‘Hayo maswali yako muheshimiwa kwangu ni
magumu sana kuyajibu,...lakini kwa vile umeniuliza na hapa ni mahakamani, mimi nitajaribu kuyajibu kama ifuatavyo, kwa ufupi,…kwanza, mimi sijaweka
sahihi yangu kwenye huo mkopo,...kwenye hizo karatsi za kuchukulia au kwenye mkataba...'akatulia kidogo
'Na kwanini mimi niweke sahihi yangu,...kwanini... maana huo sio mkopo wangu, na hata kaka hajawahi
kuniagiza niweke sahihi kwa niaba yake kwenye huo mkopo…’akasema
‘Je alishawahi
kukuambia uweke sahihi kwa niaba yake…kwenye jambo fulani la kibenki…?’ akaulizwa
‘Niweke sahihi yake...!!!….mmh….kwa
vipi , yeye ana sahihi yake, na mimi nina sahihi yangu,.. labda niweke sahihi nisema nimeweka sahihi hiyo kwa
niaba yake, lakini sio kwa maswala ya kibenki, benki wana masharti yao jamani…’akasema na kukaa kimia
‘Na dole gumba je…?’
akaulizwa
‘Hapo ndio mnaweza
kupata majibu yenu sasa..., mkiwa makini na hili swala, kwenye dole gumba ndio kwenye jibu,…jiulizeni tu, kweli kuna mtu anaweza kuweka dole gumba kwa niaba
ya mtu mwingine..hilo halipo, au sio,…
kama hilo halipo, ina maana gani sasa, ...ina maana kuwa...eeh, bro alihusika yeye mwenyewe…’akasema
Akageuka kumuangalia hakimu, na baadae akaendelea kuongea...
‘Na nasema hili, sio kwamba, nasisitiza deni hilo ni la bro,...kuna namna ya kulithibitisha vinginevyo, mbona nitafurahia hilo,…lakini je hayo yalitendekaje,..akilini
najaribu kuwaza, huenda kweli bro alifanya hivyo,..'akageuka kuangalia mbele, nahis alikuwa akitafuta wapi shemeji yake yupo.
'Nazungumza haya, sio kwamba nafurahia hilo jambo..kuwa nashabikia hilo deni kwa marehemu,..kiukweli mimi mwenyewe linanisumbua sana...mimi silifurahii hili jambo kabisa .. nitalifurahiaje wakati najua hilo deni litaiumiza familia yangu…lakini
tutafanyaje,…kama bro, aliacha hilo deni,..hivi kiukweli mimi kama ndugu yake
nilitakiwa nifanye nini sasa…, eeh, niambieni,…?’ akawa kama anauliza.
Alipoona hajibiwi
akaendelea kusema;
‘Huyo kijana kadanganya,
akisema mimi ndiye nimehusika na hilo deni, sio kweli,… 'akageuka kumuangalia hakimu.
'Nasema kutoka moyoni,...mimi sijachukua huo
mkopo,…na-na..jamani, hivi hamuoni hali halisi, kama ningelichukua hayo mapesa
yote, ningelikuwa hivi..eeh, si mngeliniona nikiwa na mabadiliko, Dalali,
ninavyokipenda.... na wala, sikujua ..sikuwa na ufahamu wa hilo deni kabisa
jamani…’akasema.
‘Lakini wewe ni tajiri, ukishirikiana na wenzako, wewe mtaalamu, na kijana wako, nyie mna vitega uchumi, kweli si kweli...?' akauliza na kwanza akakaa kimia
'Nyie…mna vitega
uchumi vingi tu ambavyo vimekuja kugundulikana baadae kuwa wewe ulikuwa mpo
ubia na huyo kijana wako kwenye miradi yake mingi tu, mkiwa mnatumia majina
yasiyo rasmi,…ina maana kwa namna nyingine nyie wawili mpo shirika, kwahiyo
mnaweza kufanya jambo mkapanga, na hiyo ilitokana na huo mkopo…’kabla hajamliza
muulizaji, Dalali akasema;
‘Hapana muheshimiwa
wakili…samahani kwa kukukatisha,…inaniuma sana, leo nateseka , nateswa, lakini
hakuna anayelijali hilo,…''akasema
'Unateswa na nani...?' aakulizwa
'Hayo ya kwangu tuyaache, nitapambana nao, ..hawaniwezi....'akasema na kutulia kidogo.
