Kitendo cha docta
kusita kunipa majibu yenye uhakika kilinifanya nihisi kuwa huenda kagundua kuwa
mimi mimi bado nina matatizo, lakini imani niliyokuwa nayo ilinifanya niamini
kuwa mimi nimepona…niliamini toba yangu, niliamini maneno ya yule kiongozi wa
imani
‘Ehee sasa
ikawaje…?’ nikamuuliza
‘Sasa
ikawaje..subiria uone majibu yake sasa…’akatulia akiwa anaangalia mbele…
‘Unajua kabla sijahitimisha kisa hiki,
nikuambie ukweli, mimi nimekuwa ni shuhuda kwa vitendo,..unajua mimi
nilishajulikana kuwa siwezi kuzaa …tasa,…tasa, na hata kamaa ningeweza kuzaa kwa vipi, maana
nilishaandamwa na maradhi mabaya
yanayovunja nguvu za kiume, nilipatwa na gonjwa la kisukari, ugonjwa wa moyo…vidonda
vya tumbo…ooh,
Sasa mtu kama miye
ambaye nilishajulikana hata hospitali kuwa siwezi kazi, ..unajua kisukari kinavyotesa..hutakiwi
ule vyakula vizuri vizuri..haya presha,..haya hata nguvu za kiumwa huisha
kabisa…hebu katika hali kama hiyo ni nani atakubali umuoe binti yake,…hebu
fikiria hapo hata ingelikuwa ni wewe, na hata huyo binti anakupenda vipi kweli
atakubali umuoe tu, kwa lipi nililokuwa nalo tena…ili aje tu kuniangalia, sina
mali, sina…nilishakwisha….’akatulia
‘Kwahiyo…?’
nikauliza
‘Ndio nakuuliza
wewe….ili uone nguvu ya toba ilivyo…..’akasema
‘Sasa nikurejeshe
nyuma kidogo,….’akaangalia saa yake halafu akaendelea kusimulia;
‘Ukumbuke docta
alishachukua vipimo vyangu,…ipo siku tulikwenda na docta akachukua vipimo
vyangu, lakini hakuweza kunipa majibu siku hiyo, ilihitajia muda wa kuvifanyia
kazi…na ikawa kila nikimpigia simu anasema nisubirie..nikajua hakuna jipya.
Na ndio yakaanza kutokea haya ya huyu binti,
kuumwa, na hata kwenda kwao..nielewe hapo kidogo, kuwa haili ilivyo, hata docta
asingeliweza kunitetea…’akatulia.
*************
Sasa huyu binti
alipofika kwao ilikuwaje…!
Huyo binti
alipofika kwao, akapokelewa kwa vigelegele..hata mwenyewe alishangaa, kumbe
alishaandaliwa kama mtarajiwa wa kuolewa,
Kumbe wazee, akina….baba
mama, mashangazi walishapitisha kuwa huyu binti anaolewa na nani,….kumbe watu
walishaleta hadi mahari, uone ilivyo kuwa ngumu..ngombe nyingi tu,
zilishapokelewa, na muoaji keshapitishwa ni nani..
Sasa ndio binti anafika
nyumbani akiwa kebeba taarifa yangu, na taarifa yenyewe ya mikono mitupu,.. eti
mie namtaka kumuoa binti yao, unajua hata binti mwenyewe awali, aliogoapa
kabisa kuliongelea hilo…Ataanzaje..
Alipoanza kuelezewa
kuhusu hizo posa na sifa za muaoji,…akataka kujitetea, akasema yeye kwa hivi sasa hataki kuolewa..na
hilo swala limekuwa kwake la kushitukiziwa, anahitajia muda wa kuliwazia, hata
huyo bwana mwenyewe hajawahi kuongea naye….
‘Kwanini, ina maana
hutuamini sisi wazazi wako….?’akauliza na hakusema moja kwa moja, kunihusu
mimi,
‘Au labda
umeshapata mwanaume mwingine, maana nyie mabinti wa siku hizi, mnajiamulia tu,…na
badala ya hata mwanaume kuja kujitambulisha nyie ndio mnajitambulisha wenyewe
kuwa mna wachumba…’akasema mjomba.
‘Hawezi kutuangisha
binti yetu, mimi ni imani hawezi kutukataliwa chaguo letu,….’akasema shangazi.
‘Haya mnataka apewe
muda gani, eti binti tukupe muda gani kuamua…?’ akaulizwa.
‘Naombeni hata
mwezi….’akasema.
