Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, June 28, 2013

WEMA HAUOZI-26


Ghafla mlango ukafunguliwa kwa kishindo, na shemeji mkubwa akawa kasimama mlangoni na kutuangalia akiwa kakunja uso, na sisi tukawa kimiya, japokuwa kwa taratibu zetu sisi kwa vile ni wadogo, ndio tulitakiwa tuanze kumsalimia, ….na nilipoligundua hili nikafunua mdomo kuanza kutoa salamu, lakini nilikatishwa na sauti yake ikisema;….’mama aliendelea mama kunisimulia maisha yake.

‘Kwanini huyu mtoto ananikimbia?’ aliuliza shemeji mkubwa akiingia ndani, akiangalia huku na kule kama anamtafuta huyo mtoto yupo wapi, na mimi hapo kama mama roho ikaanza kunikereketa nikifkiria kuwa huenda alikuwa na lengo baya na mtoto ndio maana akakimbilia ndani.

 ‘Hatujui kwanini, sisi tumemshangaa kumuona, akiingia mbio mbio, kama anaogopa kitu…. kakimbilia chumbani kwake.’nikasema. Niliposema hivyo, akaniangalia kwa macho makali na kusema kwa ahsira;

‘Mumeshaanza kuwapandikiza watoto fitina na tabia mbaya, …mnafanya hivyo makusidi ili wanione kuwa mimi ni mbaya, ….kwanini mnafanya hivyo…hamjui kuwa hawa ni malaika, hawajui lolote, hawana dhambi,….?’akasema na kuuliza kwa ukali.

‘Hakuna aliyefanya hivyo shemeji, …nahisi ni uwoga wake tu,…huenda kuna kitu alikuwa akifanya na alipokuona akahisi utamuadhibu,….’nikasema kumtetea.

‘Haiwezekani, mtoto huyu nimeishi naye vizuri wakati tupo kwenye msiba,….na mara nyingi alikuwa akiniona ananikimbilia kunipokea, leo hii mumemjaza maneno mabaya na kuanza kuniogopa, na hata kunikimbia, …kuna kitu mumempandikizia kwenye ubongo wake si bure…haiwezekani mtoto mdogo kama huyu anajua nini….’akaniangalia kwa ukali.

‘Shemeji  sijawahi kumwambia chochote kibaya kuhusu wewe…’nikajitetea.

‘Nawambia,…na narudia kuwaambia,  ole wenu nije kugundua hilo,…na kwanini mnafanya hivyo, hebu niambieni…..mnataka ili iweje,…kwani mimi ni nani kwake, nakuuliza mimi ni nani kwa huyo mtoto?’ akauliza.

‘Wewe ni baba yake mkubwa, na ndivyo alivyosema hata wakati anaingia ndani,….’nikasema.

‘Kwahiyo ulimfundiha kuwa akiniona tu akimbilie ndani maana shetani anakuja, au sio?’ akauliza kwa ukali.

‘Hpana shemeji sijawahi kufanya hivyo, na sitaweza kumharibu mtoto wangu kwa tabia kama hizo, wewe ni baba yake, na anatakiwa kukuheshimu kama alivyokuwa akimuheshimu baba yake…’nikasema.

‘Kama alivyokuwa akimuheshimu baba yake….kauli hiyo siipendi kwani hapo unaanza kujenga utofauti, mimi ni baba yake….sio kama..hakuna ukama hapa, akiwepo yeye, nikiwepo mimi, sote ni baba zake, sio kama alivyokuwa…hii lugha vipi, mbona mna…..’akatulia na kugeuka huku na kule kama anaendelea kumtafuta mtoto.

‘Samahani shemeji…..’nikasema nikitaka kuendelea kujitetea.

‘Hebu muite aje hapa, maana sitaki kabisa tabia kama hii iendelee katika familia yetu, ukoo wetu unasifika kwa nidhamu, …mimi ni kiongozi wa familia na nataka familia yote inijue kuwa mimi sina ubaya nayo, kila ninachofanya mimi,  nafanya kwa masilahi ya ukoo na familia zetu….’akasema huku akiendelea kuangalia huku na kule.

‘Hata hilo la kufika hadi mahakamani ni kwa ajili ya kulinda maslahi ya huyu mtoto, lakini masikini mtoto huyu hajui kitu, anazidi kupotezwa na watu wasiomtakia mema….sikuwa na nia yoyote mbaya kwa hili lililotokea, lakini….sijui nifanyeje watu wanielewe….jamani mimi sio mbaya kihivyo,nafanya haya kwa ajili yake tu…kwa ajili ya vizazi vya familia hii….’akasema shemeji, na sikutaka kulumbana naye, ikabidi nimuite mtoto ambaye alifika huku akiwa kajikunyata kwa uwoga.

‘Shikam-mooo baba..mkubwa’akasalimia huku akishindwa kuficha uwoga aliokuwa nao.

‘Marahaba, …sasa ndio unakumbuka kunisalimia,…kwanini unanikimbia?’ akamuuliza akishusha sauti , sio kama alivyokuwa akiongea awali, utafikiri sio yeye yule aliyekuwa akibwatuka kwa sauti ya ukali.

‘Niliogopa tu…’akasema.

‘Unaniogopa mimi au unaogopa nini?’ akamuuliza.

‘Hapana ….si… nilikuwa nachezea uchafu…nikaogopa kuwa utanichapa…’akasema.

‘Ohoo, kumbe, sasa kwanini unachezea uchafu, ….nilikuambiaje kule nyumbani?’ akamuuliza akimshika mabegani, na matoto aliposhikwa hivyo, akashituka, kama vile kashikwa na umeme.

‘Nisichezee uchafu, nitavimba tumbo kwa minyoo….’akasema huku akiangalia upande ule alioshikwa.

‘Sasa kwanini ukachezea uchafu…na wakati unajau kuwa uchafu una wadudu wanaoleta safura, wewe huogopi wadudu wakiingia tumboni mwako?’ akamuuliza.

‘Nisamehe baba mkubwa……nawaogopa wadudu…. , lakini nikimaliza kucheza nina-nawa mikono…kwa…kwa sabuni….mama alinifundisha nikishika uchafu ninawe kwa sabuni….’akaanza kulia, akijua kuwa atachapwa.

‘Sasa kwanini unalia kwani nimekuchapa…nimekufinya?’ akamuuliza,

‘Nisamehe baba mkubwa sirudii tena….’akawa anaendelea kulia huku akijikunyata huku akiniangalia na hata kutaka kumkimbilia, lakini baba yake mkubwa akamshika mikono, na kusema;.

‘Siku nyingine nikikuona unachezea uchafu nikufanyeje…au mama ndiye anakufundisha kuchezea uchafu?’ akaulizwa.

‘Unifi-fi-nye….hapana, mama huwa ananikataza kuchezea uchafu….’akasema huku akiniangalia kwa macho yaliyojaa machozi.

‘Haya kwanza kanawe mikono, halafu hii hapa ndio zawadi yako,….’akasema huku akitoa kigari kidogo cha watoto kwenye mfuko wake wa koti,’ na mtoto akasita kukichukua, na kuniangalia, nikamuashiria akichukue, na akakipokea  huku akitabasamu.

‘Haya chukua zawadi yako hii, kachezee, hizi ndio zawadi za kuchezea, usichezee uchafu, unanisikia eeh, mtoto mnzuri, mimi ni nani….’akasema.

‘Wewe ni baba mkubwa….’akasema akitabasamu na ila hali ya kuogopa ikawa imemuondoka na akawa akikishika shika kile kigari kwa furaja, na baadaye akakumbuka na kitu, akamsogelea baba yake mkubwa akafanya kama anapiga magoti na kusema;

‘Ahsante baba mkubwa….’akasema huku akiwa kainamisha kichwa chini kwa adabu.

‘Ahsante na wewe….eeh, haya nenda kachezee kigari chako,….’akasema shemeji, na yule mtoto akaanza kukichezea, na mimi nikamshukuru shemeji ambaye alikuwa akimwangalia mtoto na kile kigari, sijui alikuwa akiwaza nini, na baadaye akasema;

‘Mtoto huyu anafanana sana na baba yake, nikimwangalia nahisi namuangalia ndugu yangu, lakini ndio hivyo tena , mungu keshamchukua kiumbe wake, yeye kampenda zaidi yetu…’akatulia huku akionyesha uso wa huzuni, akatulia kidogo, na baaadaye akageuka kuangalia pembeni, na kusema;

‘ Tatizo ni kuwa watu hawataki kunielewa,hali nalirudia tena, labda ipo siku mtanielewa, lakini sijui lini, labda siku tatizo litokee kwa sababu ya kupinga mawazo yangu, hapo mtanikumbuka, labda siku nikiondoka duniani,…sijui….’akawa anaongea kwa sauti ya upole, halafu ghafla akapandisha sauti na kusema;

‘Mimi nahangaika kuzipigania mali zake….’akawa anaonyesha kidole ule mtoto alipoelekea

‘Lakini watu wananiona mimi ni mbaya, ….sasa mali hizi zikichukuliwa na wanaume wengine, unafikiri huyu mtoto atapata nini…kwanini hamtaki kunielewa, eti ndugu yangu, hebu nisaidie ….’akasema huku akimwangalia mdogo wake huku kaelekeza kiganya cha mkono juu.

‘Mhhh….’ndugu yake akaguna bila kusema kitu, na hapo ikabidi niingilie kati na kusema;

‘Lakini shemeji unaposema kuwa hizi mali zitachukuliwa na mwanaume, una maana gani?’ nikauliza lakini sikuwa na nia ya kupata jibu.Yeye akawa ananiangalia kwa uso wa kushangaa, na nilipoona hivyo, nikaamua kufafanua usemi wangu na kusema;

‘Shemji mimi simjui mwanaume gani wa kuja kuzichukua hizi mali, maana ni mali zangu, …kama ni mali zangu kwanini mwanaume aje azichukue…?’ nikaendelea kuongea kama vile nauliza na shemeji hakunijibu akawa bado ananiangalia na uso wa kushangaa, na baadaye akageuka kumwangalia ndugu yake, sijui alitaka yeye ajibu hilo swali au alikuwa na maana gani, na hapo nikaona nisinyamaze nikaendelea kujitetea, nikisema;

‘Mimi ni mama wa huyu mtoto…nina uchungu naye sana,…., ina maana mimi sina imani na huruma na huyu mtoto, mpaka nikubali mali hizi zichukuliwe na mwanaume mwingine, …na sijui huyo mwanaume ni nani, au kwa vile nilikubali marehemu aziandikishe hizi mali kwa jina lake , ndio mnafikiria kuwa nitafanya hivyo kwa kila mwanaume. …’nikasema huku nikikunja uso kwa huzuni.

‘Jamani, hata hivyo sitarajii kuolewa na mwanaume yoyote kama ndio mawazo yak ohayo shemeji…kamwe sitaolewa tena, nimeamua maisha yangu kujiendeleza mwenyewe….sitaolewa tena,…hususani kurithiwa  na yoyote kati yenu..’na nilipotamka maneno haya, akaniangalia  kwa kugeuza kichwa haraka, …na yeye akasema .

‘Unaona…kiburi…mimi nilikuwa naongea, sijakuruhusu kuongea umeshaanza kuongea, tena kwa kujiamini kabisa….’akatikisa kichwa na kumwangalia ndugu yake, kama vile anaomba msaada wa hilo alilolisema.

‘Hii ni tabia ya ajbu kabisa, unafikiri kwa vile upo huru,…ndugu yangu kaondoka, wewe sasa ni kidume, au…’ akawa kama anaiuliza .

‘Kwa vile ….eeeh,  ‘ akawa anajitingisha tingisha, na akiangalia pembeni, na kuendelea kusema.

‘Sasa unaweza kuongea utakavyo, ndivyo ulivyofunzwa hivyo, …ndio heshima hiyo kuwa ukiwa na wanaume, unaruka juu, na kusema utakavyo,…’ akatulia na kuniangalia halafu hata kabla sijajitetea akasema;

‘Kumbuka mila na desturi zetu zipo wakati wowote…ukumbuke bado wewe ni mke wa familia yetu.na kama ni hivyo, adabu, na mila zetu unastahiki kuzifuata, na kama hutaki hilo, basi, subiri wakati muafaka utafika, utakwenda huko utakapo…ukafanye hayo utakayo,na upendavyo,lakini sio hapa, na ikifikia muda huo ukaamua kuondoka….mali za huyu mtoto zitabakia mikononi mwake…..zinabakia hapa hapa, kwani zipo kwenye aridhi ya ukoo wetu….’akasema.

‘Samahani shemeji, …sikuwa na nia mbaya, nilikuwa tu nakufahamisha nia na lengo langu…’nikasema.

‘Sawa kabisa, nimelielewa lengo lako ndio maana nikakubali hadi kufika huko mahakamani, kuonyesha msimamo wa familia na ukoo wetu,…na usifikirie kuwa mimi ni sawa na hawo wanaume wengine wanaodanganyika kirahisi…..mimi…nimelelewa na kuiva kimila na desturi zetu, na wananifahamu wazazi wangu, ndio maana waliponipa hilo jukumu, hawakuna na shaka na mimi…’akasema akionyesha tambo.

‘Lakini ndio hivyo, utasemaje kwenye hii dunia ya sasa, wanawake siku hizi wanaota mapemba, eti wanadai haki, na angalia hiyo haki wanayoidai ni haki gani,….haki ya kukiuka mila na desturi zetu, haki ya kutembea uchi, ….nusu uchi….jamani, ndio haki mnayoitaka hiyo,….ole wenu, maana dunia hii ikiharibika, mtakuja kubeba lawama kubwa sana,….mnadai haki , haki ya kuwapuuza wanaume zenu...

'Yaani nyie, mnaona hayo waliyobuni wazee wetu ni mabaya, nyie sasa mna hekima zaidi yao….hata siku moja, hamtaweza kuwazidi wazee wetu kwa hekima, wao walikuwa wakiona mbali, wakiona nini kitatokea kama ikifanyiak kinyume chake, na walitaka hivyo kwa maslahi ya ukoo, na familia, sio kwa maslahi binafsi….eti nyie sasa mumesoma, ….manshika pesa, mnashika madaraka,…mnaanza kuvimba kichwa….’akacheka kwa kebehi halafu akasema.

‘Mimi siwakatazi kudai haki zenu, daini….hata mkitaka kutembea bila hati chupi mitaani, tembeeni…lakini,…. lakini angalieni ni haki gani za msingi mnazostahili kuzidai, angalieni mbali, niliwaelezea kwenye kikao, na hata baba …yule mzee wetu aliyebakia wa siku nyingi, alielezea …kwanini tunafikia kufanya hivyo…wao waliona mbali…..’akasema na akawa kama anawaza jambo, na kwa sauti ndogo ya unyenyekevu akasema;

‘Sasa aah, jamani, nawaombeni, nyie mliokulia hapa kijijini,…mkabahatika kuishi na wazee wetu hawa, mkapata amadili yao,…. jaribuni kuwa mfano,lindeni heshima  na mila zenu, ili vizazi vyetu vije kujifunza, kuna maadili na baraka zake, nyie hamuwezi kuziona lakini matokea yake mnayaona….’akatulia na kuangalia huku na kule.

‘Hebu sasa hivi angalia, mzazi anafariki, mali zinachukuliwa kama hivi, baadaye anatokea kidume mshawishi, anakuja, anazimilik hizi mali, watoto, wanatelekezwa, yule kidume, akajali damu aliyoizaa yeye, wenye haki wanaweza hata kufukuzwa…hilo jamani hamlioni’akawa kama anauliza.

‘Haya hata kama hilo hamlioni, angalieni mayatima siku hizi ni nani anawajali…hakuna, kwa vile hawajulikani tena, kwa vile mila na desturi zetu zimepuuzwa, kuwa mtoto ni mtoto wa kila mtu, mtoto kwenye familia , ukoo, jamii, ni mtoto wa kila mtu, hata kama mzazi wake kaondoka, bado aisikose matunzo, maana baab zake tupo…jamani kwanini hamtaki kunielewa…..’akashika kichwa.

‘Niwaambieni, ….ni siri hii nawatobolea, angalieni familia ya huyo mwenzetu hapo jirani, yeye kajifanya msomi, haya, binti yao mkubwa kaolewa, na mara mumewe akafariki, …mali ile akarisishwa huyo binti, maana wao ni wazungu, na yule binti kaolewa na mume mwingine….yule mwanaume, akawa mjanja kaja na mambo yake, ila mali akaiandikisha kwa jina lake….ooh, mungu hana hiyana, akamchukua na huyo binti,…..’akatulia.

‘Mali ile sasa ni ya mwanaume,….yeye akasema anauza mali yake, na anakwenda kuishi kwao…’akatulia.

‘Hebu fikirieni, huyu mwanaume anauza hiyo mali ya kizazi cha ukoo, ambao alikuja akaukuta, je ukoo huo unakua, utakuta nini tena….hilo hamlioni, …kwanini akili zenu zinadumazwa na mila za wageni wenye ubinfsi..sisi ni wajima, kuwa mali za familia ukoo, zinabakia kama za jamii hiyo, kizazi hadi kizazi…..hata shule hiyo ndogo hamuielewi, jamani…’akjikuna kichwa kama anawashwa.

‘Aaah, naona, sitaeleweka hapa,…hayo tuyaache, …’akasema na kumgeukia ndugu yake.

********
Mwanangu, siku hiyo ilikuwa siku ya aina yake, huenda ndio siku mungu alitaka kubainisha ukweli wake, kwani kichwani moyoni, nilikuwa nimejawa na mawimbi , mawimbi ya kutaka kuongea na kumuelezea vila ninavyojisikia huyu shemeji yangu mkubwa, lakini alikuwa hataki kunipa nafasi, na baadaye alipomgeukia ndugu yake, nikaona sitaweza kupata nafasi hiyo, nikatulia….’akaendelea kuhadithia mama

‘Na wewe msomi,….wasomi, wa siku hizi bwana, ….aah, ngoja nisiseme mengi, …Hebu niambie kwanini umeondoka bila kuniaga, …?’ akamuuliza mdogo wake akitabasamu kwa dharau.Ndugu yake naye akatabasamu na kusema;

‘Bro, mimi nilikuona umepumzika, …na kwa vile ulitoka kwenye kazi na mawazo ya kesi yakawa na mimi yananichanganya, basi nikaona nikuache upumzike, na mimi nipoteze mawazo kwa kutembea tembea….hata hivyo kaka, ingelikuwa sio adabu njema kukuamusha.’akajitetea ndugu yake.

‘Usinidanganye bwana mdogo,…mimi naona hadi ndani ya ubongo wako, ni nini unachokiwaza,… hakuna cha kuniacha kupumzika au nini, wewe uliona kuwa ukianiambia kuwa unakuja huku kwa huyu ….aah,… shemeji, ….’akageuka kuniangalia  huku akinionyeshea kwa kidole,….mimi sikumjali maana wakati ule nilikuwa namimina juisi kwenye gilasi,….na baaadaye akamwangalia ndugu yake, na kusema.

‘Ulifikiria nitakupinga usije kwake, au sio…nikuambie ukweli mimi mwenyewe nilikuwa na wazo hilo la kuja huku, mimi bwana mdogo, akili yangu inafikiria mbali kuliko mnavyofikiria nyie, …sawa hata hivyo hakijaharibika kitu, tumeshafika hapa, …na ingenilazimu kufika hapa , hata ingelikuwaje maana unafahamu fika msimamo wangu,…..haya niambie za kutangulia, mumeongea nini na huyu shemeji…?’akasema na kunigeukia mimi. Na aliponiona nimetulia nikiwaangalia, huku nimeshiak gilasi za juice, akasema’

‘Ahsante shemeji wewe weka hapa mezani, tutakunywa kwa muda wetu, sasa hivi mdomo una kazi ya kuongea , sio kunywa, au kula…..na usiondoke hapa, nina mazungumzo mazito na wewe…sio kwa vile kesi inaelekea vile ukafikiria basi umeshinda…..hapana kushinda kule, sio kushinda ndani ya ukoo huu, mimi kama kiongozi sitatetereka….’akasema .

Sikusema kitu nikawa nimetulia, na niliweka zile gilasi za juice mbele yao, na kuzifunika na vifuniko vyake, na mimi nikakaa pembeni, nikimenya machungwa, na yeye akawa ananiangalia kwa makini, mpaka nikahisi vibaya, halafu akasema;

‘Hongera shemeji, naona umakipata ulichokitaka…..kweli wewe king’ang’anizi, unataka kudai hata mali za watoto…unataka hiyo mali ukampe nani,….kama kweli una nia njema, basi olewa na ndugu yangu huyu, …ili mali iendelee kubakia kwenye familia hii kwa masilahi ya mtoto huyu, au watoto watakaokuja…’akasema.

‘Shemeji samahani, …..naomba nijitetete kwa hilo….’nikasema.

‘Ujitetee, kwani yule wakili wako yupo wapi, au leo unataka kujitete mwenyewe, haya sema, sioni ajabu, …wewe sema tu, …maana mdomo wako unawashwa kuongea, haya sema unachotaka kusema, usifikirie kuwa mimi sinawapi uhuru wa kuongea, ila ongea kwa hekima, haya ongea,….’akasema huku akinywa juice.

‘Shemeji mimi sijang’ang’ania  mali za mtu....au kudai mali ambayo sio ya kwangu,..kama ulivyoona kwenye mahakama, ile stakabadhi inaonyesha wazi kuwa nyumba hii nilijenga kwa pesa zangu, duka lile nilijenga kwa pesa zangu, ina maana kweli ningelidai kitu kisicho changu, hapana mimi sina tabia hiyo….ninakuapia shemeji, mimi sijajenga hii nyumba na duka kwa pesa za marehemu, pesa za  marehemu ziliibiwa kabla…..je ina maana mwanamke hana haki ya kudai kitu alichojenga kwa pesa yake?’ nikauliza.

‘Ina maana nyumba yote hii na duka ulijenga kwa hizoo pesa…za kamari, ..oh, sijui za bahati nasibu, samahani, ila mimi sioni tofauti yake, kamari na bahati nasibu?’ akauliza.

‘Ndio hivyo shemeji....huo ndio ukweli,kuwa nilijenga vyote hivyo kwa pesa niliyoshinda kwenye hiyo promosheni ya kampuni ya simu, na wala sio kamari….’nikasema na yeye akawa ananiangalia moja kwa moja machoni.

‘Mhh, mimi haliniingii akilini kabisa, wewe, mwanamke uwe na pesa kiasi hicho, uwe na akili ya kufanya hili, mmmh inawezekana kweli bwana mdogo, pesa yake, ajenge nyumba kwenye familia badala ya kwenda kujenga nyumbani kwao….?’ Akamgeukia ndugu yake, na mimi sikutulia nikasema.

‘Shemeji …kama unakumbuka, baada ya marehemu kutoka jela, hakuwa na chochote, na maisha yake yalikuwa kama mlivyomuona, akawa kazi yake ni kulewa, na hata hizo pesa za pombe, alikuwa akichukua kwenye duka…..huo ndio ukweli wenyewe,…na nilijua kuwa nimeolewa, na ukiolewa unakuwa mmoja wa familia hiyo, tuna mtoto…ataishije baadaye, kwahiyo nilijitahidi kujenga nyumba na duka, na pesa za duka, ndizo zilizoweza hata kumtibia marehemu mume wangu…..nilifanya hilo nikijua mimi ni mzazi….’nikasema kwa uchungu.

‘Hogera sana,….’ Akawa anapiga makofi, huku akimwangalia ndugu yake na baadaye akaniangalia mimi huku akitabasamu kwa dharau.

‘Mmm, mimi sijui niseme nini, maana sijui umerithi wapi hiyo tabia, …tabia hiyo hufanani kabisa na kabila letu, tabia ya kupenda sana mali….mwanamke kupenda sana mali sio tabia ya kabila letu, kabila letu mwanamke anampenda mumewe, na mali inakuwa miliki ya mumewe, vinaunganishwa hivyo, mke, mume mali ….mali haiwi kati, inakuwa juu, mikononi mwa mume…’akasema huku akimwangalia ndugu yake, ambaye alikuwa katulia kimiya, huku akionyeshea kwa mikono.

‘Ndugu yangu mbona upo kimiya, ..wewe si msomi, au ndio…nakuona ndugu yangu umeshalogwa wewe..hata hivyo hawatakuweza, kama nipo hai, hawatakuweza, hawataiweza familia hii…na naona sizani kama utamuweza huyu mwanamke, huyu anafaa kuishi na mimi…sio watu laini laini kama nyie…’akasema, huku akiangalia nje, na alioenekana kama anataka kuondoka, akasema;

‘Haya bwana mdogo kazi kwako, ..kwanza hebu niambia wewe umefikia wapi, maana hapa kichwa kimechanganyikiwa, hata sijui nifanyeje,najua umekubali kuachia hizi mali, ….kwa huyu mwanamke, kwasababu ya kupenda, au sio,kupenda nako bwana…..haya, sawa, kama ni hivyo…nahitaji matokea yenye faida kwa familia. …’akasema akimwangaia ndugu yake. Na ndugu yake akawa hasemi kitu, na kaka yake alipoona ndugu yake yupo kimiya akasema.

‘Kama umakubali mali iandikishwe kwa huyu mwanamke, na familia yenyewe, unataka kuiachia, hivyo hivyo, huyu mtoto naye ina maana hana chake, sio haki yake….eneo hili ni mali ya nani,…sawa hata kama nyumba imejengwa na unakubali kuwa isiwe ni ya familia, lakini nyumba imejengwa wapi, imejengwa kwenye ardhi ya ukoo wetu…..hayo ndio maswali ya kujiuliza…haya niamabie na hilo utaliwekaje?’ akauliza.

‘Una maana gani kaka kusema hivyo,…maana hawa wapo, hawatakwenda kokote,…nyumba hii ipo, hata kama hati miliko ipo kwa jina hilo la shemeji, ..bado ni mali ya familia, yeye na mtoto, .. na mimi nitakuwa nafika hapa mara kwa mara kuangalia kuwa hali zao ni njema,…zaidi ya hayo siwezi kumlazimisha…’akasema.

‘Kaka hilo tutakuja kuelewana, halina shaka, ni maswala madogo ya kuelewana….’akasema ndugu yake huyo, na kauli hiyo ilionekana kumkwaza ndugu yake, akakunja uso,

‘Maswala madogo…haya ni maswala madogo…..sikuelewi….hivi ina maana mimi naongea utumbo hapa, hata wewe ndugu yangu hutaki kunielewa,…..?’ akawa kaanza kukasirika.

‘Bro,…kwanza kuhusu hilo la kumuona shemeji, naona tulipe nmuda, hatuwezi kumlazimsha eeh,…’akasema na kabla hajamaliza ndugu yake akamkatiza na kusema.

‘Unaona…legelege kabisa,, kwani hapa unalazimisha au ndivyo taratibu zilivyo…yeye kwasasa hana hiari, …anatakiwa akubalia kauli ya marehemu, kuwa wewe ndiye mume wake…je ina maana alikuwa akibisha kauli za mumewe, …nafahamu kwa tabia aliyo nayo, sizani kama alikuwa akimtii mumewe…..sizani…maana hii inajionyesha wazi, niliwahi kumwambia ndugu yangu kuwa sasa yeye kaolewa, badala ya kuoa, sijui kama alinielewa, ….eti aliniambia nisiingilia ndoa yake….’akasema huku akinyosha mikono ya kukata tamaa.

‘Bro, kwa hilo….hatuwezi kumlazimisha shemeji,…kaka…unakumbuka mwenyewe , hata kwenye kikao kile cha familia ulisema, kuwa hilo la kurithiwa ni hiari yake...mimi nipo tayari kumuoa, lakini ni kwa hiari yake, lakini kama yupo tayari….hata hivyo kaka bado tunaongea, naomba hilouniachie mimi mwenyewe, nitajitahidi kadri ya uwezo wangu kuongea naye, maana yeye sio mtoto mdogo,….kama atakubali , ninamuhakikishia kuwa hatapa shida,….na sifanyo hilo kwa vile tunataka mali ziendelee kuwa mikononi mwetu, hapana, nafanya hivyo, kwa vile …..nimempenda….’akasema shemeji na mimi nikaona nikae kimiya mpaka wanatakaponiruhusu kuongea.

‘Sikiliza bwana mdogo, wanawake kama hawa walioonja pesa,hawawezi kamwe kukubali kwa hiari yao, hapa alipo anajiona kama dume…anajiona kuwa anaweza kuishi maisha bila kumtegemea mume, ndivyo anavyojidanganya, anafikiria bahati kama hiyo inaweza kuja tena…kama ulibahatisha mara moja, sio kila siku utabahatisha…maisha bila mume utafika mahali utakiuka maadili na kuanza kujiuza…’akasema.

‘Kaka naomba hilo uniachie….usimsononeshe, au kumtisha shemeji,….yeye ni mtu mzima ana akili ..’akasema mdogo wake na ndugu yake akawa anamwangalia kwa macho makali, ilionyesha kuwa alikuwa na hasira fulani na ilikuwa ikifukutua kwenye moyo wake.

‘Tatizo lako,..ndio hilo, hutaki kuiga yale ya msingi,…hutaki kunisikiliza, mambo mengine hayahitaji shule, ukifuatilia ya shuleni, utavurunda, ndio maana dunia inaharibika….watu hawajui ni nani mkubwa, ni nani kiongozi, kila mtu ni mkubwa, kila mtu ni kiongozi……’akasema huku akisimama.

‘Kaka sio hivyo, ila kila mtu ana hiari, na nafasii ya kujitetea, hatuwezi kulazimishana kwa kila jambo…’akasema.

‘Bwana mdogo ina maana hata kama mimi sipo utakuwa lege lege hivi hivi katika kuendeleza familia. 

Uongozi sio lele mama, kuna mahali inahitajika kuwa mkali, na kuna mahali unahitajika kuwa mpole. Kwa hili bwana mdogo, nakuhakikishia ukitaka siasa, lele mama….kama unatongoza mwali, hutafika kokote, utajikuta, ukiingia jikoni, ukiosha vyombo, huku mwanamke, kakaa kwenye kocho, kapak hina, anakuamrisha `nataka maji….’, fanya haraka nina njaaa…’ akawa analegeza sauti ya kike, na mwishoni akasema;

‘Ndivyo mnavyotaka wasomi au sio, haki sawa nusu kwa nusu,….bwana mdogo dunia hii ukiwaachia hawa watu watawale….kila kitu kitaharibika….tupo, mtakuja kuniambia,….haya mambo.bila kuwa mkali hutafanikiwa…..huyu anahitajika  kukemewa maana keshajenga dharau…kiburi, kwa vile keshaonja pesa , tena pesa nyingi….’akasema.

‘Kaka mimi  naomba tu, wewe niachie hili, usiwe na shaka, mimi niliongea na marehemu, akanielekeza jinsi gani ya kuishi na shemeji, alimfahamu tabia yake, na sijawahi kumsikia akimlalamikia kwa ubaya, kiujumla alikuwa akimsfia shemeji kuwa kati ya wanawake waliojaliwa kuwa waadilifu, yeye ni mmojawapo, sasa naona ajabu nikisia hivyo unavyosema wewe…’akasema mdogo mtu.

‘Mimi sidanganyiki bwana mdogo….nawafahamu sana hawa wanawake….nawafahamu sana wanaume kama ndugu yangu, mkiwa kijiweni, mnatamba, mimi bwana mke hanibabaishi, nitamuweza, fika nyumbani uone mambo ya aibu, ….anaosha vyombo chumbani, ili asionekane na marafiki zake…..sio mimi, ….na nikiona ndugu yangu  anafanyiwa hivyo, huyo mwanamke, nitamtoa mkuku kwenye hii familia…’akasema.

‘Nimekuelewa kaka, ….ndio maana sitaki kulichukulia hili jambo kwa pupa, ..yeye mwenyewe ni mtu mzima, kama analiona hili halina maana kwake, basi huenda ana mipango yake mingine, tumpeni nafasi,…tuone ni nini anakitarajia,…., hata hivyo, bado tunaongea,..’akasema mdogo mtu.

‘Bado unatongoza bwana mdogo eeeh, …aibu kabisa…..unatongoza kwani huyu ni mwali wa kutongozwa, wakati hali halisi inajulikana….sikia bwana mdogo, ukishindwa, niachie mimi…nitajua nini cha kufanya…na ukishindwa , mimi nitamchukua mwenyewe, hanishindi, wiki moja tu atakuwa kama hawo shemeji zako….’akasema akipiga piga kifua.

‘Kaka….’akataka kujitetea mdogo mtu, lakini kaka yake akamuonyeshea mkono wa kumtuliza, akasema;

‘Nisikilize bwana mdogo, nimechoshwa na hiyo kauli yako,…..Mimi kama bado ni kiongozi wa hii familia, nitahakikisha kila kitu kinakwenda kwa matakwa ya familia, na taratibu zetu, ikiwemo hili…la mali zote zilizopo kwenye familia,…unanisikia sana  ni marafuku kuandikishwa jina la mwanamke, kwasababu yeye ni mtu wa kuja tu, na siku yoyote anaweza kuondoka….’akasema na mimi nikaona niingilie kati na kuseema.

‘Hizo ni mali zangu nina haki nazo, sio mali za familia….japokuwa zimejengwa kwenye eneo la familia yenu, lakini ni kwa ajili yangu na mtoto wangu’nikasema.

‘Unasema nini, nani kakuambia uongee…`hiyo wangu ‘ imetoka wapi, mtoto wako huyo…funga mdomo wako na ukome kabisa….sitaki kusikia hiyo kauli,…mtoto wangu….ndivyo akili yako inavyokutuma eeh,’akasema kwa hasira .

‘Kaka…..’mdogo mtu akataka kuingilia, na hali ya hewa ikaanza kubadilika, maana jamaa aliona anapingwa kitu ambacho akukipenda, akasema kwa hasira;

‘Pili nataka huyu mwanamke akubali kuolewa na wewe…vinginevyo, sijui…..hatutaweza kuendelea kubembelezana na watu walioshindikana,… njia ni nyeupe….kama alivyokuja, anaweza kuondoka, lakini ukiondoka, kila ulichokikuta hapa, kila kilichopo hapa kitabakia hapa hapa…..hiyo ndiyo kauli yangu….’akasema huku akisimama na ikawa kama anataka kuondoka….

‘Shemeji..tafadhali…naomba na mimi mnisikilize….’nikataka kujitetea, …oooh, kumbe nimeharaibu, maana wakati anaongea alikuwa kamgeukia mdogo wake, sasa kusikia sauti yangu kwa mara nyingine, akanigeukia kwa hasira na kuniangalia kwa jicho la ukali na mwili ukawa unatetemeka, ….akawa ananiangalia  huku mishipa ya shingo imetuna.

‘Haya ndio nisiyoyataka, ….nimekukanya mara ngapi,…kiburi eeh,..wanaume wanaongea, wewe unajifanya kidomo domo….ni nani kakupa nafasi ya kuongea, kama nilitaka wewe uongee, ningekupa nafasi, hiyo tabia ya kunikatisha,….naona imezidi na nisipokufundisha adabu leo, hutanielewa, …ngoja, nikuonyeshe adabu za hii familia….’nilihisi hatari, maana sifa za huyu jamaa ni kuwa akikasirika au akizamiria kufanya jambo, huwa harudi nyuma, ni mpaka alifanye,hio jambo,….nikaona ananigeukia, na kuanza kunijia.

‘Hoooh, kaka imekuwa hayo tena…kaka..utaharibu kila kitu, elewa upo wapi….kaka tulia kaka’akasema mdogo mtu akitoa macho ya uwoga

‘Kelele wewe…ngoja nikuonyeshe jinsi gani ya kuishi na hawa watu,…’akasema akimnyoshea mdogo wake kidole, na akaanza kunijia mimi.

Pale alipokuwepo, ili anifikie ilibidi ampite ndugu wake kwanza, ….na ndugu yake alishashikwa na butwaa, na anamfahamu sana ndugu yake huyo kuwa akiwa na hasira hashikiki, ukimshika ujue atakugeukiwa wewe… ni bora wewe uliyesababisha hivyo ukimbie, vinginevyo anaweza akakujeruhi vibaya sana, hata kukuua….

Mdogo mtu alipomuona kaka yake kakasirika, na alivyomuona jinsi alivyobadilika, akajikuta akiogopa, na macho ya uwoga yakamwingia, hakujua afanye nini, akasema huku akiwa na wasiwasi.

‘Shemeji  toka nje kimbia…’akasema mdogo mtu, hata hivyo  pale nilipo nisingeliweza kutoka nje kabla hajanikamata, nikajipa moyo, na ujasiri ukaniingia kama wa paka aliyenaswa kwenye chumba kidogo.

Mkononi nilikuwa bado nimeshika kisu ambacho nilikuwa namenyea chungwa, nikasema moyoni, akanisogelea tu, hicho kisu kitakuwa silaha, na sitasita kukizamisha mwilini mwake, kama akinizuru…
Akawa keshampita ndugu yake, na sasa ananikaribia mimi, akiwa kakunja ngumi..uso umembadilika kwa ghadhabu, na mara mlango ukagongwa….

NB: Ni nini kilitokea


WAZO LA LEO:Haki ya kutoa mawazo kujietetea na kuelezea hisia ni za kila mtu hazijali ujinsia umri au hali ya mtu. Tusizarau mtu kutokana na ujinsia wake, au hali yake,huenda alilotaka kuongea, kujitetea ni la msingi na linaweza likajenga na kuleta maendeleo na upendo kwenye jamii, haki sawa kwa kila mtu. 

Ni mimi: emu-three

4 comments :

Unknown said...

Ni sawa kabisa unachosema dada m3 ILA huyo ni mfa maji haachi kutapatapa. Na haki itaonekana tu sisi wanawake tunanyanyasika Sana.

Unknown said...

Ni sawa kabisa unachosema dada m3 ILA huyo ni mfa maji haachi kutapatapa. Na haki itaonekana tu sisi wanawake tunanyanyasika Sana.

Unknown said...

Yaani dada sijui nisemeje unatufundisha Sana cjui wanaume wanasoma hii❓MN wamezoea kutunyanyasa sn na kutunyima haki zetu hili ni fundisho kubwa. Hongera

Anonymous said...

Everything is very open with a clear explanation of the challenges.

It was definitely informative. Your site is very useful.

Many thanks for sharing!

My web page; Cafe SD