Nilifika chumbani kwangu na kwa haraka nikaingia maktaba
nikiwa na shauku ya kuuona huo mkataba, shauku niliyokuwa nayo ilikuwa
haimithiliki, utafikiri nilikuwa nakwenda kugundua alimasi iliyofichwa, kwangu
mimi huo mkataba ulikuwa na thamani kubwa, sio kwa ajili ya kulinda masilahi
yangu tu, lakini pia kulinda utu wangu, kilichokuwemo humo, kilikuwa ni kwa
ajli ya utu wangu, na kama utapotea basi mimi nitaonekana sina maana,,
nitadhalilika,....
Nikawa natembea kwa haraka haraka,nikijua kuwa sasa ukweli
utadhiri, na wale wote waliotaka kunidhulumu, na kuishia maisha ya hadaa nyuma
ya mgongo wangu wataumbuka, ...na hilo nilishaliahidi kwa wazazi wangu kuwa
nitahakikisha, nalifanyia kazi bila ya msaada wao, na wao waliniona kama mfa
maji,....lakini sasa ukweli watauona, na kile nilichokuwa nimekiahidi mbele yao
watakiona kwa macho yao.
Sikutaka kubweteka, sikutaka kudeka,kwao kuwa kwa vile
mimi ni mtoto wa kike, sitaweza kuishi bila ya msaada wao.
Nilitaka kuionyesha jamii, kuwa hata sisi wanawake tunaweza,
tunaweza kutunza siri, tunaweza kutunaza dhamana, ...kwangu mimi kipao cha
ndoa, nilikiona ni muhimu sana, ndio maana sikutaka kughilibiwa, kama
nilijitahidi kufanya hivyo, japokuwa kulikuwa na mapungufu, kwanini mwenzangu
afikie hatua hiyo kubwa ya kunisaliti, hapana, kama kafanya hivyo, ni lazima
sheria ichukue mkondo wake, lakini sheria ipi, maana huo mkataba ndio ulikuwa
ni sheria yangu..sasa umepotea
‘Kama nitaupata huo mkataba, nitawaonyesha watu kuwa hili
linawezekana, kama kutakuwa na mkataba wa ndoa na mkaufuatilia, mwenye makosa
akahukumiwa kutokana na amkubaliano yenu, basi kila mwanandoa ataogopa kufanya
maasi, ....’nikasema huku niendelea mbele kuelekea sehemu iliyopo sheria yangu,
mkataba wangu, utakaonilinda kwa hilo...
‘Na wale wote walionisaliti, itabidi wawajibike, sitajali
kama ni rafiki yangu, au ndugu yangu...’nikasema huku nikifungua mlango wa
maktaba, ambao sasa nilikuwa na ufungua mwingine mpya,japokuwa nilipotoka
sikuwa nimefunga na ufunguo, ila nikitoka nje , nitakuwa nafunga sehemu zote
nyeti...
‘Nikimalizana na huyu shemeji yangu, nitaanza kupambana na
rafiki yangu, sitajali urafiki tena, mapaka kieleweke, na mwishi namalizia na
mume wangu,...nina uhakika kuwa mume wangu kasaliti ndoa yangu, na
ninachotakiwa kupata ni ushahidi, na ....na mkataab wetu utahukumu....’nikasema.
Nikalifungua kabati la mume wangu, kwa ufungua ambao
unafungua kwa namba maalumu, ...hata uchonge ufungua, usingeliweza kufungua,
nilifanya hivyo, ili kila mmoja awe na namba zake za siri, kwahiyo mume wangu
akija nitampa ufunguo wake, na namba zake za siri.
Nikafungia hilo kabati lake, kwa ndani kuna sehemu tatu,
nikavuta kidroo cha sehemu ya kwanza, niliona makaratasi ya malipo, stakabadhi
za malipo na vyeti vya biashara, hakuna huo mkataba...
Nikafungua sehemu ya pili, hakuna kitu, hapo hasira zikaanza
kunipanda ina maana huyu kijana kanidanganya, nikasema na kufungua sehemu ya
tatu, hakuna kitu...nguvu zote zikaisha, na sikujau nifanye nini tena, na
wakati nimekata tamaa, kwa pembeni nikaona bahasha kubwa,iliwekwa kwa kusimama,
isngelikuwa rahisi kuiona, nikaitoa ile bahasha, ilikuwa nzito, nikaitoa, na
kuigeza juu chini kukitoa kilichopo, kikatoka kitabu....
Kumbe ilikuwa sio kitabu , ulikuwa mkataba, na mwanzoni
nilifikiria ni ule mkataba wa kawaida, lakini pale nilipoona alama yangu
nikagundua, ni ule ule mkataba niliokuwa nautafuta, nikauchukua na kuanza
kuufungua, kuhakikisha kuwa ndio wenyewe, na nilipojirizisha nikafunga yale
makabati na kuanza kutoka.
Wakati nainua mguu,
nikakanyaga kitu, nikainama kukiangalia, kilikuwa kidude kidogo,cha kuhifadhia kumbukumbu, unaweza kukiweka
kwenye simu au kwenye komputa, nikakiokota, nahisi kilidondoka kutoka kwenye
hiyo bahasha, waakti nilipoiinamisha juu chini kuutoa huo mkataba,na hapo
nikakumbuka kauli ya shemeji yangu;
‘Shemeji kama kuna
kitu changu naomba uniletee, ...’
`Huenda hiki kitu ndicho anachokitafuta....’nikasema huku
nikikiangalia kwa makini, moyoni nikaingiwa na shauku ya kujua kuna nini humo
ndani, lakini kwa namna nyingine niliona nafanya makosa, nitakuwa nachunguza
vitu vya watu, na mimi sitaki tabia hiyio, hata hivyo kwa hali ilivyo kwasasa
hamasa za kufahamu ni kitu gani kimo humo ndani ikanijia, nikatoka hadi
chumbani hadi kwenye laptop yangu, nikakichomeka, na maandishi yakatokea;
‘Diary yangu,
kumbukumbu za kila siku.....’
‘Oh, kumbe ni kumbukumbu zake, hakuna shida..na wakati
nataak kukichomoa, nikaona maelezo yaliyonivutia, nikayasoma kwa haraka..
‘Kumbe...’nikasema
‘Sasa nimekupata, kama atakuwa anaweka kila kumbukumbu za
kila siku, kumbe nitaweza mambo muhimu ninayoyatafuta, amekwisha, hana ujanaj
tena, ...’nikasema na kwa haraka nikaweka sehemu ya kunakili hizo kumbukumbu
kwenye komputa yangu, ilichukua muda kidogo, na kumbukumbu zote zikanakiliwa
kwenye komputa yangu, halafu nikakitoa kile kitufe, na kukiweka kwenye ile bahasha
nikatoka nacho hadi kule bustanini.
‘Shemeji kwenye hiyo bahasha uliona kitu changu?’ akaniuliza
‘Kitu gani?’ nikamuuliza kama vile sijui,
‘Naiomba hiyo bahasha, umeshautoa huo mkataba unaoutaka,
natumai sasa tumemalizana, uliouona eeh....?’ akauliza huku akichungulia ile
bahasha kwa ndani, na mara akakitoa kile kitufe na kwa haraka akakiweka mfukoni
‘Ni kitu gani hicho?’ akaulizwa na wale maofisa wa upelelezi
‘Ni kifaa cha kazi zangu za ofisini, ni muhimu sana,
ningelipoteza kazi za watu...’akasema
Mimi nilikaa kimiya sikusema kitu na hapo yule ofisa
akaniuliza kama nimeuona huo mkataba na kama ndio wenyewe niliokuwa nautafuta,
nikamwambia ndio nimeuona ndio wenyewe.
‘Shemeji kwa hali ilivyo huyu mtu inabidi tuondoke naye...’akasema
huyo jamaa wa usalama
‘Hapana, mimi nimewaambia kila kitu, kwanini sasa
mnanigeuka, ...tulikubaliana nini?’ akalalamika huyo shemeji yangu na mimi hapo
nikamuonea huruma na kusema;
‘Kwa vile kakubali kushirikiana na sisi mimi sioni kwanini
muondoke naye, ...mimi nitamdhamini, siku mukimuhitaji atakuja, mnaonaje ombi
langu hilo?’ nikawauliza
‘Kuna mambo mengi bado anayaficha, hajakuwa mkweli, ndio
maana tunataka tuondoke naye..tunauhakika akifiak huko atasema kila kitu.’akasema
‘Nimewajibu kila kitu, sijaficha jambo, jambo gani
nimelificha?’ akauliza shemeji yangu akiwa kakasirika.
‘Tunashindwa kurudia swali mara nyingi,...wewe usituone kuwa
sisi ni watoto wadogo, hapa tulikuwa
tunakuuliza maswali ya kukupima tu, mengi tunayafahamu, kwa mfano tu,
hilo la kusema ulikwenda kutupa hiyo silaha porini halafu ikaibiwa hiyo sio
kweli,ukweli ni kwamba kuna mtu ulimpa hiyo silaha, hilo umetuficha,hukusema
ukweli, kuna mengi tunayahitajia kutoka kwako,na usiposema huo ukweli, utaozea
jela...’akasema huyo mtu wa usalama, na kumfanya shemeji yangu atulie kimia.
‘Mimi naomba nimdhamini, kwa vile bado mnafuatilia mambo
mengine, huyu niachieni mimi, nawashukuru sana, kwa msaada wenu, mimi bado nina
maongezi na shemeji yangu, mkiwa tayari kumuhoji, mtaniambia, ila kwa leo
naombeni tuishie hapa , kwani kile kitu muhimu nilichokuwa nikikihitajia
nimekipata...kama kuna zaidii tutafahamishana...’nikasema
‘Huyu ni mhalifu, ..huo aliofanya ni wizi, japokuwa
anamtupia lawama kaka yake kuwa alimtuma, hilo sisi hatulikatai, lakini
hakutaka kusema ukweli,toka awali, kwani hii sio mara ya kwanza kuhojiwa,..japokuwa
waliomuhoji awali ni watu wengine, lakini alichowaambia nikifahamu...’akasema.
‘Yeye hajui kuwa kila siku anafuatailiwa, hajui kuwa bado
uchunguzi unaendelea,na hatua iliyofikia, ni ya kuamalizia, tu, ...watafikishwa
wote wamahakamni kujibu makosa mengi, ikiwemo hilo la kumuua Makabrasha....hata
kama sio yeye aliyefanya hivyo, lakini alishiriki kwa namna moja au nyingine...’akasema
huyo mtu wa usalama.
‘Sawa kama mumefikia huko, siwezi kuwapinga, ila kwa vile
bado hamjakamilisha uchunguzi wenu, basi mimi naomba huyu mtu msimchukue, mimi
namdhamini kwa kauli, tu, namfahamu sana shemeji yangu huyu, siku mukimuhitaji,
nitahakikisha anafika huko kituoni,...’nikasema na wale watu wa usalama
wakakubaliana na mimi wakaondoka, na mimi nikabakia na shemeji yangu.
‘Shemeji sasa umefanya nini?’ akaanza kunilaumu.
‘Ndivyo ulivyotaka wewe iwe hivyo, na kuna mambo mengi bado nayahitaji kutoka
kwako, usiponijibu leo, mimi nitawaambia hao watu waje wakuchukue, ila nataka
tuyaongee mimi na wewe kwanza, ukiniambia ukweli, mimi nitajua jinsi gani ya kukulinda,...’nikasema
‘Mambo gani tena hayo shemeji hapa nilipo nimechanganyikiwa
nafahamu kaka atakuwa ananisubiri na nimechelewa kwenda kumuona?’ akauliza kwa
wasiwasi.
‘Nataka kumjua huyo mwanamke aliyezaa na kaka yako’nikamwambia
‘Shemeji mbona huyo mtu mimi simjui, na kaka hajazaa na
mwanamke yoyote, hizo ni ndoto zake tu,....waakti wmingine anawaza, na kwa vile
alikuwa akitarajia kupata mtoto wa kiume, basi nahisi mawazo yake hayo
anayapeleka kwenye hali halisi, ...mimi simjui’akasema
‘Una uhakika na hilo jibu lako, maana nikigundua kuwa
unanificha, basi sitakuamini tena, unanifahamu nilivyo, ninapokuahidi kitu,
siachi kutekeleza, na ukinidanganya, siwezi kukuamini tena, na lile nililoahidi
dhidi yako huwa sirudi nyuma.....’nikasema na yeye akaa kimiya, nikasema
‘Sawa kama hutaki kuniambai huo ukweli, mimi bado nalifuatilia
hilo, kama nitagundua kuwa unafahamu au unahusika kwa hilo, kwa namna yoyote
ile, basi, mimi na wewe hatutakuwa marafiki tena,tutakuwa kinyume chake,...sitakutambua
kama ndugu yangu wa karibu tena, , japokuwa nimejitolea kadri ya uwezo wangu hadi
ukafikia hapo ulipo, sitaajli hayo, kwani hata hivyo, nina maana gani kwenu,
mumenichukulia kama ngazi yenu ya kupaat mlichokitaka...’nikasema
‘Shemeji kwanini unataka kuniweka mimi kama rehani, mume
wako yupo, ndiye muhusika mkuu, kwanini usimsubiri apone uje umuulize yeye
mwenyewe, ukiniuliza mimi maswali kama
hayo ya mtego unaniweka mimi mahali pabaya,...nakuomba unielewe hivyo,..mimi
nafanya mengi kwa shinikizo, najikuta sina jinsi,...’akasema na mimi nikawa
nimemuangalia tu, halafu akasema;
‘Hivi shemeji, hebu niambie haya niliyoyaongea leo hapa kwa
hawa watu wa usalama, je akija kuyagundua haya niliyoyasema hapa itakuwaje, ...mimi
najuta sana, nimeshindwa ...oh, nimemsaliti kaka yangu, kaka ambaye ananipenda
sana, na ambaye kajitolea kwa hali na mali kwa ajili yangu...’akasema
‘Ina maana kaka yako ndiye aliyejitolea kwa hali na mali juu
yako, unakumbuka mwanzoni kaka yako alikuwa akisemaje juu yako, alikuwa
hakuamini, alishakuweka kwenye kundi la wavuta unga,mimi nikajitolea na
kumhakikishia kuwa nitakusaidia hadi utabadilika, je ni nani aliyejitolea kwa
hali na mali kati ya kaka yako na mimi..umesahau hayo eeh, kwasababu ya tamaa,
kuwa mtamiliki kila kitu eeh?’ nikamuuliza
‘Wote mumejitolea kila mtu kwa nafasi yake, hilo nashukuru
sana, ndio maana kuna mambo ambayo nimekuwa siyafurahiswi kuyafanya, au kuona
unafanyiwa, na ndio maana nikajitolea na mimi kule kunapowezekana, ..wewe hujui
tu ....lakini siwezi kusema zaidi, ninachoweza kusema kwa sasa ni ahsante kwa
wema wako huo..hata kama unaona kwasasa namukuwa sio mtiifu kwako, lakini sio
kwa nia mbaya, ni pale inapofikia hatu ya kuchagua kaka au wewe,hapo mimi
mnaniweka kwenye njia panda....’akasema
‘Sasa sikiliza,shemeji yangu, wewe ni mtoto wa juzi, ulipolala ndipo nilipokuwa nimelala siku nyingi, nikaamuaka na kufanya kazi,...kwahiyo sasa ni juu yako, nimewabeba kiasi cha kutosha, nimewambembeleza kiasi cha kutosha, naona sasa ni muda wenu kufanya hivyo,..jua kabisa kwasasa wewe upo kubaya, kuwa umeshirikiana na muuaji wa Makabrasha, ...unalifahamu
hilo’nikasema
‘Sijasema hivyo, ...sijashirikiana na muaji wa Makabrasha,
hivi nyie hamuelewi, jinsi gani tulivyo na Makabrasha, yule ni ndugu yetu, hivi
kuna mtu anaweza kumuua ndugu yake, na uone kaka alikwenda kuonana naye kwa
ajili ya mambo ya kisheria, yeye alijitolea kumsaidia kaka, sasa tuje kumgeuka
na kumuua, mbona haliji akilini...huo ni uzushi tu’akasema na kutulia
‘Hujasema hivyo ndio kuwa wewe ulisaidia kumuua Makabrasha,
ila umesema wewe ndiye ulichukua bastola yangu, ukaipeleka huko
ulipoipeleka,..hiyo bastola ndiyo iliyotumika kwenye mauaji,maeelzo yak ohayo yanakuponza,
hapo huwezi kukwepa mkono wa sheria baba maelezo yako uliyoyatoa hapa yanaonyesha
hivyo,...’nikasema huku nikigeuka kwenye meza ndogo iliyokuwa pembeni yetu.
‘Unaona kile kifaa pale,
kinachukua kila kitu tulichoongea hapa, kwahiyo, kwangu mimi huna
ujanja, pili nina ushahidi mwingine utakaokutia jela, ushahidi ambao, utaongea
badala yako,nina imani ushahidi huo utaniambia kila kitu...’nikasema
‘Ushahidi gani huo shemeji...’akasema huku akiniangalia kwa
mashaka.
‘Nikuulize kitu , hicho kitufe chako unahifadhia kazi za
ofisini kama ulivyodai, au kuna mambo mengine
binafsi?’ nikamuuliza
Hapo akaduwaaa, akaniangalia , na macho yakamtoka pima,
akainamana na kusema;
‘Ina maana shemeji umefikia hapo sikuhizi, mbona sio tabia
yako, kuchukua vitu vyangu bila idhini yangu...!?’akasema
‘Ni nani aliyeanza kuchukua vitu vya mwenzake bila idhini ya
mwingine, mimi sikuwa na tabia hiyo, nilikuwa nakuamini kupita kiasi, lakini
wewe na kaka yako mukanigeuka, na nimeona hakuna njia nyingine ila ni kufanya
hivyo, na nitafanya vikubwa zaidi ya hivyo, .....sikutaka kabisa kufanya hivyo..’nikasema
‘Kwahiyo shemeji unataka mimi nifanye, nini,..hebu jaribu
kuniangalia na mimi,...huku kaka huku wewe, nifanye nini, mbona mnanionea
bure, ...’akawa analalamika.
‘Shemeji mimi nakuomba tafadhali, nipo chini yamiguu yako,
kama umekiangalia hiki kitufe, naomba iwe siri yako..nakuomba tafadhali,.....’akasema
na kutaka kunipigia magoti , na mimi nikageuka kuondoka, nikisema;
‘Nimeshakupa muda wa kutosha, ...na bado hutaki kuwa upande
wangu, na nafanya haya kwa manufaa yenu, hebu fikiria jinsi kaka yako
alivyofanya, nini ingekuwa mwisho wake, unafikiri nyie mngelifaidi nini, jasho
letu lote lingeishia wapi, ....hivi nyie hamlioni hilo, au kwa vile hamna
hasara nayo, hata kama mnaona hakuna hasara nayo, lakini angalieni muda
tuliotumia, fikirieni kwa makini ..hamuaoni hiyo kuwa ni dhuluma.Mwisho wa siku
mali yote ingeenda kwa, Makabrasha, angelichukua kila kitu, na kuwaacha nyie mikono
mitupu,....’nikasema.
‘Oh shemeji,...mimi hayo nilimuonya kaka, hakunisikiliza,
kaka akiamua jambo lake, haambiliki, mpaka aone mwisho wake,...oh shemeji kama
umeangalia mambo yangu, umeniweka kubaya...’akasema huku akiangali huku na kule
‘Umejiweka mwenyewe kubaya, ..wewe na kaka yako mpo ukingoni
mwa mto uliojaa mamba, mumejichimbia wenyewe kaburi, sitaki kuwatisha, ila
nawaonya na kuwapa muda kidogo wa kusema kila kitu,bado muda mnao, jitokezeni
mseme ukweli kabla mambo hayajaharibika, vinginevyo, sijui kama kutakuwa na
suluhu juu ya hili, nenda kaongee na kaka yako, mjipange vyema...’nikasema na
kuondoka.
‘Nitaongeaje na kaka wakati anaumwa?’ akaniuliza na mimi
sikumjibu kitu, nikaondoka na kumuacha akiwa kasimama, kachanganyikiwa, na
haukujua afanye nini....mimi sikumjali, nikaondoka kuelekea ndani.
Nikasubiri kama nusu saa, nikamuona akija , lakini baadaye
akabadili mawazo, nikamuona akiondoka, huku kainama chini,alikuwa kama jogoo
aliyeloweshwa maji, akachukua pikipiki lake na kuondoka, na mimi nikaichukua
laptop yangu na kuanza kuangalia ni kitu gani kilikuwa kwenye kile kitufe,
alichokuwa nacho shemeji yangu...
NB: Kisa ndio hicho kinafikia mteremko, ndio tukaingia
kwenye hitimisho, tukiwa na maswali mengi;
‘Je ni nani aliyemuua Makabrasha, na je mdada atagundua
ukweli wa msaliti wake wa ndoa, je atatimiza ahadi yake...tusubiri tuone.
WAZO LA LEO: Kuna
watu inapofikia hatua ya kupata mali, wanapohisi kuwa kuna masilahi, wanapokuwa
na uhakika wa kupata pesa, vyeo, ....hawaangalii tena ubinadamu, wema,
unaondoka na kinachobakia moyoni ni ubinafsi,....watu kama hao wapo tayari hata
kuwadhulumu, wazazi wao, au watoto wao, au marafiki zao, achilia mbali ya bosi
kwa mfanyakazi wake. Mali , pesa , vyeo ni mtihani mkubwa kwetu, tuweni makini
kwa hilo, tuangalie na kuchunga haki ya
mtu, tuangalie na kuchunga dhamana za watu, hayo ni madeni makubwa, kama
tutahini.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment