‘Sikuweza kuamini
mjukuu wangu,….ulikuwa mkoba ule ule niliokuwa nikiuona kwenye zile ndoto
nilizokuwa nikiota kule hospitalini….ni miujuiza ya mungu…’babu akarejea maneno
hayo.
‘Unautafuta huu
mkoba?’ akaniuliza huku akinitizama huku akijaribu kila iwezekanavyo nisimuone
zaidi ya ya macho yake, amabyo pia yalikuwa hayaonekani vizuri kwa vile ile
nguo aliyojifunika ilikuwa inacheza cheza kutoka na upepo.
‘Nafikiri ndio huo….’nikasema
nikinyosha mkono kuuchukua, ili niweze kuutambua,lakini yule mtu hakunikabidhi
akaurudisha na kuuweka pale alipouchukulia, na akasogea na kukaa pale alipokuwa
amekaa, na taratibu akajifunua zile nguo alizokuwa amejifunika usoni…..na
kugeuka kuniangalia…’
Hapo ndipo babu
alipoishia, lakini akili yangu ikavutiwa na maelezo ya mama ambaye lishafika
akitaka kuendelea kuelezea nini kilitokea, kwani siku ya kesi ilishafika.
*******
Ilikuwa ni asubuhi ambapo tulipanga iwe siku ya kikao kwa
ajili ya maandalizi ya kesi yetu, ambayo ilitarajiwa kufanyika kesho yake,
kwahiyo wale wote waliotakiwa kuwa mashahidi walitarajiwa kuwepo kwenye hicho
kikao.
Mimi nikiwa na wazazi wangu, tukiwa tunawasubiri hawa
wageni, tukawa tunaongea hili na lile katika kupoteza muda, kwa ujumla hatukuwa
na matumaini sana japokuwa watu mbali mbali walishakubali kutoa ushahidi
akiwemo mjumbe, na mafundi waliojenga hiyo nyumba, japokuwa tulifahamu kuwa
ushahidi wao hautakuwa na nguvu sana.
‘Sisi tusikate tamaa, hao hao mashahidi watatosha,na nina
imani kwa vile tunachotetea ni haki yetu, watakachoongea huenda kikasaidia
kumshawishi hakimu…’akasema baba.
‘Ushahidi muhimu ni huo wa malipo ya hiyo pesa, kuwa kweli
ulilipwa na hiyo kampuni, na hapo kunahitajika stakabadhi ya kulipa hiyo hundi,
…’akasema mmoja wa mashahidi ambaye alikuwa kafika mapema nay eye alikuwa
akifahamu sheria kidogo.
‘Lakini hebu niulize….sasa yule mwanamke aliyekuja siku ile
na kusema kuwa yeye ni mwanasheria na akasema anatafuta njia ya kukusaidia
akadai kuwa mtakutana mahakamani alikuwa na maana gani?’ akauliza mama.
‘Mama yule ni mchumba wa huyo wanayemuita mwanasheria wao wa
familia, ….kweli kwa hali halisi anaweza akamsaliti mchumba wake…akaisaliti
familia ambayo anatarajia kuolewa na kuishi nao?’ nikauliza.
‘Inavyoonekana kuna kutokuelewana kati yake na huyu mchumba
wake..’akasema baba.
‘Kama ni hivyo, basi tunaweza kumtumia , hata kupata huo
ushahidi unaohitajika mahakamani,ambao nahisi wanao wao, kama kweli
hawajauharibu..’akasema mama.
‘Mimi bado sijamuamini,…..ukiangalia kwa makini, inaonyesha yule
mwanamke alifika siku ile kuchunguza, …jambo, na mimi nahisi kuwa alitaka kujua
kuwa kweli wewe upo tayari kurithiwa na huyo mchumba wake, akionyesha wivu,
nyie hamulioni hilo,….yule anampenda sana mchumba wake, lakini huyo mchumba
wake, anatamaa…na nahisi siku ile alipogundua kuwa huna nia hiyo akaona arejee
kwa mchumba wake….’akasema baba.
Mara mlango ukagongwa, na wote tulikaa kimiya , na mimi
nikainuka nikijua kuwa huenda ni hawo wageni wetu, tuliowatrajia, na nikaenda
kufungua mlango, na malngo ulipokuwa wazi, nikajikutwa nimeshikwa na butwaa, na
kwa sekunde chache nilibakia nimeduwaa, halafu kwa sauti isiyo na nguvu nikasema
;
‘Karibu..’nikageuka kuangalai ndani huku nikiwa nimekunja
uso.
