‘Sikilizeni, huu sio utaratibu,
lakini kutokana na hali isiyoweza kuzuilika, tumeona kuwa shahidi wetu wa awali
ambaye alikuwa akiendelea kutoa maelezo ya ushahidi wake, asubirie kwanza, ili tumpe nafasi mzee wetu huyu ambaye
kutokana na hali yake hataweza kusubiria, tukae kimiya tumsikilize....’akasema
hakimu akimuangalia mzee
Yule mzee alikuwa kakaa
kwenye kiti chake huku akisoma makabrasha fulani aliyokuwa nayo mkononi, na
nyuma yake kulikuwa na yule askari, akiangalia huku na huku kama kuhakikisha
kuwa hakuna lolote baya dhidi yam zee huyo.
‘Mzee tunakupa hii nafasi
japokuwa umetuvurugia utaratibu wetu, hilo unalifahamu vyema,lakini nina imani
hicho unachikitaka kukiongea kinaweza kuziba hilo kosa...’akasema hakimu na
yule mzee akatikisa kichwa kukubali
‘Sasa unaweza kuendelea na
maelezo yako, na ili uweze kuongea kwa nafasi, hebu wakusaidie ukae vyema...’akasema
hakimu na yule askari aliyekuwa nyuma yake, akamsogelea mzee kwa mbele, lakini
mzee alimuashiria kuwa yupo sawa, na hakimu akaendelea kutoa maagizo
‘Wakili muendesha
mashitaka, huyo naona ni mtu wako...au?’ akauliza hakimu, na wakili muendesha
mashitaka, akasema;
‘Ndio muheshimiwa hakimu, naona
ni mtu wangu,...lakini naona hahitajii kuongozwa, yeye anajua jinsi gani alivyojipangilia
kutoa maelezo yake....’akasema wakili muendesha mashitaka, nahakimu akamgeukia
mzee na kusema;
‘Haya mzee unaweza
kuendelea, kutuambia yale yote uliyokusudia kutuambia, hatutaki kukuwekea
pingamizi,...’akasema akiwaangalia wakili watetezi, ambao walionekana kuwa
kimiya zaidi, na mzee akaanza kuongea kwa sauti ile ile, akasema;
‘Kundi hilo haramu lipo, na
mimi nimepata bahati ya kuwa mmoja wa viongozi waliochaguliwa katika vitengo
maalumu, sikuwa kiongozi mkubwa lakini nilipewa nafasi inayonifaa, nikapewa
ulaji, ni nani anakataa ulaji eti jamani...’akasema na watu wakaguna, lakini
wakakatisha kama vile kuna sauti imetoka ya kuwanyamazisha.
‘Mimi nilikuja kuchaguliwa
kuwa kiongozi wa kundi hilo baada ya kuonekana kuwa ninafaa, kwasababu
nilishakuwa kwenye kundi la njaa kali, wakati nilikuwa mtu kwenye nafasi nzuri,
na baadaye kutupwa kijijini, hohe hahe, na wanasema fainali uzeeni, na uzee
wangu uliishia pabaya, mimi sikuwa fisadi..waulize niliowahi kufanyakazi
nao,...hata hivyo, licha ya kupata huo ulaji, mimi pia nilikuwa na lengo langu..’akasema
‘Mimi nilichukuliwa
kijijini ambapo nilishatupwa huko kusubiri siku yangu ya mwisho , maana katika
utaratibu wa nchi zetu hizi za Kiafrika, hakuna jinsi ya kuwatunza wazee,
ukistaafu, basi ujue lako, labda uwe ulikuwa na jina kubwa, mwanasiasa
labda...lakini kama ulikuwa mtendaji wa hivi hivi, ujue unalo, utaishia
kubezwa, kuwa ulikuwa hukutumia vyema meza yako,...na sana sana
wanakutayarishia bima za mazishi yako,....’akawa kama anacheka.
‘Mimi nikiwa kijijini
nilipata taarifa kuwa nahitajika kwenye kazi maalumu, sikuamini, na nikajua
labda kuna mafao yangu yalibakia, au kuna lawama za madeni natakiwa kwenda
kutoa ufafanuzi, lakini nilipofika nilikutana na jambo jingine kabisa,
nikaambiwa kuwa kuna kazi maalumu ya kuweza kulifichukua tatizo, tatizo
linalolalamikiwa kuwa kuna kundi baya...
‘Kundi gani?’ niliuliza na
nikaambiwa jinsi gani watu wanavyolalamika kuwa kuna kundi limejijenga na kula
mali ya umama, na kujiwekea himaya ya kificho...na maelezo mengi tu...
‘Ndugu zanguni, ndugu
muheshimiwa hakimu, kundi hili lipo na kweli lilianzishwa lakini kutokana na
uchunguzi wangu yote ni kutokana na hali mbaya ya kimaisha inayowakabili watu
wengi,...’akasema na nikasikia watu wachache wakipiga makofi na hakimu akagonga
rungu mezani na kukawa kimiya
‘Mimi siongei hili kwa nia
ya kulitetea hili kundi, bali huo ndio ukweli, huwezi kumuajiri mtu kwa mshahara
usiweza kukidhi mahitaji yake, akakufanyia kazi siku nzima, na baadaye
anastaafu, hajui hata ataanzaje maisha yake, angalia wakulima wanalima kwa
shida mwisho wa siku anapata nini, angalia mfanyabiashara anapata nini, kila
anachopata kinanyakuliwa kwa kodi nyingi tu...
‘Angalia sisi tuliojituma
kwa nia moja, kwa uzalendo, ni kitu gani tulikuja kukipata,...sasa hivi wale
waliokuwa na majina mazuri watatupiwa mikoani, kuwa wakuu , nakadhalika, lakini
hao ni wale waliokuwa na majina mazuri, je wale ambao hawana majina mazuri,
lakini walifanya kazi pengine zaidi ya hao wenye majina mazuri wao wanapewa
nini....
‘Japokuwa muasisi wa kundi
hili alikuwa msomi,...lakini yeye alimuona baba yake alivyoteseka baada ya
kuitumikia nchi yake kwa shida, akaingia vitani, na aliporudi kwenye vita ile
ya nduli, alikuwa kama mwehu,...unajua mambo ya vita yalivyo, ni nini alikuja
kukipata, ...mwehu atasaidiwa nini,..lakini bahati nzuri mtoto wake akapata
msaada na elimu yake, kutoka kwa baba yake mdogo, akamsaidia akaenda nje
kusoma, na huko ndipo alipokutana na wenzake wakabuni hilo jambo..
‘Yote hayo jinsi gani kundi
lilivyoanzishwa, wahusika, viongozi wake, yapo kwenye nyaraka za siri
zilizoibiwa...wapo watu wengi sana, na wengi wameunganishwa hata bila kujijua,
wanatumika tu..hao mliowakamata ni chambo tu, ...mtakuwa mnawaonea bure, wapo
wengi sana...’akasema
‘Siwatetei, na
walichokifanya sio jambo nzuri, ila ninachotaka kusema ni kuwa, ili tupate raia
wema, wazalendo, ni lazima tuwe na sheria ya kuwalinda raia, sheria ya
kuwafanya wafaidi maliasili yao, sheria ya kuwawezesha wawe na maisha bora...ni
muhimu sana twende na wakati, unaomjalia mzawa zaidi, angalieni mataifa ya nje
wanavyofanya, ulaya na marekani, wewe muafrika ukifika kule unapewa nini..
‘Haya natoa mfano mdogo wa bima
za uzeeni, mnajua thamani yake inakuwa haipo wakati mtu huyo anastaafu, wakati
anakatwa hayo makato hela hiyo ilikuwa inalipa, lakini wakati anastaafu
thamamani yake sio sawa na alipokatwa kwenye mshahara, je hili wanaliona, je hili
lipo kwenye sheria ya kulinda thamani ya bima ya uzeeni...huo ni mfano tu
mdogo.
‘Kama raia wataishi maisha
bora, wakawa wanalindwa, mimi hapa sizungumzii kulindwa kiusalama, hilo la
kiusalama linatelekezwa, mimi nazungumzia kulindwa kinafsi, mtu
arizike,..akijua kuwa ninapata pato la halali kwa haki, kutokana na jasho
langu...hebu angalieni malipo wanayolipwa watu wa nje wanapokuja kufanya kazi
hapa nchini,lile ndilo pato halali la mfanyakazi, lakini kwanini alipwe yeye
hivyo wewe ulipwe kiduchu...
'Jamani kiuadilifu ,hebu linganisha na malipo ya hawa watu wawili, wanavyolipwa, unategemea nini hapa,...utaona dhuluma ilipojikita, hilo nililiweka wazi kwenye ripoti yangu,
lakini ripoti hiyo iliwekwa kapuni....’akatulia
‘Upo ubaguzi mkubwa wa
chini kwa chini, na ubaguzi huu unazaa chuki, ni moto uliofunikwa na majivu, mtu anaona kumbe mimi
sithaminiki, kumbe kuna watu wanastahiki zaidi yangu mimi, kumbe mimi ni
mkimbizi tu,kumbe mimi,hizi kumbe kumbe ni hatari, ndio zinazaa makundi,’
‘Kwahiyo nini tena unategemea hapo, mtu kama huyu aliyekuwa kijiweni, keshakata tamaa ya maisha, mtu kama huyu anayeona anadhulumiwa, anakuja kujenga dhana kuwa ili aishi vyema ni lazima aibe, ni lazina na yeye atafute mbinu za kuchukua chako mapema, akijaribu kidogo
akafanikiwa ndio basi tena, moyoni anajenga dhamira,kuwa kumbe huo ndio mfumo wa maisha, kumbe unaweza kufanya lolote ili kutafuta
namna nyingine ya maisha....
'Sasa huyu mtu ndio akutane na hawa watu wa hilo kundi, watu
waliojipanga, watu wanaojua udhaifu wa binadamu keshamsomea binadamu na udhaifu wake, aje akutane na wabongo mwenye njaa kali,...hawa watu sio mchezo,wenyewe ukiwaona utahisi ni
wacha mungu, waadilifu, wanajua jinsi gani ya kukupika na kukupakua, mwenyewe utakubali tu, na kufanya
lolote lile watakalo kushawishi nalo...., hali hii jamani ni hatari.
‘Tunaweza kuibadili hii
hali, mimi nina imani hiyo kabisa, na sio jambo la kuharakisha lakini kidogo kidogo tunaweza kuwafanya
wazawa wakajiona na wao ni sehemu ya nchi yao...borosheni vipato vyao, na kuwe
na sheria, ya kuwalinda,..ok, mishahara sio lazima iwe sawa, lakini kuwa na mafao ya
kuweza kujikimu, kila mfanyakazi ni lazima awe na bima ya matibabu, usafiri wa
kufika kazini, kodi ya nyumba, ...haya yawe kwa wote,na yawekwe kwenye katiba ...
‘Na pia ili haya
yawezekane, huyu mtu kutoka nje, analipwa mamilioni basi tukate kidogo kwenye
malipo yake kama kodi ya kuwapooza wazawa, kama analipwa mishahara mikubwa,
basi kuwa na makato ya kumfidia huyu mzawa..tukifanya hivi tutajenga uwiano,
tofauti iwe kwenye mishahara, lakini marupurupu yawepo ya kumkimu huyu mvuja
jasho kutoka kwenye kodi ya huyu muheshimiwa sana...
' Maana sisi tunataka kuwavutia
wawekezaji, lakini wasivutiwe kuja hapa kwetu kwenye kisiwa cha amani kwa mgongo wa wazawa..tuliangalie hili kwa
makini, maana sisi sio malaika, kuwa tunaweza kuishi kwa amani miaka yote,
tukavumilia, tukafunga mikanda kikomo cha matundu yake, amani inavurugwa na mambo
madogo madogo tu, haya ya ubaguzi,...kuwagawa watu wakajiona sio sawa na
wengine. Matabaka,ya kinchi, kijinsia, kirangi,kidini, kikabila, kiwenzetu,
haya ni mabaya sana...
Chuki hazianzi mara moja
kama mnavyofikiria nyie, chuki zinaanzia chini kwa chini, watu wanalalamika,
hawasikilizwi, wakitokea viongozi wao wanaojaribu kuwatetea wanakamatwa,
wanawekwa ndani, wanauliwa kiujanja...hivi tunakuza jambo tofauti na tunavyofikiria kuwa nguvu inasaidia,..haisaidii inapumzisha kwa muda, chuko zipo moyoni, zinasubiri nafasi...
‘Tukitumia nguvu, tukaona ndio njia muafaka, huku chanzo cha yote hayo kipo, kinajulikana, lakini kwa vile ni kwa masilahi yetu, hatutaki kuleta mabadiliko, tutazidi kuwajengea chuki wananchi, hasira visasi vinajijenga chini kwa chini, itafika muda watu watasema basi liwalo na liwe,...
'Mimi nimefanya utafiti mkubwa tu, hayo ninayozungumza yapo makazini hasa makampuni wa watu binafasi ambapo kuna wafanyakazi wengi, kuna ubaguzi wa
kipato, ukienda mitaani kuna ubaguzi wa maeneo, huku ni kwa wakubwa, nyie msioweza kujenga
nyumba nzuri ondokeni,...mnamfukuza mzawa aliyewahi eneo hili likiwa pori, kwanini hao wakubwa wasiende kuanzisha makazi yao huko
maporini...si wanauwezo..chungeni sana, vita vya kudai maeneo, chungeni sana
umiliki wa ardhi kwa wasio wazawa ...hili ni balaa jingine tunajitakia
‘Mimi siwatetei wale
wanaoanzisha makundi haramu, mimi siwatetei wale wanaoleta vurugu, ila naupinga
utendaji mbovu, ambao ndio chanzo cha yote hayo,napinga ile hali za kuwabagua watu, wanaokuja wanapewa masilahi
makubwa kuliko wazawa hata kama kazi wanayofanya ni moja,
huu ni ubaguzi...wapeni haki zao stahiki kila mmoja bila kujali utofauti wao wa kiitikadi, kabila, utaifa ...tutaweza kufanikiwa kwa hilo
'Jamni , hilo linawezekana lakini ni mpaka hawa waheshimiwa, hawa watendaji wajishushe, na kuiona hiyo hali..tatizo watendaji wapo matawi ya juu, toka
lini mwenye shibe akamjua mwenye njaa, haiwezekani...
'Kwahiyo kosa limejengwa na
ile hali ya kujilimbikizia, huyu mkubwa anapata mshahara mnono, gari la bei mbaya, nyumba
bora, bado anapewa mafungu mengine mengi zaidi ya mshahara wake, huyu wa
chini,ana mshahara mdogo, bado hastahili kupata hayo mafungu mengine ya mrupurupu, anakatwa
kodi, anapata shida ya usafiri, hana bima ya matibabu, gharama kubwa za ada za watoto...yaani pesa yote aliyolipwa inaishia njiani,
basi tumuangalia na huyu namna gani tunaweza kumchangia katika gharama za kimaisha..
‘Jaribuni kujenga
ubinadamu, jishusheni chini, muangalia hali halisi,punguzeni marupurupu kwa
wakubwa na hizo punguzo wepeni walalahoi, hivi hamuwezi kukaa na kujiuliza huyu
mtu anaishije, je ya huyu mtu itatulia vip kiakilii, hivi kwa hali kama hiyo huyu mtu atakuwa
na uzalendo wa nchi yake..hilo halitawezekana, hata kama tutachonga rungu kubwa
la dola, hawa watu watarubuniwa, na amani itakuwa na mashaka..
‘Mimi nikachukuliwa kuweza kulifichua
hili kundi..nikapewa kazi ya kuzunguka, kutafiti, na kupata maoni ya wananchi,..mwanzoni nilifanya
vyema tu, nikakabidhi kazi yangu hiyo kwa wahusika, , mmmh, hutaamini,
ilichukuliwa ikawekwa kapuni, mimi nikarudi kijijini kwangu nikiwa nimelipwa
ahsante yangu, nikapaua kabanda kangu ili nipate sehemu ya kuanza umauti wangu..
Nayazungumza haya kwa
uchungu mkubwa, kiukweli, kama mtu atakuwa muaminifu, akatumia mshahara wake
bila mbinu nyingine yoyote, hawezi kujenga, nazungumzia wafanyakazi serikalini,....hutaamini
mimi mpaka nastaafu nilikuwa na kabanda kabovu tu, ningewezaje kujenga kwa
kipato nilichokuwa napata, mimi sikuwa mwizi,..nilikuwa mcha mungu, mchapakazi,
muadilifu na faida yake ndio hiyo...
Nikiwa kijijini natafakari
kile nilichokipata, nikajiwa na kijana, alikuwa kiongozi mpya wa kitengo nyeti tu, alikuwa kunitembelea, na katika mazungumzo yetu tukafikia kuelezea ile ripoti yangu niliyoipeleka huko kwa wahusika, kumbe na yeye alishaiona, na kumbe kuja kunitembelea likuwa na nia ya kuniingiza kwenye mtandao...
Mwanzoni sikujua, yeye alianza kwa kunisomesha, alianzia mbali,
maisha yalivyo, hadi akafikia hatua niliyo nayo, baadaye akaniuliza;
‘Je mzee ina maana wewe
umeshajiandaa kwenda peponi...’
‘Kwanini kijana..?’
nikamuuliza
‘Hivi wewe una njaa,
umelima ukavuna, mazao yakachuliwa na wengine, utakuwa na moyo wa kuendelea
kulima?’ akaniuliza
‘Siwezi, nitavunjika
moyo...’nikasema
‘Mzee, sisi tunakupa nafasi
nyingine,..pepo yako inaanzia hapa hapa duniani, umeteseka vya kutosha, umajituma
vya kutosha, na kazi uliyoifanya ni nzuri sana, unawajali watu wako na nchi
yako,sasa ni wakati wako wa kula, na wewe angalau uipate pepo yako, kuanzia
hapa duniani....’akaniambia
‘Unajua hawa vijana wa siku
hizi ni wasanii kweli kweli, wanajua kuitumia lugha kisanii, nilimuelewa ana
lengo gani, lakini mimi nilijifanya sijui, ..baadaye akanisomesha, akanijenga
ajuavyo yeye, na mwisho akasema;
‘Mzee, sisi tunakupa kazi
ile ile...lakini sasa angalia masilahi yako,....angalia familia yako, ona
wenzako, watoto wao wapo wapi, ona wenzako wamewekeza nini, na wewe unataka
kufanya nini, hata hiyo pepo, itakuwa haina thamani wako kama nyuma umeacha familia
inateseka, inanung’unika...
‘Huko nyuma umeacha,
familia masikini, familia ambayo itakimbilia kuuza madawa ya kulevya, je kweli watakuwa na nafasi ...tunakupa
nafasi, upate kipato usomeshe watoto wako, uwekeze ila familia yako ije ipate
mahali pazuri hata pa kufanyia ibada, wakuombee, sio wawe wanakulaani kuwa mzee
hukuwaachia kitu, ikifika muda wa kupeleka ripoti, unavunga vunga siku
zinakwenda, ndivyo wenzako wanavyokula....’akatulia
‘Hebu niambieni, ni nani
asiyetaka maisha bora, hebu niambieni ni nani asiyetaka watoto wake, familia
yake, iishi maisha mazuri....tuweni wakweli, ...’akasema na watu waliokuwa
wametulia wakaanza kunong’ona..na mzee akamuangalia hakimu na kusema;
‘Muheshimiwa hakimu hata
wewe unayataka hayo maisha mazuri, ukumbuke ulikotoka, na sasa umefikia fmilia
uzeeni, huna kitu, unajutia jinsi ulivyojitesa kwa nchi yako,na sasa umestaafu
huna kitu,..sema ukweli wako na mungu wako anakuona,.....’akasema
`Sasa muheshimiwa hakimu
naomba mtege sikio muone ni nini nilichokifanya, na kwanini hayo mauaji
yalitokea...’akasema na hakimu akaangalia saa yake
NB: NIKUULIZE NA WEWE , je WEWE hutaki maisha bora, ?
WAZO
LA LEO: Wafanyakazi ni sawa na familia yako nyumbani, wewe kama
bosi, wewe kama muwekezaji, wewe kama muheshimiwa waangalie wafanyakazi wako
kama unavyoiangalia familia yako nyumbani, kwa uadilifu na hekima, ukifanya
hivyo, tija, na uzalishaji utaongezeka, lakini kama utakosa uadilifu katika
utendaji wako, ukawabagua wafanyakazi wako kwa namna yoyote ile, haki ikawa
haitendeki, tegemea kushuka kwa uzalishaji,..., na huo ndio mwanzo wa uvujifu
wa amani. Amani ya kweli huanzia nyoyoni, punguzeni manung’uniko, kwa kuwa waadilifu
kwenye sehemu zenu za kazi.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment