Baada ya maelezo ya shahidi kijana, wakili, au muendesha
mashitaka, alisema;
‘Ndugu muheshimiwa hakimu, wakili mtetezi anaweza kuendelea
naye. Na wakili mtetezi, akatabasamu, na kusimama, kwanza alimgeukiwa mteja, na
akamnong’oneza kitu, na mteja wake akaonekana kutabasamu, na akageuka kumkabili
huyo shahidi, na akaanza kuuliza swali;
Wewe unadai ulikuwa upo kwenye kundi la ulinzi shirikishi,
na bosi wako alikuwa ni Jemedari, ina maana moja kwa moja ulikuwa ukiwajibika kwa huyo
bosi wako Jemedari, ndio au sio? akaulizwa.
‘Ndio ….lakini….’kabla hajaendelea kuongea huyo shahidi
wakili akasema.
‘Sijakuambia utoe maelezo..jibu kama nilivyokuuliza….’akasema
huyo wakili akimtolea macho huyo shahidi, na huyo kijana akaonyesha kushangaa
usoni, na kugeuka kumwangalia wakili mwanadada, na wakili mwanadada
akatabasamu, kumpa moyo.
Wakili wa utetezi, akageuza jicho upande ule wa wakili
mwanadada, huku akiwa bado anamtizama shahidi huyo, akauliza tena;.
‘Kwahiyo kazi zako huwezi kufanya mpaka huyo Jemedari
awaamrishe mfanye kama atakavyo yeye,…?’ akaulizwa.
‘Ndio, …..na…na wakati mwingine tunaamrishwa na kiongozi wa
kijiji…..’akasema kwa haraka wakati huo huyo wakili alikuwa akimzuia kwa ishara
ya mkono.
‘Jibu swali kama nilivyokuuliza,….’akasema huyu wakili huku
akijafanya anatabasamu
‘Wewe umesema mlitumwa kwenda kumkamata Mzee wa kijiji,
kwasababu alikataa maagizo halali ya kijiji, ….je ni kweli kuwa kulikuwa na
maagizo halali kutoka kwa kiongozi wa kijiji,?’ akaulizwa
‘Ndio yalikuwepo, ….’akasema na kabla hajafafanua huyo
wakili akauliza swali jingine.
‘Na mlipokwenda kwa huyo mzee, alitii hayo maagiza halali ya
serikali ya kijiji, au aliendelea kukaidi kama kawaida yake…?’ akaulizwa.
‘Sielewi hapo unaposema kama kawaida yake….’akalalamika huyo
shahidi na huku akigeuka kumwangalai wakili mwanadada, na wakili mwanadada,
alitaka kusema jambo, lakini akasita.
‘Jibu swali kama nilivyokuuliza..’akasema huyo wakili
mtetezi na wakili mwanadada akatoa pingamizi kuwa wakili mtetezi analazimisha
kujibiwa swali, ambalo shahidi hajalielewa, na hataki kumfafanulia vyema
shahidi, na shahidi anakuwa hana uhuru wa kujitetea, na hapo hakimu akamuonya
wakili aulize kwa mujibu wa sheria.
Wakili huyu akageuka kumwangalia wakili mwanadada,huku
akitaabsamu, halafu kwa haraka akageuka kumwangalia huyo shahidi , akiwa
kabadilika kwa kukunja sura, na kuuliza;.
‘Je mlipokwenda kwake, alifanya nini, alitii amari halali ya
serikali ya kijiji,au aliendelea kukaidi..amri halali ya serikali ya kijiji?’
akauliza akiwa anasisitizia hayo maneno `amri halali ya serikali ya kijiji’.
‘Alisema hawezi kuondoka kwasababu analinda mali ya mtoto
wake?’ akasema, hapo wakili mtetezi akamwangalia huyo shahidi kwa mshangao,
halafu akauliza huku akionyesha mshangao
‘Ina maana huyo mzee
ni baba yake huyo mwanamama?’ akauliza huku akiwa kama kategesha sikio moja kumsikiliza
huyo shahidi.
‘Hapana, …ila…’akasema
‘Ila alikuwa akiingilia familia za wenzake na kujifanya yeye
ni mzazi wa huyo binti kwa maslahi yake, na kuendelea kuwa mkaidi wa serikali….ndio
au sio?’akaongea kwa haraka, na akawa kama anauliza swali, huku wakili mwanadada
akiwa anatoa pingamizi kwa kulalamika kuwa wakili anatoa maelezo yake binafsi
badala ya shahidi .
Hakimu alimuonya tena huyo wakili, na kama kawaida yake huyo
wakili aligeuka kwanza kumwangalia wakili mwanadada huku akitikisa kichwa kama
anakubali jambo,, halafu kwa haraka akageuka kumwangalia huyo shahidi akiwa
kakunja uso …kuonyesha kukasirika na kusema;
‘Je mlipofika kwake, na mkiwa na mkuu wa serikali ya kijiji,
mkuu ambaye mlimchagua nyie wenyewe, na huyo mzee alifanya nini??’ akauliza
‘Alisema….’akataka kusema na huyo wakili akasema.
‘Je alitii amri?’ akauliza.
‘Hakutiii…’akasema
‘Alifanya nini?’ akauliza
‘Alisimama pale pale ndani….’akasema huyo shahidi.
‘Na ikawaje ?’ akauliza.
‘Kiongozi wa serikali ya kijiji aliendelea kumsihi, na
wakawa na maongezi ya muda ….lakini mzee hakukubali kwa sababu alizozitoa ambao
hutai nizieleze…’akasema shahidi na watu wakacheka.
Huyo wakili naye akacheka na kumwangalia wakili mwanadada
kama vile anamzihaki,
‘Nyie mlichuku hatua gani?’ akauliza.
‘Kwa kipindi hicho, walikuwa wakiongea na kiongozi wa
kijiji, na baadaye kiongozi wa kijiji, akatupa amri ya kumtoa nje, na sisi tulijaribu
kumshika mkono, ….’akasema
‘Na yeye alifanya nini?’ akauliza.
‘Alikataa kata kata,…’akasema
‘Hakuwatishia kuwapiga…?’pingamizi likawekwa na hakimu
akalikubali, kwani ilionekana wakili anamlisha shahidi majibu.
‘Unasema mliarifia mumutoe nje, kwa hiari,au sio? Akauliza.
‘Kama ni hiari angelikubali kwa kiongozi wa kijiji, lakini
kwa vile alikataa, ndio maana kiongozi wa kijiji, akasema tumtoe, kwahiyo hapo
hakukuwa na hiari tena…’akasema huyo shahidi.
‘Kama alikataa amri halali ya kijiji, na kiongozi
anayetambulikana, akajaribu kutumia hekima yake, nab ado mtu huyo akaendelea
kukata, wewe unafikiri, hapo mlitakiwa mfanye nini?’ akawa kama anauliza,
lakini kabla huyo shahidi hajajibu,akauliza.
‘Je mlipomwambia kuwa atoke, alifanyaje…?’ akauliza.
‘Sisi hatukuwa lugha ya kumbembeleza, maana kiongozi
alituambai tumtoe, sio tumbembeleze kwahiyo tulianza kwa kumshika mkono…’akasema
huyo shahidi.
‘Unaona, bado serikali ilikuwa ikimbembeleza, na hawa
mashababi, hawakutaka kwanza kutumia nguvu, wakamshika mkono, halafu ikawaje….’akauliza
huyo wakili.
‘Alikataa kutoka kwenye hiyo nyumba, na tulipojaribu kumvuta
kwa nguvu ili atoke nje, akagoma, kabisa, na hapo tukasikia mjumbe akisema kama
tumeshindwa kumtoa, basi ataongeza nguvu nyngine’ akasema.
‘Ulisikia mkuu wa kijiji akisema mtumie njia nyingine..ya
kutumia nguvu, kumpiga n a vitu kama hivyo…?’ akaulizwa.
‘Sikusikia,…ila…’akabla hajajibu huyo wakili akasema.
‘Kwa jinsi hiyo , nyie mlitumia njia ,mliyoona inaweza
kumtoa huyo mzee kutokana na ujeri wake, au sio,..?’ akaulizwa.
‘Ndio unaweza kusema hivyo….’akasema.
‘Njia ambayo mliona nyie, kama walinzi, kuwa inafaa, sio
kutoka kwenye kinywa cha kiongozi wenu, …’akawa kama anauliza lakini hata kabla
shahidi huyo hajajibu swali, akamgeukiwa muheshimiwa hakimu na kusema;
‘Muheshimiwa hakimu, mara nyingi watu kama hawa wanapotumwa
mahali, hasa hawa vijana wanaweza wakatiumia njia walizofundishwa, lakini
ukikutana na mtu mkaidi, kama huyo mzee, bila ya kutumia nguvu,…huwezi
kufanikiwa, na wao wasingeliweza kumtoa kwa hekima, ….hawa ndio wakaidi,
wasiopenda kutii amri halali ya kijiji….
'Muheshimiwa hakimu, kama tuwajuavyo vijana, bado damu inachemka,
wao huenda waliona kuafanya hivi au vile itasaidia, na kwa mzee kama huyo akiguswa
kidogo tu, ….ndivyo kama ilivyokuwa, na hali kama hiyo, mkadii hataki , vijana
wakamtoa kwa nguvu hataki,…wao wakatumia mbinu zao, na matokea yake wanamtwika
kiongozi wa kijiji mzigo wote….’akasema wakili wa utetezi na mwanadada akasema.
‘Hatuhitaji maelezo yako, tunachohitajia kwasasa ni ushahidi,
je wewe ndio umegeuka kuwa shahidi, au unataka shahidi akubaliane na matakwa
yako kinyuma na ilivyokuwa..’akasema wakili mwanadada, na huyo wakili akasema.
‘Mimi nimetoa maelezo kwa muheshimiwa hakimu, ili aelewe
hali ilivyokuwa, sioni kuna ubaya hapo,..’akasema huku akimwangalia hakimu, na
hakimuw akawa anaandika jambo kwenye makabrsaha yake., na alipoona hakimu
hajasema neno akamgeukia shahidi.
‘Wewe unasema wakati mwingine mlikuwa mnapewa kazi maalumu,
je taarifa ya kazi maalumu huwa unapewa na nani?’ akauliza.
‘Kazi maalumu zinakuwa za siri, kwahiyo kuna ishara
tunapewa, ni ishara za kiutendaji, na yule aliyekuwa akribu, au aliyepewa
taarifa hizo, anakufahamisha kuwa tunahitajika kwa kazi maalumu, lakini mara
nyingi ni kiongozi wetu wa karibu ndiye anaweza kuja kutufahamisha….’akasema.
‘Kiongozi wenu wa karibu ukiwa na maana Jemedari au sio…?’
akaulizwa.
‘Ndio….’akasema.
‘Siku unapodai kuwa mlikwenda kufanya kazi ya siri, ambayo
unadai uliambiwa umwage mafuta kwenye nyumba ya mzee wa kijiji, ni nani
alikuambia kuwa kuna kazi kama hiyo?’ akauliza.
‘Ni ….ni mlini mwenzangu, alisema amepewa taarifa kutoka….’kabla
hajaendeelea wakili huyo akamkataizi na kusema.
‘Swali langu lilikuwa wazi, ni nani alikuamba wewe kuwa kuna
kazi maalumu?’ akaulzwa tena.
‘Ni mlinzi mwenzangu…’akasema.
`Safi kabisa…jibu swali kama mtu aliyekwenda shule…’akasema
huku akitabasamu, na kugeuza kichwa kwa haraka kumwangalia wakili mwanadada, na
huku akiuliza swali.
‘Na je katika pilika pilika za kazi hiyo, ni nani aliyekuwa
akiwasimamia?’ akaulizwa.
‘Alikuwepo msaidizi wa Jemedari,..lakini baadaye nilikua
kufahamu kuwa mkuu….’akataka kusema na wakili akamkatiza.
‘Sijakuambia utoe maelezo, jibu swali
ninavyokuuliza….’akasema wakili huyo.
‘Mwenzako au kiongozi wa tendo hilo, ambalo hukujua ni amri
ya nani, … akakuambia uanze kumwanga mafuta ya taa kuzunguka jengo hilo,
unaweza kusema ni kwanini ilitakiwa mfanye hivyo?’ akaulizwa.
‘Mimi nilifuata maagizo ya mtu wangu huyo wa karibu na
sikuwa na amri ya kupinga, ama kwanini, kuna uvumi ulienea…’kabla hajamaliza
maelezo yake, wakili mwanadada akapinga kwa maelezo kuwa shahidi alikuwa akitoa
maelezo, kitu ambacho wakili hakumuuliza na hayo anayotaka kuongea ni uvumi sio
uhakika…
‘Sizani kwamba kazi maalumu kama hizo zinafanyika bila
sababu, je huyu mtu wako wa karibu hakukuambia ni kwanini ufanye hivyo?
Akaulizwa.
‘Kwa muda huo hakukuwa na muda wa maelezo, ….’akasema.
‘Kwahiyo kumbe wewe uliweza kupokea amri yoyote kutoka kwa
mtu wako wa karibu, na inawezekana isiwe imetoka kwa mkuu wa kijiji,
inawezekana ilitoka kwa Jemdari, inawezekana ilitoka kwa yoyote mwenye nia
mbaya, au uadui na huyo mzee…..’akasema na kugeuka kwa hakimu na kusema hapo
nimemaliza.
Wakili mwnadada akasimama na kumuendea huyo shahidi, na
kuuliza swali.
‘Wakati ulipojiunga na kundi hilo, uliambiwa ni nini
majukumu yako ya kazi?’ akuliza.
‘Tulipewa mkataba wa kazi zetu, na tukafafanuliwa kwa maneno
juu ya hayo yaliyoandikwa na kusisitiziwa kuwa tusije kukiuka hayo yaliyoandikwa
hapo ….’akasema.
‘Kwenye mkataba huo, kuna maelezo gani ya kipengele cha kazi
maalumu?’ akauliza
‘Kuna maelezo kuwa kazi maalumu, zitatolewa na kiongozi wa kijiji, …na kiongozi wa kundi, atasimamia
kazi hizo, kwa maslahi ya kijiji…..’akasema.
‘Kwahiyo kazi zote maalumu, kutokana na mkataba wenu,
zilikuwa zimetoka kwa nani….?’ akauliza.
‘Kwa kiongozi wa kijiji….’akasema na wakili mwanadada
akatabasamu.
‘J e katika utendaji wako wa kazi, ulishawahi kufanya kazi
maalumu na baadaye ukagundua kuwa haikutoka kwa mkuu wa kijiji?’ akaulizwa.
‘Hapana haijawahi kutokea hata mara moja, maana wote
tulikuwa tumefundishwa sheria na mkataba wa ajira yetu, na ni nini madhara yake
kama utafanya kazi kinyume na utaratibu uliowekwa…’akasema.
‘Kwahiyo hata kazi hiyo ya kuchoma moto, ilitoka kwa mkuu wa
kijiji?’ akauliza.
‘Ndio, ….’akajibu na wakili mtetezi akalalamika kuwa wakili
anamlisha shahidi majibu, nahaki akasema shahidi aendelee
‘Na wakati mnampiga huyo mzee, mkuu wa kijiji alikuwa wapi?’
akauliza.
‘Alikuwa nje….na alipoona kuwa tumeshindwa kumtoa huyo mzee
alituongezea watu tukawa watu saba, na wenzetu walipofika hawakukata kujua
zaidi wakaanza kumpiga mzee kwa nguvu zote, hadi akawa kama anapoteza
fahamu….’akasema.
‘Wewe ulifanyaje?’ akaulizwa.
‘Mimi nilikuwa nawasihi wasifanye hivyo, kwani katika
mikataba yetu hatukuruhusiwa kumuumiza mtu ambaye hana silaha, au keshasalimu
amri, hasa wazee na akinamama, labda kuwe na sababu maalumu ambayo itathibitishwa
na kiongozi, ….mkuu wa kijiji..’akasema na wakili mwanadada akageukiwa wakili
wa utetezi, na akawa kama anamuuliza. Na wakili mtetezi akatabasamu na
kumgeukiwa shahidi
‘Unasema kwenye mkataba yenu, mliambiwa kuwa msitumie nguvu, labdakuwe na sababu maalumu sababu kama ipi? akaulizwa.
‘Kama huyo mtu ana silaha, au akaanza kutupiga, …’akasema.
‘Je ,mlipofika kwa huyo mzee, alikuwa na silaha yoyote
mkononi?’ akauliza
‘Alikuwa na panga…’alipojibu hivyo huyo wakili akamgeukiwa
hakimu na kusema,
‘Ni hayo tu muheshimiwa, na wakili mwanadada, akamuendea shahidi
nakuuliza.
‘Je unamfahamu vyema huyo mzee, tabia yake …?
‘Ndio ninamfahamu
sana..’akasema
‘Je kila mara anakuwa na nini mkononi?’ akaulizwa
‘Kila mara anakuwa na panga mkononi…’akasema huyo shahidi na
wakili mtetezi, alitaka kuuliza swali lakini akawa kama kakumbuka kitu,
akasema;
‘Sina swali jingine muheshimiwa hakimu. Na hakimu akasema
‘Je kuna swali jingine kwa huyo shahidi, na wakili
mwanadada, akasema,
‘Ndugu muheshimwa hakimu, tunaendelea na maelezo ya shahidi
huyu, sehemu ya pili …..’akasema na wakili mtetezi akapinga, kwa kusema, huyo
shahidi allishamaliza maelezo, kama kuna sehemu ya pili, basi shahidi huyo
arudi, na atasimamishwa tena.
‘Kwani ni shahidi huyo ni wako au shahidi wangu, utatupangiaje
utaratibu …’akasema wakili mwanadada.
‘Uliposema kuwa tumuulize maswali, ulikuwa umehitimsisha na
huyo shahidi, hatukusikia ukisema kuwa utaendelea naye baadaye…..’akasema.
‘Huu ni utaratibu wetu,..na tunaweza kufanya tupendavyo,
wewe kazi yako ni kujietetea kwa kuumuliza maswali, kwani una shaka gani anye…..?’
akauliza wakili mwanadada na huyo wakili akageuka kumwangalai hakimu, ili
kutaka msaada, na hakimu, akatulia kama anawaza jambo, halafu akasema;
‘Sawa endelea…..lakini hata mimi sijafurahia na huo
utaratibu wako, nakuonya usifanye hivyo tena…’
‘Ahsante muheshimiwa hakimu, tulifanya hivyo kama sehemu
yetu ya kuhakikisha kila hatua inaeleweka vyema, lakini kama haitawezekana
kwake yeye kuendelea kwa sasa, tunaweza kumpumzisha na tukaita shahidi
mwingine, halafu tutakuja kumuita baadaye.Hakimu akageuka kuangalia upande wa
upinzani na wakili mtetezi akasema;
‘Sisi tunaona amuite shahidi mwingine, na kama ni muhimu,
basi atamsimamisha huyo shahidi baadaye maana hatukua kuwa kuna sehemu ya
kwanza ya pili ya tatu……’akasema huyo wakili mtetezi akifanya ka mzaha, na watu
wakacheka, na wakili mwanadada, akatabasamu na kuinua mkono juu kama
kujipongeza, kitu ambacho kilimfanya wakili wa utetezi, amwangalie kwa
mshangao.
‘Kabla shahidi mwingine hajaitwa hajasimama, ninatoa
mapumziko ya dakika tano, halafu nawahitaji mawakili wa pande zote mbili nitete
nao kidogo, dakika tano tu…’akasema .
Kila kundi lilikutana
na na kukawa na mazungumzo ya hapa na pale, na kipindi hicho, wakili mwanadada alikuwa
kaondoka kama walivyoitwa na hakimu, hawakukaa sana, wakili mwanadada akarejea,
na akasogea upande ula alipokuwa kakaa Mzee wa kijiji, kama wanavyomuita, au
baba yangu wa kufikia, na wakawa wanaongea na mzee huyo, na mazungumzo yao
yalionekana ni ya faragha, kwani walikuwa wameinama na kuongea kwa sauti ya chini
kwa chini, na hapo, na baadaye kidogo wakili mwanadada akasema;
‘Natumai wakati umefika haina haja ya kusubiri….’nikasikia
wakili mwanadada akiongea kwa sauti tofauti na alivyokuwa akiongea mwanzoni na
huyo mzee.
‘Hata mimi naona hivyo, ….’akasema huyo mzee wa kijiji, na
mimi pale nilipo nikahisi kuna jambo kubwa linataak kutokea, na
nilipoangaangalia upande ule wa watetezi, nikaona mtu mwingine kaongezeka, na
mtu huyo alikuwa naye kainama akiongea na mkuu wa kjiji, inaonekana walikuwa na
furaha kubwa kama kuna jambo ambalo wameona litawasaidia, na yule mtu
alipoinuka aliangalai upande watu.
‘Unamuona , shemeji kaweza kuja leo…’nikauliza na wakili
mwanadada ambaye bado alikuwa akiteta na mzee wa kijiji, akainua kichwa na
kuangalia upande ule wa washitakiwa na
huku akiuliza
‘Ni shemeji yupi huyo…?’ akauliza
‘Mchumba wako….’nikasema na wakili mwanadada akawa kama
kashituka kusikia hivyo, akainua kichwa kuangalia upande ule, kwa haraka halafu
akarudisha kichwa chini na kujifanaya anaendelea kuongea na huyo mzee, lakini
nilihisi macho yao yakigongana, na nini kila mmoja wao anawaza ikawa siri yao.
Mimi nikageuza kichwa
kumwangalia shemeji yangu huyo, na macho yetu yakagongana, na yeye akajitahidi
kutabsamu, mimi nikageuza kichwa haraka kumwangalia wakili mwanadada ambaye
alikuwa katulia, na baadaye akasema;
‘Huyu naye kafuata nini , mtu anaumwa, badala ya kupumzika
anakuja kujitakia mawazo mengine ya bure, hawajui hawo watu aliokuwa nao….angeliwajua
asingeliwakaribia kabisa,….’akasema.
‘Atajua tu muda wao umefika kuumbuka…’akasema baba yangu wa
kufikia, na kama vile tulipanga wote tukageuza vichwa kuwaangalia, na kumbe na
wao walikuwa na wakituongela maana wote wakawa wanatuangalia sisi, na mara
sauti ya ya hakimu ikatushitua pale aliposema;
‘Aletwe shahidi mwingine…’
Na mlango wa mashaidi
ukafunguliwa na wakati huu akaingia mwanamke akiwa kajifunika khanga sehemu
zote, kuanzia kichwani hadi miguuni. Kwa jinsi alivyovaa, kila mtu akawa
anamtizama yeye, na kwa mshangao, hata hakimu naye akajikuta akimtizama kwa
mshangao, …
NB: Je ni nani huyu.
WAZO LA HEKIMA:
Tuwe makini na marafiki, tuwe makini na taarifa zinazoletwa kutoka kwa wale
tunawajua kama marafiki, ni vyema, tukafanya uchunguzi wa taarifa hizo, kwani sio
kila taarifa inaweza kuwa kweli, eti kwa vile inatoka kwa hawo tunaoona ni
marafiki.
Ni mimi:
emu-three
3 comments :
Muda umefika wa kila kitu kuwa wazi, nimependa wazo la Leo marafiki sio hata kdg
Muda umefika wa kila kitu kuwa wazi, nimependa wazo la Leo marafiki sio hata kdg
Muda umefika wa kila kitu kuwa wazi, nimependa wazo la Leo marafiki sio hata kdg
Post a Comment