‘Kwahiyo kumbe sio yeye aliyekuokoa kwa wale wabakaji?’
nikamuuliza wakili mwanadada.
‘Ndiyo yeye,aliyeniokoa na mwenzake …lakini walipomaliza
kuniokoa na kunipeleka hospitalini, mwenzake akawa mwepesi zaidi, kwa vile
alikuwa na pesa, na pili huyo mwanasheria ilionekena hakupenda sana kubembeleza,
kwa jinsi nilivyokuja kumuona baadaye…’akasema wakili mwanadada.
‘Kwahiyo ikawaje?’ nikamuuliza.
‘Aaah…, sijui siku ile ilikuwaje, maana japokuwa kiukweli
nilishavutika na huyo mwanaume aliyenisaliti, siwezi kusema nilivutika na yeye
kwa vile nilishampenda, sikuwa na uhakika na hilo, maana akili yangu haikuwa na
mawazo hayo kwa kipindi hicho,…akili yangu ilikuwa imeliweka hilo pemebeni
kabisa, ila kwa matukio yaliyotokea hapo chuoni, ilishafikia muda nikasema,
kwanini na mimi nisiwe na rafiki wa kiume, …basi kama ni hivyo, huyo mwanaume msaliti atanifaa, huenda ndiye chaguo
langu, ngoja nijaribu kuwa naye…lakini….’hapo akasita.
‘Lakini….?’ Nikamuuliza.
‘Nilikuja kumchukia…unajua kuchukia , utazania alinifanyia
kitu gani kibaya, fikiria tulikuwa hatujakubaliana kuwa wapenzi, na ikatokea
hivyo …kumkuta akiwa na mwanamke mwingine, wakitenda tendo hilo…yaani niliona
kuwa nikamfumania. Yaani moyo wangu uliona kanifanyia mabaya yasiyosameheka….nikajigundua
kuwa nina wivu wa kupindukia…’akasema wakili mwanadada.
‘Ni ni kweli una wivu kiasi hicho….?’ Nikamuuliza, na yeye
hakujibu hilo swali akaendelea kuongea;
‘Sasa kilichofuata, ikawa kama vile nalipiza kisasi, kwani
niliamua kuwa na huyo mwanasheria, huyu aliyekuja na kunidaka wakati nataka
kudondoka, ambaye ndiye huyu, tunayemzungumzia,na tukachukuana hadi kwenye
bustani za shule na kukaa naye, yeye alikaa na kunyosha miguu, na mimi nikajilaza
kwenye miguu yake , kitu ambacho sijawahi kukifanya kwa mwanaume yoyote, na
muda huo akaja yule mwanaume mwingine akiwa kachanganyikiwa akatuona tukiwa
tumekaa vile.
‘Vipi mumemaliza…?’ rafiki yake akamuuliza, na huyu mwanaume
msalaiti hakuweza kujibu, akaja na kupiga magoti mbele yangu, huku akionyesha
kuhuzunika kwa kitendo alichokifanya, lakini mimi sikutaka kabisa kumsikiliza.
‘Nakuomba mwanadada, unisamehe, ibilisi alinizidi, na kwa
vile nimekuwa siku nyingi bila …..nikashindwa, kuvumilia…na wewe sikutaka
kukulazimisha….’akawa anaongea huku akiwa kapiga magoti. Niliinuka pale
nilipokuwa nimejilaza, nikakunja magoti, huku nimeweka kichwa kwenye magoti,
sikutaka kabisa kumwangalia machine, nikasema kwa sauti kali;
‘Tafadhali, Nakuomba uondoke,… tafadhali..nisije nikakuumbua
….’nikasema na nilipoona haondiki, nikainuka kutaka kuondoka, na yeye
akanifuata na kujaribu kunishika , niligeuka na kumwangalia kwa jicho baya,
hadi yeye mwenyewe akarudi nyuma.
‘Nisamehe mwanadada, sitarudia tena….’aaksema huku akiwa
kajishika kifuani kama vile anatubu madhambi yake.
‘Sitaki kuwa rafiki na wewe, …kuanzia leo, mimi na wewe
basi, tusijuane kabisa….’nikasema na wakati huo rafiki yake alikuwa kasimama, na kusogea pembeni
kutupa nafasi ya kuongea, na mimi nikamgeukia yeye , nikamuuliza;
‘Upo tayari kuwa na mimi au….?’ Nikamuuliza, na yeye akaja
akiwa na mshangao machoni, bila kumwangalia rafiki yake, akanishika mkono
tukaongozana hadi chumbani wanapoishi , na humo nikamkuta msichana akiwa kakaa kwenye
kitanda, huku akiwa tayari kuondoka, na alipotuona tu, akainuka kwa haraka, na
kutoka nje, na huyo mwanasheria
akaniambia huyo ndiye mwanamke wa huyo rafiki yake.
‘Ina maana unafahamu kuwa ni mpenzi wake wa siku nyingi?’
nikamuuliza.
‘Nafahamu….kabla wewe hujafika hapa chuoni, huyo ndiye
mpenzi wake, lakini huenda alitaka kumbwaga na kukuchukua wewe….’akasema.
‘Ndio tabia zenu, eeeh,?’ nikamuuliza.
‘Sio mimi, ulishawahi kuniona nikiwa na rafiki mwanamke hapa
chuon, tangu ufike ulishawahi kuniona nikiwa nimeongozana na mwanamke kama
rafiki,…. hebu ulizia watu,…mimi sijawahi, kwavile sikuwa na mpango huo kwa
sasa, ila wewe peke yake, umeonekana kunigusa
moyo wangu, wewe ndiye uliyenivutia na alipokuwahi rafiki yangu,
nikasema basi tena, na sitaku kamwe kugombea …….’akasema na nilimwamini hapo hapo sijui
kwanini.
‘Kwahiyo ukamkubali japokuwa ulikuwa hujampenda,…?’
nikamuuliza na yeye hakujibu swali kama nilivyomuuliza, akasematu;
‘Urafiki wetu ndipo ulipoanzia hapo…..
*********
Wakili mwanadada alifika kwa mjumbe akiwa na azima ya
kumuliza mjumbe baadhi ya maswali ambayo alitaka kuwa na uhakika nayo,
hakumuelezea lolote mteja wake, yaani mwanamama, alitaka hilo wazo alilo nalo
kichwani lisijulikane hadi hapo atakapokuwa na uhakika nalo. Na alipofika hapo
kwa mjumbe, akakuta watu wamejazana, akasimama, na kuangalia huku na kule,…akamsogelea
mwanamama mmoja na kumuuliza;
‘Mbona kuna watu wengi hapa kwa mjumbe?’ akamuuliza huyo
mwanamama aliyekuwa kasimama nje, maana ilionyesha wazi kuwa ndani kwa mjumbe
kulikuwa kumejaa.
‘Wewe huna habari?’ akaniuliza kwa kuonyesha mshangao.
‘Habari gani hiyo?’ mwanadada akauliza.
‘Jana usiku tumeingiliwa na maaskari…hii ni mara ya pili,
ila safari hii wamezidi, maana imekuwa kama uvamizi wa kijambaz. Wameingia kila
nyumba baada ya nyumba, wakikuta mwanaume wanamkamata wanamfunga pingu
wanaondoka naye….ndio maana unatuona wanawake watupu, hatujui ni kitu gani
kimewasibu wanaume zetu na watoto wetu…’akasema.
‘Hata watoto wamekamatwa?’ mwanadada akaulizwa akionyesha
kushangaa.
‘Waliokamatwa ni vijana wakubwa, sio watoto, lakini mtoto
kwa mzazi wake ni mtoto au sio…’aksema.
‘Kwani tatizo ni nini mpaka wote wakamatwe, sizani polisi
wangelifika na kukamata watu bila sababu maalumu?’ akauliza mwanadada na huyo
mama akamwangalia huyo wakili akionyesha kukerwa, na akasema;
‘Ndio maana tumekuja hapa kwa mjumbe tujue sababu ni nini…tungelijua
tatizo, tungelijua ni nini cha kufanya….kwani wewe ni nani…?’akauliza na huku
akimwangalia huyo wakili mwanadada, na mwenzake akasema.
‘Humjui huyo…ndio mchumba wa yule mwanasheria….humkumbuki’akasema
huyo mwanamama mwingine. Na mwanadada akauliza;
‘Sasa mjumbe yeye kasemaje?’ mwanadada akauliza.
‘Mjumbe naye hayupo, inasadikiwa kuwa huenda alipata taarifa
hii mapema akakimbia kujificha, ..’akasema huyo mwanamke mwingine.
‘Sasa kwanini akimbie kujificha?’ akauliza wakili mwanadada
kitabasamu kwa kushangaa.
‘Labda na yeye alihitajika kukamatwa, au alipata taarifa
mapema kuwa watamkamata , au watu watakamatwa, kwahiyo yeye akatafuta kisingizio
, au vinginevyo, amejificha kuogopa wananchi kuwa watakuja
kumlalamikia..’akasema huyo mama.
‘Mlipomuuliza mkewe amesema nini…?’
‘Mkewe anasema mume wake alimuaga kuwa wana kikao, …toka
jana, hadi leo hajarudi, kwahiyo hajui wapi alipo, na inaonyesha kabisa kuwa
anafahamu wapi alipo, lakini anaficha siri ya mumewe..’akasema mama mwingine
aliyetoka kwa muda huo, yeye alikuwa huko ndani.
‘Sasa nyie mna maamuzi gani?’ akawauliza.
‘Sisi tumepanga kuwa tunaandamana hadi kwa katibu kata
mtendaji, naye kama hana jibu tutakwenda ofisi za wilaya….’akasema huyo mama akigeuka
kuwaangalia akina mama wengine, ambao walikuwa wakitokea huko ndani, na
ilionyesha dhahiri kuwa huyo ndiye msemaji wao mkuu.
‘Lakini mnafikiri ni kwanini harambee au zoezi hili,
limefanyika, hivi kweli watu watakamatwa hivi hivi bila jambo, hamuoni kuwa
kuna sababu…..?’ akauliza mwanadada.
‘Tungelikuwa tunalijua hilo tusingelikuwa na wasiwasi,
tungefahamu ni hatua tufanye, ….sasa hivi wanatupa wakati mgumu, maana badla ya
kuhangaika na majukumu yetu ya ndani na mashambani, tunahangaika kuwatafuta
waume zetu, na hawa watu hawajui kuwa sisi tunawategemea waume zetu,..hiyo
serikali ituambie tutakula nini, kama wamewashikilia waume zetu…watupe pesa za
matumizi…’akasema huyo mwanamama msemaji wao, na wenzake wakamshangilia.
Baadaye kidogo ,mjumbe akafika, na alipoona kundi la akina
mama, akajifanya kushangaa, na kuwasogelea, akauliza.
‘Jamani kuna tatizo gani?’ akauliza huku akiangalia huku na
kule kama anaogopa au kama anachunguza jambo.
‘Mjumbe usijifanye hujui ni kitu gani kimetokea, …hii
imekuwa ni tabia yako, pindi kukitokea jambo, unatoweka ghafla, na unakuja baadaye,
na ukijifanya hujui lolote, hili la sasa litakuumbua..’akasema huyo msemaji wao
mkuu.
‘Jamani mimi sijui chochote kwani hakuwaambia mke wangu,
kuwa tulikuwa na vikao vya chama, tunajiandaa kwa kampeni za uchaguzi, kwahiyo
jana nimeshinda huko kwenye ofisi za chama, na tumelala huko huko, sijui kabisa
ni nini kimtetokea…’akasema.
‘Kama hujui kweli, haya, fuatilia ni kwanini wanaume zetu
wamekamatwa usiku, bila taarifa yoyote, na hatujui wamepelekwa
wapi..sisi hapa hatujala, hatuna pesa za matumizi.....mimi hapa naumwa nina presha, ’akasema mama mmoja mnene na wenzake wakawa kama wanamliwaza.
‘Sasa mimi nifuatilie wapi, nyie ndio mliokuwepo wakati
wanakamatwa, kwanini msiwaulize hao polisi, kisa cha kutuvamia usiku na kuwakamata
waume zetu ni nini, tumekuwa majambazi, kwanini hatuna amani kwenye kijiji
chetu…’akasema huyo msemaji wao mkuu.
‘Ina maana hawakusema lolote…?’ akauliza huku akionyesha
mshangao, na kutaka kujua zaidi.
‘Hawakuta kusema lolote, walifika na marungu na pingu
mikononi na silaha, kila nyumba ilipitiwa na akikutwa mwanaume, au kijana wa
kiume wote walisombwa kwenye karandinga..’akasema mama mmoja.
‘Kama ni hivyo watakuwa wamewapeleka kituo cha polisi cha
mjini, labda ni kuhusiana na hiyo kesi inayoendeshwa kwa sasa, na huenda wanajaribu
kupata maelezo, …na kama ni hivyo , haitachukua muda wataachiwa, ni bora
mkavuta subira…kwasababu kesi hiyo kesho inaanza kuskilizwa’akasema mwanadada.
‘Mbona wewe mwanadada unaongea kama vile unafahamu kwanini
imetokea hivyo..’akasema huyo msemaji wao mkuu.
‘Mimi naongea hivyo kwa vile ninajua mbinu za maaskari
wanapokuwa wanawatafuta wahalifu,…lakini sina uhakika wa moja kwa moja kuwa
huenda ni hivyo au kuna jambo jingine..’akajitetea mwanadada.
‘Wahalifu, unaita wanaume wetu wahalifu , tuombe razi wewe
binti….’akasema mama mmoja.
‘Sina maana kuwa wanaume wenu ni wahalafu, ila nasema wakiwa
wanamtfauta mhalifu, wnafnaya hivyo, na mara nyingi mhalafu anakuwa pamoja na
sisi….’akasema huyo mwanadada, na yule mzungumzaji mkuu akamgeukia mjumba na
kusema;
‘Sasa ili kuondoa huo utata, sisi na mjumbe tunakwena mguu
kwa mguu hadi kituo hicho cha polisi, hatukuachii mjumbe, maana hili sasa
limekuwa ni tatizo, hatulali…hatuna raha na waume zetu,kila siku tunavamiwa na
polisi kwanini?’ akawa kama anauliza msemaji mkuu.
‘Tumechokaa, twendeni…..’wakasema akina mama kwa pamoja.
‘Mimi kwakweli sina muda huo, ,maana nilikuja mara moja
kuchukua baadhi ya makabrasha yangu, hamuoni kuwa nipo kazini….ninahitajika
kurudi…. , ninarudi kikaoni..’akasema mjumbe akionyesha wasiwasi.
‘Mjumbe wewe ni kiongozi wetu, na kama tatizo limetoka kwenye
nyumba zako,unafikiri ni nani atatuongoza, …wewe ndiye mjumbe wetu, tunaamini
utatusaidia kwa hili, vinginevyo , ukiri kuwa kazi imekushinda, ili
tujichukulie madaraka wenyewe, na ufanye hivyo kwa maandishi…’akasema huyo
msemaji wa mkuu, na wakili mwanadada akamwangalia mjumbe ambaye alikuwa
akihangaika, akitaka kupita kwenda ndani, lakini ilikuwa vigumu, na
asingeliweza kuwakimbia watu kwa njia hiyo.
‘Mimi sijawaambia kazi imenishida, lakini nina majukumu ya
kichama, na wakubwa wananisubiri huko kwenye kikao,….’akasema na mara simu ya mjumbe
ikalia, na yeye kwa haraka akaipokea, bila hata kuangalia ni nani aliyepiga.
Akasema;
‘Mnaona wakubwa wananiita wameona nina chelewa, akaiweka
sikioni na kama vile kaguswa na kitu sikioni cha kumshitua akaisogeza mbali
hiyo simu na baadaye akairejesha sikioni na kusema;
‘Nani mwenzangu…?’ akauliza huku akiwa na wasiwasi, kwani
huenda aliyetaraji kumpigia sio yeye.
‘Unasema ni Mkuu wa kitu cha polisi, afande unasemaje..kuna
nini afande, maana watu wamejaa hapa wanauliza waume zao?’ akauliza huku
akiongea kwa sauti, lakini sauti yake ilimshitaki, kwani akionekaan kuwa na
wasiwasi,
‘Eti nini…kwani mimi nina kosa gani, mkuu …?’ akauliza ana
akasikiliza kwa muda halafu akasema kwa kigugumizi.
‘Mimi …hapana…unasema, kwanini nitafutwe..hapa mkuu, kuna
makosa…sio kweli..?’ akawa kama anajitetea na hiyo sauti nyingine na yenyewe
ikawa inaongea.
‘Sijakimbia mkuu , kwanini nikimbie,
kabisa…..nilikuwa…..niliitwa na ndugu yangu, anaumwa..ikabidi niende kumuuguza….nikalala
huko huko….’akawa anajiuma uma , akisahau kuwa alishawaambia watu kuwa alikuwa
kwenye kikao.
‘Sawa afande nitakuja…’akasema na alipokata simu, akainama
kuelekea ndani , na wale wanawake wakawa wanamuangalia wakita kujua ni kitu
gani kimetokea.
‘Sasa mjumbe mbona unatuweka hewani, unatuacha njia panda…?’
wakamuuliza.
‘Waume zenu wameshikiliwa na polisi, ili watoe ushahidi
kuhusiana na mauaji yaliyotokea hapa kijijini, kwa taarifa ya polisi , wanadai
kuna kundi linaloendeleza hilo wimbi la mauaji na ubabe, na kujichukulia sheria
mkononi, na wanasema mnawafahamu hawo wahalifu, lakini hamtaki kuwasema,…sasa
cha ajabu huyu mkuu anadai kuwa mimi ninawafahamu hawo wahalifu,..ngona niende
huko huko, nitapambana nao huko huko….’akasema akijipa moyo.
‘Mjumbe waume zetu wasipoachiwa, sisi tutasema ukweli wote,..’akasema
huyo mwanamke msemaji
‘Ukweli gani tena wewe, mbona unataka kunichanganya…’akasema
mjumbe akimwangalia huyo mwanamama.
‘Unaufahamu vyema huo ukweli wenyewe, ndio maana ulikumbia
na kujifanya ulikuwa kwenye kikao, kama sio kweli, mbona ulipoongea na hiyo
simu umewaambia polisi kuwa ulikuwa kwa ndugu yako mgonjwa, mbona hukusema kuwa
ulikuwa kwenye kikao kama ulivyotudanganya sisi, inaonyesha unafahamu fika kuwa
ungeliwaambia hivyo hawo polisi, wangefuatilia kuhakikisha kuwa kweli ulikuwa
kwenye kikao au la…’akasema huyo msemaji wao.
‘Kwahiyo mnataka kusema nini…..?’ akauliza kumkatiza huyo
msemaji mkuu, akijua kiozidi kuongea atamwanga mtama kwenye kuku wengi.
‘Kama upo na sisi, na sisi ni wanachi wako, tunakuhitajia
tuongozane mguu kwa mguu hadi huko kituoni, ili tujue makosa ya waume zetu,
vinginevyo, tutachukulia kkuwa umetuasi, na ukumbuke sisi ndio tuliokuchagua
…sasa kama hutaki kuwa na sisi , nenda kwa hawo waliokuchagua na sisi,
tutachagua mjumbe wetu mwingine….’akasema huyo mwamama msemaji wao na watu
wakamshangilia.
‘Jamani jamani..hebu tulieni….naombeni hili swala niachieni
mimi, mimi nitakwenda huko kituoni peke yangu, na nitawaletea ni nini kimetokea
, kwani tukienda kundi la watu, tutaanzisha jambo jingine….’akasema mjumbe, na
kabla hajamaliza, mara wakaonekana watu wakija muelekeo wao, na mjumbe alipowaona
, akajipenyeza kwenye kundi la akina mama na kujibanza kwenye ukuta, na
a,ipoona yupo kwenye sehemu ambayo wale watu wanaokuja hawamuoni, akatimua,
watu akabakia kushangaa.
‘Vipi jamani mjumbe mbona anakimbia, na hawa watu wanaokuja
ni akina nanii……?’ akauliza mmojawapo huku na wao wakiwa na wasiwasi.
‘Nafikiri mjumbe anafahamu kabisa ni kwanini wanaume zetu
wamekamatwa na yeye ni mwanaume, ndio maana akiwaona watu tu, anahisi ni hawo
maaskari wanakuja kumkamata na yeye, ndio maana katimua mbio…’akasema na akina
mama wakaangua kicheko, na kicheko chao kilinyamazishwa na ujio wa hawo watu, ambao
kwanza waliuliza huo mkusanyiko una maana gani.
‘Kwani nyie ni nani, maana mjitambulishe kwanza….’akauliza
msemajii mkuu.
‘Sisi tunatoka kituo cha polisi ni wanausalama, tumakuja
kuonana na mjumbe, je mjumbe yupo wapi?’ wakauliza
‘Mjumbe kaondoka sasa hivi, hatujui wapi alipoelekea,
inaonyesha ana haraka sana…’akasema mama mmoja mwenye udugu na mjumbe.
‘Anahitajika kituo cha polisi, mwambie kama tusipomuona leo,
tutamfuata kwa namna asiyoipenda yeye, …’akasema huyo jamaa na mwenzake akawa
anachunguza huku na kule, na baadaye akawa kama kaona kitu, akambonyeza
mwenzake kuonyeshea kule mjumbe alipokuwa kaelekea, na wote wawili wakakimbilia
huko alipoelekea mjuumbe
NB: JE kulikoni..
*********
WAZO LA LEO:
Unapotenda makosa, moyoni kunakuwa hakuna amani, na hutaweza kuishi kwa raha,
ukiwa na wasiwasi kuwa utagundulikana kwa makosa uliyoyafanya. Jitahidi kutenda
mema, pale unapotenda kosa, jitahidi
kutenda mema ili hayo mema yafute hayo makosa uliyoyatenda , kumbuka kuwa dawa
ya makosa ni kutenda mema.
********
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
Mmh ngoja tusubiri, wabaya ndo haooo washaanza kukamatwa.
Hi! I just wanted to ask if you ever have any problems with hackers?
My last blog (wordpress) was hacked and I ended up losing many months of hard
work due to no data backup. Do you have any solutions to protect against hackers?
Take a look at my web page: übersetzung kostenlos google (forum.anyface.ir)
Post a Comment