Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, January 31, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-6



Wakati bosi ananisimulia kisa chake akili yangu ilikuwa mbali kabisa, ikinipeleka kwenye tukio la usiku wa jana, ilikuwa kama ndoto ndani ya kisiwa cha ajabu, ambacho sijawahi kukifika, ni kweli sina tabia hiyo, na kwa siku hiyo ilikuwa ni kwa mara ya kwanza.

 Katika maisha yangu nimekuwa nikijaribu kuishi maisha mema, bila kujiingiza kwenye matatizo, na siku zote nimekuwa nikifanikiwa, lakini nilipojiunga kwenye kampuni hii nimejikuta nikitekwa na majaribu makubwa na chanzo kimekuwa ni huyu dada ambaye alijulikana kama Mdada.

Kwakweli nilishindwa kujua ni kwanini, namuwaza yeye tu, na nikimuoma moyo wangu unanienda mbio, na akinikaribu ndio basi tena, nakuwa kama mtu aliyepagawa,...sijui kanifanyia nini. Nimejaribu sana kuishinda nafsi, na kujaribu kutokumuwaza yeye, lakini imekuwa ni vigumu.

Sasa tukio la jana ndio likaharibu kila kitu,.....

‘Naona Mdada anaumwa, kanitumia ujumbe, kasema anaumwa leo hataweza kuja ofisini, na kaniomba, wewe uende kumsaidia kumpeleka hospitalini....’akasema bosi
  
‘Kwanini mimi bosi, dereva wetu si yupo...?!’ nikauliza kwa mshangao.

‘Mimi sijui, labda kwa vile mlikuwa naye jana...’akasema bosi na kunifanya nishangae bosi kafahamia vipi kuwa nilikuwa na huyu mtu jana, na hapo hapo nikamuuliza;

‘Unasema tulikuwa naye jana, wapi....?!, mimi nakumbuka tulikuwa naye hapa ofisini, akatoka na mimi nilitoka baadaye, nikaenda mazoezini, lakini mbona sifahamu kuwa anaumwa?’ nikawa najiuma uma, na bosi akaniangalia kwa mashana na kusema;

‘Je utaweza kwenda kumpeleka hospitalini au nimtume dereva wetu ampeleke, lakini ningeshauri kwa vile hakuna kazi nyingi nenda kampeleke, ili nihakikishe kuwa kweli anaumwa..’akasema bosi

‘Kwani mimi ndio nitakuwa kipimo kizuri cha kumtambua kuwa kweli anaumwa, anaweza akaigiza kuwa anaumwa, na wala mimi nisifahamu ukweli, si uamfahamu anavyojua kuigiza jambo, utafikiri ni kweli..’nikasema

‘Na ndipo maana nakutuma wewe ili niufahamu uaminifu wako..’akasema

‘Ina maana bosi huniamini mpaka sasa?’ nikamuuliza kwa mshangao

‘Kwenye swala la mapenzi, ni nadra sana kumuamini mtu, hata mume au mke wako nyumbani, huwezi kumwamini mia kwa mia, kwasababu mengi yanayofanyika katika nyanja hiyo hufanyika kwa siri, ...na siri kubwa ni ile iliyopo moyoni,...kwahiyo kwa kifupi sijaweza kukuamini katika swala kama hilo...’akasema bosi.

‘Sasa nifanye nini ili uweze kuniamini?’ nikamuuliza

‘Kwa sawala kama hilo, ni vigumu, na naweza kusema hilo halinihusu sana, hayo ni maswala binafsi, ila nakutuma uende kwa huyo binti, nataka kufahamu kama kweli anaumwa, na kama anaumwa uweze kumsaidia...ni hivyo tu, mengine niachie mwenyewe....’akaniambia na mimi akilini nikawa najiuliza bosi anataka kunipima kitu gani hasa, je anafahamu nini kuhusu jana, mbona ni kama anafahamu yaliyotokea jana, je nikikataa kwenda atanifikiriaje....

