Ghafla mlango
ukafunguliwa kwa kishindo, na shemeji mkubwa akawa kasimama mlangoni na
kutuangalia akiwa kakunja uso, na sisi tukawa kimiya, japokuwa kwa taratibu
zetu sisi kwa vile ni wadogo, ndio tulitakiwa tuanze kumsalimia, ….na
nilipoligundua hili nikafunua mdomo kuanza kutoa salamu, lakini nilikatishwa na
sauti yake ikisema;….’mama aliendelea mama kunisimulia maisha yake.
‘Kwanini huyu mtoto ananikimbia?’ aliuliza shemeji mkubwa akiingia
ndani, akiangalia huku na kule kama anamtafuta huyo mtoto yupo wapi, na mimi
hapo kama mama roho ikaanza kunikereketa nikifkiria kuwa huenda alikuwa na
lengo baya na mtoto ndio maana akakimbilia ndani.
‘Hatujui kwanini,
sisi tumemshangaa kumuona, akiingia mbio mbio, kama anaogopa kitu…. kakimbilia
chumbani kwake.’nikasema. Niliposema hivyo, akaniangalia kwa macho makali na
kusema kwa ahsira;
‘Mumeshaanza kuwapandikiza watoto fitina na tabia mbaya, …mnafanya
hivyo makusidi ili wanione kuwa mimi ni mbaya, ….kwanini mnafanya hivyo…hamjui
kuwa hawa ni malaika, hawajui lolote, hawana dhambi,….?’akasema na kuuliza kwa
ukali.
‘Hakuna aliyefanya hivyo shemeji, …nahisi ni uwoga wake tu,…huenda
kuna kitu alikuwa akifanya na alipokuona akahisi utamuadhibu,….’nikasema
kumtetea.
‘Haiwezekani, mtoto huyu nimeishi naye vizuri wakati tupo
kwenye msiba,….na mara nyingi alikuwa akiniona ananikimbilia kunipokea, leo hii
mumemjaza maneno mabaya na kuanza kuniogopa, na hata kunikimbia, …kuna kitu
mumempandikizia kwenye ubongo wake si bure…haiwezekani mtoto mdogo kama huyu
anajua nini….’akaniangalia kwa ukali.
‘Shemeji sijawahi
kumwambia chochote kibaya kuhusu wewe…’nikajitetea.
‘Nawambia,…na narudia kuwaambia, ole wenu nije kugundua hilo,…na kwanini
mnafanya hivyo, hebu niambieni…..mnataka ili iweje,…kwani mimi ni nani kwake,
nakuuliza mimi ni nani kwa huyo mtoto?’ akauliza.
‘Wewe ni baba yake mkubwa, na ndivyo alivyosema hata wakati
anaingia ndani,….’nikasema.
‘Kwahiyo ulimfundiha kuwa akiniona tu akimbilie ndani maana
shetani anakuja, au sio?’ akauliza kwa ukali.
‘Hpana shemeji sijawahi kufanya hivyo, na sitaweza kumharibu
mtoto wangu kwa tabia kama hizo, wewe ni baba yake, na anatakiwa kukuheshimu
kama alivyokuwa akimuheshimu baba yake…’nikasema.
‘Kama alivyokuwa akimuheshimu baba yake….kauli hiyo siipendi
kwani hapo unaanza kujenga utofauti, mimi ni baba yake….sio kama..hakuna ukama
hapa, akiwepo yeye, nikiwepo mimi, sote ni baba zake, sio kama alivyokuwa…hii
lugha vipi, mbona mna…..’akatulia na kugeuka huku na kule kama anaendelea
kumtafuta mtoto.
‘Samahani shemeji…..’nikasema nikitaka kuendelea kujitetea.
‘Hebu muite aje hapa, maana sitaki kabisa tabia kama hii
iendelee katika familia yetu, ukoo wetu unasifika kwa nidhamu, …mimi ni
kiongozi wa familia na nataka familia yote inijue kuwa mimi sina ubaya nayo, kila
ninachofanya mimi, nafanya kwa masilahi
ya ukoo na familia zetu….’akasema huku akiendelea kuangalia huku na kule.
‘Hata hilo la kufika hadi mahakamani ni kwa ajili ya kulinda
maslahi ya huyu mtoto, lakini masikini mtoto huyu hajui kitu, anazidi kupotezwa
na watu wasiomtakia mema….sikuwa na nia yoyote mbaya kwa hili lililotokea,
lakini….sijui nifanyeje watu wanielewe….jamani mimi sio mbaya kihivyo,nafanya
haya kwa ajili yake tu…kwa ajili ya vizazi vya familia hii….’akasema shemeji,
na sikutaka kulumbana naye, ikabidi nimuite mtoto ambaye alifika huku akiwa
kajikunyata kwa uwoga.
‘Shikam-mooo baba..mkubwa’akasalimia huku akishindwa kuficha
uwoga aliokuwa nao.
‘Marahaba, …sasa ndio unakumbuka kunisalimia,…kwanini
unanikimbia?’ akamuuliza akishusha sauti , sio kama alivyokuwa akiongea awali,
utafikiri sio yeye yule aliyekuwa akibwatuka kwa sauti ya ukali.
‘Niliogopa tu…’akasema.
‘Unaniogopa mimi au unaogopa nini?’ akamuuliza.
‘Hapana ….si… nilikuwa nachezea uchafu…nikaogopa kuwa
utanichapa…’akasema.
‘Ohoo, kumbe, sasa kwanini unachezea uchafu, ….nilikuambiaje
kule nyumbani?’ akamuuliza akimshika mabegani, na matoto aliposhikwa hivyo,
akashituka, kama vile kashikwa na umeme.
‘Nisichezee uchafu, nitavimba tumbo kwa minyoo….’akasema
huku akiangalia upande ule alioshikwa.
‘Sasa kwanini ukachezea uchafu…na wakati unajau kuwa uchafu
una wadudu wanaoleta safura, wewe huogopi wadudu wakiingia tumboni mwako?’
akamuuliza.
‘Nisamehe baba mkubwa……nawaogopa wadudu…. , lakini
nikimaliza kucheza nina-nawa mikono…kwa…kwa sabuni….mama alinifundisha
nikishika uchafu ninawe kwa sabuni….’akaanza kulia, akijua kuwa atachapwa.
‘Sasa kwanini unalia kwani nimekuchapa…nimekufinya?’
akamuuliza,
‘Nisamehe baba mkubwa sirudii tena….’akawa anaendelea kulia
huku akijikunyata huku akiniangalia na hata kutaka kumkimbilia, lakini baba
yake mkubwa akamshika mikono, na kusema;.
‘Siku nyingine nikikuona unachezea uchafu nikufanyeje…au
mama ndiye anakufundisha kuchezea uchafu?’ akaulizwa.
‘Unifi-fi-nye….hapana, mama huwa ananikataza kuchezea uchafu….’akasema
huku akiniangalia kwa macho yaliyojaa machozi.
‘Haya kwanza kanawe mikono, halafu hii hapa ndio zawadi
yako,….’akasema huku akitoa kigari kidogo cha watoto kwenye mfuko wake wa koti,’
na mtoto akasita kukichukua, na kuniangalia, nikamuashiria akichukue, na
akakipokea huku akitabasamu.
‘Haya chukua zawadi yako hii, kachezee, hizi ndio zawadi za
kuchezea, usichezee uchafu, unanisikia eeh, mtoto mnzuri, mimi ni nani….’akasema.
‘Wewe ni baba mkubwa….’akasema akitabasamu na ila hali ya kuogopa
ikawa imemuondoka na akawa akikishika shika kile kigari kwa furaja, na baadaye
akakumbuka na kitu, akamsogelea baba yake mkubwa akafanya kama anapiga magoti
na kusema;
‘Ahsante baba mkubwa….’akasema huku akiwa kainamisha kichwa
chini kwa adabu.
‘Ahsante na wewe….eeh, haya nenda kachezee kigari chako,….’akasema
shemeji, na yule mtoto akaanza kukichezea, na mimi nikamshukuru shemeji ambaye
alikuwa akimwangalia mtoto na kile kigari, sijui alikuwa akiwaza nini, na
baadaye akasema;
‘Mtoto huyu anafanana sana na baba yake, nikimwangalia
nahisi namuangalia ndugu yangu, lakini ndio hivyo tena , mungu keshamchukua
kiumbe wake, yeye kampenda zaidi yetu…’akatulia huku akionyesha uso wa huzuni, akatulia
kidogo, na baaadaye akageuka kuangalia pembeni, na kusema;
‘ Tatizo ni kuwa watu hawataki kunielewa,hali nalirudia
tena, labda ipo siku mtanielewa, lakini sijui lini, labda siku tatizo litokee
kwa sababu ya kupinga mawazo yangu, hapo mtanikumbuka, labda siku nikiondoka
duniani,…sijui….’akawa anaongea kwa sauti ya upole, halafu ghafla akapandisha
sauti na kusema;
‘Mimi nahangaika kuzipigania mali zake….’akawa anaonyesha
kidole ule mtoto alipoelekea
‘Lakini watu wananiona mimi ni mbaya, ….sasa mali hizi
zikichukuliwa na wanaume wengine, unafikiri huyu mtoto atapata nini…kwanini
hamtaki kunielewa, eti ndugu yangu, hebu nisaidie ….’akasema huku akimwangalia
mdogo wake huku kaelekeza kiganya cha mkono juu.
‘Mhhh….’ndugu yake akaguna bila kusema kitu, na hapo ikabidi
niingilie kati na kusema;
‘Lakini shemeji unaposema kuwa hizi mali zitachukuliwa na
mwanaume, una maana gani?’ nikauliza lakini sikuwa na nia ya kupata jibu.Yeye
akawa ananiangalia kwa uso wa kushangaa, na nilipoona hivyo, nikaamua kufafanua
usemi wangu na kusema;
‘Shemji mimi simjui mwanaume gani wa kuja kuzichukua hizi
mali, maana ni mali zangu, …kama ni mali zangu kwanini mwanaume aje azichukue…?’
nikaendelea kuongea kama vile nauliza na shemeji hakunijibu akawa bado ananiangalia
na uso wa kushangaa, na baadaye akageuka kumwangalia ndugu yake, sijui alitaka
yeye ajibu hilo swali au alikuwa na maana gani, na hapo nikaona nisinyamaze
nikaendelea kujitetea, nikisema;
‘Mimi ni mama wa huyu mtoto…nina uchungu naye sana,…., ina
maana mimi sina imani na huruma na huyu mtoto, mpaka nikubali mali hizi
zichukuliwe na mwanaume mwingine, …na sijui huyo mwanaume ni nani, au kwa vile
nilikubali marehemu aziandikishe hizi mali kwa jina lake , ndio mnafikiria kuwa
nitafanya hivyo kwa kila mwanaume. …’nikasema huku nikikunja uso kwa huzuni.
‘Jamani, hata hivyo sitarajii kuolewa na mwanaume yoyote
kama ndio mawazo yak ohayo shemeji…kamwe sitaolewa tena, nimeamua maisha yangu
kujiendeleza mwenyewe….sitaolewa tena,…hususani kurithiwa na yoyote kati yenu..’na nilipotamka maneno
haya, akaniangalia kwa kugeuza kichwa
haraka, …na yeye akasema .
‘Unaona…kiburi…mimi nilikuwa naongea, sijakuruhusu kuongea
umeshaanza kuongea, tena kwa kujiamini kabisa….’akatikisa kichwa na kumwangalia
ndugu yake, kama vile anaomba msaada wa hilo alilolisema.
‘Hii ni tabia ya ajbu kabisa, unafikiri kwa vile upo huru,…ndugu
yangu kaondoka, wewe sasa ni kidume, au…’ akawa kama anaiuliza .
‘Kwa vile ….eeeh, ‘
akawa anajitingisha tingisha, na akiangalia pembeni, na kuendelea kusema.
‘Sasa unaweza kuongea utakavyo, ndivyo ulivyofunzwa hivyo,
…ndio heshima hiyo kuwa ukiwa na wanaume, unaruka juu, na kusema utakavyo,…’
akatulia na kuniangalia halafu hata kabla sijajitetea akasema;
‘Kumbuka mila na desturi zetu zipo wakati wowote…ukumbuke
bado wewe ni mke wa familia yetu.na kama ni hivyo, adabu, na mila zetu
unastahiki kuzifuata, na kama hutaki hilo, basi, subiri wakati muafaka utafika,
utakwenda huko utakapo…ukafanye hayo utakayo,na upendavyo,lakini sio hapa, na
ikifikia muda huo ukaamua kuondoka….mali za huyu mtoto zitabakia mikononi
mwake…..zinabakia hapa hapa, kwani zipo kwenye aridhi ya ukoo wetu….’akasema.
‘Samahani shemeji, …sikuwa na nia mbaya, nilikuwa tu
nakufahamisha nia na lengo langu…’nikasema.
‘Sawa kabisa, nimelielewa lengo lako ndio maana nikakubali
hadi kufika huko mahakamani, kuonyesha msimamo wa familia na ukoo wetu,…na
usifikirie kuwa mimi ni sawa na hawo wanaume wengine wanaodanganyika
kirahisi…..mimi…nimelelewa na kuiva kimila na desturi zetu, na wananifahamu
wazazi wangu, ndio maana waliponipa hilo jukumu, hawakuna na shaka na mimi…’akasema
akionyesha tambo.
‘Lakini ndio hivyo, utasemaje kwenye hii dunia ya sasa,
wanawake siku hizi wanaota mapemba, eti wanadai haki, na angalia hiyo haki wanayoidai
ni haki gani,….haki ya kukiuka mila na desturi zetu, haki ya kutembea uchi, ….nusu
uchi….jamani, ndio haki mnayoitaka hiyo,….ole wenu, maana dunia hii
ikiharibika, mtakuja kubeba lawama kubwa sana,….mnadai haki , haki ya kuwapuuza
wanaume zenu...
'Yaani nyie, mnaona hayo waliyobuni wazee wetu ni mabaya, nyie sasa mna hekima
zaidi yao….hata siku moja, hamtaweza kuwazidi wazee wetu kwa hekima, wao
walikuwa wakiona mbali, wakiona nini kitatokea kama ikifanyiak kinyume chake,
na walitaka hivyo kwa maslahi ya ukoo, na familia, sio kwa maslahi binafsi….eti
nyie sasa mumesoma, ….manshika pesa, mnashika madaraka,…mnaanza kuvimba kichwa….’akacheka
kwa kebehi halafu akasema.
‘Mimi siwakatazi kudai haki zenu, daini….hata mkitaka
kutembea bila hati chupi mitaani, tembeeni…lakini,…. lakini angalieni ni haki
gani za msingi mnazostahili kuzidai, angalieni mbali, niliwaelezea kwenye
kikao, na hata baba …yule mzee wetu aliyebakia wa siku nyingi, alielezea …kwanini
tunafikia kufanya hivyo…wao waliona mbali…..’akasema na akawa kama anawaza
jambo, na kwa sauti ndogo ya unyenyekevu akasema;
‘Sasa aah, jamani, nawaombeni, nyie mliokulia hapa kijijini,…mkabahatika
kuishi na wazee wetu hawa, mkapata amadili yao,…. jaribuni kuwa mfano,lindeni
heshima na mila zenu, ili vizazi vyetu
vije kujifunza, kuna maadili na baraka zake, nyie hamuwezi kuziona lakini
matokea yake mnayaona….’akatulia na kuangalia huku na kule.
‘Hebu sasa hivi angalia, mzazi anafariki, mali zinachukuliwa
kama hivi, baadaye anatokea kidume mshawishi, anakuja, anazimilik hizi mali,
watoto, wanatelekezwa, yule kidume, akajali damu aliyoizaa yeye, wenye haki
wanaweza hata kufukuzwa…hilo jamani hamlioni’akawa kama anauliza.
‘Haya hata kama hilo hamlioni, angalieni mayatima siku hizi
ni nani anawajali…hakuna, kwa vile hawajulikani tena, kwa vile mila na desturi
zetu zimepuuzwa, kuwa mtoto ni mtoto wa kila mtu, mtoto kwenye familia , ukoo,
jamii, ni mtoto wa kila mtu, hata kama mzazi wake kaondoka, bado aisikose
matunzo, maana baab zake tupo…jamani kwanini hamtaki kunielewa…..’akashika
kichwa.
‘Niwaambieni, ….ni siri hii nawatobolea, angalieni familia
ya huyo mwenzetu hapo jirani, yeye kajifanya msomi, haya, binti yao mkubwa
kaolewa, na mara mumewe akafariki, …mali ile akarisishwa huyo binti, maana wao
ni wazungu, na yule binti kaolewa na mume mwingine….yule mwanaume, akawa mjanja
kaja na mambo yake, ila mali akaiandikisha kwa jina lake….ooh, mungu hana
hiyana, akamchukua na huyo binti,…..’akatulia.
‘Mali ile sasa ni ya mwanaume,….yeye akasema anauza mali
yake, na anakwenda kuishi kwao…’akatulia.
‘Hebu fikirieni, huyu mwanaume anauza hiyo mali ya kizazi
cha ukoo, ambao alikuja akaukuta, je ukoo huo unakua, utakuta nini tena….hilo
hamlioni, …kwanini akili zenu zinadumazwa na mila za wageni wenye ubinfsi..sisi
ni wajima, kuwa mali za familia ukoo, zinabakia kama za jamii hiyo, kizazi hadi
kizazi…..hata shule hiyo ndogo hamuielewi, jamani…’akjikuna kichwa kama anawashwa.
‘Aaah, naona, sitaeleweka hapa,…hayo tuyaache, …’akasema na
kumgeukia ndugu yake.
********
Mwanangu, siku hiyo
ilikuwa siku ya aina yake, huenda ndio siku mungu alitaka kubainisha ukweli
wake, kwani kichwani moyoni, nilikuwa nimejawa na mawimbi , mawimbi ya kutaka
kuongea na kumuelezea vila ninavyojisikia huyu shemeji yangu mkubwa, lakini
alikuwa hataki kunipa nafasi, na baadaye alipomgeukia ndugu yake, nikaona
sitaweza kupata nafasi hiyo, nikatulia….’akaendelea kuhadithia mama
‘Na wewe msomi,….wasomi, wa siku hizi bwana, ….aah, ngoja
nisiseme mengi, …Hebu niambie kwanini umeondoka bila kuniaga, …?’ akamuuliza
mdogo wake akitabasamu kwa dharau.Ndugu yake naye akatabasamu na kusema;
‘Bro, mimi nilikuona umepumzika, …na kwa vile ulitoka kwenye
kazi na mawazo ya kesi yakawa na mimi yananichanganya, basi nikaona nikuache
upumzike, na mimi nipoteze mawazo kwa kutembea tembea….hata hivyo kaka, ingelikuwa
sio adabu njema kukuamusha.’akajitetea ndugu yake.
‘Usinidanganye bwana mdogo,…mimi naona hadi ndani ya ubongo
wako, ni nini unachokiwaza,… hakuna cha kuniacha kupumzika au nini, wewe uliona
kuwa ukianiambia kuwa unakuja huku kwa huyu ….aah,… shemeji, ….’akageuka kuniangalia
huku akinionyeshea kwa kidole,….mimi
sikumjali maana wakati ule nilikuwa namimina juisi kwenye gilasi,….na baaadaye
akamwangalia ndugu yake, na kusema.
‘Ulifikiria nitakupinga usije kwake, au sio…nikuambie ukweli
mimi mwenyewe nilikuwa na wazo hilo la kuja huku, mimi bwana mdogo, akili yangu
inafikiria mbali kuliko mnavyofikiria nyie, …sawa hata hivyo hakijaharibika
kitu, tumeshafika hapa, …na ingenilazimu kufika hapa , hata ingelikuwaje maana
unafahamu fika msimamo wangu,…..haya niambie za kutangulia, mumeongea nini na
huyu shemeji…?’akasema na kunigeukia mimi. Na aliponiona nimetulia
nikiwaangalia, huku nimeshiak gilasi za juice, akasema’
‘Ahsante shemeji wewe weka hapa mezani, tutakunywa kwa muda
wetu, sasa hivi mdomo una kazi ya kuongea , sio kunywa, au kula…..na usiondoke
hapa, nina mazungumzo mazito na wewe…sio kwa vile kesi inaelekea vile
ukafikiria basi umeshinda…..hapana kushinda kule, sio kushinda ndani ya ukoo
huu, mimi kama kiongozi sitatetereka….’akasema .
Sikusema kitu nikawa nimetulia, na niliweka zile gilasi za
juice mbele yao, na kuzifunika na vifuniko vyake, na mimi nikakaa pembeni, nikimenya
machungwa, na yeye akawa ananiangalia kwa makini, mpaka nikahisi vibaya, halafu
akasema;
‘Hongera shemeji, naona umakipata ulichokitaka…..kweli wewe
king’ang’anizi, unataka kudai hata mali za watoto…unataka hiyo mali ukampe
nani,….kama kweli una nia njema, basi olewa na ndugu yangu huyu, …ili mali
iendelee kubakia kwenye familia hii kwa masilahi ya mtoto huyu, au watoto
watakaokuja…’akasema.
‘Shemeji samahani, …..naomba nijitetete kwa hilo….’nikasema.
‘Ujitetee, kwani yule wakili wako yupo wapi, au leo unataka
kujitete mwenyewe, haya sema, sioni ajabu, …wewe sema tu, …maana mdomo wako
unawashwa kuongea, haya sema unachotaka kusema, usifikirie kuwa mimi sinawapi
uhuru wa kuongea, ila ongea kwa hekima, haya ongea,….’akasema huku akinywa
juice.
‘Shemeji mimi sijang’ang’ania mali za mtu....au kudai mali ambayo sio ya
kwangu,..kama ulivyoona kwenye mahakama, ile stakabadhi inaonyesha wazi kuwa nyumba
hii nilijenga kwa pesa zangu, duka lile nilijenga kwa pesa zangu, ina maana
kweli ningelidai kitu kisicho changu, hapana mimi sina tabia hiyo….ninakuapia
shemeji, mimi sijajenga hii nyumba na duka kwa pesa za marehemu, pesa za marehemu ziliibiwa kabla…..je ina maana
mwanamke hana haki ya kudai kitu alichojenga kwa pesa yake?’ nikauliza.
‘Ina maana nyumba yote hii na duka ulijenga kwa hizoo pesa…za
kamari, ..oh, sijui za bahati nasibu, samahani, ila mimi sioni tofauti yake,
kamari na bahati nasibu?’ akauliza.
‘Ndio hivyo shemeji....huo ndio ukweli,kuwa nilijenga vyote
hivyo kwa pesa niliyoshinda kwenye hiyo promosheni ya kampuni ya simu, na wala
sio kamari….’nikasema na yeye akawa ananiangalia moja kwa moja machoni.
‘Mhh, mimi haliniingii akilini kabisa, wewe, mwanamke uwe na
pesa kiasi hicho, uwe na akili ya kufanya hili, mmmh inawezekana kweli bwana
mdogo, pesa yake, ajenge nyumba kwenye familia badala ya kwenda kujenga
nyumbani kwao….?’ Akamgeukia ndugu yake, na mimi sikutulia nikasema.
‘Shemeji …kama unakumbuka, baada ya marehemu kutoka jela,
hakuwa na chochote, na maisha yake yalikuwa kama mlivyomuona, akawa kazi yake
ni kulewa, na hata hizo pesa za pombe, alikuwa akichukua kwenye duka…..huo ndio
ukweli wenyewe,…na nilijua kuwa nimeolewa, na ukiolewa unakuwa mmoja wa familia
hiyo, tuna mtoto…ataishije baadaye, kwahiyo nilijitahidi kujenga nyumba na
duka, na pesa za duka, ndizo zilizoweza hata kumtibia marehemu mume wangu…..nilifanya
hilo nikijua mimi ni mzazi….’nikasema kwa uchungu.
‘Hogera sana,….’ Akawa anapiga makofi, huku akimwangalia
ndugu yake na baadaye akaniangalia mimi huku akitabasamu kwa dharau.
‘Mmm, mimi sijui niseme nini, maana sijui umerithi wapi hiyo
tabia, …tabia hiyo hufanani kabisa na kabila letu, tabia ya kupenda sana mali….mwanamke
kupenda sana mali sio tabia ya kabila letu, kabila letu mwanamke anampenda
mumewe, na mali inakuwa miliki ya mumewe, vinaunganishwa hivyo, mke, mume mali ….mali
haiwi kati, inakuwa juu, mikononi mwa mume…’akasema huku akimwangalia ndugu
yake, ambaye alikuwa katulia kimiya, huku akionyeshea kwa mikono.
‘Ndugu yangu mbona upo kimiya, ..wewe si msomi, au ndio…nakuona
ndugu yangu umeshalogwa wewe..hata hivyo hawatakuweza, kama nipo hai,
hawatakuweza, hawataiweza familia hii…na naona sizani kama utamuweza huyu
mwanamke, huyu anafaa kuishi na mimi…sio watu laini laini kama nyie…’akasema,
huku akiangalia nje, na alioenekana kama anataka kuondoka, akasema;
‘Haya bwana mdogo kazi kwako, ..kwanza hebu niambia wewe
umefikia wapi, maana hapa kichwa kimechanganyikiwa, hata sijui nifanyeje,najua
umekubali kuachia hizi mali, ….kwa huyu mwanamke, kwasababu ya kupenda, au sio,kupenda
nako bwana…..haya, sawa, kama ni hivyo…nahitaji matokea yenye faida kwa
familia. …’akasema akimwangaia ndugu yake. Na ndugu yake akawa hasemi kitu, na
kaka yake alipoona ndugu yake yupo kimiya akasema.
‘Kama umakubali mali iandikishwe kwa huyu mwanamke, na
familia yenyewe, unataka kuiachia, hivyo hivyo, huyu mtoto naye ina maana hana
chake, sio haki yake….eneo hili ni mali ya nani,…sawa hata kama nyumba
imejengwa na unakubali kuwa isiwe ni ya familia, lakini nyumba imejengwa wapi,
imejengwa kwenye ardhi ya ukoo wetu…..hayo ndio maswali ya kujiuliza…haya
niamabie na hilo utaliwekaje?’ akauliza.
‘Una maana gani kaka kusema hivyo,…maana hawa wapo,
hawatakwenda kokote,…nyumba hii ipo, hata kama hati miliko ipo kwa jina hilo la
shemeji, ..bado ni mali ya familia, yeye na mtoto, .. na mimi nitakuwa nafika hapa
mara kwa mara kuangalia kuwa hali zao ni njema,…zaidi ya hayo siwezi
kumlazimisha…’akasema.
‘Kaka hilo tutakuja kuelewana, halina shaka, ni maswala
madogo ya kuelewana….’akasema ndugu yake huyo, na kauli hiyo ilionekana
kumkwaza ndugu yake, akakunja uso,
‘Maswala madogo…haya ni maswala madogo…..sikuelewi….hivi ina
maana mimi naongea utumbo hapa, hata wewe ndugu yangu hutaki kunielewa,…..?’
akawa kaanza kukasirika.
‘Bro,…kwanza kuhusu hilo la kumuona shemeji, naona tulipe
nmuda, hatuwezi kumlazimsha eeh,…’akasema na kabla hajamaliza ndugu yake
akamkatiza na kusema.
‘Unaona…legelege kabisa,, kwani hapa unalazimisha au ndivyo
taratibu zilivyo…yeye kwasasa hana hiari, …anatakiwa akubalia kauli ya
marehemu, kuwa wewe ndiye mume wake…je ina maana alikuwa akibisha kauli za
mumewe, …nafahamu kwa tabia aliyo nayo, sizani kama alikuwa akimtii
mumewe…..sizani…maana hii inajionyesha wazi, niliwahi kumwambia ndugu yangu
kuwa sasa yeye kaolewa, badala ya kuoa, sijui kama alinielewa, ….eti aliniambia
nisiingilia ndoa yake….’akasema huku akinyosha mikono ya kukata tamaa.
‘Bro, kwa hilo….hatuwezi kumlazimisha shemeji,…kaka…unakumbuka
mwenyewe , hata kwenye kikao kile cha familia ulisema, kuwa hilo la kurithiwa
ni hiari yake...mimi nipo tayari kumuoa, lakini ni kwa hiari yake, lakini kama
yupo tayari….hata hivyo kaka bado tunaongea, naomba hilouniachie mimi mwenyewe,
nitajitahidi kadri ya uwezo wangu kuongea naye, maana yeye sio mtoto mdogo,….kama
atakubali , ninamuhakikishia kuwa hatapa shida,….na sifanyo hilo kwa vile
tunataka mali ziendelee kuwa mikononi mwetu, hapana, nafanya hivyo, kwa vile
…..nimempenda….’akasema shemeji na mimi nikaona nikae kimiya mpaka wanatakaponiruhusu
kuongea.
‘Sikiliza bwana mdogo, wanawake kama hawa walioonja pesa,hawawezi
kamwe kukubali kwa hiari yao, hapa alipo anajiona kama dume…anajiona kuwa
anaweza kuishi maisha bila kumtegemea mume, ndivyo anavyojidanganya, anafikiria
bahati kama hiyo inaweza kuja tena…kama ulibahatisha mara moja, sio kila siku
utabahatisha…maisha bila mume utafika mahali utakiuka maadili na kuanza
kujiuza…’akasema.
‘Kaka naomba hilo uniachie….usimsononeshe, au kumtisha
shemeji,….yeye ni mtu mzima ana akili ..’akasema mdogo wake na ndugu yake akawa
anamwangalia kwa macho makali, ilionyesha kuwa alikuwa na hasira fulani na
ilikuwa ikifukutua kwenye moyo wake.
‘Tatizo lako,..ndio hilo, hutaki kuiga yale ya msingi,…hutaki
kunisikiliza, mambo mengine hayahitaji shule, ukifuatilia ya shuleni,
utavurunda, ndio maana dunia inaharibika….watu hawajui ni nani mkubwa, ni nani
kiongozi, kila mtu ni mkubwa, kila mtu ni kiongozi……’akasema huku akisimama.
‘Kaka sio hivyo, ila kila mtu ana hiari, na nafasii ya
kujitetea, hatuwezi kulazimishana kwa kila jambo…’akasema.
‘Bwana mdogo ina maana hata kama mimi sipo utakuwa lege lege
hivi hivi katika kuendeleza familia.
Uongozi sio lele mama, kuna mahali
inahitajika kuwa mkali, na kuna mahali unahitajika kuwa mpole. Kwa hili bwana
mdogo, nakuhakikishia ukitaka siasa, lele mama….kama unatongoza mwali, hutafika
kokote, utajikuta, ukiingia jikoni, ukiosha vyombo, huku mwanamke, kakaa kwenye
kocho, kapak hina, anakuamrisha `nataka
maji….’, fanya haraka nina njaaa…’
akawa analegeza sauti ya kike, na mwishoni akasema;
‘Ndivyo mnavyotaka wasomi au sio, haki sawa nusu kwa
nusu,….bwana mdogo dunia hii ukiwaachia hawa watu watawale….kila kitu
kitaharibika….tupo, mtakuja kuniambia,….haya mambo.bila kuwa mkali
hutafanikiwa…..huyu anahitajika kukemewa
maana keshajenga dharau…kiburi, kwa vile keshaonja pesa , tena pesa nyingi….’akasema.
‘Kaka mimi naomba tu,
wewe niachie hili, usiwe na shaka, mimi niliongea na marehemu, akanielekeza
jinsi gani ya kuishi na shemeji, alimfahamu tabia yake, na sijawahi kumsikia
akimlalamikia kwa ubaya, kiujumla alikuwa akimsfia shemeji kuwa kati ya
wanawake waliojaliwa kuwa waadilifu, yeye ni mmojawapo, sasa naona ajabu
nikisia hivyo unavyosema wewe…’akasema mdogo mtu.
‘Mimi sidanganyiki bwana mdogo….nawafahamu sana hawa
wanawake….nawafahamu sana wanaume kama ndugu yangu, mkiwa kijiweni, mnatamba,
mimi bwana mke hanibabaishi, nitamuweza, fika nyumbani uone mambo ya aibu,
….anaosha vyombo chumbani, ili asionekane na marafiki zake…..sio mimi, ….na
nikiona ndugu yangu anafanyiwa hivyo,
huyo mwanamke, nitamtoa mkuku kwenye hii familia…’akasema.
‘Nimekuelewa kaka, ….ndio maana sitaki kulichukulia hili
jambo kwa pupa, ..yeye mwenyewe ni mtu mzima, kama analiona hili halina maana
kwake, basi huenda ana mipango yake mingine, tumpeni nafasi,…tuone ni nini
anakitarajia,…., hata hivyo, bado tunaongea,..’akasema mdogo mtu.
‘Bado unatongoza bwana mdogo eeeh, …aibu kabisa…..unatongoza
kwani huyu ni mwali wa kutongozwa, wakati hali halisi inajulikana….sikia bwana
mdogo, ukishindwa, niachie mimi…nitajua nini cha kufanya…na ukishindwa , mimi
nitamchukua mwenyewe, hanishindi, wiki moja tu atakuwa kama hawo shemeji zako….’akasema
akipiga piga kifua.
‘Kaka….’akataka kujitetea mdogo mtu, lakini kaka yake
akamuonyeshea mkono wa kumtuliza, akasema;
‘Nisikilize bwana mdogo, nimechoshwa na hiyo kauli yako,…..Mimi
kama bado ni kiongozi wa hii familia, nitahakikisha kila kitu kinakwenda kwa
matakwa ya familia, na taratibu zetu, ikiwemo hili…la mali zote zilizopo kwenye
familia,…unanisikia sana ni marafuku
kuandikishwa jina la mwanamke, kwasababu yeye ni mtu wa kuja tu, na siku yoyote
anaweza kuondoka….’akasema na mimi nikaona niingilie kati na kuseema.
‘Hizo ni mali zangu nina haki nazo, sio mali za familia….japokuwa
zimejengwa kwenye eneo la familia yenu, lakini ni kwa ajili yangu na mtoto
wangu’nikasema.
‘Unasema nini, nani kakuambia uongee…`hiyo wangu ‘ imetoka
wapi, mtoto wako huyo…funga mdomo wako na ukome kabisa….sitaki kusikia hiyo
kauli,…mtoto wangu….ndivyo akili yako inavyokutuma eeh,’akasema kwa hasira .
‘Kaka…..’mdogo mtu akataka kuingilia, na hali ya hewa
ikaanza kubadilika, maana jamaa aliona anapingwa kitu ambacho akukipenda,
akasema kwa hasira;
‘Pili nataka huyu mwanamke akubali kuolewa na
wewe…vinginevyo, sijui…..hatutaweza kuendelea kubembelezana na watu walioshindikana,…
njia ni nyeupe….kama alivyokuja, anaweza kuondoka, lakini ukiondoka, kila ulichokikuta
hapa, kila kilichopo hapa kitabakia hapa hapa…..hiyo ndiyo kauli yangu….’akasema
huku akisimama na ikawa kama anataka kuondoka….
‘Shemeji..tafadhali…naomba na mimi mnisikilize….’nikataka
kujitetea, …oooh, kumbe nimeharaibu, maana wakati anaongea alikuwa kamgeukia
mdogo wake, sasa kusikia sauti yangu kwa mara nyingine, akanigeukia kwa hasira
na kuniangalia kwa jicho la ukali na mwili ukawa unatetemeka, ….akawa ananiangalia huku mishipa ya shingo imetuna.
‘Haya ndio nisiyoyataka, ….nimekukanya mara ngapi,…kiburi
eeh,..wanaume wanaongea, wewe unajifanya kidomo domo….ni nani kakupa nafasi ya
kuongea, kama nilitaka wewe uongee, ningekupa nafasi, hiyo tabia ya
kunikatisha,….naona imezidi na nisipokufundisha adabu leo, hutanielewa, …ngoja,
nikuonyeshe adabu za hii familia….’nilihisi hatari, maana sifa za huyu jamaa ni
kuwa akikasirika au akizamiria kufanya jambo, huwa harudi nyuma, ni mpaka
alifanye,hio jambo,….nikaona ananigeukia, na kuanza kunijia.
‘Hoooh, kaka imekuwa hayo tena…kaka..utaharibu kila kitu,
elewa upo wapi….kaka tulia kaka’akasema mdogo mtu akitoa macho ya uwoga
‘Kelele wewe…ngoja nikuonyeshe jinsi gani ya kuishi na hawa
watu,…’akasema akimnyoshea mdogo wake kidole, na akaanza kunijia mimi.
Pale alipokuwepo, ili anifikie ilibidi ampite ndugu wake
kwanza, ….na ndugu yake alishashikwa na butwaa, na anamfahamu sana ndugu yake
huyo kuwa akiwa na hasira hashikiki, ukimshika ujue atakugeukiwa wewe… ni bora
wewe uliyesababisha hivyo ukimbie, vinginevyo anaweza akakujeruhi vibaya sana,
hata kukuua….
Mdogo mtu alipomuona kaka yake kakasirika, na alivyomuona
jinsi alivyobadilika, akajikuta akiogopa, na macho ya uwoga yakamwingia,
hakujua afanye nini, akasema huku akiwa na wasiwasi.
‘Shemeji toka nje kimbia…’akasema
mdogo mtu, hata hivyo pale nilipo
nisingeliweza kutoka nje kabla hajanikamata, nikajipa moyo, na ujasiri
ukaniingia kama wa paka aliyenaswa kwenye chumba kidogo.
Mkononi nilikuwa bado nimeshika kisu ambacho nilikuwa
namenyea chungwa, nikasema moyoni, akanisogelea tu, hicho kisu kitakuwa silaha,
na sitasita kukizamisha mwilini mwake, kama akinizuru…
Akawa keshampita ndugu yake, na sasa ananikaribia mimi,
akiwa kakunja ngumi..uso umembadilika kwa ghadhabu, na mara mlango ukagongwa….
NB: Ni nini kilitokea
WAZO LA LEO:Haki ya kutoa mawazo kujietetea na kuelezea hisia ni za kila mtu hazijali ujinsia umri au hali ya mtu. Tusizarau mtu kutokana na ujinsia wake, au hali
yake,huenda alilotaka kuongea, kujitetea ni la msingi na linaweza likajenga na kuleta maendeleo na upendo kwenye jamii, haki sawa kwa kila mtu.
Ni mimi:
emu-three
4 comments :
Ni sawa kabisa unachosema dada m3 ILA huyo ni mfa maji haachi kutapatapa. Na haki itaonekana tu sisi wanawake tunanyanyasika Sana.
Ni sawa kabisa unachosema dada m3 ILA huyo ni mfa maji haachi kutapatapa. Na haki itaonekana tu sisi wanawake tunanyanyasika Sana.
Yaani dada sijui nisemeje unatufundisha Sana cjui wanaume wanasoma hii❓MN wamezoea kutunyanyasa sn na kutunyima haki zetu hili ni fundisho kubwa. Hongera
Everything is very open with a clear explanation of the challenges.
It was definitely informative. Your site is very useful.
Many thanks for sharing!
My web page; Cafe SD
Post a Comment