Usiku wa
siku hiyo ulikuwa mrefu sana, nikawa na mawazo mengi sana...ni kila mara mara
niliishia kutaka kujua hatima ya kesi yangu, je itakuwaje...na nilichanganyikiwa sana,
nilipopigiwa simu na baba mkwe
Ilikuwa
nimepumzika, wakati alipofika askari na kusema kuna mtu anataka kuongea na mimi
kwenye simu, nikajua huyo anaweza kuwa mdada, nikaiweka sikioni ile simu
‘Ndio,
nimabie....’nikasema
‘Kuna mambo
mengi nimeyasikia juu yako, nilitaka kuhangaika ili kesi yako iishe
mapema,lakini kwa hayo niliyoyasikia, nimekata tamaa kabisa,...hebu niambie
ukweli wewe na mdada mna mahusiano gani...’ilikuwa sauti ya baba mkwe,
iliyonifanya nishituke na kutaka hata kupiga magoti
‘Oh,
baba..mkwe.....shi...shikamooo...’nikasalimia
‘Shikamoo na
wewe, umsikia swali langu?’ akaniuliza
‘Hapana,....’nikasema
‘Hujasikia
swali langu?’ akaniuliza tena
‘Mzee mimi
sina lolote na huyo dada, yeye ni mfanyakazi wetu tu..hakuna
zaidi.....’nikasema
‘Mfanyakazi
wenu uende kukaa kwake usiku kucha,..au unafikiri mimi sifahamu, nafahamu fika
n kitu gani kilitokea huo usiku....’akasema
‘Wengi
wamsikia tu...mimi na bosi wangu tulikwenda pale kumjulia hali , tukakuta amezidiwa
ndio tukapanga tumsaidie kama mfanyakazi mwenzetu, na ndio huyo marehemu
akatokea, ..kifo chake hakuna aliyekitarajia, hata sijui ni nani
kamuua...’nikasema
‘Ninachotaka
kukuambia ni kuwa, hayo ya mahusiano yako na mdada yamefikaje kwa binti yangu,
...?’ akauliza
‘Mzee mbona
sikuelewi, ni nani kamuambia uwongo huo, ..hakuna mahusiano yoyote , labda ni
watu wanataka kutogombanisha tu, ni fitina tu....’nikasema nikihisi labda mdada
katuma mapicha yake mabaya, lakini hilo sizani kama mdada anaweza kufanya
hivyo.
‘Sasa
sikiliza kwa makini,...nilishakuambia mapema, kuwa nilichelea kukuweka ndani
kipindi kile ulichomharibu binti yangu, baada yaw ewe kukiri kuwa utamuoa huyo
binti, na nisaidie kukutafutia maisha, ..hiyo kazi nimehangaika mwenyewe, bila
yaw ewe kujua, ....kuipata hiyo kazi ni kutokana na mimi kukupigia
debe,....’akasema
‘Nashukuru
sana mzee...’nikasema
‘Sasa kama
kuna ukweli wa hayo, na jinsi binti yangu alivyoyapokea hayo, nahisi
kachanganyikiwa, sijui...lakini nakukanya , nafikiri unanifahamu,....nalifuatilia
hilo kwa
karibu sana, ...nikifuatilia kesi yako inakwendaje, ....’akasema
‘Mzee, usiwe
na shaka, hakuna lolote , mimi najiapnga kesi ikiisha tu, nafika kijijini,
kufanga ndoa, unaona nyumba ile,..hata jina nimeandika jina la mchumba wangu
kuonyesha kuwa namjali, hakuna...’nikawa naongea, kumbe simu ilikuwa
imeshakatika mzee hayupo hewani,...
Basi
nilipotoka kuongea na mzee nikawa nawaza sana, nikiwa namuwazia huyo mchumba,
namfahamu sana, ni binti asiyejua kuvumilia machungu, kitu kidogo kitamsumbua
sana,..sikutaka kabisa aje kusikia lolote linalotokea huku kijijini.
********
Niliingia kwenye chumba ninachokaa, nikiwa na
mawazo sana nikajitahidi kuyapima maneno ya wakili aliyetafutwa na mdada, ambaye
alinithibitishia kuwa yeye ataweza
kuhakikisha kuwa dhamana yangu inapatikana.
‘Kama
dhamana ikipataikana ni lazima nifanye juhudi ya kulimaliza hili tatizo, sitaki
tena kuwa mtumwa, sitaki tena...’nikatulia nikiendelea kuwaza;
‘Ina maana
kweli huyu wakili anaweza kulifanya hili kama alivyosema kuwa anaweza kufanya
dhamana ikapatikana na hata kuimaliza hii kesi haraka iwezekanavyo, mhh, sijui
kwa vipi, lakini aliposema kuwa kesi kwa mdada haipo tena, nikaingiwa na
wasiwasi, kuwa huenda kinachotumiwa hapo ni pesa, lakini iwezekanaje..siamini..
Na huyu
mpelelezi anakuja na sera yake, ya kuwa mimi nijitolee kwa ajili ya taifa
langu, niakumbuka maneno yake, akisema,...
‘Kundi hilo, limejengwa na watu
mashuhuri tu, lina mawakala kila sehemu nyeti, zikiwemo sehemu hizi za usalama,
huwezi amini hata mimi siwaamini watu ninaofanya kazi nao, ...ndio maana nataka
tuwe kitu kimoja, ujitolee kwa ajili ya taifa lako....
Kauli hii
ilinitia motisha nikawa nakumbuka masomo ya shuleni kwenye kipindi cha siasa na
historia, kuhusu watu mashuhuri, waliojitolea kwa ajili ya mataifa yao na
kuweka historia, japokuwa wamekufa lakini hadi leo wanazungumziwa, nikajiuliza
hivi na mimi kwanini nisiwe kama wao...
‘Kwa vipi niwe
kama wao, ni nani ataniona, ....ina maana nijitolee kwena gerezani,
nikataabike, nikitoka niseme nimefanya hivyo kwa ajili ya taifa langu....hakuna
kitu kama hicho...kwanza wamejipanga kuniulia huko huko gerezani, .....mmh,
sikubali’nikasema
‘Sasa
nifanyeje, nitoe siri zangu kuwa mdada alinifanyia mambo mabaya, na ndio maana
nashindwa kusema lolote lakini hata hivyo ni kweli kuwa nafanya hayo kwa ajili
ya mashinikizo yam dada, au kuna kitu kingine...?’ nikajiuliza
‘Kitu
kingine kama kipi, mhh, labda ni kwa vile nimetokea kumpenda au nimezimia wake....sijui,
lakini mdada kaumbika,...mmh, ndio maana hata mtoza ushuru aliingia kichwa
kichwa...na sasa ni marehemu, na mimi je....’nikasema na nilipomkumbuka mtoza
ushuru, nikajaribu kukumbuka jinsi ilivyotokea siku ile..
‘Nakumbuka
kabisa nilitoka mle ndani, mtoza ushuru akiwa hai, japokuwa alikuwa
anajikongoja, nahisi ni kwasababu ya jinsi mdada alinyomrusha na kumbwaga chini
kama gunia, ...kwa hali ile kama wewe sio mpiga miereka unaweza ukavunjika
mifupa, ...hata hivyo jamaa alionekana kukomaa, kwani aliweza kusimama na
kuanza kujikongoja kutembea,....sasa aliuwawa vipi kwa risasi,...siwezi kujua
maana nilishatoka nje...’nikasema
‘Kwa jinsi
ilivyokuwa, ...mdada anahusika moja kwa moja, kwani nilimuacha yeye na huyo
mtoza ushuru, na mdada ndiye aliyekuwa na hiyo bastola...inawezekana pia huyo
mwtu mwingine alikuwa kajificha mahali, baada ya kunigonga mimi kichwani na hiyo
nyundo, na alipoona nimezimia, akamgeukia mdada....
‘Hata hivyo,
kinachonishangaza ni jinsi gani huyo mtu mwingine, ambaye nahisi ni mwanaume,
alivyoweza kumsogelea mdada...nijuavyo mimi akipandisha huwa hataki mwanaume
amsogelee, na nakuwa na hisia za ajabu sana, hata kuona kitu kinachokuja nyuma,
...huenda mtu alikuwa kajificha, na akamtokelezea mdada kwa nyuma kwa haraka
sana, sasa huyo mtu alikuwa kajificha wapi, mbona mimi sikumuona?’ nikajiuliza
‘Atakuwa ni
nani huyu mtu, na aliingia saa ngapi, na kwanini mlinzi asimuone, mhh, kwa
vyovyote atakuwa katumia mbinu za hali ya juu kumpita mlinzi, na kuingia ndani
bila kuonekana,huyo mtu sio wa kawaida ...sasa atakuwa ni nani?’ nikajiuliza
bila kupata majibu
Ilikuwa kama
marue rue, mwili ukaniisha nguvu, na mara nikazama kwenye usingizi, na kujikuta
nimesimama katikati ya miti iliyofungwa kama magogo, na mimi nimefungwa bara
bara...nikajiuliza kwanini nimefungwa hivyo
‘Unahukumiwa
kwa kosa la kuua ...’nikaambiwa
‘Mimi
sijamuua mtu..’nikasema
‘Tuthibitishie
kama hujaua.....’nikaambiwa, na sikuwa na cha kuthibitisha, maana hata hilo
kosa lenyewe al kuua, sikulitambua,...nikakaa kimiya
‘Umeshindwa
kuthibitisha unanyongwa...’sauti ikasema
‘Lakini mimi
sijaua..’nikajitetea
‘Thibitisha
kama kweli hujaua...’sauti ikasema
‘Sina cha
kusibitisha maana hata sijui nimemuua nani..’nikasema na mara ukaletwa mwili,
uliofunikwa, na kuambiwa, unamuona uliyemuua....unataka kumuona ni nani?’
nikaulizwa
‘Ni...ha..pa...ni
nani?’ nikauliza na mara ukafuniliwa, na nilipoona sura yake nikapiga ukelele
na kuzindukana kwenye usingizi, niliamuka huku nikiwa nahema, moyo ulikuwa
ukienienda kwa kasi, na sikutaka hata kuikumbuka hiyo ndoto, nikainuka pale
nilipokuwa nimelala, na kunyosha nyosha viuongo
‘Hiyo ni
ndoto sio kweli...’nikasema, na mara kukapambazuka na asubuhi ikaingia nikiwa
sina raha, na ile ndoto ilinitawala sana kichwani, na nikawa najiuliza kwanini
itokee vile, kwa nini nionyeshwe kuwa nimemuua mtu ambaye hata hahusiki na yote
yanayotokea, nikajiathidi nisikumbuke lakini..
`Mhasibu
kuna mgeni wako....’nikaambiwa
‘Ni nani?’
nikauliza nikiwa na hamasa , hasa ya kujua majaliwa yangu.
‘Utamjua
ukifika huko...’nikaambiwa na huyo askari, na mimi kwa haraka nikatoka hadi
sehemu ya wageni, na nilipofika hapo, nilimuona mtu kakaa kwenye kiti, lakini
alikuwa kanipa mgongo, sehemu kubwa ya chini ilifunikwa na meza, alikuwa ni mwanamke,
kwa pale alipokaa sikuweza kumuona vyema, hadi nilipomkaribia,na nilipofika
karibu yake akageuka;
‘Oh ni wewe!,
umefuata nini huku?’ nikauliza kwa mshangao, huku nimeduwaa, na huyo mgani
akasema;
‘Ina maana ulitaka
nisije,na kwanini hukutaka kuniambia kuwa umefungwa kwa kesi ya mauaji?’
akauliza
‘Mimi sijaua...’nikasema
nikiwa bado nimesimama mbali nay eye, utafikiri namuogopa, na yeye akiwa
kageuza kichwa, halafu akaendelea kuangalia mbele, kwahiyo nikawa namuangalia
kwa pembeni. Nikasogea hadi pale alipokaa, na yeye alipohisi nipo karibu yake
akasema;
‘Mimi sijui
kama umeua au la, lakini kwa namna moja au nyingine unahusika,wasingakukamata
kama hukuhusika japo kuwa karibu na tukio....niambie ukweli kuna nini kilitokea
hadi kufikia huko?’ akaniuliza
‘Ni bahati
mbaya ilitokea tu, ni kwamba siku hiyo nilikuwa kwenye tukio,tulikwenda kumuona
mgonjwa, na tukiwa hapo, ndio hayo mauaji yakatokea, na wakati yanatokea mimi
nilishatoka nje, kwahiyo hata sijui yalitokeaje...’nikasema
‘Huyo mgonjwa
ni nani?’ akauliza kwa haraka
‘Ni
mfanyakazi mwenzetu...’nikasema
‘Ni mwanamke
au?’ akauliza tena kwa haraka
‘Ndio ni
mwanamke...’nikasema nikijua jibu hilo litaleta dhana mbaya, hata hivyo
nisingeliweza kumdanganya hapo, yeye akageuka na kuniangalia usoni na kusema;
‘Unaonaeeh,
kumbe ni kweli,...mhh, nimeamini sasa, watu walikuwa wakiniambia mengi nikawa
nayapuuzia, sasa nimesikia moja kwa moja kwenye kinywa chako,..’akasema
‘Wamekuambia
nini hao watu, nilishakukanya kuwa usiwasikilie wambea, ukikaa kwenye makundi
yenu mara nyingi kuna kudanganyana,....’nikasema
‘Walioniambia
wala sio watu unaowafikiria wewe, ni watu wenye hekima zao tu, kuwa kuna
mwanamke anakuzuzua, anakufanya husiki lolote,...nasikia hata kazi hazifanyiki
vyema mbele ya huyo mwanamke, sijui kakupa nini...’akasema
‘Ni nani
kakuambia hayo mbona sio kweli, usiwasikilize wambea hao, wafitinashaji
wasiotutakia mema,,...hebu niambie ni nani kakuambia uwongo huo...?’
nikamuuliza nikijaribu kufanya kama nakasirika.
‘Ni nani
kaniambi hilo sio muhimu kwa sasa, na kauli yako ichunge sana, unawatusi watu
wazima, ambao wana heshima zao, na wasingelisema hilo kama hawana uhakika
nalo,...mimi ninachotaka kwa sasa ni kusikia kauli yako ili nijue kuwa wewe ni
mkweli au ni mwongo, na ukinidanganya, siku nikigundua,sitakuamini tena..je ni
kweli au si kweli?’ akaniuliza
‘Ni kweli au
si kweli kuhusu nini...?’ nikamuuliza
‘Kwani
tulikuwa tunaongea nini, au nia yako ni kuleta ubishi wako , usio na msingi,
hivi hata huo usomi wako, hakusaidii kitu...mimi nimekuuliza kuhusu huyo
mwanamke, yupo au hayupo, ni kweli au si kweli, kuwa kuna mwanamke
anayekuzuzua, hadi ushindwe kifanya kazi...?’ akaniuliza
‘Kama yupo
ni wewe, hakuna zaidi yako....’nikasema na yeye akatabasamu na kuangalia
pembeni , halafu akasema;
‘Nakuuliza
tena hayo niliyoambiwa kuhusu huyo mwanamke ni kweli au si kweli?’ akageuka na
kuniangalia akiwa kakunja uso kuashirikia kwa hataki utani.
‘Sio kweli, hakuna
kitu kama hicho, ahadi yangu ipo pale pale, mimi nipo huku mjini kwa ajili ya
kutafuta maisha yetu mimi na wewe, na haya yaliyonikuta ni katika harakati za
kuhangaika, ...kumbuka nilivyokuambia, wewe ni mchumba wangu, hakuna mwingine
anayeweza kuniingilia....’nikasema
‘Una uhakika
na kauli yako hiyo?’ akaniuliza
‘Ndio nina
uhakika.....kwanini unasema hivyo, una shaka gani na mimi, inakuwa kama vile
kuna kitu umekigundua na unataka kuhakikisha,...kuna nini kinaendelea maana
mpaka ufunge safari kuja huku, bila hata ya taarifa, nahisi kuna jambo?’nikamuuliza
‘Sikiliza ,
mimi nimepanga kuja hapa kukuambia ukweli, kuwa kama kuna lolote linaendelea
kati yako na huyo mwanamke, nijue mapema, nisiendelea kuumia, kwani nimeshaumia
vya kutosha, nimevumilia vya kutosha,...’akasema
‘Hakuna
ukweli hapo.....’nikasema na yeye akanikatisha na kuendelea kuongea;
‘Ukweli upo,
ila huwezi kuukubali,..sasa nakuambia ukweli, kuwa nikija kugundua, niliyoyasikia,
kuwa ni kweli,nitakachokifanya ujue wewe ndio sababu,...ukumbuke kuwa,
umeniharibia mipangilio yangu yangu, nilitakiwa na mimi niwe nasoma vyuoni kama
wenzangu, ...ningelikwua na kazi nzuri, ukanikatishia ndoto yangu....’niliona
machozi yakimtoka,
‘Lakini
tulishaongea hayo, kwanini unazidi kujisononesha...’nikamwambia.
‘Mimi
nimeganda huko kijijini, unafahamu sheria za baba, kosa nililolifanya limekuwa
kisingizio kwa kila kitu, sina haki tena ya kufanya lolote, haya ni kutokana na
wewe, nimeganda huko kijijini nikikusubiri wewe, na wewe umewapa ahadi wazazi
wangu kuwa tutafunga ndoa hivi karibu, je hiyo ndoa tutafunga huko jela,
ukienda kufungwa, ndoa itafungiwa wapi, hivi mtoto wako atakuwa na raha,akisikia
baba yake ni mhalifu, hivi hilo wewe hulifikirii... ...’akasema akionyesha uso
wa huzuni.
‘Lakini mimi
sio mhalafu..’nikajitetea
‘Sio mhalfu,
ungelikuwa sehemu kama hii, ..mimi naona hata aibu, kusikia hayo ninayoyasikia,
na sasa ndio hivyo tena, unashutumiwa kwa mauaji,...yote mambo mabaya
mabaya,...kwakweli sitafurahia, watoto wetu wayasikie haya...no bora nisiwepo
kabisa...’akasema
‘Mpenzi
wangu mbona unasema hivyo, usije ukafanya jambo baya, tafadhali...usije
ukawafanya mtoto awe mkiwa, ajisikie vibaya,...oh, mbona unanitisha, nimeota
ndoto mbaya, na wewe unongea hayo hayo...hapana, nakuomba, ...tafadhali,
uniamini mimi...sijafanya hayo wananisingizia tu....’nikasema nikijaribu
kumshika begani, akaondoa mikono yangu, na kujisogeza mbali na mimi.
‘Sikia kauli
yangu...iliyonifanya nije hapa,kama wewe unasema umeota, basi mimi karibu kial
siku naota ndoto mbaya, kukuhusu wewe,.... kama umeota ndoto mimi nafanya jambo,
basi ujua ni kweli, sitanii,mimi nitafanya kweli....nimekuja hapa kuhakikisha
mwenyewe...’akasema na kusimama.
‘Mimi
naondoka, nimefikia kwa shangazi ,nilikuja jana,nikaambiwa upo na mazungumzo,
nikaulizia, kuhusu kesi yako,nimeshaambiwa kuwa unashughulikuwa dhamana
yako,...kwa vile hatujafunga ndoa mimi na wewe,siwezi kwenda huko kwako,
nitakuwa huko kwa shangazi yangu,....’akasema
‘Shangazi
yako yupi huyo, anaishi wapi hapa mjini...?’ nikauliza nikiwa na wasiwasi, huku
moyoni nikisema kumbe ana ndugu yake anaishi huku, basi atakuwa ndio yeye
kapeleka umbea huko kijijini
‘Karibu na
hiyo hoteli kubwa ya kajificheni...’akasema
‘Oh,...kuna
ndugu yenu hapo karibu na hiyo hoteli mbona simfahamu, yupoje, mbona hatujawahi
kukutana naye, ananifahamu mimi..?’ nikasema nikionyesha wasiwasi...
‘Anakufahamu
sana...’akasema na kunifanya niangalia chini, na yeye akawa anaondoka, huku
akisema;
‘Ndio hivyo,
sitakaa sana, nilikuja kukupa pole, na kutokana na hali niliyoiacha huko
nyumbani siwezi kuendelea kusubiria hapa, sitakaa sana, kesho au keshkutwa
naondoka, japokuwa sijajua ukweli wa jambo lenyewe na ni nini...’akasema na
kugeuka kuniangalia.
‘Na baya
zaidi, sijui hatima yako itakuwaje,
maana kesi za mauaji haziishi leo au kesho, lakini hata hivyo, nitajua kwa
kupitia kwa baba, ili nione mambo yamekwendaje, baba kasema ni kesi ngumu sana,
maana hata kama hukuhusika kwa hayo mauaji, lakini inaonekana kama umjichanganya
na makundi haramu,...hebu niambie ni kundi gani hilo ulilojichanganya nalo?’
akauliza
‘Hakuna kitu
kama hicho, mimi sijajichanganya kwenye kundi lolote, nasikia tu kwa watu, kuwa
kuna makundi haramu, ....hili tukio limenikuta tu, kwa vile nilikuwepo siku
hiyo, kwa huyo mgonjwa, lakini mimi nina imani kuwa yatakwisha tu....’nikasema
‘Au ndio
huyo mwanamke kakuingiza kwenye makundi mabaya...?’ akauliza
‘Mwanamke,
....mwanamke yupi, unayemuongolea,....una maana huyo mfanyakazi mwenzetu, au..’?
nikamuuliza nikiwa na mashaka, maana aliponiambia kuna shangazi yake hapa
akribuni, kanifanya nisijiamini tena.
‘Unamfahamu
sana...’akasema
‘Hapana kama
ni huyo, sio kweli, huyo ni mfanyakazi mwenzetu, na kama yupo kwenye hayo
makundi mimi sijui, na sizani, sio kweli...hata hivyo, ni nani huyo
kakudanganya..hivi mimi unanionaje, kuwa ni mwepesi kughilibiwa, eeh,...
usisikilize maneno ya watu, yasiyokuwa na ukweli...!’ nikamwambia huku
kicjhwani nikiwaza mbali sana.
‘Lisemwalo
lipo, kama halipo lisingelisemwa, ...nyie wanaume mnatufanya sisi wanawake
hatujui mnayoyafanya, mnasahau kuwa hao mnaofanya nao ni wanawake kama sisi,kama
ni wanawake, mnaofanya nao, nabado mnaona wao hawajui, hamuoni kuwa
mnajidanganya wenyewe, msitufanye wajinga wakati ujinga mumeuanzisha nyie...’akasema
‘Hayo ni
maneno yako, na mara nyingi ni ya kusikia, na kiukweli sio sahihi,
ukiyachukulia juu juu, utajiumiza mwenyewe, achana nayo niamini mimi,
ninayekuambia....’nikasema
‘Haya....za
mwizi ni arubaini, ipo siku nitayajua tu, na ni bora uniambie ukweli sasa hivi,
kuwa ilitokea bahati mbaya, ulilewa ukapitiwa,
...kuliko nije kufahamu baadaye, na iwe ni kweli,...kwakweli, ninavyoota
ndoto mbaya, sijui nitakalolifanya, maana nimeumia sana, na sitapenda kuendelea
kuteseka tena, lolote nitakalolifanya ujue ni wewe....na hata baba nimemwambia,
nimechoka na kusimangwa...’akasema na kuinuka kuondoka
‘Lakini
tulishakubaliana, tukayamaliza hayo, wanaokusimanga mwisho wake watachoka, wewe
kaa na msimamo wako ukijua mimi nipo kwa ajili yako,...usidanganyoke na maneno
ya watu, niamini mimi...unataka nikuambieje...’nikamwambia na yeye akawa
akibenua mdomo wa kuzarau hayo maneno yangu.
‘Sikiliza nikuambie,
usije kufanya jambo lolote la kujiathiri, kwa kitu ambacho hakipo, ho watu ni...waongo,
wafitina, nakuomba tena sana, maana sasa unanitosha.....’nikasema huku ile
taswira ya ile ndoto ikawa inanijia akilini na kujawa na wasiwasi, kuwa huenda
ile ndoto ilikuwa na ujumbe fulani ambao unaweza kuwa ni kweli, ....oh,sasa
nifanya nini na mimi nipo jela...
‘Mungu
naomba isiwe hivyo, ...naomba isiwe hivyo, sio kweli ile ilikuwa ni ndoto tu....’nikawa
nimeinama nikiwaza kwa muda, mrefu, hata sikujua nimekaa pale kwa muda gani,
hadi nilipohisi mtu akinishika mgongoni, nikainua kichwa nikijua ni huyo
mchumba wangu karudi tena, nikaanza kusema;
‘Nakupenda
mchumba wangu tafadhali usifa....’nikakatiza maneno pale uso wangu ulipokutana
na sura ya mtu mwingine, aliyenifanya moyo wangu uwe kama umelipuka,kwa kimuhe
muhe, nikahisi akili ikibadilika..nikujikuta nikisema kwa kigugumizi..
‘Ume..mu..oona,....’nikasema
kwa kigugumizi, huku nikiangalia mlangoni.
‘Nimemuona
nani wewe, mimi nimekuja kukuchukua mwenyewe, dhamana yako imakubaliwa....na
nataka tukitoka hapa tupitie kwenye hiyo hoteli ya kajificheni tujipongeze...’ilikuwa
sauti ya Mdada.
NB :
Nilikwanza kidogo na malaria, na walionipa pole na kuniombea dua nawashukuru
sana, tupo pamoja.
WAZO LA LEO: Ni rahisi sana kumshutumu mwenzako
ubaya, na hata kujirizisha kuwa upo sahihi kwa shutuma japokuwa na wewe ni
mkosaji mkubwa, lakini inakuwa vigumu sana, kujishutumu wewe mwenyewe, na kuwa
mkali ukikosolewa, au kushutumiwa, hata kama tunajijua kuwa tuna makosa.
Ni vyema tukajenga tabia ya kukosoana
tukifanya yasio sahihi, lakini kwa mtizamo wa kujiangalia nafsi zetu
kwanza, kwani sisi sote ni wakosaji, hakuna aliyemkamilifu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment