Kumbuka tupo bado
mahakamani, na sasa aliitwa shahidi,….shahidi ambaye uvaaji wake, ulikuwa sio
wa kawaida, alikuwa mwanamama, ambaye alijitanda khanga mwili mzima, na kubakiza
sehemu ndogo ya macho. Hata hivyo,
haikuwezekana kumwambia avue hizo nguo, je kwanini alivaa hivyo, ni kutokana na
imani za dini, au kuna jingine na je huyu shahidi ni nani hasa, …tuendelee na
kisa hiki.
*******
Wakili mwanadada akamsogelea shahidi wake, huku hakimu akiwa
bado anamwangalia huyo shahidi kwa kuonyesha shauku au kushangaa, na alikuwa
anataka kusema jambo, lakini akawa anasita, huenda ni kwa kuogopa kuingilia
imani za watu, akageuka kumwangalia wakili mwanadada ambaye alikuwa akijiandaa
kuongea, na mwihowe akachukua kalamu
yake na kuandika jambo, na wakati huo huo wakili mwanadada akaanza kuongea;
‘Ndugu muheshimiwa hakimu, natumai kila mmoja amekuwa na
mawazo na shauku, ya kusikia mengi hususanai kwa shahidi yetu huyu, na najua
kila mmoja ana dukuduku la kutaka kujua kwanini shahidi huyu kavaa kama anavyoonekana,
na wengi watakimbilia kusema labda kava hivyo kwa ajili ya imanai za kidini, …nawaomba
muwe na subira, mtakuja kufahamu ni kwanini baadaye….’akaanza kuongea na watu
wakawa kama wanapumua. Kila mmoja mle ndani akili na macho yake yalikuwa pale
mbele, kila mmoja akijaribu kuhakikisha hakosi kitu…
‘Katika maelezo yetu ya awali tulisema kuwa tutawaleta
mashahidi, na ushahidi wao, na hata wakati tunaendelea na kesi yetu hii wenzetu wamekuwa mara kwa mara wakidai
ushahidi, na hata kusema kesi yetu hii imegubikwa na siasa na porojo nyingi,
kuliko sheria, hili tunalainza sasa, kuwa kila shahidi atakayesimama kuanzia sasa,
atakuwa na ushahidi…’akasema na kumwangalia yule mwanamke aliyekuwa kakaa
kwenye kiti.
‘Ndugu muheshimiwa hakimu, naomba nielezee kidogo,kama
nilivyokuomba awali ..japokuwa huenda wenzetu wasikubaliane na hili, lakini ni
kwa masilahi ya wote, maana tunasema usione mwenzako anafanyiwa ubaya ukacheka,
kwani huwezi kujua ya leo na kesho,…utacheka, likitokea kwa mwenzako na hata
kumlaumu, lakini kumbuka hakupenda, na huenda, imetoka hivyo kwasababu ya watu…ndio
maana tunasema leo ni kwake, kesho ni
kwako…..’akatulia kidogo
‘Pia kuna usemi usemao mwenzako akinyolewa wewe tia maji….maana
mabaya na ubaya hufanywa na watu, na huenda wakawa watu wako wa karibu tu….’akatulia
na kuangalia upande huo wa wapinzani akitarajia pingamizi lakini wakili mtetezi
alikuwa akiandika kitu kwenye makabrasha yake, aliyekuwa anaonekana kuongalia
mbele , akimwangalai yule shahidi ni mteja wake.
‘Binadamu tumefikia hatua mbaya kabisa, hatua ambayo,
tunaona maslahi ndio kila kitu, tunaona mambo yetu, ndio yana maana kuliko hata
uhai wa mtu, mtu yuko tayari kutoa roho ya mwenzake kwasababu ya mali, pesa,
sifa..…hali hii imekwenda mbali hata kutokijali wale wasio na hatia, wale ambao
hawawezi hata kujitetea,..eti kwa vile sisi tuna madaraka, kwa vile sisi ni matajiri
, kwa vile sisi ni mabosi, hatujali kabisa utu wa mtu, tonachojali sisi ni tufanikiwe mambo yetu, nakujiona tuna haki ya kila kitu….utasema nini kwa
mwenye pesa, mwenye utajiri, bosi, …muheshiwa….tunajidanganya…’akatulia.
‘Shahidi huyu atakuwa kielelezo cha hayo ninayotaka
kuyaelezeahapa, na ni vyema wanajamii mkalisikia hili, na kupata fundisho, ‘akageuka
kumwangalia wakili wa utetezi ambaye alikuwa akiangalia saa yake, na kuendelea
kusema.
‘Sio kwamba nahutubia hapa kupoteza muda, lakini inabidi
nifanye hivyo kwa msilahi ya wanajamii, na nilishamuomba muheshimiwa hakimu
kuhusu hili mbele ya wakili mtetezi, … lengo ni ili tuelimishane, ili hili na
mengine yasitokee tena….’akasema na hakimu akaonyesha ishara kuwa wakili
aendelee asipoteze muda.
‘Sisi ni binadamu, na hata tufanyeje hatuwezi kulibadili
hili, na kama ni bianadamu, fanya
ufanyalo, penda upendavyo,ishi unavyopenda kuishi….lakini upo mwisho wa
kila mtu. Na hizi tambo za utajiri, za kujiona, kuwa eeh, mimi ni mzuri, mimi
ni bosi, kiongozi, muheshimiwa, yote hayo
ni hapa duniani tu, na malipo ni mbele ya mwenyezimungu…’akasema na kugeuka
huku na kule.
‘ Kwahiyo nawaasa, na kujiasa mwenyewe, kuwa ni vyema tukajiandaa, ni vyema tukajichunga
nyendo, na taratibu zetu, ili ziendane na utu wa binadamu, na ni vyema tukachunga
dhamana tulizopewa, kwani sio zetu,…wewe ni kiumbe tu kama viumbe wegine, tukumbuke
kuwa kuna mwenye mamlaka zaidi yako,….akitaka liwe huwa, yule mwenye mamlka ya
roho yako..’akatulia na mshitakiwa mkuu alionekana kukerwa, alikuwa kama
anahangaika, lakini kwa muda ule hakuna aliyekuwa akimwangalai kila mtua alikuwa
na shauku ya kuona au kusikia kutokana na shahidi huyo hapo mbele.
Kwa jinsi alivyokuwa akihangaika, watu wangelihisi mengine,
lakini cha ajabu hata wakili wake, ambaye likuwa kakaa karibu naye, alikuwa
hana mawazo na yeye, ….kama wengine, mawazo ya kila mtu yalikuwa kule mbele.
‘Kuna imani zimejikita kwenye jamii zetu, na imani hizi
zimetupaka matope, kidunia ,na hata kulichafua jina zuri la nchi yetu kuwa eti
taifa letu ni miongoni mwa mataifa yanayo-ongoza kwa imani za kishirikina….hii
sio sifa nzuri kabisa, mimi nasema huu ni uchuro, ….na ni kwanini tukafikia
hapa…’akatulia na kuangalia,saa kwani alikumbuka kuwa alipewa dakika chache za
kutoa huo muhutasari.
‘Mimi ninakubaliana na wale waliosema, kuwa sisi tunatatizo
kubwa la Adui ujinga…’akataabsamu kidogo na kukuna kichwa.
‘Kuna maadui wengine, yupo adui, umasikini na maradhi,…hawa
ni adui wakubwa sana, lakini huyu adui ujinga, amekuwa kikwazo kikubwa sana
kuweza kupambana na maadui hawa wengine….kitu elimu, bado wengine hawajambua
elimu ni kitu gani, je elimu ni kwenda darasani, na kukariri tu….hapana, elimu
ni pana,..nasema hivi kwasababu…’akaatulia kidogo.
‘Nasema hivyo kwasababu wapo watu tunaowaita wasomi, bado
wanaamini haya,…mchana wakiwa na suti zao, utawaona ni watu, wenye wadhifa wao,
lakini usiku, wanakwenda kugonga milango ya wataalamu….msicheke haya yapo….na
wengine wana hizo zinazoitwa hirizi….’ akawa anachezesha mikono na hapo watu
wakawa wanacheka kidogo, lakini walinyamaza pale alipoendelea kuongea.
‘Wasomi hawa,wanaamini imani za kishirikina na hata
kuzikumbatia, na kuzipigia chapuo, je huyu alikwenda shule kufanya nini…kama
anafanya haya, anayaamini haya, na kuyapigia debe, basi …tunaweza kmfananisha
na yule punda aliyebebeshwa vitabu vyenye hazina kubwa, lakini yeye hajui
kuvitumia. Huyu kaenda shule, akasoma, akakariri, ili apate cheti, lakini hajaelimika,
kaibeba elimu kichwani lakini haijui kuitumia, ni sawa na huyo punda, …ni kazi
bure…’akasema na kuangalia huku na huku.
‘Elimu inatakiwa ikubadilishe bwana, elimu inatakiwa
ikujenge uwe tofauti,..ili kila ulifanyalo uwe na uhakika nalo, usiwe mtu wa
kubahatisha,…je imani hii ya kishirikiana ni ya uhakika au ni ya kubahatisha..hebu
tujaribu kujiuliza wenyewe akilini na ukipata jibu utagudua kuwa nina maana
gani?’ akawa kama anauliza.
‘Wewe unadiriki kumuita, ,eti mwenzako ni mchawi, una uhakika gani na hilo, huoni kuwa ni chuki
tu, husuda tu, ubinafasi tu, na mengi yamekuzwa na propaganda ambazo zilizopandikizwa,
kwa ajili ya hiyo chuki tu na baadhi ya watu, na hili utaliona kwenye hii kesi,
…’akatulia na uangalia saa yake.
‘Jamani utakuja kusema nini mbele ya mungu mtu kama wewe,
uliyesoma uliyepewa majukumu, …na dhamana za watu nab ado hukutimiza wajibu
wako…eti kwasababu ya chuki za imani, hasa hii ya kishirikiana, ambazo
zimekwenda mbali zaidi….zimefikia hapo kwa vilezimejengwa na dhana ya
kishetani…’ hapo alipaza sauti alipotamka neno `kishetani’
‘Watu wanafika hadi kukosana mtoto na mzazi wake, watu
wanafika hadi kuuana,….jamani, mna ushahidi gani wa kisayansi kuwa huyu mtu
mnayemshuku ni mchawi, onyesheni huo ushahidi tuuone huo au huyo mchawi
akifanya hayo…ukichunguza zaidi utakuta hakuna ushahidi wowote zaidi ya dhana
tupu, na ukichunguza zaidi utakuta ni chuki binafsi…jamani mtakuja kusema nini
mbele ya mwenyezimungu…’mara hakimu akainua mkono juu, kuashiria kuwa muda
umekwisha.
‘Sawa muheshimiwa hakimu, ni hayo kwa muhustasari…yanatosha,
ngoja tuanze kuthibitisha hayo kwa vitendo…’akasema lakini wakili mtetezi akaomba naye aongee kidogo. Na
aliporuhusiwa akasema;
‘Ndugu muheshimiwa hakimu nimeona nisinyamaze tu, maana hili
kwangu naliona ni tatizo…hapa ni mahakamani, hapa sio ukumbi wa kisiasa, mimi nilikubali
kuwa mwenzangu labda anahitajia kutoa maelezo ya ushahidi wake, nilitarajia
kuwa mwenzangu angelielezea ushahidi wake ili ueleweke vyema angelielezea jambo
kuhusiana na hii kesi, lakini cha ajabu amegeuza mahakama ni uwanja wa siasa…’akatikisa
kichwa kama anasikitika.
‘Sisi tutaendelea kudai, ushahidi na mashahidi, leteni
ushaidi,…kwakweli nyie ndio mnaoendesha hii kesi kwa dhana…kama unahitajia
kuielimisha jamii kwa hayo uliyoyaongea,…basi omba kibali nenda akayaongelee kwenye viwanja vya siasa,….’akasema
na kujipiga mikono kama kudharau.
Wakili mwanadada akatabasamu na kumwangalia muheshimiwa
hakimu, ambaye alikuwa akiandika kitu, na baadaye akasema
‘Tuendelee…’
‘Sawa muheshimiwa, ujumbe umefika, na sasa tunaanza kazi,
ndugu muheshimiwa hakimu, huyo hapa mbele yetu ana sifa zote mbili ya shahidi
na ushahidi…’akasema na watu wakaguna, na huyo wakili wa utetezi, akacheka,
hakimu akagonga rungu lake kuashiria utulivu.
‘Nawaonya kwa mara ya mwisho…kama utaratibu wa mahakama
hautafuatwa hatua kali dhidi yenu zitatekelezwa, ..mnasikia…’akasema hakimu na
mawakili hawa wawili wakainama na kusema
‘Tumesikia muheshimiwa hakimu….
‘Haya endelea na shahidi wako…’akasema hakimu.
Wakili mwanadada akamsogelea shahidi wake na kwa unyenyekevu akamwiinamia na
kumnongoneza kitu, na yule mwanamama akanyosha uso, kuangalai mbele kidogo,
lakini kwa jinsi alivyokuwa amevaa usingeliweza kumuona vyema usoni, ni sehemu
ndogo tu ya uso.
‘Shahidi unatakiwa ujieleze kidogo, japokuwa umeshataja jina
lako, lakini kwa hivi sasa elezea wewe ni nani na wanakujuaje watu wa eneo
lako…’akasema wakili mwanadada.
Yule mwanamama, akakohoa kidogo, kuondoa kitu kooni na
kuanza kuongea, huku akishikilia khanga inayofunika uso na kichwa isiondoke na hata
uso wake ulikuwa unaonekana kidogo sana, ….sauti iliyokuwa ikitoka ilikuwa kama
mtu kaweka kitu mdomoni, na maneno yake yalikuwa hayasikiki vyema, thi-thi…zilikuwa
nyingi zaidi, hata hakimu naye akaonyesha kutaka kusema neno, kwanza akamwangalia
wakili mwanadada…, lakini baadaye akatulia.
‘Samahanini sana sauti yake inasikika kwa shida,…tutakuja kuliona
hili baadaye na ni kwanini iwe hivyo,
tunaomba utulivu na umakini wa kumsikiliza…’akasema.
‘Mimi naitwa Tabu, binti Saburi,,…..jina hilo kwa wengi,
halijulikani sana, watu wengi wananitambua kwa jina la mama Mkunga….’akasema sauti ya `mama
mkunga’ haikutoka vyema na wakili mwanadada akaomba alirudie tena hilo
jina.
‘Mimi wananitambua kama ‘mama
mkunga..’ alipotamka hivyo kwa uwazi, ukatokea mguno, na mshughuliko, maana
wengi ambao walisikia, hawakuamini, na wale wasiosikia wakawa wanaulizana, na
hali ikaanzisha kitu kama zogo. Lakini majina kama hayo hupewa wakina mama
wengi wanaofanya hiyo kazi, kwahiyo bado ilibakia kitendawili kwa watu….
Hakimu akagonga rungu lake, na baadaye akamuita wakili muendesha
mashitaka, na kumwambia.
‘Shahidi wako hawezi kuongea vyema, au huend hizo nguo
alizovaa zinaweza kuwa ni sababu?’ akauliza
‘Kwa hali aliyo nayo hapo ndio sauti yake ya mwisho labda
tungeliomba awekewe kipaza sauti…’akasema wakili mwanadada, na kweli hakimu
akaamrishs kipaza sauti kiletwe, na chombo
hicho kikaletwa na kuwekwa mbele yake., na hapo sauti yake ikawa inasikika
vyema japokuwa maneno mengi yalikuwa hayatoki kama yanavyotakiwa.
‘Haya hebu rudia maelezo yake …kwa kututambulisha kuwa wewe
ni nan..’akasema wakili mwanadada.
‘Mimi naitwa Tabu, binti Saburi, lakini wengi hawanifahamu
kwa jina hilo, wananifahamu kwa jina la mama mkunga…’akasema na hali ile ya
mwanzo ikatoea tena, lakini baadaye kukatulia, na hakimu akawageukiwa wenzake
na akawa anateta nao..
‘Haya tuendelee…lakini naonya tena, sheria zetu
zinajulikana, …walinzi hakikiheni wote wanaokiuka sheria mnawatoa nje, na hatua
kali zitawaandama…’akasema hakimu.
‘Kwanini wakawa wanakuita mama mkunga?’ akauliza wakili
mwanadada.
‘Kwa vile nimekuwa nikifanya hiyo kazi ya kuzalisha wakina
mama waja wazito?’ akasema.
‘Kwani kijijini kwetu hakuna zahanati, au hospitali ya
kujifungulia akina mama ?’ akauliza.
‘Hakuna ni mpaka twende mjini…’akasema
‘Ujuzi huo umeupatia wapi?’ akaulizwa.
‘Ujuzi huo niliupatia kwa bibi, na mama yangu, ukoo au
familia yetu imebarikiwa kujua kazi hiyo, na bibi yangu alinifundisha kila
kitu, na yeye akanihakikishia kuwa nimekuwa mtaalamu kuliko hata yeye na mama…’akasema.
‘Najua wengi watasema..mnaona,
kumbe bibi yake ndiye aliyemfundisha mambo hayo mnayoyamini ya kishirikina,
lakini sivyo hivyo, huyu mama alitunukiwa kipaji cha kuweza kuwafunguza akina
mama , na alifanya hayo na kuwaokoa wanawake wengi waliofikia muda huo, na
wasingeliweza kufika hospitalini, kwa vile hospitali ipo mbali, nyote mnafahamu
hali ya nchi yetu……Imebidi nifafanue hapo kwa vile kama mnavyosikia kuongea
kwake.
Wakili wa utetezi akatoa pingamizi na kusema;
‘Mbona tunamsiki a, ..hicho kipaza sauti kimewezesha
kumsikia vyema, usijifanye mjanja wa kuingizia maneno yako ya kisiasa, fuata
sheria…’akasema wakili huyo na hakimu akasema
‘Endelea na shahidi yako wakili mwanadada, na fuata taratibu…’akasema
hakimu.
‘Kwahiyo ukawa unafanya kazi hiyo kwenye kijiji, pamoja na
bibi yako na mama yako, je hawo watu wapo hai?’ akauliza.
‘Hapana wameshatangulia mbele ya haki…’akasema huyo shahidi.
‘Pole sana yote ni matakwa
ya muumba, kwani kama wengelikuwepo hai huenda wangelisaidia hili
kuonyesha kuwa imani walizokuwa nazo watu dhidi yako ni dhana potofu sio sahihi…’akasema
na wakili wa utetezi alitaka kutoa pingamizi lakini wakili mwanadada akaendelea
kumuongoza shahidi wake.
‘Je kazi hiyo ulikuwa ukiifanya mwenyewe, ….yaani anapotokea
mtu anataka kujifungua kwa dharura na akaomba umsaidie, ..uliweza kuifanya kazi
hiyo peke yako?’ akaulizwa.
‘Mara nyingi sana, nakuwa nawasaidizi wangu,….naweza kusema
siwezi kuifanya kazi hiyo peke yangu bila msaidi, kutokana na kazi yenyewe
ilivyo…’akasema.
‘Je kuna ugumu gani katika kuitekeleza k azi yako hiyo au ni
magumu gani uliweza kukutana nayo katika kuitekeleza kazi yko hiyo?’ akaulizwa.
‘Yapo machache, na hayo machache yanatokea kama mzazi ana
matatizo mengine ambayo mimi nisingeliweza kuyafahamu, kama vile ukosefu wa
damu, au kutoka damu nyingi..au shinikizo la damu…na vitu kama hivyo.’akasema.
‘Sasa kama uliyajua hayo, uliwezaje kupambana nayo…?’
akaulizwa.
‘Kwanza ninapopata taarifa ya mja mzito, kitu kikubwa
nawauliza wahusika au muhusika kama ana tatizo kama hilo, na je ameshawahi kwenda
kiliniki, na kwanini wanaamua kumleta kwangu badala ya kumpeleka hospitalini.
Lakini hayo hutokea, mara nyingi ni kwa vile mja mzito huyo kafikia muda wake
na hakuna njia nyingine, ila nikumsaidia ajifungue…’akasema.
‘Kwahiyo ulikuwa ukiitwa kama hali ya kujifungua
imeshafikia, na je kama utamkuta hali hiyo haijafikia ulifanayaje?’ akaulizwa.
‘Kama hali yake ya kujifungua haijafikia, huwa nawaomba
wananduguu tuongozane, hadi hospitalini…’akasema.
‘Kwanini muongozane
nao?’ akaulizwa.
‘Ili kama atazidiwa njiani niweze kutoa huduma
hiyo…’akasema.
‘Ndugu muheshimiwa hakimu, naona twende hatua kwa hatua,
labda niwapishe wenzetu katika sehemu hiyo kabla sijaendelea naye sehemu ya
pili, kama wapo tayari, kama hawana maswali ngoja mimi niendelee naye…’, na
kabla hajamaliza, wakili wa utetezi akasema;
‘Nashukuru kwa taratibu zenu hizo za sehemu ya kwanza ya
pili..haya tutafanyaje, na nyie ndio waendeshaji iwa hii kesi, lakini kwetu
sisi hatuna shida,….ngoja nimuulize shahidi wako, ambaye umeamua kumficha
…sijui na huu ndio utaraibu wenu mwingine,….’akasema huyo wakili na kumsogelea
huyo shahidi huku watu wakijizuia kucheka, kwa jinsi alivyo kuwa akiigiza.
‘Mama wewe unasema ni mkunga wa jadi..je una kibali chochote
cha kazi hiyo?’ akauliza.
‘Ndio ninacho..lakini kiliisha wakati wake, na kipindi
nafuatilia kuongezwa muda, ndo yakanikuta haya…’akasema.
‘Unaweza kutuonyesha hicho kibali…’akauliza na wakili
mwanadada akaingilia na kusema;
‘Kama utakihitaji hicho kibali sisi tutakionyesha kama moja
ya ushaidi, kwa hivi sasa hana hicho kibali hapo alipo, kwasababu ambazo
tutakuja kuzielezea baadaye….’akasema mwanadada na huyo wakili wa utetezi akawa
anamwangalia huyo mwanamama kwa makini kama vile anataka kujua sura yake,
lakini hakufanikiwa.
‘Je una zahanati, au una sehemu maalumu ambayo unaifadhi
vyombo vyako, maana kazi hiyo inahitajia uangalifu wa hali ya juu, au zahanati
yako ni kila mhali kwa wakati wowote..?’ akauliza.
‘Kazi ya ukunga wa jadi ni kama huduma ya kwanza..ndio
ninavyo vifaa, lakini sina zahanati,…’akataka kuendelea lakini wakili mwanadada
akaingilia kati.
‘Kama unahitajia kuviona vifaa vyake, na jinsi gani
anavyofanya, hayo tutayatoa kama ushahidi baadaye…’akasema wakili mwanadada.
‘Wewe unasema kazi hiyo uliipata kwa bibi yako, je bibi yako
licha ya kazi hiyo ya ukunga wa jadi, alikuwa akitambulikana kwa kazi gani
nyingine….ambayo pia alikurisisha?’ akauliza.
‘Alikuwa mtaalamu wa tiba asilia..’akasema.
‘Alikuwa akitibia kwa uganga wa kienyeji, kama vile kuagua..kupiga
ramli,….mashtani , na vitu kama hivyo?’ akauliza
‘Tiba asilia zinajulikana zilivyo….na kumbuka enzi zao,
ilikuwa ndio tiba iliyotambulikana…na sasa watu wanaanza kuiletwa wazi kwa
utalaamu wa kisasa..’akasema.
‘Je pamoja na tiba hiyo asilia, hakuwa na sifa nyingine,
ambayo watu walikuwa wakimsifia nayo..?’ akauliza na watu wakaguna
‘Kama ipi, maana unavyoelezea ni kama vile unafahamu kuwa
alikuwa na sifa nyingine..ambayo sijui ni ipi?’ akauliza.
‘Watu walikuwa wakimuogopa, kuwa ana nguvu za giza…ni kweli
sikweli, kama walivyokuja kukuogopa wewe…’akasema na watu wakaguna na wengine
kucheka.
‘Je unaamini hayo?’ Shahidi akauliza.
‘Nijibu swali langu…hujaambiwa uniulize swali mama…umemuomba
muheshimiwa hakimu kuwa unataka kuniuliza swali….?’akasema huyo wakili.
‘Nitakujibu swali kutokana na imani yako, kama unaamini au
huamini, kwasababu nikikujibu kiimani hizo na wewe huamini haitasaidia
kitu..’akasema huyo mama.
‘Je mama yako aliwahi kushutumia, au kuongelewa kuwa na sifa
hiyo ya nguvu za giza, ….?’ akaulizwa tena.
‘Hayo ni maneno ya watu,…ambayo yalianza baada ya mama na
bibi kuondoka, lakini wakati wapo hai, watu walikuwa wakiwaheshimu kwa jinsii
dawa zao zilivyokuwa zikiwasaidia watu, waulize wazee wa siku nyingi
watakusimulia…’akasema.
‘Hayo maneno ya watu yalisema nini?’ akauliza.
‘Kama hivyo ulivyoosema wewe…’akasema na watu wakacheka.
‘Mama tusipoteze muda, jibu swali langu…’hapo wakili
mwanadada akaingilia kati na hakimu akasema kuwa wakili wa utetezi aulize swali
la msingi, asiulize swali la kusikia…’akasema hakimu.
‘Ni hayo kwasasa muheshimiwa hakimu….’akasema wakili wa
utetezi na kurudi sehemu yake, na alipofika sehemu yake…akamsogelea mteja wake,
ambaye alikuwa kainama kwenye kiti huku akiwa kaangalia mbele, kuonyesha kuwa alikuwa
akimuangalia shahidi kama walivyokuwa wakifanya watu wengine…lakini ule ukaaji
wake ulitia mashaka maana alikuwa katulia nakichwa kipo kama kimeinama kwa
nyuma na macho hayapepesi.
Wakili huyo akajifanya kama hakuna kitu akasogea na kukaa
sehemu yake, na hapo akamshika kwenye paja , ili watu wasimuone, na akawa kama
anamtikisa, lakini jamaa yule alikuwa kakaa vile vile, na hapo wakili huyo
akagundua kuwa kuna tatizo, akageuka kumwangalia, msaidizi wake na wakawa
wanateta.
Wote wakamsogelea huyo mshitakiwa mkuu, na kujaribu kumuita
na kumtikisa, lakini alikuwa kimiya..kimiya..hakimu kumbe naye alikuwa
akiifuatilia ile hali, akauliza kuna tatizo gani
‘Muheshimiwa hakimu, mshitakiwa anaonekana ana tatizo…’akasema
wakili.
‘Ana tatizo gani?’ akauliza hakimu, na mlinzi akamsogelea na
kumchunguza halafu akageuka kumwangalia hakimu;
‘Anaonekana kapoteza fahamu….’akasema mlinzi
‘Watu wa huduma ya kwanza wafike wamuangalie, wengine wote
mtulie kama mlivyo..’akasema hakimu.
‘Natoa dakika kumi, …baaada ya hapo tutaangalia kama
tunaweza kuendelea au kuahirisha hadi siku nyingine..’akasema hakimu, na
akawageukiwa watu wa huduma ya kwanza, ambao walikuwa wakitoa huduma zao kwa
huyo mshitakiwa mkuu, na walipomaliza, akawauliza;
‘Mnasemaje, kuna tatizo lolote?’ akauliza.
‘Mshitakiwa kapoteza fahamu…anahitajika awahishwe hospitalini
kwa matibabu…’wakasema
‘Basi kama ni hivyo, tutaahirisha hii kesi ..hadi kesho….na
taarifa zaidi mtapatiwa…’akasema na kesi
ikaahirishwa.
NB: Je ni kwanini
huyo mshitakiwa akapoteza fahamu….na je itakuwaje.. tuzidi kuwemo kwenye kisa
hiki kinachoendelea mwishoni.
WAZO LA LEO: Kuna
tabia sasa hivi ya watu kujichukulia sheria mikononi mwao, watu wanapiga hadi
kuua, wanachoma atu na nyumba zao, je ina maana ubinadamu tena hakuna, na kati
ya hawo, kuna wengine hawana kosa kabisa, walituhumiwa tu, au chuki zao
zimakimbilia kupakaziana ubaya,….kwanini tunaamua kumuadhibu mtu bila kuhakiki
kuwa kweli ni mkosaji, je tuna mamlaka gani ya kuchukua hatua hiyo..hiyo sio
vyema, kwani kosa ni kosa pale linapothibitishwa kisheria kuawa ni kosa,na
hukumu yake itaainishwa kisheria. Kama wewe utachukua sheria mikononi mwako ujue
na wewe unatenda kosa.
‘
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Mmh, majanga ndugu yng. Ngoja tusubiri tuone huyo alipoteza fahamu
Post a Comment