‘Usiwasikilize hawa watu, wote lao moja, …..angalia ni kitu
gani walichonifanyia mimi, waulize mke wangu yupo wapi,….walimchoma moto
wakidai eti ni mchawi,…wakachoma na nyumba yangu..’ Sauti iliyotoka nyuma ya
hawa watu, iliwafanya agande kwa muda kabla hawajageuka kuangalia ni nani huyu
anayeongea. Wengine walishagundua ni sauti ya nani, lakini kwa uhakika zaidi
iliwabidi wageuke.
‘Binti yangu nikuambie ukweli, yote haya wamesababisha na hwa watu, waliovaa
ngozi ya kondoo kumbe ni chui,…. na sasa wanakunyanyasa na mali yako, nia na lengo
lao ni kutaka kukudhulumu…’ile sauti ikaendelea.
‘Nakuonya, ole wako uingie kwenye mtego wao,ukifanya tu
wanavyotaka, ujue huna lako, nia na lengo lao ni moja, kutaka kukudhulumu, kwa
visingizio vya mila na desturi,….ni nani mgeni wa hizo mila, sio kweli kuwa
mila zetu zinawakandamiza akina mama, hata kwa kile chao walichokipata kwa
jasho lao, …sio kweli, mimi sio mgeni wa hizo mila….usiwasikilize, na
ukiwasikiliza, sio tu umepoteza jasho lako, lakini pia utakuwa umewadhulumu
wengine, kwani watu kama hawa wameshaonja asli, wataendelea kuwadhulumu wengine, tunataka hii
dhuluma ikome,…’ wale watu wakawa wanamuangalia huyo msemaji huku wakiwa
wamekodoa macho yao, kama hawaamini kumuona tena huyu mzee, na wale wasio na
simile, wakaanza kunong’ona kimiya kimiya….
‘Huyu mtu katokea wapi?’ wa kwanza kunong’ona alikuwa ni
mjumbe.
‘Mimi nilijua keshakufa…’akasema mzee mwingine.
‘Hawa ndio wanga wa hiki kijiji….hawafi haraka….’akasema
mzee mwingine.
Na wakati huo huyo mzungumzaji akawa keshawakaribia, na bila
kuwaogopa, akaja kusimama karibu nao, kama vile alikuwa miongoni wa hilo kundi
la wageni, na kuwaangalia mmoja baada ya mwingine huku akisema;
‘Ongeeni kwa sauti, tuwasikie, nyie si ndio wababe wa hapa
kijijini,….kwanini mnanong’ona nong’ona ongeeni kwa sauti kama kweli
mnajiamini, si nyie mnaiona sheria ipo juu yenu mnafanya mnavyotaka, sasa
yamewafika shingoni…au sio, mumejikunyata kama paka aliyelowana, hata aibu
hamna…sasa, mnaanza kupita majumbani na kurubuni watu, haya niambieni ni kitu gani mlichomfanya huyu binti yangu,
na sasa mnakuja kuomba msamaha kwake?’ akauliza.
‘Hayakuhusu haya mzee mwenzangu, tunaomba usiingilie haya
mambo, ni mambo yanayohitaji hekima, na tusipofanya hivi, kijiji hiki
kitaharibika , ….’akasema mjumbe.
‘Mimi sio mzee mwenzako..futa hiyo kauli, kama ningelikuwa
mzee mwenzako, siku ile ulipoamrisha vijana wako wanipiga hadi kutaka kuniua,
ungenihurumia ukifahamu kuwa mimi ni mzee, lakini hukujali, lengo lako lilikuwa
nipigwe hadi nife, ili haya yanayotokea, yaweze kufanikiwa….hujafanikiwa,..nakuambai
ukweli hujafanikiwa, na hutafanikiwa…usitamke tena hilo neno eti mzee mwenzangu….
hawo ulio nao ndio wazee wenzako, na kundi lenu la muaji’akasema baba yangu
huyo wa kufikia na watu wakaguna.
Kuna kundi la watu wasiotaka kisiwapite, walishaanza
kujitokeza na kuskiliza ni nini kulikoni.
‘Chunga mdomo wako mzee mwenzetu, kauli yako
itakuponza,….’akasema mzee mwingine.
‘Sijali lolote kwa sasa, mumebakiza nini kwangu, kama
mnataka kunimalizia haya waiteni hawo
vijana wenu waje wanimalizie, maana nina uhakika, nyie hakuna mweney ubavu wa
kupambana na mimi, kama yupo ajitokeze,…msione nachechemea nah ii fimbo
mkafikiria mumeshanimaliza,…bado….kama mnabisha, njooni mnimalizie,..nyie si ndio mnajifanya wababe
wa hiki kijiji, njooni sasa mnimalizie, ….na msipofanya hivyo, nitahakikisha
kundi lenu lote linawajibika kisheria,….’akasema baba huyo wa kufikia.
‘Mzee mwenzetu, tunashukuru umefika tulikuwa mbioni kuja
kwako, nia na lengo letu ni kuweka maafikiano na matengamano ya hiki kijiji,nafahamu
mengi yametokea na wengi wameumia , lakini ifike sehemu tuseme basi, imetosha,…..mimi
kama kiongozi wa hiki kijiji, nimegundua kuwa kuna dalili za kinyongo, uadui na
fitina katika kijiji chetu, sasa hiyo sio dalili nzuri, …tukae tuongee,
tuyamalize kihekima kama wazee, tuonyeshe mfano’akasema mjumbe.
‘Hayo ndio maneno yako ya kinafiki…na yanajitokeza pale
mabwana zako wanapojikuta hawana njia nyingine….mimi hunadanganyi kwa maneno yak
o hayo, ….utawajibika na utaumbuka kiukweli…’akasema huyo mzee, na wote
wakageuka kumwangalia huyo mzee kwa kauli yake hiyo, maana wote wanamuheshimu sana
huyo kiongozi wa kijiji, na kusikia shutuma kama hizo zikielekezwa juju yake,
wakahisi kuna jambo nzito sana, na wengine wakakimbia kuwaita watu wengine, na
kundi likazidi kuongezeka.
‘Mjumbe leo kapatikana…’mmoja akawa ananong’ona kwa
mwenzake.
‘Mwache apashwe, anafikiria wote ni watu wakudanganywa kwa
maneno yake ya kisiasa, ….mimi simuoni huruma…’akasema mama mmoja.
‘Lakini kwani kafanya nini…?’ akauliza baba mmoja.
‘Sikiliza hayo maneno ya huyo mzee, unakumbuka walichomfanya
huyo mzee, wamemuua mke wake kwa kumchoma moto, na kuchoma nyumba yake, na
hawakutosheka na hilo, wakampiga mzee wa watu akimtetea huyo binti mjane….’akasema
huyo mama.
‘Kwani hiyo nyumba ni ya nani, kwasababu nijuavyo, tatizo
kubwa, ni kuwa hizo familia zinagombea urithi wa mali…baada ya mume wa huyo
binto kufariki?’ akauliza jamaa mwingine.
‘Inasemakena, hiyi nyumba ilijengwa na pesa za huyo binti,…’akasema
mama mmoja.
‘Nyie,…hiyo sio kweli, huyo binti alipata wapi pesa za
kujenga nyumba kubwa kama hiyo….’akasema baba mwingine.
‘Alipata pesa baada ya kushinda ile michezo inayochezeshwa
na makapuni ya simu…’akasema dada mmoja.
‘Hivi kweli mnayaamini hayo…wale ni wajanja tu, hawawezi
kutoa pesa nyingi kwa watu,..wanpeana wenyewe kwa wenyewe…uliwahi kusikia mtu
mwingine wa hapa kijijini kashinda,…hamna kitu kama hicho, akishindi labda awe
na udugu na hawo wafanyakazi wa kampuni hizo, ili baadaye wagawane..huo ni
uwongo….’akasema jamaa mmoja.
‘Ili uhakikishe kuwa sio uwongo, ..huyo binti alishinda, na
ushahidi umeshaonyeshwa mahakamani, sasa hivi imebakia kutoa hukumu, lakini ujuavyo,
mnyinge hana haki, tarehe zinaanza kupigwa, ili hata huo ushahidi uyeyuke….’akasema
mama mmoja.
‘Hizo ni hisia zako, kama ushahidi umeshafikishwa
mahakamani, hakuna ujanaj hapo, ..hata wapige tarehe vipi, jamii,
imeshathibitisha hilo, haki ya huyo mwanamke haitapotea, na sisi wanawake, tupo
nyuma yake, ikitokea kubatilishwa…wakaharibu huo ushahidi, tutaandamana…’akasema
mwanamke mmoja.
‘Hayo unaongea tu, …siku ikifika utakuwa umejificha chumbani
kwako, kama hukuwepo, nyie ndio waoga wakutupwa, mangapi mnafanyiwa, lakini
hamlalamiki, japo tu kulalamika…usitudanganye hapo….’akasema jamaa mmoja.
‘Hebu tulieni tusikie nini mjumbe anapashwa…’akasema jamaa
mmoja akitaka kusikia ni nini kimetokea.
********
‘Mimi nimekuwa mnafiki mzee mwenzangu…?’ mjumbe akawa
anamuuliza huyo mzee aliyekuwa akiongea kwa sauti kama anahutubia jamii, na
alijitahidi kuongea kwa sauti ya chini ili watu wasisikie. Mzee huyu alikuwa
anafahamu jinsi gani ya kuongea na watu kutegemeana na hali ilivyo, na ndio
maana wakamchagua kiongozi wa kijiji, lakini sasa …
‘Ndio wewe ni mnafiki mkubwa,..wewe ni ndumila kuwili, …ukifika
kwa hawo unaowaona ni matajiri, unasema hivi, ukija kwetu, unatudanganya hivi….mimi
wewe nimeshakufahamu fika,…hasa siku ile
ulipokuja hapa na vijana wako na kuwaamrisha wanipiga karibu ya kuniua, imefuatilia
mambo yako, na hatimaye nimekugundua, wewe ni mnafiki,….mnzandiki mkubwa,
muongozaji wa kundi la wauawaji, na nitahakikisha unakwenda jela…’akasema huyo
mzee, na wale wazee wengine aliongozana naye wakainamisha vichwa vya chini kama
vile wanaona aibu.
‘Hapa hapakaliki mjumbe, fanya jambo, tuondoke, vinginevyo,
watu watajazana hapa na mwishowe ataropoka mengi na utashindwa la
kufanya….’akasema mzee mmoja.
‘Tunakushukuru mzee mwenzetu, lakini tunakuomba utupishe
kwani tuna maongezi na huyu binti, kwa ajili ya usalama wa hiki
kijiji….’akasema mjumbe akimsogelea huyo mzee, na huyo mzee, akamnyoshea fimbo
kuwa asimkaribie.
‘Naomba usinikaribie, hasira nilizo nazo juu yako,
hazipimiki…kwanza siondoki hapa, mpaka nyie muondoke, mtambue kuwa mimi ni mzazi
wake, aliyenitambua hivyo,…na kwa vile
ninajau ni nini lengo lenu, la kutaka kumrubu huyu binti , sitaondoka kamwe, …nyie
hamna jipa, nia yenu ni kumshawishi, huyu binti ili afute kesi, hilo la kwanza,
lakini kubwa lao, ni kuwa mnataka akamtete huyo mnayemuita jemedari wenu,
wakudhulumu hata mali ya mayatima….’akasema huku akitembea kuelekea pale
aliposimama huyo binti.
‘Huyu binti, hatafanya hivyo kamwe, na kifanya hivyo, basi
mimi sio baba yake tena….’akasema huyo mzee, na wale wazee wakageuka wakiangaliana na mmoja akamwambia mjumbe.
‘Tuondokeni….hapa, hapa hapakaliki tena, hatutaweza kuongea
lolote …..’wakasema na kweli wakaanza kuondoka,na baadhi ya watu wakaanza
kuzomea.
Walipoondoka akabakia
yule mwanasheria akiwa kainama hakutaka kusema neno, akatulia hadi pale mzee
aliposema.
‘Na wewe unasubiri nini?’ akauliza huyo mzee
‘Mimi nimekuja kwa mengine….’akasema akisita.
‘Hamna linguine hapa, wewe ndiye uliyekutana na hawo wazee
mkapanga mje kumbembeleza huyu binti, ili akaseme mahakamani kuwa kaka yako
hakufanya hilo aliloshitakiwa nalo,….kweli wewe unataka kupindisha sheri, eti,
ni kweli huyo binti hakutaka kunyongwa na huyo kaka yako..?’ akawa kama
anauliza.
‘Karibuni ndani, nashkuru baba, umefika na kuniokoa maana
nilishaingiwa na wasiwasi sikujua kabisa nitakuja kusema nini, maana sikuwa
nimetambua huo ujio wao na lengo lao, naombe tusiongelee hapa nje, maana watu
wanatuskiliza, na wengine hawana nie njema…..’nikasema kukatisha malumbano
mengine kati yam zee na huyo mwanasheria.
‘Sawa, lakini huyu mtu aondoke…mimi sijamuamini kamwe…kama
anashindwa kukutetea wewe na mali yako, halafu anajfanay kuwa yeye ndiye
aliyeachiwa kukurithi wewe…kweli ni mtu huyu..’akasema akimnyoshea huyo
mwanasheria fimbo,na huyo mwanasheria akarudi nyuma kuikwepa hiyo fimbo.
‘Mzee samahani huko unakwenda mbali…’akasema huyo
mwanasheria.
‘Haya sema ni kitu gani kimekuleta hapa,?’ akauliza huyo
mzee
‘Nilikuwa na mazungumzo na shemeji…’akasema.
‘Unalotaka kuzungumza, zungumza mbele yangu, kwani unataka
kumuoa, unataka kumtongoza, au ni maswala haya haya ya huyo kaka yako?’
akauliza huyo mzee.
‘Ni maswala hayo hayo ya kaka mzee wangu…’akasema huyo
mwanasheria kwa unyenyekevu.
‘Kama ni hayo, ongea tuone jinsi gani tutakusaidia, sina
neno na wewe kijana, usiogope, hapa ilibidi nipandishe hasira maana nina usongo
na hawa watu,…na wewe kama utakuwa upande wao, ujue, umepotea…na sijui kwanini
familia yenu imebadilika kiasi hicho,…kaka yako yupo pabaya, ….’akasema huyo
mzee.
‘Lakini mzee….’akataka kujitetea huyo mwanasheria, na huyo
mzee, akawa kama hakusikia huko kujitetea akaendelea kuongea;
‘Hawa watu nawafutilia kila hatua, na kikao chao cha kuja
hapo kilifanyika mapema kabla hata ya
huyu kijana hajakwenda kuonana na hawo wazee, walikuwa na ajenda moja, ya
kutaka kuhakikisha wanaiharibu hiyo kesi yako…’akasema akimwangalia binti, na
baadaye aakmgeukia huyo mwanasheria na kusema;
‘Na pia kujaribu kujifanya wanamtetea huyo kaka yako…na
hivyo vikao vilifanyika kwanza kwa uficho na abadaye kikao cha mwisho ambayo na
wewe ulikuwepo kilifanyika kwa mjumbe, yote hayo mimi nayafahamu….wewe
ulipofika kuwapa hiyo taarifa ya kukamatwa kwa kaka yako, wenzako walishajua na
walikuwa kwenye mikakati ya kwenda kumtetea, ha hata kumuwekea dhamana…’akasema
huyo mzee.
‘Sasa mzee, utatusaidiaje maana yote haya ni hasira za kaka,
hataki kutuliza hasira zake…sizani kama ni mbaya kiasi hicho, cha kuhusika
kwenye mauaji yaliyowahi kutokea haap kijijini.’akasema mwanasheria.
‘Kaka yako ana hasira na kuburi, kama huheshimu wazee wa
wenzako, ukaona wewe ndiwe mwenye mamlaka kwenye familia na unataka mamlka hayo
yavuke mpaka hadi kwa familai za wenzako, unafikiria mwisho wake utakuwaje…hebu
niambie wewe uliyesomea sheria, ni mamlka gani aliyopewa kaka yako, ya
kuingilia familia za wenzake?’ akaulizwa na kabla hajajibiwa huyo mzee
akaendelea kuongea’
‘Ufahamu kijana, kila familia, kila jamii ina utaratibu
wake, huwezi ukalazimisha utaratibu wa familia fulani ukawa sawa na familia
yako eti kwasabbau wewe ni kiongozi wa familia yako, kama wewe ni kiongozi wa
famila yako na mna utaratibu wenu, basi heshimuni na taratibu za familia
nyingine…ni muhimu sana hilo, muwe makini sana, msijifanye kuwa eti nyie mna
taraibu nzuri, mna kiongozi, mpo pamoja, na mnaonyesha mfano, kwahiyo kila family
hapa iwe ianwasikiliza nyie….mnakosea.’akasema mzee.
‘Mimi nakubaliana na wewe mzee, lakini tukumbuke kuwa
mawazo, akili, na utashi wa maamuzi unatofautiana kati ya mtu na mtu, wengine
wameshajijengea hali fulani kuwa wao wakati
wote wapo sahihi, na kwa vile ni viongozi wa jamii zao, na wanajua kuwa
wamepewa mamlaka na jamii hizo, wanafanya kila wawezavyo kulinda kile
walichokabidhiwa….kwao masilahi ya familia zao wanayaweka mbele kuliko kitu
chochote….’akasema.
‘Mimi sikukatilii kijana….ni sahihi kwa mtizamo huo, lakini
kama kweli wanavyofanya ni sahihi na kwa
haki , kama ni sahihi na haki, isingelikuwa ni neno,hakuna ambaye
angeliwanyoshea vidole, lakini sivyo hivyo, wenzenu wana ajenda ya siri…..ndio
maana nikamuita mjumbe wetu ni mnafiki, maana yeye kama mjumbe ana takiwa
kufuata sheria, lakini sheria kwake ina sura mbili, wakikosa wakubwa, au watu
wake, hawo watatafutiwa sababu za kusamehewa,…utasikia lugha kama bahati
mbaya,…kakosea tu…. Tuongee, tuitishe vikao, kamati zitaundwa eti kufuatilia,…ujanja
ujanja tu….
'Lakini wakikosa wanyonge watu wa upande wa kushoto kwao, wanasakamwa
na kwanza wanachokifanya wao ni kuwaita hawo wanyonge majina mbaya, walalahoi,
waongo, wafitinashaji, wachochezi,…siasa kali,…sijui nini kali….ilimradi
waonekane hawo wanyonge ni wabaya…tufika kweli kwa utaratibu huo…?’
‘Lakini mzee, kukosea kupo, na kusameheana kupo, tukiishi
kwa kuadhibiana kwa kila kosa, huoni mwisho wa siku watu wote watakuwa na
majeraha kwenye mioyo yao, na kinyongo kitakuwa hakiondoki kwa vile kila mmoja
atataka mawnezake afanyiwe hivyo hivyo….
‘Mzee mimi ninafikiri, wakati mwingine inabidi tufika mahali
tusema sasa basi tukae tuongee tuelewane, na tusameheane, na wale waliokosewa,
wataangaliwa jinsi gani ya kutibiwa majeraha yao….mimi mwenyewe imeniuma sana
kusikia hayo uliyofanyiwa, sikujua kuwa ilifikia hatua hii, hayo nilifichwa
kabisa,…mimi kama mwanasheria wa familia nisingelikubaliana na hilo…na jingine
ni kuwa kama kuna wakosaji, watawajibika kinamna ambayo itakubalika, bila na
wao kuumizwa zaidi,…’akasema mwanasheria.
‘Tatizo lako unaongea hivyo kwa vile unamtetea kaka yako,
kama angalikuwa ni mtu mwingine, nina uhakika ungelisema sheria kali itumike
dhidi yake, ili iwe fundisho kwa wengine ni kweli si kweli…, si ndivyo
mnavyopenda kusema mkiwa mahakamani, sasa wakati umefika hawo watu waliokosa na
kusababisha kijiji hiki kiwe hakikaliki kwa amani, waadhibiwe ili iwe fundisho
kwa wengine….’akasema mzee.
‘Sio hivyo mzee….nazungumza hivyo kwa vile namfahamu vyema kaka
yangu. Kaka ni mtu mwema sana, na kinachomponza ni kuwa yeye kama kiongozi,
anataka kila lililosemwa au kuwepo kwenye mila, lifuatwe kama lilivyo, na
atajitahidi kuhakikisha kila mwanafamilia analindiwa haki zake kwa taratibu za
kimila na desturi,…, na bila kujali kuwa ndani ya jamii kuna wanaojificha wenye
maovu, …’akasema mwanasheria huku akiwa kainama chini.
‘Mzee, ninafahamu kuwa kuna …kwa mfano hawa kina mama
walioolewa ndani ya familia, wenye haki zao,…ambazo wamekuja nazo , ni kweli
kuna wengine walijaliwa wakaja na mali zao, hizo huwezi kuzilamisha kuwa ni
mali ya familia yote, labda mwenyewe apende kuwa hivyo….na vitu kama hivyo,…lakini
bay zaidi kaka yupo tayari kuwabeba hata
wakosaji ndani ya familia, kwa vile ni mwenzetu,….mwisho wa siku yeye ndio anaonekana
kuwa ni kiongozi wa wahalifu….’akasema.
‘Kijana, sikiliza, hayo unayoongea mimi nayaelewa sana,…na mimi
ninamfahamu sana kaka yako kuliko unavyomfahamu wewe…kaka yako, kinachomuharibu
ni kuwa kajiunga na kundi hilo la watu wanajifanya wao ni mashuhuri wa hiki
kijiji, waheshimiwa, mabwana wakubwa….’akatulia kuonyesha uchungu .
‘Kijana mimi nimeapa kuwa nitakula nao sahani moja, wakitaka
kuniua waniue, sijali tena. Kundi hilo, ndilo limewaua wazee,…wewe sijui kama
unafahamu hilo, ila hilo limetokea hapa kijijini na limetia doa kubwa sana hapa
kwetu, wazee wasio na hatia wameuliwa, kwa shutuma, imani za kinafiki, eti
wazee hawo ni wachawi,….hivi kuwa mzee ni kosa, watu wameshahu kabisa kuwa
isingelikwua ni hawo wazee wao wasingelikuwepo hapa….
'Jamani vijana , mnataka nini, ....mnasahau kabisa mlipotoka, au niambieni mnataka dunia hii
iende wapi,…kama mnawaua wazee...kwani nyie mtaendelea kuwa vijana milele,kesho na kesho kutwa utelekea huko huko....hiyo ni laana, ndio maana baraza zinapotea hakuna neema tena….kwa mtindo huo nawaambia kamwe hamtafanikiwa… sijui kama wewe hilo umejaribu kulifuatilia, au la…kama bado utambue
hilo…lipo na kuna watu wanakinyongo na hilo…msipolitatua hilo, bado kuna kisasi
moyoni…’akasema huku akijinyosha mgongo.
‘Angalia walivyonifanya mimi, karibu waniue, kisa kwa vile
natetea haki za huyu binti, na kama isingelikuwa huyu binti kunisaidia
matibabu, na kuniwekea walinzi kule hospitalini sasa hivi mngelikuwa mananiita
marehemu…nap engine kunivika makosa kuwa mimi ni mmoja wa wachawi wa kijiji,
kama walivyomvika mke wangu makosa ambayo hana…hana kabisa, mungu mwenyewe
ndiye anajua.’akatulia kidogo huku akikunja uso kwa huzuni.
‘Mzee….nakuomba unisikilize kidogo..’akasema huyo
mwanasheria, lakini mzee hakumsikiliza akaendelea kuongea.
‘Katika hilo kundi kuna wazee wanajiona kuwa wao ni watu wa
mila na desturi, wanafahamu mila zote na wanataka zifuatwe, …wapo wazee
wanajiita wao ni watabiri, waanjimui,..sijui watu gani, nashindwa hata kutaja
majina yao…eti wao wanawafahamu wachawi, …kwahiyo atakayebainika kuwa ana
dalili hizo, anatungiwa uwongo, hadi anauwawa…’akatulia.
‘Je ni nani kweli anafahamu kuwa huyu ni mchawi, au yule sio
mchawi, ?’ akauliza.
‘Mara nyingi wanaofanya hivyo kutabiri, ni waganga wa
kienyeji…’akasema mwanasheria.
‘Sasa humo kwenye kundi lao, kuna waganga wa kienyeji
wanaotambulikana, na hawo wanalindwa hata wakikosea hawachukuliwi hatua
yoyote…mwenzao mmoja katoweka kiajabu, hajulikani wapi alipo, na huyo ndiye
alikuwa kinara wao…lakini hata hivyo, kuna watu wapo nyuma ya hilo kundi,
wafadhili wakuu wa hayo yote, wanaolinda huo uchafu, na wana majukumu ya
serikali….sasa bila sisi wananchi kusimama bega kwa bega na kulalamika, …hata kuwachukuli
hatua hatutaweza kumaliza huu uozo hapa kwenye kijiji….’akasema.
‘Sawa mzee nimekuelewa….’akasema mwanasheria huku akiangalia
saa, lakini mzee hakumpa nafasi akaendelea kuongea.
‘Yaliyotoea kwa mke wangu, nisingelipenda tena yajirudie, na
….ndio maana nimeipeleka hiyo kesi mahakamani, kama kwei ipo sheria kwa
wanyonge, basi, …..hawa watu lazima waadhibiwe.. ili iwe fundisho kwa
wengine….ndio maana nasema kama kweli huyu binti ananijali, na kujali yaliyotokea
kwa mke wangu, basi asije akarubuniwa na nyie na kundi lenu, akakubali kwenda
kumtetea ndugu yako…’akageuka kumwangalia binti yake.
‘Mzee nakuomba…taafdhali, usimkataze shemeji yangu kwa
hilo,nakuomba wanza hebu nipe nafasi niongee kidogo, maana ninawahi …kuhusu
maswala ya kaka, na tulikuwa tunataka tuondoke na shemeji..’mwanasheria akaanza
kujitetea huku akimwangalia huyo binti, kwa wakati mmoja na huku akimwangalai
huyo mzee.
‘Hilo halitawezekana, binti yangu haendi popote…….’akasema
mzee na kwenda kusimama mlangoni,
Yule mwanasheria akamwangalai shemeji yake, halafu
akamwangalia huyo mzee…
NB: Je ni hayo tu, tutaonana sehemu ijayo mungu akijalia.
WAZO LA LEO:
Maafikiano ya kweli yatafanikiwa kwanza kwa kuangalia pande zote mbili, ili
kuleta mlinganyo wa sawa sawa, ili kujaribu kutibu majeraha ya waliokosewa. Usuluhishi
wa kweli hautafanikiwa kama waliojeruhiwa na kuonewa, hawajatambulikana na
kutetewa haki zao. Tuwape wenye haki zao haki wanazostahiki kupata, ili
kutokuleta manung’uniko, na maumivu ya chini kwa chini.
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
kweli mwisho wa ubaya ni aibu, na sasa wamekaribia kujitambua wanako kwenda. nzuri sana
Jamani,jamani huyu dada asikubali kwani kasahau aliyofanyiwa EE mungu hembu muongoze huyu mja wako. Hongera sana ndugu yng kwn kila cku twapata fundisho jipya.
Post a Comment