Wakati nipo uwanja wa
ndege nikapokea simu kutoka kwa rafiki wa mume wangu akinitaka nionane naye kwa
haraka iwezekanavyo, na kwa jinsi nilivyoiskia sauti yake, ilionyesha
msisitizo.kwahiyo sikutaka kupingana naye.....
Na niliamua nifike
nionane naye hasa pale aliponielezea kuwa ana maelezo muhimu kuhusu wakili wa
mume wangu, na kwa ufupi aliniambia kuwa amegundua kuwa huyo mtu ni hatari sana, lakini hakutaka
kuniambia zaidi, akisema hayo anayotaka kuniambia hayastahili kuongelewa kwenye
simu.
Mimi namfahamu sana
huyo wakili, kuwa pamoja na kazi yake hiyo ya uwakili, lakini sio mtu
mwaminifu, na wengi wamekuwa wakimnyoshea kidole kwa mambo yake anayoyafanya,
kuwa ana mambo mengine anayafanya kwa mgongo wa taaluma yake hiyo, lakini watu
wa usalama hawajaweza kumkamata maana hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa madai
hayo..
Niliposikia kuwa
rafiki wa mume wangu ana taarifa kuhusu huyo mtu, moyoni nilisema ni yale yale
ninayoyafaham mimiu, kwa vile mwanzoni huyu rafiki wa mume wangu hakuwa na
umuhimu wa huyu mtu, alikuwa hajajihangaisha kumtafiti, sasa nahisi kafanya
uchunguzi na kumgundua jinsi alivyo, na sasa kaanza kuamini kuwa sio mtu mwema,
yeye anahisi mimi sifahamu hayo...
Hata hivyo sikutaka
kumkatisha tamaa,nikaonanifike tuonane naye, huenda kuna la ziada.
‘Huyu mtu ni hatari sana, kama tusipofanya haraka, utakuja kujijutia,
nimegundua mambo mengi sana juu yake, na sipendi niyaongelee kwenye simu,
tuonane tuongee tuone tutafanya nini, ni muhimu sana, kabla hujachelewa...’maneno haya yalikuwa yakijirudia kichwani,
na kunifanya nihamanike, kusikia kama kuna zaidi kaligundua, ....
‘Na kama lipo la
zaidi, basi kumbe ni wakati muafaka wa kumfikisha kwenye vyombo vya dola, ili
niweze kumuokoa mume wangu, vinginevyo,kwa jinsi hali ilivyo, itanibidi mimi
nifanye kazi ya ziada kumtenegnaisha na mume wangu,...na kwa vile huyu mtu kaamua
kuingilia anga zangu,basi kanichokoza waziwazi, na mimi sinabudi, itanibidi
nichukue hatua zangu mwenyewe...siwezi kumuachia aniumize, ni lazima nimuwahi
yeye kwanza....’nikawa naongea kimoyomoyo nikiwa ndani ya gari...
Endelea na kisa
chetu....
***********.
Usiku ulikuwa umeshaanza kuingia, wakati nafika ofisini kwa
rafiki wa mume wangu, nikasimamisha gari langue neo la maegesho ya mgari.
Niliingia ndani ya hospitali hiyo anayomilikiwa na huyo rafiki wa mume wangu,
na nilipofika mapokezi, niliangalia mlango wa kuingia kwenye ofisi ya huyo
rafiki wa mume wangu, nikawaona watu wachache wanasubiria kuonana naye.
Nilitaka nimpigie simu kumuelezea kuwa nimeshafika, lakini
nikaona nimpe muda, maana nitawadhulumu hawo watu wenye shida ya kumuona, wao
ni waginjwa wamefika kutibiwa, na mimi siumwi, japokuwa nina mambo muhimu na
huyo docta, ....
Na wakati natafakari hayo, mara mlango wa ile ofisi yake
ukafunguliwa, na yeye akatoka, na kuangalia sehemu mapokezi, ambapo, nilikuwa
bado nimesimama, inaonyesha alikuwa keshajua kuwa nimeshafika. Akanionyeshea
ishara ya tano, nikafahamu kuwa ananiambia nimpe dakika tano, na mimi
nikatikisa kichwa kumkubalia,...
Nikasogea sehemu ya kupumzikia wageni, kuna masofa,
nikachagua sehemu ya kukaa, ili niwe naone kule kwenye ofisi ya huyo mwenyeji
wangu,nikawa naangalia runinga. Na baada ya dakika tano, nilimuona akitoka tena,
na safari hii, alionekana akimuita mtu, nahisi alikuwa akimuita msaidizi wake, na
huyo aliyeitwa alipofika,wakaongea naye kidogo. Walipomaliza kuongea, nikamuona
akija sehemu hiyo niliyokuwa nimekaa, na aliponikaribia, akanionyeshea ishara
kwa mkono kuwa twende sehemu ambayo alihitajia tukaongee, ni kwenye chumba
kingine.
‘Kwanini usingemalizana na mgonjwa wako kwanza...naona kuna
watu wawili walikuwa wakisubiria kukuona’nikamwambia.
‘Wale sio wagonjwa, wale ni vijana wangu wamekuja kunipa
taarifa mbalimbali, hawana haraka, wanaweza kunisubiria tu..’akasema, na akaungua
mlango wa hiyo ofisini aliyotka tukaongelee, na tulipoingia, akasimama kidogo,
kama vile ananipisha, lakini, nikamuona akinisogelea, kama anataka
kunikumbatia, na mimi nikamsukuma;
‘Jiheshimu, kumbuka nafasi yako na yangu pia....’nikasema.
‘Nilikuwa nataka kukusalimia, ....kwani kusalimia kwa
kukumbatiana kuna nia mbaya,....usiwe mshamba bwana....’akasema.
‘Sawa acha niwe mshamba, lakini nafahami ni kitu gani
ninachokifanya...’nikasema.
Akaguna kidogo, na kusogeza kiti, ili mimi nikae, na
nilipokaa, yeye akasogea upande wa pili yake wa meza, kwenye kiti kikubwa,
ilikuwa ofisi yake, maalumu, kulikuwa na kila kitu muhimu cha ofisi,
akajiegemeza kichwa kwenye kiti cha kikubwa, huku akiniangalia na tabasamu
kubwa mdomoni, na mimi sikujali
nikatulia kama vile mgonjwa anavyosubiria kuhudumiwa na dakitari, kama mgonjwa
unasubiria kuambiwa na dakitari una tatizo gani, ndio aanze kuongea tu.
Nilisubiri kidogo, kumuachia nafasi hiyo ya kuniangalia,
maana sijui hawa wanaume wana tabia gani, kwa jinsi alivyokuwa akiniangalia,
utafikiri ni mtu anayemwangalia mpenzi wake, na hali kama hiyo sikuipendelea,
lakini kwa vile nilishamfahamu tabia yake, sikujali, ...nikatulia kimiya, na
aliponiona nipo kimiya sicheki nimeangalia mbele, akasema;
‘Nimekuita hapa sio kama mgonjwa, nakuona unaigiza kama vile
wewe ni mgonjwa wangu....’akasema.
‘Mhh,....’nikaguna tu, na yeye akasema;
‘Sawa ...nimekuita hapa kwasababu ya taarifa niliyoipata
kutoka kwa vyanzo vyangu vya habari, unafahamu ukiwa katika hali kama hii yetu
ya kujiajiri, hasa ukawa na miradi yenye wateja wengi ni lazima pia uwe na vyanzo
vyako vya kukupatia taarifa muhimu...na siku ile nilipoona mume wako yupo na
huyo wakili, nikaingiwa na mashaka, maana huyo wakili wake, nimeshasikia tetesi
kuwa sio mtu mwaminifu....’akasema.
‘Sawa ..endelea...’nikasema.
‘Nafahamu una kazi nyingi sana,...na hivi sana nafahamu
umetokea uwanja wa ndege kumfuatilia rafiki yako, ambaye hana habari nawe
kabisa, ....’akasema.
‘Umefahamu vipi kuwa nilikwenda huko kumfuatilia huyo rafiki
yangu, mbona unapenda kunifuatilia sana nyendo zangu, unanitafutia nini wewe ?’
nikamuuliza.
‘Nimeshakuamba kuwa nina vyanzo va kunipatia taarifa kama
nina umuhimu na jambo fulani, na kufuatilia nyendo zako ni kwa ajili ya
kuhakikishia usalama wako, na nitahakikisha nafanya hivyo,utake usitake, kwani
niliahidi mbele ya wazazi wako, na kwako pia, kuwa nitafanya hivyo, ...mimi
sivunji ahadi yangu, japokuwa wewe ulikuwa wa kwanza kufanya hivyo........’akasema.
‘Yatakushinda, hizo tuziite zilipendwa, wewe niambie
ulichoniitia masaa yamekwenda sana ..’nikasema huku nikiangalia saa yangu.
‘Aaah, okey, ni kweli, ...’akasema na kukaa vyema, halafu
akaniangalia machoni, na kusema;
‘Haya nitakayokuambia sasa hivi, ni muhimu kuliko hayo
unayoyafuatulia, nakuomba unisikilze kwa makini, hili nalifanya kwa nia njema
kabisa, ..japokuwa kuna mambo bado nayafuatilia kwa karibu, hayo mambo
yakikamilika nitakuambia ila kwasasa nataka kukuelezea jambo kubwa
tuliloligundua....kwa kukutahadharisha...’akasema, na mimi nikatulia
kusikiliza.
‘Mpendwa, sio kwamba nakulaumu, na mimi kama walivyo wazazi
wako, tulishakuambia kuhusu mume wako, kwani tabia ya watu haibadiliki,
wanaweza kujificha kwa muda, lakini wakifikia mahali fulani, yale matendo yao
hujirudia,...’akaanza kusema.
‘Na nafahamu hali uliyo nayo kwa sasa, kwani mume unampenda,
na ulijitolea kwa moyo mmoja kuonyesha jisni gani unavyompenda na
kumjali...lakini huko kunapoelekea, itabidi ufikirie mara mbili, sio kwamba
nakushauri uachane naye, hapana, ...hayo ni maamuzi yako...na sisi tupo nyuma
yako...’akasema.
‘Ndio uliyoniitia hayo....?’ nikamuuliza kwa hasira.
‘Huo ni utangulizi mpendwa.....’akasema
‘Haya sema uliyoniitia, hayo hayana maana
kwangu,...nimeshayasikia sana kutoka kwako, kutoka kwa wazazi, ...lakini
msimamo wangu ni ule ule,...msipoteze muda wenu, kama kuna zaidi, ya hayo,
najua mwenyewe ni nini cha kufanya, sihitajii usaidizi wenu, na kama kuna mbinu
ili hayo yatokee ili niweze kufanya hayo mnayoyataka nyie, hamtafanikiwa
kamwe....’nikasema.
‘Sawa mpendwa, mimi ninachotaka kukuambia kwa sasa ni kuhusu
huyo wakili wa mume wako, anayejiita wakili wa kujitegemea,kuwa ni mtu hatari
sana, na kwa sasa anashirikiana na wale wale unaowaona ni marafiki zako wakubwa...cha
muhimu ni kuwa, ukienda ovyo utahatarisha maisha yako, kwani wenzako
wamejipanga kuhakikisha wanachokitaka wanakipata, na wana tahadhari zote kuwa hawaingii
matatani, na inavyoonekana ni dili ya siku nyingi,...’akasema, na mimi nikaendelea
kutulia.
‘Natumai huyu jamaa unamfahamu kwa juu juu tu, nitakuelezea
sifa za huyu mtu, ambaye kitaaluma ni wakili wa kujitegemea, na polisi wamekuwa
wakitafuta kila njia kumnasa, kutokana malalamiko ya watu wengi, waliowahi
kufanyiwa utapeli na huyu mtu, akitumia mgongo wa taakuma yake hiyo, lakini
kutokna na ujanja wake hajawahi kukamatwa.....’akasema.
‘Unaposema huyo jamaa una maana wakili Makabrasha...?’
nikauliza.
‘Ndio huyo,...mtu huyu ni rafiki wa mume wako toka utotoni, na
tabia zao zinafanana, japokuwa mume wako
alikuja kubadilika baada ya kukuoa wewe,....’akatulia kidogo.
‘Mume wako, alikuwa akishirikiana na huyu jamaa kabla kwenye
mambo mbalimbali, unafahamu kipindi hicho mume wako alikuwa akihangaika na
maisha, kwa hiyo tunaweza tusimlaumu, ....na alipokupata wewe akaona ajitoe
urafiki na huyo jamaa,....na hili lilitokana na wewe kumjenga katika masiha
mazuri....
Ulipoona na mumeo,, jamaa huyo akawa anahamu sana ya kuwa
nanyi, hasa katika taaluma yake hiyo, akawa anaipigania hiyo nafasi kwa kupitia
kwa mume wako, lakini wewe ulimshitukia, hakukata tamaa, akawa anatafuta njia
ya kuwaingilia,...na sasa keshafanikiwa, na akiingia mhali, anaacha kilio,..anaharibu,
na mnakuaj kungundua baadaye ikiwa majuto ni mjukuu, na huwezi kumfanya kitu,
kwani anajua nini anachokifanya....’akasema.