‘Kwani bosi huyu binti unamfahamu kivipi, zaidi ya kikazi,...?’ nikamuuliza na yeye akaniangalia huku akionyesha uso wa kushangaa

'Kwanini leo unaniuliza hivyo, jana umeingia kwenye msimamo gani, maana nakuona una waza sana, na pili ni kama kuna jambo umelitenda na unajishuku...?' akaniuliza

'Hapana bosi hakuna kitu, ila inanipa mashaka sana kuhusu huyu binti, naona kama ananiweka kwenye wakati mgumu, ...'nikasema, na yeye akaniangalia kwa makini halafu akasema

'Katika maswala ya mapenzi, kuna mambo unatakiw auwe makini nayo, kuna mshawasho wa kutamani,na kuna kupenda. Nafasi inaweza ikaona kitu, na kukitamani, na hapo unatakiwa uweze kuitawala ile nafsi kwa kujiuliza je kuna faida gani, au kuna uhalali w hicho kitu, ukiona kina madhara, unatakiwa kuikataza hiyo nafsi kwa haraka, ...ndio kama vile unapoona pombe au sigara, kwa mara ya kwanza, .....'akatulia.

'Ukianza kuvuta sigara au kunywa pombe, ni kwamba umeshaikubali ile hali ya nafsi yako, lakini kumbe ungeliweza kuikataza na ukaishinda, ...ukiendekeza hiyo hali, ndio unakuwa mlevi, mzinzi, mwizi na kadhalika...

'Sasa basi hapo ulipo, unapambana na nafsi yako, umeona kitu nafsi imekitamani, je kinafaa, je ni halali, ...unatakiwa uiulize nafsi yako , na muda wa kujiuliza ni sasa...ukifanya makosa, utakuja kujijutia, ....'akasema na kuniangalia machoni.

'Ndio maana nataka kumfahamu vyema huyo binti.....'nikasema

'Ili iweje, ....kwanza iulize nafsi yako, ichanganue kwa yale uliyoyaona, sawa, ...kama umempenda, na sio mshawasha wa kutamani, una haki ya kumchunguza vyema, ...kupenda ni mtihani, ...'akatulia na kuniangalia kwa makini.

‘Unauliza namuelewaje huyo binti, huyo binti namuelewa kama ninavyokufahamu wewe, ..., nikuambie ukweli, huyo binti, nilipompokea hapa kazini, nilimtendea kama binti yangu, nikawa najaribu kumsaidia, kwa jinsi nilivyoona mimi inafaa...lakini mimi ni muajiri wake tu, sina mamlaka ya undani zaidi kama mzazi....'akatulia kidogo.

'Kwanza nilimuona kama mtu mwenye matatizo, ambaye kaishi kwenye mateso au kukosa haki za mtoto, lakini nikagundua kuwa tabia aliyo nayo ni ya kwake binafsi, ni ya kujiingiza kwa tamaa, ...nikajaribu kadri ya uwezo wangu kumnyosha, lakini kama wanavyosema wahenga samaki umkunje akiwa mbichi, akishakauka ...mmh....'akatulia kidogo.

'Una maana huyo binti hana tabia nzuri,...hanifai...mbona jana ulinishawishi....'nikatulia.

'Sijasema hana tabia nzuri, hilo halipo akilini mwangu, nimesema kuna mambo anayaendekeza, na anaweza kuyaacha akiamau, ni mnzuri tu, tatizo lake anaona kuwa labda wanaume ndio wataweza kumsaidia, nilimkanya kuhusu hilo, nikamwambia kuwa kila mtu ana mattizo yake, na msaada mkubwa wa matatizo ni mtu mwenyewe, kama mwenyewe hutaweza kujisaidia usitegemee mtu mwingine akaja kufanya miujiza...’akaniambia.

‘Mhh, umesema huyo binti alionekana kama ana matatizo, kwani ulivyoona wewe, huyo binti ana matatizo gani?’ nikamuuliza

‘Kama kweli anakupenda kama anavyodai, ipo siku mwenyewe atakuambia, utamuona na kila kitu kama utakuwa mwangalifu, kitajionyesha cheyewe, cha muhimu uwe mwangalifu, uwe makini kwa kila hatua, maana yeye anaonekana kuwa mjanja kuliko hata wewe...’akaniambia na kuniangalia machoni, na mimi nikawa nimetulia nikiwa nimetingwa na mawazo, hasa nikiwazia tukio la jana..

'Mhh...'nikaguna na kushika kichwa, na bosi aliponiona hivyo akawa anaandika ujumbe kwenye simu yake halafu akaniangalia na kusema;

‘Ngoja sasa nikusimulie kidogo sehemu ya maisha yangu, nikimaliza, nitakuruhusu uende umpeleke huyo binti hospitalini , nimeshamwambia aanze kujiandaa, ukifika mnandoka, sio tena unafika ndio anaanza kujiandaa, siunafahamu akina mama tulivyo.

‘Japokua hisia zangu zinanituma kuwa huenda jana atakuwa alilewa sana, kwani kuna siku huyu binti anakunywa, ....kupitiliza, nimejaribu sana kumkanya hiyo tabia, kuwa mawazo hayandolewi kwa kuyaahirisha kwa kulewa, lakini ..mmh, ni sikio la kufa halisikii dawa,..sasa kama kweli anaumwa, ni muhimu uhakikishe anafika hospitalini.

'Kama ukirudi mapema tutaendelea na sehemu nyingine ya maisha yangu...lakini kwa sasa ngoja nikusimulie sehemu hii ndogo ya yaliyotokea baada ya baba kutoa maamuzi yake,....’akaniambia na mimi sikuweza kupinga tena, nikakaa kimiya nikimsikiliza bosi kuhusu maisha yake, huku moyoni nafahamu vyema, huyo binti sio mgonjwa, bali ni kutokana na tukio la jana, sikutaka kumwambai bosi ukweli,..

******

Ni kweli baba akanisimamisha shule, hakutaka tena kuwasikiliza watu, si majirani wala ndugu zake, waliokuja kumshauri, yeye akasema ameamua na hataki mtu kumuingilia maisha yake na familia yake;

‘Mimi nimeshaamua, sitaki kusikia upuuzi wowote, nafahamu kabisa huyu binti akienda kubeba mimba huko shuleni mtakuja kunilaumu mimi,....’akasema pale alipokuja kaka yake kumuomba aniruhusu kwenda shule.

‘Lakini broo, hata akiwa nyumbani anaweza pia akafanya hayo unayohisi anayafanya huko shuleni, cha muhimu ni elimu, elimu ni wajibu kwa mzazi kumpatia mtoto wake, awe wa kike au wa kiume, hata dini zinatushauri hivyo...’akamwambia kaka yake.

‘Hiyo elimu aliyoipata inamtosha kabisa, kwa mtoto wa kike anataka nini zaidi, akizidi kusoma anakuwa na kiburi, angalia tangu alipofika hicho kidato cha tatu, akirudi hafanyi kazi anasingizia kuwa eti ana hiyo wanaita homework, kila siku homework, ni ujanja ujanja wa kipuuzi, ili asifanye kazi, hapo ni mwanzo tu, je akifika huko juu, itakuwaje,...’akawa kama anauliza na ndugu yake akawa anatikisa kichwa kwa kusikitika.

‘Sasa mimi nimeamua sitaki kusikia lolote, atabakia hapa hapa nyumbani kama ndugu zake wengine, hawo mabinti wengine wapo nyumbani, wana maadili mema, sijasikia maswala ya uhuni au umalaya, huyu kaenda shule, ndio kila siku kesi, kafumaniwa, kaonekana, sasa nitakuwa kazi yangu ni kesi, nitafanya kazi saa ngapi...’akasema baba .

‘Ndugu yangu, hayo ya kesi, ugomvi, ni majukumu ya wazazi wote, sio kwamba wengine hawakumbani na majukumu kama hayo,yapo, lakini wewe maamuzi yako sio ya hekima, kumzuia mtoto asisome, na wakati kafaulu, ni makosa makubwa sana, unamdhulumu mtoto haki yake...’akasema ndugu yake huyo.

‘Nimeshasema tusiingiliane katika maswala ya kulea watoto, sijafika kwako na kukulaumu kuhusu mambo yako, haya niachieni mwenyewe, nafikiri tumelewana, sina zaidi..’akasema kwa hasira na ndugu yake akashindwa na kuondoka.

Kwakweli hatua hiyo ya kukatazwa kabisa kwenda shule, iliniuma sana, nikawa mtu wa majonzi, hata machozi yakawa hayatoki tena, kwani kila nilipowaona wenzangu wakienda shule,niliumia sana moyoni,  nikabakia kumuomba mungu ashushe ehema zake, huenda baba akabadili msimamo wake, lakini hilo halikuwahi kutokea, na kila siku iliyopita ilikuwa ni aheri ya jana,..

‘Hivi mimi nina kosa gani hadi nitendewe hivi?’ nikajiuliza nikiwa nimejikunyata baada ya kuchoka na kazi za nyumbani, nilikuwa nimekonda, nguo ni zile zile, sitamaniki,....

‘Au ni kwa vile mama yangu hayupo hapa?’ nikazidi kujiuliza, lakini hakukuwa na majibu ya haraka, kwani huko mama alipo anapelekewa taarifa kuwa mimi bado nasoma.

Basi tena, ikabidi nikubali hali ilivyo, nikukijua tena mimi shule ndio basi, na kwahiyo hata maisha yangu ya baadaye yamefikia kikomo, kwani ni nani angelinioa mimi, kama wanavyodai wao,kuwa mimi ni muhuni malaya sina adabu, ni mwanaume gani atapenda kuoa mtu kama mimi, kila sehemu watu wameshaniona mimi ni mbaya, malaya muhuni, kwani mama alikuwa akimuhadithia kile aliyefika hapo nyumbani;

‘Mtoto huyu mimi amenishinda, ana tabia chafu, sijui kamfundisha nani, labda huko alipotoka, maana ni muhuni malaya, akifika shuleni yeye ndiye mwalimu wao...’akasema mama.

‘Lakini una uhakika na hayo unayoyasema mama nanihii....?’ akauliza jirani yake akitaka kunitetea.

‘Nafahamu yote, si alikuwa akisoma na huyo ndugu yake darasa moja, alikuwa akimuona. Kaka yake alikuwa akijaribu kumkanya, lakini hakusikia, yeye alimuona kwa mcho yake akimuona akitembea na wavulana hapo shuleni, na kwasaabbu ni kaka yake amdogo wake kikamponza kwa kusema siri za ndugu yake huyo, maana mtoto huyu alishafikia hatua ya kutembea na walimu...’akasema mama wa kambo.

‘Oh, ilishafikia huko, mbona bado mdogo sana, na haonekani kuwa hivyo...!’ akashangaa huyo jirani.

‘Ana udogo gani huyo, mwali mzima wa kuolewa, udogo ni wa umri tu, lakini kwa matendo hata mimi simfikii, anafahamu kila kitu, hebu muulize hapo, mamb anayoyajua ya mapenzi, uzazi, hutaamini....’akasema mama.

‘Lakini hayo ya uzazi, ni masomo yao wanayofundishwa mashuleni, ....mimi nijuavyo, watoto wa sekondari, wanafundishwa mambo ya uzazi, ni sehemu ya masomo yao, sio uhuni huo...’akasema huy jirani.

‘Wanafundishwa wakafanye mapenzi, vichakani na madarasani na walimu wao, mbona wenzao hawafanyi hivyo, ni tabia yake chafu tu, huenda ni ya kurithi toka huko alipotoka, yeye akifika shuleni, mazungumzo, matendo yake ni hayo, umalaya uhuni...’akasema mama.

‘Mhh, hayo makubwa, hata siamini, ni mtoto huyu huyu ninayemfahamu mimi, ...?’ akauliza

‘Sasa unahisi sisi tunamsingizia, ili tupate nini, angalia kaka yake huyo, wanayesoma darasa moja kafukuzwa shule, kisa eti kwa vile katoa siri za mahusiano ya dada yake na walimu wake. Ikabidi wamsingizie mtoto wangu huyo kuwa kafeli mitihani, wakati mtoto wangu ana akili, na wakati mwingine yeye ndiye aliyekuwa akimfundisha huyo dada yake...sasa na huyo naye utasema tunamsingizia, na akae nyumbani kama ndugu yake...’akasema mama.

 Baada ya mda nilikubaliana na matokeo nikamua kuendelea kutii amri ya baba,hata ule mtindo wa kuomba madaftari kwa wenzangu nijisomee, kuwa huenda baba akabadili msimamo wake nikarudishwa shule ukasimama, kwani waliligundua hilo nikapigwa amrufuku kuonekana nimeshaika madaftari, basi nikaona haina haja, ngoja nikae kama wanavyotaka wao.

Hata baada ya kutii kila wanachokitaka bado haikusaidia kitu, kwani mitihani iliendelea kuniandama,baba akaamua kabisa kutokuaongea na mimi, akanitenga, akiniona ni mimi ni kama kaona takataka fulani.Mwanzoni nilifikiria baba ananichukia kwa vile mimi ni mtoto wa kike, lakini mbona hakuwafanyia hivyo, watoto wa mama huyo wa kambo, kwanini hayo ananifanyia mimi tu.

‘Watoto wangu wenyewe wapo hapa nyumbani, hawasomi, wanasingiziwa hawa akili shuleni, ...’siku hiyo akasema mama.

‘Lakini kwenye mitihani yao ulikuwa ukifuatilia kama kweli wamefelishwa kwa makusudi...?’ akaulizwa.

‘Muda huo wa kufuatilia sina, waache wote wakae hapa nyumbani, kinachonisumbua ni watu kuniona eti mimi namnyanyasa huyu binti, kwa vile haendi shule, mbona hawaulizi kuhusu watoto wangu ambao wapo hapa nyumbani...’akasema.

Ikafika siku ya sikukuu, ambapo watoto wanatakiwa kuvaa vizuri na kufurahi na wenzao, baba hakutaka hata kuniona kabisa, kitu ambacho kiliniuma sana kuona baba ananitenga kiasi hicho. Nilihuzunika sana kuona,wenzangu wakiwa na furaha na shangwe, wananunulia hiki na kile lakini mimi nilikuwa kama sio mtoto wake wa kumzaa, nikabakia chumbani na kulia, hadi nikashikwa na usingizi.

Kwakweli nilijiuliza sababu ya msingi ya baba yangu kufanya hivyo sikuweza kuijua  mpaka sasa nimekaa kwa shida sana na kutengwa na asilimia kubwa katika familia bila kujua sababu ila sikutaka kufanya kitu chochote cha ajabu maana nilikua nampenda sana baba yangu. Nilijua baba anachofanya sio yeye, ni kutokana na mama, mama alijitahidi kupandikiza fitina, hadi moyo wa baba ukajaa chuki zidi yangu, kwahiyo, moyoni nikawa sina kinyongo na baba yangu.

Pamoja na yote hayo sikukata tamaa, maisha yakawa yanasonga mbele, hata hivyo kila siku mamb yalikuwa yakizidi, kila siku kunazuka jipya kubwa zaidi ya la jana, shida nazo zikawa zinazidi, mateso yakawa yanaongezeka, na kulikuwa hakuna wa kunitetea hata pale nilipojaribu kujitetea, hakuna aliyenisikiliza kabisa, ni kama vile walikuwa hawanitaki kabisa nionekane kwenye hii dunia,....

Siku moja nilitoka kwenda nyumba ya jirani nikiwa na mtoto wa kaka yangu wa kambo , nikiwa huko , mara akaja msichana wa kazi;

‘Dada unaitwa haraka nyumbani...’akasema huku akihema.

‘Kuna nini tena ...?’ nikauliza nikiwa na wasiwasi, na mwili ukaanza kuogopa.

‘Mimi sijui , nimeambiwa nikuite haraka uende nyumbani...’akasema
 Nikawaaga jirani zangu na kukimbilia nyumbani, nilipofika sikumuona mama wala baba, na hata yule mfanyakazi alikuwa hayupo ili nimuulize ni nani aliyeniita, na wakati naangalai huku na kule, mara ghafla kaka zangu wawili wakaanza kunipiga bila kujua sababu ya kipigo hicho.

Wakanibeba na kunipeleka chumbani, na wote wakaanza kunipiga bila huruma utafikiri wanapiga mwizi, hawakuangalia wanapiga wapi, kichwani, mwilini, ni kama wanataak kuniua, kwasababu ya kipigo cha muda mrefu nilianza ku tokakwa na damu, puani mdomoni, hadi sehemu za siri,  hadi nikapoteza fahamu....

NB: Je kuna kitu gani kilitokea,


WAZO LA LEO: Ukiwa peke yako jaribu kufikiri hekima ya mawazo yako, na uwaze kadri ya uwezo wako, na wakati unaongea na watu chunga sana maneno yako, kwani kauli ikitoka mdomono ni sawa na risasi, inaweza ikaua , ikajeruhi au ikaleta kitoweo, kitoweo ni mambo mema kutokana na hekima ya kauli yako. Twawatakia Ijumaa njema.

Ni mimi: emu-three

No comments :