Mambo yalianza hivyo…
Jamaa akalazwa hospitalini akiwa na homa kali na alikuwa
kama kachanganyikiwa, ikafikia hatua
akapoteza fahamu… na watu waliokuwa karibu naye, walisema alipozindukana alikuwa
akiongea peke yake kama vile anaongea na mtu asiyeonekana , lakini alikuwa akitaja maneno
kama bro na mara nyingine , anasema ….nimekosa nisamhehe bro..ni kama anatubu
hivi, halafu…anaanza kupiga kelele kuwa hataki kufa hataki kufaa…
‘Labda alikuwa akiongea na mzimu wa kaka yake…’nikasema na
docta aliyekuwa naye karibu akasema;
‘Kwakweli sijui mambo hayo,…ya mizimu, zaidi ya hicho nilichokuambia…’akasema docta
na mara akaingia mpelelezi kabla sijapata muda wa kumuhoji vyema huyo docta, …na
kumbe wakati mpelelezi anaingia alisikia yale tuliyokuwa tukiongea na docta na
hakutaka kimpite kitu, kwahiyo moja kwa moja akaanza kwakuuliza;
‘Walikuwa wanaongea nini…?’ akauliza mpelelezi kwa hamasa, na docta akatikisa kichwa kama
kutokutaka kuyaongea hayo mambo, lakini akasema;
‘Kama nilivyomwambia mwenzako, unajua haya mimi kama docta
siruhusiwi kuyaongea, …. sema kwa vile mlivyoniambia
jana, nikaona ni muhimu nimsikilizie tu…, ili muweze kupata hizo taarifa, hebu niwaulize
kwanz, je ni kuhusu mgonjwa tu au kuna jambo jingine, …?’akasema na kuuliza docta.
‘Ni kuhusu mgonjwa….’akasema docta na mimi nikaona hakuna
haja ya kumficha huyu docta, nikasema
‘Kiukweli docta, ni
muhimu sana kwetu kujua chochote kama kaongea,…., maana kuna utata mkubwa, kuna deni….’nikaanza kuongea na mpelelezi
akawa kama hataki kuliongelea hilo, lakini mimi nikawa na malengo yangu
tofauti, nikaendelea kuongea tu.
‘Ni hivi,…kuna deni limetoka benki, na deni hilo lina
ushahidi wote kuwa lilichukuliwa na marehemu,… lakini kuna hali inayotuonyesha
kuwa kuna mbinu zimefanyika, huenda hakuchukua marehemu na huenda huyu mgonjwa
anaweza kuwa na ufahamu nalo…’nikasema
‘Kwa vipi…?’ akauliza docta.
‘Kwanza ni ndugi yake, na pia, yeye ndiye alikuwa mtu wake
wa karibu sana, sasa …kama kweli hakuchukua marehemu , basi tutaweza kuokoa
mali ya marehemu ambayo inatakiwa kuchukuliwa, unaona docta…tuiokoe mali ya mjane
na watoto wake …’nikasema na docta akainamisha kichwa chini kama anawaza jambo.
‘Je aliongea nini….?’ Akauliza mpelelezi
Docta akatikisa kichwa kwa kusikitika, halafu akasema;
‘Kama ni hivyo …nitawaambia kile nilichoweza kukisikia
japokuwa sio sana , maana mtu akizindukana anaweza kuongea maneno hata hayashikiki,
au hata huwezi kuyaelewa vyema…., labda uwe unafahamu ni nini anakizungumzia,….sasa
kama ni hivyo,…oh, inasikitisha sana kama inaweza kuwa kuna mtu kafanya hivyo
ili kuwadhulumu mjane na watoto, inabidi
haki itafutwe hapo…sasa huyu mgonjwa kweli anaweza kusaidia kitu, kwa maneno
hayo tu, au …?’akasema docta na kuuliza
‘Ndio….ndio maana
tunajitahidi kuupata huo ukweli kwa njia yoyote ile…huenda huyu mgonjwa anaweza
kujua lolote, maana hali imetokea wakati tunamuhoji huyu mgonjwa, kabla hajatuambia
mambo yote , huenda anafahamu jambo, …na hasa kwa vile, yeye alikuwa karibu
sana na marehemu….je aliongea nini…?’ akauliza mpelelezi
‘Sasa kwanini hamsubirii akili itulie,…nina uhakika
atawaambia ukweli, kwa vile ni shemeji yake , na ni kaka wa marehemu au sio,…kwani
kakataa kuwaambia ukweli..?’ akauliza docta akionyesha wasiwasi
‘Hapana….ni kutaka tu kujua…kama kuna lolote aliongea, sio
kwamba kakataa kusema ukweli, hapana….je kuna lolote aliongea…?’ akauliza
mpelelezi
‘Nilijaribu kuwa naye karibu kama mlivyonielekeza, na
alipozindukana, mara ya kwanza, na alikuwa bado yupo kwenye marue rue, ya
kuchanganyikiwa..homa ilikuwa haishuki, na
baadaye ndio akaanza kuongea , anaongea peke yake, lakini ni kama
anaongea na mtu….’akasema docta na sisi tukamsogelea docta tusikie hicho
alichokiongea huyo mgonjwa
‘Akiongea na mtu gani…?’ akauliza mpelelezi
‘Alivyotaja, alikuwa anaongea na mtu aliyekuwa akimtaja kama bro…mara ya kwa
mara alikuwa akitumia neno hilo bro, bro..,unasikia bro,…nakuambia bro.. vitu
kama hivyo na walichokuwa wakiongea ni -ni ,…vitu kama mashamba ,mara
nyumba…mara deni….havieleweki, … halafu baadaye jamaa anakuwa kama anaomba
msamaha na mwishowe akawa anapiga ukulele kuwa hataki kufa…..’akasema huyoo
docta.
‘Kwa jinsi ulivyosikia alipoongelea hilo deni, aliongea nini
zaidi,, …?’ akaulizwa docta na docta
akasema;
‘Ndio aliongea akisema kuna deni, kitu kama hicho, …unajua, huwezi kuunganisha zaidi ,ila
nilisikia kitu kama hicho, akisema kuna deni,…linatakiwa kulipwa,… …na alitaja
akisema ni deni lako…ni deni lako bro…, akawa anarudia rudia hayo maneno, deni
ni lako bro, deni ni lako bro, ni lazima liwe lako,…kabla hajaanza kusema
nisamehe, mimi sitaki kufa…’akasema docta.
‘Hapo haijatusaidia,…Dalali yaani huyo mgonjwa anasisitiza
kuwa huyo anayeongea naye ambaye tunahisi ni bro wake,…anasisitiza kuwa deni la
huyo bro wake…, kama ni hivyo, basi, hiyo mizimu inashirikiana na huyo
aliyetaka kudhulumu,…je huyo anayeongea naye alisema nini..?’ akauliza
mpelelezi.
‘Mimi sijui,….maana huwezi kusikia huyo anayeongea naye
anaongea nini,unasikia hicho anachokijibu huyu mgonjwa….’akasema docta.
‘Unaona,….mimi sioni
kama hayo maongezi yake yana umuhimu kwetu,…. ‘akasema mpelelezi akionyesha
kukata tamaa, halafu akanigeukia na kusema.
‘Eti mtu wa mitandao kuna lolote la kuweza kutusaidia hapo…?.’akasema
mpelelezi. na kuniuliza mimi na mimi nikasema;
‘Kama alivyosema docta, huenda mgonjwa aliongea mambo mengi,
na mambo hayo yangeliweza kutusaidia lakini alikuwa akiongea bila mpangilia au
kwa sauti ya kutoweza kusikiwa vyema…., na kwa vile docta hakuwa na dalili ya
nini tunakitafuta,kwahiyo hakuweza kuzingatia …’nikasema.
‘Nikweli….’akasema docta
‘Kwahiyo, mimi sizani kama maelezo yake yatasaidia kitu, mtu
wa kuweza kutusaidia ni yeye mwenyewe muhusika…labda tukuulize docta kama kuna
jingine zaidi uliweza kulisikia, zaidi ya kutaja deni, mashamba na nyumba, hakuna
jingine aliweza kuliongea zaidi ya hayo…?’ nikauliza
‘Ni hivyo hivyo tu ninaweza kusema,,nilisikia akizungumzia nyumba ipo, nyumba ipo…italipa deni kitu kama hicho, na nilisikia akisema mashamba
tumeuza…kitu kama hicho, na …nahisi ni hivyo tu, mhh, kwani, labda
niulize,kwani huyu mgonjwa ana kosa lolote, mnamshuku kwa jambo gani, kuwa huenda anahusikana na hilo deni mlilosema
au kuna jambo jingine zaidi ya hilo…?’ akauliza, na hakuna aliyetaka kumjibu na
mimi nikasema;
‘Kwani kuacha kuongelea mashamba, deni na nyumba kuna kitu
kingine ulikisikia akikiongelea huyo mgonjwa, ambacho kinaweza kutusaidia kwa
namna moja au nyingine, kwa kutaja tu sio kwa kuleta maana, labda alitaja nini
, neno gani , au kauli gani…?’ nikamuuliza.
‘Mhh….sikumbuki,…kama kuna jambo aliongelea…mmmh….., hapana
siwezi kuunganisha na kuleta maana yoyote, kama ilivyo hiyo ya deni….shamba,
nyumba…, ndio hivyo…nimeweza kuunganisha na kuweza kuwaelezea kihivyo…, mengine
..mmmh, hayana maana hayaunganishiki….siwezi kusema kitu…..’akasema, lakini
mimi nikahis kuna kitu anaficha, lakini sikuelewa ni kwanini!
‘Je hukuweza kusikia kauli kama ajali, kitu kama hicho….?’
Nikauliza na mpelelezi akaniangalia kama vile hakutaka niliulize hilo swali, na
docta akasema;
‘Ajali mhh, ..ajali,ajali…mmmh….mhh, sikumbuki k neno…ooh,
ajali, mhhh….. ndio…nimekumbuka, aliongelea neno kama hilo..hakutamka neno,
ajali,…alitamka akisident…. ndio alisema
neno hilo …kitu kama hicho, kweli yawezekana alikuwa na maana hiyo
ajali, alitamka neno ‘accident,…’ .na
ndio akaanza kupiga ukelele wa kuwa yeye hataki kufa, asamehewe…..ni hivyo tu
ninaweza kusema….’akasema docta
‘Kwahiyo hiyo ya kusema asamehewe, au hataki kufa, inatokana
na maneno hayo ya ajali, yaani alipoanza kuongelea maneno ya ajali, au
inatokana na hilo deni kwa jinsi ulivyomsikia….?’ Akauliza mpelelezi.
‘Siwezi kujua zaidi hapo…maana niliunganisha hayo maneno kwa
kukumbuka na siwezi kukumbuka alitamka wakati gani, nimeweza kuyasema hayo kama
kukumbuka kuwa alitamka hivyo,,…..siwezi
kuwasaidia zaidi ya hapo samahani sana…’akasema docta, na kabla hatujamuuliza
swali mara akaingia mama mjane kukawa na kusalimiana, tuliona mama mjane
akimsalimia huyo docta kama shemeji, ni kama wanafahamiana.
Yule mama mjane ndio akaanza kuelezea kuwa yeye alipitia kwa mgonjwa kwanza;.
‘Mimi nilipitia moja kwa moja kumuona mgonjwa kwanza…sikujua
kuwa nyie mpo huku na wakati nataka kuondoka, nesi akaniambia mpo huku, nikaoa
nije niwasalimie, vipi kwani kuna jipya maana mimi nataka kuondoka,…?’akauliza
mama mjane huku akionekana ana haraka.
‘Unasema ulipitia moja kwa moja kumuona mgonjwa, je uliweza
kuongea naye..japo kuwa kidogo?’ akauliza mpelelezi
‘Mhh, mwanzoni kwa shida, … ‘akasema na docta akakunja uso
kama hakutaka hilo na mpelelezi akauliza
‘Mwanzoni kwa shida, una maana gani…?’ akauliza
‘Ndio….nilipofika alikuwa kama kanitambuaa akawa anahangaika kuniambia jambo, alikuwa
akitetemeka kama mtu mwenye ……kama wale wagonjwa wa madawa ya kulevya
wanavyokuwa wakikosa dawa zao na wanahitajia
wazipate, si mnajua wanavyopata shida, basi ndio hivyo,,…..na baadaye
akatulia, tukaongea naye kwanza kwa shida, na jinsi muda ulivyozidi ndio akaanza
kuongea vizuri….’akasema mama mjane.
‘Kwahiyo sasa hivi katulia , joto halipo tena, na sisi tunaweza
kuongea naye…eti docta?’ akauliza mpelelezi na docta akasema;
‘Hapana , hapana,hamuwezi kuongea naye kwa hivi sasa…,na
…hata shemeji hapa kafanya makosa kwenda kumuongelesha ..hakutakiwa kuongea na
mtu mpaka mimi nione kweli anastahiki….’akasema docta
‘Waliniambia manesi hivyo,… lakini kilichonifanya niweze
kuongea naye, ndio hivyo, alikuwa kama anataka kuniambia jambo,…..’akasema mama
mjane.
‘Sawa …imeshafanyika hivyo, hilo ni kosa, sitaki lijirudie
tena, nyie hamuwezi kuongea naye mpaka nionane na huyo mgonjwa, nihakikishe
kama kweli anaweza kuongea na watu, ….’akasema docta akitaka kuondoka, na mimi
nikamgeukia mama mjane na kumuuliza;
‘Dada unasema mgonjwa
kwasasa, …anaongea au sio, sio kama ilivyokuwa awali, kwahiyo
kifupi sasa hivi anaweza kuongea na mtu
ukamuelewa anachoongea …?’ nikauliza na docta akasimama kusikiliza , hakuondoka
kwanza!
‘Yaani, kaka, ukifika sasa hivi huwezi kuamini kuwa ndio
yule alikuwa kama kachanganyikiwa,…..’akasema huyo mama Mjane na wote tukaangaliana
kwa mshangao, na kila mmoja alikuwa na hamasa ya kwenda kumuona.
‘Basi naona hali imerejea kama awali…docta tunaweza kwenda pamoja,
tukamuone tu, hatutamuuliza maswali, ni kumuona tu….na labda yupo kwenye hali
nzuri, huenda tunaweza kuongea naye kwa
leo….’akasema mpelelezi akiwa na hamasa ya kwenda kumuona, na docta akasema
‘Kwakweli kwa leo haiwezekani kuongea naye….huyo ni mgonjwa
wetu…, na kama mlivyoona , ndio katokea kwenye hali hiyo ya kuchanganyikiwa…alipoteza
fahamu…, anahitajika kufanyiwa uchunguzi kwanza,….naombeni mnielewe…’akasema
docta na sisi tukawa hatuna la kufanya, na docta akaendelea kusema
‘Ngojeni kwanza nikamuangalie mimi mwenyewe kwanza…’akasema docta na kuondoka kwa
haraka, na sisi tukabakiwa pale tukiongea mambo mengine,..baadaye tukaruhusiwa
kwenda kumuona..na tulimkuta kakaa kitandani akisoma gazeti, huwezi
kuamini kuwa ni yule mtu aliyekuwa
kachanganyikiwa. Na alipotuona tu akaweka gazeti pembeni.
*********
Mgonjwa alipotuona tu, akaweka gazeti na kutuangalia kwa
hamasa, akasema;
‘Karibuni …mimi sijambo, nataka niondoke haraka, kuna mambo
yangu yanalala…..si unajua tena mimi ni jembe la familia mbili,…na nyie ndio
mnasababisha haya yote, haya isaidieni familia yangu, au ndio mumekuja
kunisumbua kwa maswali yenu tena….’akasema na sisi tukaangaliana tukitaka tuanze
kumuhoji, lakini docta akatuwahi kwa kusema;
‘Kwahivi sasa siwezi kuwaruhusu kumhoji, ….anahitajia muda
kidogo, hajakaa sawa….’akasema docta
‘Basi mimi naondoka nitarudi baadaye kuna watu nimesikia
wamekuja huko nyumbani sijui ni akina nani ngoja nikawasikilize …..’akasema
mama mjane akionyesha kuwa na wasi wasi
‘Labda ni watu wa kupiga mnada nyumba, waambie ….ninakuja..ni
lazima nionane nao kwanza….’akasema Dalali, akiwa kama anataka kujiandaa
kuondoka!
‘Sawa… tukikuhitajia tutakuambia, maana hata sisi haina haja
ya kuendelea kukaa hapa, kama alivyosema docta, ila hatuwezi kusubiria zaidi, ni muhimu
tukaongea naye haraka iwezekanavyo…’akasema mpelelezi
‘Huyo kwa ujumla mungemuita yule mtaalamu wake….’akasema mama
mjane akimuangalia shemeji yake akiwa anatafuta kitu kwenye kikabati cha hapo
hospitali, lakini hakumuuliza anatafuta nini.
‘Mtaalamu wake yupi huyo? ….’akauliza docta
‘Kuna mganga mmoja wa tiba asilia, ndiye wanamuita mtaalamu,
…’akasema mpelelezi.
‘Ok…lakini kwa jinsi nilivyomchunguza haina haja ya kuonana
na huyo mtu, yupo safi, joto sasa lipo safi, na akili yake imeshaanza kukaa
vyema, tunahitajia muda kidogo wa kumchunguza kwanza halafu tutakuambieni kama
mnaweza kumuhoji,…’akasema na kutulia kidogo halafu akauliza
‘Na mnasema anahitajia mtalaamu wake..huyo ni docta nani,…ni,
mtaalamu wa nini…?’akasema docta akimwangalia mdada, halafu mimi, halafu
mpelelezi, na mpelelezi akasema;
‘ Ooh, hawa watu bwana, wanahisi kapatwa na mashetani, na
watu wanaoweza kushughulikia hayo mambo wanaitwa wataalamu, sasa kwa huyo wanayemuita mtaalamu wake,
sizani kama anaweza…’akasema mpelelezi akitikisa kichwa kama kukataa jambo
‘Kwanini,….! Maana ndiye alimsaidia hata mtoto, akizidiwa ndiye aliweza
kumtibia…na hayo ya mtoto naona kama yanafanana na …..na tatizo la
shemeji…’akasema mama mjane.
‘Ni kutokana na hali aliyo nayo huyo mtaalamu kwasasa…hali
yake ni mbaya sana, kalazwa hospitali ya kwetu, chini ya uangalizi mkali…huyo hawezi kufanya
lolote kwa hivi sasa….’akasema mpelelezi
‘Na yeye ana matatizo gani, ni kama haya…?’ akauliza docta,
na mpelelezi akasema;
‘Huyo ana matatizo yake mengine, tuachane naye …..’akasema mpelelezi na mama
mjane akauliza;
‘Kwani yeye litokeaje
mpaka akalazwa, unajua mimi sijaelewa bado,mambo yamekuwa mengo kichwani hapa
nilipo nipo nipo tu…?’ akauliza mama mjane.
‘Kilichomponza ni huko kutaka kutoroka kwake rumande , na cha
ajabu alikuwa bado hajafunguliwa mashitaka yoyote aliitwa tu kwa ajili ya
kuisaidia polisi,..mwanzoni alitoa ushirikiano mnzuri tu alipoulizwa maswali,…baadaye
akaambiwa hawezi kuondoka, kiusalama,….akatakiwa kuwekwa rumande, ,..hapo ndipo akawa mkali kweli….’akasema mpelelezi.
‘Jela sio nzuri jamani…hata kama ni hiyo mnayoita
rumande, ina maana kutokana na hilo ndio
akazidiwa, ndio akachanganyikiwa na yeye…?’ akauliza mama mjane.
‘Yeye sio tatizo la kuchanganyikiwa, tatizo, alijeruhiwa na risasi akitaak
kutoroka, …na kabla ya hapo alileta fujo kweli…, Ilibidi polisi wafanye kazi ya
ziada ya kumgongagonga kwenye magoti
mpaka akalainika…’akasema mpelelezi.
‘Sasa usiku ndio sijui aliwafanyia nini walinzi, kwani walinzi wote walikutwa wamelala fofo, ile ya
kutokujiweza. na ilikuwa ni bahati tu mkuu wa kituoa aliweza kupita hapo
kituoni usiku…., na ndio muda huo huyo jamaa alikuwa akitoka mlangoni, akitaka
kutoroka,…aliwezaje kufungua mlango, haijulikani, maana mlango ulifunguliwa ….hana
ufunguo….sasa wakati anatoka mlangoni akaonekana na mkuu,…akaamrishwa asimame
hakukubali akaanza kukimbia ndio, akaipigwa risasi ya mguuni,…’akasema
mpelelezi…..
‘Sasa ilitarajiwa labda
kwa kujeruhiwa hivyo atasimama, lakini wapi akawa anakimbia na mguu mmoja,
wanasema alikuwa kama anapaa, akitua kwa mguu mmoja akiinuka anaruka hewani na
kuwa kama anapaa, na kwa muda mfupi akawa keshatoweka…lakini sasa alipoteza
damu nyingi sana, na sehemu aliyopigwa
risasi imeanza kuoza…’akatulia
‘Mbona ni kuwa muda mfupi tu,kwani hakupatiwa matibabu ya
haraka…?’ akauliza docta
‘Hata madakitari wa pale wanashangaa, maana haikuwa sehemu
ya kuoza,…ndio akahamishiwa hopitali kuu, na huko ikaonekana wakiacha …italeta matatizo,maana
ilishaonyesha dalili za kansa….ikabidi amri itolewe mguu ukatwe..’akasema
mpelelezi.
‘Mguu ukatwe…..’ilikuwa sauti ya Dalali..ambaye kwa muda
wote huo alikuwa kimia, na alikuwa kama kajiandaa kuondoka, kwa jinai
slivyokuwa kakaa pale kitandani.
‘Ndio umekatwa….ungeachwa ingeleta madhara zaidi…..’akasema
mpelelezi.
‘Unajua huyo jamaa ni mbishi sana, alipoambiwa hivyo akagoma
akasema yeye , hataki, atakwenda kujitibu yeye mwenyewe, ….ikabidi itumike njia ya kumpoteza fahamu ili
mguu ukatwe,….mguu umekatwa, alipozindukana kuona hiyo hali, mguu amekatwa…..
ndio hapo na yeye akaanza kuchanganyikiwa, akawa hashikiki, anasema; mumenia, mumeniua…….mpaka akapigwa masindano ya
kumtuliza, na kila akizindukana, ni kelele, mumenia mumeniua… …’akasema
mpelelezi.
‘Mungu wangu kweli wamemuua…kumbe
ndio maana, ….alikuja kuniaga,…..oh, masikini mtaalamu, ndio kwaheri
hiyo…..sasa ni zamu yangu, hapana, mimi sikubali…’tulisikia sauti kutoka
kitandani kwa Dalali, ilikuwa sauti ya
majonzi
Tuliposikia hivyo tukageuka kumuangalia, alikuwa kakaa ile
ya kutaka kusimama, alikuwa akitutizama,
kwa macho yakuonyesha ana wasiwasi, na docta akamuuliza;
‘Vipi….wewe tulia ,lala ….’akasema docta
‘Mimi sijambo, ….msiwe na shaka kabisa na mimi ,ila hiyo
habari ya mtaalamu ndio imenishtua kidogo, kama wamemkata mguu, wameshamuua,
wangelimuachia yeye mwenyewe angejua cha kufanya, wameshamuua mtu wangu…’akasema
Dalali, na mimi nikajikuta nikisema;
‘Umeonaeeh Dalali, …unajua ni kwa nini hayo yamemtokea hayo,
, ….’nikasema.
‘Si ndio hivyo…kapigwa risasi…na …kiutaaratibu mtu kama yule
hatibiwi hospitalini, ikifanyika hivyo, anapatwa na mambo kama hayo….angeachiwa
angelijua mwenyewe jinsi ya kujitibu…’akasema
‘Dalali…ujaribu kuelewa, hatutakiwi kukusumbua, lakini hiyo
ni kutokana na hiyo mikono iliyoinuliwa juu,….nimeshakuambia, mtu akiinua
mikono juu akasema namuachia mungu, ogopa sana…. ogopeni sana duwa ya mwenye
kudhulumuiwa, ’ nikasema na Dalali akabakia kimia akiwa kama kazama kwenye
mawazo, mpelelezi akamuuliza
‘Dalali vipi unajisikiaje ?’ akaulizwa
‘Mimi sijambo….ile dawa aliyonieletea shemeji imefanya vitu
vyake….unajua niwaambie ukweli mambo
mengine sio ya hospitalini, nyie hamjui tu, mnaweza kuua mtu,…’akasema akijinyosha, na shemeji yake akageuza kichwa
kuangalia pembeni , kama kuona aibu, kumbe alimletea dawa huyo jamaa bila ya
sisi kufahamu. Na huenda alifanya hivyo, ili madakitari wasijue, sasa Dalali
karopoka, hapo ikabidi mjane ajitetee na kusema;
‘Huyu naye bwana…ilikuwa siri sasa sio siri tena….unajua niliona ni matatizo kama yale ya mtoto, ndio
nikaamua kumletea hiyo dawa, na hiyo dawa aliileta yeye mwenyewe kwa ajili ya
mtoto, na nilipomletea alipoiona tu….akaitambua, ndio akafanya kama alivyokuwa akimfanyia mtoto,
akapiga chafya na kusema,;
‘Hapa sasa basi nimepona….ahsante shemeji yangu umeniokoa,sasa mapambano yanaendelea…alisema
hivyo…..’akasema shemeji mtu akiigiza sauti ya kidume
‘Mapambano…!?’ akauliza mpelelezi akimuangalia Dalali
‘Ndio mapambano je…’akasema Dalali na kuendelea kusema
‘Ni mapambano ndio ya kuhakikisha kile nilichokianza
kinakamilika,….deni lilipwe, siwezi kukubali hii hali iendelee tena, kaka yangu
anapata taabu huko alipo, na sisi tutakufa mmoja mmoja, ndio hivyo kaanza
mtaalamu, sijui atafuata nani…’akasema Dalali
‘Lakini mtaalamu hajafariki…bado yupo hai na yupo
hospitalini anapatiwa matibabu, japokuwa hali yake sio nzuri….’akasema
mpelelezi
‘Nyie hamjui tu…huyo ndio kwaheri, na hao waliomkata mguu
ndio wamemuua, wangelijua wasingelifanya hivyo….na hata mimi sitakubali,… hapa
tu mnanipotezea muda, natakiwa nikawahi kuweka mambo sawa,…hili sasa
linahitajia nisafiri, kwa mabingwa, vinginevyo….na kwanini mumenipiga hayo
masindano yenu, mumeharibu, hata sijui nitafanya nini….’akasema.
‘Sasa tulia,…kama ulivyosema upo kwenye mapambano , ni
muhimu uwe na afya njema…una kazi mbele yako inayokuhitajia uwe na afya, …..’akasema
docta.
‘Kazi gani…?’ akauliza Dalali, akimwangalia docta na docta
akawa kama anamkwepa kumuangalia usoni, na kusema;
‘Wewe tuliza kichwa chako, huoni hawa jamaa zako
wanahitajika kukuhoji, lakini siwezi kuwaruhusu mpaka uwe umatulia, uwe na afya
njema…’akasema docta.
‘Hawa hawanitishi, wameshindwa, na watazidi kushindwa….hawana
jipya, mimi nilishawaambia waende benki, …lakini bado wananing’ang’ania
mimi,haya, …mimi nipo tayari anzeni hayo maswali yenu, maana mnaniuliza
utafikiri tupo mahakamani…hahaha, hamniwezi kabisa…’akasema akikaa kitandani ,
lakini tulishangaa alivyokatisha kicheko na kugeuka kushoto na
kulia….anavyofanya unaweza kufikiria anaigiza!
‘Hapana sio leo, hawaruhusiwi kukuuliza hayo maswali yao hii
leo…wewe unachotakiwa ni kutuliza kichwa chako, …..cha muhimu kwasasa ni afya
yako….’akaambiwa.
‘Mimi nia na lengo
langu ni kuhakikisha hilo deni limelipwa…hicho ndio cha muhimu…shemeji unasema wale
watu wa mnada wamefika, ….au sio?’ Akauliza akimgeukia shemeji yake, na shemeji
yake alibakia kimia,halafu akasema
‘Unajua sio kwamba nang’ang’ania hilo jambo..hapana…sababu kubwa, ni kuwa ,…kiini
cha yote haya ni hilo deni, na tusipofanya hima kulilipa hilo deni, mzimu wa kaka
utakuwa ukitusumbua kila siku, na kama
umeshaanza kumtafuna mtaalamu….’hapo
akasita na kugeuka huku na kule halafu akasema
‘Mnasema mtaalamu…yupo wapi…huyo ndio basi tena, ….sasa,
ndio kazi imeanza, ukitoka hapo sijui utakuja
kwa nani, wasiwasi wangu ni kwa hao watoto, maana ndio damu yake,….sisi sijui
kwanini, unatufuata… mimi najua imenitokea tu kama kunikumbushia, lakini kwa
mtaalamu,….hata sijui kwanini…’akawa kama anajiuliza mwenyewe.
‘Labda alishirikiana na hao wanaotaka kumdhulumu marehemue…’nikasema
na jamaa akaniangalia na kusema;
‘Sio hivyo, …mara nyingi vitu kama hivyo vinafuata damu
yake,…ndio maana uliona mtoto alianza kuumwa, ….wengine kama mke, kaka, ni kama
kukumbushiwa tu…mnielewe lakini,….mimi niliambiwa haya yote na mtaalamu sio
mimi, …oh, na yeye ndiye angeliweza
kunisaidia katika mambo haya, siyataki lakini utafanya nini, sasa eeeh, ndugu
zanguni … itakuwaje, …’akasema akituangalia;
‘Lakini Dalali, hebu
tuambie ukweli, kuna nini…unajua sisi lengo letu ni hilo, tulimalize hilo
tatizo, na ili tulimalize hilo tunahitajia ushirikiano wako,ili kulitambua hilo
deni vyema, hatuwezi kukubali kuwa ni deni la kaka yako, kwasababu mpaka sasa
kuna kila dalili kuwa hilo deni sio lake, sasa kama sio deni la kaka yako, ni nani yupo
nyuma ya hilo, lilikuwa ni deni la nani….’tukasema kama kumuuliza.
‘Nyie ndio mniambie hilo deni ni la nani…kama sio la kaka,…na
swali kama hilo kweli ni la kuniuliza mimi, …hebu tumieni akili, mlitakiwa
kwenda kuwauliza benki,..au sio…kwa vile huko kuna ushahidi mnashindwa
kuwaingia mnataka kunisumbua mimi,…hilo deni ni la kaka…ni lake…’ akasema
akisimama lakini alionyesha kuwa ana wasi wasi kwani alivyotamka hivyo akawa
anageuka huku na kule kwa mashaka.
‘Sasa unataka kwenda wapi…?’ akaulizwa na docta, Doacta akatuashiria kuwa jamaa bado
hajatulia.
‘Mimi nataka kuondoka, siwezi kulala hapa….siwezi kabisa
kukaa hapa hospitalini, kunanukia kifo,….mimi naondoka kabla huyu jamaa
hajafika tena …’akasema
‘Jamaa gani …’tukamuuliza na akawa anageuka huku na kule
kama ana wasiwasi fulani…
NB Sehemu hii iliishia hapo kwani tuliondoka, tukamuacha na
dakitari wake, na tuliporudi mambo yalikuwa mengine huwezi amini…
WAZO LA LEO: Mwenyezimungu ana namna nyingi za kutukumbusha madhambi yetu ili tutubu, lakini wengi wakikutwa na mambo hayo, wanajifanya kama sio yenyewe, ...zaidi ni kujipa matumaini kuwa bado maisha yapo, ...ndugu yangu kumbuka haya maisha anayejua lini kesho ni muumba mwenyewe!
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment