‘Ni kweli unayoyasema,
naanza kuamini hivyo,..na hao wanaojifanya ni marafiki zangu kumbe ni maadui
zangu nimeshaanza kuwagundua mmoja mmoja,.....
Maneno haya niliyasema nilipoanza kuwashuku
watu niliokuwa nikiwaamini japokuwa moyoni mwangu nilikuwa sijathibitisha hivyo, ilikuwa kazi ngumu kwangu, kumshuku rafiki yangu ubaya, lakini kutokana na matukio yanajitokeza nilianza kuwatilia mashaka rafiki zangu, japokuwa sikujua ni yupi wa kumtilia mashaka...na kwa hali hiyo, nikawa nashindwa kufahamu ni nani rafiki wa kweli na ninani rafiki wa uwongo.
‘Hata wewe wewe mwenyewe sikuamini, ....’nilisema moyoni
pale nilipomtamkia huyu rafiki wa mume wangu maneno haya;
‘Katika watu waliokuwa
marafiki zangu wakubwa, wewe ulikuwa mmoja wapo, nikakuamini kupita kiasi, lakini
kutokana na yanayotokea hivi sasa, hata wewe mwenyewe sikuamini tena, usijifanye kuwa wewe haupo kwenye
hilo kundi la watu wanajifanya marafiki kumbe ni wanafiki, maana nimekugundua kuwa wewe unauma na kupulizia,...upande mmoja unajifanya rafiki upande
mwingine, upo kwenye maadui zangu,...’
Nilimwambia hivyo
kwasababu kubwa, kwamba yeye anafahamu ukweli, lakini hataki kuniambia huo ukweli, kuna mambo mengi
anayafahamu dhidi yangu, lakini kwasababu zake binafsi aliamua kunificha,sasa ni urafiki gani huo, na nidio maana nikamwambia:
Yeye nimeshafahamu kuwa ana ajenda zake za siri na ya kuwa, kuna jambo analitafuta kwangu, ..'
Ili kumvunja nguvu kabisa nilimwambia;
'Nyie siwajli, na wala siwaogopi, nitapambana nanyi, mmoja baada ya
mwingine....hilo nawathibitishia...’ Niliongea kwa kujiamini, na yeye
ananifahamu kuwa sitanii,...
Sasa je kweli nitaweza kutimiza hayo kivyangu
vyangu....
Tuendelee na kisa chetu....
***********
Nilipotoka pale hospitali, niliendesha gari huku akili yangu
haijawa sawa, kitu ambacho nilikuwa sikipendelei, hasa baada ya kuona ajali ya
mume wangu, ambayo kwa wengi ilionekana kuwa aliipata kwa kuchanganyikiwa,...na
sio kwasababu ya ulevi, hakuonekana amelewa, baada ya hiyo ajali. Na siku ile
hata mimi ningejikuta kwenye ajali, kwa jinsi nilivyoendesha gari.
Kwa hali kama hiyo, ikanibidi niwe na tahadhari,nilishaamua
kuwa makini sana nikiwa barabarani. Na hata
hivyo, japokuwa nilijitahidi
kuendesha kwa tahadhari, lakini bado akili yangu ilikuwa kwenye mawimbi ya
mawazi, na hata wakati naingie kwenye barabara kuu, nilikuwa sijapangai
nielekee waoi kwanza.
Nilitakiwa nifike nyumbani, maana kulikuwa na mambo
nilihitajika kuyachunguza, lakini pia nilihitajika kwenda kuonana na rafiki
yangu, ambaye tangu afike kutoka huko masomoni, nilikuwa sijaonana, naye, na
nilitumaini kuwa yeye, anaweza kunisaidia kwa haya yanayotokea,...sikufahamu
kwanini karudi haraak hivyo,
Nikaona bora nifika hapo anapoishi huyo rafiki yangu, kwani
sehemu ile ya mwanzo, alishahama, na baadhi ya vitu vyake vipo kwangu, kuna
chumba alichukua kwa dharura, na kuweka baadhi ya vitu vyake, ni kwa ndugu
yake, na niliwaza hivyo nikaongeza mwendo wa gari hadi nikafika hapo anapoishi.
Nlipofika hapo niliambiwa hayupo, walisema rafiki yangu huyo
aliaga kuwa anakwenda hospitalini kumuona mgonjwa, na aliondoka
muda,nikashangaa, kwani kama likuja kumuona mgonjwa, ambaye ninahisi ni mume
wangu, basi tungelikutana huko.
‘Na mtoto yupo wapi?’ nikauliza.
‘Mhh, hayo utamuuliza mwenyewe, hatujui....’akasema huyo
ndugu yake.
Basi nikaona hakuna haja ya kupoteza muda, nikaamua kurejea
nyumbani kwangu, nilipofika nyumbani kwangu nikaanza kuwahoji, watu kuanzia
mlinzi hadi wafanyakazi wa ndani, kama kuna mtu yoyote aliwahi kufika hapo,
kabla, ambaye walimtilia mashaka, au kunitafuta mimi au mume wangu, nikaambiwa
hakuna, nikaona nifanye jambo moja kwa haraka, sikupendelea kufanya hivyo,
lakini nikaona ndio muda pekee ninaoweza kufanya jambo kama hilo,
Nikaanza kupekua vitu vya mume wangu, sehemu zote nyumba, au
kile chumba alichokuwa akipendelea kulala, kwenye nguo zake,kama ninaweza kupata
kitu chochote cha kunisaidia,lakini sikuweza kupata kitu chochote cha maana,
mwishowe nikaona nirejee kwenye maktaba niangalie vyema.
Nikafungua tena lile kabati langu, safari hii kwa uangalifu
kidogo, na cha ajabu niliona ile nakala ya mkataba wangu na mume wangu, ukiwa
umewekwa pale pale nilipopendelea kuuweka,...kwanza sikuugusa, nikachuka kitu
cha kuzuia alama za vidole mkononi, nikaanza sasa kuukagua huo mkataba, kwa
haraka nikagundua kuwa sio ile nakala yangu, maana ile lama niliyokuwa nimeweka
haikuwepo,
‘Hii nakala imewekwa baadaye....sio ile nakala yangu.’nikasema
,
Nilichukua ile nakala na kuanza kuipitia kwa haraka haraka,
sikuweza kugundua mabadiliko, sijui kwa vile muda huo sikuwa nimetuliza
kichwa,...nikaona nipumzike kwanza, na wakati napumzika nikagundua kitu, kwenye
sehemu ya kipengele cha watoto, ....nikaanza kuisoma sehemu hiyo kwa makini,
ilikuwa sio kazi rahisi, ila niligundua sehemu moja, inasema hivi;
‘Watoto wote wana haki
sawa, na mali ya urithi , itagawiwa sawa, kama wazazi watakuwa wamefariki,...’hili
neno `wote’ sikumbuki kama ilikuwa hivyo mwanzoni, nakumbuka tulitumia neno `wetu’
na hili neno wetu kwenye ufafanuzi tuliandika, kuwa linasimama badala ya
wanandoa mimi na mume wangu kwa kutaja majina. Nikafungua kwenye ufafanuzi,
sehemu ya huo ufafanuzi, ilikuwa imeondolewa....’
‘Kwanini wafanye hivyo, na ni nani huyu, ni mume wangu na
wakili wake....mmh, nahisi kuna jambo, nimewapata sasa....’nikasema kwa kujipa
moyo.
Hapo nikaanza kuingiwa na mashaka, kumbe nia yao ilikuwa
kubadili huo mkataba, nikaanza kusoma tena sehemu nyingine kuna sehemu zimeondolewa
na kuongezwa maneno mengine ili kuleta maana fulani, sikuelewa ni kwanini
walifanya hivyo.
Nikafungua sehemu nyingine lakini sikuweza kugundua
mabadiliko mengine, japokuwa nilihisi kuwa kuna sehem fulani fulani
zimebadilika, lakini kiutalaamu zaidi, na hapo nikaona niwasiliane na wakili
wangu, nikampigia simu.
Simu iliita kwa muda bila kupokelwa, na baadaye akaipokea,
na kusema alikuwa akimsaidia mgonjwa, maana alikuwa kwao, akimuuguza mzazi
wake, nikamwambia hayo yaliyotokea, na akasema;
‘Kuna mtu ana nia mbaya, maana mimi nilipoondoka tu, nilipata
taarifa kuwa kunawatu waliingia ofisini kwangu wakaiba baadhi ya vitu, sasa
sina uhakika kama ni pamoja na hiyo nakala ya huo mkataba, ni mpaka nikirudi
huko.....’akasema.
‘Kumbe lengo lao ni kuhakikisha kuwa wameiba nakala zote, je
kwenye mtandao hukuhidhi chochote?’ nikamuuliza.
‘Katika vitu ambavyo nasikia wameiba, ni pamoja na komputa
yangu ambayo nimehifadhia mambo yote, na sikumbuki kuhifadhi sehemu nyingine
zaidi, maana sikuwa na mashaka kuwa hali kama hiyo inaweza kutokea, hii ni
changamoto kwangu, kazi zote sasa nitaziweka kwenye mtandao ya kudumu...japokuwa
napo kuna matatizo yake, huwezi kuwa na uhakika wa usiri’akasema.
‘Sasa kama nakala ya huo mkataba imechukuliwa huko kwako na
komputa imeibiwa, tunawezaje kuipata nakala nyingine wapi, maana nahisi
wamebadili huu mkataba kwa makusudi maalumu, na cha ajabu wameweza kutumia
sahihi yangu kama ilivyo,..ina maana huyu mtu ni mtaalamu kweli wa kunakili
sahihi za watu....’nikasema.
‘Kama wameamua kufanya hivyo, basi nina imani kuwa hata huko
serikalini watakuwa wameshafanya hivyo hivyo,watakuwa wameshabadili huo mkataba
na kuweka huo wanaoutaka wao,....’akasema.
‘Kwa vipi sasa, ?’ nikauliza
‘Unafahamu hali ilivyo, kama una pesa lolote linaweza
kufanyika, sina uhakika sana, wanaweza hata wasitumie pesa, wakatumia ujanja
ujanja....cha muhimu nataka niipate hiyo nakala mpya waliyoitengeneza wao, ili
na mimi niupitie upya,mimi nitagundua ni sehemu gani wamebadili, na kwanini...fanya
kila juhudi unitumie hiyo nakala, haraka iwezekanavyo?’ akaniuliza.
‘Kwanza nitakutumia kwa mtandao..nitainakili kwenye mtandao
na kukutumia kwa njia hiyo, halfu nitatoa nakala nyingine, na kukutmia kwa njia
ya DHL, huko kuna ofisi zao, kama hakuna nitakutumia kwa njia ya mabasi,
......’nikasema,
‘Itakuwa vizuri, kama hatujachelewa....’akasema na kauli
yake hiyo ilinikatisha tamaa.
***********
Wakati nataka kuondoka nyumbani, nikakumbuka jambo, nikarudi
kule kwenye maktaba yetu na kufungua kabati sehemu ninapohifadhia silaha,
yangu, niliikuta ipo pale pale, lilinijia wazo la kuichukua niwe natembea
nayo,
kwa usalama wangu, lakini nikaona kwa vile ni mchana, hakuna umuhimu nayo,
nikaondoka hadi ofisini kwangu, na nilipofungua kabati langu, nikakuta nakala
ya mkataba, nikaichunguza na kugundua kuwa sio ile nakala yangu ya awali,
hakuna alama niliyokuwa nimeweka,
Nikaifungua na kuanza kuisoma, ni kama ile ile niliyoikuta
nyumbani kwangu, na safari hii nilitulia kidogo, nikagundua sehemu kubwa ya
vipengele vya umiliki wa mali, vimbebadilishwa, hapo nikaanza kuingiwa na
wasiwasi, kuwa hawa watu hawana nia njema kwangu, wameingilia hata mali
yangu,...na kwahiyo, kuna mambo mengi yamebadilishwa kitaalamu,....na hapo
nikaanza kumshuku mume wangu vibaya;
Kuna sehemu iliandikwa hivi;
‘Mume ndiye atakayekuwa muangalizi wa mali yote na mwenye
mamlaka ya mali zote, na atakuwa na uhuru wa kumuingiza mtu yoyote katika
umiliki wa mali kama atakavyoona yeye inafaa, hata bila ya idhini ya mke wake...’nikashangaa
sehemu hiyo imetoka wapi, mbona haikuwepo, na kwanini mume wangu akubali sehemu
hiyo iongezwe ni ili aweze kufanya lolote kwenye mali zetu, haiwezekani,
sikubali,...
Nikasoma maelezo mengine, lakini akili yangu ilikuwa imechafuka,
hasira zilianza kunipanda, hapo hapo nikampigia simu, tena wakili wangu
kumuulizia hicho kipengele, mbona hakikuwepo, ndipo akaniambia kuwa hawo watu
wamefanya hivyo makusudi, huenda kuna mtu wanataka kumuingiza kwenye umiliki wa
mali...
‘Kumuingiza kwa vipi?’ nikamuuliza.
‘Kwenye maelezo ya mwanzo, ilikuwa imesema kuwa hakuna mtu
atakayeruhusiwa kuingizwa kwemue umiliki wa mali, kampuni , zaidi ya wewe na
mume wako na watoto wenu. Nyie wawili mnamiliki mali kutokana na mitaji yenu na
hakuna anayeruhusiwa kumuingiza mtu yoyote kama mwekezaji kwenye mali zakifamilia....’
sasa hicho kipengele kimeondolewa, na wameweka hicho kipengele ili kumruhusu
mume wako kufanya atakavyo..’akasema wakili.
‘Kwa mtizamo huu, mume wangu ndiye yupo nyuma ya haya?’
nikamuuliza.
‘Kwa jinsi ilivyo inaonyesha hivyo....lakini huwezi kumshika
moja kwa moja, nahisi anafanya hivyo kwa shinikizo fulani, ....’akasema.
‘Kwa ushauri wako nifanye nini, nitoe taarifa polisi....?’
nikamuuliza.
‘Ukitoa taarifa polisi kwa sasa moja kwa moja, atakayekamtwa
ni mume wako, na kutokana na hali yake unaweza ukammaliza kabisa, ...’akasema.
‘Sasa nifanyeje?’ nikamuuliza.
‘Ngoja kwanza niupitie huo mkataba wote, halafu nitakuwa na
nafasi ya kusema lolote,...usijali hawo wamechukulia kienyeji sana, huwezi
ukafanya hayo waliyoyafanya kirahisi hivyo, labda wawe na mtu fulani kwenye
sehemu za uandikishaji wa mikataba hiyo , vinginevyo, kuna kitu kibaya
kinaendelea ujaribu kuwa makini, huo ni ukiukwaji wa sheria, na huyu aliyefanya
hivyo anaonekana ni mtu anayefahamu sana kazi hii ya kubadili badili maandiko
ya kisheria...’akasema.
‘Nahisi anaweza kuwa huyo wakili wa mume wangu...’nikasema.
‘Wakili gani tena huyo wa mume wako, kaamua kuchukua wakili
mwingine zaidi yangu...?’ akaniuliza
‘Ni wakili Makabrasha.....’nikasema.
‘Oh, balaa, huyo mtu tena, nakumbuka nilishawaonya kuhusu
huyo mtu, ...’akasema.
‘Mume wangu sijui kaingiwa na wazimu gani, nahisi kuna
tatizo kubwa kwa mume wangu, sio yeye, sio mume wangu ninayemfahamu, sasa wewe, utarudi lini?’ nikamuuliza.
‘Kiukweli sijui, maana hali ya mzazi wangu sio nzuri, na
siwezi kumuacha katika hali kama hii, kama hali yake itakuwa hivi, nitachelewa
sana, na ikibidi nitakuja naye huko kwa ajili ya matibabu zaidi japokuwa yeye
mwenyewe kakataa, ningelishamchukua, nije naye huko, lakini hakubali, kabisa,
yeye anasema anataka afie nyumbani kwake, kwahiyo kwa hivi sasa siwezi kusema
lolote, ....’akasema.
Nilipoona hiyo nakala imeweka hapo, nikaona nimuhoji huyu
mtu anayehifadhi funguo, nikamuita huyo mfanyakazi , Safari hii nikawa mkali,
nikamuuliza anieleze ukweli, kama kweli hakuna mtu analiyewahi kuingia kwenye
hiyo ofisi yangu;
‘Niambie ukweli ni nani ambaye aliingia ofisini kwangu,
maana nina ushahidi kuwa kuna mtu aliingia wakati mimi sipo kazini, na kuchukua
vitu vyangu muhimu kwenye kabati langu?’ nikamuuliza.
‘Bosi hakuna mtu aliyeingia,mimi nina uhakika, maana ufungua
ninao mimi, na sijawahi kuuacha popote, kama ulivyoniagiza,....’akalalamika
akionyesha wasiwasi.
‘Sasa sikiliza, kama nitakuja kugundua kuwa kuna mtu
aliyeweza kuingia ofisini kwangu, na wewe unafahamu ujue ndio mwisho wa ajira
yako, na nitahakikisha unakwenda jela...’nikasema kwa ukali na yeye akaniangalia
kwa mashaka, lakini aliendelea kukataa kuwa hakuna mtu aliyewahi kuingia,
au yeye kumruhusu mtu yoyote kuingia
kama nilivyomuagizia.
‘Sawa nitaiarifu polisi, na watafanya uchunguzi , na ujue
wewe ndie uliyekuwa na mamlaka ya ufunguo kwahiyo wewe ndiye utakayekuwa
mshukukiiwa mkuu, utalala jela hadi hapo huyo mtu aliyeinga kwenye ofisi yangu
na kuchukua vitu akapopatikana..,kama sio wewe uliyefanya hivyo’nikasema.
‘Bosi, mimi sijui lolote, na kama polisi watanikamata,
watakuwa wakinionea bure, maana sijui, na sijawahi kumruhusu mtu kuingia
ofisini kwako..nakuomba bosi, unisaidie, nasema ukweli sijawahi hata siku moja
kufanya hayo .......’akasema kwa uchungu, huku akipiga magoti, kitu
nisichokipenda mtu kunifanyia hivyo, mimi ikabidi nimwamini tu, ila nikamwambia
kuwa nifanya uchunguzi kama nitagundua kuwa anafahamu sitakuwa na msamaha na
yeye.
Akilini mwangu nilijiuliza maswali mengi ni nani huyo
angeliweza kuingia ofisini kwangu na kujua wapi nimeweka vitu vyangu vya siri,
na kuweka kila kitu, kama kilivyokuwa na aliingia muda gani maana kama aliingia
kwa uficho, basi itakuwa ni usiku , na kama ni usiku, walinzi walikuwa wapi.
Hapo nikaona niwahoji walinzi.
Niliwaendea walinzi na kuwahoji, na wote walikana kabisa
kuwa hakuna mtu angeweza kuingia usiku bila ya wao kumuona,wakasema kama ni
kuingia hko ofisi, basi itakuwa imefanyika mchana sio usiku....nikajikuta
nikikosa ushahidi wa kuwabana hawa walinzi, lakini nilihisi kwa vyovyote vile
ni lazima kuna mtu wa ndani anayehusika,hakuna mtu angeliweza kuingia hadi
ofisini kwangu, kama sio mtu anayenifahamu, na kufahamu taratibu zangu.
Sikutaka kuwahoji wale wote ninaowahisi, kama katibu
muhutasi wangu, ambaye sizani kama angelifanya hivyo,...niliona hilo swala
niende nalo kimiya kimiya, na ikibidi nitatafuta mpelelezi wa kujitegemea.
Nilimpigia jamaa yangu wa mambo ya komputa, nikamuomba
aniwekee vifaa vya kunasa matukioa ili kama huyo mtu ataingia tena aweze
kuonekana, japokuwa nilikuwa na uhakika kuwa huyo mtu hakuwa na sababu ya
kuingia tena kwani walichokitaka wamekipaa, sasa ataingia ofisi kwangu kufanya
nini....
Hapo nikamkumbuka rafiki yangu , kuwa angelikuwepo kazini
ingelikuwa ni rahisi kuyagundua hayo yote, na nilipomkumbuka nikaona nimpigie
simu, na akaipokea kama vile alikuwa akisubiria simu kutoka kwangu;
‘Nilikuwa na maongezi na wewe, tunaweza kukutana wapi?’
nikamuuliza.
‘Hata mimi nimekuwa nikikutafuta sana, ...kuna mambo
nilitaka kukuweka wazi, kuhusu ile kazi uliyonipa kabla sijaenda kusoma,...na
nimejitahidi ili tuonane, lakini imeshindikana....’akasema.
‘Kwanini ishindikane, kwangu unakufahamu, ofisini
unakufahamu, kwanini usinifuatilie huko kote?’ nikamuuliza.
‘Nilifanya hivyo, lakini ni kama vile imepangwa tusionane, maana
nilifika kwako kwa mara ya kwanza nikaambiwa haupo, mara ya pili nikaambiwa
umekwenda hospitalini niliwafuata huko, na bahati mbaya nilipofika nikaambiwa
umetoka muda huo huo,nikakufuatilia nikijua upo nyumbani,...nilipofika kwako
sikukuta,nikahisi umekuja kwangu, na nafika kwangu nikaambiwa ulifika...umetoka,
sasa nina mambo mengi yakufuatilia, na muda ni mchache sana, ...’akasema.
‘Unaonaje nikafika kwako, ...nije tuongee huko kwako, au?.’nikasema.
‘Mimi kwa sasa nipo uwanja wa ndege kwa jamaa yangu, maana
natarajia kuondoka leo usiku, nikaona nikakae kwake, ili iwe rahisi kuwahi
kuondoka , ninaondoka leo usiku, na ndege ya usiku kurudi masomoni...’akasema
na kuniacha hoi.
‘Ina maana ulikuja mara moja tu, ,..?’ nikauliza.
‘Ndio nilikuja mara moja, kwa dharura,....’akasema.
‘Dharura gani?’ nikauliza.
‘Kuna mkataba nilihitajika kuja kuweka sahihi yangu, ni
muhimu sana kwa ajili ya mtoto na mimi mwenyewe, na kutokana na wakili alisema
mimi ni muhimu nije mwenyewe ....’akasema.
‘Mkataba gani huo?’ nikauliza nikihisi kichwa kikizunguka.
‘Ni mkataba wangu na huyu mtu....aliyenibebesha mimba, naona
kang’ang’ania niingie mkataba naye, kwa ajili ya mtoto, sikupendelea nilitaka
mambo ya mtoto yasimuhusishe yoyote, lakini naona kang’ang’ania na hata
kunitishia kunishitaki, nikaona isiwe taabu kama ndivyo anavyotaka, mimi sina
shida ilimradi tu mtoto wangu asichukuliwe....’akasema.
‘Huyo mtu ni nani?’ nikauliza kwa ukali.
‘Kwa hivi sasa siwezi kukuambia, maana naona hali
imeharibika...nikirudi kutoka kwenye masomo nitakuambia kila kitu, maana
haitakuwa na haja ya kukuficha, ila kwasasa kwa vile kuna mambo ya kisheria
yanayofuataliwa na wakili wangu, sistahili kukuambia lolote...’akasema.
‘Na mtoto wako yupo wapi?’ nikamuuliza.
‘Natarajia kuletewa leo......’akasema
‘Sijakuelewa, kwanini unasema unatarajia kuletewa leo, kwani
alikuwa wapi?’ nikamuuliza.
‘Alichukuliwa kama dhamana,....waliponiita, kwa ajili ya
kuweka sahihi ya huo mkataba, sikufahamu kama itakuwa hivyo, na nilifahamu kuwa
lengo lao ni jema tu, siku nilipofika nikiwa nyumbani kwangu, wakati nipo
bafuni naoga, walifika watu nisiowafahamu, wakamchukua mtoto wangu..nilichanganyikiwa,
maana kwa muda huo sikuwa na mfanyakazi wa ndani, ...mtoto nilimuacha kalala
chumbani,lakini baadaye wakanipigia simu, kuwa kama namtaka mtoto wangu, akiwa
hai basi nifanye wanavyotaka wao, nikawaulize nifanye nini......’akatulia.
‘Kuna mambo mengi walitaka niwafanyie, sitaweza kukuambia
yote kwa sasa, ila moja wapo ikawa kuweka sahihi kwenye huo mkataba,
...’akasema.
‘Mkataba gani huo, na una nini ndani yake?’ nikamuuliza.
‘Una mambo mengi sana, lakini muhimu ni kuwa mtoto huyo,
atakuwa na haki sawa na watoto wengine..maana huyo mtu ana watoto wengine..na
yeye kutokana na huo mkataba kwasasa atatambulikana kama baba yake halali, ina maana mtoto wangu kwasasa ni mtoto wake halali,, na ana haki sawa ya kurithi mali ya baba yake, .....'akatulia kidogo, na moyoni nilimpongeza kwa hilo
'..na kwa
vile ni mtoto wa kiume, yeye atapewa kipaumbele cha kusimamia mali yote, hapo
umri wake ukifika,.... lakini kwa vile bado ni mdogo, mimi mama yake, nimepewa
uhalali wa kusimamia mali zake..'akatulia kidogo, halafu akakohoa na kusema;
'Mimi sikuona ugumu wa hilo, na sikuona kwanini
nisitie sahihi yangu kwa ajili ya makubaliano, hayo, lakini sikupenda kufanya
hivyo,ila ni kwa shinikizo,....maana sio halali, sio mali iliyotokana na jasho langu, ..ooh.’akasema.
'Sasa kwanini ukatae, na ni kwa masilahi ya mtoto wako?' nikamuuliza
'Hebu nikuulize wewe, kama ingelikuwa wewe, unasikia mwanamke, anakuja kurithi mali yako ya jasho lako kihivyo ungelikubali?' akaniuliza.
'Mali yangu mimi, thubutu...usiongelee mali yangu, hayo ni yenu, na wewe hujataka kunishirikisha, ila nakuuliza hivi, tena na tena..'nikatulia kidogo
‘Ni nani huyo baba wa mtoto wako, mbona inakuwa siri, au
....’nikamuuliza na mara simu ikakatika,ilionekana kama kakatishwa na mtu,
...nilijaribu kupiga tena , lakini ikawa haipatikani,...nikaona nitafute ndugu
wa huyu rafiki yangu anayeishi huko uwanja wa ndege, lakini sikuweza kumpata
ndugu kama huyo, ila nikaona niende huko huko maeneo ya uwanja wa ndege huenda
nikaonana naye, lakini haikuwa kazi rahisi.
Moyoni nilihisi huyu rafiki yangu yupo matatani, ni kama mtu kamnyang'anya simu, ili asiendelee kuongea, na sikujua nifanye nini, niliogopa kabisa kuwahusisha polisi, maana sikujua niwaambie nini...na wakati nawaza mara simu yangu ikalia,...nilipoangalia ni nani anayenipigia nikagundua kuwa ni rafiki wa mume wangu;
'Upo wapi wewe, nakutafuta sana.....'akasema.
'Unanitafutia nini?' nikamuuliza kwa sauti ya chuki.
'Kuna mambo muhimu sana, nataka kuongea na wewe....'akasema
‘Mambo gani?’ nikamuuliza kwa mkato,niliona kama ananipotezea muda wangu.
‘Kuhusu huyo wakili wa mume wako.....’akasema
‘Ana nini huyo wakili wa mume wangu..hebu ongea moja kwa moja?’ nikauliza
‘Huyu mtu ni hatari sana, kama tusipofanya haraka, utakuja
kujijutia, nimegundua mambo mengi sana juu yake, na sipendi niyaongelee kwenye
simu, tuonane tuongee tuone tutafanya nini, ni muhimu sana, kabla
hujachelewa...’akasema na sauti yake ilinitia mashaka, inaonyesha msisitizo
...’nikasema;
‘Nitakuja nyumbani kwako....’nikasema.
‘Hapana, njoo ofisini kwangu....’akasema
‘Sawa vyovyote utakavyo, nipo njiani, nakuja....’nikasema na kuingia kwenye
gari , sikujali tena mambo ya rafiki yangu.
NB: Sehemu hii ina mambo mengi sana yalitokea, ngoja kwa leo
tuishie hapa
WAZO LA HEKIMA:Usalama
wa majumbani kwetu, usalama wa watoto wetu, au usalama wa maofisini, ni muhimu
sana, na ni vyema, vitu kama ufunguo, ulinzi, na usafi, vikapewa kwa watu wanaoaminika,
kwa mkataba maalumu. Tatizo kubwa lililopo, ni kuwa watu hawo hawalipwi vizuri,
na kutokana na hali ngumu za kimaisha, ni rahisi kwao kushawishiwa na
kurubuniwa kwa pesa ndogo tu. Cha muhimu ni kuwajli sana hawa watu, na
kuwatimizia mahitaji yao muhimu, ili waione hiyo kazi kama yao.
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
Hello, i believe that i noticed you visited my weblog thus i got here to go back the want?.I'm attempting to in finding issues to
improve my website!I guess its ok to make use of a few of your ideas!!
Howdy very cool web site!! Man .. Beautiful .. Amazing .. I will bookmark your
blog and take the feeds additionally? I'm satisfied to search out a lot of useful information here in the post, we want work out more techniques in this
regard, thank you for sharing. . . . . .
Post a Comment