‘Shemeji samahani nilikuwa nataka tuongee mimi na wewe
faragha…’akasema huyo mgeni huku akiwa kasogea na kuwa karibu na pale
niliposimama, na kwa hali hiyo akawa anaonekana na wazazi wangu waliokuwa ndani.
‘Mimi sina kitu cha kuongea na wewe faragha, nakumbuka kwa
mara ya mwisho niliweka wazi msimamo wangu, …sasa sioni kwanini bado unanifuata
fuata, kama umeamua kunidhulumu haki yangu, basi fanyeni hivyo….lakini mimi
siwezi kujizalilisha kwenu, na nakuomba unielewe hivyo…’nikamwambia.
‘Shameji siku ya kesi imekaribia…, na ukiangalia kiukweli
wewe huna ushahidi wowote utakaokusaidia, na mimi nisingelipenda kukuona wewe
ukienda kuumbuka mahakamani, na pili mimi sina haja ya kukudhulumu,
ninachokifanya ni kusaidia pale ndugu yangu alipoishia na kuhakikisha kuwa mali
yake inakuwa salama, na kwa jinsi alivyotaka yeye..kuwa niiweke kwenye mikono
salama na wewe uwe na mimi…kama familia yangu…’akasema
‘Hayo ni maneno yenu na hiyo ni mipango yenu, sisi hatuwezi
kuwaiingilia,….endeleeni hivyo hivyo na mipango yenu ya uwongo wa kutunga, mimi
nina imani kabisa kuwa mume wangu hakuwahi kusema hayo, na kama alisema,
ilikuwa ni kipindi kile alichokuwa kachanganyikiwa na ulevi, lakini baadaye
alitulia….. , mimi nina imani kabisa kuwa alikuwa keshafahamu ukweli kuwa
nyumba na duka nilijenga kwa pesa yangu…na
tuliongea naye hadi akasisitiza kuwa tukabadili hiyo hati ya nyumba iwe kwa
jina langu…’nikasema.
‘Shemu, mbona unarudia hayo hayo….kama ni kweli ushahidi upo
wapi,…tusaidieni kwa hilo, nionyeshe huo ushahidi ili nijirishe nafsi yangu,
hujui ni kiasi gani ninavyotaabika kiakili, nikisikia hivyo, wakati kaka yangu
alianiambia tofauti na hayo unayoyaongea….?’ akauliza.
‘Kwani wewe ni hakimu, ….mpaka uhitaji huo ushahidi wetu,
huo ushahidi wetu unautakia nini, hili swala kwa sasa lipo mahakamani, na kama
kuna ushaidi basi utakutana nao huko mahakamani, wasi wasi wako ni nini?’
akauliza baba kuingilia mazungumzo yetu.
‘Wazee wangu shikamooni, samahani sana kwa kutokuwaslimia,…..’akasema huku akiweka mikono kifuani kuonyesha kuwa
ana adabu kwao, na wazee waakmuitikia, na baadaye akasema;
‘Mzee…, mimi ndio maana nimefika hapa kwa nia njema kabisa
ya kumsaidia shemeji yangu huyu, ..huyu ni shemeji yangu, na nimejaribu kuwa wazi
kwake, kuwa nipo tayari, kufuata taratibu zote za kimila,…ikiwemo hiyo ya kumrithi
mjane…., na labda hilo neno sio sahihi kwake, linaleta hisia mbaya, lakini ni
ukweli usiopingika kuwa mtu akifiwa, na mumewe, sio kwamba ni adhabu kwake, ….kuwa
basi yeye hawezi kuishi na mume mwingine tena…..na kama ikibidi, labda
sihitajiki kuliongea hapa kwenu, kama mtoto, ila nitataka kufuata taratibu zote
zinazohitajika, ili , kama hilo kurithi linaleta hisia mbaya, tusiseme hivyo……mimi
nipo tayari kufuata taratibu nyingine, …’akasema na kutulia.
‘Taratibu gani hizo….?’ akauliza mama kwa mshangao.
‘Mimi naweza kuja kumposa binti huyu kwenu, ili awe mke
wangu..nazungumza hili kwa nia njema kabisa, nafanya hivi kwa ajili yake na mtoto, kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mke
aliyeachwa na ndugu yangu hapati shida, na juhudi zake hazipotei bure…’akasema
huku akiwa kaweka mikono kifuani kwake na wazazi wangu wakawa wanamwangalia kwa
makini.
‘Nani kakuambia kuwa mimi nahitaji mume…..sina haja ya ndoa
na mtu yoyote, ….nilishawaamba wazi, na msifikirie kuwa mimi nitakubali kwa
kutumia mitego yenu hiyo..kamwe sitakubali kwa hilo, hata kama mtachukua kila
kitu changu…bado nitabakia kwenye msimamo wangu….’nikasema.
‘Shemeji, hakuna mtu atakayechukua kitu chako…hili
nakuhakikishia…kama kuna kitu chako kama chako, hakuna atakyekigusa….hilo
nakuthibitishia, sisi tunachokilinda ni mali ya ndugu yetu,.na kauli yake,….na nafahamu
kuwa kwa aslimia kubwa huenda mlichuma wote, ni sawa, …ndio mama sisi kama
wanafamilia tuliliona hili, ..wewe bado utaendelea kuchuma na kufaidikia na
kile mlichokianza na kaka marehemu,… ila sisi kama wanafamilia tunachokikataa
ni wewe kumiliki, na kudai kuwa ni mali yako binafsi, na ulijenga hiyi nyumba
kwa pesa zako ….wakati hilo sio sahihi..’akasema.
‘Sio sahihi kwa vile mumechukua ushahidi wote,…sio sahihi
kwa vile mumejenga hiyo hoja kinafiki mbele ya hakimu…, lakini mkumbuke kuwa
kamwe jasho la mtu na haki ya mtu haipotei bure, ..hiyo haki ni yangu, na nina
uhakika kuwa nimejenga kwa pesa zangu,….mungu wangu ni shahidi hata kama nyie
mtalipinga, hata kama nitakosa shahidi wa kidunia, ila mungu wangu anatosha
kuwa shahidi yangu…’nikasema.
‘Shemeji, kama kungelikuwa na namna yoyote ya
kunishawishi,…nisingelifanya haya, maana mimi siwezi nikaamini hayo
unayoniambia,…..nitaaminije,….wakati ndugu yangu mwenyewe alinitamkia , na hata
kuniomba nikaandikishe….hati miliki kwa jina langu kwa vile alitaka mimi na
wewe tuwe familia moja…..’akasema huku akiniangalia, halafua akawageuka wazazi
wangu kama vile anaomba msaada wa
‘Shemeji….hapana shemeji,…mimi bado sijaamini,..nionyesheni
ushahidi kama mnao, na kama nikiuona, nakuhakikishaia kuwa ni kweli,…shemeji, wazazi
wangu,…mimi nitakwenda kuiambia mahakama kuwa kweli hiyo ni mali yake, na
sitasubiri familia itoe uamuzi,…’akasema.
‘Hayo ni maneno ya mfa maji,…naona mumehisi kuwa tumeshaupata
huo ushahidi na mtakuja kuumbuka mahakamani, ..ndio maana mnajaribu kutafuta
upenyo wa hadaa…..sisi tutakutana huko huko mahakamani…’akasema baba
akijiamini, huku nikiwaza jinsi gani ya kuupata huo ushahidi.
Huyu jamaa aliposikia maeneo hayo toka kwa wazazi wangu,
akaonekana kutulia, na baadaye akanigeukia na kusema;
‘Shemeji,..bado nasisitiza kuwa nina mazungumzo kati yangu mimi
na wewe ya faragha, hili ni muhimu tuongee tukiwa wawili,…sina nia mbaya yoyote
juu yako,…mimi kama mtu niliyekabidhiwa wewe na mtoto nina wajibu wa
kuhakikisha mnaishi kwa amani na salama….’akasema.
‘Nashukuru kwa hilo…., tupo salama na amani, hamna shida,
unaweza kwenda …’nikasema.
‘Shemeji tafadhali, nakuomba…’akasisitiza na wazazi wangu
wakaingilia kati na kuniambia nikamsikilize kuwa anataka kusema nini.
********
‘Haya niambie unanitakia nini kwa faragha..?’ nikamuuliza
pale tulipoingia kwenye chumba kingine.
‘Ni hivi shemeji,…sina uhakika kuwa yule mchumba wangu amewahi
kuja hapa na mkakutana naye au vipi, ila nahisi hivyo kuwa huenda amefika
akaongea na wewe….cha muhimu ninachotaka kukuambia ni kuwa, yule anatapatapa…kuna
mambo ambayo tunasigishana, likiwemo hili la kutimiza wajibu wangu nilioachiwa
na ndugu yangu….’akatulia na kuniangalia , na machoni alionekana hana raha.
‘Kwahiyo unahitaji ushauri wangu au..?’ nikamuuliza.
‘Shemeji, nikuambie ukweli, huenda hilo ulikuwa hulijuia
kwasababu sikuwahi kuoanana na wewe uso kwa uso, lakini mimi nakufahamu muda
mrefu tu….na kiukweli moyo wangu ulikuwa umevutika na wewe, kwa vile ulikuwa
mke wa ndugu yangu, niliheshimu hilo, japokuwa moyoni, nilitamani nipate mtu
kama wewe…’akasema huku akiwa anaonyesha huzuni, au sikumuelewa.
‘Shemeji…hili nakuambia toka moyoni, siliongei leo kwa vile
kuna jambo lolote jingine, hapana, shemeji, nimeamua leo nikuambie ukweli, wa
kutoka moyoni kwangu….’akatulia na kuniangalia usoni, mimi nilikuwa nimeinama
chini.
‘Mara nyingi nilikuwa nafika hapa na kaka yangu, lakini
nilikuwa siingi ndani, ….na moja ya saabbu ni hiyo, kuto….siunajua shemeji, mtu
unampenda na ni mke wa kaka yako, utafanyaje….inabidi uheshimu na uumie
kiundani ndani, na niliona jambo jema ni kuwa mbali na wewe kadiri
ilivyowezekana….’akatulia kidogo.
‘Yaani nasema hayo kutoka kwenye moyo wangu,…nilikuwa
najaribu kukuangalia kwa mbali, wewe nafikiri hukuwa na umakini na mimi, kama
ungelikuwa mdadisi ungeligundua hilo, lakini hilo halina maana kwa sasa…ila
nilitaka tu kutoa lile lilokuwa moyoni kwangu, kuwa sio kwamba nayafanya haya
kwa vile unahitajika kurithiwa….silipendi hilo neno, lakini inabidi iwe hivyo,
nayafanya haya kwanza kwa ajili ya kutimiza yale niyoyaahidi kwa ndugu yangu,
lakini kubwa zaidi ni kwa vile nakupenda……..’akasema.
‘Nakusikiliza shemeji….naomba ufanye haraka kutoa maana kma
ulivyoona sisi tuna kikao, na wageni ndio hao wanaanza kuingia….’nikasema
niliposkia mlango ukigongwa.
‘Oh, shemeji huna habari…ina maana hujaambiwa, haiwezekani,
kesi imeahirishwa ni mpaka kesho kuwa asubuhi…’akasema na mara tukasikia hodi
nyingine,….na baaadaye nikasikia mtu akisema kuwa kaleta barua.
‘Inawezekana ndio barua hiyo ya kukuarifu kuwa kesi ni kesho
kutwa asububuhi sio kesho tena…na kama unataka, mimi ninaweza hata hiyo kesho
kesi ikaahirishwa na hata kufutwa kabisa….’akasema.
‘Ufute hiyo kesi kwani wewe ndio umeshitaki…..?’ nikamuliza
nikimwangalia kwa zarau.
‘Nafahamu hilo, ….ila tukikubaliana , mimi nitakwenda
kuongea na hakimu, na kesi ikafutwa kabisa…’akasema.
‘Utafutaje kesi ambayo wewe sio uliyeshitaki…?’ nikamuuliza
huku nikiwa nimekunja uso kwa hasira.
‘Unisikilize kwa makini shemeji, nasema `tu-ki-ku-baliana’,
na tukasema hili swala tutalimaliza nyumbani, ….basi wewe na mimi tunakwenda
pale mahakamani, tunamwambia muheshimiwa hakimu kuwa tumeshakubaliana,…sioni
kwanini tufikie hapa,shemeji mimi nakupenda sana, nahitaji nishike ile nafasi
ya ndugu yangu, …..’akasema.
‘Shemeji, nimekusiliza kwa makini…kwakweli jisini
unavyofanya nazidi kukuona kuwa hufai….Hivi wewe una akili kweli, una ubinadamu
kweli, wewe una mchumba, unafikiri huyo mchumba wako atakuelewa vipi, au
ulikuwa unampotezea muda wake bure..usiwe na roho ya kinyama…jaribuni
kuwafikiria na wengine, …’nikamwambia.
‘Hilo shemeji lisikuumize kichwa, mimi na huyo mchumba wangu
tunajuana,….na uchumba wetu ulikuwa na msharti, kadhaa…ambayo kama hayakutimia,
au hatukukubaliana, basi uchumba huo unavunjika, na hayo tumeshayaongea,…sina
unyama wa anmna hiyo, …..yeye mwenyewe karizia hilo, iwe hivyo, na kakubali
kama utakubali wewe uwe mke wangu, basi yeye atakaa pembeni….’akasema.
‘Hata sikumoja, usije ukaota hilo…kwa ufupi nakuomba,
ukamrejee mchumba wako umwambia kuwa mimi sitaki kuolewa na wewe…sitaki kuolewa
kwenye hiyo familia yenu tena…ni bora niishi
hivi hivi hadi kufa kwangu kuliko kuolewa kwenye hiyo familia yenu…’nikasema
‘Kwanini shemeji unasema hivyo,…tumekukosea nini,familia
yetu imefanya nini kibaya kwako …?’ akauliza kwa uchungu
‘Wewe haya mliyoyafanya mnafikiri ni mazuri….hamjui ni kiasi
gani mlivyoniumiza, na bora haya yangelikuwa kati yangu na nyie, lakini mumefikia
hadi ya kumuumiza yule baba yangu wa kufikia, kwa ajili ya mali ambayo sio
halali yenu..sitawasamehe kwa hilo….kamwe.nakuomba uondoke…na sitaki kuongea na
wewe kuhusiana na hilo ombi lako…natumai umenisikia…mengine tutakutana
mahakamani’nikasema.
‘Kwa hilo shemeji, sitaacha kukuomba…, iwe itakavyokuwa,
lakini mimi kila siku nitakuja kwa ajili ya hilo, kwa vile nafanya hivyo sio tu
kwa matakwa ya ndugu yangu, lakini pia ni kwa vile nakupeda…’akasema
‘Lakini mimi sikupendi, kwahiyo huwezi kulazimisha mapenzi,….wewe
ni msomi naomba ulielewe hilo, ….sikupendi na sitatokea kupenda mtu yoyote
kwenye hiyo familia yenu, na ipo siku mtaumbuka, kwa tabia hiyo ya kutaka
dhuluma, ..ipo siku mtaumbuka….’nikasema kwa sauti.
Na mara ghafla huyu shemeji akapiga magoti mbele yangu, na
huku akiwa katoa kiboksi kikionyesha kuwa ni cha pete….na akawa anakifungua
huku kapiga magoti mbele yangu…nikawa nimetahayari kwa kitendo chake hicho, na hata
kabla sijaweza kusema neno, huku nimekunja uso kwa hasira, mara mlango
ukafunguliwa, ….
`Shemeji….nakuomba ukubali uwe mke……’akaanza kuongea, na
ndip hapo mlango ukafunguliwa na aliyekuwa kasimama kati kai ya mlango alikuwa
yule mchumba wake, akaniangalia huku akionyesha tabasamu kidogo, lakini lilifia
pale alipomuona huyu jamaa akiwa kanipigia magoti na mkononi kashika pete…..mimi
nikiwa bado nimetahayari , nikamwangalia shemeji yangu huyo aliyekuwa bado
kapiga magoti, na aliposikia mlengo ukifunguliwa akageuza kichwa na kuangalia
huko mlangoni, alimuona mchumba wake, akiwa anatuangalia na tabasamu lililojaa
huzuni machoni
Yule shemeji yangu alipoona huyo aliyeingia ni nani, kwa
haraka akasimama, huku akifuta futa kwenye magoti yake kuondoa vumbi kwenye
suruali yake.
‘Wewe umefuata nini huku…?’ akauliza , na sauti yake
ilionyesha unyinge fulani, sio ile sauti ya kujiamini aliyozoea kuiongea.
‘Samahani…kidogo, nataka kuongea na mteja wangu…’akasema
huyo mchumba wake.
‘Mteja wako…?’ akauliza huyo shemeji yangu kwa uso
uliosawajika, alikuwa kama kaishiwa nguvu,….
NB: itakuwaje?
WAZO LA LEO: Tuwe
makini na kauli zetu, tuwe makini na mtendo yetu, ambayo tukiyaongea au
kuyafanya yanaathiri hisia zetu. Hili ni kwa wale waliotokea kupendana, na
kuotokana na misigishano kukawa na kutokuelewana, ni vyema kuwa makini
kutokuumizana zaidi na kujenga chuki
zaidi. Pendaneni kwa wema, na kama ikibidi kuachana achaneni kwa wema.
Ni mimi:
emu-three
5 comments :
kweli, ni muhimu kuwa makini na kauli zetu...
Visa kama hivi vinafunza sana nakusihi andika kitabu kitawasaidia wengi maana wengi hawana nafasi/uwezo wa mtandao kama wengine ila kununua kitabu najua wengi wana uwezo..Bonge la shule hapa....amani kwa wote.
Mbona haiendelei mnatunyima uhondo bhana
Mbona haiendelei mnatunyima uhondo bhana
Niliadimika kidogo kutokana na mitihani ya hapa na pale...tuendelee sehemu inayofuata, nawashukuru sana @Justine Kasyome, dada wangu @Yasinta, ndugu yangu @Nancy Msangi na wale wote wa Kimiya kimiya. Tupo pamoja
Post a Comment