‘Jamaa huyu, pamoja na kazi hiyo ya uwakili, lakini pia ni
mtaalmu wa elimu ya nyota, anaifahamu elimu hiyo ya nyota na mambo ya
kisaikolojia ya kumsoma mtu, alisomea mambo hayo ulaya, sijui kwanini alisomea
hiyo taaluma, wakati yeye alikwenda huko kusomea uanasheria, ...unafahamu huyu
jamaa alikaa sana huko
Ulaya,akisoma ...na aliporudi, akafungua ofisi yake ya
mwanasheria wa kujitegemea, lakini ofisi yake ilikuwa kama zile za wamachinga,
leo yupo hapa kesho yupo pale....ndio maana wengi wanashindwa kumuelewa.
Kuna kipindi watu walisema huenda ni usalama wa taifa,
lakini kwa taarifa rasimi, hana nafasi hiyo, serikali haiwezi kumweka mtu kama
huyo sehemu hiyo nyeti, huyu ni tapeli,...na kitu kinachowashangaza wengi, ni
jinis gani anavyoweza kuwalaghai watu, wakamuamini, na kumpa kazi, jinsi
anavyoweza kumuingiza mtu katika anga zake, na mwisho wa siku mtu huyo analizwa,
na bado anashindwa jinsi gani ya kumshitaki huyo jamaa.....’akasema.
‘Mimi nilipoona huyo jamaa kaingia kwa mume wako,....nikashituka,
na sikutaka kuongea na wewe hivi hivi, nilitaka kwanza nipate ushahidi, ndio
maana kwa haraka nilikimbilia kwa jamaa
yangu, ofisa upelelezi, na nikamuelezea hayo niliyoyaona na hisia
zangu....’akasema, hapo nikamkatisha na kusema;
‘Nilishakuambia mambo yangu kwasasa sitaki kuyapeleka
polisi, maana mwisho wa siku itatokea kashifa ambayo itaniharibia shughuli
zangu, na wazazi wangu wameshaniasa kwa hilo, sitaki, nije kusutwa na wazazi
wangu...’nikasema.
‘Kwa taarifa yako wazazi wako, walishakuacha, hawataki
kuingilia mambo yako tena, wakijua wewe sio mtoto tena, unaweza kujimudu,...ila
ni kweli waliniomba mimi niwe nakusaidia saidia, kuhakikisha hupotoki, na
kukuonya kuhusu maadui zaki,...kwa hiyo hilo la kuwa wazazi wako watasema hivi
au vile,mimi nakuhakikishia kuwa wao wameshanawa mikono. Ila ni kweli,wao
hawataki kashifa itakayokwenda kuwagusa wao, ukifanya ujinga wako, na kashifa
hiyo iwaguse wao, hapo utawajibika, ....hawana mchezo na hilo, nawaheshimu sana
wazee wako kwa hilo...’akasema.
‘Wewe wasema tu, mzazi kwa mtoto wake, haina mwisho, mwisho
wake labda kifo...nafahamu kabisa wananifuatalia nyendo zangu kila siku....na
kwa kupitia wewe’nikasema.
‘Kama wanafanya hivyo, mimi sijui, ...mimi nakuelezea yale
ninayoyafahamu. Nilipoongea na huyo mpelelezi, sikuwa na maana ya kulipeleka
hilo swala kwa vyombo vya dola, hapana, ilikuwa ni jinsi gani ya kupata taarifa
walizo nazo, kuhusu huyu mtu, na huyo jamaa niliyeongea naye kwa vile ni rafiki
yangu, akaniambia mambo yote ya huyu jamaa yetu, ...na ametoa tahadhari sana
kuwa tuwe makini na huyo mtu,wao kama wao , wanasema bado wanamfuatilia kwa
karibu, ila inasemakana huyu jamaa, pamoja na yote hayo, ana mtu mkubwa
anamlinda...’akasema.
‘Hilo la kusema kuwa eti ana mtu mkubwa anamlinda siliafiki,
....hamsini zake hazijafika, na kama kaingilia anga zangu tena, mimi sitajali
huyo mtu wake, sizani kama kuna mtu ana uwezo juu ya sheria....’nikasema.
‘Wote wanasema hivyo, hata huyo mpelelezi anasema hivyo
hivyo, lakini tujue kuwa hata huyo jamaa mwenyewe anajua hilo, na ndio maana
anakuwa makini kwa kila analolifanya, huyo jamaa alivyo mjanja, hajipeleki kwa
mtu ovyo ovyo, mambo yake ni kimiya kimiya, taratibu, kama tai anavyomvizia
adui yake.
Ukiona anafanya akzi fulani ujue, keshapitia kila njia, na huwezi
kumuona akijipeleka, ... mara nyingi wateja wake, ndio wanamuita....na kila
anayemuita, anahakikisha anafuata taratibu zinazokubalika kisheria, ..yupo
makini sana...’akasema.
‘Umakini gani wa kufoji mikataba ya watu, kuibadili, na
kuiba nyaraka kwenye maofisi ya watu...’nikasema
‘Unasema nini, kaiba,..haiwezekani, ....una uhakika na
hilo!?’ akaniuliza.
‘Sina uhakika wa moja kwa moja na hilo, ..lakini kwa mtizamo
wa haraka haraka, atakuwa ni yeye tu, na sitalala mpaka nihakikishe nimemuweka
ndani, na kama analindwa, basi mimi nitajua jinsi gani ya kumfanya...’nikasema.
‘Kuwa makini na kauli zako, kauli zako zinaweza kukufunga...na
usije ukatamka maneno kama hayo kwake,...nilikuona ulivyokuwa ukiongea naye
pale hospitalini, na kwa vile nilikuwa sijamjua, sikuweza kuingilia mazungumzo
yenu, lakini kauli kama zile,...usizitamke tena kwa huyo jamaa,..tamka kitu
kama una ushahidi nacho...yeye anajihami, na kwenye ule moba wake, ana vifaa
vya kurekodi, mazungumzo’akasema
‘Kwani nimesema nini kibaya hapa...ndivyo ilivyo, wewe
utaona jinsi gani nitakavyomuweka ndani, hayo maneno ya kumvimbisha kichwa,
yataishia kwenu, lakini sio mimi?’ nikasema
‘Mimi ninachokushauri ni kuwa ujue unapambana na watu walio
makini kisheria,wao wanasubiria kosa dogo, wanakunasa, huyo mtu tuachie sisi, tumeshamfuatilia, na tunajua
jinsi gani ya kumnasa, ilivyo sasa, wewe hangaika na mume wako tu na ujifanye
hujui lolote...’akasema.
‘Nitahangaika vipi na mume wangu, wakati huyo jamaa keshasema
ni wakili wake, halafu wanaponiacha hoi, na pale anaposema kuwa, hata mimi siwezi
kuongea na mume wangu mambo muhimu, yenye mlengo wa kisheria, mpaka huyo jamaa
awepo, hapo, ina maana gani, ni kuwa mume wangu na mimi sasa ni kama watu
wawili tofauti...’nikasema.
‘Ndio maana ya ule utangulizi wangu wa mwanzo, sasa hivi
mume wako anaanza kuyaonyesha makucha yake, maana anahisi kile alichokuwa
akikitaka kwako, kitapotea....na akirudi mitaani, ataadhirika, ...sasa afanye
nini, ndio maana kaamua kujiunga na rafiki yake huyo....sina nia mbaya na
rafiki yangu huyo, lakini ndivyo ilivyo, ....mimi nakujali wewe, na sitakaa
kimiya nione unaumia....’akasema.
‘Nimeshakuambia kuwa mimi sihitaji msaada wa yoyote yule,
usijiingize kwenye maswala yangu, ukafikiria kuwa nitakuunga mkono, sitaki kuja
kumbebesha mtu lawama, niachini hayo ni mambo yangu, msije mkaanza kusema,
`ooh, tulikuambia....’nikasema.
‘Usilichukulie hili swala juu juu, ...wewe unaliona kama ni
swala dogo, lakini ujue hata watu wa dola, wameshindwa kumkamata huyu mtu,
unafikiri wao ni wajinga, ya kuwa hawana njia ya kumnasa, ....hii ni kuonyesha
kuwa, hayupo peke yake, kuna watu wanamlinda,.....’akasema.
‘Sawa tutaona...’nikasema.
‘Kama nilivyokuambia hawa watu ni wajanja sana, wameliweka
hilo jambo lionekane hivyo linavyoonekana, wameanzia mbali sana,...mtaliona
kama ni swala la mapenzi, swala la mikataba...ni swa yote hayo yana nafasi
yake, lakini kwa mlengo fulani, ...sisi kwa miono yetu tunayachukulia mambo
kama yanavyotokea, lakini kwa wajanja, wameshajipanga, wanajua ni kwanini
litokee hilo, ili kufanikisha malengo yao....... tusipokuwa waangalifu,
tutajikuta tunaingia kwenye mitego yao,...’akasema
‘Ok, nimekuelewa, sasa unataka tufanye nini?’ nikamuuliza.
‘Kwanza tuwe makini, pili tushirikiane , na tatu na muhimu
sana, usimwamini mtu yoyote kwa hivi sasa...kuanzia huyo rafiki yako, na hata
mume wako,...hilo ni muhimu sana...’akasema
‘Hata wewe sio mtu wa kuaminika,.....’nikasema.
‘Unaweza kusema hivyo, ila kwa hili, mtu pekee unayetakiwa
kumwamini, kwa sasa ni mimi,...upende usipende ...mwenyewe utaona...’akasema.
‘Hahahaha..maelezo yako ya mwanzo yalikuwa ni mazurii, kuwa
nismuamini mtu yoyote, na hilo nalikubali moja kwa moja...ukisema mtu yoyote ni
pamoja na wewe, au sio....?’nikasema.
‘Sasa sikiliza, wakati tupo hospitalini, huyo wakili wa mume
wako, alionekana akiongea na rafiki yako nje ya jengo,..unalifahamu hilo,...?’
akaniuliza na mimi nilishajua hilo, lakini nilifahamu ni moja ya kazi za rafiki
yangu, nilizompa, kama ningelikutana naye ningemuuliza, na nina uhakika
angeniambia ukweli,...lakini aliponielezea mambo yake kuwa alikuwa na maswala
ya kusaini mikataba, na kakutana na wakili yake ambaye sijawa na uhakika ni
nani, nimeanza kuingiwa na mashaka.
‘Nafahamu, lakini sioni kama kuna tatizo hapo....’nikasema.
‘Huyo rafiki yako alipofika hapo hospitalini, hakuteremka
kwenye gari,alifika na gari lisiloonyesha ndani, akasimama , na wakili wa mume
wako, alipotoka, akasimama kwenye hilo gari wakawa wanaongea, ....huyo rafiki
yako alishusha kiyoo kidogo sana, kiasi cha kuweza kuongea na huyo wakili,na
walipomaliza kuongea, huyo rafiki yako akaondoak bila kuteremka...kwanini
hakuenda kumuona mgonjwa.....!’akasema.
‘Vijana wangu wakamfuatilia, wakitaka kujua ni nani huyo,
hilo gari liliendeshwa hadi mjini, na kumbe lilikuwa ni la kukodi, akaliacha
kwenye kampuni hiyo, ya kukodi magari, akatoka na kuingia ndani huko, aliingia
chooni, akabadili nguo, akatoka na kuchukua usafiri wa taksi, uliompeleka hadi
hapo anapoishi, watu wangu walimfuatilia, na wakamgundua kuwa ni yeye....’akasema.
‘Mhh, nafahamu kuwa alifika hospitalini, aliniambia mwenyewe..’nikasema
japokuwa sikuwa nina habari zote hizo.
‘Lazima angekuambia hivyo, ili kuficha ukweli zaidi,... sawa
hakuna shida, ila ninachotaka kukuambia hapo ni kuwa huyo wakili, ana kitu kinachowaunganisha,
rafiki yako na mume wako, kwahiyo wakili huyo anaongea na mume wako, halafu
huyo wakili anapeleka taarifa kwa rafiki yako...wameamua kutokukutana
....lakini kuna jambo kati ya wawili hawo’akasema.
‘Inawezekana ikawa hivyo, kwasasa siwezi kukataa moja kwa
moja,...lakini kumbuka usemi wako, ulisema nini, tuwe makini, maana
inavyonekana sivyo ilivyo, ..kweli si kweli.?’nikasema kwa kumuuliza
‘Ni sawa,..lakini cha muhimu hapo ni kuwa usimwamini tena
rafiki yako, kihivyo, ila usimuonyeshe kuwa humwamini, na kuna kitu ambacho
rafiki yako kakifuata,kutoka huko ulaya, hakuja kwa sababu ndogo, amekuja kwa sababu
kubwa ambayo, inahusiana na mume wako....’akasema
‘Unaweza kusema kaja kwasababu gani ?’ nikauliza
‘Kuna mkataba alikuja kuweka sahihi yake, ...’akasema
‘Hebu fafanua hapo..huo mkataba ni upi...?’nikasema.
‘Kuna mkataba ambao rafiki yako, alikuja kuweka sahihi yake,
mkataba huo unasimamiwa na Makabrasha,na unaweza ukawa na mafungamano na mume
wako,...lakini hilo halijathibitishwa, na kama sio mume wako, basi kuna mtu
kawekwa kati kwa ajili ya kufanikisha hilo...’akasema.
‘Lakini huna uhakika na hilo?’ nikamuuliza.
‘Hilo halijathibitishwa, ila vyanzo vyangu, vinajaribu
kuutafuta huo mkataba ni mkataba gani, na je unasema nini, ukionekana, itakuwa
rahisi kufahamu ni nini kinachoendelea, na wanaohusika ni akina nani...’akasema
‘Mimi ninahisi kuwa mojawapo wa hilo kundi ni huyo aliyezaa
na rafki yangu..au sio?.’nikamuuliza
‘Exactly...ndivyo
ilivyo....lakini huyo mtu hajabainishwa wazi ni nani, na wengi wanahisi huenda
ni mume wako....’akasema na mimi nilikuwa kama mtu aliyepigwa kibao usoni.
‘Kwa ushahidi gani?’ nikauliza, nikijifanya sijali
‘Naufuatilia huo ushahidi, ukikamilika nitakuambia, ila uwe
tayari kwa hilo, mume wako anaweza kuwa ndiye baba wa huyo mtoto wa rafiki
yako....lakini hiyo ni sehemu ndogo ya mpangi mzima...uelewe hilo, ni kama
funika macho...’akasema na mimi nikabakia kimiya, sikutaka kukataa moja kwa
moja, na sikuwa na wasiwasi wowote kwa hilo, kwani huenda watu wanasema hivyo
kwa vile mtoto anafanana na watoto wangu, ....na ...pia anafanana na mume
wangu,... hata hivyo, niliposikia hivyo, nilihisi mwili ukinyong’onyea, hasira
wivu, vilianza kunijaa mwilini, lakini nilijaribu, kujizuia.
‘Hebu nikuulize wewe , kwasababu upo karibu na mume wangu,
na umesema kuwa tushirikiane, na ili nifahamu kuwa kweli upo na nia njema, basi
niambie ukweli, je mume wangu hakuwahi kukuambia lolote, kuwa ana mtoto nje?’
nikamuuliza.
‘Hajawahi kuniambia moja kwa moja, ila anaongea kwa hali ya
shauku, kuashiria hivyo ...kiukweli hata mimi sijathibitisha hilo maana
hajaniambia moja kwa moja, na anafahamu akiniambia mimi, ninaweza kukuambia
wewe, na ingesababisha madhara makubwa, huenda kalificha hilo kwa madhumuni maalumu...’akasema.
‘Mimi bado namtetea mume wangu maana anafahamu madhara
yake...’, nikasema.
‘Madhara gani, ?’ akaniuliza
‘Yeye anafahamu sana,haina haja kukuambia...’nikasema
‘Wewe unazungumzia madhara kutokana na mkataba wenu, au sio,
huo mkataba wenu haupo tena, umeshapotea, kwahiyo kama ulikuwa na msimamo wa
kumshika mume wako kwa kutumia huo mkataba, usahahu hilo,...tafuta njia
nyingine....’akasema
‘Wewe umejuaje hayo yote?’ nikamuuliza.
‘Unataka kila mara nikukumbushe, kuwa nina watu
wanaohakikisha kuwa upo salama...’akasema
‘Yah, nimekuamini, maana umeshaafahamu kila kitu changu,
hadi sehemu ninapoficha vitu vyangu vya siri, ...lakini uwe makini nitakunasa
tu...’nikasema
‘Sijakuelewa una maana gani’akasema huku akiniangalia kwa
mashaka.
‘Utakuja kunielewa tu,...haiwezekani ufahamu mambo yangu
yote ya siri, ambayo sijawahi kumwambia mtu,...umeyajuaje, basi wewe utakuwa ndiye uliyeiba nakala ya mikataba
yangu ofisini kwangu.....’nikasema.
‘Ili nipate nini?’ akaniuliza
‘Utajua mwenyewe....’nikasema huku nikimwangalia kwa dharau.
‘Ndio maana nakuambia uwe makini sana,..mchezo huu,
unachezwa na wataalamu kweli kweli, ukikimbilia kuwashuku watu, utajikuta
unakosana na watu ambao hawana makosa, na hilo ndilo lengo la hao watu, na
mwisho wa siku unakosa kila kitu,,...’akasema.
‘Ni kweli nimeliona hilo, ....’nikasema huku nikiangalia saa
yangu.
‘Sijamaliza kukuambia yote...’akasema
‘Kwani kuna mengine tena?’ nikauliza
‘Hivi wewe unafahamu wapi Makabrasha anaishi?’ akaniuliza
‘Huyu mtu sijui anaishi wapi , ni mtu wa kuhama hama, na
nijuavyo mimi ofisi yake ipo mikononi, popote ni ofisi yake,..wakati mwingi
ukitaka kumpata, nenda ofisi za wanasheria, alikuwa anapenda sana kukaa hapo,
lakini baadaye akawa anatumia hoteli, leo hii kesho ile,..kwa ujumla anahama
hama, hana sehemu maalumu, ila ana nyumba kama tano hivi,, hutaamini hata mke
wake, hayupo hapoa Dar...’nikasema.
‘Ndivyo unavyomfahamu hivyo, au sio, huyu mtu anaishi maeneo
ya uwanja wa ndege...kuna nyumba mpya ipo karibu na majumba sita, ina
ghorofa...inasadikiwa kuwa mkabrasha ana hisa nayo...ndipo ofisi na makazi yake
yalipo kwa sasa’akasema
‘Eti nini...una uhakika na hilo?’ nikauliza huku nikisimama
‘Sasa unataka kwenda wapi..?’ akaniuliza huku akinishangaa
‘Rafiki yangu atakuwa yupo hatarini...’nikasema
‘Kwa vipi, wakati wao ni kundi moja, ...na sasa hivi atakuwa
yupo uwanja wa ndege, akijiandaa kuondoka...’akasema.
Nikakumbuka jinsi
rafiki yangu huyo, alivyokuwa akiongea kwenye simu, na sauti yake ilikuwa sio
ya usalama,kama vile anakwazwa kuongea kwa sauti, ilikuwa kama ya kunong’ona,simu
ikakatika, kama vile kuna mtu alimnyang’anya...
Hapo akili yangu ikaniambia kuwa huenda rafiki yangu huyo alikuwa
matatani, na alikuwa akiongea kwa kujificha, na bahati mbaya, huyo mtu au watu
waliomshikilia wakamuona,...sikutaka kumwambia huyu jamaa maana sikumwaminini,
nikasema.
‘Tutaongea nikirudi...’nikasema.
‘Unataka kwenda wapi, hatujamalizana...’akasema
Unataka kuniambia nini tena zaidi.....hapa tunacheza na
muda, na huenda sasa hivi tunaweza kusikia taarifa ya kifo...’nikasema
‘Cha nani?’ akaniuliza
‘Nahisi rafiki yangu atakuwa mikononi mwa huyo wakili, kwani
aliniambia mtoto wake, alitekwa nyara na watu wasiojulikana, na akalazimishwa
kusaini mkataba, hakuwa na hiyari, kwani hawo watu walikuwa na mtoto wake,
kwahiyo kusaini kwake, kungelimfanya ampate mtoto wake, na kwa vile mkataab huo
hauna madhara kwake, akaona asaini tu..’nikasema
‘Huo mkataba unasema nini, na ni kwa masilahi ya nani?’
akaniuliza
‘Hilo sio la kuniuliza mimi maana sijauona huo mkataba, na kwa
hivi sasa, ni lazima nifanye jambo..’nikasema na kuanza kuondoka, usiku ulikuwa
umetanda, giza, na mihangaiko ya watu wakirejea makazini na wengine kwenda
kwenye starehe, mimi sikuwajli hao, nikachukua gari langu kuelekea maeneo ya
uwanja wa ndege .
NB: Haya wapendwa mambo yanaanza kukorogeka,....kwa leo
inatosha.
WAZO LA LEO:
Ukisikia taarifa yoyote ifanyie kazi kwanza, hata kama unaona kuwa ni taarifa yenye
masilahi kwako, usiwe na papara nayo, inaweza ikawa nzuri kumbe ndani yake kuna
ubaya, inaweza ikawa kama asali yenye sumu ndani yake, kumbuka kuwa sio kila
taarifa ina lengo jema. Ipokee taarifa, ichunguza ukweli wake, halafu ndio
uchukue hatua stahiki.
Ni mimi:
emu-three
3 comments :
Dah najifunza mengi sana kwenye hii story je ni true story idont trust anybody nimeamini hata mume anaweza kukugeuka even friend dah dunia haina huruma nasisimka yani utasema mimi ndio huyu dada but aliamini kupitiliza yani anaelezwa ukweli but kichwa kinagoma ndugu mwenyewe anakusaliti sembuse rafiki tuwr makini sana na tumtangulize Mungu tusijiamini sisi
M3 hope utafanyia kazi ombi langu la kutuandikia hata weekend!
huyu mke wa mtu ananitia uvivu kwa ubishi asante kwa kupitia huyu tunajifunza kuwa waangalifu na watu walio karibu nasi.
Mwanamke ana hulka mbaya aisee....mbishi na mjuaji hadi kero
Post a Comment