Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, August 17, 2011

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli-16
`Masikini jamaa wa watu, mimi nilijua tu sio yeye, sijui atakuwa na hali gani, maana ile jela ni ya mauaji, ile jela mtu akitoka sio mtu tena, sasa Bosi tufanyeje, maana ….lazima tufanye jambo, mimi akili hainitulii kabisa…’ akasema Rose huku akiangalia juu. Halafu akamwangalia bosi wake ambaye alikuwa anasoma kitu kwenye faili mojawapo lililokuwepo mezani kwake. Aliendeela kuongea kuongea kwa kusema, ‘Mimi sijawa na amani moyoni, hadi nijue nini kinaendelea kuhusu huyo jamaa, asiyejulikana jina…?’ akasema Rose akiwa ofisini kwa Bosi wake, na kumfanya bosi wake amtizame huyo binti kwa mashaka. Aliendeela kuongea huku akimkazia macho bosi wake ambaye alionekana kutomjali kwa kile anachoongea.

Na ghalfa Docta Adam aliliweka lile faili pembeni na kumwangalia Rose kwa macho ya mshangao na kujikuta akijiuliza kwanini huyu binti kabadiliaka hivi, na hasa alipoonekana huyu mtu asiyejulikana,…inaonyesha kabisa kuwa mtu huyu kambadili kabisa Rose, na inaonyesha ana hamasa sana na mtu huyo asiyemjua vyema. Mtu ambaye alikuwa hataki kabisa kuambiwa kuhusu wanaume, kuhusu kuwa na mume, leo hii anamtetea, mwanaume…na wakati alishamtamkia siku moja, kama kuna watu anaowachukia kwa sasa ni wanaume, na kama ingebidi, asingeoenda kabisa kuwatibu wanaume, lakini anafanya hivyo kwasababu ni kazi yake.

‘Rose, sikia mimi kwasasa sitaki kuumiza kichwa na mambo kama hayo, unayaona haya mafaili hapa mezani, yote ni watu tunaowadai,…hela hakuna kabisa, natafuta nia ya kuwasiliana na mwanasheria wetu tuwafikishe mahakamani, kuna bili kibao za kulipa, kuna kodi….sasa wewe unaniletea gharama nyingine, kwa ufupi hiyo siyo kazi yetu, kazi yetu ni mgonjwa akiletwa hapa apatiwe huduma ya matibabu, na hilo tumeshalifanya …na bahati mbaya akaondoka kabla hatujamalizana na yeye, na kwa vile tulikuwa hatuna mkataba wowote na yeye, tumeshakubali kuingia sehemu ya hasara, ingawaje kuna barua tumeituma wizara ya ulinzi wachangie badhi ya ghrama…sasa huyu mtu kwa sasa hatuhusu tena, labda awe amekuja kutulipa gharama zetu na anahitaji matibabu yaliyokuwa yamebakia…’ akasema Docta Adamu huku akitafuta faili la huyo mgonjwa aliyetoroka

‘Unajua Docta Rose, ni vyema nikakuonyesha vielelezo vyote, ili uone gharama za huyo mtu wake, na ujiulize mwenyewe ni nani ataweza kuzilipa hizo gharama. Ukumbuke dawa, vipimo, ….na….vyote ni pesa, na mwisho wa siku watu wa kodi hawajui kuwa umelipwa au vipi wanadai chao…sasa kwanza yule mtu makubaliono na sisi ya kumfuatilia, yule mtu alishavunja makubaliano kwa kutoroka hospitalini,pia hata hivyo hatukuwa na makubaliano naye ya matibabu sisi tulichofanya nii kujitolea, kama ulivyoona tumemtibia lakini hakuna hata senti moja yak wake iliyoingia, je tutakwenda kumdai nani? Na sasa wewe unataka kuzua mengine, angalia sana Rose, huko unakokwenda ni kubaya…naona umeingiwa na kimuhemuhe , sijui cha mapenzi…sikuelewi Rose, kutoka kwenye chuki hadi kupenda kusiko na manufaa…’ akasema Docta Adamu, huku anacheka akifanya kama utani.

‘Tatizo lako Bosi, hujanielewa, yule mtu alishaniomba nimlinde kwasababu kwanza hajijui, hajui na haelewi nini kimemkuta, akaniomba sana na mimi nikamkubalia kuwa nitajitahidi kufanya hivyo, …mimi naamini kabisa kuwa ahadi ni deni, na …kuna usemi mwingine usemao, kuwa `akufaanye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli, na yule mtu yupo kwenye dhiki,na alishaniona kuwa mimi ni rafiki wa kweli na mimi nikakubali hivyo, leo hii nikiuke ahadi, leo hii nigeuke kuwa sio rafiki maana yake mimi ni adui yake, haiwezekani, …mimi nitajitahidi kumtafuta iwe na kwa kupata masaada wako au hata kama sitapata msaada wa yoyote, nitafanya hivyo…’ akasema Rose huku akiinuka pale kwenye kiti.

‘Rose usinielewe vibaya, mimi nipo tayari kukusaidia pale inapowezekana, kama ujuavyo karibuni mipango yako ya masomo itakamilika,…hilo ndilo ungeniomba, na hata hivyo sikuhitaji maombi yako nimejitahidi kwasababu na kujali. Rose, kumbuka tulipotoka, kumbuka siku ile nilipokutamkia yale maneno kuwa wewe nakuona kama unafaa kuwa mwenza wangu wa maisha, ukanikataa, ukamwendea yule mhuni kwasababu …ulimuona kama mzungu, au sio…lakini sikukata tamaa ingawaje sasa nina mke, lakini mke wangu hatuivani. Nilishakuambia hilo, kuwa nina taabu kubwa sana, sina amani ya ndoa, mke wangu hanielewi, imefikia hatua hatuongei, kisa kwasababu najali kazi , yeye simjali, kisa eti sijamnunulia gari, kisa, sijamjengea nyumba…yaani ukisikiliza madai yake hutaamini, ….’ Akanyamaza na kuinama chini.

Rose alimwangalia Bosi wake kwa huruma, na licha ya kumuogopa kama bosi, lakini wamekuwa karibu sana, kiasi kwamba wamefikia hatua ya kuelezana siri zao za ndani na kuombana ushauri. Na tangu bosi wake amuoe huyo mke wake, hajawahi kuwa na amani ya ndoa,…na siku moja Rose alimuulizia bosi wake vipi, mbona alitarajia kuwa kwasababau kaoa, mke mzuri, angekuwa na raha kama wanndoa wengine. Mwanzoni Bosi wake alimdanganya hivi na vile, lakini baadaye kwa vile walizoeana akaanza kumwelezea shida aliyo nayo. Na ilifiki hatua ya kusema kuwa hawaaminiani tena kati yake na mke wake, kwani alishawahi kurudi mapema akamkuta mkewe akiwa na mwanaume, na walifikishan hadi kwa wazee, yakamalizwa kimiya kimiya….hata hivyo mkewe hajatulia.

Rose alimuonea huruma sana bosi yake kwa hali kama hiyo, lakini hata yeye alikuwa na matatizo yake makubwa, matatizo ambayo hakuna angeweza kumsaidia kwa insi alivyojisikia, alimuona bosi wake sawa na huyo aliyemsaliti,..akawa moyoni kajenga imani kuwa wanaume wote ni sawa. Ni kweli alimkataa kabisa huyu bosi alipomtamkia kuwa anampenda anamtaka wawe wachumba, lakini yeye hakuwa na mapenzi na yeye…hajamkaa, zaidi ya kujuana kama wafanyakazi, ila kiukweli walikuwa karibu sana, lakini sio kwa mapenzi ya moyoni, mapenzi ya kutamaniana, hilo halikuwa moyoni kabisa, na hata hivyo kipindi hicho alikuwa na mtu anayempenda sana, mtu aliyempenda kwa moyo wake wote-mchumba wake aliyemsaliti, na hakumpenda eti kwasababu aliyoizungumza bosi wake…alimpenda kwa hisia za kimpanzi ya kweli na aliposalitiwa ikiwa mara ya pili akawa kawachukia kabisa wanaume wote duniani...

Bosi hayo ni ya kale, na sijawahi kukutamkia kuwa nakuchukia au nakupenda, na kiukweli, mtu mnaoana ikiwa wote mna hisia moyo ya kupendana,…mimi nilikuwa na mtu nampenda,…wewe ulitaka nikudanganye kuwa simpendi, hebu jiweke sehemu yangu halafu utumie hekima, kama wewe ungelikuwa mimi ungefanyaje….’ Akasema Rose huku akiwa kashika shavu.

‘Sawa yale ni ya kale, sasa tugange yajayo…nakuomba basi tuwe wapenzi….kwasababu hapa ninapoongea mke wangu hakulala nyumbani, na kuna mtu nilimtuma kunichunguzia anasema alikuwa kwa huyo mwanaume, wake tofauti na alivyoniaga kuwa anakwenda kwa shangazi yake na alipofika huko kamkuta anaumwa….akirudi hakieleweki kitu, talaka yake mkononi…kwasabau ushahidi ninao…lakini nikimuacha nataka wewe uingie ndani, uwe mke wangu…nakuomba sana Rose, nakupenda sana Rose
‘Bosi , bosi achana na hayo maneno, nimekuja hapa kwa lengo moja la kunisaidia tumpate huyo mtu, sio swala la mapenzi, mimi moyoni mwangu kuna mtu nampenda, sijapata bado, ….sijui ni nani …lakini haupo kwako kabisa moyo wangu , naomba unielewe hivyo, na nimekuwa mkweli kwako toka siku nyingi, siwezi kukudanganya kwa hilo, …..’ akafika mlangoni, halafu akamgeukia bosi wake na kumkuta anamwangalia kwa macho ya huruma, …ile sura ya ubabe akiwa kazini ilikuwa haipo kabisa…akarudi na kukaa mezani.

‘Bosi nakuomba sana, hilo swala la mapenzi na mimi tuliweke pembeni…nakuomba sana, kwasababu utakuja kuumiza moyo wako bure. Nakuomba tafadhali bosi, jitahidi sana kuniweka mimi pembeni kama ulivyojitahidi na kuweza kupata mwenza wako. Na kama imefikia hatua ya kuachana na mke wako, tafuta mtu mwingine tafadhali lakini sio mimi, tafuta …najua utampata. Lakini nakuomba mimi usinifikirie kabisa… sitaweza kupendana na mwanaume yoyote kwa sasa, na…mwanaume yoyote, …wewe kwangu ni kaka yangu, basi…’ akainuka na kuondoka hata bila kugeuka nyuma.

Bosi Adam aliachwa akiwaza mengi, kwanza kuhusu mkewe ambaye hajarudi nyumbani tangu alivyoondoka jana, na imegundulika kuwa kalala kwa mwanaume mwingine na sio yule aliyewahi kumfania mwanzoni huyu inasemekana ni mwanaume mwingine mgeni, mfanyabiashara tajiri. Mke aliondoka akimdanganya kuwa aankwenda kwa shangazi yake , …na alivyodai, alipofika huko alimkta shangazi yake ni mgonjwa, kwahiyo ikabidi abakie kumsaidia hadi usiku ukaingia. Hakujua kuwa yupo mtu nyuma yake aliyeondoka naye toka walipotoka nyumbani hadi hapo alipofikia,na kuwasilina na shangazi yake amlinde….! Kumbe sio mke wa kuishi naye, …iliyobaki ni kumuacha ilia pate uhuru wa kutembea na kila mwanaume anayempenda, akahitimisha hilo wazo kihivyo!

Kulikuwa na wazo jingine, hilo ni kuhusu mambo ya kikazi,… madeni yanazidi kuwa mengi, kila wanavyojitahidi kulipa, wanashindwa kuyamaliza kwani kila siku yanaongezeka, dawa, vifaa na mahitaji mengine ya kiutawala, yanaongezeka kila kukicha. Akawaza atafute njia gani zaidi ya kupunguza gharama hizo, je apunguze nini, au aongeze nini, ili kuwa na mafanikio? Alikosa jibu la haraka, akaona njia bora ni kukaa na mhasibu wake waangalie nini cha kufanya.

Na mara akageukia tatizo la usalama, tatizo ambalo lilimfanya akawa na uhasama na wanajeshi, hilo kwa sasa limepungua, lakini anaona kwa mshangao, tatizo hilo linatakiwa kurudishwa tena, na mtu muhimu sana kwake. Rose anataka kulirudisha tatizo hilo tena. Haiwezekani, huu sio wakati wa kuiingiza tena kwenye matatizo hayo, lazima apinge hilo jambo, lakini je inawezekana kirahisi hivyo…alipofika hapo akamuwaza Rose, na tabia yake, huwa akitaka jambo lake, atalivulia njuga, hasa akiliunganisha na fani yake, huwezi kumwambia kitu mpaka aone kafanikiwa. Sasa inavyoonekana asipomsaidia Rose, kuhusiana na hilo jambo lake, ingawaje linaweza kumkwaza tena hataweza kumuonyesha kuwa anamjali…moyoni alikiri kuwa kweli anampenda Rose, toka siku nyingi, ingawaje ilivyonekana Rose hampendi, au hataki kumuonyesha kuwa anampenda, sijui kwanini…lakini hata kama hataki kuonyesha hivyo, labda ndio silka ya wanawake, yeye hatakata tamaa…lazima ahakikishe anakuwa mke wake , alitaraji kuwa wakioana watapendana tu…akajipa moyo!

*************
Rose alipotoka pale moja kwa moja alielekea kwenye mgahawa mmoja, mgawa huo wanapenda sana kuwepo wanajeshi, licha ya kuwa hana tabia ya kufika hapo mara kwa mara, lakini kwa ajili ya uchunguzi wake aliona sehemu ambayo anaweza kupata uhakika wa jambo analolifuatilia na hapo, hapo anaweza kuonana na yoyote anayejua habari za mtu wake muhimu. Kwahiyo leo alikuwa na lengo moja la kuonana na mmoja wa wakuu wa kambi, ili adadisi na ajue yule jamaa yupo wapi, kafa au kapelekwa wapi.

Hakutaka kuweka wazo la kuwa huyo jamaa kafa, lakini lolote linaweza kutokea, kutokana na hali ya yule jamaa, na jinsi alivyoona, akipokea vipigo, ambavyo huenda hakuwahi kuvipata, mateso ambayo huenda yangeweza kumzidishia hali aliyokuwa nayo. Aliomba sana awe hai, hata kama yupo katika hali mbaya, lakini alipenda angalau amuone ili ajue kuwa kweli anatunza ahadi yake. Alijikuta moyo wake ukisononeka kwa kutokutimiza ahadi yake, moyoni aligubikwa na yale maneno ya yule jamaa alipomwambia `…na nakutegemea wewe Sweetie, maisha yangu yapo mikononi mwako…nakuomba sana, unilinde, sijui kwanini nakuambia hivyo, ila nakuamini hivyo…..ila cha muhimu na cha kwanza nakuomba unisaidie nitoke…’

Alikumbuka kabisa aliahidi moyoni atamsaidia huyo mtu hadi aone mwisho wake, hisia za ajabu zilimtuma hivyo, na hata hivyo, hata ujuzi wake ulimtaka afanye hivyo…na sasa inavyoonekana huyo mtu kama yupo hai anahitaji sana msaada wake kuliko wakati wowote, kwani kama kateswa, kama…akili yake itakuwa imetaharuki na atajiona kuwa hana rafiki duniani, na watu wengine wenye matatizo kama hayo wakifikia hatua hiyo wanaweza wakafanya lolote hata kufikia kujiua. Yeye kama docta aliona umuhimu sana wa kumsaidia mtu kama huyo na hiyo ni moja ya vitu alivyovisomea, na ni vyema kuutumia ujuzi wake vyema kwa watu kama hawa, iwe kwa pesa au bila pesa….alipofika hapo akatafuta kiti kinachoangalia sehemu kubwa ya watu wanaoingia ili akimuona huyo anayemuhitaji iwe kwake rahisi kumwalika kwenye meza yake na kumdadisi kuhusiana na huyo mtu anayemtafuta, na kabla hajatulia vyema mhudumu akaja kumuulizia mahitaji yake, yeye akaagiza soda tu.

Wakati anamimina soda yake kwenye gilasi, mara akamuona mkuu msaidizi wa kituo kile alichoplekwa huyo jamaa anayemuhitaji, akawa anamfuatilia kwa macho hadi alipofika kwenye meza iliyopo tupu na kukaa, ilionekana kuwa mkuu yule alikuwa akimsubiri mtu, na hapo hapo Rose akainuka haraka na kwenda kumkabili yule mkuu.

‘Mkuu, tafadhali niwie radhi nilikuwa na maongezi mafupi na wewe, kama hutojali..’ akasema Rose, na yule mkuu msaidizi wa kikosi akashikwa na mshangao kidogo, akaangalia saa yake halafu akamuashiria Rose akae, na hakusema neno akawa katulia kumsikiliza Rose

‘Mimi nilikuwa na shida moja, siku zilizopita, nyingi kidogo, tulikuwa na mgonjwa, ambaye alikuwa na matatizo ya kumbukumbu,na ilisadikiwa kuwa huenda ni mtu ambaye kikosi chenu kilikuwa kikimtafuta, lakini invyoonekana sio yeye, sasa kwa vile mtu huyo alikuwa katika dhamana yangu, nilikuwa namuulizia ili nijue hatima yake, ….’ Akasema Rose.

‘Alikuwa katika dhamana yako kwa vipi, hebu fafanua haraka maana nina ugeni muhimu hapa, nisingependa waje wanikute naongea na raia, alikuwa ndugu yako, rafiki yako…?.’ Akauliza yule mkuu huku akiangalia saa yake.

'Sio ndugu yangu kabisa, wala simjui kihivyo kuitwa rafiki, ila kiutendaji pale kazini mimi ndiye niliyekuwa nimekabidhiwa, na nilitakiwa nihakikishe usalama wake, na afya yake pia ,…ikatokea hivyo ilivyotokea, kabla matibabu hayajaisha’ akasema Rose akishindwa kuelezea zaidi.

‘Nakumbuka sana hilo tukio na namkumbuka sana huyo jamaa, na nilipopewa hiyo taarifa kuwa kakamatwa, nilistaajabu sana, na nikawa mpingaji wa kwanza kuwa sidhani kama ndiyo huyo ninaye mjua mimi, nilipinga moja kwa moja kuwa siyo yeye, kwasababau huyo jamaa aliyekuwa akitafuta tunaomfahamu…tunajua kashkashi zake, lakini muda, …inaweza ikafikia hatua mtu akajirudi, akapona, kwasababu wakati mwingine ile hali ilikuwa ikimtokea sio kwa matakwa yake, ni ugonjwa ule…kwakeli kama angelikuwa yeye asingekubali kukamatwa kirahisi namna hiyo….!’ Akasema yule mkuu na kuangalia saa yake.

‘Hata hivyo jamaa huyo aliyekamatwa kimakosa, hatupo naye…na hali aliyokuwa nayo kipindi kile sidhani kama yupo hai, inawezekana yupo hai, nisikukatishe tamaa…kwani kwa taarifa za mwishoni, alikuwa kazidiwa sana, haongei, hatembei, yupo yupo tu…na ikabidi akalazwe kwenye hospitali yetu ya kambini, na alipoonekana kuwa kazidiwa kiasi cha kwamba, anahitaji huduma zote akiwa kitandani tukaona sasa hili lipo juu ya uwezo wetu, na ikizingatiwa kuwa ni raia, ikabidi ahamishwe apelekwe hospitali ya serikalini, na huko sijui kilichoendelea , ila alichukuliwa akiwa mahututi….hilo ndilo ninaloweza kukusaidia, na nakuomba uondokea maana wageni wangu hawo wamefika….’ Alisema akiangalia kwa dirishani, kulionekana gari likisimama...

‘Oh, masikini Sweetie…’ Rose alijikuta akitamka lile neno bila kujitambua na yule mkuu alimtupia jicho mara moja, halafu akawa anasimama kujiandaa kupokea wageni zake naye Rose, akiwa hana nguvu aliinuka na nywele zake nyingi zilikuwa kama zinamfunika na hii ilizuia watu wasione yale machozi yaliyokuwa yameanza kumtoka, alijikuta nguvu zikimuishia, hata hivyo alijilazimisha kuinuka kwenye kile kiti na kuondoka, akiwa kainamisha kichwa na kujifanya anaangalia cheni aliyoivaa, kumbe ni kuficha watu wasimuone usoni…

Ni mimi: emu-three

4 comments :

Pam said...

ooh dr Rose pole sana usicheze na kupenda!

samira said...

m3 haya sasa doctor ndo kapenda
tungoje tuone
big up m3

Candy1 said...

huku kuwa busy busy kusikoeleweka nakosa uhondo huku lakini lazima nirudi nyuma nisome nilizo-miss and right now bibie Rose simuelewi hehehe, kawa kigeugeu ama?..mambo ya sitaki nataka lol haya mi nipo kama kawa kaka :-)

Swahili na Waswahili said...

Mmmhhh kweli ndugu yangu akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli,nazidi kushuhudia!!Pamoja sana Ndugu wa mimi.