Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, February 13, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-80



‘Wewe umesema uliwahi kusikia mambo kuhusu mkataba wa familia kupitia kwa rafiki yako, na ina maana kuwa wewe ulikuwa unafahamu vipengele vyake, na ulifahamu kuwa ukifanya lolot baya, inakuwa ni tatizo kwa mume wa familia, huoni hapo unatudanganya,..kuwa wewe ulijua hatari yake na bado ukatumia mbinu ili umpate mume wa familia, ukijua kuwa utapata masilahi fulani baadae…?’ akauliza wakili 

'Masilahi gani...' akauliza mdada

'Mali, na hata kama ndoa hiyo ikivunjika wewe utaolewa na mume wa familia

'Kwanza umesema mali, kama ndoa itavunjika, huyo mume atapataia wapi mali, wakati hana kitu, atarudia kwenye umasikini wake, maana atanyang'anywa kila kitu si ndivyo mkataba unasema wao halali unasemaje...?' akauliza mdada.

'Kwahiyo kumbe wewe ulikuwa unafahamu kila kitu, kwanini sasa hukufanya juhudi za kuhakikisha hilo tendo halifanyiki...?' akaulizwa

'Tendo gani...?' akaulizwa

'Lililokufanya upate huo ujauzito..kama kweli hukudhamiria hilo litendeke kwa kuangalia masilahi fulani kwako...'akaambiwa.

Tuendelee na kisa chetu

*************.

'Kuhusu undani wa huo mkataba nilishasema nilikuwa nasikia rafiki yangu akiongea baadhi ya vipengele vyake,  na moja ya vitu alivyoviongea kuhuus vipengele hivyo, ni kuhusu miiko ya ndoa, alinielezea kuwa mume wake asingeliweza kusaliti ndoa yake, kwani anafahamu ugumu wa mkataba wao ulivyo…’akasema

‘Kwahiyo kwa vile ulilifahamu hilo ukataka umshawishi mume wa familia ili umpate wewe, kwa yeye kuvunja hiyo miiko, ili ndoa yao, ivunjike, na wewe uchukue nafasi ya mke wa familia au sio…’akaulizwa

Mdada huyo kwanza akamuangalia huyo wakili kwa makini, halafu akatabasamu na kusema

‘Kama ni kufanya hivyo ningelifanya hivyo zamani sana, lakini hiyo sio tabia yangu, ulizia, utaambiwa, usitake maneno ndio yawe ushahidi, wakati matendo yalikuwepo, mume wa familia alikuwa akijifanya mpole kwa watu lakini mkibakia naye wawili huwezi amini kuwa ndio yeye, …’akasema

Mume wa familia akatikisa kichwa kama kulipinga hilo.

‘Kiukweli hata walivyoniambia kuwa mkataba wao unawapa mamlaka ya kufanya kila kitu sikuamini, maana mkataba ulikuwa umesajiliwa iweje leo mkataba uwe tofauti,…nikajua kuna jambo limefanyika, nyie mawakili tunaowaamini mnageuza batili kuwa haki, au sio...baadhi yenu nyie, mnathamini sana pesa, na kuacha taaluma zenu pembeni…’akasema na hapo wakili akanywea, na kuangalia pembeni

‘Niambie muheshimiwa wakili, kwanini mligushi huo mkataba, maana hilo sasa lipo wazi,..wewe ndiye wakili wa kutetea mkataba wa kugushiwa, kwanini ulikubali kuusimamia mkataba uliogishiwa,...?’ akauliza mdada

‘Wewe hutakiwi kuniuliza maswali mimi, wewe kama shahidi, unatakiwa ujibu maswali yangu, na sio wewe kuniuliza maswali…’akasema wakili

‘Haya uliza hayo maswali yako, lakin ukae ukitambua kuwa wewe unatetea mktaba batili,.. na ukizungumzia mkataba ujue unazungumzia mkataba upi, mliogushi nyie , au huo wa kitapeli, au..wa halali, ubainishe maswali yako, maana wewe ndiyewakili wao, na unawatetea matepeli…’akasema mdada na mume wa familia akataka kuongea lakini wakili wake akamzuia

‘Endelea na maelezo yako…’akasema mwenyekiti.

 ‘Kwahiyo kiukweli ndugu mwenyekiti, mimi nilikuja kuutambua ukweli kuwa mkatba umegushiwa,  baada ya kurudi masomoni. Na nikagundua ubabaishaji wao wote…na ushahidi ninao, mkitaka kila kitu naweza kukiweka hadharani..’akasema

‘Endelea na maelezo, ushahidi baadae…’akasema mwenyekiti

‘ Huyu mume wa familia kwa kujiamini aliniambia kuwa akitoka huku kwenye kikao atakuwa kamaliza kazi, kila kitu kitakuwa kwenye miliki yake, kwahiyo kinachofuatia ni kuhakikisha kila kitu sasa kinakuwa wazi, mambo ya urithi, na umiliki za mali, nay eye kuchukua hatamu kama mume wa familia…’akasema.
‘Kiukweli kimoyo moyo nilicheka sana, maana ukweli nimeshauafahamu,  nikajua huyu mtu keshaharibiwa akili, nilitumia lugha ya kumuonya kuwa hilo haliwezekani, yeye aliniona mimi ndiye mjinga nisiyeelewa, na akaniambia, kama ikishindikina yeye ana plan B, sasa muulizeni plan B, ni ipi hiyo, ndugu wakili mtetezi…’akasema mdada, akimuangalia wakili.

 Wakali akawa kimia, akimuangalia tu

' Mimi nilimwambia cha muhimu kitakachomsaidia, ni yeye kupigania ndoa yake tu, vinginevyo, atakosa kila kitu, ndoa, na mali, nilimuambia kuwa kilichomuharibia ni tabia yake hiyo mbaya, tamaa, na umalaya, ..na nilipotamka neno hilo akanijia juu, kuwa nimemtukana, nahisi ndio maana alipokuja hapa, akawa na jaziba hizo hizo za kauli hiyo, lakini matendo…yanajionyesha….’akasema

'Je sio haki kwa baba kudai haki za mtoto, je sio haki kwa mume mliyezaa naye kudai haki za mtoto wake,…?’ akauliza wakili

‘Anaweza kufanya hivyo, lakini sio kwa kugushi, sio kwa utapeli, na mimi nilishamuambia ukweli, kuwa huyu mtoto ni wangu, haina haja ya yeye kuhangaiia, nitaweza kumuhudumia mwenyewe, ….’akasema.

‘Lakini ni lazima mtoto awe na baba yake, na mtoto kama mtoto ana haki ya kuja kumfahamu baba yake, kwanini utake kuuficha huo ukweli, huoni hapo unatuficha mambo kwa kujikosha, ili uonekane wewe ni bora…?’ akaulizwa

‘Ni kweli kuwa mtoto ni lazima awe na baba yake, lakini kwa mazingira niliyompatia huyu mtoto sikutaka kuwe na mtu anayeitwa baba, ukumbuke kuwa hii mimba nimeipata kutoka kwa mume wa mtu, na katika maisha yangu niliipa kuwa sitatembea na mume wa mtu..

'Kuna uwongo ulipangwa kuwa mimi nilikuwa na mahusiano na huyu mwanaume kabla sio kweli...yaliyoyokuwa yakiendelea kati yangu na huyu mwanaume yalikuwa maswala mengine kabisa ya kazi nyingine...sio lazima kuyataja, hayahusiani na hii familia, mimi nina mambo yangu mengi ya kimaisha...lakini pia nilitumia muda huo kumlinda huyu mwanaume, hamjui tu alivyo...kuna mengi nimemuokoa nayo..

'Na pia hili lazima niliseme tu,...hadi mimi kufikia kutembea na mume wa mtu, sio kazi rahis kama inavyoonekana kwa wengi, mimi sipo hivyo jamani.., ilitokea baada ya hawa watu kunifanyia huo ubaya,...na baada ya tendo hilo, sikuwa nimejihakikishia kuwa kweli nina mimba, au mimba ni ya nani hasa,..mtasema kwanini sikuchukua hatua...nisingeliweza maana hata mimi nitaonekana tu nilipenda iwe hivyo,..

'Baada ya kugundua kuwa nina mimba,nikawa nimechanganyikiwa,nilianza kujiuliza ni ya nani, ni ya …unajua usiku ule sikuwa na ufahamu kabisa,..hata hivyo, niliomba mungu na kuvuta subira…

‘Unaona unaanza kujionyesha mwenyewe, unasema, hukujua ni nani aliyekupachka hiyo mimba, kwasababu gani, ulikuwa na wanaume wengi au sio…?’ akaulizwa

‘Hapana sio kuwa na maana hiyo, mimi sikuwahi kukutana na mwanaume mwingine kabla, na mimi sina tabia hiyo ya kihuni, ukiniona na wanaume ujue naongea tu nao tu, au nipo kazini..

‘Tutaaminije hilo, una ushahidi gani wa kulithibitisha hilo..?’ akaulizwa

‘Ushahidi upo…mimi huyu mtoto sikumpata tu kama unavyofikiria wewe,…’akasema

‘Utoe sasa huo ushahid wako, ulimpataje huyo mtoto, kama sio umalaya wako…’aliyesema sasa ni mume wa familia

‘Endelea na maelezo…’akasema mwenyekiti

**********

' Ndugu mwenyekiti, kuna jingine ambalo nataka kulisema hii leo, japokuwa wengi watanishangaa,...inabidi na lenyewe nilisema tu, kuwa ushauri wakati mwingine unaweza kukutumbukiza kubaya, sio kweli kuwa mimi nachukua ushauri tu bila kufikiria, hapana, lakini ushauri mwingine unategemea kama una manufaa,...'akasema

Alipoanza kusema hivyo nikajua sasa anataka kunilaumu mimi, lakin sikujali hilo, nikasubiria tu aongee apendavyo...

'Mimi nilikuja kupata ushauri kwa watu, ni kipindi ambacho, hata mimi nilikuwa kwenye wakati mgumu, unatamani na wewe uwe na mume, uwe na watoto, lakini hajapatikana, ufanyeje…unatamani upate mtu wa kukushauri ufanye nini ili ufanikiwe hilo…kiukweli umri umri wangu ulishakwenda…’akatulia

‘Naombeni mnielewe hapo, simlaumu mtu kwa hilo,..ila naongea ukweli, wa nafsi yangu, nilivyovutika hadi kuhamasika, na hata ilipotokea , sikupenda kujilaumu sana, na siwezi kusema nilivutika kufanya hivyo, kwa vile mimi sikufanya kiutashi wangu pia,…sasa ukiwa kwenye hiyo hali, na ghafla unakutana na ushauri, tena sio wa hivi hivi, wakitaalamu, kutoka kwa mtaalamu mwenyewe, utafanyaje, ..na zaidi unakuja kuupata ushaudri huo huo, kwa watu wako wa karibu unaowathamini,  kuwa ukichelewa hutaweza kuzaa tena, au ukizaa unaweza kuwa matatani..hivi kweli tuangalai kote kote, hali niliyokuwa nayo, ilinishinikiza kujiingiza kwenye …’hapo akatulia

‘Mimi ni binadamu, na siwezi kukwepa ukweli kuwa mimi ni mwanamke pia, sisi tulivyo tuna hulka zetu aaah, ndio, naweza kusema hivyo,… ‘akashika kichwa kama anawaza jambo

‘Ni hivi.., nataka muone jinsi hali hiyo ilivyojijenga akilini mwangu hadi kufikia huko, hata kujichanganya na wale ambao nilikuwa nakutana nao, lakini sikuweza kuwapatia ukaribu ule,…ni kweli, nilijikurubish kihivyo, hata hivyo dhamira yangu ilikuwa bado haijakubaliana na kutenda tendo hilo…sikupenda hivyo, sikutaka hivyo, nahasa kwa ..mmh nataka niliongee hili ili munielewe...'akasema huku anakatisha kumalizia..

‘Ndio sikudhamairia hilo…huyo mume wa familia, moyoni analifahamu hilo, hata mbele ya mungu atakuwa ni shahidi..hapa duniani anajidanganya tu..huyo ni kigoo jamani msimuone anatembea kichwa chini…’akasema

Wakili akacheka, na mume mtu akatikisa kichwa kusikitika…n watu wakacheka kidogo.

Kabla ya kuja kulielezea hilo, kuna jambo jingine nataka liwe wazi kwenu, kama mna vichwa vya kuomba mbali, mnaweza kuafikiana name, maana naona muda umekwenda, kuna mambo ambayo hatuyaoni kwa jinsi yalivyo,..kwa ukaribu wa akili zetu, lakini yapo, kwa wenye kuona mbali, sikuwa makini na hili, ila baadae nimakuja kuliona hilo..

‘Yawezekana ikawa ni bahati mbaya, au wanzetu wanasema ‘coincidence’  haya kutokea, au kuna mipango ya kitaalamu ilitengenezwa, hapa sisemi kuhusu kupata mtoto, nasema yawezekana  kashfa zilipangwa iwe hivyo, siwezi kuwalazimsiha kuliamini hivyo, maana ushahidi wake ni mgumu kupatikana, ila kwangu mimi nimeamini kuwa kuna namna hiyo ilipangwa, chochote chawezekana kwenye uwanja wa kisiada..’akatulia

‘Unajitetea, au unatoa ushahidi..?’ akauliza wakili

‘Nimeshakuambia, mwenyekiti akiruhusu ‘ushahidi’ hilo litafanyika, usitake kunipotezea muda, hapa…’akasema mdada

‘Endelea na maelezo yako..’akasema mwenyekiti

' Nasema hili hata baba, mwenyekiti wetu hapa ni shahidi, hili tukio zima limekuja kutumiwa kisiasa baadae, je lilijulikana kuwa litatokea, au ni hiyo ‘bahati’ kuwa limetokea sasa tutumie hiyo, kashfa kisiasa, hapo ndio pale tunamuhitajia, mume wa familia afunguke, auseme ukweli, atatusaidia sana kwa hilo…’akasema

Mume wa familia kusikia hivyo, kwanza alionyesha ishara ya ‘huyu anasema nini’ halafu akacheka

‘Kama nilivyosema wengine hatutaweza kuliona hili kwa uoni wetu wa kawaida,..haya kama yalipangwa au la, ila baadae haya sasa yamegeuzwa kisiasa kama kashfa, kwa jaili ya kuibomoa familia ya mzee, na sisis wahanga tunakuwa kwenye wakati mgumu hasa mimi ambaye nilikuwa mmoja wa watekelezaji na walinzi wa hizi familia, inaniuma sana,..’akasema

‘Hayo unayoyaelezea kuwa ni mbinu za kisiasa, ni kujitetea au umeyatoa wapi…?’ akaulizwa

‘Haya nimekuja kuyagundua, baada ya mimi kuingizwa huko, ili nitoe ushahidi kuwa haya yapo, nitaje kuwa nimezaa na nani, na kuahidiwa pesa nyingi, ikiwemo vitega uchumi, na hata kupewa hisa kwenye makampuni mbali mbali, …’akasema

‘Na akina nani…?’ akaulizwa

‘Na akina nani siwezi kuwataja,…lakini mimi sio kama walivyonifikiria wao, kuwa nipo hivyo..hawakupata kitu kutoka kwangu, na hawatapata kitu kutoka kwangu,..nimekana na kukataa mipango yao yote, hilo mniamini, na vitisho vyao kwangui haviwezi kufua dafu,..nimezoea vitisho…’akasema

'Sasa muone ajabu kwa huyo mnayemuita mume wa familia,…hata yeye aliitwa huko, je anaweza kulikiri hili, kuwa hata yeye aliitwa huko, na je aliweza kuitetea familia,je hakuweza kuukubali ukweli, maana haya yote yamejulikanaje huko, ..kiukweli mimi nililificha sana hili,lakini hutaamini huko wanafahamu mengi ya haya,..’akasema

‘Ni nani aliyetoa siri za upande huu na kuzipeleka huko,..yeye asema ukweli, kama hakutumiwa, na huenda alipoahidiwa manono akakubali kushirikiana nayo,…’akasema.

‘Uwongo, acha fitina, toa ushahidi wa jinsi ulivyobeba hiyo mimba, kumbe ulikuwa na mabwana wengi, eeh…ndio maana ulikuwa unaficha ukweli, sasa nimeshagundua.’akasema mume wa familia.

‘Kiukweli huyu mume wa familia alishatekwa huko…na asiposema ukweli, tunaweza kumuona ni msaliti wa hii familia, ndio maana nikasema hapa hapa tutaweza kulibaini hilo, ni nani msaliti wa hii familia,..na huenda hajijui hivyo, na huenda hajataka ila wanamtumia bila ya yeye kufahamu, atuambie basi, akiri ukweli, kama mimi hapa…’akasema

‘Mwongo wewe, kwanini unajenga fitina zisizo za ukweli, unataka nini , ili ndoa yangu ivunjike, ili wewe upate nini…’akasema mume wa familia

‘Kama hujakubaliana nao, na unafahamu fika ni maadui wa mkwe wako, uliwahi kuwaelezea lolote wakwe zako, au mkeo kuwa kuna maadui wa mzee  wanataka kukutumia wewe kwa masilahi yao..sema ukweli wako..je uliwahi hata mara moja kuwaonya wanafamilia wenzako, maana hili sio jambo dogoa..?’ akamuuliza mume wangu.

‘Nisingeliweza kukimbilia kuwaelezea hayo, mimi mwenyewe nilijua namna ya kupamabana nao, mimi ni mume wa familia nilijua ni namna gani ya kuilinda familia yangu, maana kama ningelichukulia pupa, je wangekuja kuifanyia ubaya familia yangu, ingelikuwaje,…wewe kwa vile ..huna familia, ok, ndo sasa umepaata mtoto jiulize mtu akitishia familia yako utafanya nini,…’akasema

‘Kwahiyo kumbe ulitishiwa ndio maana ukajiunga na hao watu, kisiri au sio..?’ akauliza mdada

‘Mimi sijasema nimejiunga na hao watu, kwanza hao watu akina nani, sikuelewei kabisa, mimi sio mwanasiasa,..na kuna watu ndio waliniuliza hayo kuwa eti nimzaa na wewe, na vitu kama hivyo, lakini sikuwa na majibu ya kuwaambia, na nilichofanya ni kwa masilahi ya familia yangu, siwezi kuyaonga hapa maana nafahamu athari zak kwenye familia yangu…’akasema mume wa familia, na wakili akawa anamzuia asiendelee kuongea.

‘Mimi nina ushahid mkubwa zaidi ya unavyofikiria wewe, natumai unanifahamu ninafanya kazi gani, kwahiyo siongei haya kwa nia ya kukufitinisha wewe na wakwe zako, hapa na ongea ukweli ulivyo, ukitaka ushahidi upo….’akasema halafu akawageukia wajumbe na kusema
‘Huyu mtu, nilishamuambia akitaka kupambana na mimi ajipange vyema, yeye kwangu kwa mambo hayo sio saizi yangu kabisa, hapa nina kila kitu, ushahidi na sheria bado inanilinda, maana mimi sivunji sheria, mimi sigushi, natafuta hakika na kweli, kama vielelezo viambata, huyu mtu atakuwa alitekwa na kuanza kutoa siri za familia hii, apinga kama nasema uwongo…’akasema

Mume wa familia akasimama na kusema;

