Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, July 11, 2013

WEMA HAUOZI-33


‘Kwahiyo kumbe sio yeye aliyekuokoa kwa wale wabakaji?’ nikamuuliza wakili mwanadada.

‘Ndiyo yeye,aliyeniokoa na mwenzake …lakini walipomaliza kuniokoa na kunipeleka hospitalini, mwenzake akawa mwepesi zaidi, kwa vile alikuwa na pesa, na pili huyo mwanasheria ilionekena hakupenda sana kubembeleza, kwa jinsi nilivyokuja kumuona baadaye…’akasema wakili mwanadada.

‘Kwahiyo ikawaje?’ nikamuuliza.

‘Aaah…, sijui siku ile ilikuwaje, maana japokuwa kiukweli nilishavutika na huyo mwanaume aliyenisaliti, siwezi kusema nilivutika na yeye kwa vile nilishampenda, sikuwa na uhakika na hilo, maana akili yangu haikuwa na mawazo hayo kwa kipindi hicho,…akili yangu ilikuwa imeliweka hilo pemebeni kabisa, ila kwa matukio yaliyotokea hapo chuoni, ilishafikia muda nikasema, kwanini na mimi nisiwe na rafiki wa kiume, …basi kama ni hivyo, huyo  mwanaume msaliti atanifaa, huenda ndiye chaguo langu, ngoja nijaribu kuwa naye…lakini….’hapo akasita.

‘Lakini….?’ Nikamuuliza.

‘Nilikuja kumchukia…unajua kuchukia , utazania alinifanyia kitu gani kibaya, fikiria tulikuwa hatujakubaliana kuwa wapenzi, na ikatokea hivyo …kumkuta akiwa na mwanamke mwingine, wakitenda tendo hilo…yaani niliona kuwa nikamfumania. Yaani moyo wangu uliona kanifanyia mabaya yasiyosameheka….nikajigundua kuwa nina wivu wa kupindukia…’akasema wakili mwanadada.

‘Ni ni kweli una wivu kiasi hicho….?’ Nikamuuliza, na yeye hakujibu hilo swali akaendelea kuongea;

‘Sasa kilichofuata, ikawa kama vile nalipiza kisasi, kwani niliamua kuwa na huyo mwanasheria, huyu aliyekuja na kunidaka wakati nataka kudondoka, ambaye ndiye huyu, tunayemzungumzia,na tukachukuana hadi kwenye bustani za shule na kukaa naye, yeye alikaa na kunyosha miguu, na mimi nikajilaza kwenye miguu yake , kitu ambacho sijawahi kukifanya kwa mwanaume yoyote, na muda huo akaja yule mwanaume mwingine akiwa kachanganyikiwa akatuona tukiwa tumekaa vile.

‘Vipi mumemaliza…?’ rafiki yake akamuuliza, na huyu mwanaume msalaiti hakuweza kujibu, akaja na kupiga magoti mbele yangu, huku akionyesha kuhuzunika kwa kitendo alichokifanya, lakini mimi sikutaka kabisa kumsikiliza.

‘Nakuomba mwanadada, unisamehe, ibilisi alinizidi, na kwa vile nimekuwa siku nyingi bila …..nikashindwa, kuvumilia…na wewe sikutaka kukulazimisha….’akawa anaongea huku akiwa kapiga magoti. Niliinuka pale nilipokuwa nimejilaza, nikakunja magoti, huku nimeweka kichwa kwenye magoti, sikutaka kabisa kumwangalia machine, nikasema kwa sauti kali;

‘Tafadhali, Nakuomba uondoke,… tafadhali..nisije nikakuumbua ….’nikasema na nilipoona haondiki, nikainuka kutaka kuondoka, na yeye akanifuata na kujaribu kunishika , niligeuka na kumwangalia kwa jicho baya, hadi yeye mwenyewe akarudi nyuma.

‘Nisamehe mwanadada, sitarudia tena….’aaksema huku akiwa kajishika kifuani kama vile anatubu madhambi yake.

‘Sitaki kuwa rafiki na wewe, …kuanzia leo, mimi na wewe basi, tusijuane kabisa….’nikasema na wakati huo  rafiki yake alikuwa kasimama, na kusogea pembeni kutupa nafasi ya kuongea, na mimi nikamgeukia yeye , nikamuuliza;

‘Upo tayari kuwa na mimi au….?’ Nikamuuliza, na yeye akaja akiwa na mshangao machoni, bila kumwangalia rafiki yake, akanishika mkono tukaongozana hadi chumbani wanapoishi , na humo nikamkuta msichana akiwa kakaa kwenye kitanda, huku akiwa tayari kuondoka, na alipotuona tu, akainuka kwa haraka, na kutoka nje,  na huyo mwanasheria akaniambia huyo ndiye mwanamke wa huyo rafiki yake.

‘Ina maana unafahamu kuwa ni mpenzi wake wa siku nyingi?’ nikamuuliza.

‘Nafahamu….kabla wewe hujafika hapa chuoni, huyo ndiye mpenzi wake, lakini huenda alitaka kumbwaga na kukuchukua wewe….’akasema.

‘Ndio tabia zenu, eeeh,?’ nikamuuliza.

‘Sio mimi, ulishawahi kuniona nikiwa na rafiki mwanamke hapa chuon, tangu ufike ulishawahi kuniona nikiwa nimeongozana na mwanamke kama rafiki,…. hebu ulizia watu,…mimi sijawahi, kwavile sikuwa na mpango huo kwa sasa, ila wewe peke yake, umeonekana kunigusa  moyo wangu, wewe ndiye uliyenivutia na alipokuwahi rafiki yangu, nikasema basi tena, na sitaku kamwe kugombea  …….’akasema na nilimwamini hapo hapo sijui kwanini.

‘Kwahiyo ukamkubali japokuwa ulikuwa hujampenda,…?’ nikamuuliza na yeye hakujibu swali kama nilivyomuuliza, akasematu;

‘Urafiki wetu ndipo ulipoanzia hapo…..

*********

Wakili mwanadada alifika kwa mjumbe akiwa na azima ya kumuliza mjumbe baadhi ya maswali ambayo alitaka kuwa na uhakika nayo, hakumuelezea lolote mteja wake, yaani mwanamama, alitaka hilo wazo alilo nalo kichwani lisijulikane hadi hapo atakapokuwa na uhakika nalo. Na alipofika hapo kwa mjumbe, akakuta watu wamejazana, akasimama, na kuangalia huku na kule,…akamsogelea mwanamama mmoja na kumuuliza;

‘Mbona kuna watu wengi hapa kwa mjumbe?’ akamuuliza huyo mwanamama aliyekuwa kasimama nje, maana ilionyesha wazi kuwa ndani kwa mjumbe kulikuwa kumejaa.

‘Wewe huna habari?’ akaniuliza kwa kuonyesha mshangao.

‘Habari gani hiyo?’ mwanadada akauliza.

‘Jana usiku tumeingiliwa na maaskari…hii ni mara ya pili, ila safari hii wamezidi, maana imekuwa kama uvamizi wa kijambaz. Wameingia kila nyumba baada ya nyumba, wakikuta mwanaume wanamkamata wanamfunga pingu wanaondoka naye….ndio maana unatuona wanawake watupu, hatujui ni kitu gani kimewasibu wanaume zetu na watoto wetu…’akasema.

‘Hata watoto wamekamatwa?’ mwanadada akaulizwa akionyesha kushangaa.

‘Waliokamatwa ni vijana wakubwa, sio watoto, lakini mtoto kwa mzazi wake ni mtoto au sio…’aksema.

‘Kwani tatizo ni nini mpaka wote wakamatwe, sizani polisi wangelifika na kukamata watu bila sababu maalumu?’ akauliza mwanadada na huyo mama akamwangalia huyo wakili akionyesha kukerwa, na akasema;

‘Ndio maana tumekuja hapa kwa mjumbe tujue sababu ni nini…tungelijua tatizo, tungelijua ni nini cha kufanya….kwani wewe ni nani…?’akauliza na huku akimwangalia huyo wakili mwanadada, na mwenzake akasema.

‘Humjui huyo…ndio mchumba wa yule mwanasheria….humkumbuki’akasema huyo mwanamama mwingine. Na mwanadada akauliza;

‘Sasa mjumbe yeye kasemaje?’ mwanadada akauliza.

‘Mjumbe naye hayupo, inasadikiwa kuwa huenda alipata taarifa hii mapema akakimbia kujificha, ..’akasema huyo mwanamke mwingine.

‘Sasa kwanini akimbie kujificha?’ akauliza wakili mwanadada kitabasamu kwa kushangaa.

‘Labda na yeye alihitajika kukamatwa, au alipata taarifa mapema kuwa watamkamata , au watu watakamatwa, kwahiyo yeye akatafuta kisingizio , au vinginevyo, amejificha kuogopa wananchi kuwa watakuja kumlalamikia..’akasema huyo mama.

‘Mlipomuuliza mkewe amesema nini…?’

‘Mkewe anasema mume wake alimuaga kuwa wana kikao, …toka jana, hadi leo hajarudi, kwahiyo hajui wapi alipo, na inaonyesha kabisa kuwa anafahamu wapi alipo, lakini anaficha siri ya mumewe..’akasema mama mwingine aliyetoka kwa muda huo, yeye alikuwa huko ndani.

‘Sasa nyie mna maamuzi gani?’ akawauliza.

‘Sisi tumepanga kuwa tunaandamana hadi kwa katibu kata mtendaji, naye kama hana jibu tutakwenda ofisi za wilaya….’akasema huyo mama akigeuka kuwaangalia akina mama wengine, ambao walikuwa wakitokea huko ndani, na ilionyesha dhahiri kuwa huyo ndiye msemaji wao mkuu.

‘Lakini mnafikiri ni kwanini harambee au zoezi hili, limefanyika, hivi kweli watu watakamatwa hivi hivi bila jambo, hamuoni kuwa kuna sababu…..?’ akauliza mwanadada.

‘Tungelikuwa tunalijua hilo tusingelikuwa na wasiwasi, tungefahamu ni hatua tufanye, ….sasa hivi wanatupa wakati mgumu, maana badla ya kuhangaika na majukumu yetu ya ndani na mashambani, tunahangaika kuwatafuta waume zetu, na hawa watu hawajui kuwa sisi tunawategemea waume zetu,..hiyo serikali ituambie tutakula nini, kama wamewashikilia waume zetu…watupe pesa za matumizi…’akasema huyo mwanamama msemaji wao, na wenzake wakamshangilia.

Baadaye kidogo ,mjumbe akafika, na alipoona kundi la akina mama, akajifanya kushangaa, na kuwasogelea, akauliza.

‘Jamani kuna tatizo gani?’ akauliza huku akiangalia huku na kule kama anaogopa au kama anachunguza jambo.

‘Mjumbe usijifanye hujui ni kitu gani kimetokea, …hii imekuwa ni tabia yako, pindi kukitokea jambo, unatoweka ghafla, na unakuja baadaye, na ukijifanya hujui lolote, hili la sasa litakuumbua..’akasema huyo msemaji wao mkuu.

‘Jamani mimi sijui chochote kwani hakuwaambia mke wangu, kuwa tulikuwa na vikao vya chama, tunajiandaa kwa kampeni za uchaguzi, kwahiyo jana nimeshinda huko kwenye ofisi za chama, na tumelala huko huko, sijui kabisa ni nini kimtetokea…’akasema.

‘Kama hujui kweli, haya, fuatilia ni kwanini wanaume zetu wamekamatwa usiku, bila taarifa yoyote, na hatujui wamepelekwa wapi..sisi hapa hatujala, hatuna pesa za matumizi.....mimi hapa naumwa nina presha, ’akasema mama mmoja mnene na wenzake wakawa kama wanamliwaza.

‘Sasa mimi nifuatilie wapi, nyie ndio mliokuwepo wakati wanakamatwa, kwanini msiwaulize hao polisi, kisa cha kutuvamia usiku na kuwakamata waume zetu ni nini, tumekuwa majambazi, kwanini hatuna amani kwenye kijiji chetu…’akasema huyo msemaji wao mkuu.

‘Ina maana hawakusema lolote…?’ akauliza huku akionyesha mshangao, na kutaka kujua zaidi.

‘Hawakuta kusema lolote, walifika na marungu na pingu mikononi na silaha, kila nyumba ilipitiwa na akikutwa mwanaume, au kijana wa kiume wote walisombwa kwenye karandinga..’akasema mama mmoja.

‘Kama ni hivyo watakuwa wamewapeleka kituo cha polisi cha mjini, labda ni kuhusiana na hiyo kesi inayoendeshwa kwa sasa, na huenda wanajaribu kupata maelezo, …na kama ni hivyo , haitachukua muda wataachiwa, ni bora mkavuta subira…kwasababu kesi hiyo kesho inaanza kuskilizwa’akasema mwanadada.

‘Mbona wewe mwanadada unaongea kama vile unafahamu kwanini imetokea hivyo..’akasema huyo msemaji wao mkuu.

‘Mimi naongea hivyo kwa vile ninajua mbinu za maaskari wanapokuwa wanawatafuta wahalifu,…lakini sina uhakika wa moja kwa moja kuwa huenda ni hivyo au kuna jambo jingine..’akajitetea mwanadada.

‘Wahalifu, unaita wanaume wetu wahalifu , tuombe razi wewe binti….’akasema mama mmoja.

‘Sina maana kuwa wanaume wenu ni wahalafu, ila nasema wakiwa wanamtfauta mhalifu, wnafnaya hivyo, na mara nyingi mhalafu anakuwa pamoja na sisi….’akasema huyo mwanadada, na yule mzungumzaji mkuu akamgeukia mjumba na kusema;

‘Sasa ili kuondoa huo utata, sisi na mjumbe tunakwena mguu kwa mguu hadi kituo hicho cha polisi, hatukuachii mjumbe, maana hili sasa limekuwa ni tatizo, hatulali…hatuna raha na waume zetu,kila siku tunavamiwa na polisi kwanini?’ akawa kama anauliza msemaji mkuu.

‘Tumechokaa, twendeni…..’wakasema akina mama kwa pamoja.

‘Mimi kwakweli sina muda huo, ,maana nilikuja mara moja kuchukua baadhi ya makabrasha yangu, hamuoni kuwa nipo kazini….ninahitajika kurudi…. , ninarudi kikaoni..’akasema mjumbe akionyesha wasiwasi.

‘Mjumbe wewe ni kiongozi wetu, na kama tatizo limetoka kwenye nyumba zako,unafikiri ni nani atatuongoza, …wewe ndiye mjumbe wetu, tunaamini utatusaidia kwa hili, vinginevyo , ukiri kuwa kazi imekushinda, ili tujichukulie madaraka wenyewe, na ufanye hivyo kwa maandishi…’akasema huyo msemaji wa mkuu, na wakili mwanadada akamwangalia mjumbe ambaye alikuwa akihangaika, akitaka kupita kwenda ndani, lakini ilikuwa vigumu, na asingeliweza kuwakimbia watu kwa njia hiyo.

‘Mimi sijawaambia kazi imenishida, lakini nina majukumu ya kichama, na wakubwa wananisubiri huko kwenye kikao,….’akasema na mara simu ya mjumbe ikalia, na yeye kwa haraka akaipokea, bila hata kuangalia ni nani aliyepiga. Akasema;

‘Mnaona wakubwa wananiita wameona nina chelewa, akaiweka sikioni na kama vile kaguswa na kitu sikioni cha kumshitua akaisogeza mbali hiyo simu na baadaye akairejesha sikioni na kusema;

‘Nani mwenzangu…?’ akauliza huku akiwa na wasiwasi, kwani huenda aliyetaraji kumpigia sio yeye.

‘Unasema ni Mkuu wa kitu cha polisi, afande unasemaje..kuna nini afande, maana watu wamejaa hapa wanauliza waume zao?’ akauliza huku akiongea kwa sauti, lakini sauti yake ilimshitaki, kwani akionekaan kuwa na wasiwasi,

‘Eti nini…kwani mimi nina kosa gani, mkuu …?’ akauliza ana akasikiliza kwa muda halafu akasema kwa kigugumizi.

‘Mimi …hapana…unasema, kwanini nitafutwe..hapa mkuu, kuna makosa…sio kweli..?’ akawa kama anajitetea na hiyo sauti nyingine na yenyewe ikawa inaongea.

‘Sijakimbia mkuu , kwanini nikimbie, kabisa…..nilikuwa…..niliitwa na ndugu yangu, anaumwa..ikabidi niende kumuuguza….nikalala huko huko….’akawa anajiuma uma , akisahau kuwa alishawaambia watu kuwa alikuwa kwenye kikao.

‘Sawa afande nitakuja…’akasema na alipokata simu, akainama kuelekea ndani , na wale wanawake wakawa wanamuangalia wakita kujua ni kitu gani kimetokea.

‘Sasa mjumbe mbona unatuweka hewani, unatuacha njia panda…?’ wakamuuliza.

‘Waume zenu wameshikiliwa na polisi, ili watoe ushahidi kuhusiana na mauaji yaliyotokea hapa kijijini, kwa taarifa ya polisi , wanadai kuna kundi linaloendeleza hilo wimbi la mauaji na ubabe, na kujichukulia sheria mkononi, na wanasema mnawafahamu hawo wahalifu, lakini hamtaki kuwasema,…sasa cha ajabu huyu mkuu anadai kuwa mimi ninawafahamu hawo wahalifu,..ngona niende huko huko, nitapambana nao huko huko….’akasema akijipa moyo.

‘Mjumbe waume zetu wasipoachiwa, sisi tutasema ukweli wote,..’akasema huyo mwanamke msemaji

‘Ukweli gani tena wewe, mbona unataka kunichanganya…’akasema mjumbe akimwangalia huyo mwanamama.

‘Unaufahamu vyema huo ukweli wenyewe, ndio maana ulikumbia na kujifanya ulikuwa kwenye kikao, kama sio kweli, mbona ulipoongea na hiyo simu umewaambia polisi kuwa ulikuwa kwa ndugu yako mgonjwa, mbona hukusema kuwa ulikuwa kwenye kikao kama ulivyotudanganya sisi, inaonyesha unafahamu fika kuwa ungeliwaambia hivyo hawo polisi, wangefuatilia kuhakikisha kuwa kweli ulikuwa kwenye kikao au la…’akasema huyo msemaji wao.

‘Kwahiyo mnataka kusema nini…..?’ akauliza kumkatiza huyo msemaji mkuu, akijua kiozidi kuongea atamwanga mtama kwenye kuku wengi.

‘Kama upo na sisi, na sisi ni wanachi wako, tunakuhitajia tuongozane mguu kwa mguu hadi huko kituoni, ili tujue makosa ya waume zetu, vinginevyo, tutachukulia kkuwa umetuasi, na ukumbuke sisi ndio tuliokuchagua …sasa kama hutaki kuwa na sisi , nenda kwa hawo waliokuchagua na sisi, tutachagua mjumbe wetu mwingine….’akasema huyo mwamama msemaji wao na watu wakamshangilia.

‘Jamani jamani..hebu tulieni….naombeni hili swala niachieni mimi, mimi nitakwenda huko kituoni peke yangu, na nitawaletea ni nini kimetokea , kwani tukienda kundi la watu, tutaanzisha jambo jingine….’akasema mjumbe, na kabla hajamaliza, mara wakaonekana watu wakija muelekeo wao, na mjumbe alipowaona , akajipenyeza kwenye kundi la akina mama na kujibanza kwenye ukuta, na a,ipoona yupo kwenye sehemu ambayo wale watu wanaokuja hawamuoni, akatimua, watu akabakia kushangaa.

‘Vipi jamani mjumbe mbona anakimbia, na hawa watu wanaokuja ni akina nanii……?’ akauliza mmojawapo huku na wao wakiwa na wasiwasi.

‘Nafikiri mjumbe anafahamu kabisa ni kwanini wanaume zetu wamekamatwa na yeye ni mwanaume, ndio maana akiwaona watu tu, anahisi ni hawo maaskari wanakuja kumkamata na yeye, ndio maana katimua mbio…’akasema na akina mama wakaangua kicheko, na kicheko chao kilinyamazishwa na ujio wa hawo watu, ambao kwanza waliuliza huo mkusanyiko una maana gani.

‘Kwani nyie ni nani, maana mjitambulishe kwanza….’akauliza msemajii mkuu.

‘Sisi tunatoka kituo cha polisi ni wanausalama, tumakuja kuonana na mjumbe, je mjumbe yupo wapi?’ wakauliza

‘Mjumbe kaondoka sasa hivi, hatujui wapi alipoelekea, inaonyesha ana haraka sana…’akasema mama mmoja mwenye udugu na mjumbe.

‘Anahitajika kituo cha polisi, mwambie kama tusipomuona leo, tutamfuata kwa namna asiyoipenda yeye, …’akasema huyo jamaa na mwenzake akawa anachunguza huku na kule, na baadaye akawa kama kaona kitu, akambonyeza mwenzake kuonyeshea kule mjumbe alipokuwa kaelekea, na wote wawili wakakimbilia huko alipoelekea mjuumbe

NB: JE kulikoni..
                                                    *********

WAZO LA LEO: Unapotenda makosa, moyoni kunakuwa hakuna amani, na hutaweza kuishi kwa raha, ukiwa na wasiwasi kuwa utagundulikana kwa makosa uliyoyafanya. Jitahidi kutenda mema, pale unapotenda kosa,  jitahidi kutenda mema ili hayo mema yafute hayo makosa uliyoyatenda , kumbuka kuwa dawa ya makosa ni kutenda mema.


                                                     ********
Ni mimi: emu-three

2 comments :

Unknown said...

Mmh ngoja tusubiri, wabaya ndo haooo washaanza kukamatwa.

Anonymous said...

Hi! I just wanted to ask if you ever have any problems with hackers?
My last blog (wordpress) was hacked and I ended up losing many months of hard
work due to no data backup. Do you have any solutions to protect against hackers?


Take a look at my web page: übersetzung kostenlos google (forum.anyface.ir)