‘Haiwezekani,
tunataka kauli yako hii leo,..labda unaona aibu kutuambia hapa,haya nenda
ukaonge na shangazi yako faraghani na mama yako …’akaambiwa
Kweli ikabidi
watoke na shaangazi, na mama kwenda kuongea faragha, na huko binti akaanza
kuonywa, na kwa maneno makali ,..kuwa asije kuikataa hiyo ndoa, maana ina
umhyimu mkubwa.
Binti akaona
autumie mwanya huo kujieleza.
‘Eti nini unasema
nini, wewe binti mbona una hatari,
unataka kutuletea mtihani gani huo,..huyo mtu hatakiwi, na unakumbuka, alikuwa
haelewani hata na mkewe, mpaka anafariki, sasa unakuja na hoja, hiyo,..sisi
hilo hatuwezi kabisa kuliongelea….’wakasema lakini binti aliposisitiza, ikabidi
akina mama hao kuja kutoa taarifa kwenye kikao.
Wazee waliposikia
hilo, walipandisha zile mori za kiasili,….baadaye mjomba akatuliza kikao na
kusema;
‘Tulijua tu…wewe
umekaa na huyo muhuni huko mjini, kakughilibu akili yako...na nyie watu hivi
kwanini mlimruhusu huyu binti mwenye
maadili yetu aende kuishi na huyo muhini huko mjini, mnaona madhara yake
haya…’akasema mjomba
‘Au ni kwa vile nilisikia
kuwa huyo mwanaume anaumwa, hawezi kazi…au…?’akauliza mjomba kwa hasira na baba
akawa kainamisha kichwa chini tu kwa aibu…huku akitamani kumrarua binti yake
mbele ya kikao.
‘Hivi nyie watu
kwanini mkamruhusu….’wakaulizwa tena wazazi.
‘Lakini kaka, hebu
kwanza tumsikilize mwanetu, unajua yeye ndiye anatarajia kuishi na
mumewe..hatujui ni kwanini akafikia uamuzi huo…lazima ana sababu za msingi ,
mnamfahamu vyema huyu binti yetu, hawezi
kutuabisha…’akasema mama
‘Haya atuambie
tumsikie..au labda keshapachika mimba ..tuambie sasa…’akasema baba sasa.
‘Atapachikwaje
mimba, wakati tunasikia huyo mwanaume, jogoo haliwiki, au ilikuwa uwongo,e…hapo
tena labda mumsingizie….’akasema shangazi kwa mdhaha.
‘Sasa huyu binti
ana sababu gani, atuambie la sivyo, asubirie maamuzi yetu, msimbembeleze huyu,
hawa mabinti mkiwaachia mwisho wa siku aibu ni zetu..haya tuambie…’akasema
mjomba
Binti alikaa kimia,
hakujua hata aanzie wapi, na baba akasema;
‘Mimi naona
tuchukua uamuzi wetu, maana huyu binti
anataka kutuabisha, hapa kijijini wamekuwa wakituongelea vibaya, wanatudharau,yote
haya ni sababu ya mama yake, eti anamuheshimu marehemu, marehemu hayupo, …’sasa
akajitetea baba.
‘Usimlaumu mkeo,
kama ni makosa haya ni yenu wote….’akasema mjomba.
‘Sasa sikiliza wewe
binti…, sisi kwa pamoja, tumeamua utaolewa na huyo mtu wetu tuliyemuona
anakufaa, nay eye anatoka kwenye familia tunayoifahamu sisi…’akasema baba, hapo
binti akaamua kufungua mdomo, na kusema;
‘Baba,..na wazazi
wangu kwa ujumla… naombeni sana, mnisikilize na mimi… wazazi wangu mimi sitaki
kuwakatalia mawazo yenu na maamuzi yenu, nawajali sana wazazi wangu, lakini
hebu rejeeni nyuma, mkumbuke mema mangapi aliyowahi kuwafanyia
marehemu..mumeshasahau hayo jamani….ni nani aliwasaidia hata kufikia kuwajengea
hiki kibanda, mumeshamsahau kwa vile hayupo duniani…’akasema binti
‘Hayo yana maana
gani kwetu, yanahusiana nini na maamuzi yetu…?’ akauliza shangazi.
‘Ndio…yana maana
kubwa sana…, ili mfahamu ni kwanini nikakubali huyo mwanaume anioe….’akasema
binti.
‘Hakuna kitu kama
hicho,..usituletee uhuni hapa,….haya elezea, inahusianaje na hili….?’ Akauliza
mjomba.
‘Marehemu hatuna
ubaya naye, sisi ubaya wetu ni kwa huyo mume wake, mume ambaye alimtenda sana
mke wake, kila mtu anazifahamu sifa zake, japokuwa mkewe hakutaka kumtangaza
ubaya wake....’akasema shangazi.
‘Na hata yeye
mwenyewe unamafahamu sana, umeshasahau
alichotaka kukufanyia kipindi kile,..ukaapa kuwa hutarudi tena
kwake..unakumbuka,..huyo kawafanyia mangapi mabinti wa wenzake..ni mume gani
huyo, unataka kutuletea mbegu mbaya kwenye kizazi chetu…wewe hujui tu..tabia nyingine
mbaya hurithiwa…’akasema baba.
‘Baba huyo mnaye
mzungumzia nyie alikuwa mwingine, huyu wa sasa ni tofauti baba, huyu wa sasa ni
mcha mungu wa kweli, kabadilika kabisa…, alichokifanya sio rahisi mtu wa
kawaida kukifanya, …niulizeni mimi niliyeishi naye hapo nyumbani..wazazi wangu
nilichotaka kuwaambia ni kuwa, marehemu ndiye yeye mwenyewe aliacha usia kuwa mimi
nije kuolewe na huyu mtu…’hatimaye binti akapasua ukweli.
‘Eti nini…marehemu
aliwahi kukuambia hivyo….hapana kama ni watu wamekuambia hivyo, wao wamekudanganya,
yule mtoto haweze kumchuuza mwenzake, mfupa ulimshinda yeye kwanini amtupie
mwenzake, hana tabia hiyo, usimsingizie …’akasema mama.
‘ Ni kweli mama,
..hakuwahi kuniambia mimi moja kwa moja..lakini aliacha usia huo kwa watu , na hao
watu ni watu kuaminika, na wao ndio walionishawishi mimi, sasa je mnataka
nimkane marehemu…., nikiuke usia wake, mtu tuliyemuona kama ndugu yetu,
nilimpenda sana, na niliahsi kumfanyia chochote….’akasema binti kwa sauti ya
kusikitika.
‘Oh…unaona
ulivyoghilibiwa, yeye mwenyewe mfupa ulimshinda, au sio… sasa anataka na wewe
ukautafune , wewe una meno gani, kwanza hebu tuulize sisi wazazi wako kwanini
hatutaki wewe uolewe naye,…tuulize, tunasababu za msingi…’akasema mjomba
akiwaangalia baba na mama.
‘Je una hakika gani
kuwa marehemu alitoa kauli hiyo, kuwa yeye akifariki uje kuolewa na mumewe,,..?’
akauliza baba akionyesha kushitushwa sana na kauli hiyo, na ilionekana
imemgusa.
‘Ndio baba…ushahidi
na mashahidi wapo…mimi sikukubali tu …..’akasema binti
‘Lakini sasa
utaolewaje na mtu mgonjwa, si unafahamu matatizo yeka, au unataka kwenda kuwa
mfanyakazi wake tu..hutaki kizazi…au ndio mumeshapimana huko maana nyie vijana
wa siku hizi ni hatari, mnajiingiza kwenye mambo makubwa kabla ya umri wenu…?’
akaulizwa shangazi.
‘Ngojeni kwanza…,
unasema una ushahidi na mashahidi…eeh, hebu tumuache atupe huo ushahidi na
mashahidi,… lakini hayo, hayawezi
kubadili msimamo wetu maana tulishakubali, unatuelewa, haya elezea huo upuuzi
wako….’akasema baba.
NB: Naona hitimisho
litakuwa na sehemu mbili, tuwe na subira, tuone sehemu ya pili itakuwaje, je
binti atakubaliwa , …ukumbuke wazazi wameshapokea mahari….
WAZO LA LEO: Wakati mwingine ni
muhimu kuwasikiliza watoto wetu, hasa inapofikia sehemu ya kuchagua ni nani
anayefaa kuwa mwenza wa maisha. Yawezekana, ikawa ni heri kwa wawili hao, yawezekana mwenza
aliyemuona yeye akawa ni mwenza mwema, lakini ni muhimu, wazee kufanya
uchunguzi wa kina, tusikimbilie kuangalia mali, mahari, na utajiri tu wa mwenza
wa watoto wetu, tuangalie yake mambo ya
msingi, maana, ndoa ndio chimbuko la kizazi chema, ndoa ni sababu ya jamii
njema , tukiharibu hapo, tumeiharibu jamii.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment