Usiku huo kwangu ulikuwa wa
historia,
Niliendelea kufuatana naye, nikawa sasa nachoka, lakini
nitafanyaje, na ikafika sehemu sasa nikahisi anarudi nyumbani, nilipoona hivyo,
nikajiuliza, haya akirudi nyumbani itakuwaje, mume sasa naanza kumuogopa!.
‘Haya tisa, usiku nitalalaje naye, akiamua kuniua, au kuleta fujo….?’
Nikajiuliza na muda huo bado nipo nyuma yake kila anapokwenda nipo naye. Kwa
haraka wazo likanijia, ..nikampigia simu mdogo, huyu ndiye wanawezana.
‘Shemeji kuna tatizo gani?’ akaniuliza, alipopokea simu yangu
‘Nakuomba uje nyumbani, ni muhimu sana ...’nikasema
‘Kuna nini tena shemeji…unajua mimi bado nipo kazini, ?’ akauliza
kwa mashaka, yeye kazi zake wakati mwingine anafanya hadi usiku
‘Kuna kitu nataka unisaidie kuhusu kaka yako,....’nikasema,
sikutaka kumwambia ni nini kinaendelea kwa wakati ule, lakini nilifahamu
nikimwambia kuwa ni mambo ya kaka yake, atakuja haraka.
‘Sawa nakuja shemji, lakini haumwi sana?’ akauliza
‘Haumwi sana.., ni jambo dogo tu nitakuambia ukifika nyumani
kwangu, lakini kwa hivi sasa sipo nyumbani, nitakuarifu nikifika…’nikasema na
kukata simu, sikutaka kumpa maelezo mengi
Nikaendelea kumfuatilia
mume wangu, badala ya kueleka nyumbani sasa anaelekea njia ya kwenda ofisini
kwangu,…alipofika getini kuingia kwenye jengo la ofisini yangu akasimamisha
gari, akapiga honi, na mlinzi akatoka, na nikasikia akimuuliza;
‘Mke wangu yupo ofisini kwake?’ akauliza
‘Hapana, sio muda wa kazi sa hizi…’akasema mlinzi
Wakati huo nilikuwa nimeshasimamisha gari langu, na hatua chache
nyuma ya gari lake, na kwa vile mlinzi anaongea akiwa ndani kwa kupitia
kidorisha, hakuweza kuona pale nilipokuwa nimesimamisha gari langu. Pale
nikaona nikatoke ndani ya gari langi, ili niweze kusikia ni nini
wanachokiongea,
Kwa haraka nikatoka kwenye gari langu na kusogea karibu kidogo na
wao,sehemu ambayo hawo wawili hawawezi kuniona, nikawa nawasikiliza, nilisikia
na maswali hayo ya kutaka kujua kuwa mimi nipo ofisi, akauliza ni kwanini sipo
ofisini na yeye anajua kuwa mimi nipo ofisini
Mlinzi alimjibu vyema tu, japokuwa ilikuwa na maswali ya
kushangaza, hapo nikaona nitumie mbinu, nikachukua simu yangu na kutuma ujumbe
kwa yule mlinzi.
‘Mwambie mimi nipo nyumbani namsubiria, je yupo wapi...’nikatuma ujumbe
huo wa maneno kwa yule mlinzi, ambaye kwa vile gari la mume wangu limemzuia,
hakuweza kuliona gari langu, akasikia sauti ya ujumbe kwenye simu yake, akawa
anausoma, halafu akamwambia mume wangu.
‘Mbona mke wako anasema yupo nyumbani anasema anakusubiri,
anauliza wewe upo wapi...’akamwambia
‘Hapana mimi nina uhakika yupo ofisini kwake, nina uhakika huo,
..nataka kwenda kuonana naye fungua geti, unanifahamu mimi ni nani au sio...’akasema
‘Hapa ofisini kwasasa hayupo bosi, na haturuhusiwi kumfungulia mtu
yoyote zaidi yake, saa kazi zimepita na
mke wako aliondoka mapema tu, hakuna mtu ndani, zaidi ya sisi walinzi huku nje...’yule
mlinzi akasema
‘Mh, oh, ina maana muda wa kazi umekwisha, sio hamnijali mimi, ok,
sawa,..oh, samahani, kwa usumbufu ....’akasema na kulirudisha gari lake
nyuma na kuligeuza, nikajua kwasasa atakuwa akielekea nyumbani.
*******
Nilimfuatilia hadi tukafika nyumbani
Tulipofika nyumbani, nikaliona gari la mdogo wake limeshafika,
mjamaa, kwa akateremka kwenye gari, hakuangalia pembeni, kwa haraka haraka
akakimbilia ndani, wala hakuangalia pembeni,
Mimi nikateremka na kukagua gari lake kama kila kitu kipo sawa,
mlango kafunga, na nilipohakikisha kama kila kitu kipo sawa, nikaingia kwenye
hilo gari, na kulisogeza sehemu salama, na mimi nikaingia kwenye gari langu na
kuliingiza sehemu maalumu ya magari, halafu, kwa haraka nikakimbilia ndani.
Nilipofika ndani nilimuona mdogo wake, akiwa kakaa kwenye sofa,
lakini mume wangu hakuwepo, nikamuuliza
‘Umemuona kaka yako akiingia?’ nikamuuliza
‘Ndio kaingia, lakini hakunisemesha, alionekana kama hanioni,
kanipita kwa haraka akakimbilia chumbani kwenu, kwani kuna nini shemeji, maana
hata machoni, sio w wa kawaida?’ akaniuliza
‘Nitakuambia, ila muhimu nataka ulale hapa leo, kesho inabidi
tumpeleke kaka yako hospitalini, kaka yako anaonekana kuchanganyikiwa
kidogo....’nikasema.
‘Ina maana hiyo hali imejitokeza?’ akauliza, na mimi nikamuangalia
kwa mshangao na kumuuliza;
‘Ina maana ulikuwa unafahamu kuwa kaka yako ana hali kama hiyo ya kuchanganyikiwa,
kwanini unasema hiyo hali imejitokeza?’ nikamuuliza
‘Ndio nafahamu… kipindi kile akiwa kule hospitali kwenye uchunguzi
walisema hivyo, lakini jinsi alivyokuwa na maendeleo mazuri wakati anaruhusiwa,
tuliona kuwa haitaweza kutokea tatizo kama hilo, hata docta, rafiki yake,
alisema huenda hiyo hali haitajitokeza tena, baada ya yeye kumfuatilia kwa
muda.....’akasema
‘Sasa ndio hivyo imejitokeza, na kwa hali kama hiyo, kunahitajika
mtu wa kuwa naye karibu wakati wote, naogopa usiku nisije nikashindwa,
nikapitiwa na usingizi, ndio maana nikakuita. Sasa hivi cha kumsaidia hapa ni
dawa, nahisi ndio maana walikuwa kuna madawa yale ya usingizi,..’nikasema
‘Ndio, sib ado zipo..?’ akauliza
‘Zipo tele tu, hazitumii siku hizi..’nikasema
‘Tunaweza kumpa au sio…’akasema
‘Sawa tutampa,ila wewe inabidi ulale hapa, sasa kama kuna lolote la
kufuatilia huko kazini kwako nenda kalimalize urudi haraka , au wapigie simu,
...kuwa kuna dharura, hutarudi tena huko...’nikasema
‘Hakuna shinda shemeji mimi nimesha waaga kabisa,...’akasema na
mara mume wangu akatoka na kuniangalia alionekana kama kunishangaa,
halafu akasema;
‘Mke wangu, sijui kuna nini kinaendelea kwenye kichwa changu...hivi
nipo sawa kweli…’akasema akishika kichwa chake.
‘Kwani unajisikiaje?’ nikamuuliza
‘Hivi nikuulize ni lini tulikuwa tunaongea kuhusu mtoto,
ukaniuliza kuwa labda mimi nina mtoto nje, tena mtoto mwenyewe wa kiume?’
akaniuliza akiniangalia kwa macho ya kujiuliza. Kidogo, macho yanaanza kurejea
kwenye uhai, lakini…
‘Mchana, au…jioni hivi,…tuliongea ndio, kwani vipi?’ nikamuuliza
‘Nimekwenda kumfuatilia huyo mtoto, hayupo,... hayupo kabisa
…nahisi kuna tatizo, unajua hata huyo mama anayekaa na huyo mtoto
hayupo.....nahisi watakuwa wameamua kutukimbia na mtoto wetu, huenda wameamua
kunisaliti, una uhakika, kuwa nina mtoto ....tuna mtoto wa kiume, una uhakika?’
akawa ananiuliza
‘Hamna kitu kama hicho mume wangu, nilikuwa nakutania tu, nilikuwa
nakuuliza kama kukupima akili yako, kwani vipi tena ...’nikasema
‘Huo sio utani mke wangu, nikweli nina..tuna mtoto...ni lazima
tumchukue mtoto wetu, Yule mama eeh, hawezi kumlea kabisa…eti siku moja anadai kuwa
mtoto ni wake na mimi hanitambui…wewe, hahaha, eti yeye ni mama yake na mimi
sina haki naye,..’akasema
‘Mama yake!! Kwani mama yake ni nani…?’ nikamuuliza bila kujali
kuwa namuongezea mawazo
‘Mama yake, eeh!!!,…mama yake si wewe, tatizo wewe
umechanganyikiwa, sijui kwanini, hivi kwanini ulitaka kumtupa mtoto wetu…niambie
ni kwanini, sasa mimi namtaka mtoto wangu , leo hii hii…hili sio jambo la
mdhaha, mimi namtaka mtoto wangu haraka…’akasema kwa hasira sasa.
‘Sikiliza mume wangu tutamtafuta huyo mtoto kesho, unasikia, kesho
tutakwenda mimi na wewe hadi kwa huyo mama yake unasikia, usiwe na wasiwasi…’nikasema
Kidogo akatulia, na akatizama saa yake mkononi, halafu akasema;
‘Tatizo ni huyo Makabrasha nilimpa
kazi sasa sijui imekuwaje, unajua nimefika hadi ofisin kwake, ili aweze kulifuatilia
hili jambo kisheria, yaani hiyo ndio njia sahihi, kwenye sheria, na mikataba
ikiwepo, mtu hawezi kuvuka kihunzi, sheria itambana,…kiukweli mimi siwezi
kuacha damu yangu ipotee hivi hivi, halafu mtoto mwenyewe ni wa kiume,…’akasema
na mimi hapo nikawa kimia
‘Mke wangu, si wewe ulikuwa unataka mtoto wa kiume, ni wewe au ni
mimi, …haah, ndio, sote tulikuwa tunataka mtoto wa kiume si ndio hivyo…?’
akauliza
‘Ndi-ndio hivyo…, mungu lakini hatuja-jalia kumpata mtoto wa
kiume.., tutampata tu, mungu akipenda…’nikasema
‘Keshatujalia bwana, wewe vipi, si ndio huyo, huyo mwanamke ni
mwizi tu…kamchukua, nikuulize kwanini ulikuwa unataka kumtupa, mtoto wetu…eeh..?’
akanigeukia tena kwa hasira.
‘Si nimekuambia mume wangu kesho tutamfuata sijamtupa..’nikasema
‘Yah…kesho,..maana yule ni mwizi tu, unasiki,a huyo ni mtoto wetu,
…sasa tuyaache hayo, wakili atalishughulikia hilo, Yule wakili hana mchezo,
yaani vyovyote utakavyo, anakufanyia, ni mjanja kweli kweli, sasa mke wangu, ni
kuhusu ule mkataba wetu, eeh, si unaujua
eeh…’akasema
‘Ndio ule wa zamani…’nikasema
‘Kwani kuna wa zamani na wa sasa…mke wngu umechanganyikiwa nini…ngoja
nityampigia wakili aje, tumalizane, nataka tulimalize leo hii , hii, sitaki cha
zamani na sasa, mkataba ni mmoja, au sio mke wangu..?’ akaniuliza na mimi hapo
nikamuuliza
‘Huyo wakili ni nani ..?’ nikamuuliza
‘Si Makabrasha, na wewe bwana umeshamsahau tena, ndio huyo huyo,
sasa hivi nimetoka ofisini kwake, yeye hayupo, walinzi wake wababaishaji, eti
wanadai, kafariki, hawa watu bwana, kama hawampendi mtu watamzushia uwongo tu ,
hivi kuna mtu anaweza kumzulia mwingine kifo, ngoja nitamuambia, na Yule
atafukuzwa kazi, wewe subiria tu…’akasema
‘Basi usijali mume wangu…hilo tutalifuatilia hiyo kesho usiwe na
wasiwasi kabisa…’nikasema
‘Sawa kabisa mke wangu, mtoto yule ni wa kwetu, kwahiyo tuna
watoto hawa....’akasema akionyesha vidole vitatu.
‘Hapana mume wangu sisi tuna watoto wawili,....’nikajikuta
nimesema hivyo
‘Usinibishie mimi, ...., mimi ndio najua, mimi ndio mume
wako,...tuna watoto hawa…w-nne, ...na ...’akasema
‘Wanne tena…’nikasema, na kabla hajanijibu, ndugu yake akakohoa,
sijui ni makusudi au ilitokea tu, na hapo hapo akageuka ndio akamuona mdogo
wake, kwanza alimuangalia kama anamshangaa, baadae, akatabasamu na kwa haraka
akamsogelea, kama vile anataka kumkumbatia, lakini mdogo wake akanyosha mkono
wakashikana kusalimiana.
‘Jembe,…hahaha! Jembe langu umekuja, sasa mambo safi, utanisaidia
kazi moja..kuna kazi moja usiku huu huu…unazijua zile zetu, kwanza sina pesa,
lazima tufanye dili la nguvu, pili, kuna yale mambo yetu,..mmh,…, hiyo ni siri
yetu,..unasikia, sitaki mke wangu afahamu,...unasikia jembe....’akasema
na hayo maneno kuwa hataki mimi nifahamu akawa kama anamnong’oneza, .
Mdogo wake akawa anamwangalia kaka yake kwa mashaka.Nilimuonyeshea
ishara akubali tu, na mdogo wake, akamsogelea kaka yake na wakawa kama
wanakumbatiana, nilimuona mdogo wake akijizuia kutoa machozi. Nahisi kuna hisia
za kulia zilitaka kumjia, anampenda kaka yake pamoja na wakati mwingine
hawaelewani.
Niligeuka na kuangalia pembeni, maana kwa hali kama ile hata mimi mwenyewe
hiyo hali ilinijia, nikiwazia mbali, kuwa huenda mume wangu ndio hivyo
kaharibikiwa hatapona tena, karibu hata mimi nilitaka kutoa machozi,..kiukweli
mimi nilishajua kuwa mume wangu keshapona, na tunatakiwa kuganga yajayo.
‘Sasa hili tatizo litaisha lini..?’ nikajikuta nimejiuliza hivi
tena kwa sauti, na sijui kama walinisikia, kumbe kweli walinisikia kwani mume
wangu akasema;
‘Kesho…unasikia mke wangu, kesho, litaisha,..’akasema mume wangu
hivyo, sijui alikuwa na maana gani, na muda huo alikuwa bado kamuangalia ndugu
yake, wanaongea
Na ndugu yake akaingilia kati na kumuongelesha kitu kingine muda
huo huo, kwahiyo wakawa wanaongea sasa wao wawili , na mimi nikaa kimia…kama
vile mimi sipo, na kuna wakati anamuambia mdogo wake kuwa hayo ni ya siri hata
mke wangu hatakiwi kujua, keshasahau kuwa na mimi nipo hapo karibu.
‘Sasa hili ni tatizo…’nikajisema kimoyo moyo sasa.
Kwa muda huo nikamkumbuka docta rafiki wa mume wangu, nilitamani
nimpigie mambo kama hayo angenishauri vizuri tu, lakini kwa hapo nisingeliweza
kufanya lolote
Aliendelea kuongea na mdogo wake mambo mengi tu, na kama kweli
hayo anayoyaelezea kayafanya basi mume wangu yupo kwenye mambo ya hatari ambayo
yatamweka pabaya.
‘Mdogo wangu, tuna mtoto wa kiume, nilikuambia, ukanibishia ni
kweli sio ndoto, sasa nimeamini…’akasema na mdogo wake akawa anaitikia tu
‘Tatizo ni hawa wanawake hawaeleweki kabisa, mambo mengine ya siri
wanaharibu, sasa kaharibu…na mke wangu akijua mmh..lakini usijali nitayamaliza
tu…si unanifahamu, ..we acha tu..’akasema na mdogo wake akawa ananiangalia
mimi, hapo akaharibu, kwani mume wangu akageuka kuangalia nyuma, ndio
akaniona...
Aliponiona akawa kama kashtuka, halafu akasema
‘Oh kumbe upo, umekuja saa ngapi…oh, nilikuwa nongea na bwana
mdogoo, siunajua tena, huyu ndiye mtu wangu kabisa..lakini mke wangu kama
tulivyoongea, eeh, usiniangushe, Yule ni mtoto wetu kabisa, ukimuona
utaniambia…wanafanana na watoto wetu kabisa,…’akasema.
‘Sawa, sawa nimekuelewa, sasa unywe dawa ukalale…’nikasema
‘Mimi nilale saa hizi, ...hapana bado naongea na bwana
mdogo…’akasema
‘Unatakiwa kunywa dawa zako kwanza huu ndio muda wake..’nikasema
nikijua akizinywa hizo dawa, atazidiwa, ataishia kulala tu
‘Dawa kwani mimi naumwa bwana, usiharibu mada,…’akasema na
kumgeukia mdogo wake
‘Unaona ndio mambo siyataki haya, hawa akina mama…mmh, unajua
bwana mdogo nikuambie kitu, hapa
nikutoka tu, sisi tutoke hapa twende sehemu, tukafanye mambo yetu,
halafu kitaeleweka, au sio..mimi hapa sina pesa, tutapata wapi pesa..dili
kwanza..au sio?’ akasema sasa akiwa kanisahau kidogo, akasimama na kumshika
mdogo wake mkono ili waondoke.
‘Sasa mke wangu nataka
kutoka na mdogo wangu, tutaonana baadaye...’akasema na mdogo wake akawa anasita
kuondoka, na wakati huo kashikwa mkono ili watoke naye
‘Kaka hebu kunywa dawa kwanza ni muhimu, si unajua afya ni bora
kuliko mambo mengine, mimi nipo, tutatoka tu..’akasema mdogo wake
‘Usimsikilize shemeji yako,..twende bwana, amri, kaka akiongea
jambo ni amri,..twende, halafu.., tutarudi, kwani dawa zitaharibika…’sasa akawa
anamvuta mdogo wake waondoke.
‘Mke wangu usijali, mimi nitarudi, sifanyi fujo, mwenyewe utaona,
hapa,..nikiwa na hili jembe, sina wasiwasi, huyu ndiye mimi, ukimuona huyu
umeniona mimi, hata nikifa leo, usije ukamtupa mdogo wangu huyu,
unasikia…’akawa anaongea sasa kama kalewa.
‘Mume wangu…mbona haupo sawa…’nikasema
‘Nani kasema sipo sawa, halafu wewe mjanja kweli kweli,…hahaha,
umejuaje,…nilipoingia ndani, kuondoa mawazo, nilikunywa kidogo tu…kidogo…,
hahaha, hamuwezi kininyima starehe yangu, hahaha’ akacheka sana tu
‘Sasa sikiliza, huyu ni jembe langu,,....usije ukamnyanyasa mdogo
wangu, hata kama nimekufa, mimi nitafufuka na kuja kumtetea, nampenda sana
mdogo wangu huyu, achana na Yule mwingine, Yule … Yule anajifanya mtakatifu
saana,.....hili ndilo jembe langu...’akasema na kumshika mdogo wake mkono,
wakatoka naye nje…
Nilibakia mle ndani nikiwa sijui nifanye nini, …lakini kwa vile
sasa yupo na mdogo wake, nilihisi amani kidogo,…
‘Ngoja sasa nione kitakachofuata,..hili ni langu tena..’nikasema
Na hata kabla sijasimama,
ili nielekee chumbani, mara simu yangu ikaita, moyo phaaa! Mlio wa simu sasa
unanipa kero, naogopa na kuogopa…
Nikaangalia mpigaji,.. ilikuwa ni namba ya nje, kidogo nikatulia,
nikijua huyo atakuwa ni yule rafiki
yangu anayesoma nje….
**********
‘Habari za huko?’ nikauliza
‘Nzuri tu, bosi, tumemaliza mitihani mmoja kesho tunafanya
mwingine, na huenda nikaja huko siku za karibuni...’akasema
‘Itakuwa vizuri sana, maana kuna mambo nataka
tuyamalize...’nikasema
‘Yale yale..au?’ akauliza
‘Ndio,..yale yale, na hapa tunapozungumza mume wangu anaonekana
hayupo sawa..kachanganyikiwa…’nikasema
‘Mhh, hiyo hali imeshajitokeza tena ehe..?’ akawa kama anauliza
‘Ina maana unafahamu?’ nikamuuliza
‘Ndio, nilipofika kwa docta wake, moja ya jambo alilonielezea ni
hilo, nilijua na wewe unafahamu..’akasema
‘Hapana…’nikasema
‘Basi ni hivyo uwe makini naye sana…na bora umueleze docta yake
achukue hatua anaweza kufanya jambo baya...’akasema
‘Kwanini docta alikuambia wewe na hayo ni mambo ya siri ya mgonjwa
au mke wake ?’ nikauliza
‘Umesahau kuwa mimi ni ndugu yako wa karibu na hakuniambia kwa nia
mbaya, ...’akasema
‘Ni ndugu yangu wa karibu,ehe, ...kweli wewe ni ndugu yangu wa
karibu, kama ungelikuwa ni ndugu yangu wa karibu ungelinifanyia hayo
uliyonifanyia…’nikasema kwa hasira
‘Yapi tena bosi, mbona kila siku unakuja na hoja mpya, ...?’
akauliza.
‘Unayafahamu sana.....’nikasema.
‘Bosi nakuomba bosi, usichukulie hayo mambo kwa hasira, nikirudi
tutaongea, nina imani hakitaharibika kitu..’akasema
‘Kama ni kweli, ninavyosikia, kama ni kweli, wewe umezaa na mume
wangu...sizani kama tutakaa kwenye meza moja tuongee, hilo sahau, na
nilishakuambia, kama kuna mtu anataka ubaya na mimi ...basi atembee na mume
wangu, sitajali kama ni nani, hata kama ni ndugu yangu wa tumbo moja, nitafanya
yale yale niliyowahi kukuambia...’nikasema.
‘Lakini...’akaanza kujitetea.
‘Sasa hivi mume wangu anaumwa, na hali aliyo nayo siwezi kufanya
lolote, lakini akipona tu,...kama ni kweli, basi, ...mkataba utafanya kazi
yake, na mengine yatafuta baadaye....’nikasema.
‘Mkataba upi bosi ...maana kama nilivyoona, na kuambiwa, kwenye
mkataba hakuna tatizo, ...mume wako ana uhuru wa kufanya lolote, huoni kwamba
ukitumia huo mkataba utakuwa umejimaliza wewe mwenyewe..’akasema
‘Kumbe hata hayo ya mkataba unayafahamu au sio…naanza kupata
picha, sasa kama ndivyo mlivyopanga hivyo, tutapambana mahakamani…si ndio
ujanja wenu huo, kuwa mumegushi mkataba ili mtoto wake aje kurithi mali yangu,
au sio?’ nikauliza
‘Mimi sijapanga lolote, mimi niliitwa kuja huko kwa dharura, na
nilipofika hapo, nikajikuta naingizwa kwenye mambo ambayo hata siyafahamu, na
kuhusu mtoto, mtoto ni wangu, hana baba,..hayo ni yao, na ndoto zao, wala usiwe
na wasiwasi na mtoto wangu…’akasema
‘Kwahiyo wewe kilichokurudisha huku, ilikuwa nini hasa…?’
nikauliza
‘Mimi sikurudi kwasababu hiyo, nilirudi kwasababu niliambiwa
kibali change kina matatizo, kwahiyo nahitajika kurudi kukirekebisha, kwanza
nilijua ni wewe umefanya hivyo, ili kuondoa udhamini wako, nikaona isiwe shida,
na bahati nziri akapatikana mdhamini mwingine,…sasa sijui kama ni wewe ulifanya
hivyo, au kuna jingine ndani yake, mimi sikutaka kulichunguza muhimu nimalize
haya masomo mengine nitakuja kuyafahamu baadae…’akasema
‘Usinidanganye kila kitu nimeshakifahamu, na kwanini hukuniuliza,
kuhakikisha hilo, na kwanini nifanye hivyo, maana mpaka unakuja mimi sijui
lolote kuhusu ujio wako, nimesikia siku ulipofika, ndugu yangu, dunia hii ni
mapito, acheni hayo jamani…’nikasema
‘Kiukweli, utaamini utakavyo, sikulaumu kwa hilo,… lakini ukweli
ninaokuambia mimi ni huo, kuwa hiyo mipango yao sikuwa na ufahamu nayo kabisa,....walipanga
wao wenyewe, ..kama ningelifahamu hivyo nisingelikuja huko kabisa, ningetumia
njia nyingine ya kulimaliza, bila hata ya wao kuhusika,…mimi kilichonirejesha
hapo ni taratibu za kibali changu…’akasema
‘Tutakutana tu…dhuluma hata siku moja haidumu,..kiukweli kama ni
kweli, umefanya kosa kubwa sana ambalo …sizani kama naweza kukusamehe,..mpaka
sasa sijaamini hilo, siwezi kuamini kuwa wewe unaweza kunifanyia hivyo, …’nikasema
‘Bosi, niamini haya ninayokuambia, sikuwa nafahamu lolote…mimi nilipofika
tu, yakatokea hayo yaliyotokea, kama nilivyokuambia awali, na ndio nikauona huo
mkataba, sijui lolote jingine, na hata kama nimeweka sahihi yangu hapo,
sihusiki, na hawatafanikiwa mipango yao ....’akasema
‘Sawa, endelea kunidanganya, najua nalipa fadhila zangu kwenu,
lakini ahadi yangu na dhamira yangu ipo pale pale, mwenyewe utaona ukirudi ,
labda upotelee huko huko, hilo nakuahidi, nyie si ni wajanja sana, ngoja urudi
....’nikasema kwa sauti ya dhamira
‘Jamani dada, ...bosi, usinifikirie hivyo kabisa, sipo kabisa
kwenye hayo mambo yao, ndio maana wakatumia mbinu hizo walizotumia, ...hebu
niambie mimi ningelifanya nini kwa hali kama hiyo,...Bosi, nakuhakikishia mimi
nikirudi tutayamaliza hayo, wala sipotei, nitarudi...’akasema
‘Najua utarudi labda na ndoto ya kuwa mke mwenza, au
mshirika mwenza, au nani utakavyojua mwenyewe na hawara wako ?’ nikamuuliza
‘Mimi sielewi una maana gani kusema hivyo bosi..hayo yametoka wapi
tena, mimi ni mdogo wako jamani…’akasema
‘Unaelewa sana nina maana gani, sasa hivi sipo kule kwenye kuamini
kinyume chake, wengi waliniona mjinga kuwa ukweli upo, lakini akili imefungwa,
sasa akilio imefunguka, na sitaamini uwongo wenu tena, na sitaki utetezi wako
wowote....’nikasema.
‘Basi wewe subiri nirudi, naona hapa kwenye simu
hatutaelewana, ila nakuhakikishia kuwa sijui lolote kwenye mambo yao, na
mimi siwezi kufanya jambo baya dhidi yako, na ukiona nimefanya jambo, ujue ni
kutokana na ushauri wako, sijawahi kukusaliti mimi, niamini hivyo....’akasema
‘Niliwahi kukushauri uje ufanye ufusuka na mume wangu?’
nikamuuliza
‘Bosi, ufuska gani jamani, mmh mimi naona hapa hatutalewana tena,...kwahivi
sasa, naomba uniache ili nimalize masomo yangu kwanza, hayo na mengine mengi
tutayamaliza tu.., hakuna tatizo kabisa....mimi sijawahi kufanya jambo kinyume
na matakwa yako, kweli si kweli ? sema
ukweli wako, na kwahiyo hata hili, litakwisha tu kwa amani, hilo
nakuthibitishia, ...’akasema
‘Sina amani na msaliti mimi,..rafiki anyekuwa nyoka, sina amani nay
eye tena,….wewe hujui nitavyoteseka huku, hujui kabisa, wewe na mwenzako ni
nyoka wanafiki wakubwa....’nikasema
‘ Oh imekuwa hayo..lakini sawa, samahani kwa hilo, nina imani yatakwisha
tu bosi, pole sana,…’akasema na nikahisi analia
‘Unalia nini sasa…’nikasema
‘Inaniuma sana…hujui hata mimi ninavyoumia, sikutarajia haya
kabisa, ila mimi nakuthibitishia kuwa hilo
litakwisha kwa amani tu, kama utanielewa, maana unavyofikiria wewe sivyo
kabisa, samahani sana kwa kukufikisha hapo, na matatizo yote yanayokukumba,…
nakuomba niwahi darasani tafadhali, kwaheri,… nisalimie shemeji na watoto, ..’akasema
na kukata simu.
NB: Kisa kinarudi kuleee..hii ni kuashiria kuwa mambo sasa yanaanza
kuwekwa hadharani.
WAZO LA LEO:
Tuwe makini na kauli zetu , ulimi unaweza ukasababisha mema na mabaya,ukiutumia
vyema ulimi wako unaweza ukaleta faida kubwa kwenye jamii, lakini ulimi huo huo, ukiutumia vibaya, unaweza
ukaleta majanga makubwa kwenye jamii za watu, tena wenye elimu zao. Ulimi unaweza kugeuza marafiki wakawa maadui. Tumuombe mola wetu atujalie tuweze kudhibiti ndimi zetu, ili jamii ziishi kwa amani na upendo.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment