Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, August 17, 2015

RADHI YA WAZAZI-30



Muendesha mashitaka alielezewa kuhusu kesi yote, japokuwa alishaongea na mpelelezi, kabla,... na jinsi kesi yenyewe ilivyo, na ni mmoja aliyewahi kufika eneo la tukio, siku kulipotokea hayo mauaji, kwahiyo alikuwa ana ufahamu kiasi wa hiyo kesi, alichokuwa akihitajia zaidi ni ushahidi ...

Basi wakaanza mazungumzo, sasa akiwemo muendesha mashitaka, ambaye alikuwa muulizaji maswali hapa na pale...

‘Mara nyingi kesi zenu zinakuwa na utata, ...kwasababu mnakuwa na mambo mengi ya kibinafsi, na wakati mwingine mnakuwa hamkubaliani kwa baadhi ya mambo....’akasema muendesha mashitaka

‘Ukisema mambo yetu ya kibinafsi una maana gani..?’ akauliza mkuu

‘Inawezekana kukawa na mshitakiwa lakini kwasababu za kibinafsi mkaanza kusema hiki usiseme hiki usifanye, mambo kama hayo huwa yananipa wakati mgumu....’akasema

‘Sasa unataka rufanye nini, wewe siunatakiwa kuwafuata maelekezo ya mteja wako, ilimradi yanaendana na sheria...’akasema mkuu

‘Mimi niwaambie ukweli kama kweli mnataka hili tatizo liishe, niachieni mimi na huyu mpelelezi,msiingilie kitu hata kimoja...tutalimaliza hili tatizo kabisa....’akasema muendesha mashitaka

‘Ni lazima niingilie, nikiona ni jambo linalogusa taifa, linalogusa masilahi ya taifa, sio mimi napanga haya...,wakati mwingine napata shinikizo toka juu,kwa masilahi ya taifa...’akajitetea.

‘Ok,sasa hebu niambieni,ni nini kusudio lenu,hapa...mpaka sasa tuna watuhumiwa wakubwa wawili, tukiacha hawa washitakiwa wengine,...je hawa washitakiwa wakubwa wawili wana tatizo, kuna kikwazo kwao, kuna masilahi ya taifa ...?’ akauliza

‘Mimi sioni kama kuna tatizo hapa mkuu...,kwasababu ushahidi wote tunao,  ....kama nilivyokuonyesha na sasa ni kibali tu cha mkuu hapa...kwangu nimemaliza kazi....’akasema mpelelezi

‘Kwahiyo kumbe mlishaongea na kuonyeshana kila kitu, sasa hiki kikao kina umuhimu gani...?’ akauliza na wenzake wakamuangalia wakionyesha mshangao.

‘Ok, hebu nifafanulieni, wapi mlipofikia...?’ akasema mkuu alipoona hiyoo hali.

‘Mkuu, unakumbuka ulimwambia msaidizi wako mambo yakiwa tayari aendelee, na ndicho tulichkifanya, sasa ukisema kama tumeshaongea hiki kikao kina maana gani.....ni kama unatulaumu kuwa tumefanya mambo wakati wewe haupo au....’akasema mpelelezi

‘Ok, nimeshawaelewa....ninachoshangaa ni kuona msaidizi wangu hayupo, sijui ana dharura gani hajanipigia simu, sijaongea naye....lakini mnielewe, ilibidi nifike kabla kesi haijaanza, kwani kuna mambo natakiwa kuyasikia, kuna wawezekaji, kuna masilahi ya taifa,.....’akasema

‘Mimi naona ushahidi upo kamili,..na kama ulivyoona yote ni mambo yapo wazi, sizani kama yanagusa masilahi ya taifa,...ni kero kwa taifa...watu kama hawa wanastahiki adhabu kali, ili iwe ni fundisho, na .....hawa wahamiaji,......’akasema mpelelezi, akiendelea kutoa ushahidi alioukusanya...

*********

‘Umesema mmoja wa washitakiwa ni huyu jamaa wa mitandao, huyu jamaa amekuwa akiisaidia sana serikali, amekuwa akiwaajiri vijana,...nashangaa sana kusikia kuwa na yeye ni jambazi....hebu niambieni ujambazi wake upoje..?’ akauliza mkuu akiwaangalia wenzake

‘Kwa nje ndivyo anavyoonekana, na ni kweli ana kampuni kweli inahusika na mambo ya mitandao,na anauza vifaa mbali mbali vya komputa na mitandao..,ni kweli amekuwa msitari wa mbele kusaidia vijana, hasa kwenye ajira...’akaelezea

‘Sasa hamuoni kuwa huyu ni mtu muhimu kwa maendeleo ya taifa?’ akauliza

‘Lakini kiundani anakiuka sheria za nchi, ni fisadi, na kama unavyona kwenye ushahidi, yeye anashughulikana na mikakati ya wizi... katika uchunguzi wetu tumelibaini hilo kwa asilimia kubwa.....’akasema

‘Ngoja kwanza, ..unasema yeye ni fisadi,...pia ana mikakati ya wizi, lakini haionyeshi moja kwa moja kuhusika na kesi ya mauaji ...tunachoangalia hapa ni hii kesi ya mauaji, kwanza’ akasema akionyesha kumtetea mshitakiwa huyo.

‘Huyu mshitakiwa anahusika,kama utakavyozidi kuona kwenye ushahidi wetu....’akasema

‘Una uhakika na hilo....sio kwamba namtetea,...mmh, sasa hii ni hatari...nilimuamini sana huyu mtu, na kwenye kikao huko kwa wakubwa ni mmoja ya watu, niliowapigia debe, oh, sasa, ok, tuendelee...’akasema mkuu

‘Mkuu huyu mtu ni mjanja sana, yeye anadai huwa yeye hujihusisha tu na mikakati ya uzalishaji, au mikakati ya biashara,... kuacha utaalamu wa mitandao na mawasiliano, kwahiyo ukifika kwake, anakuwa na vitengo viwili, utaalamu wa mitandao na komputa,...hili lipo wazi....

‘Lakini ana shughuli nyingine,...mikakati ya biashara, kama anavyoiita, sasa hapa kwenye mikakati ya kibiashara kuna mambo mengine yaliyojificha ndani yake kutegemeana na wewe uliyefika kwake...’akasema

‘Kutegemeana .....! Sasa mumegunduaje kuwa anahusika na mikakati ya ujambazi, mara ufisadi na tena kuhusika na haya mauaji....?’ akaulizwa sasa akikuna kuna kichwa.

‘Ilikuwa kazi ya ndani kwa ndani,...mwanzoni tulipata shida sana, lakini tukaja  kupata msaada kutoka kwa  yule mpelelezi,... wa kujitegemea,...ilibidi tumtumie huyu mtu’akasema

‘Na huyu mpelelezi anahusikaje, na y eye ni mmoja wa washitakiwa....?’ akaulizwa

‘Hapana, ila tulimtumia tu....yeye sio miongoni mwa washitakiwa, atakuja kuwa shahidi muhimu mahakamani, ikibidi....’akasema

‘Ikibidi,....? Ok endelea,...’akaambiwa

‘Kwa kumtumia huyu mpelelezi,ndiye aliyetupa njia mbadala ya kuja kumnasa huyu mtu,...huyu mpelelezi tulikuwa tunamshuku kwa makosa mbali mbali,...tulimuhusisha sana na uharabifu wa amani, na harakati hizo, lakini alikuja kutuonyesha kuwa yeye sio chochote, kuna mtu ambaye hatujamshuku, na ni hatari zaidi.....’akasema

‘Kwahiyo mumefanyaje ili akakubali kuisaidia polisi, maana mara nyingi  huyu mpelelezi wa mitaani, anakuwa hapendi kushirikiana na polisi, anasema polisi ilimuasi, ilimsaliti,....?’ akaulizwa

‘Tuliamua kumshirikisha kinamna, tulimuahidi kuwa leseni yake atarejeshewa, unajua tulishaisimamisha leseni yake kutokana na yeye kuhusishwa kwenye mambo mengi ya kijambazi..., na kwa vile alikuwa hana kazi kwa muda, njaa imembana, akakubali kushirikiana na sisi, na jambo moja likafichua jingine....’akasema

‘Kwa vipi?’ akauliza

‘Tulimpa hiyo kazi ,kama kumuajiri....kwa makubaliano ya kuja kumlipa,...ilibidi tufanye hivyo,ili tupate undani wa hilo kundi,....na imetusaidia sana, na nina uhakika mwisho wa siku tutalimaliza hilo kundi na huyu jamaa naye tutamdhibiti kabisa, kwa vile kila sehemu sasa tuna watu wetu....’akasema

‘Kwahiyo akaweza kuongea na huyu mtaalamu, au huyu mpelelezi aliwezaje kuwasaidia hadi mkagundua kuwa huyu mtaalamu anahusika na ujambazi, ufisadi na hata haya mauaji...?’ akaulizwa

‘Ilibidi tumuachie huyu mtu, afanya anavyojua yeye, na huku hajui kuwa kuna watu wetu wapo nyuma yake  wakimfuatilia, ...na huyu mtu,hakufahamu kuwa tumemtegea, tulishagundua kuwa huyu mtu haaminiki, ....kwa tamaa zake anaweza kutuficha mambo...tukamtegea vyombo vya kunasia matukio, kila anapokwenda tukawa tunapata anachokifanya...’akasema mpelelezi.

‘Huyu mtu una maana mpelelezi, au sio, je hakuweza kuligundua hilo....?’ akauliza

‘Hakuweza, siku hizi mkuu, kuna utaalamu wa kila namna, haina haja ya kuweka vifaa vikubwa, haina haja ya wewe kuwekewa kitu kikubwa, na ndivyo tulivyofanya kwa huyu jamaa, na pia tukaweka watu wetu kwenye mitandao ya simu....’akasema

‘Mitandao ya simu...?’ akauliza

‘Ndio mkuu,  simu siku hizi zimekuwa ni  sehemu muhimu ya kupata mambo yanayoendelea, na ni rahisi sana kufuatilia kila kitu,...hizi simu zenye mitandao. 

Tunazokuwa nazo majumbani,...zinafichua kila kitu kinachofanyika tukitaka kukufuatilia, kama utakavyokuja kuona kwenye ushahidi wetu huu mkuu

‘Ok,...kazi nzuri,ehe...kabla sijaona huo ushahidi zaidi....,hebu naambieni kuhusu huyu mtaalamu, maana mimi nilikuwa namuamini sana,imekuwaje kujiingiza kwenye haya magenge....?’ akauliza

‘ Ni kweli ni mtaalamu sana, alifaulu masomo yake ya komputa, na mitandao, katika ngazi ya hali ya juu,na alipomaliza  masomo yake chuokikuu, alikuwa na malengo ya kupata kazi nzuri, kwenye makampuni makubwa,lakini ikawa sio bahati yake....’akasema

‘Mhh, kama vijana wetu...’akasema mkuu

‘Huyu mtu, yaani mtaalamu, alihangaika sana kutafuta kazi, lakini kila alipopata, ikawa halipwi kama anavyotaka yeye, na kunatokea muda, anakosana na waajiri wake, anaachishwa kwa sababu hizi na zile....na sio kwamba ni mbaya wa kazi, kazi anaweza sana,lakini unajua tena waajiri wengine, hawataki kumuona mtu anajifanya anajua sana zaidi yao....’

‘Baadaye huyu mtaalamu akakutana na jamaa mwingine, huyu jamaa ni mtundu wa mitaani, yeye hajasoma sana,...aliishia vyuo vidogo vya ufundi,  lakini ana kipaji cha ufundi, hasa kuhusu komputa na mitandao...

‘Mkuu, kama huyu mtundu angelisoma zaidi huenda angelikuwa mkali zaidi ya huyu mtaalamu, lakini ubaya wake hapendi shule..au nikutokana na hali za wazazi wake hawakuwa na pesa za kumsomesha zaidi...

‘Huyu mtundu, ndiye aliyekuja kujenga sumu kwa huyu mtaalamu,...hutaamini, mtaalamu na usomi wake, alikuja kugundua...lakini ni baadaye kuwa rafiki yake alikuwa na maana kubwa kwake....’

‘Huyu mtundu yupo wapi kwa hivi sasa....?’ akaulizwa

‘Huyu alikuja kukamatwa na kushitakiwa, ndio ni yule aliyeshitakiwa kwa makosa mengi likiwemo la mauji, yaliyotokana na biashara ya mlungula(blackmail),...kwa hivi sasa yupo anatumikia  kifungo,...’akasema.

‘Yawezekana historia ikajirudia,...’akasema muendesha mashitaka na mkuu akatikisa kichwa kama kukubali.

‘Ni kweli yawezekana,...unajua hawa marafiki walipokutana, kipindi hicho, huyu mtundu ndiye aliyemshawishi mtaalamu kuwa haina haja ya kusumbuka na ajira, alimwambia hivyo, kwani yeye alikuwa na uzoefu wa mitaani, kazi za hapa na pale za kujiajiri alizijulia, na maisha kwake yalikuwa hivyo...

‘Unajua wewe ni ajira tosha,utaalamu ulio nao, huhitajiki kusumbuka,...wewe unaweza kujiajiri....’akashauriwa na mwenzake wakati wanaongea.

‘Kujiajiri, ni kazi kubwa sana,sina mtaji, sina akiba yoyote, pesa niliyokuwa napata ni hand to mouth...,hilo ndilo tatizo ‘akasema mtaalamu.

‘Huhitaji mtaji mkubwa kwa sasa...kwanza ni kuanza kutengeneza kile kisichohitajia pesa,  na kama ni vifaa, atanunua mteja...na kama ni vifaa vingine mimi ninavyo, tutasaidiana kidogo kidogo, ...wewe nitakuelekeza, usiwe na wasiwasi...’akaambiwa

Na kweli akavutika na hilo wazo, japokuwa alikuwa na wasiwasi mkubwa, ....yeye alisomea kuajiriwa, na ndio lengo yakena lengo la wasomi wengi....’akasema.

‘Huyu aliyejifunza kutokana na utundu wa mitaani, na kipaji alicho nacho, akaanza kumuelekeza huyu mtaalamu wa kusomea, ...wakaelekezana na ndipo huyu mtaalamu, akamfundisha mwenzae kuwa mkopo yawezekana na utawasaidia, a kweli baadaye wakapata mkopo kama mtaji wa kuanzia, wakaanzisha kampuni yao.

‘Kiukweli kwa mtaalamu, ambaye alizoea ikifika mwisho wa mwezi anapata chochote, Ilikuwa mwanzo mgumu kwake,  lakini baadaye wakafanikiwa...walikuja kupata wateja kutoka kampuni mbali mbali, na kuweza kujitangaza, na hatimaye kampuni yao ikajulikana ...

‘Ndio hii kampuni iliyopo sasa....?’ akauliza mkuu

‘Hapana sio hii iliyopo sasa...’akaambiwa

‘Kwahiyo kumbe,...hiyo ya utapeli sio hii,...hebu endelea kunifahamisha....sijui mwanasheria, unanielewa kwa kuuliza maswali yangu, ni ili upate ufafanuzi zaidi....mnielewe hapo....’akasema akionekana mwingi wa mawazo.

‘Unajua hapa walikutana watu wenye mitazamo miwili tofauti, japokuwa waliweza kufanikiwa, lakini kulikuwa na migongano ya hapa na pale kwenye utendaji wao wa kazi, mtundu akawa ana mambo yake ya chini kwa chini, na mtaalamu akawa haafikiani na hayo mambo ya chini kwa chini...

‘Mambo gani hayo ya chini kwa chini...?’ akaulizwa

‘Huyu wa mitaani , alitaka mambo yasiyo na utaratibu ule unajulikana, kama kulipa kodi, kuwalipa wateja kwa wakati, kazi za halali, na vitu kama hivyo...yeye alipendelea mambo yaende kiujanja ujanja, hata kazi nyingine ziwe za ujanja ujanja, ilimradi pesa ipatikane...hali kwa mtaalamu ilikuwa kinyume, yeye alitaka kutumia elimu yake zaidi....’akasema.

‘Elimu ilimsaidia eeh,....sasa ikawaje akajiingiza huko...?’ akauliza mkuu

‘Kwa hali hiyo, wakaja kutofautiana kabisa, na walipokaa kwenye kikao chao maalumu, wakaona iliyo bora ni kuachana kila mmoja akawa na kampuni yake binafsi. 

Wakakubaliana na kweli kila mmoja akawa na kampuni yake binafsi, ....’akasema

‘Sasa wakiwa na majina tofauti, ila walijitahidi wateja kuwafahamu, na haikuwa vigumu sana kwa kipindi hicho...’akaambiwa

‘Sasa huyu mtundu, akawa huru, kufanya mambo anavyojua yeye, mwanzoni alifanikiwa sana,.... alikuwa na biashara halali na biashara haramu...hii biashara haramu ndiyo iliyomuinua sana,...’akasema mplelezi.

‘Kama ukiangalia kesi ya huyu mtundu,  utakuja kugundua kuwa, alikuwa na mipango ya kuwasaidia majambazi, kubuni mikakati, ya kimitandao, na kuwaibia watu hata pesa zao kwenye akiba zao,....kwa ama kuwahadaa, na watu hutoa kumbukumbu za amana zao bila kujijua,..au kwa kutumia mbine za ujanja za mlungula,au kitaalamu blackmail....tukaja kumkamata na akafungwa kifungo cha miaka mingi tu...sasa hivi yupo jela, anatumikia kifungo....’akasema

‘Ok, huyo alikuwa mtundu, sio huyu mtaalamu, au sio....huyu mtaalamu akawaje kujihusisha na mambo hayo na elimi yake, na kuaminika kote na .....hata mimi, bado,maana kaajiri vijana wetu, analipa kodi....anasaidia mambo mengo ya kijamii...’akasema mkuu akionekana kama kutoakuamini.

‘Mkuu, sio vyote ving’aavyo ni dhahabu,...’akaambiwa

‘Sawa, endelea...lakini niulize yeye katika mikakati yake alikuwa akiwashirikisha watu wake, wafanyakazi wake....vijana aliowaajiri...?’ akauliza hilo swali

‘Mkuu....kiutendaji aliweza...japokuwa huenda walikuwa hawajui, au wanajua, lakini wasingeliweza kufichua siri za kampuni...’akasema

‘Mlichunguza hilo kwa wafanyakazi kuwa wanahusika...na nani na nani anahusika...?’ akauliza

‘Kwanza mkuu, ngoja tuendelee na huyu mhusika mwenyewe...umuone alivyoweza kujiingiza huko, na ndipo utagundua mwenyewe kuwa wanahusika au hawahusiki.....’akasema

‘Ok, endelea

NB: Naona niishie hapa kwa leo , msione tunakawia kuingia kwenye undani wa jina la kisa chenyewe, lakini haya yanatolewa,...yanagusa jamii, yalitokea kwenye kisa chenyewe, na diary yangu, inatumia mfumo wa visa kama njia ya kufichua uovu kwenye jamii, kueleimisha nk....

WAZO LA LEO: Elimu yako itakuwa na umuhimu sana kama itakusaidia katika maisha yako lakini katika misingi ya haki na ukweli,...na itatumika kusaidia jamii, kwa kuleta maendeleo katika kiu-adilifu... ukiwa kama kiongozi, uwe ni wa siasa, maofisini, nk...timiza wajibu wako, kama taaluma yako inavyokutuma ... na sio kuitumia kiujanja ujanja kunufaisha tamaa zako binafsi, huo ni ufisadi wa taaluma.


No comments :