‘Sikiliza wewe si unataka tusaidiane kwa hili, kama kweli una nia
hiyo, niambia huyo mpenzi wa zamani ambaye unasema mna mapenzi naye ya
asili,…?’ nikamuuliza
Ilikuwa ni kama kitu kimemusa moyoni, akasimama, na taratibu
akageuka kuniangalia, akasema;
‘Kamwe siwezi kukuambia ni nani, hata hivyo nimekuambia mengi
ambayo sikuhitajika kukuambia, tulipatana mimi na yeye mapenzi yetu ya nyuma
yawe ni siri kubwa sana,…kumuongelea hapa, ni kama kumsaliti..kwaheri…’akasema
na kuondoka zake.
Tuendelee na kisa chetu
************
Siku zikazidi kwenda na
mimi nahitajika kwenda kusoma, na hali ya hatari inazidi kuniandama, na kama
nisipokuwa makini hata huko kusoma sitaweza kwenda kusoma tena, na nikikwama
hilo, basi malengo yangu ya mbeleni yangelikwama kabisa.
Kilichokuwa kikinikwaza ni
kuwa bosi wangu yaani mke wa familia,
anataka nimuambie ukweli kuwa huyo mtoto nimezaa na nani, nahisi kuna kitu
kilikuwa kinamsukuma hivyo, huenda, ameshanishuku.
Siku rafiki yangu ananitamkia kuwa siku akimgundua mtu anayetembea
na mume wake atamkamatisha kwa wale wahuni hatajali kuwa ni ndugu yake au ni
rafiki yake ndio siku aliyofunga kauli yangu ya kumuambia ukweli, …hapo
nikaomba zoezi la kwenda kusoma lifanyika kwa haraka.Nilichofanya ni kuongea na
wale watu wanaosimamia mchakato huo mnzima wa masomo yangu ili uwe tayari
iwezekanavyo. Ilikuwa ni kazi rahisi kwangu.
‘Ninachoshukuru, pamoja na yote hayo , mke wa familia hakuwa
akilifuatilia hilo, ilikuwa kama kalisahau, kwahiyo mipango yangu ya kusoma
ikawa inakwenda vyema, japokuwa sikuwa na amani,…na nilishukuru mungu kuwa muda
ulipofika tu, nikaondoka kwenda kusoma.
Sasa kabla sijaondoka, nilitaka nifanye mambo fulani ya kuniweka
kwenye amani, kwanza kuna huyo mdudu mtu, ambaye alishaingilia maisha yangu,
sikutaka hili la picha liishe hivi hivi, japokuwa mume wa familia alishasema
kazi hiyo keshampatia Makabrasha, lakini ni nani huyu Makabrasha,..ni mtu
asiyeaminika!
Ukumbuke kabla sijaondoka, rafiki yangu au bosi wangu, mke wa
familia aliwahi kunipatia kazi, kuwa nimtafuta mtu anayemzuzua mume wake, kwani
kasikia kuwa mume wangu ana mwanamke, ambaye anamfanya asiwe na amani, ..na
anasikia kuwa huyo mwanamke kazaa na mume wake…sasa hiyo kazi nilitakiwa
nimpatie mume wa familia kwa haraka.
‘Atakuwa ni huyo mpenzi wake wa asili…’ niliweka mikakati ya
hivyo, ndio maana nilitaka kumfahmu huyo mpenzi wa asili wa mume wa familia,
nilijua nikimfahamu tu, mizigo yote ataibeba yeye, tatizo ni hilo, la kuwa
kazee na yeye, je kama hana mtoto,..lakini muhimu ni kumfahamu huyu mtu ..maana
asipopatikana yeye, basi huyo mwanamke atakuwa ni mimi..’nilijisemea hivyo.
Mikakati ya kwanza na muhimu kumpata huyo mpenzi wa
asili,..mikakati ya pili, kumpata huyo mdudu mtu, hapokuwa kwa akili yangu ya
haraka, nilishaanza kumshuku huyo Makabrasha
Hapo nilikuwa na siku moja
ya kuyafanikisha hayo, sio kazi rahisi, nikaona kwa vile mikakati ya safari imeshakamilika,
hiyo hakuna wa kuzuia tena, labda mdada, bosi wangu kama angeliamua, kufanya
hivyo, angeliweza, lakini ingemchukua muda,…
Usiku huo nikapanga jambo, ...
Usiku huo, nikawaza sana,
na hatimaye nikaona haina budi, ni lazima nimpate mtu, ninayemuamini, nikaanza
kuwachuja rafiki zangu ninaowatumia kwenye kazi zangu, nikagundua kuwa kuna mtu
wangu mmoja wa karibu sana ambaye nikimpa hiyo kazi anaweza kuifanya bila
matatizo.
Tatizo la huyo mtu wangu wa karibu, yeye, kikazi ni mtu kivuli,
huwezi kufahamu kabisa kuwa anafanya kazi na mimi, napenda sana kumpa kazi huyu mdada,
nilishafanya kazi naye za siri, alitokea kuipenda hiyo kazi, lakini alikwama
kusonga mbele, mimi nikamuwezesha kisiri, ..na kiukweli huwezi kujua kabisa kuwa
huyu mtu anafanya kazi hizo, kabisa,…tatizo yeye alishaniambia kuwa hataki tena
hizo kazi,…
‘Mimi hizi kazi sitaki tena, nataka kutuliza maisha yangu na
familia yangu, sitaki kujipa presha…’siku moja aliniambia hivyo.
‘Lakini kazi ninazokupatia ni zile ambazo, huwezi kujulikana
kabisa, muhimu iwe hivyo hivyo, siri ndio ufunguo wa kufanikisha hilo, usije
kulogwa kumuambia mtu kuwa uanafanya hizo kazi, unasikia, sasa niambie ni kwanini
unaogopa kuendelea kuzifanya, ina maana juhudi zangu hadi kukusomesha hazina
maana tena..?’ nikamuuliza
‘Nina maana yangu kubwa, na sitaki mtu afahamu hilo, hata wewe,
haya nayafanya kwa ajili ya maisha yangu ya baadae, mimi nataka kuwa mke wa
familia muadilifu, na hili litakuwa linavunja uaminifu wngu kwa mume wangu…’akasema
‘Sio bosi wangu kakushauri uache kazi hizi au sio , kwa vile bosi
wangu keshaanza kunichukia mimi..,?’ nikamuuliza
‘Hapana , wala mimi sina ukaribu naye, unajua kazi zetu zilivyo,
sizani kama yeye anafahamu kuwa nafanya kazi kama hizo, ukumbuke hili ulinionya
wewe mwenyewe, na ndivyo nilivyo, …’akasema na kweli nilimuamini.
Unapofanya kazi kama zangu unaweza ukawa na watu wako, hata
muajiri wako asiwafahamu hata kama huyo mtu ana mume wake , huyo mume wake pia anaweza
asijue kuwa mke wake anafanya kazi kama hizo…inakuwa baina yangu mimi na yeye,
na yeye anafahamu ni kwanini inatakiwa iwe hivyo. Na malipo yake sio mchezo.
Huyu msaidizi wangu ni mdada, na sio mchezo, kwenye kazi kama hizo
namuaminia, anaijulia kazi, anajua mbinu za kila namna za kupata siri fulani zilizojificha,
na ni msiri mkubwa sana, na kilichonipa nguvu na kumuamini, ni kuwa kweli hata
mume wake alikuwa hajui kuwa mke wake anfanya hiyo kazi.
Siku aliponiambia hataki
hizi kazi , nilipata shida sana,maana ni mtu niliyekuwa nikimtegemea kwenye
kazi zangu za namna hiyo, sio kwamba sikuwa na watu wengine,lakini huyu
nilimuamini sana kwenye hizo kazi, na hata aende wapi nikimuita atafika hapa
mjini hata bila kujulikana, akafanya kazi, na akatoweka bila mtu kumfahamu kuwa
alikuwa hapa jijini, ni mbinu zetu za kujibadili.
Nilipomkumbuka hapo hapo nikamtafuta kwenye simu, nikampata, nikamwambia,namuomba anisadie kazi mbili muhimu
sana, akaniuliza kazi gani, hakusema nilishakuambia sitaki kazi, nikajua huenda
sasa hivi huyo mdada hana pesa.
Mimi nikamwambia, moja kwa moja bila kuficha, kuwa kuna mtu anatakiwa
yeye amchunguze, kwa ukaribu nahisi huyo
mtu anataka kuingilia maisha yangu..
‘Mtu gani bosi, unajua nilishakuambia…’akataka kujitetea
‘Ni Makabrasha, …’nikasema kwa haraka
‘Mungu wangu, huyo mtu tena…’akasema
Hilo neno ‘tena’ nikahisi lina jambo, lakini sikutaka kumdadisi
zaidi, mimi nikasema;
‘Sizani kama unamuogopa huyo mtu, ni saizi yako kabisa, mimi
nakuaminia,..nafahamu kuwa watu wanamvumishia ujasiri ambao hana, wewe ni
jasiri zaidi yake, unaweza kuzivunja nguvu zake kwa siku moja tu, au
umeshalainika, na mume wako, usiniangushe, nakuamini kwa kazi hiyo..’nikasema
‘Kwanini unamtaka huyu shetani....’akasema, na alivyotamka hilo
neno ‘shetani’ nikahisi kweli kuna jambo kati yake na huyo Makabrasha. Mimi
nikamwambia kwa kifupi;
‘Huyu mtu anataka kuniingila kwenye maisha yangu binafsi,…usiniulize
ni kwa vipi, muhimu kwako, ni kumfuatilia, kumchunguza, na utakuja kugundua ni
nini kipo anakifanya ili kutaka kuangamiza maisha yangu, na ni ni lengo lake, hakuna
mtu ninayemuamini kwa kazi hii zaidi yako wewe, malipo yatakuwa zaidi ya
unavyofikiria…’nikamwambia.
‘Nilijua tu, ....huyu mtu anataka kumjaribu kila mtu, nahisi
anataka kufanya jambo kubwa sana,… na kinachonishangaza ni kuwa hata polisi
wanashindwa kumkamata huyu mtu, ana ulinzi gani huyu mtu, kiukweli yeye, ni… ni
mjanja kupita maelezo, lakini …mimi naona hapo alipofikia kavuka mpaka, kuna
haja ya kumuwahi kabla hajafika mbali...’akaniambia.
Hapo nikajua kweli nimelifikisha kwa mtu ambaye huenda naye
katendwa, huenda alishaingizwa kwenye mitego ya huyo mtu, na jamani sio kwamba
namteta vibaya marehemu, huyu mtu alikuwa mbaya sana, na kama angeliendelea
kuwa hai, sijui tungelizunguza nini leo, alishafikia kubaya…’mzungumzaji akaendelea na
maelezo yake.
‘Kwahiyo unasemaje, upo tayari kuifanya hiyo kazi, ...au?’
nikamuuliza
‘Umesema kuna kazi mbili, hiyo ni ya kwanza , hiyo kazi nyingine ya
pili ni ipi, na unataka niifanyeje, na kwa hiyo ya kwanza, umesema unataka nimchunguze,
kuwa kuna jambo kakufanyia, au anataka kukufanyia, au niwekezeje nguvu zangu
kwa hiyo kazi …?’ akauliza na hapo nikajua kakubali hiyo kazi.
‘Kumchuza nyendo zake, na kujua ni nini kakifanya dhidi yangu,
nahisi kuna kitu anakitaka kwangu, sasa wewe fuatilia ujue ni kitu gani,na
kwanini anafanya hivyo, je ni kwa ajili yake au kuna mtu kamtuma, mengine utajua mwenyewe lakini nataka iwe
siri…’nikasema
‘Toka lini kazi zako kwangu zikawa sio za siri, najua kabisa kila
kazi ukinipa ni ya siri, au sio…’akasema
‘Hii ni ya siri zaidi…’nikasema
‘Upo wapi Dar, au Zanzibar, na lini utasafiri…?’ akaniuliza
‘Nipo Dar, natarajia kusafiri kwenda kusoma hivi karibuni, ila
nitakuwa nikiwasiliana nawe, wewe ndiye utakuwa mawasiliano yangu, nilitaka
nikuachie majukumu yangu lakini wewe haupo ofisini ulishaacha kazi, ila kwa
kazi hii inabidi nikuachie…’nikasema
‘Ile safari yako…, imeshafika sio umeweza kuruka vihunzi,..sawa
nenda kasome uje uanzishe kampuni yako, uachane na hizo kazi za kutumwa…huenda huko
baadae , lakini sijui, nimechoka na hizi kazi, …naweza kuja kwako kuomba kazi,…
lakini sio kwa sasa…’akasema
‘Usijali, wewe ni mtu wangu ninayekuamini sana, ni wewe tu
kukimbilia kuacha kazi ngoja nimalize masomo, utarudi tu..’nikasema
‘Najua..hilo usiwe na shaka kabisa…nataka tu unielewe, siwezi
kukuambia hili, kuacha hizi kazi nina maana yangu kubwa, kwahiyo unasema
tutawasilianaje sasa…’akasema na kutulia
‘Unajua hii kazi inahitajia uharaka fulani, mimi nitakupatia namba
ya kuwasiliana na mimi, ikifanikiwa haraka nitashukuru zaidi, na malipo yake kama kawaida yetu..’nikasema
‘Swala la malipo sio tija, wakati wote nikiwa na shida, ni wewe
unanisaidia, hiyo nitaichukua kama kulipa fadhila tu…ila msimamo wangu ni ule
ule, kwa hivi sasa sitaki ajira, sitaki kazi za mikataba, nitafanya kimia
kimia, na tutamalizana hivyo hivyo…’akasema
‘Usijali, ni lazima nikulipe…’nikasema
‘Na hiyo kazi ya pili ni ipi…?’ akaniuliza
‘Huyo mume wa familia, mke
wa bosi wangu, eeh, ana mpenzi wake wa zamani, kabla hajaoa, walikuwa naye huko
kijijini, nakata unitafutie huyo mpenzi wake alikuwa ni nani,..’nikasema
‘Unasema nini, mmh, kwanini unataka kumuingilia bosi wako, kuna
nini, ..?’ akauliza kama hajasikia vyema, na ilinipa mashaka huko kuitikia
kwake, kama kushtuka, na maswali yake hayo
‘Unitafutie huyo mchumba wake alikuwa ni nani, ni muhimu sana
kwangu kumfahamu, ilikuwa siri kubwa,, hakuna aliyelifahamu hilo, nimelifahamu
lakini sijamfahamu huyo mchumba wake ni nani..’nikasema
‘Subiri kwanza kuna mtu ananisumbua hapa…’akasema na kukata simu,
basi nikasubiria na baadae nikampigia simu, simu yake ikawa haipatikani. Nilimpa
muda, kama masaa mawili nikampigia tena..
Alipokea na nikamuuliza kwanini alikata simu, akaniambia kuna mtu
alifika, na hakutaka asikie anaongea nini na mimi, mimi nikamuelewa maana
kiukweli kazi zangu mimi na yeye ni za siri kubwa.
‘Ni hivi, mimi nataka umtafute huyo mtu ni nani, na nimegundua
jambo, kuwa mume wa familia, (hapo nilimtaja jina lake) ana ukaribu na
Makabrasha, nataka kufahamu ni kwanini wapo na ukaribu hivyo, na pia, nahisi
huyo mchumba wa huyu mume wa familia, anaweza akawa na ukaribu na huyo
Makabrasha, nataka kufahamu ni kwanini, na je kuna kitu mume wa familia
kafanyiwa, sasa sina uhakika kama ni Makabrasha au kuna mtu mwingine..’nikasema.
‘Sikiliza rafiki yangu, bosi wangu, mara nyingi mimi napokea kazi
zako bila masharti, nikijua ni nini ninachokifanya, ila hii kazi, sio sitaki
kuifanya, ila …inanipa ukakasi, huyu mtu anayeitwa Makabrasha sio mtu mwema,
nilishamchunguza kabla, huyu mtu haaminiki , pili inaonekana ni kazi ndefu,
maana hapo umeshamgusia hata mume wa familia, ni zaidi ya watu watatu hapo,
natakiwa kuwachunguza, no, wanne...’akasema
‘Kwahiyo utazifanya hizo kazi mbili nilizokupa, au ndio
unanikatalia hivyo..kwangu mimi ni muhimu sana, na wewe ndiye mtu wangu wa
karibu wa kazi zangu za siri, na nilitaka chochote utakachogundua kiwe siri
kati yangu mimi na wewe, unasikia..?’ nikamuuliza
‘Siwezi kukukatalia, lakini …mmh, kumchunguza huyu mtu, ni
kunitaka mimi nihatarishe maisha yangu na familia yangu, nilishakorofishana
naye na akanitegea, si unajua mambo yake,…’akasema
‘Mambo gani yake..?’ nikamuuliza
‘Huyu mtu anaendesha biashara za mlungula(blackmaili), na akitaka
akupate kwa jambo fulani, atafanya kila hila ili akuingize kwenye biashara
hiyo, na ..bila kukuficha alishanitega kwa hilo…’akasema
‘Mhh, ndio maana unaogopa..hujamalizana naye ?’ nikauliza
‘Sio kwamba naogopa, ila nakuelezea ni kwanini nasita kuifanya
hiyo kazi..mtu kama huyo kumalizana naye sio rahisi, kila akikutaka atatumia
vitisho, …si unajua biashara hiyo ilivyo,…ila nitapambana naye nione mwisho
wake ni nini.’akasema
‘Sasa utaifanya hiyo kazi au hutaifanya…maana kumbe ulishaianza au
sio?’ nikamuuliza
‘Bosi unajua , sitaki kufanya kazi hizo tena, nilishakuambia,
lakini pia sipendi kukukatalia, na nikikutolea udhuru, ujue kuna sababu ya
umuhimu...’akasema
‘Na mimi ukiona ninakupa kazi hiyo wewe peke yako ujue ina umhimu
sana kwangu, tafadhali, ..huwa wakati wote natoa amri kwako, lakini hii
ninakuomba, ni muhimu sana kwangu..’nikamwambia.
‘Mhh,.... ama kwa Makabrasha, hiyo kazi ninaweza nikaifanya,..kwa
vile… lakini sio kwa hiyo kazi nyingine, ya kumchunguza huyo mchumba wa mtu,
naona huko kuna safari, kuna mambo mengi, na sitaki kushikilia kazi zaidi ya
hii, na hii ni kwa vile inanigusa na mimi..’akasema hivyo na kunifanya
nishangae kidogo.
‘Kwahiyo kumbe kuna kitu kakufanyia,..ok, huwezi kuniambia ni kitu
gani…au umeshaingia kwenye ajira yake nini…?’, nikamuuliza .
‘Hapana sina hisa naye kabisa, lakini sitaki kuchukua kazi mbili
kwa sasa, nina majukumu mengi, na..nimekubali hiyo moja tu , kwa vile wewe ni
rafiki yangu, na unanidai sana, fadhila zako kwangu ni nyingi sana…vinginevyo
sina sababu nyingine ya msingi, ya kuikataa kazi hiyo ya pili, na zaidi ya
kwanini, siwezi kukuambia, unielewe tu…’akasema.
‘Hizo kazi zote mbili kwangu ni muhimu sana, unajua mimi nakwenda
masomoni, sitakuwa na muda wa kufuatilia, na wewe ndiye unyeweza kuzifanya
kazi hizo kwa uamakini na kwa siri kubwa,..Nakuomba
sana...’nikajaribu kumsisitizia, na yeye akasema;
‘Sitaweza kukufanyia kazi zote mbili hiyo moja sawa, maana
Makabrsha namfahamu na nilishawahi kuifanya kazi inayomuhusu, lakini hiyo
nyingine hapana, sitakuwa na muda huo, nielewe hivyo,...’akasema.
‘Kwahiyo hiyo kazi kumuhusu Makabrasha, utaifanya, lakini kwa kunisaidia
kumtafuta huyo mtu mwingine, ndio umesema hutaiweza, unanipa mashaka ujue, je
nikikuambia uiache hiyo ya makabrsha uifanye hiyo nyingine je…?’ nikamuuliza,
na yeye akasema.
‘Hiyo ya makabrasha nitaifanya tu kwa vile nimeona huyo mtu na
mimi namtafuta sana, nataka nimfahamu vyema, nije kulipiza kisasi kwake,,...japokuwa
kwa ujumla sikutaka niifanye kazi zozote za namna hii tena, lakini kwa vile na
wewe una muhitaji, basi ndio nikaona niichukue hiyo, ...’akasema.
‘Kwani kuna nini kikubwa huyo Makabrasha alikufanyia mpaka utake kulipiza
kisasi kwake niambie ili nijue huenda ni yale yale..?’nikamuuliza.
‘Unaona, ....sitaki mtu kuniingilia hayo mambo yangu, kama unataka
niifanye hiyo kazi, sitaki kuniuliza-uliza maswala kunihusu mimi binafsi,
nitakuambia yale unayoyataka kuyafahamu kwenye kazi yako, ya kwangu niachie
mimi mwenyewe, nina maana yangu na sitaki mambo yangu yaje kuwaumiza wengine...’akasema
‘Mhh, safari hii nakuona mwenzangu unaniacha njia panda, sijui
kuna nini kinaendelea kwenye maisha yako, ujue mimi nipo tayari kukusaidia,
tusaidiane ndio urafiki wa kweli ...’nikasema.
‘Kwa hili huwezi, hutaweza kunisaidia, haya ni maswala binafsi tu
sipendi yakumguse mtu mwingine, sipendi…’akasema
‘Haya sawa nimekuelewa…’nikasema
‘Wewe nenda kasome, kwa kazi inayomuhusu huyu jamaa, anayejiita wakiliw
a kujitegemea wa kimataifa, nitaifanya..ila nimjuavyo mimi huyu mtu ni mbaya,
na hatari,kuliko unavyofikiria wewe, hata hivyo, siwezi kukuambia lolote mpaka
nimalize uchunguzi wangu, na sikutaka niyaongee haya kwenye simu na kwa mtu
yoyote, mpaka nimalize kazi yangu...’akasema
‘Ok, itakuwa vyema, kama ulishaianza…’nikasema
‘Saana, niamini kwa hilo, utapata taarifa nzuri tu…’akasema
‘Basi ukiwa tayari kuhusu huyo mtu tutaongea ili nijue tufanye
nini, ni muhimu sana kwangu,..na nakuomba ulifanyie kazi hilo kwa haraka
iwezekanavyo, na kwa huyo mtu mwingine nitajua ni nini cha kufanya, hata hivyo
nina ombi moja kwako zaidi...’nikamwambia
‘Ombi gani hilo...’akaniuliza
‘Nina mikakati ya kazi kubwa baadae…, nina mipanglio mingi ya
kimaisha, nikimaliza elimu yangu huku nataka tuwe wabia mimi na wewe.,.kwahiyo
ninakuomba ujiandae kwa hilo, weka kumbukumbu za kazi zetu za zamani, kusanya
ukweli wa kusaidia kwenye kazi zetu, tengeneza maktaba fulani yenye kumbukumbu
za kesi na matukio, hasa za watu mashuhuri, nk..si unajua ninachotaka
kukuambia..’nikasema .
‘Hilo halitawezekana..hujanielewa mimi sitaki tena hizi
kazi,..nilikuambia ukija utaniajiri awali nilikuwa nasemea tu, nataka
kubadilika, kuwa mtu mwingine kabisa, kama uhai bado upo, kiukweli kazi hizi sio
nzuri, zinamuweka mtu mashakani muda wote, mimi sitaki kujishughulisha na haya mambo
tena, kwa manufaa yangu ya baadae...’akasema.
‘Sawa nimekuelewa, lakini mimi nina imani kuwa tupo pamoja, hata
kama kuna mambo yametokea ya kukwaza, bado tuna mafungamano ya kikazi,
unafahamu kazi zetu hizi zilivyo, unaweza ukasema humuhitaji mtu, baadaye ikatokea
jambo ukamuhitajia sana mtu wako wa zamani, usitupe mti na jongoo
wake..’nikamwambia
‘Kwa maisha haya ninayopambana nayo, sizani kama kuna mashikamano
na mtu kwenye kazi kama hizi, naomba tuishie hapo ,na ni vyema usitake kujua
mengi zaidi kunihusu mimi, usiniulize tena , samani sana....’akasema akitaka
kukata simu
‘Sawa kama unataka iwe hivyo…’ nikasema
‘Kiukweli nataka iwe hivyo..’akasema
***********v
Ndugu mwenyekiti ili uweze kuipata hii picha vyema, nawarejesha
kidogo nyuma, nilishaliongelea hili kabla, awali, jinsi gani nilivyoweza
kurejea nyumbani kwa dharura, lakini kuna mambo sikuweza kuyaongea awali,
kwasababu za msingi.
Sasa hivi nitafichua yale yaliyojificha kwenye kurejea kwangu, ambayo
sikuyaongea awali , hayo ninayoongea sasa yanafichua ukweli mwingine ambao
utahitajika sana kama nilivyogusiwa, sitakiwi kuingilia maswalaya mauaji ya
Makabrasha, nitajaribu kufanya hivyo.…’akasema.
‘Sawa endelea, lakini ni muhimu ukalichunga hilo, swala la mauaji
halipo kwenye kikao chetu hiki, hilo swala lipo mikononi mwa polisi….’akasema
mwenyekiti
Siku nilipokuwa masomoni,
wakati najiandaa kufanya mtihani fulani muhimu, nilipokea ujumbe kama huu… ‘
‘Utahitajika ‘’Dar kwa haraka,
kusaini mkataba wa hiari, dhidi yako na mzazi mwenzako, lakini bado ninamdai pesa
nyingi sana, kama itatokea sitalipwa pesa zangu, sitakuwa na jingine bali
kuwakilisha hizi picha kwa rafiki yako,…’’ ule ujumbe ukaambatishwa na
picha, mojawapo ya picha mbaya, ambazo zilionyesha yale niliyokuwa nikifanya na
mume wa familia, hiyo ikiashiria vitisho, kuwa nisipofanya hivyo, picha hiyo
itafikishwa kwa walengwa.
Nilipopata huo ujumbe nikampigia simu huyu mtu wangu wa karibu,
nikamwambia anifanyie uchunguzi, ni kitu gani kinachoendelea kati ya Mume wa
familia na mke wa familia, na hapo mtu
wangu huyo, akaniambia hilo ameshalifanyia kazi, na kusema;
‘Mume wa familia kaingia kwenye mtego na adui yetu,..’akasema
‘Una maana wakili Magumashi..’nikamwambia
‘Huyo huyo, …. kwahiyo inabidi afanye kila anachotakiwa kukifanya
, na mengi ni kwa ajili ya masilahi ya huyo adui yetu, ikiwemo kukubali kuingia
na adui yetu kwenye mkataba unaoidhinisha adui yetu kupata hisa kwenye
makampuni ya bosi..’akaniambia.
‘Haiwezekani...ooh, mbona hilo ni
gumu sana…unauhakika na hilo..?’nikasema kwa mshituko mkubwa.
‘Ndio hivyo, kuna mengi yamefanyika, na mshika usukani ni huyo
adui yetu, inavyoonekana ni kuwa huyu adui yetu kaingilia mambo mengi, lakini
nia na lengo lake ilikuwa kuingiza makucha yake kwenye mali za bosi wako…’akasema
‘Una uhakika na hilo…?’ nikauliza
‘Zaidi ya uhakika… na ukumbuke kuwa bosi wako na mume wake hawapo
kwenye mahusiano mazuri, hawajui yote hayo yalipikwa na huyu adui yetu,
ingawaje hadi sasa wana ndoa hao, wapo kwenye kutimiza wajibu wa kibinadamu,
kutokana na huo wajibu, itawabidi waendelee kuwa wanandoa, vinginevyo, kitu
kinachoitwa ndoa ni kama hakipo...’akasema.
‘Hali gani hiyo ya kibinadamu?’ nikamuuliza.
‘Mume wa familia kutokana
na hiyo ajali, kuna matatizo mengi
yanazidi kutokea, kuna dalili za maradhi ya kuota kwa vitendo, kuna
kuchanganyikiwa, …unaona..na inaonekana hali aliyo nayo sio ya kupona leo, na
mke kama mke hatakiwi kumtelekeza mumewe kwenye hali kama hiyo.., nahisi kama
isingelikuwa huo ugonjwa sasa hivi tungeliongea mengine...’akasema.
‘Kuna nini kikubwa ulichokigundua, kilichosababisha hadi
hiyo ndoa iingiwe na tatizo kubwa kiasi hicho, ni mambo yao ya ndani kwa ndani
au kuna msukumo mwingine kutoka nje...?’ nikamuuliza.
‘Hayo unayafahamu sana wewe, sioni haja ya mimi kukuambia,
japokuwa kuna mbinu zilizotoka nje, zilizojengwa kitaalamu sana na wajanja, ili
ionekane hivyo ilivyo, kwa muda niliofanya uchunguzi wangu, nimegundua mengi,
kumbe hata wewe upo kwenye mchakato huo, sikutegemea, kumbe unanipa kazi ambayo
unaifahamu ...’akasema
‘Mimi kwa vipi..sielewi kitu ndio maana nikakupa hiyo
kazi..niambie kwa vipi?’ nikamuuliza
‘Hahaha..usijali, ..japokuwa imeniuma sana, kuwa kumbe nafanya
kazi kwa mtu ambaye ni mmoja wa watu wanaonichoma kisu moyoni mwangu...’akasema
akiongea kwa sauti yenye huzuni.
‘Una maana gani, ‘mimi kukuchoma kisu..’ ?’ nikauliza
‘Usijali, utakuja kujua , lakini sio sasa…’akasema
‘Ni kwanini sasa hutaki kuniambia ukweli...nimekufanyia nini mimi
kibaya , niambie ukweli, kama kuna jambo nimekukosea, ni bora uniambie, huenda
kuna sababu ya msingi ya mimi kufanya hivyo, ila wewe hufahamu’ nikamuuliza na
kujaribu kumuelezea, ili nifahamu ni jambo gani hilo, nililolifanya hadi
mwenzangu afikie kuumia kiasi hicho.
‘Ukweli unaoufahamu wewe unatosha, na nakushauri ufanye kama wao
walivyotaka, na watakavyotaka, kwa hivi sasa…hakikisha umefika huku nyumbani
bila kukosa,…, ufanye kama watakavykuambia, baada ya hapo, mengine yatafuata,
kwa hivi sasa wameshikilia mpini, ukikosea kidogo utakuja kujuta,..’akaniambia.
‘Ina maana hata wewe upo kwenye huo mchakato au umeligundua hilo
kutokana na ule uchunguzi niliokuambia…?’ nikamuuliza
‘Hata siku moja siwezi
kushirikiana na hao mashetani, hili ninalokushauri ni kutokana na
uchunguzi wangu, nifanyavyo kazi zangu hutaweza kunielewa, lakini mwishi wa
siku nitakupatia taarifa yako..’akasema
‘OK…’Nikasema hivyo, halafu akasema
‘Siku nikimaliza hii kazi, kila kitu kitakuwa hadharani, na
nitahakikisha kuwa kama kuna kundi, kama kuna njama, basi zitafikia kikomo
chake...kama ni kundi, nikitoka kwa huyu mtu, basi nitamuendea mwingine, mpaka nihakikishe nimemaliza
kazi...’akaniambia
‘Unaposema kundi, au watu wengine ni akina nani, inaonyesha
umeshawagundua hao watu au sio?’ nikamuuliza
‘Mhh, ,,kwa hivi sasa siwezi kukuambia kitu, nipe muda kidogo, cha
muhimu ni kuhakikisha kuwa hili jambo nimeliweka sawa, nataka kuhakikisha kuwa
hawa wananitesa moyo wangu, wanasambaratika, na hakuna kitu kama hicho tena, na
kama ni njama, zinazofungamana na mwenza wangu, nitahakikisha nazifahamu, na
kama yeye anahusika,…oh, hata yeye mwenyewe atajuta kufanya hivyo, ..’akasema
‘Mhh, sasa hapo unazidi kunichanganya, na huyo mwenza wako ndio
nani tena, ndio huyo mume wako ?’ nikamuuliza
‘Usinidadisi sana kuhusu hilo, ila yeye ndiye moyo wangu,
unasikia, ni, ni....’ simu ikakatika, na ilikatika kama vile mtu kapatwa na
tatizo, ikanibidi nipige simu, kwa mtu wangu mwingine, yeye ni msaidizi wake,
katika mambo yetu ya utendaji, nikamhoji,
‘Unamuulizia bosi, mbona alishaacha zile kazi zetu…’akasema
‘Yupo salama ..ebu mfuatilie hata kwa simu tuone kama yupo
salama..’nikasema na ikachukua muda, halafu akawa hewani na kusema
‘Yupo salama bosi..’akasema
‘Je kwa hivi sasa anafanya kazi gani..?’ nikamuuliza
‘Hajulikani sana bosi, nahisi yupo nyumbani…’akasema
‘Kwahiyo hana kazi yoyote yupo nyumbani tu, au ana kazi gani
maalumu anaifanya kwa sasa y akumuingizia kipato..?’ nikamuuliza
‘Si kwamba yupo nyumbani, si unajua alivyo, anaweza kuacha kazi
hii, kumbe ana kazi nyingine, kuna sehemu anafanya kwa muda,…anakwenda huko mara
chache chache, ila mara nyingi anaonekana yupo peke yake, yaonekana kuna jambo
linamtatiza, anakuwa kama kachanganyikiwa hivi..’akasema.
‘Kwa mtu gani huyo anapoonekana akifanya kazi ...unamfahamu huyo
bosi wake mpya?’ nikamuuliza
‘Ndio namfahamu huyo bosi wake, japokuwa awali alifanya ni siri,
lakini nilimfuatili mpaka nikaja kugundua wapi anapofanyia hiyo kazi, japokuwa
sio kwa siku zote,...’akasema
‘Au labda anafanya kazi hapo kwa ajili ya kupata taarifa, ..?’
nikamuuliza
‘Mhh, sizani,…hapo sina uhakika bosi …’akasema
‘Ni kwa nani hapo anapofanyia kazi, nipe taarifa kamili, sio
unanipa taarifa kama unaogopa, ni kwa mtu gani anapofanya kazi kwa sasa?’
nikamuuliza kwa hasira
‘Ni kwa Makabrasha bosi, ...mara nyingi anaonekana ofisini za siri
za kwa Makabrasha, inaonekana kaajiriwa na Makabrasha, au kuna kazi maalumu anaifanya
kama ulivyosema, sina uhakika na hilo...’akasema na hapo hapo nikakata simu.
Sikupoteza muda nikapanda ndege na kuja Dar,ndivyo ilivyokuwa kuja
kwangu Dar, kwa ghafla .... na sasa safari yangu hiyo iligundua nini, na
ukumbuke ndicho kipindi Makabrasha aliuwawa, ukumbuke ndipo kipindi mume wa
familia anaumwa…kuna mambo mengi hapo yamejificha…akatulia pale alipoona
mwenyekiti akiongea na simu
‘Niendelee mwenyekiti…’akauliza
WAZO LA LEO:
Mambo yanayohusu imani za watu , hisia za watu, upendo wa watu…, mambo hao ni
nyeti sana, ni vyema, ukikutana na vitu kama hivi uwe makini sana kuviingilia.
Mtu akiamini, akapenda, huona vingine vyote havina maana, anaweza hata akafumbia
macho elimu yake, na akafanya mambo ambayo kwa elimu yake, hastahili kuyafanya
hayo. Ndio maana wanasema, mwenye kupenda haoni, hata akiona kibaya kwake, ni
kizuri, akiona chongo ataita ni kengeza.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment