Majogoo yana tabia yake, kwenye mitaa, akija jogoo mgeni ni
lazima kutatokea kupigana na majogoo wenyeji, kupimana nguvu, na wakikutana
majogoo wenye nguvu sawa, wanaweza kupigana siku nzima, kisa nini hasa, kwanza ni kuonyeshana
ubabe nani zaidi, lakini pia kumiliki mitetea,…na kutawala, hayo ndio maisha yao..na maumbile yao…, ubabe
ubabe.
Mitetea nayo hujibaragua kwa hayo majogoo, hasa wakiona huyo
jogoo ndiye mwenye nguvu, hata vifaranga havichezi mbali, kwani kwa kawaida
majogoo hupenda vifaranga, na wakati mwingine huwaita virafanga kwenye chakula…wakifanya
hivyo hata mitetea nayo huja karibu karibu, na hapo jogoo anakipata kile
anachokitaka.
Wakati nafurahia maisha haya ya kuku, nikasikia mkuu wa
taifa kubwa akisema yeye ni taifa kubwa na ana uwezo wa kufanya mambo kwa
masilahi ya taifa lake,hata ikibidi kuwahamisha wageni wote, ambao kwake yeye
anaona ni adui wa taifa lake, ..ubabe, lazima ajionyeshe kuwa yeye ni nani, na
taifa lake ni nani….!
Ni kweli wapo wakorofi, wapo wenye sera mbaya, lakini pia
kuna wenye shida, sizani kama mtu atakimbia nyumbani kwake au nchini kwake kama
kweli hakuna shida, na shida nyingine chanzo ni huko huko, …tujiulize silaha zinatoka
wapi…, propaganda za kuwagawa watu wapigane ili kuwe na namna ya kupata mali
ghafi, zinatoka wapi …ni ujanja ujanja wa ukoloni mambo leo…
Kwa ufupi,
sio kwamba wao wamependa, wameona sehemu nzuri ya kuishi ni huko,… lakini leo hii wao sasa wanaambiwa mkafie kwenu, `kama hamuwezi kujitawala tuje sisi tuwatawale…' ni kebehi,…
japokuwa ukweli mwingine unauma!
Hata hivyo pamoja na mengine nimefurahia sana sera ya huyu
bwana mkubwa, sera ya kupiga vita ni hiki kizazi cha hatari , kizazi ambacho kinataka kueneza maisha ya ‘Sodoma na Gomora’, hawa watu wanataka
kuiangamiza dunia,…hawa watu ni kizazi kile kilichlaaniwa na sasa kimekuja na
mtindo mpya wa `haki za binadamu’, jamani huo ni ubinadamu au ni unyama, kwa hili mimi nampongeza huyu mkuu kwa kulivalia njuga hili janga.
Na wakati sijaendelea kulitafakari hili mara nikasikia mkuu
wetu wa kaya naye akiongoza vita vya kupambana na janga jingine kubwa, la ‘madawa
ya kulevya’.. ambalo limewashinda viongozi wengi,..sijui kwanini, nasikia kuna ‘kuogopa’
maana mtandao huo ni mkubwa, una wakubwa na matajiri wa hali ya juu, lakini
uongozi ni nini…, kiongozi ni yule anayefanya mambo kwa masilahi ya watu wake
bila kujali hatari yake, kwani uongozi ni dhamana, uongozi ni deni, na usipoifanyia
kazi hiyo ambayo ni dhamana kwako, utakuja kuulizwa
mbele ya haki.
Wengi wa viongozi wanapoingia madarakani wanajaribu kutimiza wajibu wao,...kuonyesha wao ni nani, lakini baadae wanafikia sehemu wanaonjeshwa asali ..na asali hulambi mara moja,…na ukilamba
sana unalewa, dhamana inasahaulika, na matokea huja kuwa `nguvu za soda..', nawaombea
viongozi wetu wasifikie huko, vita hii iwe ni endelevu…
Nakumbuka kisa cha viongozi wa imani, walikuwa hawalali,
usiku wanapita mitaani wakiwa wamejibadili kama raia wa kawaida, nia ni kutaka
kujua hisia na matatizo ya raia zake, walikuwa hawalali, hawali wakashiba, hata
kuvaa vizuri wanaogopa,…..hawanenepi..watanenepaje wakati hata kula
wanaogopa, kwani wakila wakishiba, wanajiuliza hivi na raia zangu wameshiba…hawa
ndio viongozi wa kweli..., raia wangu kwanza, mimi mwenyewe baadae…
Wakati sasa umefika, tuwasaidie viongozi kama hawa, ambao
kweli ndio tuliokuwa tunawataka, …tuondakane na majanga haya yasiyokwisha,
..tunaona raha gani tukiwaona vijana wetu wanateketea kwa madawa ya kulevya,
ushoga, usagaji..ulevi, wizi na ujambazi, wakati huo huo watu wengine wananeemeka, wanajenga
mahekalu kwa kafara la vijana wetu….inaumiza, na dhambi kubwa sana mbele ya mungu,..ndio maana
hata ile baraka na neema ya sili inakimbia, tukikaa kimia, kwasababu eti sio watoto wangu wanaoumia,…ni leo kwao kesho matatizo
hayo yatahamia nyumbani kwako, na ukienda mbele ya haki una mashitaka makubwa….
Tumuombe mola atusaidie vizazi vyetu viondakane na majanga
haya hatari, na viongozi wetu watimize wajibu wao kwa uadilifu, na wale wote
wenye nia mbaya ya kuangamiza wenzao kwa masilahi yao, washindwe na
wafichuliwe.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment