Siku hiyo nilikuwa
nimekaa nyumbani, sebuleni, na mume wangu alikuwa amelala chumbani baada ya
kupata dawa. Dawa hizo huwa akishazitumia, zinampa usingizi mnzito. Na
nilipohakikisha amelala, niaona nitoke kidogo nje, na ikibidi nifike madukani,
lakini wakati najiandaa kufanya hivyo, nikasikia hodi, mlangoni.
Kwanza ilibidi nigeuke huku na kule kumwangalia mfanyakazi
wangu wa ndani, kwani msaidizi wangu alikuwa katoka kidogo,, nilihisi anaweza
kuwa ni mgeni wao, maana mimi muda kama huo wengi wanafahamu kuwa nipo kazini...kabla
sijafungua mlango, nikachungulia kupitia dirishani, nikagundua kuwa kumbe ni
mdogo wa mume wangu.
Kwanza nikataka nimzuie asiingie ndani, kwani sikutaka mtu
yoyote kumsumbua mume wangu, japokuwa nafahamu kuwa mdogo wake, atakuwa
analifahamu hilo, lakini moyoni nilikuwa na hamu sana ya kuongea na huyu mtu, na
nikaona huenda ndiyo nafasi pekee ya kujua lolote kuhusu kwa shemeji yangu
huyu..hata hivyo sikutaka kufanya jambo ambalo ninaweza kujijutia baadaye
nikikumbuka onyo kutoka kwa rafiki ya mume wangu.
Hata hivyo, japokuwa nilijua kuwa mume wangu kalala fofo
kutokana na hizo dawa, lakini sikuwa na uhakika hizo dawa zinaweza kuchukua
muda gani kabla mue wangu hazijazindukana,na mara nyingi akiwa hana usingizi,
hapendi kukaa ndani, anapenda kuzungushwa nje na kigari chake cha kukokotwa.
Nikaona nitumie muda kidogo kuongea na huyu mtu, lakini kwa tahadhari.
Baada ya kuwaza hivyo,nikafungua mlango, na kutoka nje, nilihakikisha
nimeusindika mlango nyuma yangu, na nikawa naangaliana uso kwa uso na shemeji
yangu huyu, ambaye inaonekana hakutarajia kuniona hapo nyumbani, akabakia mdomo
wazi akishindwa hata kuongea, nikatabasamu ili kumuondoa wasiwasi, na yeye kwa
aibu akatizama chini..
‘Habari yako shemeji, mbona unaonekana kama umeona kitu cha
kukuogofya, hukutarajia kuniona mimi nini, au una wasiwasi gani?’ nikamuuliza
‘Ni kweli, sikutarajia muda kama huu hapa nyumbani, nafahamu
muda kama huu upo kazini....’akasema.
‘Hapa ni nyumbani kwangu bwana, naweza kuja wakati wowote, kwahiyo,...unaogopa
kuniona nipo hapa nyumbani, au kwanini unaonekana kuwa na wasiwasi, kuna nini
kinaendelea kati yako na mfanyakazi wangu?’ nikamuuliza.
‘Hakuna kitu shemeji, na mfanyakazi wako hakuna kitu kabisa
...mimi hufika hapa kwa ajili ya kumwangalia kaka, na kama kuna lolote la
kusaidia, nasaidia, ...na kwanini useme hivyo, wakati hapa ndipo nilipotafutia
maisha, ...nafika mara kwa mara....’akasema,
Ni kweli shemeji yangu huyu, alimchukua mume wangu kutoka
huko kijijini, tukawa tunaishi naye hapa kwangu, nia na lengi ni kumsaidia
kujiendeleza, haa katika kumsomesha na kumjenga kimaisha, na kwa vile kwa muda
huo alikuwa amemaliza kidato cha sita,mimi nilimshauri mume wangu tumuendeleze
ndugu yake huyo ili asome chuo kikuu.
Alipofika hapo tumamweleze nia na makusdio yetu, yeye kwa
muda huo,, hakutaka kusoma tena,alidai hata kusoma huko hadi kidato cha sita,
alisoma kwa shida sana, na kuna muda alitaka kuacha kabisa kusoma, ....maisha
yalikuwa magumu, na japokuwa kaka yake alijitahidi kumsaidia lakini yeye
alitaka kuanza maisha ya kujitegemea haraka, ili apate pesa, na kuliko
kutegemea pesa za kuomba omba...alisema yeye alishakata tamaa ya kusoma zaidi,
lakini tukapa moyo, na kumuelezea umuhimu wa elimu katika maisha yake. Mimi
mwenyewe nilijitahidi sana kumpa moyo hadi akabadilika, na akatulia na kuanza
kusoma.
Nilimwangalia alivyokuwa akipata taabu ya kutaka kujieleza ,
na baadaye akasema;
‘Shemeji hapa kwangu ni nyumbani , bila ya nyie watu wawili
sijui maisha yangu yangelikuwaje, ndio maana japokuwa nimeshapata makazi yangu,
lakini bado siachi kufika hapa, na ikizingatiwa kwa sasa kaka ni mgonjwa,
inanibidi nifike kumuona....’akasema.
‘Mhh, ni ya kweli hayo...?’ nikauliza nikimwangalia.
‘Ni kweli shemeji, mimi nyie ni watu muhimu sana, maana
nilishakata tamaa ya maisha, niliona kama maisha yangu yameshaharibika, hasa
nilipokuwa nikiwaona wenzangu wa umri wangu wakiwa na maisha
mazuri....’akasema.
‘Ni kweli, ..hata hivyo mimi sijazungumzia hilo, nafahamu
kabisa hapa ni nyumbani kwako, unaweza kufika muda na wakati wowote upendavyo,
lakini wasiwasi wangu ni kuwa unaweza ukawa unafika hapa kwa nia nyingine
kabisa, ambayo sitaifurahia, ....’nikasema.
‘Niamini shemeji, huyu mfanyakazi wa hapa nyumbani
namchukulia kama mdogo wangu, na sitafanya lolote baya dhidi yake, namjali
sana, na kumharibia maisha yake ni kosa kubwa sana kwangu....’akasema na mimi
nilimwamini hivyo, na sikuwa na nia ya kumshutumu kwa lolote kuhusu huyo
mfanyakazi, nilikuwa natafuta njia ya kumweka sawa kabla sijaongea naye lile
nililitoka kumuuliza,
‘Nakuamini sana shemeji yangu, wewe ni sawa na mdogo wangu,
....nakuona sawa kama anavyokuona kaka yako, ndio maana wakati wote nimekuwa
nikihakikisha kuwa maisha yako yanakuwa bora, ili uweze kusimama kwa miguu yako
mwenyewe, na natumai hayo yameshakamilika...na hapa ni nyumbani kwako, wakati
wowote unaruhusiwa kufika, nilishangaa tu, kukuona unakuwa kama unaogopa
uliponiona mimi...’nikasema.
‘Mimi niliingiwa na wasiwasi kuwa huenda kaka
kazidiwa,...maana muda kama huu, mara nyingi unakuwa ofisini..’akasema.
‘Hakuna tatizo kwa kaka yako , hajambo yupo ndani, kalala,
....na nisingelipenda akazindukana, akute tunaongea hayo ninayotaka kuongea na
wewe, ni kati yangu mimi na wewe tu, ....’nikasema na hapo akaniangalia kwa
macho yaliyojaa wasiwasi.
‘Unataka kuongea na mimi kuhusu jambo gani..?’ akaniuliza
kwa mashaka ikionyesha kuwa kuna mambo huenda alishaonywa, au kwa mtizamo wake,
hakutaka kuongea na mimi.
‘Usiwe na wasiwasi, sio jambo kubwa sana,....unaweza
kuja tukaongea huku nyumba kwenye
bustani, sijtachukua muda wako mwingi’nikasema huku nikitangulia kwenda kwenye
eneo la bustani ambapo ulikuwa na shemeu maalumu tuliitengeneza kwa ajili ya
kupumizikia, kulikuwa na viti maalumu, nilifika na kukaa, na mfanyakazi wangu
akafika akiniuliza kama anaweza kulete chochote.
‘Tuletee vinywaji, na hakikisha kuwa mume wangu akiamuka
unaniita mara moja....’nikasema.
‘Nitafanya hivyo dada.....’akasema.
Na mara akafika shemeji yangu bado akiwa na wasiwasi,
nikamwambia akae, na yule mfanyakazi wangu akawa anamminia kinywaji, na
alipomaliza akauliza kuna kitu gani tunahitaji, nikamwambia kwasasa hakuna,
baada ya kumuuliza shemeji yangu akama anahitaji kitafunio chochote, na kusema
kinywaji kinatosha, nilisubiri hadi huyo mfanyakazi wangu alipoondoka, ndipo
nikaanza mazungumzo.
*********
‘Mume wako anaendelea vyema, lakini nilikuwa nakushauri,
nafahamu kazi kwako ni muhimu sana, lakini pia mume wako ni muhimu, ikizingatia
kuwa hata ukiwa kazini bado mawazo yako yatakuwa nyumbani ukiwa huna uhakika
kuwa hudumu muhumu zinatolewa kwa mume wako.....’akasema docta
‘Ulikuwa unataka kusema nini docta?’ nikamuuliza.
‘Nilikuwa nataka kusema hivi, kama inawezekana,
ningelishauri uchukue likizo, angalau ya mwezi mmoja, ili uweze kuwa karibu na
mume wako, hii inaweza kumsaidia mume wako kupona haraka, na kwa faraja,.....’akasema
na mimi nikawa sina jinsi, japokuwa ni kipindi ambacho kulikuwa na kazi nyingi
ambazo nilihitajika kuzisimamia, lakini ikabidi niwaachie wafanyakazi wangu na
kuwaambia kama watashindwa kabisa wanipigie simu.
Mimi nikaamua kuchukua likizo ya mwezi mnzima, kwa ajili ya
mume wangu,...kuna kazi nyingine za kiofisi nilikuwa nazifanyia nyumbani, na
kama ni lazima nilikuwa nafika ofisini mara moja moja kusaini hundi, ...na,
labda kama kuna dharaura, niliwaambia wanipigie simu, na nitaweza kujipanga na
kufika ofisini kuzimaliza.
Baada ya wiki nikaona kumbe inawezekana, kumbe nilikuwa
nabeba mzigo mkubwa mwenyewe, kumbe ningeliweza kuzigawa kwa watu wangu na
wakazifanya itakiwavyo, japokuwa kulikuwa na makosa ya hapa na pale , lakini
mengi yalikuwa ni ya kibinadamu.
‘Kama kutakuwa na mabadiliko yoyote, au mkiona kuna hali
inamtokea isiyo ya kawaida, naomba unifahamishe haraka iwezekanavyo, na mna
bahati kwani mnaishi karibu na dakitari, huyo anaweza kuwasaidia
sana...’akaniambia akiwa na maana ya huyo dakitari rafiki wa mume wangu.
‘Ndio yeye ni rafiki mkubwa wa mume wangu, anatusaidia sana,
kama kuna lolote tunaweza kumuita yeye pia, lakini huyu ni mgonjwa wako,
tutakuwa tukikusumbua wewe .....’nikasema.
‘Sio kunisumbua hilo ni jukumu langu, na ni bora mnisimbue
kuliko kukaa kimiya au kumuita dakitari mwingine ambaye hafahamu historia ya
huyu mgonjwa....jitahidini sana kufuata masharti, mimi nina imani haitachukua
wiki nyingine tatu, kabla hajaweza kusimama tena...’akasema
‘Nitafanya hivyo
docta..’
*********
Sasa ni mwezi umepita, nipo namuhudumia mume wangu, kila
siku nahakikisha namfanyia yale yote muhimu yanayohitajika, tukisaidia na dada
mmoja niliyemchukua kama msaidizi wangu kwa ajili ya mume wangu tu, ili yule
mfanyakazi wa nyumbani asije kushindwa kazi zake nyingine, kwa kisingizia cha
kumshughulikia mume wangu.
Ilikuwa sio kazi rahisi, ikizingatia kuwa mume wangu wakati
mwingine alikuwa akitaka kuongea yale yaliyopita, yale yaliyosababisha awe
hivyo, na mimi nilishaonywa kabisa kuyakwepa kuyaongea hayo, hadi wakati
muafaka utakapofika. Na nikajitahisi sana kufanya hivyo.
Hatua kwa hatua hali ya mume wangu ikaanza kuimarika,
japokuwa ilikuwa kama hatua zile za mtoto mchanga, akaanza kuinua mguu kidogo, lakini alikuwa
hajaweza kusimama,lakini kuweza kuinua mguu akiwa amekaa ilikuwa ni hatua kubwa
sana, ila wakati wote kigari cha kukukotwa, kilikuwa ndio miguu yake...
‘Kila siku mfanyishe mazoezi, na kuna dakitari maalumu wa
mambo hayo, atakuwa anakuja nyumbani kwako mara moja moja, kwa ajili ya
mazoezi,....lakini wakati huo unahitajika uwepo karibu ili kumuonyesha
unamjali...’akaniambia rafiki wa mume wangu ambaye alijitolea kumuhudumia mume
wangu, na ilibidi tufanye hivyo, ili kupunguza gharama, na muda wa kwenda
hospitali.
‘Nafahamu huyu ni rafiki yako, na mimi naona uchukue jukumu
la kumuhudumia wewe, ..na utanipa gharama zake kila mwezi...’nikamwambia na
yeye akakubali huku akitaka shughuli zote hizo azifanya kwa kujitolea, lakini
mimi sikukubali, nikamwambia nitalipa.
‘Hii haina shida, nitafanya hivyo, kwa ajili ya urafiki
wetu, na kwa ajili ya mapenzi yangu kwako,....’akaniambia.
‘Sijakuambia ufanye hivyo bure, nataka uwe unanipa gharama zote,
bila kuficha, sitaki iwe kisingizio cha kukufanya ushindwe kuingiza kipato
chako kwa ajili yangu, nafahamu kabisa wewe upo kazini, usije na ajenda nyingine za siri...’nikamwambia.
‘Hamna shida, nitafanya hivyo mpendwa, na itakuwa vizuri,
kwani nitaweza kukudhibiti wewe usije ukafanya jambo ambalo utakuja
kujijutia...’akasema.
‘Siwezi kufanya hivyo, namjali sana mume wangu...’nikasema.
‘Nashukuru kusikia hivyo...’akasema
Mimi moyoni, nilikuwa na yangu, pamoja na kukubali hilo,
lakini nilikuwa natafuta nafasi ya kupata taarifa muhimu, kujua yote
yaliyotokea hadi kufikia hatua, hiyo, nilikuwa nimeshajipanga, lakini sikutaka
kabisa mume wangu afahamu lolote, kwahiyo nikiwa nyumbani, najitahidi kila niwezavyo,
kutokumuonyesha chochote kibaya, na nikawa najitahidi kutokuongea na mtu
mwingine,jambo lolote linalomuhusu mume wangu. Na ndio siku hiyo akafika huyo
mdogo wa mume wangu, nikaona kuwa moja ya malengo yangu yanaweza kutimia.
Na tulipokuwa peke yangu tukaanza mazungumzo na shemeji
yangu ambaye alionekana kutokuwa na amani, ....nikamwambia;
‘Shemeji, nataka tuyafupishe mazungumzo yetu iwezekanavyo, kwani kaka yako
akiamuka natakiwa niwe naye karibu, kwahiyo nakuomba nikikuuliza swali
ujitahidi kunijibu kwa ufasaha, bila ya kuogopa....’nikamwambia.
‘Uliza tu shemeji.’akasema.
‘Ninachotaka kukuuliza ni mambo ya kawaida tu usiwe na
shaka...’nikasema.
‘Sawa nakusikiliza,...lakini kama ni kuhusu kaka, mimi sijui
lolote...’akaanza kwa kujitetea.
‘Usijali,....wewe utaongea tu kile unachokifahamu, sio swala
la kesi au swala la kukulazimisha kuongea kitu ambacho hukijui ,ila haya yote
nayafanya kwa manufaa ya kaka yako,sizani kama unafurahia hii hali, sizani kama
unafurahia kumuona kaka yako akiwa hivyo, na ikaja ikatokea hivyo au zaidi,
huwezi jua, ni muhimu tujue tatizo ni nini, ili tuweze kumsaidia....’nikasema.
‘Kwakweli shemeji mimi sifurahi kabisa hii hiyo, kaka amekuwa
ni kama mzazi kwangu, wazazi wetu kama unavyowafahamu, hawana mbele wala nyuma,
wewe ndiye umeisaidia familia yetu kupitia kwa kaka,sasa naogopa sana kaka sije
akaondoka..sijui itakuwaje, japokuwa nimeanza maisha lakini bia yeye nitapata
taabu sana,...’akasema.
‘Basi kama unafahamu hivyo ni vyema, tukamsaidia kaka yako,
kwani japokuwa kiafya anaendelea vyema, lakini mpaka sasa sijajua ni nini
kilichomfanya hadi afikie hatua hii, je ni jambo la dharura tu, au kuna jambo jingine
ambalo huenda bado lipo, na huenda akipona atakumbana nalo tena, je kuna mtu
alimuhadaa,kama yupo mtu kama huyo, atakuwa akimsubiria, akipona atazidi
kumuandama,kwa hivi sasa hawezi kujitokeza kwa vile kaka yako hana chochote cha
kufanya..’nikasema.
‘Unaposema hivyo unaonyesha kama unahisi kuwa kuna mtu yupo
nyuma ya hata yote, mimi nilijua kuwa ni ajali ya kawaida tu, ambayo anaweza
kupatwa mtu yoyote’ akasema.
‘Ndio najaribu kuwaza hivyo, lakini hali kama hiyo,
inahitajia mawazo ya watu wengi, hasa nyie ambao mnakuwa naye kipindi cha
mchana, kama ujuavyo, mara nyingi tumekuwa kwenye kuhangaika, na kukutana kwetu
ni usiku, je huko anapokuwa mchana kutwa, anakuwa na nani, anafanya nini, ndio
hilo nataka tusaidiane,kama kweli unamjali kaka yako..’nikasema.
‘Shemeji mimi sio kwamba mchana kutwa nakuwa naye, unafahamu
hilo, kwani hata mimi ninakuwa kwenye mishe mishe zangu,....baada ya kumaliza
kusoma, na mimi najaribu kutafuta jinsi ya kusimama mwenyewe...japokuwa
mumenisaidia sana, nisingelipenda kuwa tegemezi hadi muda huu,....kwahiyo skai
sana ofisi kwa kaka,..sipndi nifanye kazi kwenye ofisi yake, kama tulivyowahi
kuongea..’akasema.
‘Ni kweli wanandugu mkiwa kwenye ofisi moja mnaweza
mkalemaa, mkaleta udugu badala ya uwajibikaji, hata mimi nililiunga mkono wazo
lako, na nashukuru kuwa umejitahidi hadi umepata ajira, ila ninachokusisitizia,
usilemae sana kwenye ajira za watu, jaribu kuhangaika uwe na ajira yako,
ujiajiri,na kuwa na kampuni yako, utaona manufaa yake....’nikasema.
‘Ni kweli shemeji, ndio maana napenda sana kuwa karibu nawe,
japokuwa kiujuma nakuogopa, kama vile mwanafuzni anavyomuogopa
mwalimu...’akasema
Ni kweli shemeji yangu huyu, amekuwa akiniogopa, ..ni kwa
vile nilikuwa mkali sana kwake, sikutaak mchezo, nilimfanya kama mdogo wangu,
ili kuhakikisha anabadilika, na kuondokana na tabia ya kudeka,...alikuwa kaishi
na wazazi wake, akawa hajielewi, kila kitu anategemea wazazi, nilifanya juhudi
ya ziada kuhakikisha hali hiyo inamuondoka, na sasa keshaanza kujifunza kuishi
maisha ya kujitegemea.
‘Usiniogope shemeji, nia yangu ilikuwa njema kwako,
..unafahamu, hata kaka yako, angekuwa na msimamo, kama alivyokuwa awali aisingeliweza
kuingia kwenye mtgeo kama huo ...nahisi kakutana na mtu akamlemaza, ...unatakiwa ujue ni nini
unakianya, ambacho unafahamu faidia na hasara yake baadaye, bila ya
tegemezi..ndio maana nimekuwa hivyo kwa kaka yako, ..huenda hakunielewa, akaona
labda nakataa kutimiza wajibu wangu, sivyo hivyo..nataka ajiamini, nataka asiwe
lelemama..hakunielewa.’nikasema.
‘Mhh, shemei hapo hata mimi sijakuelewa, kwasababu vyovyote
iwavyo, ndoa nayo ina mahitajio yake, huwezi ukaifanya ndoa kama unavyofanya
kazi nyingine, siwezi nikakulaumu, ila nahisi kama anahisi humtendei yale
wanawake wanavyowatendea waume zao...’akasema , hapo nilitak kupndisha lakini
nikaona niende naye taratibu huenda nikagundua jambo.
‘Unahisi nimekosea nini, ...?’ nikamuuliza.
‘Mimi siwezi kukufundisha, maana sijawahi kuoa, ila nahisi
kama kuna jambo ambalo linamkwanza kaka, na nahisi nikutokana na wewe,
nikutokana na nda yenu, ...kaka huwa hapendi kuniambia mengi, na hapendi sana
kuiongelea ndoa yake, ..maana anakupenda sana, ...’akasema.
‘Unavyosema hivyo, ni kama vile aliwahi kulalamika,
ukasikia....hajawahi kulalamika mbele yako, kuwa kuna tatizo analipata dhidi
yangu?’ nikamuuliza.
‘Shemeji hapana, lakini mimi nimeishi na nyie, kwahiyo
mengine nayafahamu, wakati mwingine nilikuwa natamani kukuambia, lakini
naogopa, ...’akasema
‘Sasa usiogope, naomba uniambia waziwazi, nitafurahi sana kuyasikia hayo uliyokuwa ukiogopa kuniambia, niambie ukweli shemeji, kwa mfano unaweza kuniambia na mambo gani nilikuwa
nayafanya ambayo yanamkwaza kaka yako?’ nikamuuliza.
‘Ukaribu wa mke na mume..mimi naona kama mlijali sana kazi
kuliko, ndoa yenu,..nafahamu kazi ni muhimu sana, lakini kazi na dawa,....mimi
nimesoma dini, kuwa ndoa ni sehemu kubwa ya starehe kati ya wanandoa,
mkishachoka kwenye kazi, mnakutana kama mke na mume, mnasahau madhila yote ya
dunia,...inatosha kuwa burudisho kuliko kwenda kulewa,...sasa nahisi kaka alikosa
hilo, ndio maana akaona pombe ndiyo starehe yake...’akasema.
‘Hebu niambia ukweli maana umeishi name hapa, ina maana
kweli tulikuwa hivyo, ..hatuthamini ndoa, tukawa tunathamini kazi kuliko
ndoa,...inawezekana , sikatai, lakini huoni yote hayo yalikuwa kwa amsihali
yetu, kwa masilahi yenu pia, kama tusingelifanya hivyo, ...tusingelikuwa
hapa,..wewe hulioni hilo?’ nikamuuliza.
‘Ni kweli shemeji, lakini nakumbuka ulinifundisha kuwa ili
ufanikiwa , inabidi uwe na mipango, uwe an ratiba ya kila siku, ukiwa na
mipango, ukawa na ratiba ya kila siku, hata ukwia na shughuli nyingi kiasi gani
utazimaliza kwa wakati..ndoa ni moja ndani ya ratiba ya wandoa, sasa kwanini isitendewe
haki yake, mimi ndivyo nionavyo, sio kwamba nalaumu, sio kwamba nasema
mumekosea, ila najaribu na mimi kushauri tu...’akasema.
‘Kwahiyo wewe unahisi tatizo la kaka yako limeanzia ndani ya
ndoa, sio nje...?’ nikamuuliza.
‘Inawezekana kuna tatizo nje, mimi na wewe hatulijui, lakini
kwa uoni wangu mdogo, kama wanandoa watajitahidi kuondoa matatizo yao ndani ya
ndoa wakawa na amani na upendo, basi hali hiyo ingewawezesha kutenda mambo
mengine ya nje, kwa amani, kwasababu, kwanza huyo mtu, atakuwa katuliza kichwa
chake, hana msononeko...'akasema
'Pili, kuna baraka za mungu, na tatu, mnakuwa kitu
kimoja, na umoja ni nguvu, ...sizani kama kaka angelidanganyika kirahisi hivyo,
kama wewe nay eye mngelikuwa kitu kimoja..., kama kweli kuna mtu kama huyo nje
kama ulivyodai.....mimi ndivyo nionavyo shemeji’akasema.
‘Shemeji nimekuelewa sana, na nashukuru kwa kuwa mkweli
kwangu, sasa mimi nimekubali kuwa huenda nilikuwa nafanya makosa,na kwahiyo
nitajitahidi sana kujirekebisha, nitahakikisha natimiza wajibu
wangu,...japokuwa mimi nilifanya hivyo kwa nia njema kabisa, lakini huenda
nilivyotaka mimi watu hawakunielewa, na itakuwa ngumu kueleweka...kwa minajili
hiyo basi, naona kwa masilahi ya wengi, nijirudishe nyuma, nifanye mnavyotaka,
nifanye wanavyotaka wengi, kwangu haina shida...’nikasema.
‘Lakini shemeji sijasema ubadilike na kuacha juhudi zako ya
kazi,kazi ni msingi wa maendeleo ....mimi nimetoa kama ushauri, kwa jinsi
nionavyo mimi, kuwa msijichoshe sana
kwenye kazi, jaribu kujiliwaza kama mke na mume, tokeni pamoja, tembeeni siku
moja moja pamoja, kazi zipo na hazitaisha,...kwanini mjichoshe saana,...huenda
mimi nimekosea, lakini nimetoa yale ninayoona moyoni...’akasema.
‘Ni kweli, ni mekuelewa, na ulivyosema ni muhimu sana, hata
mimi nimeliona hilo ....sasa sikiliza, pamoja na hayo, kuna mambo nataka
kukuliza, baadhi nitakuuliza hapa, lakini mengina nahitaji muda maalumu wa
kuongea na wewe, sio hapa...’nikasema
‘Kuhusu kaka?’ akaniuliza akionyesha wasiwasi, na nilimuona
akiangalia , kama vile kaona kitu nyuma yangu, mimi sikujali, maana namfahamu
sana shemeji yangu huyu, niliendelea kumkazia macho. Nikasema;
‘Ni mambo ya kawaida, kuhusu kaka yako, kuhusu mimi, kuhusu
huyo ambaye hajulikani,....nahisi kuna mtu mwingine kati yetu, sijawahi kuwaza
hivi kabla, ila nimelazimika kutokana na haya yaliyotokea, ..sijawahi kumshuku
kaka yako vibaya, hata siku moja, na hata sasa hivi sijaamini kuwa kuna mtu
katikati yetu....lakini kwa vile watu wanasema, kwa vile hali kama hii
imetokea, inabidi na mimi nianze kuwa na mashaka ..’nikatulia kidogo.
‘Ingawaje mimi sipendi kufuata fuata sana watu, huwa nina
tabia ya kuamini, wale ninaoona ni marafiki zangu. ...Mume wangu namwamini
sana, halikadahalika wewe na rafiki zangu..lakini naona kuna kitu
kinachoendelea kwa siri, na kinanitia mashaka. Kuna sintofahamu inayoendelea,
na hiyo sintofahamu inanitia mashaka, ...mimi sipendi kukaa na mashaka, sio
kawaida yangu, ndio maana nawaamini watu, ila ikitokea hali kama hii, inabidi
nifanye jambo.....’nikasema
‘Unataka ufanye nini shemeji..mbona ni ya kawaida tu, hayo
yaliyotokea kwa kaka ni ajali tu, kama kuna mengine, ni ya kawaida tu,
yataisha, sioni kwanini mkosane na kaka , shemeji kaka yangu anakupenda sana..’akasema
kwa unyonge huku akitamani kunipigia magoti.
‘Sijasema kaka yako hanipendi, na wala sina mawazi hayo, na
sijawahi kufikiria hivyo, ila ninachotaka ni ukweli...na nisipoambwa ukweli,
kutoka kwako, kutoka kwa rafiki ya kaka yako, kutoka kwa rafiki yangu, ni nani
mwingine ataniambia ukweli. Na kama mnafahamu ukweli mkanificha, nitajua kuwa
ninaishi na watu wanaojifanya ni marafiki kwangu kumbe sio, kumbe ni wanafiki.....na
kama ni hivyo, ina haja gani ya kuishi na watu kama hao, ambao nawasaidia,
lakini hawataki kunisaidia mimi...’nikasema na hapo nikamfanyashemeji yako
aniangalie kwa macho yaliyojaa uwoga.
‘Sasa sikiliza, mimi ninakupa wewe muda wa kuyatafakari haya
kwa makini, nitaongea na wewe tena
kesho, lakini sio hapa nyumbani, nataka tuyaongelee haya na mengine ofisi
kwangu,....’nikasema.
‘Kuhusu nini tena shemeji..mimi naona kama tumemaliza, sina
jingine ninalolifahamu’akalalamika.
‘Nimefurahia sana maongezi yako ya leo, hatujawahi kukaa na
kuongea hivi, ukaniambia ukweli kutoka moyoni mwako,,..nimefurahi sana, na wakati
wote ninakuona kuwa ni mtu mwema, unayejali, wale wanaokujali, nimefurahi
sana...’nikasema.
‘Nashukuru sana shemeji, kama umenielewa, na mimi ninakujali
sana shemeji zaidi ya unavyofikiria wewe, sitaki wewe na kaka mkosane,ningelifurahi
ninawaone mnaishi kwa raha wakati wote....’akasema.
‘Kama ni hivyo basi, kama kweli hayo yanatoka moyoni
mwako,naomba tusaidiane kwa hili.....unisaidie ili nimsaidia kaka yako, ili
nifanya yale yanayostahiki kwa kaka yako, kwanza nimekubali ushauri wako,
naahidi kuwa nitabadilika na kuwa mke mwema, au sio....?’nikasema na nikawa
kama namuuliza.
‘Lakini shemeji wewe ni mke mwema, kila mtu anafahamu hilo,
hata wazazi wangu wanakusifia sana..’akasema na mimi sikujali maelezo yake,
nikaendelea kusema;
‘Pili, nataka kuisafisha nyumba yangu, nataka ndoa yetu iwe
ndoa safi, siyo na kashifa,hili ni urithi kutoka katika fanilia yangu...kashifa
mbaya, haitakiwi kwenye familia yetu,..na kama kumejitokeza kitu kama hicho,
nataka tukiwahi kabla hakijafika mbali,...na nilitarajia rafiki yangu
angenisaidia hili, lakini hayupo, lakini hakijaharibika kitu, ...’nikatulia
kidogo.
‘Ila nahisi, kuwa wale niliowapenda kama marafiki, wale
nilijitahidi kadri ya uwezi wangu ....wawe ni marafiki zangu huenda....sina
uhakika, ...huenda wananigeuka. Hilo sitalikubali..sasa nataka nianze
kuwatambua marafiki zangu wa ukweli ni akina nani.’nikasema.
‘Hapana shemeji, hakuna aliyekugeuka huenda hujatuelewa tu,
wengi tunaishi kutokana na ushauri wako, hasa mimi najitahidi sana kuishi kama
ulivyonishauri na kweli nimefanikiwa sana, huenda hata wenzangu wanafanya
hivyo, kwa nia njema kabisa.....’akasema.
‘Kwanini nisiwaelewe, kama mtaniambia ukweli...unafahamu
shemeji, huoni leo umeniambia ukweli, kwani nimekasirika?’ nikamuuliza
‘Hujakasiriak shemeji...’akasema.
‘Sasa kwanini watu hawanielewi, kwanini wasiniambie ukweli,
kabla hawajaamua kufanya makosa, ...haya tuseme wameteleza, kwanini hawatubu
madhambi yao kiukweli, na nijuavyo mimi kutubu makosa yako kiukweli ni kusema ukweli, na
kwenda kwa yule uliyemkosea ukatubu mbele yake, si ndio hivyo, shemeji yangu
maana wewe ni muumini mzuri wa dini,....’nikasema nikimwangalia moja kwa moja.
‘Kwahiyo mimi ninavyoona kwasasa, na nitambue hivyo, ni kuwa
kuna kosa limeshafanyika, ...basi kama ni hivyo,nimabiwe ukweli, ..mbona wote
mnakuwa mabubu ninapowauliza hivyo, hii inaonyesha nini, kama sio
unafiki,...kwa hali kama hiyo mnatarajia mimi nifanye nini,....msione ajabu
tukitengana, nasema ukweli kama hamtaniambia ukweli sasa
tutatengana....’nikasema na mara shemeji yangu akasimama na ghafla akapiga
magoti.
‘Shemeji usiseme hivyo, mtatengana na nani shemeji una maana
unataka kutengana na kaka, hapana shemeji usifanye hivyo, mimi nipo chini ya
miguu yako shemeji, nipo tayari kufanya lolote unalotaka, ilimradi tu usimuache
kaka yangu, niambie nifanye nini shemeji...’akasema huku akinipigia magoti,
sikutarajia tendo hili kutoka kwa huyu mdogo wa shemeji yangu,..na mara simu
yake ikalia; Mimi nikasema kwa ukali.
‘Sipendi mtu kunyongea mbele yangu, mimi sio mtu wa kupigiwa
magoti, usifanye hivyo hata siku moja mbele yangu, nilikufundisha nini,
....nilikufundisha kuwa uwe mjasiri, huo sio ujasiri, huo ni unyonge, huo ni
utumwa, usikubali kuwa mnyonge, usikubali kuwa mtumwa wa mwenzako, mtu wa
kupigiwa magoti na kuombwa ni mungu peke yake..unajidai kuwa umuumini wakati
matendo yako yanakusaliti.....inuka haraka....’nikasema, na yeye akasimama kwa
haraka na kufuta futa majani yaliyoganda kwenye suruwali yake.
‘Pokea simu yako,..’nikasema huku nikiwa nimekunja uso, kama
vile nipo ofisini, na hapo nikakumbuka, ..nikakunjua uso wangu na kutabasamu,
tabasamu la kubandika.
‘Ni docta, rafiki yake kaka, nilimwambia nitapitia kwake,
naona kaona nimechelewa ndio maana kaamua kunipigia simu,..’akasema huku simu
ikiendela kunilia, na akawa haipokei
‘Ongea naye tu sasa, mwambia unakuja,....’nikasema na yeye
akasogea pembeni kidogo, na waliongea kwa muda mfupi, baadaye shemeji
akanisogelea na kusema;
‘Haya shemeji ngona mimi niende,,nakwenda kwa huyo docta, na
sizani kama nikitoka huko nitafika hapa nyumbani, ...., sijui naye ananihitajia
kwa jambo gani maana kaniambia nisikose kwenda kwake...’akasema akionyesha
kutukupendezewa na hali iliyotokea
‘Ukiongea naye, usimwambia kuwa tulikuwa na maongezi mimi na
wewe, na pia kuwa nimekuambia tukutane na wewe kesho,unasikia, usimwambia
lolote kuhusu maongezi yetu haya, kama kweli unamjali kaka yako, ..vinginevyo,
utakuja kujuta, maana hujui ni nani adui wa kaka yako,hujui adui wa familia
yetu hii,....mimi nasema hivyo kama mke wa kaka yako, ambaye namjali sana kaka
yako kuliko hawo watu wengine wa nje wanaojifanya wanamjali kaka yako....’nikasema.
‘Ni kweli shemeji, lakini huyo docta, ni rafiki mkubwa na wa
karibu wa kaka, na sio mtu mwingine wa nje na nijuavyo mimi, yeye amekuwa akimsaidia sana
kaka, wakati wote, ....na yeye ndiye amemfanya kaka, asitaabike zaidi,
.....’akasema.
‘Kutaabika zaidi kwa vipi, kwani kaka yako alikuwa akitaabika
!?’ nikamuuliza kwa mshangao.
‘Kama nilivyokuambia shemeji, kwa mtizamo wangu , kaka alibadilika
na kuwa mlevi, ili kuondoa mawazo, akawa mtu wa kunywa kunywa pombe, na kila
siku akawa anazidisha ...labda akiona kakwazika kwa hili na lile....mimi sijui
zaidi...’akasita kidogo, halafu akasema.
‘Kuna siku niliamua kumuuliza akaniambia ni maswala yake
binafsi, na siku moja nikiwa na rafiki yake huyo akaulizwa na kubanwa sana na
maswali, akasema ni mambo yake ya ndoa hayamuhusu mtu mwingine..na kumbuka pia aliwahi
kuniambia ni subiri nioe, nikioa, nitakuja kujua kwanini anafanya hivyo...nafikri
shemeji wewe unafahamu zaidi kuliko mimi, ngoja niondoke,.....docta
ananisubiria.....’akasema na kuniancha nikiwa nimeshikwa na bumbuazi.
‘Sawa lakini kumbuka hatujamalizana na wewe, nataka uje
kesho ofisini kwangu, muda wa saa nne, tukutane huko, nataka uje ukiwa
umekamilika, tayari kwa kuniambia ukweli wote unaoufahamu kuhusu kaka yako,
....nataka ukweli ili nisije nikachukua uamuzi ambao wewe na wengineo hawataupendezewa
nao....’nikasema huku nikisimama kuondoka.
‘Kama hamtaniambia nikachukua jukumu la kuutafuta mwenyewe,
...sizani kama mtanielewa, ni bora mniambie ukweli ili mimi nipate muda wa kutafakari
nah ii itanisaidia kutokukimbilia kuchukua maamuzi ya haraka, na huenda
nikasamehe, kutegemeana na kosa lenyewe,..lakini kama mtanificha, nikaja
kugundua mwenyewe..sitamsameeh mtu, hilo naahidi...nitachukua uamuzi wangu,
ninaoujua mimi,....ambao huenda utaumiza wengi...mnanifahamu nilivyo...haya unaweza
kwenda...usijali shemeji, wewe ni mtu mwema, basi endelea kuwa mwema....’nikasema
Shemeji yangu aliondoka huku akiwa kanyong’onyea,..mpaka
nilimuonea huruma, lakini niliona bora iwe hivyo, hiyo ndio njia pekee ya
kupata ukweli, nikaingia sebuleni,na kukaa kwenye sofa huku nikiegeemza kichwa
kama mtu anayetaka kusinzia, sikuwa na mawazo ya kuingia chumbani kuangalia
kama mume wangu bado kalala, nilichokuwa nacho kichwani ni hayo maneno ya huyo
shemejii yangu:
‘Ni kweli, lakini huyo
ni rafiki yake wa karibu, na sio mtu mwingine wa nje na nijuavyo mimi, yeye amekuwa akimsaidia
sana kaka, wakati wote, ....na yeye ndiye amemfanya kaka, asitaabike zaidi...’
‘Asitaabike zaidi, ina
maana yote niliyofanya kwa mwenzangu ni kazi bure...’nikajiuliza.
‘Na kwanini
asiniambia....’nikazidi kujiuliza
Wakati maneno mengine yakiendelea kujirudia akilini na
kuzidi kunipandisha hasira, mara nikasikia sauti za watu wakiongea nje, .nikainuka
na kuangalia nje....
Nikashituka kutoka kwenye lindi la mawazo, kwanza nilitaka kukimbilia
chumbani kuhakikisha kuwa mume wangu bado kalala, ..., lakini haikuwa na haja
kwani nilipochungulia nje kwa kupitia dirishani nilimuona yule msaidizi wangu
akiwa anasukuma kile kigari cha mume wangu, na mume wangu akiwa kakaa na
alikuwa kama kasinzia, lakini hiyo ilikuwa ni dalili, kuwa alikuwa na mawazo.
Kumbe msaidizi wangu alikuwa amerudi, na kuingia ndani
akamkuta mume wangu keshaamuaka, na wakatoka naye nje,inaonekana walikuwa
wanazunguka huku na kule na kigari....ndivyo anavyopenda mume wangu, hataki
kukaa sehemu moja kwa muda mrefu.
Kwanza nikaingiwa na wasiwasi, nikijiuliza huyu mtu alitoka
muda gani, isije ikawa,walifika hadi kule bustanini, wakasikia maongezi yetu na
shemeji yangu,kitu ambacho muda wote nilikuwa nikikikwepa, nikaona nithibitishe
hilo, nikafungua mlango na kutoka nje,....
Mume wangu aliponiona, kwanza aliniangalia kwa macho
yaliyojaa huruma, nikatabasamu, lakini yeye hakutabasamu kama ilivyokuwa
kawaida yake, ...nikamuona akikunja uso kama vile mtu anayehisi maumivu, na
kabla sijasema neno akauliza;
‘Mdogo wangu kakukosea, nini.....’ nikagwaya, na simu
ilikuwa tayari mkononi tayari kumuita dakitari.
NB: Kwa leo inatosha ....eeh, two-in-one, zawadi maalumu hii.
WAZO LA LEO:Katika
maisha yetu ya ndoa, na katika maisha yetu ya kila siku, tujifunze kuwa
wakweli, kila mmoja amwamini mwenzake ....kwani, ukweli wakati wote, ni kinga
ya uhasama,...japokuwa kuna wakati mwingine inatulazima kukwepa kusema ukweli
kwa wakati fulani, ili kukwepa madhara...ikiwa ni kwa nia njema, lakini kwa
vyovyote iwavyo, tujifunze kuwa wakweli kwa wenza wetu, ili kujenga uaminifu,
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment