Ni mbiu ya mgambo, na mbiu ya mgambo ikilia ina jambo, na
hasa ikiwa inapigwa na tan-tan-lila mpiga mbiu mashuhuri ambaye mitaani wamempa
jina la ‘Tantalila…’
‘Ndugu wa kazi wa nchi hii ya ‘Boraliende..’ akaanza mpiga
mbiu, na wakati huo wakazi wengi walishatega masikio, na akina mama walishatoka
nje na wengine kusimama milangoni kusikia mbiu hiyo ya mgambo...., maana mpiga mbiu huyo ni mtaalamu na
mara nyingi , yeye akipewa hiyo kazi ujue kuna ujumbe muhimu sana...
Lakini sio tu kwa ujumbe muhimu, lakini pia na mbwembwe zake
za utangazaji.., kila akiongea jambo huwaacha wakazi wengi kwenye teta-teta
nyingi na gumzo la siku, hata wenzetu wauza magazeti na vyombo vya habari soko
lao hupanda maradufu.
‘Wana Boraliende, mtege masikio vyema, na yule asiye na sikio
akaazime sikio kwa jirani yake, kwani
ujumbe huu unamuhusu kila mkazi wa N-NCHI..ya bora liende… na hata yule asiye
mkazi,…unawahusu pia, ilimradi ana uhai…hata mifugo ifungulieni milango isikie
maana litawagusa hata wao,….’akaanza mbwembwe zake.
‘Ndugu zanguni tumeingiliwa…’hapo akapiga tantalila lake
kidogo….
‘Tanta –ta-ta-rararara… Tanta –ta-ta-rararara….’
‘Tumeingiliwa majumbani mwetu,..tumeingiliwa mpaka chumbani, ….maisha
yetu yamewekwa rehani, na tusipoangalia tutaishia kuzimu…’ akatulia.
‘Huo ndio ukweli….lakini niwaulize jamani, hivi jamani hamlioni
hili,…’ akatulia
‘Jamani…tunalima,…tunafuga, ni nani asiyeijua nchi hii, toka
zama za mababu, kulima na kufuga ndio jadi yetu,…pia tunafanya kazii kwa bidi
tu…tunazalisha sana tu….’akatulia
‘Lakini cha ajabu mauzo, mazao hatuyavuni, na hata tukivuna
hatuuzi, na hata tukiuza hatupati, na hata tukipata hatujui kina kwenda wapi…sababu
ni nini…au nadanganya…?’
‘Kipato chetu kimekuwa ni duni…umasikini umekithiri…hivi hili
jamani hamlioni….’akawa kama anauliza na wakazi wale wale waliokuwa karibu
karibu wakawa wanaangaliana na kutikisa kichwa kukubali.
‘Kuna mdudu anapekenyua maisha yenu, amavuruga akili zetu, za
vizazi vyetu maisha yetu, huyu mdudu ni hatari maana anaweza kuingia hadi
kwenye akili zetu, atatughilibu, na kufanya kile anachokitaka, huyu mtu lakini
ni mdudu…’akatulia
‘Ukweli ni kuwa tumeingiliwa…na hili ni janga, tumeingiliwa
na ‘MDUDU-MTU…’akatamka maneno hayo ya mwisho kwa sauti kubwa na mbwembwe
‘Huyu mdudu mtu ni mchawi mkubwa duniani, ..huyu kazi yake ni
kusubiria, ulime, uvune uuze, halafu kwa ulaini anazichukua pesa zetu,….hamulioni
hilo jamani, mkuu anauliza hamlioni hili,..hali sasa zimekuwa sio nzuri, njaa,
hali ngumu, ndoa zina migogoro,….tumekondeana kama tunaumwa nanihino…’hapa
wenye kucheka wakacheka.
‘Hatuumwi nanihino kabisa kabisa mkuu kasema hakuna huo
ugonjwa,….kwani keshaligundua hilo tatizo….’akatulia
‘Mkuu kasema keshampata huyo mdudu mtu, na keshaipata dawa
yake…..kampata mtaalamu kutoka milimani, mganga mwenye siha, mwenye nguvu,
mwenye utaalamu, mganga anayeona mbali….yeye ataimaliza hii kazi mara moja,
hiyo ni ahadi yake….’hapo akakohoa.
‘Jamani ni nani asiye na shida…?’ akauliza kama vile
anahutubia, lakini anapita mitaani, na tantalila lake, wakazi kila mmoja
akasema, ‘tuna shida,..kila mtu ana shida, mimi nina shida…ni kweli tuna shida…’
japokuwa wengine walisema kimoyo.
‘Sasa tunataka kumtoa huyu mdudu mtu, …tunataka kumtoa
majumbani kwetu, kwa udi na uvumba, tunajua wapi alipo, tunajua wapi anafanyia
shughuli zake tunawafahamu na washirika wake…na yeye ni wakala tu, wenzake
wakubwa wapo, tunaishi nao tunakula nao…lakini kwa vile …hatuna ufahamu wa
kuwajua, …hatuwajui…sisi hatuna utani,…kazi ni moja tu, utekelezaji, si
mnatufahamu jamani…kazi ni moja tu…’akapuliza tantarira…..
‘Wengine ni ndugu zetu, jamaa zetu, marafiki zetu….tutawataja
hatutaogopa…’akatulia,
‘Sasa ndugu zanguni, mjumbe hauwawi….wakati umefika,..wakati
wa kumfichua huyo mdudu-mtu, na mawakala zake….je huyu mdudu mtu ni nani, na
anafanya nini, mhh, huo ni mzigo mzito kwangu,…….’akasema mpiga mbiu
‘Huo ni mzigo wa Mkuu wa nchi ……’
‘Huyu mdudu mtu alikuwa kajificha, kava ngozi ya kondoo,
mawani ya giza,…ana walinzi wa juu na chini, ana ….kila kitu, anajua kujibadili
kama kinyonga,… lakini sasa keshapatikana….mnasikia mkuu wa nchi keshampata huyu
mdudu mtu, na washirika zake….’akasema na kulipuliza tantarira lake.
‘Huyu mdudu mtu kawafanya vibaya watoto wetu,,….watoto wetu ,
kizazi cha leo na kesho, hata kazi hawawezi sasan, watoto wetu wamelegea hawana
nguvu tena, wanatoa maudenda tu…..inasikitisha…’akatulia
‘Jamani hili janga hamlioni ….ni nani asiye na uchungu wa
mwanae,..eeh, niambie,..sasa wakati umefika,….tushirikiane, na kushirikiana
huku ni kusaidia kumtoa, kumfichua, mkuu anawafahamu lakini nyie ndio mnaishi
nao…toeni ushirikiani tuharakishe hii kazi….’akatulia
‘La mgambo ndio hilo mwenye macho atizame, mwenye masikio
asikie, ukimaliza kusikia kama uliazima sikio kwa jirani usisahau kulirejesha kwa mwenyewe…mkuu
katoa siku saba tu, hao watu wajisalimishe, la sivyo, ataingia nyumba hadi
nyumba… ’akamaliza kwa kupiga tanta-rira lake
Wakazi wa Bora liende wakabakia wanaulizana..ni nani,..ni
yupi…, ikawa ni soga ya siku, magazeti yakapambwa kwa vichwa vikubwa, mdudu mtu
keshapatikana, mkuu anataka kumtaja mdudu mtu....na wauza gumzo ikawa ndio kazi
yao…..wambeya, watesi….wakapata cha kuongea…mdudu mtu mdudu mtu……sasa fupa
limepata mtafunaji…
‘Mhh…haya jamani, fupa lilomshinda fisi ni nani wa
kulitafuna..
Tutaona sehemu ya pili
‘Huyu mdudu –mtu ni nani?’
Wakatabahu mzee wa Busara.
emu-three
No comments :
Post a Comment