CHOZI KUTOKA
MOYONI…
UTANGULIZI
Nilifika ofisini asubuh kama kawaida yangu, nikafanya shughuli
zangu kwa haraka, nikijua leo bosi akija cha kwanza tu nafika ofisini kwake
nimpa ripoti yangu ya wiki, ya kazi zangu nilizofanya , ndivyo tunavyofanya, …
halafu namkabidhi barua ya mkopo...lengo la mkopo, kulipa ada za watoto,
mengine ni siri yangu..
Moyoni nikawa namuona mke wangu akifurahi, ..kama vile
nimeshaupata huo mkopo na sasa namkabidhi sehemu ya fungu anampeleka mtoto
hospitali na nyingine atafanyia biashara..na mawazo hayo yalikatishwa na
mawingu ya sauti zenye kunitia mashaka …sauti za kumbukumbu…
'Kama usipolipa ada yako mwezi huu… watoto wako wasije tena hapa
shuleni..'barua ya shule ilisema hivyo, na ujumbe wa simu, kwenye simu yangu..
Hawa walimu bwana...hivi hawajui hali halisi,...ngoja nipate
pesa, mimi nitawalipa pesa yao yote,
niwe huru, watoto wangu na wao wasome kwa amani, najua elimu ni bure lakini
nimeona niwalete huku angalau wasome kama watoto wa bosi, japokuwa shule
yenyewe sio sawa na ile ya bosi,..angalau lakini..nikawaza moyoni,
‘Lakini wapi pa kuzipata hizo pesa…’nikasema moyoni
‘Mhh, hizi sasa. ni ndoto za Alinacha…’nikazidi kujisemea.
Mara nikasikia sauti nyingine akilini hii ni ya kutisha kabisa…hadi
mwili ukazizima kwa uwoga.
'Unasikia, kama usiponilipa hilo deni,...nitakachokifanya usije
kunilaumu...'hiyo ilikuwa sauti ya muuza duka. Huyu muuza duka wanasema awali
alikuwa ni jambazi mkubwa, na pesa alizoanzishia hilo duka ni za uporaji, na
wanasema yeye kwake kuua ni kazi ndogo tu, askari wameshindwa kumpata kwa vile
hajawahi kukamatwa, na ushahidi.
'Nitakulipa ndugu yangu...kesho nikifika kazini nitaomba mkopo,
najua bosi atanipatia tu...huwa najituma sana kazini..'nikasema nikiwazia wazo
la mke wangu.
'Mkopo ulipe mkopo, hahaha, unanishangaza sana wewe mtu, sawa,
ila niamini, sitaki mzaha kwenye pesa yangu...'akasema muuza duka
'Wewe hujui maisha...ndivyo tunavyoishi, wewe subiria pesa yako,
na kama nisipokulipa,...njoo, kachukue chochote nyumbani...'nikasema kwa
kujiamini
'Hahaha haya bwana,...wewe hutaamini nitakachokifanya...'akasema
, ni kweli muuza duka huyu ni rahisi kukukopesha, lakini muda ukipita, wewe
sikilizia vumbi lake, wengi wanamfahamu wakikipa haraka hurudi kumlipe deni
lake, kwahiyo wengi wanakopa wakiwa na uhakika wa kuja kumlipa, hana wasiwasi
kukupa kitu.
Mimi nilikuwa na imani nitapata pesa, maana nimekuwa nikijtuma
sana kazini, wakati mwingine nafanya kazi hadi usiku, bila hata malipo ya
ziada,..,..na sijawahi kuomba mkopa kwenye hiyo ofisi kwa vile naifahamu
ilivyo, huyo bosi kutoa mkopo ni nadra sana
Na tokea awali sikuwa na wazo kabisa la kukopa ofisini hapo, kwa
jinsi nimjuavyo huyp bosi na hali halisi ya ilivyo, lakini hadi kufikia uamuzi
huo, ni kutokana na ushawishi wa mke wangu ndiye alinishauri,
'Mume wangu waonaje kutokana na hii hali, ukakope kiasi fulani
ili nikifanyie biashara,..na kiasi kingine tulipie ada, watoto wasifukuzwe wapo
mwaka wa mwisho...na kufukuzwa fukuzwa kuna wavunja nguvu..na nyingine tumtibie
huyu mtoto wetu anayeumwa, unajua tunazarau hali yake, inaweza kutuletea
matatiz baadae…tukaja kulaumiwa na madocta..'akasema mke wangu.
'Mhh, mke wangu, ..ungelijua...ofisini kwetu, mpaka bosi akupe
mkopo labda, itokee miujiza...bosi wetu hajali kabisa masilahi ya mfanyakazi
zaidi ya mshahara wako,.na imefikia hata mshahara analipa tarehe 35 au 40….na
hata hivyo hali ya kiofisi ni mbaya,biashara hakuna, na pesa hakuna kampuni ina hali mbaya sana..'nikasema
'Wewe nenda kajaribu tu, huwezi jua, muelezee hali halisi yeye
kama mzazi ataelewa, si yeye ana watoto pia, anasomesha kama sisi, anauguliwa
kama sisi, wewe mjaribu tu.....usijitwike
mzigo kabla haujatua kichwani mwako...'akasema mke wangu .
'Mhh...haya...'nikasema hivyo.
Hapo ndio na mimi niliingiwa na wazo hilo la kukopa kazini…,
nikajipanga, nikiona kweli kwasasa ina haja ya kufanya hivyo,.utaenda wapi
sasa, muajiri wako ndiye wa kukufaa wa wakati wa dhiki…nimefanya mengi ya
kuiaidia kampuni, kwanini mimi wasinisaidie na mimi..
‘Nikipata huo mkopo, sehemu yake nitamlipa yule muuza duka deni
lake, maana mhh…asija kunkata kichwa, …sura hata macho yake yanatisha..na hilo
deni hata mke wangu halifahamu..’nikajisemea hivyo.
**************
Japokuwa nilikuwa nawajibika sana kazini, lakini siku hiyo
moyoni mwangu nilihisi wasiwasi,…ni kama vile unahisi kitu kibaya chaweza
kukutokea, labda ni mawazo ya maisha, na nikakumbuka labda….
Nikahisi labda ni ile taarifa niliyoisikia wiki iliyopita,
kutoka kwa wafanyakazi wawili wakiongea,...ni mazungumzo ya kawaida tu ambayo
yanaongelewa kila siku.
'Nasikia bosi kapanga kupunguza baadhi ya
wafanyakazi...'nilisikia mfanyakazi mmoja akisema.
'Acha afanye hivyo bwana..’akasema huyo mwingine
‘Yaani wewe unaona ni sawa tu..’akasema mwingine
‘Ndio hata mimi ..namuunga mkono bosi…, maana wanaajiriwa
wafanyakazi wapya , eti wasomi, halafu wanalipwa mishahara mikubwa zaidi yetu
sisi. Hebu wewe angalia, sisi tupo hapa kwa muda gani, tokea kampuni hii
inaanzishwa, hatuongezwi kitu, tunakuwa wasindikizaji tu, mimi nitafurahi
wakiondolewa tu....'akasema mwingine.
'Wewe una uhakika gani kuwa hutaondolewa hapa kazini?'akaulizwa.
'Mimi najua tu, siwezi kuondolewa, mshahara wangu ni mdogo sana,
hauwezi kuitia kampuni hasara, …nakuambia kitu,…wote wamekuja na wote
wataondolewa, wewe niamini hilo…’akasema
‘Mhh…unajiamini …’akasema mwenzake.
‘Mimi nakuambia..hao, wataondolewa wote..wametukuta, na
watatuacha na kampuni yetu,.."akasema kwa kujiamini na kucheka, sikujua
kwanini huyo mfanyakazi anajiamini hivyo.
'Ni kweli, uzuri wake sisi bosi tumeshamjulia, hawa wageni
wakija , wanajifanya wanajua kuliko hata bosi,..hawamjui huyu bosi wetu alivyo,
anakupenda akiwa na shida na wewe, shinda yake ikiisha, hajali, atakuondoa
tu...'akasema mwingine.
Wafanyakazi hao kazi yao ndio hiyo, wakifika ofisini asubuhi,
asilimia kubwa ni kuteta, magumzo vibarazani, hawafanyi kazi mpaka wamuone
bosi..
Bosi akiingia hutaamini,...wanajituma utafikiria sio wale
waliokuwa wamekaa , wakiongea, kusoma magazeti…au kupiga gumzo la mipira au
siasa..lakini ngoja bosi afike, huwezi amini, watakavyowajibika,..na bosi
akiwepo, kweli wanawajibika,...na wanahakikisha bosi anaona kile wanachokifanya....kiukweli
wanajua kuigiza. na wanampatia sana huyo bosi
'Ukitaka bosi huyu akupende iwe hivi, na jingine eeh…usije kumuomba
pesa, anaipenda pesa zaidi ya benki…na jingine usije kumlalamikia shida zako,
hapendi kusikiliza shida za mtu, kwake yeye umuonyeshe kazi, uongee naye kuhusu
kazi zake, atakuwa rafiki yako,…ole wako uende kulalamika mambo ya mshahara
hautoshi, umechelewa,…hahaha, utaniambia..'aliniambia mmoja wa wafanyakazi siku
nilipomuuliza kwanini wanafanya hivyo.
