Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Saturday, August 26, 2017

DUWA LA KUKU...42


Nilifika getini kwa baba mkwe wakati huo nilimuona yule mlinzi akiwa bado kaishikilia ile bahasha mkononi , nikajua ndio hiyo video ambayo mtoto wangu kaileta hapo kwa babu yake,…mimi pale nikawa najiuliza nifanye nini, ..sikutaka kusubiria nikakimbilia kwenye mlango wa geti, labla lile geti halijafungwa, nia ni kumuwahi huyo mlinzi asije kumpatia huyo baba mkwe…na huku nyuma bajaji inafukuza, kwa wakati huo sikujua inanifukuza mimi..

Nilipofika getini, nikaita jina la yule mlinzi kwa sauti kubwa, na wkati huo yule mlinzi anaongea na bosi wake, akiwa bado ndani ya, na yule mlinzi aliposikia jina lake, jina la utani tunaitana mimi na yeye, akageuka akaniona mimi nikamuonyeshea ishara kuwa hiyo bahasha ndio naihitajia, yeye ni askari akanielewa kwa haraka

‘Kuna mzigo wangu wowote…’nikasikia bosi wake akimuuliza hapo nikahisi mapigoa ya moyo yakiongezeka

‘Mzigo upi mzee, ukiwepo nitakueletea, bosi…’akasema.

‘Na hiyo bahasha ni ya nini..?’ akaulizwa

‘Kuna mtu kaacha huu mzigo nimpatie jamaa yangu mmoja….’akasema.

'Sawa sitakawia kama kuna mzigo wowote niletee ndani...'akasema na kuingia na gari la geti lkafungwa.

Nikasubiria kwa nje, nikiwa naomba asije kumpelekea kabla hajaonana na mimi, na mlinzi alipohakikisha bosi wake kaingia ndani, haraka akanifuata na ile bahasha mkononi, na kusema.

‘Bosi unaniweka pabaya…’akasema

‘Kwa vipi…?’ nikamuuliza

‘Huu mzigo nimeambiwa nimpatie huyo mzee akiingia, na aliyeuleta hapa ni kijana wako, alikuwa na haraka sana, anaonekana hayupo vizuri, na alipoulizia kuwa babu yake yupo, nikamwambia hajafika, akasema huu mzigo nihakikishe umefika mikononi mwa babu yake, sasa niambie, una nini..?’ akauliza.

‘Una mambo fulani ya kifamilia, tulikuwa tunataka kumshirikisha babu yake, nikamtuma aulete, sasa kuna mambo ya kurekebishwa kabla huyo mzee hajauona, nimejaribu kumpigia huyo kijana simu, lakini hapatikani, …ndio maana nikaamua kuja mwenyewe, …’nikasema.

‘Basi kumbe sio tatizo, mimi nitampatia mzee na wewe ukiwemo umuelezee tatizo lipo wapi, unajua mimi ni mlinzi siwezi kukiuka masharti ya kazi yangu japokuwa tunaelewana kihivyo…’akasema.

‘Aaah, usitake kuharibu, …haitakiwi kufika kwa huyo mzee kwanza unielewe hapo, huyo ni baba mkwe wangu kuna mambo sitakiwi kuharibu...nataka nilete mambo yakiwa hayana makosa, ni muhimu sana, sutakiwi nikuambie kila kitu…’nikasema.

‘Hapana, nahisi kuna jambo, mzee..bosi, sikiliza mimi nitakaa na hii bahasha, wewe wasiliana na kijana wako kwanza, ili niwe katika usalama zaidi, nahisi kuna jambo, na huyo mwenye bajaji anasemaje..’akasema na hapo ndio nikakumbuka nikageuka na kumuona mwenye bajaji yupo nyuma yangu.

‘Hujanilipa pesa yangu mzee…’akasema huyo mwenye bajaji

‘Oh, samahani sana…’nikasema na kumpatia pesa yake, na mara nikasikia mzee ndani akimuita  huyo mlinzi, na mlinzi akasimama na kukimbilia ndani, nikamfuatilia, na alichofanya yeye, akaicha ile bahasha kwenye droo za meza hakujua nimemfuatilia hadi ndani,.

Hapo nikasema, mungu akupe nini, sikuwa na uvumilivu tena, nikaivuta ile droo na kuichukua ile bahasha kwa haraka na nilihakikisha ina jina la huyo mzee hapo, ilikuwa ni ile ile bahasha aliyokuwa kashikilia yule mlinzi,,,,nikatoka mle kwenye kibanda cha mlinzi na kumuwahi mwenye bajaji

‘Twende, narudi huko nilipotoka…’nikasema, sikutaka hata kugeuka nyuma, najua huyo mlinzi akitoka huko atakutana na mashangao, nitakuja kumweka sawa nikikutana naye, nakama alishamuambia bosi wake kuwa kuna bahasha alitakiwa ampatie. basi atajua mwenyewe cha kusema.

‘Hukujua kilichotokea huko kwa mlinzi na bosi wake…?’ akaulizwa

‘Kwa muda  hapana, mimi nilikuwa na haraka za kwenda kumuwahi mke wangu, kabla hajapatiwa hiyo bahasha nyingine na kijana wangu.

‘Ehee, ilikuwaje..?’

*************

Nilipofika nyumbani nilisikia kijana akiongea na mama yake, nikajua tayari mambo yameshaharibika,…nikaingia kwa haraka na kuwakuta mama na mwanae wanaongea, na mkononi mwa kijana niliona bahasha kama ile niliyoiona kule kwa baba mkwe..

‘Naona nimewaingilia, lakini nina haraka kidogo naweza kuongea na kijana wangu kwanza…?’ nikauliza

‘Kitu gani cha kuongea wewe na yeye ambacho mimi sitakiwi nikisikie…?’ akauliza mke wangu.

‘Leo hii unasema hivyo mke wangu…ajabu kabisa, siku zote matatizo ya huyu kijana akitaka kukuambia unamwambie kamwambie baba yako, hayo ni matatizo ya kiume…, sasa leo nataka kuongea naye mambo ya kiume, unaingilia kati…’nikasema na mama akamuangalia kijana wake, na kusema;

‘Ni kweli kuna mambo mnataka kuyaongea wewe na baba yako ambayo , mimi sitakiwi kuwepo…?’ akauliza

‘Mimi sijui baba anataka kusema nini, hata hivyo, nilikuwa na mzigo wako mama..kama nilivyokupigia simu, nimekuwa nikikutafuta siku nzima ya leo..nataka uupokee mkono kwa mkono…nataka hili lifanyike kabla sijaenda kuongea na baba…sijui anataka kuniambia jambo gani jipya, …’akasema sasa akinyosha mkono kutaka kumkabidhi mama yake hiyo bahasha..

‘Mama, naomba uichukue, utaona kilichopo ndani, na kila kitu kitajieleza, nashindwa kuvumilia tena, haya mambo yamenishinda, sina maana tena, mama.. …’akasema akijizuia kulia.

‘Kijana, wewe ni mwanaume kwanini unajilegeza hivyo, nilishakuambia haya mambo nitayamaliza mimi, ukideka kwa mama yako unafikiri ataweza kukusaidia kwa hilo, na hiyo bahasha unayompa mama yako ina nini, kuna nin ikipya wakati tulishaongea, huo ni udhaifu mwanaume hatakiwi kuwa hivyo,.unasikia au unataka kumuua mama yako…?’ nikamuuliza

‘Kama nilivyokuambia baba, muda umekwisha na mimi ni lazima nitimiza nadhiri yangu…’akasema na muda huo bado bahasha ipo mikononi mwake, nikavutika kutumia nguvu kuichukua lakini nikaona nisifanye hivyo, namfahamu mke wangu namfahamu kijana wangu,..najua jinsi gani ya kuwaweka sawa.

‘Sikiliza kijana wangu ndio maana nimefika kwa haraka nikitoka hapa kuna sehemu tutakwenda, tutayamaliza hayo matatizo yako …nimeshapata ufumbuzi wake, wewe achana na mama yako, mama yako kwa hivi sasa ana mambo mengi yakufuatilia, usimzidishie presha…’nikasema.

Mke wangu kwa muda huo alikuwa akiweka kitambaa kwenye meza vizuri, huku katega sikio, hakutaka kuingilia moja kwa moja, na mimi namfahamu mke wangu alivyo, sio mtu wa papara, nikaona nichukue nafasi hiyo kuyaweka haya mambo sawa, nikasema.

‘Mke wangu kijana wetu ana matatizo, lakini kama nilivyokuambia kuna matatizo mengine ya kiume, na mimi nimeshajua jinsi gani ya kumsaidia,..lakini naona kama haamini, unajua vijana walivyo, wanataka kila kitu kiende kwa haraka..sio vitu vyote vinakwenda hivyo,.. na njia anayotumia yeye itazidi kumuharibu…’nikasema na mama yake akasimama na kumuangala kijana wake, akasema.

‘Ni kweli anayosema baba yako..?’ akamuuliza, na kijana akawa anaangalia pembeni, huku akijipiga piga na ile bahasha mguuni.

‘Mimi  sijui baba ana maanisha nini, lakini kwa vyovyote iwaavyo, mimi najua baba anachotaka ni nini, na keshashindwa kwenye mambo yake, lakini hataki kuukubali ukweli…mimi nitahangaika kivyangu, ikishindikana, basi maamuzi yangu hayatakuwa tofauti na wengine….sitakuwa mtu wa kwanza kulifanya hilo…’akasema hivyo, na mama yake hapo akageuka sura na kusema.

‘Kwani ni kitu gani kinachoendelea hapa, nimekuuliza mara nyingi, una tatizo gani hutaki kusema, mwishowe unasema baba anajua una tatizo gani, haya baba yako kaja anasema kapata namna ya kukusaidia, unasema sio kweli, ..haya niambie tatizo ni lipi ili na mimi niweze kukusaidia…’akasema.

‘Mama utayajua tu….’akasema akiiangalia ile bahasha.

‘Nitajua kwa vipi, unajua polis wanakuchunguza, nimeambiwa unatumia madawa la kulevya, wewe unakana,…na hilo baba yako anakutetea, kuwa hutumii, nyie watu wawili mna nini, mbona mnataka kuniua kwa shinikizo la damu…’akasema mama mtu.

‘Mke wangu hili swala la kijana wetu niachie mimi mwenyewe, nitalimaliza…sema yeye hataki kunielewa,..nimeshamuambia kuna mambo mengine ni ya kiume zaidi, mama yako hataweza kukusaidia, mimi peke yake ndiye naweza kukusaidia,..kijana wangu niamini mimi, na acha mawazo yako ya haraka haraka, unachofikiria kukifanya…, sijui ni kitu gani, lakini nakuambia, hakitakusaidia, mimi ni baba yako niamini…’nikasema.

Kijana akageuka kuniangalia na kusema;

‘Uliyemtegemea kukusaidia ameshafariki, na niliyetegemea kunisaidia mimi na yeye ameshafariki, najau siku nzima ya leo umekuwa ukinifuatili nyendo zangu, kila sehemu ulipopitia nimepigiwa simu, sasa sikiliza baba, hatua hii ilipofikia, sizani kama una loloye jipya la kunisaidia,..’akasema

‘Ninalo la kukusaidia,  unajua mimi nimetokea wapi…?’ nikamuuliza

‘Ulitokea kwa yule binti alikuwa akifanya kazi hapa, ukaenda kwa babu…’akasema

‘Kwa yule binti kufanya nini…?’mke wangu akauliza na mim sikujali swali la mke wangu, nikasema

'Huko nilikuwa nakutafuta wewe ili kukuelezea hatua niliyofikia kuwa nimeshampata mtu wa kukusaidia...'nikajitetea hivyo.

‘Mama yote utayaona humo, baba anachoongea ni kutafauta njia ya kupoteza muda, najua yameshashindikiana, …ngoja mimi nikajaribu bahati yangu huko ninapokwenda, mkiniona kimia, basi mjue mambo yameharibika…lakini kama nilivyoahidi, kabla ya kuondoka, nataka kila kitu wewe mama ukijue…’akasema sasa akinyosha mkono kumkabidhi mama yake ile bahasha.

Sikutaka kuchukua papara , japokuwa kiukweli bahasha hiyo akija kuiona mke wangu akaona yaliyomo humo, najua atazidi kunichukia, na itakwua ushahidii wa kuvuinja ndoa yetu....mimi hapo nikatabasamu na kusema;

‘Vizuri kijana, hata mimi nilikuwa nataka mama yako ayaelewe hayo mambo yote.. kama yana ukweli,..lakini ukumbuke mimi ni baba yako nimeiona dunia kabla yako,..na siku zote nimekuambia, unapokutana na matatizo usikimbilie kuona kuwa watu watakusaidia, kwanza fikiria jinsi gani ya kujisaidia wewe mwenyewe kwanza.., halafu ukihitajia msaada angalia mtu ambaye anaweza akawa keshakutana na tatizo kama hilo, na sio wote watakaoweza kukusaidia…’nikasema nikionyesha sina wasiwasi.

Muda huo mama yake alikuwa anasita kuipokea ile bahasha, namfahamu mama yake alivyo, yeye sio mtu wa papara, aliona huenda akiichukua hiyo bahasha bila kujua undani wake anaweza kuharibu kabisa akasema;

‘Hebuni kwanza nyote wawili…, kijana wangu, hiyo bahasha unayotaka kunipa ina kitu gani…?’ akauliza mama

‘Ukweli wote kuhusu mambo ya humu ndani…’akasema akinitupia jicho mimi.

‘Mambo gani, sikiliza wewe mtoto, usifanye mambo ya kijinga, ukatoa siri za humu ndani kwa vyovyote vile, mpaka unatengeneza vitu kama hivyo ina maana ulipeleka mahali wa kutengenezee,…sikiliza mwanangu usione mimi nipo hivi nimekutana na matatizo mengi sana, kati yangu mimi na baba yako,.. lakini siwezi kamwe kutoa siri za humu ndani, maana hujui ni nani adui yako…’akasema mama yake

‘Unaona kijana wangu…sisi ni watu wazima tuna hekima zetu…wewe unachokifanya ni utoto….msikilize vyema mama yako…’nikasema

‘Mimi mama sijatoa siri za humu ndani, nalifahamu hilo sana na kama ningelitaka kufanya hivyo ningelikuwa nimeshafanya hivyo mapema tu…, ndio maana haya mambo ya humu ndani ambayo najua kwa hivi sasa yamefikia kubaya, yanahitajia msaada wa mtu baki ambaye sio mbaya ,..ndio maana nikamshirikisha na babu, sijampa mtu mwingine wa nje…’akasema

‘Unasema nini wewe mtoto ina maana humo kuna mambo ya humu ndani, na umempelekea babu yako, una akili kweli wewe..babu yako muda wote anataka nitengane na baba yako, ndivyo unavyotaka wewe..sii kila siku siku wewe unataka mimi na baba yako tuwe na furaha..nafahamu hilo halitawezekana tena, lakini..sio kwa jinsi unavyotaka wewe, wewe ni kijana mdogo sana..’mama yake akasema kwa ukali

‘Mama nisikilize na mimi, huenda kuna mambo ambayo nashindwa kukuelezea kwa moja kwa moja ndio maana nimetumia njia hiyo, kuna mambo ambayo hata wewe huyafahamu ndio maana nimetumia njia hii,kuna mambo ambayo kiukweli yakiachiwa yatakuja kuleta matatizi makubwa kwenye familia hii ndio maana nimetumia njia hii..kuna mambo ambayo yananitesa,…..ndio…’akatulia, maana simu yangu ilikuwa inaita, nikasema

‘Sasa sikiliza, wewe si unataka mama yako ayaona yote hayo, haya mpe hiyo bahasha tuone atakavyokusaidi, kama hutakuja kujuta..utamuua mama yako kwa shinikizo la damu, halafu utajuta ukiwa umeshachelewa…unasikia, na likitokea hilo, ndio hapo utaona ni nani kama wazazi wako..’nikasema na hapo kidogo akahisi jambo, sasa akawa karudisha ule mkono uliokuwa umeshika hiyo bahasha, na mimi nikapokea simu

‘Halloh ni nani wewe..?’ nikauliza

‘Ni mimi bosi…’ilikuwa sauti ya yule mlinzi kwa baba mkwe

‘Unasemaje..?’ nikauliza

‘Umeshaangalia hiyo bahasha uliyochukua, kwanini umefanya hivyo bosi…?’ akaniuliza na muda huo ile bahasha niliweka kwenye koti langu , koti langu ni kubwa tu, nikasema.

‘Bado kwani kuna tatizi gani..?’ nikauliza

‘Mzee, kumbe huniamini…’akasema

‘Kwanini..nakuamini sana, ila kuna mambo yanahitajia haraka wewe hujui nilichotaka kukuelezea, lakini usijali sana, kwani kuna tatizo?’ nikamuuliza.

‘Usingelifanya hivyo bosi..., ulichokifanya kimenifanya nikufikirie vibaya, kuwa kumbe hata wewe hunitakii mema, hivi huyo mzee akiligundua hili, mimi nitakuja kusema nini…’akasema.

‘Usiwe na shaka, aliyekupa hiyo bahasha ninaye hapa, nimeshayamaliza, ni kijana wangu na ni mambo ya kifamilia, usiwe na shaka na hilo..’nikasema.

‘Lakini hayajaisha kwangu bado, kwani huyo kijana wako alimpigia babu yake simu kuhakikisha kuwa keshaupata huo mzigo na babu yake akaniuliza kuna mzigo ambao nimepewa na huyo kijana, ..ulitaka mimi nisema nini hapo..?’ akauliza

‘Sikiliza mimi nipo na huyu kijana, tunayaongelea hayo mambo, nitakupigia nikimalizana na yeye usiwe na wasiwasi..unasikia, hebu niache kidogo ,….’nikasema.

‘Sikiliza bosi nayaongea haya kwa vile bosi anasubiria hiyo bahasha, na ….’akasema nikataka kukata simu

‘Usikate simu bosi,..maana sitaki kupoteza kazi yangu..mimi nitampa hiyo bahasha kulinda kitumbua changu,…’akasema

‘Utampa bahasha ipi tena,..sikia, nimeshakuambia …?’ nikauliza nikishika pale kwenye koti langu kuhakikisha kama ile bahasha ipo.

‘Hiyo aliyonipa kijana wako, ni lazima niifikishe kwa bosi maana ameshapigiwa simu na anajua ipo kwangu…’akasema

‘Usiwe na wasiwasi na hilo, nitaongea na bosi wako, nitayamaliza…’nikasema.


‘Sawa wewe ongea naye tu, ila mimi ndio hivyo  nataka kumpelekea bosi ndani...'akasema

'Utampelekea vipi bosi wkati bahasha hiyo ninayo..'nikasema

'Hahaha bosi, usifikirie mimi ni mtoto mdogo bosi, bahasha hiyo bado ninayo hapa, nilitaka kukujua unanithamini vipi, hebu iangalie hiyo bahasha ina nini...'akasema na kabla sijajibu kitu akaongezea kwa kusma

'Na  kama una lolote utampigia  bosi mwenyewe ..mimi nakwenda kumpa..’akasema hapo, nikahisi mwili ukinicheza cheza, ikabidi niitoe ile bahasha niliyokuwa nayo  bila kujali kitu na nilipotoa na kuifungua ndani nikakuta kadi ya mualiko wa harusi..

NB: Ndivyo ilivyokuwa siku hiyo, je kuliendelea nini, tukutane kwenye sehemiu ijayo

WAZO LA LEO: Wengi wetu tunapenda kujiangalia wenyewe kwanza, ndivyo asili yetu ilivyo, mtu upo tayari kudanganya au kufanya lolote ili upate wewe kwanza, na mwenzako akose, hata kama unajua haki ni ya mwenzako. Ubinafsi wa namna hiyo ndio unaipeleka dunia kubaya, uhasama, chuki, propoganda, ilimradi mtu au taifa linataka kumiliki hata ikiwezekana kila kitu. Mola wetu katuambia, tukitaka tuwe na imani sahihi ya kumuabudu yeye, basi ni mpaka pale itakapofikia mtu yupo radhi mwenzake apate yeye akose, au yupo tayari kumpendelea jirani yake zaidi yake yeye...je imani hiyo tunayo.


Ni mimi: emu-three

No comments :