Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha
Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..
Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.
MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.
TUPO PAMOJA DAIMA
Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;
https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:
https://www.facebook.com/diaryyangu/
`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;
Tuesday, July 13, 2010
Uchungu wa mwana-2
Hakuamini masikio yake pale dakitari alipomueleza kuwa hana malaria au ugonjwa wowote ila vipimo vinaonyesha kuwa ana ujauzito na huenda umeshafikisha miezi mitatu. Inawezekana kwani tangu akose siku zake ni zaidi ya hiyo miezi mitatu, lakini hiyo humtokea mara kadhaa. Hakuamini, yaani tendo la muda mfupi na mara moja limemuweka njia panda.
Ilikuwa taarifa ya mshituko, kiasi kwamba hakujua afanyeje, alichofanya ni kukurupuka mle hospitali mbio moja kwa moja kwa Yule muuza duka, ili amueleze kuwa ana mimba yake. Na ikiwezekana waende pamoja kwa wazazi wake wakajitambulishe, angalau ingesaidia kitu. Alipofika alimkuta Yule muuza duka akiwa anafunga mlango wa duka nafikiri alikuwa anakwenda kununua bidhaa zingine. Aligeuza kichwa mara moja na kuendela na shughuli zake kama vile hakuwahi kukutana naye.
‘Nina maongezi na wewe muuza duka’ alisema yule binti huku akiwa na kwikwi na hapohapo akuanza kulia, na kumfanya muuza duka aache kazi ya kufunga duka na kumgeukia yule binti.Akaona kuna jambo zito, na si vyema kuivuta hadhira na kusikia madhambi yake, akamshika mkono yule binti mkono na kumuingiza ndani.
‘ Haya sema, na sitaki kilio hapa nini tatizo lako, naomba usiniletee uchuro hapa dukani kwangu, kumbuka sina muda mrefu wamaongezi na mtu nawahi mjini kununua bidhaa, sema unataka nini, mimi sina hela , hela zilizopo ni za biashara, sema haraka unataka nini’ Yule muuza duka alisema kwa hasira akikumbuka jana amepewa barua toka shuleni kuwa amekuwa akiwaharibu Watoto wa shule na kama ukipatikana ushahidi atachukuliwa hatua ikiwemo kufungiwa duka lake.
‘Nimekuja kukuambia kuwa nina ujauzito wako, na sasa…’ alianza kulia kwa sauti.
Yule muuza duka alikuwa ameshika fungua mkononi zikamdondoka, akasema moyoni, sasa ule ushahidi waliokuwa wakiutaka ndio huu, jela inanukia, nikitoka hapa kituo cha basi hadi kwetu Moshi, mpaka hali itulie.
‘Wewe sikia, mimi wewe kwanza sikujui, pili kama una mimba nenda katoe, kamwambie yule rafiki yako anajua nini cha kufanya. Na ukiniletea uchuro wako hapa, nitakuitia watu kuwa wewe ni mwizi. Wewe unatembea na wahuni huko unataka kunibambikia mimi, hunipati abadani. Toka ndani kwangu, kwanza nachelewa...' Akamshika yule binti mkono na kumvutia nje, huku jamaa akiendelea kutoa maneno ya kashifa ambayo yule binti hakuyajali kwa muda ule, kwani akili ilishachanganyikiwa na hakujua nini cha kufanya.
Yule muuza duka akafunga kibanda chake na mbiombio akapotolea mitaa ya pile na kumuacha yule binti akiwa hana la kufanya. Alishaogopa kuitiwa mwizi na akikumbuka katoroka shule ili akahakikishe kuwa anavyohisi ni sawa.
Binti wa watu alikaa pale kibarazani huku analia, mpaka machozi yakaisha. Aliogopa kurudi shuleni kwani hakuaga, na huenda sasa anatafutwa. Kawaida shule yao wanasindikizwa kutibiwa, lakini yeye alikuwa na wasiwasi na mabadiliko anayoyapata, alikuwa akisikia vibaya, kichefuchefu, homa si homa, akasema moyoni isije ikawa ndio hiyo mimba wanayosema. Akaona akajichunguze mwenyewe mapema kabla hajaadhirika.
`Je kama ni mimba nitafanyeje' Alianza kutafakari bila muafaka. Kumbukumbu za nyumbani kwao zilimuandama, aliiona ile sura ya baba yake akiwa kawiva kwa hasira, akiongea kwa jaziba. Baba yake ni mkali kupita kiasi familia ya kwao wote wanamuogopa. Alimuona mama yake akihangaika kumbembelza baba yake ili akasome hadi akakukubaliwa. Mwanzoni baba yake alikataa katakata akisema kuwasomesha Watoto wa kike ni hasara kwani wengi wao huishiwa kupewa mimba.
‘Haya mimi nitalipa hiyo ada lakini ninaapa , na kuapa mara mbili siku nikisikia kuna tatizo la mimba, kuwa huyu binti kapata mimba, nitakachokifanya hutaamini macho yako, na sijui kama mimi na wewe tutaishi kwa amani tena, sijui…nadhani itakuwa mwisho wako wa kuishi na mimi’ Hiyo ndio kauli ya baba yake ambaye katika familia yao alijulikana kwa hasira zisizo na mpaka.
‘Hayo ni Maneno tu mume wangu, huyu ni mwaneti hata akiwa wa kike ana haki ya kusoma kama wanaume, kwa yovyote itakavyokuwa ujue huyu ana haki sawa na wengine, tunachotakiwa tumuombee masomo mema na sio kumuombea mabaya’ Hii ilikuwa kauli ya mama yake ambayo akiikumbuka anaiona kama msaliti.
`Mungu wangu kwanini imekuwa hivi kwangu, nitasemaje kwa wazazi wangu, je mama yangu atasalamika kwa kosa hili, ambalo yeye hahusiki, kwanini aje aumie kwa ajili yangu, hapana, kama ni kosa nimefanya mimi, sitakubali mama apate shida nikiwa naona. Lazima nifanye kitu’ Akainama kufikiria lakini hakupata jibu.
Kwa mara ya kwanza katika maisha yake alitamani kifo kitu ambacho alikuwa akiwalaumu sana watu wanaojiua. Alifikiri sana, akaona hiyo inaweza iakawa njia nzuri ili, asione mateso atakayopata mama yake: ` Ohhh, nifanyeje jamani, heri nikajiue ijulikane moja.
Je ni hatua gani binti aliichukua,?
Jaribu kujiweka katika nafasi yake halafu uone mateso na adhabu aliyoipata kiakili, na uiangalie jamii yetu kwa moyo huo kuwa huyu ni mmoja kati ya wengi wanaokumbwa na janga hili. Wewe kama wewe ungalisaidiaje, toa maoni na ushauri kwa huyu jamii kwa ujumla.
Tuonane kesho kwa muendelezo wa kisa hiki sehemu ya tatu. usisite kutuma maoni yako kwa e-mail: miram3.com@gmail.com
emu-three
1 comment :
Yaani nimesoma nikajikuta machozi yananidondoka. kweli wanaume wana roho za ajabu. Huwa naandika pale kwangu kila siku duh! kaazi kwelikweli nasubiri muundelezo.
Post a Comment