'Sasa hiyo kauli yako, kusema sisi, au mimi ni tajiri...sio sahihi, hivi unamfahamu vyema huyo
kijana, kila alichokifanya kakifanya kwa kunitega, kulipiza kisasi, kwa hayo,
anayohisi kuwa mimi nimemfanyia mama yake,..mengine mimi sijayafanya…’akasema
‘Tutaaminije hayo
wakati ushahid upo , kuwa wewe uliyafanya ,…na kauli zako nyingi zimekuwa kinyume,
na utetezi wako wa sasa, kuonyesha wewe sio mkweli,..nyie wawili mnajua ni nini mlichokifanya, na inavyoonekana huu ni mkakati
wenu wa pamoja, ushahidi upo…’akambiwa.
‘Ni sawa tupo wabia kwenye
miradi fulani, fulani, lakini angalieni
kiasi cha hisa, tulichopewa sisi wabia hewa…, ni nini tunachokipata hapo, sana sana
kiasi hicho kinaishia kwenye kulipia madeni anayotudai, kama nilivyowaambia,
huyo kijana ni mjanja sana, alituingiza kinamba na kutufanya sisi ..eti
wakurugenzi, …’akatulia.
‘Huyo kijana
ana..lengo lake, na lengo lake analifahamu yeye mwenyewe…mimi narudie tena,
…sikujua jinsi gani deni hilo lilivyofanyika,..na mpaka sasa bado siamini, kama
benki wanaweza kuchezewa kiasi hicho, kama ni kweli wamefanyiwa hivyo, mimi
sitaweza kuwasamehe, maana wametutesa sana…’akasema.
Wakili akacheka na
kutikisa kichwa, halafu akamuangalia Dalali machoni,…baadae akamuuliza…
‘Je kwa hali kama hii,
baada ya maelezo ya kijana wako, je bado unakubaliana na benki, kuwa hilo deni
ni la marehemu kaka yako, huoni kwamba ukiendelea kusema hivyo, au kuamini
hivyo, wewe haupo katika kuisaidia familia yako, bali wewe unaangalia masilahi
yako binafsi..?’ akaulizwa
‘Kiukweli , awali,… mimi sikukubaliana na hilo deni…, kuwa
bro anaweza kukopa pesa nyingi hivyo, hata mimi kweli nisifahamu,…lakini sasaah…ushahidi
upo wapi, kiukweli nilipoangalia ushahidi wa benki, nikajua ni kweli, bro alikopa
hizo pesa, maana taratibu za benki zinajulikana,…niliangalia vitu muhimu, sahihi ipo ya bro,…halafu kuna dole gumba, la
bro, hilo nani anaweza kugushi, …mimi nitasemaje
hapo…’akatulia.
‘Hata mke wa marehemu
alisema kuwa sahihi hiyo ni ya mume wake,..na zaidi ni baada ya mahakama
kupitisha hukumu, mimi ningesemaje hapo jamani, hebu nisaidieni na nyie…’akasema.
Wakili akatabsamu na
kusema;
‘Mbona hujasema , na
mizimu yenu…au hiyo ilikuwa ni geresha yenu, kuwachezea watu…?’ akaulizwa.
‘Ndio, ndio…nilisahau
hilo, ..na mizimu ikatusaidia,…lakini marehemu naye, aah, unajua, niseme
ukweli, imani zake zilinitega sana akili yangu, na kunifanya niamini kila kitu
anachoniambia…hata hilo la mizimu, liliniongezea imani kuwa kweli hilo deni ni
la bro..’akasema.
‘Hayo ya mizimu si
ilikuwa ni mbinu zeni za kuwatishia watu ili wakubaliane na hilo deni, sio
mbinu zenu wewe na marehemu, mtaalamu,
tuambie ukweli, maana yeye hayupo hapa…?’ akaulizwa.
‘Ni kweli mimi na
marehemu tunajuana,…kwa vile namuamini, na nilipomuomba anisaidie kwa hilo,
akasema hivyo, kuna mizimu, …kiukweli nilimuamini, nilijua yeye ni rafiki yangu
hawezi kunidaganya…’akasema.
‘Swali kwa maelezo yako
hayo, na kumbukumbu zilizopatikana zikiwa zimefichwa na huyo kijana wako,…Je
kwa hivi sasa baada ya ushahidi huo wote, wewe bado …una imani hiyo kuwa hilo deni
ni la kaka yako?’ akaulizwa, kulitokea pingamizi kutoka kwa hakimu wa benki,
lakini kwa hivi sasa hakimu hakutaka pingamizi …
‘Mhh…hapo mimi aah…sijui
mnataka mimi nisemeje,..kiukweli hadi sasa nachanganyikiwa, kwa namna nyingine
mimi nimeaanza kumuhisi huyo kijana kuwa huenda alifanya jambo,.’akatulia
kidogo.
‘Lakini najiuliza-aah…mmmh,…,
alifanyaje sasa..eeh jamani..alifanyaje.., unajua benki ilivyo, labda kwa vile
aliwahi kufanya kazi huko benki labda… lakini hata hivyo kwa vipi, si lazima
wakubwa wake wapitishe eeh..…kwa upande mwingine kuna eeh,… kuna sahihi ya
kaka, na zaidi kuna dole gumba, hapo mimi na ujanja wangu wote siwezi kuwa na
uhakika wowote..’akasema
‘Kwahiyo unataka
kusema nini hapo, kuwa huenda kijana wako ndiye alifanya hujuma na wewe
ukatumbukizwa bila kujua, maana kwa ushahidi ulivyo, wewe unahusika
kulifanikisha hilo deni…?’ akaulizwa.
‘Ushahidi upi sasa
jamani…kwa vipi mimi nimeweza kulifanikisha hilo, niambie kwa vipi, sahihi ni
yangu,..hapana, dole gumba ni langu, hapana…ushahidi upi ndugu muheshimiwa, kwa
kauli tu ya huyo bwana mdogo,…mimi sijui kitu jamani, mnanionea bure, niambieni
wenyewe…?’ akauliza kwa mashaka.
‘Kutokana na kauli ya
Majaliwa, wewe ndiye ulikuwa mara nyingi unahusika kwenye kuchukua pesa za kaka
yako…na ikatokea pesa zikachukuliwa bila ya ridhaa ya kaka yako,..na kwa
ushahidi mwingine, kaka yako aliwahi kuandika barua benk kulalamika, na zaidi kumbukumbu zote za benki
nyumbani kwa marehemu zikapotea na wewe ndiye ulikuwa na mamlaka wakati shemeji
yako hajitambui,..unakwepa nini hapo..’akaambiwa.
Hapo Dalali akakaa
kimia…na wakili akaendelea kuuliza…
‘Je kaka yako hakuwahi
kukulalamikia kuhusu hilo…kuwa kuna pesa zimechukuliwa benki bila ya ridhaa
yake…?’ akauliza na akabakia kimia
‘Sasa tuambie ukweli, wewe ndiye uliyekuwa ukitumwa kuchukua pesa
benki na kaka yako…, sasa kama kaka yako alilalamika hivyo…kuwa kuna pesa
zimechukuliwa bila ya ridhaa yake…, ni nani wa kumshuku, kama sio wewe...na
zaidi ukifika benki wewe ulikuwa mkikutana na Majaliwa, ushahidi upo…’akaambiwa.
Dalali, akahema
kidogo, halafu akaanza kuzungumza, kwa sauti ya kinyonge kidogo…
‘Mhh…nakumbuka kuwa
kweli kaka, alilalamika kuhusu hilo..lakini mimi sikuwa nachukua pesa bila ya
kibali chake, …na aliponilalamikia mimi, kiukweli niliumia sana, ina maana bro
haniamini…’akatulia
‘Hata hivyo, nikaja
kujiuliza kama kweli hilo limeetndeka, basi bro ana haki kulalamika jambo
nzuri, ni benki watuambie kwanini …na hizo pesa zimekwenda wapi, nikamshauri
bro, aandike barua benki ya kulalamika…’akatulia
‘Hilo hukuwahi
kulisema, ..awali uliulizwa ukasema hujui lolote kuhusu hiyo barua, sasa hivi
unasema ni wewe ulimshauri kaka yako…’akaambiwa.
‘Hapa ni mahakamani…huenda
nilisema hivyo kwa minajili fulani, lakini hapa sasa naongea ukweli ulivyokuwa…kuwa
bro..ilikuwa ni haki yake kulalamika
hivyo, ilikuwa ni haki yake kuninyoshea kidole mimi….na nilipoongea na Bro,
baada ya mimi kumthibitishia kuwa kweli sihusiki na hilo, akaandika barua kuwalalamika benki…’akatulia
‘Na bahati mbaya,…sikuweza
kupata nafasi ya kuliongelea hilo na bro, siku zikapita,…sijui banki walimjibu
nini…na bahati mbaya zaidi haya yametokea… .’akasema kwa sauti ya unyonge.
‘Haya yametokea….’akasema
wakili alipoona Dalali katulia
‘Kwanini haya yametokea…?’
akauliza wakili
‘Mimi sijui….’akasema
‘Ndio utasema
hujui..haya yametokea baada ya kuonekana
kuwa njama zenu zimebainika, mkaona njia nzuri ni kumuangamiza kabisa huyo bro
wako, …ili hayo malalamiko yapotee, ili muweze kumbambikia bro wako deni, na
ndivyo ilivyotokea,, na ndivyo ilivyofanyika, unabisha nini hapo bwana Dalali …’akaambiwa
Dalali akakohoa, na
kusema;
‘Sio kweli
jamani…naapa, ..haya ninayoyasema ni kweli tupu, mimi sihusiki na hilo
deni,…labda huyo bwana mdogo aje atuthibitishie kauli zake hapa za kusema mimi
nahusika, maana yeye alikuwepo huko benki kipindi hicho, je ni kweli
nilishirikiana naye, aje hapa ayatamke hayo…’akasema
‘Kwa kauli yako hiyo unatuthibitishia
kuwa kijana wako ndiye aliyewezesha hizo mbinu,, za kuchukua mkopo, na
kuuwekeza kwa kaka yako…lakini sahihi ya kaka yako ilipatikanaje, hapo ni kazi
yako wewe….kweli si kweli…?’ akaulizwa
‘Mimi
sijui..na..na…’kabla hajaendelea akaendelea kuulizwa.
‘Ngoja tukusaidie
mlivyofanya…baada ya huo mpango, mliouita mpango moto kutengezwa, wewe ulipewa
jukumu ya kupatikana kwa sahihi ya kaka yako na dole gumba…’akasema wakili.
‘Hiyo haikuwa kazi
ngumu kwako, ungeliweza kufika kwa kaka yako ukamvunga kwa vile anakuamini,
yeye akaweka sahihi bila kusoma huo mkataba,..wewe uliweza kumdanganya kuwa huo
ni mkatana wa kurekebisha akaunti yake ya benki…’akasema wakili, kwa kazi za
kibenki, hilo lilikuwa jukumu la kijana wako, je hivyo si ndivyo mlivyofanya…?’
akaulizwa
‘Kamleteni huyo kijana
wa benki,labda kama mimi hamuniamini… yeye mwenyewe ataweza kulielezea hilo…kama
kweli kadai kuwa mimi nahusika, basi aje atamke hapa mbele yangu, …zaidi ya
hayo, mimi nakataa hayo madai yako, ..sijapewa jukumu kama hilo, na sijui
lolote kuhus huo mpango moto…’akasema.
Wakili akawa anaoma
makabrasha yake, halafu kama kakumbuka jambo haraka akamuendea Dalali…
‘Kijana wako kasema mama yake alikupenda sana,..na hakutakiwa
akuingize wewe kwenye matatizo yoyote,..mbona wewe unamuingiza huyo kijana wako
kwenye matatizo, ina maana wewe hukuwa
na upendo na mama yake, na wala hujali kitakachokuja kutokea kwa huyo kijana
wako, au hizi ni mbinu mbinu tu za kupotea muda,…?’ akaulizwa.
‘Upendo…!! Hivi
mnaelewa ni nini maana ya upendo, mnajua alichonifanyia huyo mwanamke..’akasema
kwa sauti ya hasira kidogo, halafu akatikisa kichwa na kusema;
‘Jamani, mimi
nilishawaambia, …mimi sitaki kuyasema hayo, maana yeye sasa ni marehemu, na sio
vizuri, kuyaingiza haya mambo yake hapa…, ndio maana hadi leo, sijaweza
kukubali moja kwa moja kuwa huyo mtoto ni mtoto wa kwangu, ila kama huyo kijana
atakuja kwangu akasema kweli ananikubali mimi kama baba yake, nitakubali tu,
yaishe, kwani wangapi wana watoto sio wao wa damu…’akasema.
‘Ina maana hadi sasa
hujaamini kuwa huyo mtoto ni wako, wakati wewe ndiye ulimbaka huyo mwanamke…na
kwa kitendo hicho ukamsababishia mimba …au unamshuku nani kwa hiyo mimba, kaka
yako au nani mwingine…?’ kabla hajamaliza, Dalali kwa hamaki , akasema
‘Kaka yangu..!!! Ni
nani kasema hivyo,…hapana jamani, mimi siongelei hilo kuhusu kaka yangu hapa, siwezi
kumshuku kaka yangu kwa hilo, kaka yangu hakuwa na tabia hiyo chafu,..mimi hapa
naongelea kumuhusu mtaalamu…’hapa akatulia kidogo.
‘Mtaalamu…alifanyaje
kuhusiana na huko kwa wewe kumbaka mdada wa watu baada ya wewe kumtegea kwa madawa
ya kulevya…?’ akaulizwa
‘Muheshimiwa…mimi nasema
hivi, pamoja na ya kuwa mtaalamu alikuwa
ni rafiki yangu, lakini eeh, samahani
kwa kauli hii, mungu anisamehe tu…mimi nilikuwa namshuku mtaalamu vibaya, kuwa
huenda….’akatulia kama anasita kuongea
‘Ongea..au unautafuta
uwongo mznzuri…’akaambiwa
‘Mmhh….unajua kama
binadamu tuna madhaifu yetu, ..hasa kwenye maswala ya mapenzi…moyo huwa
hauamini…hasa ukiona mpenzi wako yupo karibu na …na…kibinadamu inakuwa hivyo…,
mtu unaweza kujenga shaka-shaka…na nilijenga shaka shaka hizo kwa mtaalamu
kuhusiana na huyo binti…’akasema
‘Shaka shaka gani,
tufafanulie hapo Dalali…?’ akaulizwa
‘Mara nyingi,
mtaalamu, alikuwa anapenda kuwa karibu na huyo binti, na alishawahi kunisifia
kuwa huyo bint ni mnzuri..na..akifika kwetu, ni lazima amuite, amtume kitu…unaona…na
mambo mengine tu..kiujumla moyoni nilikuwa naumia, maana mimi nilishampenda
huyo binti…na alipokuja kunishauri jambo, ndio kabisa nikajua tayari…’akatulia
kidogo.
‘Alikushauri nini…?’
akaulizwa na badala ya kujibu swali hilo akaendelea kuongea;
‘Ila jamani…mimi siwezi
kuwa na uhakika wa moja kwa moja, na hili hapa tunamsema marehemu, na nyie
mumenilazimisha niyaseme haya....maana sikuwahi kuwafumania ile ya moja kwa
moja, hapana, niliona dalili hizo tu, moyo wangu ukajenga wivu..na siwezi
kukataa mpaka leo, bado …aah, mwenyezimungu nisamahe tu, bado naamimi mtaalamu,
ali…aah…ali…jamani sitaki kuyasema haya mume-nifanya ni-ni ya-seme tu……’akatulia
akionyesha huzuni fulani.
Wakili akatabasamu na
kutikisa kichwa kusikitika, halafu ..akamuangalia Dalali..
‘Unataka kusema huenda
huyo mtoto ni wa mtalaamu..lakini ukumbuke, kutokana na maandishi ya mama yake
Majaliwa,..yeye aliandika kuwa wewe ndiye uliweka dawa..za kumpoteza fahamu , na
ukatumia mwanya huo kumbaka, kweli hukufanya hivyo…?’ akaulizwa.
‘Unajua hizo dawa
alinipatia nani,..?’ akauliza.
‘Je hukufanya hivyo…?’
akaulizwa tena
‘Ndio nilifanya, lakini…’watu
wakacheka.
‘Ulimbaka..usiogope
kusema hivyo…haya tuambie ulimbakaje, au ulifanyaje kwa lugha unayotaka wewe…’akaambiwa
‘Hizo dawa, alinipatia
huyo huyo mtaalamu, na ndiye
alinifundisha hilo…’akasema
‘Yeye ndiye
aliyekufundisha kumbaka binti wa watu…una uhakika na hilo, unamsema vibaya
marehemu..?’ akauliza wakili.
‘Nisikilize kwanza…yeye,
alipoona nampenda huyo binti, akaniuliza je namtaka huyo bint, ..kwa vile mimi
nampenda na nimejaribu kila njia,..nimeshindwa, nikasema ndio..ndio akanipatia
hizo dawa…’akatulia.
‘Ehee, endelea…’akasema
wakili.
‘Kiukweli mimi…,
sikutaka kulifanya hilo, kiukweli baada ya hilo tendo, nilijilaumu sana,..binti
wa watu…na..niliogopa sana, akija kumwambia bro, sijui itakuwaje,…ikabiid
nitoroke nyumbani kwenda kuishi kwa ..ndugu yetu mwingine..lakini sasa yalishatokea,..sijui
kwanini sikuweza kulifikiria hilo jambo wakati ule, aliponishauri huyo
mtaalamu, na zaidi aliniambia kuwa yeye hufanya…ndi- ndio tabia yake…’akasema
na watu wakacheka..
‘Ndio tabia yake
kufanya nini…?’ akaulizwa.
‘Akiwataka wanawake
huwa anawafanyia hivyo, kuna mashetani yake yanataka yeye afanye hivyo,
aliniambia hivyo-hivyo…na anafanya hivyo,..ili dawa zake zifanye kazi vyema…’akatulia
‘Sipendi kuyaongea
haya….ila ndivyo aliniambia, kuwa..kuna aina ya shetani, ili aweze kumsaidia
kwenye ammbo yake, inabidi yeye atembee na mabinti wadogo…’akatulia
‘Oooh…unajua
mumenilazimisha nyie….mimi niliapishwa nay eye nisije kulisema hili,..lakini
sasa, aah, hata sijui itakuwaje,..nimeshasema..mizimu inisamehe tu…’akasema
Dalali, sasa akionyesha kuogopa kabisa.
Mimi pale nilipokaa,
nikawaza jambo, nikamsogelea huyo wakili
, nikamwambia…
‘Hapa tutapoteza muda
mwingi bure kuna kitu muhimu bado hatujakigundua hapa…ukweli kuhusu sahihi na
dole gumba, vilitoka wapi,..huko kwingine tunazunguka tu, na bado hatujapata
ushahidi wa hilo, sahihi na dole gumba, lilipatikanaje..’nikasema kumuambia
wakili, …
‘Sawa…wewe usijali,…tutafika
huko….’akasema wakili na kumgeukia Dalali.
‘Tuachane hayo ya kumbaka
binti wa watu, kazi mliyoifanya wewe na mtaalamu, hebu sasa…turejee kwenye ajenda
yetu, jinsi mlivyoweza kuipata sahihi ya marehemu…ilikuwaje sahihi ya kaka yako
ikapatikana kwenye hilo deni…wakati hata wewe unaamini kuwa hilo deni sio…la
kaka yako..?
‘Mimi hilo sijui, ndio
maana napata shida kulikataa hilo deni….’akasema,
Dalali alipojibu
hivyo, mimi nikamsogelea huyo wakili
nakimwambia;
‘Samahani muheshimiwa,
ninaweza kumuhoji huyu mtu kidogo, kuna kitu ……?’ nikauliza na hakimu wakati
huo, alikuwa akiongea na wazee wa baraza,…nahisi aliona muda mwingi umetumika
kwa huyo shahidi…
‘Sawa endelea, ‘kabla hajaniruhusu akasema
‘Muheshimiwa hakimu,
nipo na msaidizi wangu hapa leo,…nataka amuhoji kidogo huyu shahidi, …’akasema wakili, wakili wa benki akasimama na
kutoa pingamizi
‘Anasimama kama nani…shahidi
au…?’ akauliza hakimu
‘Kama msaidizi wangu
kwa leo…kuna ushahid anautaka kuupata kutoka kwa huyu mshukiwa…itasaidia sana
kulimaliza hili tatizo la jinsi sahihi ya marehemu ilivyopatikana…’akasema
wakili
Hakimu akaniangalia
kwa makini, halafu akasema
‘Ni kweli, hata hivyo,
wewe ulipewa nafasi ya shahid na hukuweza kumalizia ushahidi wako je ndio huo
unataka kuendelea nao…na kwanini unataka kumuhoji huyo shahidi…?’ akauliza
hakimu.
‘Muheshimiwa
hakimu..kuna utata kwenye hii kesi, utata upo kwenye jinsi gani sahihi ya
marehemu ilipatikana, na dole gumba…hapa kuna kitu kimejificha, na mtu wa
kutusaidia, ni huyu na kijana wake..naomba nimuulize maswali machache…’nikasema
na hakimu akaangalia, saa na kusema
‘Sawa endelea…’akasema
hakimu
Mimi nikamsogelea
Dalali,…nikamuangalia machoni, halafu nikasema;
‘Dalali hebu simama…’nikasema
na Dalali akaniangalia kwa macho ya kushangaa
‘Nisimame,
nitasimamaje, na wakati,…mimi siwezi kutembea…na…’akasita, mimi nikatoa picha,
na kumuonyesha
‘Hii picha hapa ni ya
nani…?’ nikamuuliza
‘Ya kwangu…’akasema
‘Ukiwa umevaaa nguo za
hospitalini, hapa ulikuwa unakwenda wapi…?’ nikamuuliza
‘Sikiliza muheshimiwa…haya
ndio mambo nimeanza kuyalalamikia hapa , kuwa kuna hali inanitokea, nachukuliwa
bila kujijua…sijui kinachoendelea, …napelekwa,..wakati mwingine hadi baharini…’akatulia.
‘Jamani mnaweza
kuyaamini hayo…’nikasema nikimuangalia hakimu.
‘Kwani anaweza
kutembea…?’ akauliza hakimu
‘Kuna video hapa
inaweza kulithibitisha hilo,..huyu mtu pale hospitalini alipolazwa, amekuwa
akitoka usiku na kwenda baharini, sehemu nilipogundua hizo nyaraka za benki,
sasa atuambie aliwezaje kutembea, aliwezaje kufika huko,…?’ nikauliza
‘Ni kweli Dalali,
unaweza kutembea , kwanini sasa unatudanganya…?’ akuliza hakimu
‘Muheshimiwa hakimu,
mimi siwezi kutembea,..hayo yanayofanyika ni ….kitu mimi sikijui….ni…’akawa
analalamika kwa mikono.
Ple mimi nikamuangalia Dalali usoni…nikijua
kile nilichokitaka kwake nimeshakipata , kumjenga hofu, kwa haraka nikasema;
‘Naomba kitambulisho
chako…’nikamwambia Dalali, na Dalali
kwanza akasita baadae akakitoa kitambulisho chake,..na kunikabidhi, hisia zangu
ziliniambia kuna jambo,..na nilipokiangalia kile kitambulishi, nikahisi mwili mzima
ukinisisimuka,…nikatikisa kichwa, kukubali, na tabasamu likajaa mdomoni, halafu
nikamuuliza;
‘Dalali hapa kwenye kitambulishi
ndio sahihi yako..?’ nikamuuliza.
‘Ndio kuna tatizo gani
kwenye sahihi yangu..?’ akauliza na mimi nikachukua ile karatasi ya malipo ya
mkopo, nikaangalia, halafu nikageuka kumuangalia wakili..nikamuonyesha sehemu
ya sahihi, nikamuuliza huyo wakili…
‘Unaona nini hapo…?’
nikamuuliza wakili naye akabakia kushangaa, halafu akasema;
‘Oh…Sahihi
zinafanana…’akasema, hapo nikamgeukia Dalali,
‘Dalali sasa
umepatikana….’nikasema kwa sauti na Dalali akawa kanitolea macho ya kujiuliza
tu..
NB: Je ndio hitimisho
hilo, NI DALALI AU NI MAJALIWA?
WAZO LA LEO: Kibinadamu ni rahisi sana kumshuku mwingine ubaya, …na hata
kujaribu kuthibitisha ubaya wake,..lakini kumbe ubaya huo, tunaowashuku wengine
na kuwanyoshea vidole, sisi wenyewe tunao..na huenda tuao ubaya zaidi ya ubaya
wa huyo tunayemnyoshea kidole.
Ni sawa kibinadamu tunatakiwa kushauriana,
kukatazana mabaya,.na kuelekezana mema, huenda katika kufanay hivyo hata sisi
wenyewe tunaweza kujirudi…lakini iliyo vyema, kabla ya kutoa ushauri huo, au
kuelekezana au kunyoshea wengine vidole, tuanza kwanza kwetu sisi wenyewe, kwa
vitendo, ushauri wa vitendo hujenga mahusiano mema zaidi. Ushauri wa vitendo ni mwalimu mnzuri
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment