Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, August 22, 2011

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli-18‘Unauhakika na unalosema Docta, kwasababu shutuma hiyo ni kubwa sana, na kama itafuatiliwa ionekane sio sahihi unaweza ukafikishwa pabaya…’ akasema mganga mkuu wa hospitali ya serikali, na mbele yake walikuwepo madocta wakuu wa vitengo mbalimbali na pia alikuwemo mkuu wa ulinzi
‘Mimi nimewasikia wakiongea na bahati nzuri wakati wanaongea hawakuwa wakiniona, kwahiyo kama ingekuwa uongo, wangeuongopa wakijua kuwa nipo, lakini hawakujua kabisa kuwepo kwangu hapo, na hata walipogundua kuwa nipo na nimewasikia, yule nesi mwingine alikuwa kashika sinia la vyombo, likamponyoka kwa woga….sasa ni kweli au sikweli inatakiwa kuwaulizia wao wenyewe , lakini kama niwajuavyo watakana futi mia, labda muwahusishe polisi wao wanajua jinsi gani ya kuwabana vyema..’akasema Rose.
‘Mimi naona haina haja ya kuwahusisha polisi haraka kihasi hicho, kwanza hili swala bado lipo mikononi mwetu, na kama tutashindwa tutafanya hivyo,…kwanza napendekeza kujichunguza wenyewe, ili tujua kiini cha haya matukio, tukianzia na huyo mgonjwa tuchunguze kuona kapoteaje, maana sio mara ya kwanza kusikia tuhuma kama hizi, na mimi nilitaka kulifuatilia hili kipindi fulani mkanizuia, na nisingependa kitengo change kiwe kinahusishwa mara kwa mara na mimi nisichunguze na kugundua uzaifu huo upo wapi, na hata kama ni mimi siwajibiki nitakuwa tayari kujiuzulu, naona wakati huu ndio wakati muafaka, ili kuondoa hili doa katika hospitali hii….’ Akasema mkuu wa kitengo cha ulinzi.

‘Sawa…mkuu, lakini huko naona umekwenda mbali, sana hatujafikia kunyosheana kidole, na nakubalina na wewe ila nilitaka kumuondoa huyu eeh, Docta…kwani kwa minajili hiyo hili ni swala la ndani, na huyu sio mfanyakazi wetu hastahili kuwepo’ akasema yule mkuu wa ile hospitali na kumgeukia Docta Rose, `Ila Docta Rose nilitaka kuliweka sawa kwako kujua uhakika wa hiyo shutuma…tunakuomba utupishe…’ akawageukiwa wengine na kusema, `Sasa kwahiyo mnakubaliana na Docta Rose, kuwa hilo kweli limetokea na linahitaji kuwajibika sisi wenyewe ndani ya hospitali, maana nilitaka kwanza alithibitishe kwanza Docta Rose, yeye mwenyewe kwa mdomo wake kuwa anauhakika na anachokisema, kabla hatujaingia ndani ya kiini chake chenyewe,…ok’ halafu akamgeukia tena Docta Rose na kusema ‘Sawa Docta Rose, nakuomba hili swala utuachie, na tukikuhitaji tutakuita, samhani sana kwa hilo, …’ akasema yule mganga Mkuu na Rose akainuka kuondoka.

Hata Rose alipofika kazini kwake hakuwa na moyo wa kutulia, alikuwa katoneshwa pabaya, `Ina maana huyu mtu kama kafa kweli basi watakuwa wao hawa hospitali ya serikali kwa namna moja wamehusika kumuondoa duniani, na kwanini wafanye hivyo…?’Akajikuta anaongea mwenyewe kama mtu aliyechanganyikiwa na akafikia hata kuamini kuwa huenda huyo jamaa hajafa….`lakini hata,… bado kuna mashaka,…’ Alipowaza hivyo, haraka akakimbilia ofisini kwa Docta Adamu kutaka kupata mawazo kuhusiana na wazo lake hilo jipya , lakini cha ajabu hata alipomhadathia Docta Adam nini amewaza, mwenzake alifikia kumkatisha tamaa kabisa, kuwa huyo mtu keshakufa, ndio maana wenzake hawakutaka kulifuatilia zaidi,..akamkazania ajiandae kwa safari ya kwenda kusoma, na ikiwezekana wapange maisha ya baadaye pamoja, aliposikia hivyo akaona heri ajiondokee nyumbani ili atafute njia zake mwenyewe za kugundua nini kimetokea kwa huyo mgonjwa.

‘Wewe na mambo yako bosi, safari, safari…imekuwa wimbo, na…hilo la mipango ya baadaye na mimi sahau…moyo wangu upo kwingine kabisa, najisikia sana uchungu na kujiona nimefanya kosa, kumtelekeza yule mgonjwa, na kama kafa kweli, sijui…lakini moyoni nahisi kama bado yupo hai….’ Akasema Rose, huku akitoka nje, na kumuacha Bosi wake kashika shavu akimwangalia kwa makini…na kusema ‘Wewe wangu tu…huyo keshaondoka duniani….’

Siku ya pili yake akawa anatembea ufukweni hakuwa na sababu ya mazoezi, ila alitaka kupunga upepo, na alipofika kwenye mti uliokuwa na kivuli akaona mtu amelala , akiwa kajikunyata sana, inaonekana alikuwa akitetemeka baridi na hakuna mtu aliyemjali. Akamsogelea na kabla hajamgusa mara akasikia yule mtu akiongea maneno kwa sauti ya chini na maneno hayo yaliyomshitua sana Rose, na kusononeka moyo wake.

‘Ohhhh, Sweetie….umeamua kuniacha nife…nilikuomba unilinde, leo nakufa kwa mateso makubwa, …bila hata kosa, hebu niambieni nimekosa nini, nina kosa gani mimi, mnanipiga kama mwizi , mnaniunguza na nyaya za umeme, mnanitesa, eti nikiri kuwa mimi ni gaidi….jamani…halafu hamtaki hata kunitibia…Sweetie upo wapi , sweetie….’ Mara yule mtu akalala na kunyosha miguu, na mara akawa kama anatingishwa, kama vile mtu anayetaka kukata roho. Rose akamsogelea haraka akaanza kutoa huduma ya kwanza, na mwishowe aliamua kutoa koto lake la udakitari na kumvika yule mtu ili apate ujoto.

Baadaye aliomba msaada kwa watu waje wamsaidie, na usafiri ukatafutwa wa haraka, na yule mgonjwa akafikishwa hospitalini kw Docta Adam. Na kwa muda ule alipofikishwa mgonjwa docta Adam hakuwepo, Rose kama msaidizi wake akatoa amri kwa madakitari wengine kumuingiza chumba cha wagonjwa mahututi, na kazi ya uchunguzi na vipimo mbali mbali ikafanyika haraka, …na baadaye docta Adam alifika na kuwakuta Madocta wake wakiwa wanamhudumia huyo mgonjwa, naye bila ajizi , akijua ni mgonjwa mahututi anahitaji huduma zaidi, akaingia kazini, hadi pale mgonjwa alipooekana yupo katika hali ya kuridhisha na kupelekwa kwenye wodi ya wagonjwa wa kawaida.
‘Hebu docta Rose, huyu ni nani, maana mimi nimefika nikakuta mumeshaanza matibabu, nahisi kama niliwahi kuiona hii sura kabla, hebu nipe muhutasari wake kidogo….kiukweli huyu mgonjwa, kama asingewahishwa hapa mapema, ….mmh, kwanini watu hawa wanasubiri mpaka mgonjwa anakuwa mahututi , …..unaona ilivyo ana imonia kali kweli, ana malaria kali , ana….kila gonjwa analo, na nilikuwa na wasiwasi wa TB, lakini naona hilo halipo, kwahiyo ni magonjwa ya kawaida nahisi baada ya sindano hizo kuisha atakuwa na hali njema….poleni sana wataalamu wangu’ Akasem Docta Adam.
‘Ki ukweli labda niseme nahisi kuwa ni nani,maana nilivyomkuta katika ile hali, sikutaka hata kuangalia kuwa ni nani , nilichojali ni kuokoa maisha yake, kwani alikuwa katika hali ya mbaya, kama ya kukata roho ……’ akashindwa hata kumalizia.

‘Huyu sio yule mgonjwa aliyetoroka… , ambaye kwa mara ya mwisho ulisema kuwa umeambiwa kuwa keshakufa….au wanafanana tu..’ akauliza Docta Adam.
‘Hata mimi nahisi hivyo, ila kama ni yeye kapigika kweli, maana kawa mzee, kaisha sana, utazani ana TB, …’ akasema Rose.

‘Lakini sizani kama ni yeye, yule ulishaambiwa keshakufa…lakini huenda ni yeye…sura ni yake, …ila kaisha…kama kweli ni yeye, amepitia hali ngumu sana. Unajua ile jela haifai wka maisha ya mtu, halafu matibabu yenyewe nahisi hakuwahi kupata ya kutosha, lazima atakuwa hivyo….sasa nahisi mzigo, unatujia tena, nashindwa hata kuwalaumu, maana huyu ni binadamu na hali kama hiyo, hata angekuwa nani angejitolea kumsaida, naomba faili lake liwekwe kwenye watu wanaohitaji wahisani wa kujitolea kumsaidia na docta Rose, naomba ujaribu kuwasiliana na wafadhili wetu na kutoa tangazo kutafuta wahisani wa kujitolea, maana hapa nilipo sina ujanja, lazima tuombe msaada…’ akasema Docta Adam.

‘Docta Adam, hata mimi niweke kwenye orodha ya watu wanaojitolea, nipo tayari kukatwa kidogo kidogo kwenye mshahara wangu, …’ akajikuta Rose akitamka hayo maneno na baadaye akashituka na kujiuliza moyoni kwanini katamka vile.
‘Acha mzaha Docta Rose, hayo matibabu yake unajua ni kiasi gani, hapo bila wafadhili hatuwezi …wewe fanya nililokuambia,…na kama inavyoonekana anahitaji bado uchunguzi wa kina, na unakumbuka, kama kweli ni yeye, alihitajika kufanyiwa CT-scan, achunguzwe kichwa, ….huku tunaweza kugundua vyema kuna nini na unajua kipimo hicho kilivyo na gharama. Mimi sikatai kumsaidia na mpaka hapa tumesaidia vya kutosha, vyema tusaidie na sisi tusaidiwe, na kama wapo watu ambao wapo tayari hujitolea, kwanini tusiwaombe hawo, ili kuipunguzia mzigo…’ Akasema Docta Adam

‘Sawa Bosi nitalifuatilia hilo, lakini bado nasisitizia kuwa naomba mimi name niwekwe kwenye watakaojitolea, na…tusitulie kuendelea na matibabu yake mengine kwasababau ya kuogopa gharama, mimi nitamdhamini kwa hapa….’ Akasema Rose na kuondoka kufuatilia hilo aliloagizwa na bosi wake. Bosi wake alibakia akiwa ameduwaa na kumuwaza Rose, halafu akamgeukia yule mgonjwa kumwangalia kwa makini, huku moyoni akisema ina maana kuna kitu fulani kinamgusa Rose kuhusu huyu mgonjwa, sio jamaa yake, hamjui kabisa, lakini kaamua kujitolea kwake kama jamaa yake…mabadliko ya ajabu sana haya,…na namuona kila mara anapokutana na huyo mgonjwa anabadilika kabisa,…mmh, hapa sasa kuna jambo na nina uhakika kuwa ni yule mgonjwa karudi tena, na hii ina maana tatizo lile la mwanzo limerudi tena mezani kwangu, na inavyoonekana Rose hataweza kuambiwa lolote, kuhusiana na huyo mgonjwa mapaka apatiwe kinachohitajika…ok, tutaona hili.

Akaondoka pale wodini akikuna kichwa huku anaongea kimoyomoyo akisema ‘Iliyobakia ni kuhakikisha huyu mgonjwa anapewa huduma zote kama alivyodai Rose, na bili yote itawekwa katika jina lake, na ilivyo, matibabu ya mgonwa kama huyu gharama zake zitakuwa kubwa sana na Rose hataweza kuzilipia…’ akakuna kichwa kuwaza zaidi, akagongesha vidole na kutoa sauti ta taa, kama vile kakumbuka kitu au kagundua wazo la muhimu. Akaondoka hadi ofisi ya mhasibu na kumpa maagizo kuwa bili ya huyo mgonjwa iwekwe kwenye jina la Rose kama mdhamini, na ahakikishe anamsainisha Rose kwani kakubali kumdhamini.

Baadaye aliondoka pale kwa mhasibu na kurudi ofisini kwake huku akiwaza mpango wake huo utakavyofanya kazi, ingawaje…akawa anaingiwa na mashaka na mpango huo akasema kwa sauti `Ninauhakika mwisho wa siku Rose atakuja kwangu kunipigia magoti kuwa gharama hataiweza mwenyewe, labda awe kawapata hawo wafadhili…lakini vyovyote iwavyo, kazi ya kuzikusanya hizo hela za msaada ni kazi nzito inahitaji uzoefu wake, lazima atakua kumomba msaada na hapo nitamweka sawa,….’ Akatabasamu alipofikiria wazo hilo.

Rose alipofika nyumbani kwake akawa kamkuta jirani yake Docta mwenzake, rafiki yake, hajaondoka, akamhadathia nini kinachoendelea kuhusu huyo mgonjwa na kumuomba akifika ajaribu kuwa karibu na huyo mgonjwa ilia pate huduma zote. Mwenzake akamwangalia kwa jicho la kushangaa, na kwa vile hakuwa na muda wa kuongea zaidi yeye akamkubali, lakini mwishowe akaongeza maneno na kusema;

‘Kweli sasa naamini maneno ya watu kuwa apendaye haoni….’ Akacheka kicheko cha kebehi na kundoka, huku Rose akiwaza huo usemi, akijiuliza akilini ina maana kweli analofanya ni kwasababu ya kupenda, ina maana kweli amegubikwa na mapenzi, hapana siwezi kujiingiza tena kwenye mateso, kwanini niteswe na watu, eti kwasababu ya kupenda, ina maana unaweza ukapenda wakati mwenzako hakupendi, sasa ina maana gani, je mapenzi yanaweza kugeuka kutoka kupenda kwenda kwenye chuki, kwanini mapenzi, na chuki….baadaye akatabasamu, akijaribu kuivuta ile sura ya yule mtu ambaye anadhania kuwa anampenda, lakini sasa haikuja ile sura ya kawaida, ya mvuto, ilikuja sura ya mtu aliyekonda, akionekana mdhaifu, mzee kalala kitandani hajiwezi…akakuna kichwa na kusema, ni swala la muda tu atarudia hali yake kwasababu…sura ile ikawa inatawala ubongo wake, sura ya mtu aliyekwisha kabisa na anachosubiri na kusaidiwa tu…..
********
Wakati huo kule hospitalini kwenye moja ya kitanda, alikuwa kasimama Docta Adam, akimchunguza yule mgonjwa , na alipohakikisha mambo yamekwenda vyema mara akaingia yule docta, jirani yake na Rose, akasalimiana na bosi wake, halafu akamchungulia yule mgonjwa, na baadaye akamgeukia Bosi wake ambaye alikuwa kasimama nyuma yake akimtizama kwa makini, na wakawa sasa wanangaliana na Bosi wake, hawakuongea, waliendelea kuangaliana kwa muda na baadaye yule docta akatizama chini, na kujifanya anamtizama yule mgonjwa, na hapo Docta Adam, ageuke kutaka kuondoka.

‘Bosi kwanini umeniangalia sana, na baadaye unaondola bila kusema neno, ina maana sisitahli kuongeleshwa, na wewe ulikuwa ukimpima mgonjwa, hutaki hata kunipa taarifa zake, ndio najua sio kazi yako kunipia hiyo taarifa , lakini nimesikia mwenzangu ana dharura kaondoka mapema…sasa bosi,…mbona …ooh, sijui nisemeje..’ akajikuta akikosa la kuongea.

‘Nakusikiliza wewe, maana ulivyokuja, na ulivyovaa, haiendani na kazi yako, hiyo ndio sare ya kazi, usifikiri nilikuwa nakuangalia tu, nilikuwa nawaza mengi hususani nidhamu ya hapa hospitalini inavyozidi kupungua siku hadi siku, mnashindwa hata kuniheshemu, ….wewe ulivyokuja ulitaka mimi nikupe hiyo taarifa, kwasababu mwenzako hayupo, ndio utaratibu wako uliojiwekea au sio….kwanza tuonane ofisini, na hali ya huyo mgonjwa inahitaji vipimo vya haraka vya TC-Scan, tuangalie huko kichwani kuna nini, lakini tunamuhitaji mdhamini wake…’ akasema huku anaondoka.
‘Nani mdhamini wake Bosi…?’ akauliza akijifanya hajui.

‘Rose…mpigie simu haraka aje’ akajibiwa kwa mkato.

Rose, alipata taarifa kuwa anahitajiwa haraka hospitalini kuhusiana na mgonjwa wake, aliposikia hivyo hakukawia haraka haraka akafika na akaambiwa kuwa anahitajiwa kusaini bili yake ya udhamini , kwani mgonjwa wake anatakiwa kufanyiwa kipimo cha bei mbaya, na haiwezekani kifanyike hivi hivi bila kuwa na uhakika, angalau hata mdhamini au kuwa na njia yoyote ya kufidia hiyo gharama.

‘Sawa lete hiyo bili nitasaini hakuna matatizo..’ akasema Rose, na kuisaini ile bili hata bila ya kuangalia ni gharama kiasi gani. Hata yule mhasibu akashangaa na kumwangalia Rose kwa makini kwa macho ya huruma , na baadaye akamuuliza Rose, imekuwaje akakubali kubeba huo mzigo, na gharama za huyo mgonjwa ni kubwa, zinaongezeka siku hadi siku, ana uhakika gani kuwa huyo mgonjwa atazimudu ukizingatia haijajulikana anatokea wapi au anafanya kazi gani.

‘Usijali, …mmh, hilo litakuwa deni katika mshahara wangu, ..deni halimfungi mtu…’ akasema na kuondoka kuelekea wodini kule alipolazwa mgonjwa wake. Alipofika pale kitandani akakuta kila kitu kipo tayari na mgonjwa alikuwa katayarishwa kwenda kufanyiwa hivyo vipimo, ilivuoonekana mgonjwa alikuwa keshazindukana, kwani alimkuta anaangaza macho huku na huko, akiwa kama anajaribu kujiuliza hapo yupo wapi.

Rose alifika pale kitandani na kumwangalia kwa makini, lakini yule mgonjwa alikuwa akitizama sehemu moja halafu anageuza shingo anatizama sehemu nyingine na baadaye akamtizama Rose, alimtizama kwa muda bila kusema kitu, na Rose akamsogelea na kumuinamia karibu yake.
‘Unajisikiaje mgonjwa…?’ Rose akamuuliza.

‘Unasema, ….?’ Akauliza yule mgonjwa kama vila hasikii nini anachoulizwa, halafu baadaye akasema `Sijui najisikiaje, kwani naumwa nini…sijui nijisikiaje , kwani wewe nani?’ akauliza yule mgonjwa akionyesha uso wa mshangao.

‘Mimi ni Docta Rose, na …’ akasema Rose huku akijaribu kutafakari nini cha kumwambia huyu mgonjwa , na pia alikuwa akiwaza kiundani kutafakari tatizo la huyu mgonjwa litakuwa ni nini, nini kiini cha hilo tatizo, huenda hicho kipimo kikasaidia sana…
‘Unasema unaitwa Docta Rose, lakini hujavaa kidakitari, ndio maana nikakuuliza, nilidhania wewe umekuja kumtizama mgonjwa wako kama wengine…mimi naona sina ndugu wa kunisalimia…sijui ndugu zangu ni nani, nitawauaje wakati hata mimi mwenyewe sijijui ni nani…’ akasema huku anawaangalia watu mbali mbali wakisalimia wagonjwa wao.

‘Mimi mgonjwa wangu ni wewe, na pia ni ndugu yako, ndio maana nimekuja moja kwa moja kitandani kwako kukuangalia, sijaja kama dakitari, kwani leo nipo mapumziko , kwahiyo usijali sana, tupo pamoja, nimekuja kwa ajili yako tu…’ akasema Rose.

‘Nashukuru kama ni hivyo, maana …sijui ilikuwa ni ndoto, au ni kweli ila nahisi nilikuwa nateswa sana, napigwa, nachomwa na umeme…sijui ni akina nani hawo wenye unyama wa aina hiyo, na kwanini wanifanyie mimi hivyo,..nahisi kama ilikuwa ni ndoto, ndio maana nilikuwa naangalia huku na kule, kuhakikisha kuwa kuna usalama, vinginenyo ningetoroka…’ akasema yule mgonjwa.
‘Nakuomba usije ukafanya hivyo…Usijali hayo utayakumbuka polepole, na siui wewe unaitwa nani vile…?’ akauliza Rose kwa kumtega.

‘Mimi sijui naitwa nani, lakini …hapana, sikumbuki jina langu…na sikumbuki kumetokea nini, na kwanini nipo hapa hospitalini…wewe umesema mimi ni mgonjwa wako, ilikuwaje, nilipata ajali, nili…au nilizama majini…’ alipotamka hilo la kuzama majini akawa kama kaguswa na kitu akawa anakodoa macho tu kwa muda mrefu.

‘Kwanini unasema ajali au kuzama majin?’ akauliza Rose.

‘Nahisi kitu kama hicho na nikiwaza kuzama majini, nahisi kama masikio yakiwa yamejaa maji…
masikio yangu nahisi yana maji, au kichwa kina maji…’ akasema na kujaribu kukitikisa kichwa.
‘Sawa, hilo tutaligundua muda sio mrefu…kuna kipimo kinatakiwa kuchukuliwa,…’ akasema Rose.
‘Kwani hapa ni hospitali ya serikali, ….maana siui gharama zitakuwaje, kama sikosei …na naiona hii hospitali kama sio ya serikalini..?’ akawa anasema huku anaangalia huku na kule.
‘Ni kweli hii hospitali siyo ya serikali ni ya mti binafsi, lakini hilo lisikusumbue kichwa, kuna watu wapo tayari kujitolea, kwa watu kama nyie, baadaye tutaangali ukipona, kama utamudu kuzirudisha hizo gharama au la…lakini kwasasa usiwe na wasiwasi na hilo..nitalisimamia mwenyewe..’ akasema Rose.

‘Nashukuru sana, wewe ni mtu mwema sana na inaonyesha una huruma ya ajabu, na sijui nikuite nani…naona nikuite Sweetie..’ akasema yule mgonjwa na kumwangalia Rose kwa macho yaliyoonyesha kuchoka, lakini yakiwa na uhai fulani!

‘Sweetie….!,mmmh, kwanini uniite Sweetie?’ Akauliza Rose huku akionyesha uso wa mshangao na huku anatabasamu.

‘Kwasababu kwanza sijui jina lako,….’ Akawa kama anafikiri halafu akaendelea kuongea kwa kusema `….Na hilo jina limenijia tu kichwani mwangu, nahisi kama niliwahi kulijua kabla au ni kwasababu wewe unavyoonyesha upendo wa kweli…labda niite hivyo, na kama wanadamu wote wangekuwa kama wewe, duinia ingekuwae na raha sana, kama sio kisiwa cha amani! Nakiri kuwa wewe umenionyesha kuwa unanijali hasa kipindi kama hiki ambacho sijijui…na naweza kusema wewe ni rafiki, rafiki wa kweli…nashindwa hata nikuelezeja’ akawa anazungumza haya huku machozi yakimtoka, sijui ni kwasababu gani. Na Rose akatoa leso yake na kumfuta,..na hapo yule mgonjwa akasema ‘Ahsante rafiki wa kweli, Sweetie….’.

‘Sweetie, ndilo jina lako toka sasa, kama hutojali nitakuwa nakuita hivyo, na naahidi kuwa kama nikipona, nitalipa ghrama zote hizi, nitahakikisha naizirejesha, hata kama ni kwa kufanya kibarua, au popote, …nahisi kuwa uwezo huo upo, ingawaje sijui kwa vipi, lakini nahisi nilikuwa na kazi fulani…sina uhakika, maana kumbukumbu hazipo..ila hilo nikuahidi…Sweetie…’ akasema yule mgonjwa na kutoa tabasamu. Tabasamu ambalo liliganda kichwani mwa Rose,…na hapo Rose naye akatoa lile tabasamu lake adimu ambalo lilikuwa limetoweka miaka mingi, na hata kabla hawajapata nafasi ya kuongea zaidi, mgonjwa akachukuliwa kupelekwa chumba cha vipimo, huku Rose akiwa kabakia pale wodini akiwaza hilo jina jipya alilopewa, la Sweetie…..

‘Mhh, Sweetie…’ akasema huku akiwa kaweka shingo upande akiwaza.
NB, Ndugu wapendwa je huyu mgonjwa atapona, na jina Sweetie lina siri gani, ngoja tuingie sura ya tatu ya kisa hiki, kwa kurudi upande mwingine wa tukio hili, kule kwa akina kwa akina Maua na Maneno.

Ni mimi: emu-three

3 comments :

Anonymous said...

Pam said...
duh navuta pumzi kweli turudi kwa maua umeniwahi nilikuwa najiuliza kuhusu hao wa upande mwingine
August 22, 2011 11:36 AM

Mimi said...
jamani dear mbona umeruka ukurasa umetupeleka sehemu ya kumi na tisa badala ya kumi na nane. hadithi inazidi kuwa tamu. ubarikiwe sana. asante pia kwa kutupa burudani, tunaburudika na kujifunza pia. keep it up.
August 22, 2011 12:05 PM

Pam said...
m3ni sehemu ya 19 au 18?? rekebisha kimya kimya.
August 22, 2011 12:58 PM

samira said...
nzuri na inavutia
mauwa duh tulikuwa tumemsahau
big up m3
August 22, 2011 1:38 PM

emu-three said...

Nashukuruni sana kwa kunishitua kweli niliruka ukurasa, na kweli ulikuwa ukurasa wa 18 na 19, lakini nimeufupisha ukawa ukurasa mmoja, tutaendeela na sehemu ya 19, kwa kurudi kwa akina Maua na Maneno msijali sana TUPO Pamoja...SWAUMU KALI

chib said...

Swaumu kali! Pole Mkuu, ha ha haa