Kesi yangu iliahirishwa na kesi kubwa ikatangazwa kuanza
rasmi, kesi hii ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu na wengi, kwani watu wengi
walikamatwa.
‘Kwanini wanaipia kesi yangu kalenda, au kuna jambo?’
nikamuuliza wakili mwanadada, akaniangalia kwa makini , kama anawaza ni kitu
gani cha kuniambia hadi nikaingia na wasi wasi kuwa huenda kuna tatizo kwenye
hiyo kesi yangu na huenda keshafahamu, lakini hataki kuniambia ukweli
Akasema kuwa hakimu kajitetea kwa kusema ;
‘Nimefanya hivyo kwa vile, ndio nimefika kwenye mahakama hii hapa kwa
mara ya kwanza, na kwa bahati mbaya sikuweza kupata muda wa kuongea na
mwenzangu aliyeondoka, kwani nilipatwa na dharura, na yeye aliwajibika kwenda
haraka kwenye kituo chake, kipiya,huko alikohamishiwa kabla hatujakabidhiana,
kwahiyo imeniwia vigumu kutoa hukumu bila ya kuipitia upya ili nijue ni kitu
gani kilichokuwa kikiendelea….’akaelezea.
‘Na tatizo jingine, nimeambiwa kuwa wahusika wengi wa kesi
hii , pia wanahusika na kesi nyingine inayoendeshwa kwenye mahakama za juu,
kwahiyo hawataweza kusimama kwa wakati mmoja, wameniomba hivyo, kwahiyo tuwe na
subira, ….’akasema hakimu.
Wakili mwanadada hakutaka kushinikiza lolote kwa hilo,
akamshauri mteja wake kuwa avute subira kwani kesi zote ni za ushindi, na
matokea ya kesi hiyo kubwa, yataamusha ari za wengi, kwani wakosaji
watajulikana na kulimaliza kabisa hilo tatizo kwenye kijiji chao.
‘Mimi nimependelea iwe hivyo, kwani kesi hiyo kubwa
itafichua mengi,…kuna mengi yamejificha hayajagundulikana, na kuna watu ambao
wameshajiona kuwa hawawezekani, kwa vile walishakuwa na ukaribu na wasimamizi
kwenye mahaka hii ya mwanzo,na hata kuwarubuni wasimamizi mbali mbali waliopewa
dhamana za usalama, na haki za raia…sasa huko juu wataumbuka…’akasema wakili
mwanadada.
‘Kwani hiyo kesi huko juu itasaidia nini, wakati muhusika
mkuu alikuwa ni marehemu?’ nikamuuliza wakili mwanadada.
‘Marehemu alikuwa ni chambo tu,….yeye amejikuta akiingia
kichwa kichwa kwenye bwawa la ruba, ..wewe subiri utaona jinsi gani kundi hilo
lilivyojipanga….kuna kundi, ambalo limekita mizizi hapa kijijini kwenu, na
liliweza kubuni mbinu nyingi ikiwemo hii ya kumulikisha mali za wanyonge isivyo
halali…na wana matawi, …wana watu wao kila kwenye vitega uchumi vikubwa’akatulia.
‘Sasa wewe umeyajuaje hayo?’ nikamuuliza.
‘Mimi ni wakili, na wakili mara nyingi, ili aiweze kazi yake
vyema, inabidi ajifunze upelelezi,ashirikiane na vyombo vya usalama…kwanii
unaweza ukakutana na mteja mjanja, au mteja, asiyetaka kusema kila kitu, na
wewe unahitajika kumtetea, na hujui kabisa uanzie wapi, utafanyaje…’akawa kama
anauliza.
‘Kama ni mteja wako, kwanini asiseme kila kitu, kwanini
akufiche?’ nikamuuliza.
‘Kuna wateja wengine lengo lao ni kuficha mambo yao, ….na
mawakili wengine wapo kwa ajili ya kupata pesa, kwa ajili ya maslahi, kwahiyo
wanafaya vile wateja wao watakavyo, hata kama wamegundua kuwa wateja wao sio
wakweli….na kuna wateja wengine wahakujui lolote kuhusu sheria na nin kilichowazunguka,kama
ilivyo ksei yako, kesi yako sio hivyo tu, kama unavyofikiria, kuna chanzo, kuna
tatizo la muda mrefu,lenye mizizi mirefu….’akasema.
‘Noja kwanza nikuulize swali, kwa mfano,wewe umepata mteja
wa namna hiyo, na lengo lake ni kutaka tu maovu yake yafichike, utafanyaje?’
akamuuliza swali na yeye akatabsamu, na akawa kama anachezea simu yake, na
kusema.
‘Hilo jibu lipo wazi, lakini ngoja nikuambie kitu, wakili
mzuri ni yule anayejali siri za mteja wake,…na hata kama atagundua hivyo, sio
vyema, kama wakili wake, kufichua siri hizo kwa vyombo vya usalama, au sio,
wakili ni kama dakitari anayeficha siri za mgonjwa wake……, cha muhimu ni kutoa
ushauri kwa huyo mteja,…sasa ni mawili kama kazi yako ni kwa ajili ya maslahi,
basi, utafanya apendavyo mteja wako, na mwisho wa siku utakuja kuumbuka, na
mimi sitaki iwe hivyo…’akasema wakili mwanadada.
‘Mimi sijakuelewa, ni nini maana ya wakili, ….mmh, wakili wa
kujitegemea?’ nikamuuliza.
‘Wakili wa kujitegemea ni wakili ambaye sio wa serikali, ina
maana yupo huru kufanya kazi kwa mtu yoyote, lakini akizingatia sheria na
kanuni za nchi…yeye kazi yake ni kumsaidia mteja wake, katika mambo yake
kisheria, baada ya kujua kiini cha tatizo, na kusikiliza maombi ya mteja wake, ni
nini anahitaji, ni nini tatizo, na kwanini inahitaji hivyo, sasa kazi yako kama
wakili wa kujitegemea, ni kuangalia sheria inasemaje, je ana haki, je kuna
uhalali, na wewe utamshauri mteja wako jinsi gani sheria inasema,na jinsi gani
anatakiwa afanye……’akasema wakili mwanadada.
‘Kwahiyo unasimama badala ya mteja wako, sasa kwanini
akishindwa wewe kama wakili usiwajibike, maana hukumtendea kile
alichokihitajia, na yeye alikuamini hivyo…na anakupia …au?’nikamuuliza.
‘Kama nilivyokuambia, kazi hii kama kazi nyingine ina
utaalamu wake, na sio wote mawakili ni mawakili kwa lengo moja la kutetea haki,
….kama ilivyo kazi nyingine, wengine wapo kimasilahi zaidi…na hawapo tayari
kumwambia mteja wake, kuwa hilo halitawezekana,….na wakati mwingine mteja
anafahamu hivyo kuwa halitawezekana, lakini kwa vile anahitajia kutetewa, anakuomba
ufanye uwezevyo, ….’akasema wakili mwanadada.
‘Ndio kazi yako hiyo?’ nikamuuliza na yeye akatabasamu, na
kuniangalia machoni, na kusema;
‘Kwasasa ndio kazi yangu….lakini katika kutetea haki , na
nia yangu ni kutetea haki za wanyonge wasiojua sheria, maana nimeona wengi wakidhulumiwa,….na
wengi wanajikuta haki zao zinapotea kwa vile tu hawajui sheria, kwa vile tu
wanapata vistihso kutoka kwa jamii, ….lakini kazi hii haitawezekana kama
wanyonge, kama hwo wanaodhulumiwa, hawatajitokeza na kusema …’akatulia kidogo
akipepeza macho.
‘Mkikaa kimiya, mkaogopa, basi haki zeni zitaendelea kupotea
na wajanja wataendelea kuneemeka…msiangalia gharama, kuwa labda sitaweza
kumlipa wakili….’akasema na kuonekana akiwaza jambo, na akaangalia saa yake, na
kusema.
‘Lakini mimi ninajua kuwa dhuluma ina mwisho wake,
wataneemeka mwisho wake waatumbuka…’nikasema.
‘Kuumbuka kwao kutategemeana na nyie kujitoa na kusema basi….kwasababu
imefikia hatua wanaodhulumu wameshajiamini…..wanajua nyie hamjui lolote,
wanajua kuwa kila nyanja, ipo mikononi mwao,…., na kila siku wanagundua mbinu mpya,
hasa huku vijijini….na kama nilivyokuambia, kuwa hawa wadhulumaji, wana pesa,
na kama wanapesa, wanataka pesa zao zifanye kazi, na ndio maana wengi wana
mwakili wao…hawaendi hivi hivi…’akasema.
‘Basi kama ni hivyo , kuwa wana pesa, na pia wana mawakili,…..wanyonge
hatuna chetu, tutatetewa na nani wakati hatuna pesa za kumlipa wakili…’nikalamika.
‘Pesa sio tatizo, pesa zitatoka kwa hawo hawo wadhulumaji…maana
ukimpata wakili akajua haki zako ni nini kisheria, atakusimamia, na huyo
anayekudhulumu,lazima atashindwa, na kwa vile mambo hayo yamekwenda kisheria,
huyo aliyetaka kukudhulumu na sasa ameshindwa anahitajika kulipa gharama zote….kwahiyo
wewe hujapoteza kitu, ila umefaidika kwa vile haki yako imerejea mikononi mwako…’akasema.
‘Ina maana nikishinda kesi yangu, sitahitajika kukulipa?’
nikamuuliza.
‘Utanilipa kwa kupitia kwa hawo,…..’kabla hajamaliza simu
yake ikaita, na yeye kwa haraka akaipokea na kuangalia ni nani aliyepiga, akasema
samhani kidogo, na kusogea pembeni kuisikiliza hiyo ilionekana hakutaka ni jue
ni kitu gani anaongea, na hili limekuwa likipa wasiwasi, nikijiuliza ni kwanini
huyu wakili wangu anakuwa msiri kwangu,….je kuna kitu gani kumbwa, ambacho mimi
sitakiwi kukijua,…nikasema ni ni lazima nimuulize
Yeye akaendelea kusikiliza hiyo simu, na baadaye nikasikia
akisema;
‘Kwahiyo una uhakika ndio yeye..na kama ni hivyo kwanini
hajakamatwa na polisi?’ akauliza na kusikiliza tena kwa muda, na baadaye
akauliza swali lile lile.
‘Sasa kwanini hawamkamati?’ akauliza.
‘Ok,sawa nimekuelewa…..baadaye.’akasema na kukata simu.
Akanisogelea akiwa na tabasamu mdomoni, akasema ;
‘Haki wakati wote ina nguvu…na ni bora ukasimamia kwenye
haki na ukweli hata kama ni kujitolea kuliko kusimamia kwenye dhuluma, ambayo
utapata uatajiri usio na heri.Mimi ndio dhamira yangu, na hii kazi ukiwa na
msimamo huo, hutayumba na wakati wote, unajiona tajiri, hata kama huna pesa
mfukoni, ….unajiona wewe ni mshindi….’akasema.
‘Kwani vipi?’ nikamuuliza.
‘Utaona huko mahakamani, maana wahusika wakuu, waliojificha
chini ya kivuli cha dhuluma, watajitokeza wenyewe mmoja baada ya mwingine, cha
muhimu ni kuwa walioshikwa wote, wamekubali kusema ukweli, na kutoa sirii yote,
na wamesema hatawaficha kitu…’akasema.
‘Ina maana gani hiyo?’ nikamuuliza.
‘Ina maana kuwa zoezi lilipita hapa kijijini lilikuwa la
kuwaokoa watu ambao kama tungelichelewa, huenda wangeliuwawa kwa vile wanajua siri,
na walionekana kuwa wanaweza kuitoa hiyo siri…na kiukweli,katika zoezi hilo
lilifanywa makusudi, kwa waliokuwepo na wasiokuwemo ili kuficha kusudio …lakini
lengo ni kupata ushahidi, hayo utakuja kuyagundua baadaye,…na wengi waliokufa,
hawakufa kwa vifo vya kawaida, waliuwawa,….’akasema.
‘Una maana gani, ina maana hata shemeji aliuwawa, ….alipewa
sumu, kama tulivyokuwa tukifikiria?’ nikauliza.
‘Wewe subiri…sasa hivi kuna kikosi maalumu, ambacho
kimatumwa rasmi, hakijulikani, na wala hakibabaishwi na pesa za hawo watu, kipo
kwa ajili ya kazi moja,….kuitafuta haki, …haki iliyokuwa imenyang’anywa kwa
wanyonge…’akasema mwanadada.
‘Mbona huniambii ukweli..na naona kama unanificha ficha, ….unanipa
wasiwasi na mimi’nikalalamika.
‘Ukweli utapatika mahakamani..sisi tuatongea tu, lakini
mwisho wa siku sheria itasimamia haki na ukweli utajulikana, usiwe na wasiwasi…nipo
na wewe na kwa ajili yako nay a wanyonge wengine.’akasema.
‘Kwahiyo wewe utasimamia hiyo kesi kubwa?’ akaulizwa.
‘Wameniomba iwe hivyo, nimewaambia nitakuwa msaidizi tu…..lakini
hapo sasa sitakuwa wakili mtetezi, nitakuwa nikiisaidia serikali, ili haki ya
wanyonge irudi kwa wahusika…’akasema.
Na mara mlango ukagongwa, akaja baba yangu wa kufikia, na
alipotuona, kwanza alikunja uso, na baadaye , akatabasamu kidogo na kusema;
‘Sikutaka kabisa kuja hapa, ….uliniuzi sana siku ile,
kutokubali ushauri wangu,…lakini nimefikiria sana, nikaona sio kosa lako…’akasema.
‘Lakini baba….’nikaanza kujietetea.
‘Najua sio kosa lako…nimekuja kulifahamu hilo, ila ujue kuwa
hawo watu sio watu wema kabisa, hata kama utajitahidi kuwakumbatia vipi, …hawatakusaidia
kitu, wakipata wanachokitaka,…watakugeuka, hawana urafiki wa kudumu, urafiki
wao ni wa maslahi tu…’akasema.
Wakili mwanadada akaingilia kati na kusema;
‘Msijali, yote hayo yanatokea kwa jinsi maalumu, sio hivi
hivi tu, kila hatua ina jambo lake,..cha muhimu ni kujaribu kufuta kila
nitakachowashauri…wakati mwingine tunaweza kuwatumia kama chambo, lakini kwa
nia safi, huku tukilinda usalama wenu, nakushukuru sana, baba, nilijua
hutaogopa…’akasema wakili mwanadada.
‘Mimi nimeshajitolea,..hata nikifa, sitajutia, kwani ninajua
nimekufa kifo cha kihalali, kama shujaa , ….sitaweza kukaa kimiya na kufa
kikondoo, kwasasa nipo tayari kwa lolote, lile, …’akasema baba wa kufikia na
mimi sikujua kabisa wanaongea nini, na hata nilipojaribu kuuliza , wakili
mwanadada alisema;
‘Ni bora usijue ni kitu gani kinachoendelea kwasasa hadi
wakati muafaka utakapofika, yote ni kwa ajili yenu, ..mliodhulumiw haki zenu,
ni kwa ajili ya wale, wasio na sauti,…ambao kila kukicha wanajikuta wakitoa
machozi moyoni, kwani machozi ya machoni yalishatoka na kukauka, …..’akasema
wakili mwanadada, huku machoni akionekana kama analengwa lengwa na machozi, na
baba akamsoegelea na kumshika , kama vile anamkumbatia, akasema;
‘Tupo pamoja, wakili mwanadada, hata nikifa sasa, ninajua
kuwa nimejitahidi kutimiza adhima yangu, ninakushukuru sana, na kuanzia leo
wewe ni binti yangu wa pili, …..wa kwanza ni huyu hapa…’akasema akinionyeshea
mimi nimsogelee na kunivuta na wote tukajikuta tumekumbatiana, na huku sijui ni
ni kitu gani kinaendelea.
NB: Haya kesi hiyo inanukia, kuna nini.
WAZO LA LEO:
Usiogope kutetea haki yako, hata kama hawo wanaokudhulumi ni matajiri, wana
nguvu. ni viongozi, wenye mamlaka. Nguvu zao hazina maana mbele ya haki , ukiwa kwenye haki na ukweli, upo
pamoja na mwenyezimungu, na mwenyezi mungu hashindwi na yoyote yule.
Ni mimi:
emu-three
3 comments :
Yaah, Ni kweli hakuna zaidi ya mungu ndugu yangu. Gd day.
Yaah, Ni kweli hakuna zaidi ya mungu ndugu yangu. Gd day.
Muy, muy
shayaOi bb4arg48
Post a Comment