Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, February 5, 2013

Uchungu wa mwana Aujueye ni Mzazi-56
‘Unasema ana uja uzito, sasa kama ana ujauzito mimi ndio dakitari, ….’akasema huyo Tajiri, huku akikunja uso, na lile tabasamu alilokuwa nalo usoni likawa limeyeyuka na uso ukabadilika na kujenga makunyazi, akageuka kuwaangalia mabaunsa wake, akitaka kuwaambia jambo, lakini akaghairi.

Mama mdogo, na Maua walikuwa wametulia wakimwangalia huyu jamaa, na waliona huenda muda wowote wakafukuzwa, na Mama mdogo, alijua kama asipofanya jitihada, anaweza asipate kile alichokitaka, akataka kufunua mdomo kuongea, lakini kabla hajasema kitu yule jamaa akasema;

‘Kwahiyo mnataka kusema nini?’ Yule jamaa akauliza na kumwangalia mama mdogo, wakati huo alikuwa akikwepa kabisa kumwagalia Maua, tofauti na alivyokuwa akifanya mwanzoni, ambapo kila mara akiwa anaongea, jicho lake lilikuwa halibanduki kumwangalia Maua huku uso ukimeta meta na tabasamu kilikuwa halibanduki mdomoni.

‘Sisi….tumekuja kukufahamisha, …..utasamehe kama lugha yetu imekukwaza. Sisi, yaani mwanangu hapa, ana uja uzito, na tuna imani kabisa ujauzito huo aliupata siku ile…..’akatulia mama mdogo, pale alipoona huyo jamaa akamwangalia kwa macho ya kutisha.

‘Siku ile ipi…….?’ Akasema Tajiri, akiangalia saa yake.

‘Siku ile ya lile zoezi..’mama mdogo akakatisha pale alipogeuka na kumuona Maua akimwangalia kwa mshangao. Kwani Maua aliposikia hivyo, mama yake akisema siku ile ya `zoezi’ akili yake ilimtuma kuwa, mama yake mdogo alikuwa akijua kila kitu kilichotendeka hapo, na ilikuwa imepengwa

‘Ina maana hilo lilikuwa zoezi na mama yake alikuwa akijua….’akawa akiongea akilini

‘Haiwezakani, na ni nani atawaamini maneno yenu…mnaweza mkafanya njama, kwa vile mnaona labda..’akatulia kidogo, na baadaye akaendelea kuongea,

‘Na…..na hili wengi wanakosea, mimi sio tajiri kiasi hicho, wapo matajiri bwana, mimi ninajihidi kadri ya uwezo wangu,na kidogo ninachopata ninajitahidi kushirikiana na wenzangu, lakini wale wenye akili dhaifu wanaona mimi ni tajiri, na kuniona eti ninagawa pesa….sio hivyo,….na wengi wanachukuliwa mwanya huo kunibambikia mambo kama haya….’akatulia na akapitisha macho kidogo kumtizama Maua.

‘Una maana gani kusema hivyo?’ Maua akauliza kwa sauti ya haraak haraka, ilikuwa suti ya mkwaruzo kama vile anaumwa kikohozi…au koo limekauka.

‘Sijaongea na wewe binti, …tukiongea watu wakubwa inabidi utulie kwanza, huo ni utomvu wa adabu…binti mdogo kama wewe unakosa heshima’akasema huku akimwangalia Maua kwa jicho kali.

‘Sasa hivi unaniona mimi ni mtoto…..eti binti mdogo, na kwa vile mimi ni mtoto na umeona hivyo, basi sheria itachukua mkondo wake, kwasababu ulinibaka, na sasa nina ujauzito wako…’akasema Maua.

‘Hahahaha…..umesahaueeh, unakumbuka ule mkanda, …ulijileta mwenyewe, ukawa unajilazimisha mwenyewe kwangu…..lakini hilo sio hoja sana, kama mnataka kwenda mahakamani njia ipo wazi, ..lini mnataka kupeleka hiyo kesi yenu, ….?’ Akauliza kwa dharau.

‘Sio hivyo, mzee…’akasema mama mdogo, na akasahau kuwa huyo jamaa huwa hataki kuitwa mzee, akasahihisha na kuita na kusema ; `sio hivyo Tajiri….’akaweka mikono kifuani kama mtu anayeomba jambo kwa unyenyekevu.

‘Ndio hivyo….’ Akasema kwa hamaki, na huku kamkazia mama mdogo macho, hadi mama mdogo akawa anaonyesha kuogopa, na kuwa kama anajikunyata.

‘Na mimi namuunga mkono kabisa huyu binti, kwani ni vyema haki ikafutwa, ..na sheria ikachukua mkondo wake, …nendeni mahakamani, na mimi nitawasaidia kumlipia wakili,….ili huyo mwenye hiyo mimba awajibike, au sio?’ akawa kama anauliza.

‘Mimba hii ni ya kwako, usijidangaye kukwepa, …na kama ukiikataa…..mimi nitaitoa,…’akasema Maua.

‘Safi sana…kumbe una akili….mimi sijali lolote utakaloamua, …’akasema huku akitoa tabasamu la uwongo, na dharau.

‘Nikuambie ukweli, ……wengi wameshawahi kuja kwangu kwa wazo kama hilo, nahisi wengine walifanya hivyo, na hata wengine hawakutaka hata kuniuliza,….wamefanya hivyo..sasa na wewe uamuzi ni wa kwako…nasikitika kwa hilo…natumai tumelewana, kama unahitaji gharama yoyote kwa hilo au lile la kwanza sema,…..’akatoa pesa mfukoni na kuziweka mbele ya meza, pale alipokaa Maua.

‘Mimi sijaja hapa kwa ajili ya pesa zako, ……wewe ulituma ujumbe kuwa unanihitaji nije tuonane, na ndio hivi nimekuja…’akasema Maua bila kujali, bila kumjali mama yake mdogo aliyekuwa akimfinya, ili asiongee hivyo.

‘Na, pili na hili la huu uja uzito, kwa vile umeniharibia maisha yangu, ….wewe unahitajika kuwajibika , uhakikishe unailea hii mimba hadi hapo nitakapojifungua,…na nikishajifungua, tutakwenda kupima,kama hii sio mimba yako, nitakulipa gharama zako zote, na kama ni ya kwako,….’akatulia kidogo.

‘Nitakulipa mara mbili….’akamalizia huyo tajiri, na kwa haraka, kama vile alikuwa kajiandaa kwa hilo, akatoa karatasi kwenye mkoba wake, na kalamu, na kuandika maelezo haya;

Mimi Tajiri….nimekubali kwa hiyari yangu, kuitunza mimba ya binti, ….Maua, hadi hapo atakapijifungua, na akijifungua, ili kuondoa utata, vipimo vya kutambua uhalali wa huyo mtoto vitafanyika, kama kweli huyo mtoto ni damu yangu, nitamlea, nitamhudumia kama mwanangu, na kulipa faini yoyote, lakini kama sio damu yangu, gharama zote nilizotumia atazirudisha……….’ Akaweka saini yake

‘Huu hapa ushahidi , ili kukuonyesha kuwa mimi sio mtu mbaya,….nimefanya hivyo kwa wengine, kwanini nikufanyie wewe ubaya…hata hivyo, mmmh, bado nitakuhitaji, …’akatabasamu,

‘Utanihitaji kwa lipi?’ akauliza Maua huku akiwa kakunja uso, na huku mkono mmoja akiwa kashikilia ile karatasi.

‘Bado wewe ni mfanyakazi wangu, umesahahu mkataba wa ajira,…leo hii nitahitaji kuitumia ile ofisi, na wewe unatakiwa uwepo kwa ajili ya huduma mbali mbali….’akamgeukia mama mdogo.

‘Naomba umuelekeze mwanao, ….kama mnataka mambo yaende kisheria basin a nyie timizeni wajibu wenu, la sivyo, naweza kubadilika….nitaitumia sheria hiyo hiyo, mkaenda kuozea gerezani, …na ngoja kwanza,….’akafungua mkoba wake na kutoa kanda za video mbili.

‘Maua nakuhitaji faragha, maana haya ni maswala ya mimi na wewe, ili kukuonyesha kuwa nakujali, na najali ubinadamu wako…’akasema huku akiingia chumbani kwake, na Maua akabakia ameduwa, na akili yake akakumbuka jambo, akautizama mkoba wake, na kukumbuka kitu, bila kumwangalia mama yake akamfuata huyo Tajiri wake na kuuchukua ule mkoba wake.

Alipofika ndani akamkuta yule Tajiri akiwa kakaa huku kashikilia zile kanda za video , akiwa anazichezea chezea mkononi, akageuka kumuangaliana Maua.

‘Mimi sipendi ugomvi, wala uhasama na watu, hasa warembo kama wewe…sioni haja ya wewe kubeba kisu,..kisu cha nini, unataka uniue, kwa kosa gani nililokufanyia, hayatoa hicho kisu, njoo nichome nacho…’akasema na kumuacha Maua akiwa kaduwaa, hakujua ni kwa vipi huyo mtu kagundua kuwa aliweka kisu kwenye mkoba wake.

‘Nilisahau nikaja nacho…’akasema Maua akionyesha uso wa kushangaa.

‘Haina shida mrembo…mimi sina ubaya na wewe, na nasikitika sana kwa hayo yaliyotokea, …huenda ndivyo, ..lakini wakati mwingine nafsi inajuta, ….nakumbuka siku ile sote tulikuwa tumelewa, lakini mimi nalewa mara nyingi, sihamaniki,…sipotezi ufahamu na kufanya yasiyotakikana, ….hata hivyo pombe  ni pombe, pombe haina rafiki…’akawa bado kashikilia zile kanda za video.

‘Nilipoangalia tena hizi kanda za video, kuna kitu kimekuwa kikinisuta, na kujiuliza yote haya ni ya nini,…ni kwa ajili ya kupata utajiri, mbona utajiri ninao, …nataka nini tena,….hapana nikaoana kuwa haya yanatosha, kama ni utajiri wa zaidi, hautanisaidia kitu….’akawa macho yake yameangalia kwenye mkoba wa Maua.

‘Mimi sioni haja ya kukuumiza zaidi, naomba utoe hicho kisu chako, unichome hapa,..’akaonyesha kidole chake kwenye moyo wake, na huku akimsogelea Maua.

‘Ili moyo wako utulie..au sio…hata mimii nimechoka, nimechoka kutenda makosa, madhambi, dhuluma,..na wengine wananiita eti mbakaji,…..sikumbuki kubaka, kwasababu nina ushahidi, kwa hatua, kwa kila jambo langu, nakuwa na kumbukumbu….huenda hata hili litakalofanyika hapa, litakuwa na kumbukumbu yake….’akaangalia juu.

Maua naye akaangalia juu, akaona kitu kama kinamulika, kipo kama tochi, hakuelewa kina maana gani, lakini akili yake ikamkumbusha picha za video alizowahi kuona kuwa kwenye chumba kunaweza kuwekwa kitu kinachonasa matukio, na ukifanya jambo unaonekana, akashituka..

‘Kwahiyo ina maana umefanya hivyo, ili kujihami,….?’ Akauliza Maua.

‘Sio kujihami, hiyo ni kawaida yangu…popote ninapokwenda ninakuwa na wataalamu wangu wa kuweka kumbukumb u zangu, sina shida, siogopi, kwanini nifiche, …’akasema.

‘Sasa kwanini safari zako za kuja huku ni za kificho, …na hukai hoteli moja kwa muda mrefu,…?’ akauliza Maua.

‘Hayo ni mambo ya kawaida, pamoja na hayo, bado nina maadui…hawo maadui hawajali sheria…hao ndio nawakwepa, lakini sikwepi sheria…ndio maana naweka ushahidi….’akazingalai zile kanda.

‘Siku ile niliuaharibu ule mkanda ulionionyesha, hiyo mingine imetoka wapi?’ akauliza Maua huku kashikilia mikono mbele bila kuogopa.

‘Mikanda kama ile inawezekana kitengenezwa mingi….lakini nimena kwako wewe haina haja, nitaharibu kumbukumbu zako, na hizi ni mikanda nilizokuwa nimerokodi, na..kama tutakubaliana nitakukabidhi, uziharibu mwenyewe, na ungelikuwa mtaalamu wa mitandao, ningekuonyesha wapi kulipokuwa na hizo kumbukumbu ukaizifuta zote….’akasogelea komputa yake.

Mkono wa Maua ukawa unatikisika kwa hasira, kuna kiu kilikuwa kikimuhimiza afanye lile alilokuwa kakusudia na hakikujali kuwa kuna kumbukumbu, …hakikujali kuwa kufanya hivyo, kutamletea matatizo, 

‘Unaogopa nini, maisha yako yameshaharibiwa, na aliyeharibu ni huyo hapo, tumia nafasi hiyo, ukimaliza, vunja kila kitu…’sauti ikamwambia.

‘Sogea hapa kwenye hii komputa uone wapi ninapohifadhi kumbukumbu zangu,…..unaona hata haya yanoyotea hapa, yanahifadhiwa humu, unaona…..’akawa anaonyesha. Na Maua macho yake, yakawa yanaangalia yale matukio ya liyotokea siku ile…

Akaanza kutetemeka, ….akahisi mwili ukibadilika, akajaribu kufunua mkoba wake, ili aichukue ile dawa, lakini hakuiona, akaanza kubadilika,…..sauti isiyo yake ikatokea.

‘Sasa nimekuaj mwenyewe, nimekuja kulipiza kisasi….kwa mtendo uliyomfanyia kiti wangu…’sauti nene ya kiume ikaongea. Tajiri, akageuka huku na kule kutafuta wapi sauti inapotokea, hakuona mtu mwingine zaidi ya Maua.

Alishangaa, alipomtizama Maua, sio yule Maua aliyemjua, sura ya mvuto, na macho ya malegavu kama alivyopenda kuyaita, na kuyaona, hayakuwepo tena…..kilichoonekana ni macho meupe, macho yaliyojaa hasira na uchu wa kuua, meno yalikuwa yametokeza nje, na hata mate kumtoka mdomoni, ….

‘Kumbe wewe ni shetani…..’aaksema huyo Tajiri

‘Hahaha….wewe hujioni, wewe nishetani zaidi ya ibilisi, mangapi mbaya uliyowahi kufanya ,ambayo hata sisi mashetani hatukuwahi kuyafanya…umesahau, ..umefanya mabaya mangapi, umeua watu wangapi, umebaka watu wangapi..ili tu uweze kupaat utajiri….eti ili upate utajiri mpaka upate vigoli, upate mwili wa binadamu,…huo ni ushetani, huo ni zaidi ya ushetani….’sauti ile ikasema.

Tajiri, akahisi hatari, akawa anasogea nyuma, na Maua akawa anamsogelea, …hadi wakafika mwisho, nyuma ni ukuta, na meza, …..Maua kwa haraka akatoa kile kisu kwenye mkoba wake….

‘Sasa leo ndio mwisho wa yote hayo, unahitajika uje huku kuzimu, tukawe pamoja….’ile sauti ikasema …

‘Hapana…nisameheni, sitarudia tena, nitahakikisha namuoa na kumtunza huyu ….wewe. huyo binti…’akawa anasema huku akili yake ikikumbuka ahdithi za mashetani, kuwa mtu anaweza akatwekwa an mashetani, akaabdilika na kuwa kama hivyo, na kwahiyo huenda Maua ana hayo mashetani, na asipoyabembeleza anaweza kuuwawa…

‘Semeni mnataka nini……?’ akauliza akili ilipokumbuka mambo hayo ya mashetani.

‘Tunataka roho yako…..’Maua akainua kile kisu juu

**********

NB: N I kazi sana kuandika sehemu kama hii asubuhi asubuhi, kwani ina mambo mengi, lakini sehemu hiyo inatosha kwa leo

WAZO LA LEO: Uzuri wa sura, katu hautadumu , lakini uzuri wa tabia, matendo mema, hudumu milele. Tujitahidi kuwa wema wa tabia, na kutenda matendo mema.

Ni mimi: emu-three

3 comments :

Mumy victoria said...

Hongera sana miram mimi sikosi hata siku moja kuangalia blog yako maana napenda sana hadithi pia unajitahdi kuandika hadith ndefu hakika inabamba big up!

emu-three said...

Nashukuru sana Mumy Victoria, na nakukaribisha sana tuwe pamoja na wewe kama una kisa chochote kilete , hata kwa ufupi, mimi nitajua jinsi gani ya kukiendeleza....TUPO PAMOJA

Mumy victoria said...

Waoo nashukuru miram kuna kisa kimoja kinasikitisha sana kimemtokea frnd wangu ntajitahidi nikupe hata kwa ufupi naamini kitawasaidia sana wasichana.pia nakumbuka kuna kipindi nilisoma blog yako ukatuomba radhi kuwa comp ya ofcn uliyokuwa unatumia umeachishwa kazi hukuruhusiwa kunyonya hata hadith zetu najua ushapoa lkn nilisikitika sana nawish sasa una yako pole sana pia kumbuka ubinadamu kazi? ilike ure blog sana