'Kiukweli mimi hivyo siwezi, nitafanya kazi kwa mujibu wa
taaluma yangu, akiwepo au asipokuwepo, na akija kama sina zaidi, nimemaliza
kazi nahitaji kupumzika kidogo nitafanya hivyo, ilimradi nimetimiza wajibu
wangu…mimi sio mtumwa wa kuigiza...'nikasema
'Hahahaha haya, na kwa jinsi anavyowalipa, moyoni hafurahii
kabisa, ipo siku wewe utaniambia wewe jitume tu...'akasema jamaa huyo.
Pamoja na kujituma kwangu, kuwajibika kwa mujibu wa kazi yangu,
niliona kama wafanyakazi hao walikuwa hawaniangalii kwa jicho jema, mimi
sikuwajali nikijua udhaifu wa binadamu ulivyo, husuda na chuki ni hulka zetu.
**************
Basi mara nikasikia bosi mwenye kampuni kafika, kwa haraka
nikaweka barua yangu vyema na kuhakikisha kila kazi niliyotakiwa kuifanya
nimeikamilisha, nikatengeneza taarifa ya kazi yangu ya wiki ili iwe chambo cha
kuanzia, sikutaka matatizo
Wakati ndio nataka niende ofisi kwa bosi, mara nikasikia
nikiitwa.
Nilihisi moyo ukinilipuka, phaa...sijui kwanini,.. hata hivyo
sikujali sana, nikajua labda bosi leo kanianza mimi, anahitajia kujua
nilichofanya wiki nzima iliyopita.
'Hamna shida sasa nimepata wapi pa kuanzia...'nikasema nafsini
mwangu.
Kwa haraka nikakusanya makabrasha yangu, na laptop, ili niwe
kamili kamili,...sikutaka uzembe kwenye kazi zangu, kwa haraka nikaelekea huko.
Sasa wakati natembea kuelekea kwenye hiyo ofisi, nikakutana na
wafanyakazi wale wawili, , wakaonyesha tabasamu, kama la kujali na kunipa moyo
na nilipogeuka kuangalia ninapokwenda, wao wakaangaliana na mimi nikawa
nimegauka kwa haraka kuwaangalia
Niliwaona wakionyesheana ishara ya dole gumba...mimi sikuwajali,
haraka nikaingia ofisi ya mkubwa wa kampuni.
'Habari za asubuh bosi...'nikasalimia kwa heshima na bosi kwanza
akahema kwa nguvu, halafu akasema.
'Nzuri tu,...hebu kaa hapo, nina mazungumzo na wewe..' akasema
hivyo. Hapo, nikaanza kukata tamaa, maana nilitaka aanze kuniulizia hali za
familia, ili niweze kuchomeka matatizo yangu halafu, phaa...namkabidhi barua ya
mkopo.
'Bosi mimi ripoti yangu ipo tayari kama ndio
uliyoniitia...'nikasema
'Sio kuhusu ripoti, nimekuitia,jambo jingine tu, wewe kaa hapo,
na weka pembeni kazi zako. ...'akasema na kutulia kidogo, hapo nikaanza kuwaza
mengine, kaniitia jambo jingine kuhusu nini...binadamu unaweza kuwaza mambo
mengi kwa sekunde chache tu.
' Kiukweli, mimi nimefurahishwa na utendaji wako wa kazi, hata
kwenye vikao vyetu, huwa tunakupongeza sana...'akaanza kusema hivyo.
Hapo moyoni kidogo nikaanza kuingiwa na tumaini jema,..nikajua
labda natakiwa kuongezwa mshahara, japokuwa katika hiyo kampuni kuongezwa
mshahara haijawahi kutokea.
Jingine lilinitia mashaka kidogo, niliona bosi kama anakwepa
kuniangalia machoni...sio kawaida yake , yeye huwa akikuita ofisini kwake
akianza kuongea na wewe anahakikisha anakuangalia moja kwa moja machoni.
'Nashukuru bosi...'niliposema hivyo, akainua uso sasa kunitizama
machoni.
'Lakini kwa hali ya kampuni, nashindwa hata kuelezea, hata wewe
mwenyewe umeiona au sio, kama tumefikia hatua hatuwezi kulipana mshahara kwa
wakati...eeh,...na hata tukilipana twalipana nusu.mishahara, ni jambo mimi
sipendi kabisa..'Hapoi nikahisi moyo ukinienda mbio.
'Wewe ni mmoja wa wafanyakazi tunaowalipa vizuri, na nilipenda
niendelee kufanya hivyo...ndio kwanini nisikulipe hivyo wakati, elimu yako
inaruhusu, achilia mbali utendaji wako...'akasema
'Ahsante bosi najitahidi tu..bado, sijafanya kile ninachokitaka...'nikasema
'Inatosha,..umefanya vyema tu...'akasema hivyo, halafu kama vile
hataki niongee zaidi akasema
'Kiukweli, umekuwa ukinipa moyo,..uliyoyafanya ni makubwa
sana...ndio maana nilipowaza,..eeh kutokana na hali ya kampuni ilivyo ngumu,
niliona labda niwapunguze mshahara, ili tuweze kumudu hali halisi...kwako wewe
niliona sio sahihi...'akatulia
'Kutokana na hali halisi ilivyo, ...hili nimeamua mwenyewe,
usije kusema ni ushawishi wa mtu,...mimi nimeona tukupatie nafasi, ili utafute
kazi sehem nyingine...'hapo akaangalia pembeni.
'Bosi mbona sijakuelewa...'nikasema
'Kiukweli sina uwezo wa kuendelea kukulipa, ...nimejitahidi kila
mwezi, hata kukopa huku na kule, lakini uwezo wangu umefika mwisho...na naanzia
kwako, pengine hata nikiona naweza kufunga kampuni....'akasema
'Oh...bos lakini...nilikuwa na matatizo...ndio nilitaka
nikuelezee...'nikasema
'Matatizo ...hasa yanayohusu pesa, sitayaweza tena, mimi
nakuomba ufanya jambo moja..muda wa mwezi huu, jitahidi kutafuta sehemu nyingine
ukipata, basi...lakini baada ya mwezi huu,...sitaweza kukulipa tena
mshahara...'akasema
Hapo, nikanywea,...akili ikaganda...nguvu zote zikaisha...kila
nikitaka kumuangalia huyo bosi nashindwa, macho yameshakuwa mazito...
'Ndio zaidi ya hayo, ningeliomba uanze kumzowesha yule mwenzako
kazi zake...najua utapata kazi sehemu nyingine wewe ni mchapa kazi mnzuri
sana..na ukipata mimi mwenyewe nitakudhamini, maana nakufahamu sana...'akasema
sasa akiweka mambo yake vyema mezani kuwa niondoke.
Taratibu nikasimama, na kuanza kutoka, sasa mwili hauna nguvu,
akili ikaenda mbali,...watoto shule tena basi, nilijaribu kuwatoa kwenye shule
za awali walizokuwa wakisoma ili wasome kwenye shule za kulipia, angalau wawe
japo sio sana na watoto wa mabosi,…sasa haitawezekana tena.. na itakuwaje, kwa
yule muuza duka, asiponiona leo, familia yanagu inaweza kuwa hatarini, na
nikimuendea, kwa hasira alizo nao anaweza kunikata kichwa,…lakini la zaidi ...mtoto
anaumwa anataka matibabu nifanyaje.
Niliwaza hivyo hata sijui nilifikaje mezani kwangu,
...nilipofika nikainamisha kichwa, nikawaza, na kuwazua, sijui ilikuwaje, chozi
likanitoka, ...sijui chozi la nini, na sijui namlilia nani sasa mie mtoto wa
kiume,..kiukweli lilikuwa chozi lenye hisia kali....'CHOZI KUTOKA MOYONI..
'NB: hiki ni kisa kifupi cha rafiki yangu, kanitumia,..kwa
yaliyomkuta....nashindwa kukiendeleza kwa hivi sasa maana na mimi nipo kwenye
mitihani hiyo ya maisha…ila kwa faraja nimeona nikitume siku isipite bure.
WAZO LA LEO: Baada ya
dhiki huja faraja, baada ya magumu fulani mwisho wake huja mafanikio, je inapotokea
umefanya jitihada zote, umepitia ,magumu mengi sana, na inafika muda wa
kutegemea faraja, bahati mbaya, ikaja kutokea machungu utafanyaje...
‘litakutoka chozi …’
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment