, hata hivyo, sikuweza kumlaumu mtu au kuweka kinyongo dhidi ya yoyote yule.

Ilipofika saa za usiku kukawa na chakula cha usiku na walialikwa majirani baadhi tu kama ilivyo kuwa kwenye ndoa wakajumuika kupata chakula rasimi cha usiku. Na baada ya chakula cha usiku mie na mume wangu tukaenda kupumzika kama ilivyo kuwa kasumba ya ndoa.

Ukumbuke kuwa mume huyu sikuwa na mazoea naye, na moyo wangu hakuwa umempenda, kwahiyo hapo sasa nilitakiwa kuyaondoa hayo, na kujenga hisia nyingine kuwa sasa huyo ni mume wangu, ...nikajitutumua na kutimiza yale niliyofundishwa, kuonyesha upendo wa dhati kwake, hasa siku hiyo muhimu ya kwanza.

Kwenye maeneo yetu, na taratibu zetu, kuna jambo linafanyika, unapoolewa, na usiku huo wa kwanza wa kukutana na mume wako ni usiku muhimu sana, wa kupima uvumilivu wa mwanamke, je kweli aliweza kujitunza, na ili usiku huo aweza kumpa mume wake zawadi muhimu,...

Ni mila na desturi, ambazo zilimlenga zaidi mwanamke, kwa mwanaume, hana tatizo, yeye, ni kufanya kazi yake,na baada ya akzi hiyo, ushahidi huo hutolewa asubuhi na mapema, bila kificho,

Kwahiyo kama ada, kesho yake baada ya kufunga ndoa, na tendo la usiku wa kwanza kati ya mume na mke, watu hufika asubuhi kusubiria kwa hamu matokeo ya tendo hilo la kwanza lililofanyiaka usiku kwa wanandoa hao, hilo litampa sifa mama mzazi na muolewaji au kuwaumbua, na watu hawana dogo, hata wale wasioalikwa hufika asubuhi na mpema, ili yasiwapite.

Na kweli, kama ilivyo ada, watu wakafika wakiwa wana yao, kama ilivyokuwa nyuma, wengi walishanipaka matope kuwa mimi ni muhuni wa siri, japokuwa sikuwa anjionyesha, na wengine wakasema nilifukuzwa shule kwa sababu ya uhuni wangu, hata kutembea na walimu, na wengine wakawa wananitetea, na kwa malumbano hayo kukajenga makundi mawili, yenye mtizamo tofauti.

Bila kutarajia, watu wakawa wengi sana, asubuhi, kuhakiki, vinywa vya watu,na waliyosikia juu yangu, na wengi walishajiandaa kuniumbua, kuwa kweli mimi ni muhuni, na sikuwa nasingiziwa, na hata wale wasio na simile, wakaanza kusema;

‘Hivi mumewahi kuja asubuhi hapa kusubiria nini, huyu anawezaje kuwa bikira kwa jinsi ya tabia yake ilivyo, mnajisumbua bure...,?.’wakasema wale walionipaka matope

‘Ni muhimu tufike tuhakikishe...’wengine wakasema.

Ikafika muda muafaka,Matroni, akaingia chumbani, akalibeba shuka jeupe, ambalo lilikuwa limetandikwa rasimu kwa kazi, hiyo, na kutoka nalo nje,huku akiwa kalifunua ili kila mtu aone, na watu hapo wanasukumana, kuhakiki, kama unavyojua wafunua vinywa, wasiotaka kupitwa na kitu.

Kinyume na matarajio ya wengi, kinyume na matope waliyonipaka, kila mtu liyeliona hilo shuke, alibakia mdomo wazi, na wengine, wakajifanya kama hawakuona, ilimradi kukazuka namna fulani ya gumzo la chini kwa chini, ooh, unaona, eeh, ilikuwa hivi, aaa, wewe ndiye ulisema,....aibu, wakashushuka, hasa wale waliojaribu kunipaka matope, wakiongozwa na mama wa kambo.

‘Mumeona hamjaoana...?’ akauliza matroni kwa kusheheneza

‘Tumeoana,...’wakasema watu na kupiga viegele

Watu wengi walishikwa na aibu na matron kwa kushabikia, akawa anawapitishia watu kwa karibu ili waone, hizo ni mila na desturi zetu, na kwa muda huo wazazi wanakuwa pale mbele, ili kupewa pongezi, au kinyume chake.

Wazazi wangu ambao hawakutaka hata kukaa pale mbele wakijua ni aibu, waliposikia watu wanashangilia, wakajitokeza, na mama wa kambo ambaye alihisi kuwa watu wanashngailia kiushabiki tu, kwa vile nimeumbuka, akajitokeza kidogo, na alipoona ule ushahidi, akawa kashikwa na aibu, baba ndiye aliyebakia mdomo wazi,akionyesha kama haamini,  maana yeye ndio kabisa, alikuwa keshaamini maneno ya watu wa nje, kuwa mimi ni muhuni, malaya, na mara nyingi alikuwa akimsikiliza mke wake, bila kujali utetezi wangu.

Basi mume wangu akatoa zawadi kwa mama yangu mzazi kwa malezi bora, na kushukuru kwa kumpa mke aliyekamilika, na harusi ikawa imekamilika kihivyo, na kilichobakia kwa siku hiyo ni kupata chai maalumu ya asubuhi ya kuagana, na sisi , yaani mimi na mume wangu na watu wake aliokuja nao,tukajiandaa kwa safari ya kwenda huko kwa mume.

Hapo kikafuata kipindi cha majozi, maana mtu unaagana na familia yako,wazazi wako unawaacha, ndugu zako unawaacha, unakwenda kukutana na wazazi wengine, ambao hata kuwafahamu vyema, huwafahamu, na hujui utakwenda kukutana na maisha gani huko mbele, zaidi ya mungu wako kukusaidia.

Nikaagana na ndugu zangu, na baba, na mama wa kambo, ambaye aliona aibu hata ya kuongea na mimi, zaidi alisema, ; `haya, nenda sasa ukayaone maisha halisi ya mume na mke, maisha ambayo wengi walinilaumu, ...utajionea mwenyewe jinsi gani ya kuishi na watoto wa wenzako...’akasema kwa kujitetea, na mimi sikumjibu kitu.

Nikaagana na mama, mama chozi lilimtoka, akanikumbatia na alishindwa hata kuongea, na baada ya kunikumbatia kwa muda, akasema;

‘Mwanangu kumbuka niliyokuhusia, huko unakwenda kwa baba na mama mwingine, unatakiwa kuwaheshimu kama ulivyokuwa ukituheshimu sisi, utakutana na mitihani mingi, lakini ipokee yote kama maisha ya kawaida,mtii mume wako, kwani yeye ndiye kila kitu kwako..nakutakia kila-laheri, tukijaliwa tutakuja kukuona...’akasema mama, na mimi nikashindwa kuvumilia, nikajikuta nikilia...

‘Muda umefika mwache aondoke, ...’akasema baba, na kweli, safari ikafika, na ikabidi niondoke kutoka mikono ya familia yangu na kuingia kwenye familia ya mume.

Ilikuwa safari ndefu kidogo, ya kwenda mkoa mwingine, na ili kufika huko ilibidi kwanza kupitia kwa shemeji yangu, ndugu wa mume wangu, na hapo tukakaribishwa kidogo, na shamra shamra za hapa na pale,...

Niliona kuna sintofahamu inaendelea, kwani mume wangu aliitwa, wakawa an kikao chao, baadaye akaja kuniona akaitwa tena, nikahisi kuna jambo ambalo halipo sawa, baadaye, shemeji akasema;

‘Mama hamtaki shemeji....kama mlivyojua,hakutaka hiyo ndoa, na kashikilia msimamo wake huo huo, kasema kabisa yeye haitambui hiyo ndoa...’akasema shemeji, na kunifanya nibakie na mshangao, sikuelewa kwanini huyo mama mke haitambui hiyo ndoa yangu na mtoto wake.

'Na kwanini hanitaki mimi..'nikajiuliza kwani sikumbuki kukutana naye kabla, na nilishindwa hata nimuulize nini mume wangu, maana hata yeye alionekana hana raha kwa akuli hiyo, wakawa wanajadili na ndugu wafanye nini, baadaye mume wanagu akafika, nikasubiri kusikia atasema nini...

NB: Ni kwanini, tutapata sehemu ijayao.


WAZO LA LEO: Ndoa ni kati ya mume na mke, na iliyotokana na ni kiapo cha ndoa, cha kukubaliana, baada ya kiapo hicho, hiyo ni familia inayojitegemea, japokuwa ina mfaungamano na wazazi wa pande zote. Cha muhimu kwa wanandoa ni mipangilio ya jinsi gani ya kuishi. Wengine watahitajika tu kama washauri, lakini sio kuingilia ndoa hiyo tena, labda kama kuna tatizo ambalo mnaona ni muhimu ili kuiokoa hiyo ndoa. Kuna watu wanapenda kuingilia ndoa za watu, na hata kumkataa mume au mke,...tusifanye hivyo, tunakiuka mikataba ya ndoa, na kuhini imani zetu.

Ni mimi: emu-three

No comments :