'Wewe ni mwongo, mfitini mkubwa wewe..na kuambia, shauri lako, unafikiri kwa kusema hivyo, ndio watakuona ni mnzuri kwao, kuwa uniharibie mimi ili wewe wakuone ni mnzuri,.., kama umeharibu umeshaharibu tu..na ole wako, hao watu wakija kusikia unavyoongea hapa, unafikiri marehemu kafariki vipi, hao watu hawana simile wakiona kuwa wewe umewasaliti, hawasiti kukumaliza, au mtoto..'akasema

'Hahaha, unaogopa eeh, mimi ndio uwanja wangu huo, kifo kwangu kimeshaandikwa, mimi nipo vitani, ndio maisha yangu yalivyo, vitisho, ndio sehemu ya maisha yangu..lakini pamoja na hayo, niliapa kuwa sitakwenda kinyume na mkuu wangu wa kazi, hiyo ni ahadi hata kama hataniamini, yeye ndiye alinijenga hivyo, na yeye ndiye alinionyesha njia, haya yaliyotokea ni bahati mbaya tu...'akasema

‘Hahaha ‘bahati mbaya tu’…, wadanganye  hao hao, lakini sio mimi, namimi nina ushahid kuwa wewe una wapenzi wengi na mimi hatukuanza mapenzi..nini, acha niseme…’hapo akatulia, wakili akimzuia kuendelea kuongea

‘Ongea mbona unasita, sema, mimi na wewe tulianza lini, nilipokuwa naishi kwenu au sio……hahaha, ulikuwa unanitongoza, nikawa sikutaki, sema ukweli ili wakusikie huo ni ushahidi mwingine wa kauli yako hiyo, hiyo kauli yako japokuwa wakili wako kakuwahi ni ushahidi mwingine…’akasema

‘Wewe ni mnafiki tu wewe… mbona hutoi maelezo ya ushahidi kuwa huyo mtoto hukumpata kwasababu ya umalaya wako, eeh, jitetee sasa, unanitumia mimi kama ngazi ya kuficha maovu yako au sio…’akasema mume wa familia

 'Tutakuja kuliona hilo kuwa mimi na wewe ni nani Malaya au mnafiki, eeh,…’akasema rafiki yangu.

‘Endelea na maelezo yako, tusipoteze muda, mnajichelewesha wenyewe..’akasema mwenyekiti naona hata sauti yake, iliashiria hayupo sawa, nahisi kuna kitu kimegusa nafsini mwake.

********
‘Ndugu mwenyekiti, kwanini  huyu mtu hataka kusema ukweli wa hiyo mimba ilitungwaje ,  sio kwa tabia zake zisizisahihi, na akaja kumrubuni mteja wangu..?’ akauliza wakili, na mwenyekiti akamgeukia mzungumzaji..,

‘Nimeshasema kuwa huyu mtoto hadi kuzaliwa kulikuwa na michakato yake, kabla hata sijafikiria hivyo, kuwa natakiwa kuwa na mtoto, kuna watu walinishauri, kuwa nipate mtoto kwa kila hali..,hata ikibidi nitembee na mume wa mtu,..mimi sikuwa na tabia hiyo kabla, wengi wananifahamu hivyo.., lakini kauli hiyo ilikuwa moja ya sababu iliyonijenga kisaikolojia kuwa kumbe yawezekana eeh..’akasema

'Ni kweli, kiubinadamu labda nisingelitakiwa nifanye hivyo, maana huyo nitakaye tembea naye kama ni mume wa mtu, ana mkewe, je huyo mkewe atajisikiaje, je kama ningelikuwa mimi nimefanyiwa hivyo ningekubali,,..’akatulia kidogo

‘Kiukweli mimi sikupenda hilo litokee hivyo, nilitamani nipate mtoto kwa mtu asiyekuwa mume wa mtu, na ingelikuwa bora zaidi awe ni mume wangu, lakini kwa bahati mbaya sikujaliwa kumpata mume wa kunioa…

‘Sio kwamba sikuwahi kutakwa,  au mtu kunitaka kunioa, wapo sana na mmoja wapo ni huyo mume wa familia,lakini kuolewa na mtu asiyekuwa moyoni mwako ni jambo ambalo sikupenda kulikaribisha kwangu, huyu mume wa mtu, ni mume wa mtu nilijua fika hizo ni hadaa zake za kutaka kunitaka, nikamkataa, wapo wengi, siwezi kuwataja, niliwakataa kwasaabu hizo hizo.....'akasema

'Pamoja na ushauri huo kuwa nijitahidi kupata mtoto hata kwa mume wa mtu, lakini mimi sikuwa na dhamira ya kweli ya kutembea na mume wa mtu hususani mume wa rafiki yangu hilo halikuwepo kabisa akilini mwangu..huyu kwangu ni shemeji..’akasema

‘Shemeji eeh…’aliyesema hivyo ni mama, na watu wakacheka

‘Ni kweli mama,..nitawaelezea yote ili muweze kunielewa,..hili jambo lilitokea kwa mbinu za huyo mwanaume kama ni mkweli atalikubali hilo, sio mimi nilifanya juhudi hizo, ni yeye, sijui kama alishirikishwa  kulifanikisha hilo, au ni mbinu zake  za kufanikisha malengo yake, …ila hilo sio muhimu, ila yeye ndiye anabeba lawama hizo, ...'akasema

'Na sio kweli kuwa mimi nilimtaka yeye, kuwa eti mimi nilimuendea na kumwambia hivyo, kuwa nataka mtoto, na nimeshauriwa hivyo, hapana hiyo sio kweli kabisa, asema kutoka moyoni kuwa nilifika kabla na kumuambia hivyo, hayo ni maneno ya uzushi, tukio zima liligubikwa na mbinu zao, walizozipanga, yeye na ndugu zake, na huenda kama nilivyosema awali, alilifanikisha hilo kukidhi matakwa ya upande wa pili, kw kujua au kwa kutokuelewa, akatumiwa na ikaja kutokea hivyo…’akasema

'Kiukweli mimba yangu ilitokea katika mazingira ambayo sikutegemea kabisa,na mabaya zaidi ikaja kutokea kwa mume wa mtu, na mbaya zaidi kwa sehemu ambayo, najuta kiukweli,…imekuwa ni mtihani kwangu…baada ya kuipata hiyo mimba kiukweli nilikuwa na wakati mgumu sana…hata kujipa matumaini ilikuwa tu, ili nisije kupatwa na ugonjwa wa shinikizo la damu.

‘Kipindi hicho nilijaribu kujificha sana, na hata ilipokaribia siku nikatoweka kinamna lakini kwenye kujifungua ikabidi nije kujifungulia hapa Dar…na ndio ikaliweka hilo wazi kwa jamii… nahisi ni mwenyezimungu alitaka hili tukio libainike, kw avile halikufuata utaratibu ulio sahihi….’akatulia na kuhema

‘Hata hivyo mimi nilijipa matumaini kuwa, kwa vile haya yalitokea ni pamoja na ushauri wa watu, tena sio watu wa hivi hivi, ni watu ninaowaamini, washauri wangu, na wao walisema kwa kauli thabiti kuwa haijalishi, ..muhimu nipate mtoto, basi nimeshampata mtoto, wao kama ni wa kweli kwa ushauri wao wataendelea kunilinda na kunitetea kwa hilo.

'Sio rahisi, kama nilivyofikiria, ilifikia hatua nikajuta,…basi ndio imetokea hivyo sasa nitafanyaje, labda hli ndilo litathibitisha urafiki wetu kwa hao watu kuwa kweli walikuwa wakinijali mimi, au wakijali, yale ninayowafanyia, na walifanya hivyo kuniweka kwenye hali ya kuwaona kuwa wao ni marafiki zangu, naliongelea hili sio kwa kujitetea, maana hata hivyo mimi sikupenda litokee hivyo, huo ndio ukweli wa hilo, sikupenda kabia, mungu wangu ndiye shahidi nafahamu hapa hakuna atakayenielewa kwa hilo..'akasema

 Baada ya tukio hilo niliwapoteza marafiki zangu, nikawa sasa naonekana mimi ni mbaya,..kwanini, kwanini,  kwanza kwanini simtaji baba wa huyo mtoto,..kwanini namficha huyo mtoto, kwanini…basi ikawa ni taabu kwangu,.. urafiki sasa ukaja kugeuka kuwa ni uadui,…maana lisemwalo lipo halijajificha,..

‘Lakini jamani si nyie mlinishauri, kuwa nikishapata mtoto hiyo iwe siri yangu…na ikibidi, hata huyo baba yake asifahamu, hayo yote yakashindikana,..ni nani alifanya yasshindikane, ni mimi au ni nani, na hadi hapo alaumiwe nani, ..’akatulia

‘Najiuliza ni kwanini sasa nigeukwe, nahata kukamatishwa watoto w a kihuni, ili waje kunizalilisha, hili kiukweli limeniuma sana, lakini hata hivyo hao watoto wakihuni hawakufanikiwa,je ni kwanini hawakufanikiwa, jiulizeni kwa akili za kutafakari na kujifunza, ina maana kweli na mbinu zao, kwanini wakashindwa, maana walishaniziba pumzii na madawa ya kupoteza faamu iliyokuwa imebakia ni kutenda matendo yao maovu, lakini ..mungu akaniokoa, nasema mungu akaniokoa, si vinginevyo,…jiulizeni ni kwanini…kuna jambo la kujifunza hapo…’akasema.

‘Ila sasa najiuliza, kwanini, mumesahau urafiki wetu, mumesahau kuwa nyie ndio mlikuwa washauri wangu wa kubwa, je mliponishauri, hamkulifikiria hilo…sawa limekuwa ni kosa, lakini je hamtaki hata kunipa muda wa kutubu, …’akatulia akiwa anatikisa kichwa kama kusikitika

‘Ni sawa nastahiki adhabu, je mlimfikiriaje yule aliyefanya hili litokee, yeye mlianga adhabu gani kubwa kwake, ambayo nistahiki yake,… je mwafahamu ukweli halisi wa tukio zima hadi mimi kushika mimba hiyo, ilitokeaje, kiukweli, …hili lilitakiwa watu watulie kwanza, wajiulize kwanza, kabla ya kuhukumu,..kuna mambo mengi hapo, hata hilo la kisiasa laweza kuwa ni sababu, litizameni kwa macho mapana..’akatulia

'Kwa bahati mbaya, mungu wngu alitaka nisipate hiyo adhabu kabla ukweli haujabanika, maana kama kweli wangelifanikiwa hao watu, sizani kama ningelikuwa na ubavu wa kuja kusimama hapa hii leo..ila nina amini, hata wao wasingeliweza kuishi…haaah,..hawanijui tu, ingeliwa jino kwa jino, kabla sijafanya walichowahi kufanya wengine…’akasema

‘Siwezi kujiaminisha hivyo, maana kihabari ninayoifahamu kuhusu hao watu wao wakafanikiwa kwako, huwezi kuishi, utatamani ujiue tu, ila mimi nisingejiua kabla hawajauwawa wao kwanza, …akatulia

‘Ila mimi hapo najiuliza kama lengo hilo ni kunifundisha mimi adabu, je ingelitokea kuwa mimi nimepata hii mimba na mume mwingine adhabu hiyo ingelikuwepo pia, au ni mkuki kwa nguruwe tu…najiuliza tu hapo..’akasema

‘Ninachoshukuru ni kuwa wahuni hao hawakufanikiwa, walishindwa kufanya hivyo, baada ya mbinu zao kugundulikana na polisi, vijana hawo sasa wapo jela, na nitahakikisha wanaozea huko jela, na humo wanakipata cha moto, humo nina watu wangu wanaifanya hiyo kazi, waonje uchungu wa kile walichokuwa wakiwafanyia wengine,..na nina uhakika, wakitoka jela, sizani kama watatamani kuishi hapa Dar tena, sasa mkuki umewageukia wao...'akasema

'Nyie mliowatuma mkawatoe kabla haja-ozea huko jela, maana kumbe walikuwa wakitafutwa kwa ushahidi, sasa ushahidi umepatikana,  nyie sasa...mnahitajika kuwadhamini, kiutu,..lakini kwangu mimi, wataiona hii dunia ni chungu..wamechezea kusipochezewa..’akatulia

‘Sio vyema jamani, ni kweli inauma…ni kweli kilichofanyika ilikuwa sio sahihi.., lakini hata mimi sikupenda hili litokee hivi jamani…hata hivyo, hivi sasa mimi nimekuwa, nakushukuru sana rafiki yangu uliyejitolea kwa ajili yangu hadi hatua hii, ni wewe uliyenijenga hivi, na sasa nipo zaidi ya vile ulivyonijenga, ninaweza kuishi mwenyewe, bila huo utapeli wao…’akasema

‘Kiukweli mimi sihitajii kujiingiza kwenye utapeli huo ulitakiwa kwangu mimi, lakhasha, nipo kivyangu na namuomba mungu niweze kuishi hivyo, kwenye maisha yangu ya haki, na sio dhuluma,  nafahamu fika rafiki , nimekukosea sana, ila wewe ndani ya moyo wako, unanifahamu nilivyo, haya yaliyotokea ni mtihani tu, ni mbinu, na mungu mwenyewe ndiye anajua...’akasema.

‘Ni nani huyo aliyekushauri, maana naona unajitetea hivyo..kusingizia uovu wako..kwa watu wengine?’ akaulizwa

‘Hahaha, mimi sisemi kwa kujitetea, nasema ukweli wa nafsi yangu, kuwa wapo walionishauri hivyo,, kuwa nikazae kwa vile umri wangu umeshapita, hata kama huyo nitakayetembea naye…ni..ni… ,sina haja ya kumtaja huyo mtu, ni utomvu wa adabu, na mim sikulelewa hivyo,..’akasema

‘Kwanini humtaji, mbona mume wa familia, hujajali, umekuwa mwepesi kumnyoshea kidole kwa kila kitu, mabaya yote umeyaelekeza kwake,.. yeye hakuwahi kukutendea wema, wewe uliwahi kuishi kwenye nyumba yao, yeye ni mume wa familia, alikulea, leo hii umesahau fadhila zake…’akaambiwa

‘Tatizo ni kuwa mume wa familia hakubali kosa, kama yeye angelikubali kosa,haya mengine yasingelijulikana, mbona mimi nimekuali makosa yangu nimeelezeakilakitu,..’akasema

‘Lakini pia yeye kama shemeji, mlezi wangu alitakiwa kunilea katika maadili mema, lakini yeye alitumia mwanya huo kunirubuni, kunishawishi, kutumia kila mbinu za kuniingiza kwenye ushawsihi huo mbaya, je huyu anastahiki kuheshimiwa,..niambieni, ukweli, ….’akasema

‘Sasa hata baada ya hayo, kwanini hakubali kusema ukweli,.. je yeye hajakosea, kwanini hakubali sasa..kwa vile yeye ni mume wa familia, kijogoo, au sio,.., sasa hivi mimi nina ushahid hapa wa mazungumzo yake mimi na yeye , kwenye maongei hayo kajieleza alivyo, nilimchota akaongea kila kitu ..naona..eeh, sasa ni wakati wake muafaka auseme ukweli, akiri makosa yake la sivyo, ushahidi huo ufanye kazi yake…’akasema..

‘Hapana, hatuendi hivyo, …’akasema wakili

‘Kwanini, hatuendi hivyo… nyie si mnajiona hamjakosa..mpo sahihi, ngoja wayasikie yale tuliyoyaongea ili kikao hiki kibaini je ni mimi nilimshawishi hadi akanipa mimba au ni mipango yake, huenda hata hiyo mipango, ilipangwa kisiasa na mume wangu akashawishiwa kuikamilisha, kama ni hivyo basi alibainishe hilo, lakini kwa ushahidi sio kwa kujikosha,..’akasema

Mume wa familia akawa kimia…

‘Je mume wa famalia, upo radhi wayasikie au utakubali makosa yako ili kuwasaidia hawa watu, kuwa wewe kweli ndivyo ulivyo, na nia yako mbaya kwao, ili na wao wapate muda wa kukufikiria, au kama hutaki, basi, waniruhusu wasikie japokuwa kidogo, kauli zako, dhidi yao, nafahamu wakisikia hayo, watakufahamu ulivyo…’akatulia

‘Nasema na wewe… au unaogopa kwa vile wakisikia uliyoyaongea kamwe hawatakusamehe..’akasema.

‘Mwongo wewe..hizo ni mbinu zako  tu….’akasema

‘Mimi mwongo, eeh,..Je niweke hayo mazungumzo bayana, watu wayasikie…?’ akageuka kumuangalia wakili wake, na wakati huo mume wa familia alikuwa akitaka kuongea jambo lakini akaghairi, na baadae akainamisha kichwa chini

‘Ndugu mwenyekiti, mimi nataka nimalize hii kazi, ili isiwe ni kazi sana kwenu, msipoteze muda wenu bure, wakati ukweli upo bayana, na mimi nashukuru mungu kwa ujuzi nilio nao, niliufanyia kazi, nilijiahidi kukusanya yote…akashika mkoba wake.

Hapa nimekamilika, na sio hapa tu,maana wengine wanaweza kufany ambinu za kuninyang’anya huu ushahidi , ushahidi huu upo sehemu nyeti, na muda wote ukihitajika, unapatikana, …tunaenda kidigitali…

‘Sasa kama mimi nimetangulia kuyasema madhambi yangu, wengine nao wafuate, aje mume wa familia akiri madhambi yake ili aokoe yale ambayo bado sijaanza kuyasema, ninao mengi, hasa sehemu ya pili, hapa ndio kwanza naanza…’akasema

Mwenyekiti akageuka kumuangalia mkewe, kuna kitu mkewe alitaka kumuelezea, wawili hao wakawa wanateta kidogo, halafu mwenyekiti akainua kichwa kuniangalia mimi, kama anataka mimi nisema jambo.

Kiukweli mimi pale nilikuwa nimeshahama kimawazo, kuna muda nilianza kujilaumu, kuna muda nilikuwa na hasira za kutaka kufanya ubaya, kuna muda...niliona sina la kufanya,, lakini hasira chuki, vilikuwa vinikinisakama kooni...pale pale nikawatupia macho watoto wale wawili

Nilimuangalia mtoto wa yule binti, alikuwa anafanana kwa kila kitu na mtoto wa rafiki yangu,...nikajiuliza hao watoto wana hatia gani, kwanini haya yametokea kwenye familia yangu...

'Upo na sisi mke wa familia,...?' nilishituka nikiulizwa na mwenyekiti, sikuelewa niliulizwa swali gani awali, nikajikuta nikisema

'Nipo mwenyekiti, tupo pamoja,...'nikasema

Mara wakili wa mume wangu akanyosha mkono, na ikaonekana kama vile mume wa familia anamzuia,....

‘Mnataka kusema nini…?’ akauliza mwenyekiti akimuangalia wakili huyo, na huku simu yake ikiingia ujumbe akawa anausoma huo ujumbe, na baadae akainu uso kumuangalia huyo wakili. Uso sasa ulikuwa umekunjamana, ina maana ujumbe huo , aliousoma mwenyekiti ulikuwa na jambo nzito...


WAZO LA LEO: Tunapopewa dhamana ya kuhukum, tuhukumu kwa uadilifu, na tunapopewa dhamana ya utetezi, tutetee kwa wema ili haki ukweli uwe bayana, na tunapotoa ushahidi tuwe na uhakika na ushahidi wetu, kwani hapo tunacheza na maisha ya mtu, tunawakilisha sehemu ya haki na ukweli , ukipindisha ukweli na haki ikaenda kusipostahiki, utabeba hiyo dhamana na mzigo huo utakufa nao.
Ni mimi: emu-three

No comments :